Nav bar

Jumatatu, 30 Novemba 2020

SAUTI YETU WIKI HII


 

SAUTI YETU WIKI HII


 

MAZIWA BONANZA


 

WAFUGAJI NA WAKULIMA KUNUFAIKA KUPITIA KIWANDA CHA NYAMA NGURU HILLS

Serikali imesema katika kuboresha na kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji katika maeneo mbalimbali nchini ukiwemo Mkoa wa Morogoro, inasisitiza uwepo wa miradi ambayo itakuwa na manufaa makubwa kwa makundi yote mawili.

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema hayo (28.11.2020) katika Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro alipotembelea ujenzi wa mradi wa kiwanda cha nyama katika Ranchi ya Nguru Hills na kubainisha kuwa mradi huo unaotarajia kukamilika mwezi Aprili Mwaka 2021 utakuwa na manufaa makubwa kwa wafugaji na wakazi wa Mkoa wa Morogoro.

 

“Tumekuja kuangalia shughuli zinazoendelea kutokana na kikao ambacho tulikuwa nacho katika ofisi ya katibu tawala wa mkoa na mkuu wa Mkoa wa Morogoro katika kuboresha shughuli za mifugo kwenye mkoa huo na kuondoa changamoto za migogoro ya wafugaji ambapo uongozi wa mkoa waliniambia juu ya mradi huu ambao utakuwa na msaada mkubwa sana kwa wakulima na wafugaji wa mkoa wa Morogoro na nchi kwa ujumla.” Amesema Prof. Gabriel.

 

Prof. Gabriel amebainisha kuwa mradi huo wa kipekee ambao mara baada ya kiwanda hicho kukamilika kitakuwa na uwezo wa kuchinja ng'ombe zaidi ya 200 na mbuzi zaidi ya 1,000 kwa siku, kumejengwa mabwawa makubwa ambayo yatakuwa yanakusanya maji yanayotoka kwenye machinjio, kisha kutibiwa kabla ya kutumika tena kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji.

 

“Mradi huu una jambo mahsusi kuliko mingine, maji haya ya mabwawa yatatumika kwa ajili ya umwagiliaji huu ni moja kati ya miradi ambapo wafugaji na wakulima watanufaika ili wote waone huu mradi ni wa kwao kwa ajili ya uchumi wetu.” Ameongeza Prof. Gabriel.

 

Aidha, amesema mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 25, ambao unashirikisha wabia mbalimbali ukiwemo Mfuko wa Pesheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), ni azma ya serikali katika kuzidi kuboresha mazingira ya uwekezaji hapa nchini kwenye sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Mifugo hivyo kuwataka wafugaji kuboresha mifugo yao kwa kufuga ng’ombe bora wa kisasa na kupitia miradi ya kunenepesha mifugo ili waweze kuuza mifugo yenye ubora katika viwanda vya kusindika mazao ya mifugo hapa nchini ili sekta izidi kukua na kuchangia pato la taifa kupitia uchumi wa viwanda.

 

Pia katibu mkuu huyo amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha Tanzania inakuwa na mifugo mingi na bora kwa kuhakikisha mifugo inaogeshwa ili kujikinga dhidi ya magonjwa na kuwataka wakurugenzi wa halmashauri kote nchini, kuhakikisha maeneo yao yana majosho ya kutosha kwa ajili ya kuogeshea mifugo na kuwataka wayafanyie ukarabati majosho ambayo hayafanyi kazi.

 

“Tufuge kisasa Namibia, Botswana wana ng’ombe wachache lakini wanauza kwa wingi nyama nje ya nchi, ndiyo maana tunaimarisha afya za mifugo, ndiyo maana nchi nzima tunashughulika na masuala ya uogeshaji niwatake wakurugenzi wa halmashauri wahakikishe kwenye maeneo yao kuna majosho ya kutosha na niwatake yale ambayo hayafanyi kazi vizuri yaboreshwe. Ameongeza Prof. Gabriel.

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amelitaka pia Dawati la Sekta Binafsi lililo chini ya wizara hiyo pamoja na Idara ya Uzalishaji na Masoko kwa kushirikiana na PSSSF kukutana haraka ili kujadili changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika mradi wa kiwanda cha nyama Nguru Hills ili mradi huo ukamilike kwa wakati.

 

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Bw. Hassan Chama Hassan amemwambia katibu mkuu huyo kuwa, mradi huo ukikamilika kwa wakati wafugaji watanufaika kwa kuwa wanakabiliana na changamoto ya kuuza mifugo yao kupitia minada ambapo wanakutana na madalali ambao wanafanya bei za mifugo kuwa chini, huku Meneja Ujenzi wa mradi huo kutoka PSSSF Mhandisi Grayson Bambaza akibainisha kuwa wafugaji watakuwa wanauza mifugo yao kwa kilo na siyo kwa kukadiria kulingana na umbo la mfugo.

 

Mradi wa kiwanda cha nyama katika Ranchi ya Nguru Hills unaotarajia kukamilika mwezi Aprili Mwaka 2021, unategemewa kutoa ajira kwa wafanyakazi 120 hadi 200 kulingana na uzalishaji.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel (wa kwanza kushoto) akizungumza na baadhi ya viongozi wa Ranchi ya Nguru Hills juu ya mradi wa kiwanda cha nyama kinachojengwa katika ranchi hiyo huku akiwataka wahakikishe mara baada ya kiwanda hicho kitakapoanza kufanya kazi, kitoe bidhaa bora ili kushindana na soko la kimataifa. Meneja Mkuu wa ranchi hiyo Bw. Paul Phillips (aliyesimama katikati) amemuhakikishia katibu mkuu huyo kuzingatia maelekezo yake. (28.11.2020)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akikagua mabwawa yanayojengwa katika Ranchi ya Nguru Hills, ambayo yatapokea maji yatakayokuwa yanatoka kwenye machinjio na kutibiwa kabla ya kutumika kwenye kilimo cha umwagiliaji. Prof. Gabriel ameambatana na viongozi wa ranchi, viongozi wa halmashauri ya Wilaya ya Mvomero na baadhi ya watumishi kutoka wizarani. (28.11.2020)

Muonekano wa moja ya mabwawa yanayojengwa katika Ranchi ya Nguru Hills, ambayo yatapokea maji yatakayokuwa yanatoka kwenye machinjio na kutibiwa kabla ya kutumika kwenye kilimo cha umwagiliaji. (28.11.2020)

Muonekano wa nje wa ujenzi wa kiwanda cha nyama Nguru Hills kinachotarajiwa kutoa ajira kati ya wafanyakazi 120 hadi 200 kulingana na uzalishaji. (28.11.2020)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akikagua ujenzi wa kiwanda cha nyama Nguru Hills huku akijihakikishia vipimo vilivyobainishwa katika mchoro wa jengo hilo. (28.11.2020)

Muonekano wa moja ya maeneo ya ndani ya kiwanda cha nyama Nguru Hills kitakachokuwa na uwezo wa kuchinja mbuzi zaidi ya 200 na ng’ombe zaidi ya 1,000 kwa siku. (28.11.2020)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa Ranchi ya Nguru Hills viongozi kutoka halmashauri ya Wilaya ya Mvomero na Wizara ya Mifugo na Uvuvi. (28.11.2020)







Jumamosi, 28 Novemba 2020

WAFUGAJI WASHAURIWA KUWEKEZA KATIKA KILIMO CHA MALISHO.

WAFUGAJI WASHAURIWA KUWEKEZA KATIKA KILIMO CHA MALISHO

 

Wafugaji wa Ng’ombe wameshauriwa kujikita katika kilimo cha Malisho ili wawe na uhakika wa malisho bora kwa ajili ya mifugo yao na kuachana na uchungaji wa kutafuta malisho.

 

Mtendaji Mkuu wa Shamba la Ndoto, Hartmut Rottcher aliyasema hayo kwa Wakurugenzi na Mameneja wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliotembelea shamba la mfano la Ndoto lililopo Mkoani Iringa Novemba 27, 2020.

 

Rottcher alisema kilimo cha malisho yaliyo bora kinasaidia kuwapatia mifugo uhakika wa chakula bora huku akieleza kuwa mifugo ni muhimu kupewa pumba kwa kiasi na sio kuzidisha kwani kufanya hivyo hupelekea ng’ombe kupata asidi tumboni na kuuwa bakteria ambao husaidia kukata kata majani tumboni kwa mnyama.

 

Alisema kuwa yeye anafanya kilimo cha malisho kwa kumwagilia na ametenga maeneo katika mashamba yake illi kusaidia kulisha mifugo kwa mzunguko na kuipatia mifugo  mahitaji  wanayotaka na sio kuletewa chakula kwenye maboma yao.

 

“Njia ya kulisha kwa mzunguko husaidia kupata muda wa kuondoa magugu na kufanya shamba kuwa safi na malisho kustawi vizuri kwa wakati na linakuwa na rutuba ya kutosha,” alisema Rottcher

 

“Kulisha chakula cha kutosha na cha aina tofauti husaidia mnyama kupata virutubisho vingi vinavyosaidia kujenga afya ya mifugo,” Aliongeza Rottcher

 

Aidha, aliwashauri Wakurugenzi na Mameneja wa mashamba ya Serikali kutoa mifugo kwenda kujitafutia chakula na sio kuwaletea katika maboma yao kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia mifugo kupata kile wanachotaka na sio kuwapimia chakula jambo ambalo litawezesha kupata mifugo iliyo bora yenye nyama nyingi na maziwa ya kutosha yenye viwango.

 

Akieleza kuhusu ziara yao katika Shamba hilo, Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ugani Dkt. Kejeri Gillah alisema lengo ni kujifunza na kubadilishana uzoefu katika kuboresha kosaafu na utunzaji wa mifugo, ustawishaji wa malisho bora kwa mifugo ya aina mbalimbali na namna ya uhifadhi wa malisho kwa matumizi ya kipindi cha kiangazi.

 

“Ni mategemeo yetu kwamba safari hii itakuwa ya mafanikio makubwa sana kwetu na tutaweza kuboresha mifugo yetu na kustawisha malisho ya mifugo kama tutafuata yale yote tutakayoelekezawa” alisema Dkt. Gillah

 

Ziara hiyo iliratibiwa na Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani, ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ugani, Dkt. Kejeri Gillah, wengine walishiriki katika ziara hiyo ni Mameneja kutoka Shamba la kitulo, Sao hill, Langwira, Vikuge, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) Uyole na meneja wa Ranchi ya Kalambo.






Afisa Utafiti Mifugo Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Felista Kimario akitoa neno la shukrani kwa Mtendaji Mkuu wa shamba la Ndoto, Bw. Hartmut Rottcher (hayupo pichani) kwa kutumia muda wake kuwatembeza kwenye shamba hilo na kuwaelimisha mambo mbalimbali katika upandaji wa malisho, namna ya kutunza na kulisha Mifugo. (27.11.2020)

Mtendaji Mkuu wa shamba la Ndoto, Bw. Hartmut Rottcher (wa pili kutoka kulia) akiwatembeza watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliofika shambani hapo  kujionea na kujifunza namna ya ustawishaji wa malisho, uboreshaji wa kosaafu na utunzaji Mifugo. (27.11.2020)

Kaimu Mkurugenzi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Uyole Mbeya, Dkt. Edwin Peter Chang'a (katikati) akiuliza swali kwa Mtendaji Mkuu wa shamba la Miombo, Bw. Rex Fey (wa pili kushoto) wakati wa safari yao ya Mafunzo Mkoani Iringa. (27.11.2020)

Mtendaji Mkuu wa shamba la Ndoto mkoani Iringa, Bw. Hartmut Rottcher akiwaeleza watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi aina ya nyasi za malisho zilizopo shambani hapo na namna anavyofanya kilimo cha malisho ya Mifugo. (27.11.2020)

Watumishi kutoka katika mashamba mbalimbali ya Mifugo yaliyopo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakimsikiliza Mtendaji Mkuu wa shamba la Miombo, Bw. Rey Fey (kushoto) wakati akizungumzia kuhusu mbegu, malisho na namna bora ya kulisha Mifugo kwenye shamba la Ndoto lililopo mkoani Iringa. (27.11.2020)

Kaimu Mkurugenzi Ugani Mifugo kutoka WMUV, Dkt. Kejeri Gillah akieleza lengo la safari yao ya Mafunzo wakati walipotembelea shamba la Ndoto mkoani Iringa, kuwa ni kubadilishana uzoefu katika uboreshaji wa kosaafu, utunzaji Mifugo, uhifadhi bora wa malisho, Udhibiti wa Magonjwa na matumizi ya madawa. (27.11.2020)

Kaimu Mkurugenzi Ugani Mifugo kutoka WMUV, Dkt. Kejeri Gillah akieleza lengo la safari yao ya Mafunzo wakati walipotembelea shamba la Ndoto mkoani Iringa, kuwa ni kubadilishana uzoefu katika uboreshaji wa kosaafu, utunzaji Mifugo, uhifadhi bora wa malisho, Udhibiti wa Magonjwa na matumizi ya madawa. (27.11.2020)







 

SERIKALI YAJIPANGA KUIMARISHA SEKTA YA UVUVI NCHINI

Na Mbaraka Kambona, Singida.

 

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ipo katika mchakato wa kukamilisha Mpango kabambe wa miaka 15 ijayo kuanzia 2021 utakaosimamia sekta ya Uvuvi na kutoa dira ya kulinda rasilimali za uvuvi ili sekta hiyo iweze kutoa mchango mkubwa na endelevu katika pato la taifa.

 

Hilo limefahamika wakati Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akifungua Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Uvuvi wa kupitia, kujadili na kuidhinisha masuala ya kipaumbele yanayopaswa kuingizwa katika Mpango huo Kabambe unaofanyika Mkoani Singida Novemba 26-28, 2020.

 

Dkt. Tamatamah alisema kuwa lengo la Serikali ni kuona sekta ya Uvuvi inaendelea kutoa mchango mkubwa katika pato la taifa zaidi ya ilivyosasa na ndio maana inaanda Mpango huo ili usimamizi wa rasilimali za uvuvi uwe imara.

 

“Ni mategemeo yetu kuwa mpango huu utatoa hamasa kwa sekta ya uvuvi katika kulinda usalama wa chakula kuanzia ngazi ya kaya na taifa, vilevile tunatarajia utuingize katika uchumi wa viwanda na uchumi wa bluu,” alisema Dkt.Tamatamah

 

Alisema kuwa pamoja na juhudu za Wizara za kusimamia maendeleo ya Sekta ya Uvuvi nchini, Sekta hiyo imeendele kukabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo kwa ujumla zimekuwa zikiathiri ukuaji na uendelevu wa sekta hiyo.

 

Aliendelea kueleza kuwa ili kukabiliana na changamoto hizo, Wizara imekuwa ikitekeleza mipango, mikakati na programu mbalimbali zinazolenga kuendeleza sekta ya uvuvi nchini, miongoni mwa mipango hiyo ni Mpango huo Kabambe wa Uvuvi unaotarajiwa kuanza kutumika mwaka 2021.

 

Mratibu wa Masuala ya Uvuvi kutoka Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), ambao wanafadhili maandalizi ya mpango huo, Dkt. Oliver Mkumbo alisema shirika hilo limeamua kufadhili mpango huo ikiwa ni sehemu ya malengo yao ya kuhakikisha dunia inaondokana na njaa, umasikini na kuimarisha usalama wa chakula ili ifikapo mwaka 2030 pasiwepo na mtu atakayekuwa na njaa.

 

Aidha, wadau wa Sekta ya Uvuvi hawakusita kuonesha matumaini yao na mpango huo huku wakisema kuwa ukikamilika utajibu changamoto nyingi ambazo zimeendelea kukabili sekta hiyo.

 

Kiongozi wa Wavuvi Mkoani Kigoma, Francis John alisema kuwa mpango huo ambao utasimamia rasilimali za uvuvi utawasaidia kuimarisha biashara yao ya dagaa kutoka ziwa Tanganyika kwani mpango huo utawahakikishia uwepo wa dagaa wengi ambapo wataweza kuwa na mzigo wa uhakika wa kusafirisha kwenda kuuza dagaa wao katika nchi za Marekani, Astralia, Kanada, Uingereza na Denmark.

 

Naye, Raphael John, mdau wa sekta hiyo ya Uvuvi alisema kuwa  moja ya mambo yatayokwenda kuimarishwa kupitia mpango huo ni ufugaji na ukuzaji wa viumbe maji jambo ambalo anasema litasaidia kupunguza utegemezi wa kupata mazao ya uvuvi kutoka maji ya asili pekee.

 

“Katika nchi nyingi zilizoendelea, ufugaji na ukuzaji wa viumbe maji umepewa kipaumbele sana, ni muhimu kuimarisha eneo hilo ili tusitegemee tu uvuvi wa mazao ya samaki katika maji ya asili, ni lazima tuanze sasa kabla rasilimali za asili katika bahari, mito na maziwa hazijaisha,” alisema John

 

Mpaka sasa sekta ya uvuvi inachangia asilimia 1.7 katika pato la Taifa huku ikielezwa kuwa sekta hiyo inatoa ajira ya moja kwa moja kwa wananchi takriban 202,000 na wananchi wengine wasiopungua Milioni 4.5 wamaendelea kutegemea kupata kipato chao kupitia sekta hiyo.

 

Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) limetoa Dola za Kimarekani 195,000 kwa ajili ya kufanya mapitio na kuandaa Mpango huo Kabambe wa sekta ya uvuvi ili sekta hiyo iweze kusimamiwa vizuri na kuendelea kuleta maendeleo yenye tija nchini.

 

Uandaaji wa mpango huo ni sehemu ya mipango mingi ambayo serikali imekusudia kuitekeleza, wakati akifungua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Novemba 13, 2020 jijini Dodoma, Mhe. Rais, Dkt. John Joseph Magufuli alieleza mipango kadhaa ya kuboresha sekta ya uvuvi ikiwemo ununuzi wa meli nane (8), ujenzi wa Bandari kubwa ya uvuvi itakayotoa ajira elfu thelathini (30,000).

PROF. OLE GABRIEL AWAFUNDA WASOMI HOMBOLO

Na Mbaraka Kambona,

 

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel amewaeleza wanafunzi wa Chuo cha Serikali za Mitaa- Hombolo kuwa wao ni Viongozi watarajiwa hivyo wanawajibu wa kuhakikisha watakapokuwa viongozi wanakidhi matarajio ya wale watakaokuja kuwaongoza.

 

Prof. Gabriel aliyasema hayo wakati akiwasilisha mada iliyohusu nafasi ya viongozi wa kuchaguliwa katika kuleta maendeleo kwa jamii anayoiongoza kwenye hafla ya kuwatunuku zawadi wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao na wafanyakazi bora wa chuo cha Hombolo iliyofanyika katika chuo hicho kilichopo Dodoma Novemba 25, 2020.

 

Alisema kuwa katika kipindi hiki ambacho nchi ya Tanzania imeingia katika uchumi wa kati viongozi wanawajibu mkubwa wa kuhakikisha kwamba wanakidhi matarajio ya Watanzania.

 

Prof. Gabriel aliongeza kuwa nchi nyingi na taasisi zimekuwa zikikwama kufikia malengo tarajiwa kwa sababu ya kukosa usimamizi mzuri.

 

“Kuwa na rasilimali ni jambo moja, lakini kusimamia rasilimali hizo ni jambo la muhimu zaidi, taasisi nyingi zimekwama kwa kushindwa kusimamia rasilimali zake ikiwemo rasilimali watu, rasilimali fedha na rasilimali miundombinu,” alisema Prof. Gabriel

 

Kwa mantiki hiyo aliupongeza Uongozi wa Chuo cha Hombolo kwa kusimamia agenda ya uongozi huku akisema kuwa elimu hiyo wanayoitoa kwa wanafunzi wa chuo hicho itawasaidia wanafunzi hapo mbeleni watakapokuwa viongozi.

 

Aliendelea kusema kuwa kiongozi yeyote wa kuchaguliwa au kuteuliwa ili awe kiongozi bora ni muhimu kuzingatia mambo matatu ambayo ni kufahamu hasa anaowaongoza wanamahitaji gani? pia Kiongozi atambue kuwa hatakumbukwa kwa cheo chake bali kwa mchango wake kwa jamii ile anayoiongoza na tatu, awe mtu anayewashirikisha wale anaowaongoza katika kutatua changamoto zao.

“Washirikishe wale unaowaongoza na ndipo utakapoweza kutatua changamoto, kiongozi mzuri ni yule anayeziona changamoto na kuzibadilisha kuwa fursa, na kwa kufanya hivyo ndipo utaweza kukidhi matarajio ya wale unaowaongoza,”alisisitiza Prof. Gabriel

 

Katika hafla hiyo ya kumi na mbili (12) ya chuo hicho, Prof. Elisante Ole Gabriel alikuwa Mtoa mada maalum na aliwasilisha mada hiyo ya nafasi ya viongozi wa kuchaguliwa na wakuteuliwa katika kuleta maendeleo kwa jamii ili kuwakumbusha wajibu wao mkubwa kwa jamii.

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia), akifurahia jambo alipokuwa akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anayeshughulikia Elimu, Gerald Mweli (kushoto)  walipokutana kwenye Hafla ya Kutunukiwa zawadi wafanyakazi na wanafunzi wa Chuo cha Serikali za Mitaa- Hombolo waliofanya vizuri katika masomo.  Prof. Elisante Ole Gabriel alikuwa Mtoa mada maalum katika hafla hiyo iliyofanyika katika chuo hicho kilichopo Dodoma. (25.11.2020)

Sehemu ya Wanafunzi na Wafanyakazi wa Chuo cha Serikali za Mitaa - Hombolo waliohudhuria hafla ya kutunukiwa zawadi wafanyakazi na wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo iliyofanyika katika chuo hicho kilichopo Dodoma. (25.11.2020)

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akiwasalimia Wanafunzi na Wafanyakazi wa Chuo cha Serikali za Mitaa- Hombolo (hawapo pichani) alipokuwa akitambulishwa katika hafla ya kutunukiwa zawadi wafanyakazi na wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo iliyofanyika katika chuo hicho kilichopo Dodoma. (25.11.2020)

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akiwasilisha mada katika hafla ya kutunukiwa zawadi Wafanyakazi na Wanafunzi waliofanya vizuri wa Chuo cha Serikali za Mitaa-Hombolo iliyofanyika katika chuo hicho kilichopo Dodoma. (25.11.2020)





BARAZA LA VETERINARI LAKIFUNGIA KITUO CHA AFYA SENDEU

Baraza la Veterinari Tanzania limekifungia kituo cha huduma ya afya ya wanyama cha Sendeu kilichopo Wilayani Longido, Mkoani Arusha kwa kubainika kutokuwa na wataalam waliosajiliwa na Baraza hilo.

 

Baraza limefikia hatua hiyo mkoani humo Novemba 22, 2020 kufuatia ukaguzi unaoendelea kufanywa katika mikoa mbalimbali nchini na wakaguzi wa baraza hilo ikiwa ni sehemu ya majukumu yao ya kila siku. 

 

Msajili wa Baraza Veterinari Tanzania, Dkt. Bedan Masuruli alieleza kuhusu uamuzi huo wa baraza ofisini kwake, jijini Dodoma Novemba 23, 2020.

 

Dkt. Masuruli alisema kuwa uamuzi huo wa baraza umefikiwa baada ya kujiridhisha kuwa kituo hicho cha afya ya wanyama kinaendesha shughuli zake kinyume cha taratibu.

 

Aliongeza kuwa wakaguzi wa baraza walipoenda kufanya ukaguzi katika kituo hicho walibaini mapungufu hayo ambayo kimsingi ni kinyume cha taratibu na ni hatari kwa afya ya wanyama.

 

 Aidha, Dkt. Masuruli aliwahimiza wamiliki wote wa vituo vya afya ya mifugo kuhakikisha kuwa vituo hivyo vinasimamiwa kikamilifu na huduma zinazotolewa na wataalam wa mifugo waliosajiliwa na baraza la veterinari Tanzania.

 

Dkt. Masuruli amevisisitiza vituo vingine vyote nchini kuzingatia taratibu zote za kutoa huduma, na baraza halitasita kuchukua hatua kwa vituo vyote vitakavyoshindwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utoaji huduma ya afya ya wanyama.

 

Awali msajili wa Baraza hilo alisema walifanya ukaguzi kwenye mikoa ya Tanga, Shinyanga, Simiyu na Ruvuma na kubaini changamoto za ukiukwaji wa maadili ya utoaji huduma ya afya ya wanyama na kupelekea kulipishwa   faini na wengine kufungiwa kutoa huduma ya afya ya wanyama.



JINSI YA "KU-SUBSCRIBE" MIFUGOUVUVI ONLINE TV

 


WADAU WA UVUVI WAKUTANA KUPITIA MPANGO KAZI UVUVI MDOGO

 Na Mbaraka Kambona,


Wadau wa Sekta ya Uvuvi kutoka maeneo mbalimbali wamekutana kujadili na kupitisha rasimu ya mpango wa kitaifa wa kutekeleza mwongozo wa hiari wa kuhakikisha uvuvi mdogo unakuwa endelevu nchini.


Akiongea wakati akifungua kikao kazi cha kupitia mpango huo wa kitaifa kilichofanyika jijini Dodoma Novemba 21, 2020, Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Emmanuel Bulayi alisema sekta ya uvuvi inatoa ajira ya moja kwa moja kwa wavuvi wadogo wapatao 202,053 na zaidi ya wananchi milioni 4.5 wanategemea shughuli zinazohusiana na uvuvi ikiwemo uchakataji na biashara ya samaki na mazao mengine.


Aliongeza kuwa pamoja na hali hiyo bado wananchi wengi wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi ni masikini huku akisema kuwa hali hiyo haikubaliki na ni kinyume na maelekezo ya sera na miongozo mbalimbali ya maendeleo ya kitaifa ya nchi yetu ikiwemo Sera ya Uvuvi ya mwaka 2015.


Bulayi aliendelea kueleza kuwa Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kutatua changamoto zinazowakabili wavuvi ikiwemo uandaaji wa mpango wa kitaifa wa kutekeleza mwongozo wa hiari wa kuhakikisha uvuvi mdogo unakuwa endelevu.

Alisema mwongozo huo umeibua na kutoa njia ambazo zikitumika kikamilifu hali ya kiuchumi na kijamii ya wavuvi wadogo itaboreka kwa kiasi kikubwa huku rasilimali za uvuvi zikiendelea kuvunwa kwa njia endelevu.


