Nav bar

Jumanne, 31 Oktoba 2023

WADAU WAHIMIZWA KUFUGA SAMAKI KUKUZA SEKTA YA UVUVI NCHINI


Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe amewahimiza wadau wa sekta ya uvuvi kujikita katika ufugaji wa viumbe maji ili kusaidia kukuza mchango wa sekta ya uvuvi katika Pato la Taifa kutoka asilimia 1.7 walau kufika mpaka asilimia 5 ifikapo mwaka 2025.

Prof. Shemdoe alitoa rai hiyo wakati akifungua kikao kazi cha wadau wa Ukuzaji  Viumbe maji kilichofanyika jijini Dodoma Oktoba 31, 2023.

Alisema kuwa hivi sasa wanaandaa kanuni zitakazosaidia kuwa na usimamizi madhubuti wa tasnia ya uvuvi kwa lengo la kuimarisha ukuzaji wa viumbe maji ili kuchangia vyema katika Pato la Taifa.

"Tunaandaa kanuni kwa ajili ya ufugaji viumbe maji , kwenye ufugaji wa samaki na mavuvi ya samaki ili kuona  namna tutaweza ndani ya miaka hii miwili  kuchangia  asilimia 5 kwenye pato la taifa," alisema Prof. Shemdoe

Aliongeza kuwa kanuni hizo zitakwenda kuboresha namna tasnia ya ukuzaji viumbe maji inasimamiwa na kuwezesha kile kinachozalishwa kiweze kufika kwenye masoko makubwa ya kikanda na kimataifa

Naye Naibu Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi Bi. Agness Meena amesema kupitia kikao hicho wadau watapata fursa ya kubainisha changamoto zinazoikabili tasnia ya ukuzaji viumbe maji na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na changamoto hizo na kuongeza uelewa kuhusu usimamizi shirikishi na kuwa na tasnia endelevu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji, Dkt. Nazael Madala amesema tasnia ya ukuzaji viumbe maji itakuja kuwa na mchango mkubwa sana kwenye  Sekta ya Uvuvi kwa vile bado ni ndogo na inakuwa kwa haraka.

"Tanzania tuna bahati ya kuwa na rasilimali nyingi za maji kwa maana ya maziwa, mabwawa makubwa, maji ya chini ya ardhi, ambayo yanaweza kuchimbwa na sehemu yoyote ikafanyika ufugaji wa samaki katika mabwawa na tukiweza kufanya hivi tunaweza tukaongeza fursa zaidi za ajira, na kuongeza kipato cha mwananchi mmoja mmoja na jamii kwa ujumla" Alisema Dkt. Madala

Kikao hicho, kimefanyika kwa ushirikiano wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Shirika la Chakula na kilimo Duniani (FAO) Tamisemi pamoja na wafugaji wa samaki na mwani, lengo likiwa ni kujenga uelewa wa pamoja kuhusu changamoto zilizopo na kubaini mikakati ya kuzitatua.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe akiongea na washiriki wakati akifungua kikao kazi cha wadau wa ukuzaji viumbe maji kilichofanyika kwenye ukumbi wa Rafiki hotel jijini Dodoma,  Oktoba 31,2023

Naibu Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi Bi. Agness Meena akitoa neno fupi wakati wa kufungua kikao kazi cha wadau wa ukuzaji viumbe maji kilichofanyika kwenye ukumbi wa Rafiki hotel jijini Dodoma,  Oktoba 31,2023

Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Nazael Madala  akiwasilisha mada wakati wa kikao kazi cha wadau wa ukuzaji viumbe maji kilichofanyika kwenye ukumbi wa Rafiki hotel jijini Dodoma,  Oktoba 31,2023

Afisa Uvuvi anayeshughulikia minyororo ya thamani ya uvuvi na ufugaji wa viumbe maji kutoka Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) Bw. Hashim Muumin akitoa neno wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha wadau wa ukuzaji viumbe maji kilichofanyika kwenye ukumbi wa Rafiki hotel jijini Dodoma Oktoba 31,2023


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na sehemu ya wadau walioshiriki kikao kazi cha  ukuzaji viumbe maji  mara baada ya kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa Rafiki hotel jijini Dodoma Oktoba 31,2023


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni