Katibu Mkuu, Wizara ya
Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe amewahimiza wadau wa sekta ya uvuvi
kujikita katika ufugaji wa viumbe maji ili kusaidia kukuza mchango wa sekta ya
uvuvi katika Pato la Taifa kutoka asilimia 1.7 walau kufika mpaka asilimia 5
ifikapo mwaka 2025.
Prof. Shemdoe alitoa rai
hiyo wakati akifungua kikao kazi cha wadau wa Ukuzaji Viumbe maji kilichofanyika jijini Dodoma
Oktoba 31, 2023.
Alisema kuwa hivi sasa
wanaandaa kanuni zitakazosaidia kuwa na usimamizi madhubuti wa tasnia ya uvuvi
kwa lengo la kuimarisha ukuzaji wa viumbe maji ili kuchangia vyema katika Pato
la Taifa.
"Tunaandaa kanuni kwa
ajili ya ufugaji viumbe maji , kwenye ufugaji wa samaki na mavuvi ya samaki ili
kuona namna tutaweza ndani ya miaka hii
miwili kuchangia asilimia 5 kwenye pato la taifa,"
alisema Prof. Shemdoe
Aliongeza kuwa kanuni hizo
zitakwenda kuboresha namna tasnia ya ukuzaji viumbe maji inasimamiwa na
kuwezesha kile kinachozalishwa kiweze kufika kwenye masoko makubwa ya kikanda
na kimataifa
Naye Naibu Katibu Mkuu
Sekta ya Uvuvi Bi. Agness Meena amesema kupitia kikao hicho wadau watapata
fursa ya kubainisha changamoto zinazoikabili tasnia ya ukuzaji viumbe maji na
kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na changamoto hizo na kuongeza uelewa
kuhusu usimamizi shirikishi na kuwa na tasnia endelevu.
Kwa upande wake Mkurugenzi
wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji, Dkt. Nazael Madala amesema tasnia ya ukuzaji
viumbe maji itakuja kuwa na mchango mkubwa sana kwenye Sekta ya Uvuvi kwa vile bado ni ndogo na
inakuwa kwa haraka.
"Tanzania tuna bahati
ya kuwa na rasilimali nyingi za maji kwa maana ya maziwa, mabwawa makubwa, maji
ya chini ya ardhi, ambayo yanaweza kuchimbwa na sehemu yoyote ikafanyika
ufugaji wa samaki katika mabwawa na tukiweza kufanya hivi tunaweza tukaongeza
fursa zaidi za ajira, na kuongeza kipato cha mwananchi mmoja mmoja na jamii kwa
ujumla" Alisema Dkt. Madala
Kikao hicho, kimefanyika
kwa ushirikiano wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Shirika la Chakula na kilimo
Duniani (FAO) Tamisemi pamoja na wafugaji wa samaki na mwani, lengo likiwa ni
kujenga uelewa wa pamoja kuhusu changamoto zilizopo na kubaini mikakati ya
kuzitatua.
Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe akiongea na washiriki wakati akifungua
kikao kazi cha wadau wa ukuzaji viumbe maji kilichofanyika kwenye ukumbi wa
Rafiki hotel jijini Dodoma, Oktoba
31,2023
Naibu Katibu Mkuu Sekta ya
Uvuvi Bi. Agness Meena akitoa neno fupi wakati wa kufungua kikao kazi cha wadau
wa ukuzaji viumbe maji kilichofanyika kwenye ukumbi wa Rafiki hotel jijini
Dodoma, Oktoba 31,2023
Mkurugenzi wa Idara ya
Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Nazael Madala akiwasilisha mada wakati wa kikao kazi cha
wadau wa ukuzaji viumbe maji kilichofanyika kwenye ukumbi wa Rafiki hotel jijini
Dodoma, Oktoba 31,2023
Afisa Uvuvi anayeshughulikia
minyororo ya thamani ya uvuvi na ufugaji wa viumbe maji kutoka Shirika la
Chakula na Kilimo Duniani (FAO) Bw. Hashim Muumin akitoa neno wakati wa
ufunguzi wa kikao kazi cha wadau wa ukuzaji viumbe maji kilichofanyika kwenye
ukumbi wa Rafiki hotel jijini Dodoma Oktoba 31,2023
Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na
sehemu ya wadau walioshiriki kikao kazi cha
ukuzaji viumbe maji mara baada ya
kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa Rafiki hotel jijini Dodoma Oktoba
31,2023