“Usimamizi thabiti wa mwongozo huu unaweza kupelekea kuongezeka kwa ajira, kipato, chakula na lishe na hivyo wavuvi wengi kujikwamua katika umasikini uliopitiliza,”alisema Bulayi


“Nichukue fursa hii kulishukuru sana Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa kuandaa na kusimamia utekelezaji wa Mwongozo wa Hiari na kuhakikisha uvuvi mdogo unakuwa endelevu katika muktadha wa chakula na kuondoa umasikini,” aliongez Bulayi

Aidha, alisema pamoja na mwongozo huo kuwa umepangiliwa vizuri, kama utekelezaji wake hautasimamiwa ipasavyo, hautaweza kutoa tija inayotarajiwa na kwa kutambua hilo Wizara iliunda Kikosi Kazi cha Kitaifa mwaka 2018 ili kusimamia utekelezaji wa mwongozo huo.


Naye Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Dkt. Oliver Mkumbo alisema umuhimu wa mpango kazi kwa nchi ya Tanzania uko wazi ukizingatia sekta ya uvuvi inategemewa na watu wengi kwa shughuli mbalimbali za kujipatia kipato na lishe.


“Tunatambua juhudu za Serikali, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zinazotekeleza mpango huu, tunaipongeza serikali na wadau kwa kuona umuhimu wa mpango huu na ni matumaini yangu utasaidia kuleta maendeleo kwa wavuvi na jamii kwa ujumla,” alisema Mkumbo


 Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la kusimamia mazingira nchini (EMEDO), Elitrudith Lukanga aliishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa mpango huo na alitoa wito kwa mashirika mengine kuhakikisha wanashiriki vyema katika mchakato wa utekelezaji wa mpango huo.


“Sisi kama sehemu ya wadau wa utekelezaji wa mpango huu tutashiriki kikamilifu katika kuhamasisha wadau mbalimbali hususani Wanawake kuuelewa mpango huu ili uwe sehemu katika shughuli zao za kila siku,” alisema Lukanga.

Sehemu ya Wadau wa uvuvi wakisikiliza kwa makini hotuba ya Mgeni rasmi katika warsha ya kupitisha rasimu ya mpango wa Kitaifa wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Kuhakikisha Uvuvi Mdogo Unakuwa Endelevu nchini iliyofanyika jijini Dodoma. (21.11.2020)

Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Emmanuel Bulayi akiongea na wadau wa uvuvi (hawapo pichani) wakati akifungua warsha ya kupitisha rasimu ya Mpango wa Kitaifa wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Kuhakikisha Uvuvi Mdogo Unakuwa Endelevu nchini iliyofanyika jijini Dodoma. (21.11.2020)

Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Uvuvi, Stephen Lukanga akiongea na wadau walioshiriki warsha ya kupitia rasimu ya Mpango wa Kitaifa wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Kuhakikisha Uvuvi Mdogo Unakuwa Endelevu nchini iliyofanyika jijini Dodom. (21.11.2020)

Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Kitaifa, Mpango wa Kitaifa wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa kuhakikisha Uvuvi Mdogo Unakuwa Endelevu, Alhaj, Yahya Mgawe akieleza jambo katika warsha ya kupitisha rasimu ya Mpango wa Kitaifa wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Kuhakikisha Uvuvi Mdogo Unakuwa Endelevu nchini iliyofanyika jijiji Dodoma. (21.11.2020)


Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Uvuvi), Emmanuel Bulayi (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wadau walioshiriki warsha ya kupitisha rasimu ya Mpango wa Kitaifa wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Kuhakikisha Uvuvi Mdogo Unakuwa Endelevu nchini iliyofanyika jijini Dodoma. Kutoka kulia ni Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Uratibu wa Sekta kutoka TAMISEMI, Dismas Teti, wapili kutoka kulia ni Mkurugenzi, Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji, Nazael Madala na watatu kutoka kulia ni Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Uvuvi, Stephen Lukanga. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Uvuvi, Merisia Sebastian, wapili kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa kikosi Kazi cha Kitaifa, Mpango wa Kitaifa wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Kuhakikisha Uvuvi Mdogo Unakuwa Endelevu, Alhaj, Yahya Mgawe na watatu kutoka kushoto ni Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Dkt. Oliver Mkumbo. (21.11.2020)


Jumamosi, 21 Novemba 2020

MRADI WA SWIOFISH WASHIRIKISHA WANANCHI KULINDA RASILIMALI ZA UVUVI NCHINI

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah amesema Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi Mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) umewezesha uboreshaji wa miundombinu ya taasisi za wizara hiyo katika kuhakikisha serikali kwa kushirikiana na wananchi inalinda rasilimali za uvuvi katika Ukanda wa Bahari ya Hindi.

 

Akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwafahamisha manufaa ya mradi wa SWIOFish, Dkt Tamatamah amesema mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia umewanufaisha pia wavuvi wa Pwani ya Bahari ya hindi, wakulima wa Mwani, wafugaji wa viumbe maji na wachakataji wa mazao ya uvuvi wakiwemo wanawake na jamii inayozunguka maeneo hayo.

 

“Lengo kuu la mradi huu ni kuimarisha usimamizi madhubuti wa uvuvi katika ngazi ya kijamii, kitaifa na kimataifa na malengo mengine ni kujenga uwezo wa nchi katika kusimamia rasilimali za uvuvi, kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika ulinzi wa rasilimali za uvuvi wa Bahari kuu, kuinua uchumi wa jamii ya watu wa Pwani na kuinua pato la taifa kutokana na rasilimali za uvuvi,” Amesema Dkt. Tamatamah.

 

Aidha, Dkt. Tamatamah amesema tangu mradi huo uingie hapa nchini mwezi Juni mwaka 2015 ambapo unatarajia kukamilika mwezi Septemba mwaka 2021 uvuvi haramu wa kutumia baruti na mabomu umedhibitiwa kwa asilimia 100 kutokana na kuimarishwa kwa doria pamoja na kuongezeka kwa uelewa wa jamii ya Pwani kuhusu madhara ya uvuvi haramu.

 

Pia, amesema usajili wa vyombo vya uvuvi umeongezeka hadi kufikia asilimia 58 kutoka asilimia 25 ya awali kabla ya mradi kutokana na usimamizi wa utekelezwaji wa sheria na kanuni za uvuvi. Mradi umewezesha tafiti mbalimbali ambapo matokeo yake yametumika kurekebisha baadhi ya kanuni za uvuvi ambazo zimesaidia kuongezeka kwa samaki wanaovuliwa pamoja na kuongezeka kwa uvuvi wa karibu wa kutumia ndoano kwa maeneo mengi.

 

“Mafanikio mengine ya Mradi wa SWIOFish ni pamoja na kuongezeka kwa mapato yatokanayo na uvuvi hususan kwenye halmashauri ambapo Halmashauri ya Pangani yameongezeka kutoka milioni 55 mwaka 2016/17 hadi kufikia Milioni 235 mwaka 2018/19,” Amebainisha Dkt. Tamatamah. 

 

Katika kikao hicho na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah ametumia muda huo kuelezea pia namna mradi wa SWIOFish ulivyoimarisha Sekta ya Uvuvi kwa kufadhili mafunzo ya uvuvi endelevu ambayo yamesaidia baadhi ya wavuvi kutekeleza kwa hiari usimamizi wa rasilimali za bahari.

 

Ameongeza kuwa mradi umeanzisha vikundi hamsini vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) katika Wilaya tano za mfano na kuimarisha utunzaji wa mazingira ya Pwani, viwango vya dagaa pamoja na Mwani vimeandaliwa na kupitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

 

Katibu mkuu huyo pia amesema mradi umewezesha ujenzi wa maabara ya utafiti iliyoko Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) jijini Dar es Salaaam, ujenzi wa nyumba tatu za watumishi wa Kitengo cha Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU), kituo cha Tanga Silikanti kilichopo Kigombe, wilayani Muheza, na ujenzi wa ofisi tano za BMU katika Wilaya za Mkinga (Zingibari), Pangani (Kipumbwi), Chalinze (Saadani), Bagamoyo (Dunda) na Lindi vijijini (Sudi).

 

Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa SWIOFish Tanzania Bara, Bw. Nichrous Mlalila amesema licha ya mafanikio ya mradi changamoto mbalimbali zimekuwa zikijitokeza zikiwemo za ugumu wa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli za kila siku za BMU, kutokea kwa baadhi ya matukio ya uvuvi haramu wa kutumia nyavu zisizofaa kisheria na upatikanaji wa takwimu sahihi katika mifumo ya ukusanyaji taarifa.

 

Bw. Mlalila amesema hadi sasa asilimia 65 ya shughuli za mradi zimetekelezwa na kukamilika, ambapo asilimia nane (8) zipo katika utekelezaji kwa zaidi ya asilimia 75, asilimai 19 ya shughuli za mradi zinaendelea kutekelezwa kati ya asilimia 25 hadi 75 ya utekelezaji. Asilimia nne (4) zipo katika utekelezaji wa asilimia chini ya 25.

 

Ameongeza kuwa mradi unaonyesha matokeo chanya na upo katika mwelekeo mzuri wa utekelezaji.

 

Akizungumza kwa niaba ya wahariri wa vyombo vya habari waliohudhuria kikao hicho Kaimu Mhariri Mkuu wa gazeti la Habari Leo Bw. Mgaya Kingoba ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sekta ya Uvuvi kwa kuendelea kuwapatia taarifa mbalimbali na elimu juu ya sekta hiyo ambazo zinawasaidia kutoa taarifa sahihi kwa umma. 

 

Pia, amewaomba wahahriri wenzake kuendelea kuiunga mkono wizara hiyo katika kuhakikisha inatoa taarifa ambazo zitasaidia kulinda rasilimali za uvuvi pamoja na kupambana na uvuvi haramu katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

 

Mradi wa SWIOFish unatekelezwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA) na Kitengo cha Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) katika maeneo ya Pwani ya Tanzania katika wilaya tano za mfano zikiwemo Mkinga, Tanga Jiji, Pangani, Bagamoyo na Lindi Vijijini. Kwa upande wa Zanzibar, Mradi unatekelezwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo, Maliasili na Uvuvi pamoja na Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA).

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akizungumza na Wahariri wa Vyombo mbalimbali vya habari, baada ya kufungua kikao hicho chenye lengo la kuelezea mafanikio ya Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) katika ofisi ndogo za wizara hiyo jijini Dar es Salaam. (20.11.2020)

Mratibu wa Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) Tanzania Bara, Bw. Nichrous Mlalila akiwaelezea wahariri wa vyombo vya habari (hawapo pichani) waliohudhuria kikao hicho kilichokuwa na lengo la kuwaelezea wahariri hao mafanikio ya mradi wa SWIOfish. Kikao hicho kimefanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi jijini Dar es Salaam. (20.11.2020)

Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini wakipata maelezo na kushuhudia namna serikali inavyofuatilia vyombo vya majini vinavyofanya shughuli za uvuvi maeneo ya bahari kuu, wakati wa kikao cha Sekta ya Uvuvi na wahariri wa vyombo vya habari kilichokuwa na lengo la kuwafahamisha mafanikio ya Mradi wa (SWIOFish). Kikao hicho kimefanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi jijini Dar es Salaam. (20.11.2020)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (aliyekaa katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wahariri wa vyombo vya habari nchini, na baadhi ya maafisa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya mradi wa SWIOFish, baada ya kufungua kikao cha Sekta ya Uvuvi na wahariri wa vyombo vya habari kuelezea mafanikio ya mradio huo. Kikao hicho kimefanyika katika ofisi ndogo za wizara hiyo jijini Dar es Salaam. (20.11.2020)


USHIRIKIANO WA BODI YA MAZIWA NA SEKTA BINAFSI KUONGEZA USINDIKAJI WA MAZIWA HAPA NCHINI

Bodi ya Maziwa yasisitiza ushirikiano na sekta binafsi katika kuongeza usindikaji wa maziwa nchini.

 

Hayo yamesemwa na Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa, Bw. Noely Byamungu wakati wa kikao kazi cha kubainisha maeneo ya ushirikishwaji na Sekta Binafsi kilichofanyika jana (20.11.2020) jijini Dar es Salaam.

 

Kikao kazi hicho kililenga kupitia Mpango Mkakati wa miaka mitano 2020/21-2025/26 wa Bodi ya Maziwa na kubainisha namna ya bora ya ushirikishwaji wa sekta binafsi katika utekelezaji wa majukumu ya Bodi.

 

Kikao hicho kilihudhuriwa na Wakurugenzi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Viwanda na Makampuni ya Wasindikaji Maziwa ya UHT nchini kutoka kampuni ya Asas Dairies, Tanga Fresh, Milkcom na Azam Dairies, Wabia wa maendeleo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Mradi wa Wasindikaji wa Maziwa Tanzania (TMPP).

 

Bw. Byamungu alisema kuwa lengo la Bodi ya Maziwa ni kuwezesha viwanda kuongeza uwezo wa kusindika maziwa ambao kwa sasa usindikaji wa maziwa katika viwanda hivyo ni asilimia 23.52.

 

Aidha, Msajili amesema kuwa Bodi ya Maziwa ipo tayari kuunga mkono jitihada za wadau wa Tasnia ya Maziwa kufikia malengo yao ya kuzalisha maziwa kwa kiwango kilichosimikwa.

 

Bw. Byamungu alisema kuwa kikao hicho kitaleta mtazamo wa muda mrefu wa Tasnia ya maziwa katika usindikaji na kutoa ramani ya kuongezeka kwa ushirikishwaji wa wadau, mawasiliano na ushirikiano miongoni mwa sekta binafsi, wabia wa maendeleo na wadau wengine kwenye sekta.

 

"Bodi ya Maziwa iko tayari na ina nia njema ya kufanya kazi pamoja nanyi kufikia malengo ya kuwa sekta endelevu katika uzalishaji, usindikaji na masoko ya maziwa na bidhaa zake nchini" Alisema Bw. Byamungu.

 

Nae Mkurugenzi wa Mradi wa Wasindikaji Tanzania, Bw. Mark Tsoxo amesema wapo tayari kuisaidia Bodi ya Maziwa kutekeleza majukumu yake ya kuongeza usindikaji wa maziwa nchini ili kuimarisha mnyororo mzima wa thamani. Pia ameiomba Bodi ya Maziwa kuendelea kushirikiana na Sekta Binafsi kwa Ukaribu ili kufikia azma iyo.

 

Tasnia ya Maziwa ina mchango mkubwa katika kuhakikisha usalama wa chakula na kupunguza umaskini.

Washiriki wa kikao cha "Stakeholder Engagement Towards Sustainable Dairy Industry in Tanzania" wakiwa kwenye picha ya pamoja katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam. (20.11.2020)

Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa, Bw. Noel Byamungu (wa kwanza kushoto) akisikiliza kwa makini mada zinazowasilishwa na mdau (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi cha kuimarisha mahusiano kati ya Sekta Binafsi na Serikali kilichofanyika jijini Dar. Es Salaam. Kulia ni mwakilishi kutoka Azam Dairies, Bw. Yunus Ibrahim. (20.11.2020)

Mhandisi kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Emmanuel Zakayo (kushoto) akifuatiwa na Mchumi Mkuu kutoka Wizara ya Viwanda, Bi. Genoveva Kilabuko na Mchumi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Francis Makusaro wakati wa kikao kazi cha kuimarisha mahusiano kati ya Sekta Binafsi na Serikali kilichofanyika jijini Dar. Es Salaam. (20.11.2020)

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo na Usalama wa Chakula na Lishe (WMUV), Bw. Gabriel Bura akisikiliza kwa makini mada zinazowasilishwa wakati wa kikao kazi cha kuimarisha mahusiano kati ya Sekta Binafsi na Serikali kilichofanyika jijini Dar es Salaam. (20.11.2020)

Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Tanga Fresh, Bw. Innocent Mushi akisikiliza mada zinazowasilishwa wakati wa kikao cha kuimarisha mahusiano kati ya Sekta Binafsi na Serikali kilichofanyika jijini Dar. Es Salaam. (20.11.2020)

Baadhi ya Wasindikaji wa Maziwa wakiwa kwenye kikao cha kuimarisha mahusiano kati ya Sekta Binafsi na Serikali kilichofanyika jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni Mwakilishi kutoka Milkcom Dairies, Bw. Abubakar Faraji, akifuatiwa na Abdul Ally kutoka ASAS Dairies na wa kwanza kulia ni Mkurugenzi mtendaji kutoka Tangafresh, Innocent Mushi. (20.11.2020)