Nav bar

Jumatatu, 30 Novemba 2020

WAFUGAJI NA WAKULIMA KUNUFAIKA KUPITIA KIWANDA CHA NYAMA NGURU HILLS

Serikali imesema katika kuboresha na kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji katika maeneo mbalimbali nchini ukiwemo Mkoa wa Morogoro, inasisitiza uwepo wa miradi ambayo itakuwa na manufaa makubwa kwa makundi yote mawili.

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema hayo (28.11.2020) katika Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro alipotembelea ujenzi wa mradi wa kiwanda cha nyama katika Ranchi ya Nguru Hills na kubainisha kuwa mradi huo unaotarajia kukamilika mwezi Aprili Mwaka 2021 utakuwa na manufaa makubwa kwa wafugaji na wakazi wa Mkoa wa Morogoro.

 

“Tumekuja kuangalia shughuli zinazoendelea kutokana na kikao ambacho tulikuwa nacho katika ofisi ya katibu tawala wa mkoa na mkuu wa Mkoa wa Morogoro katika kuboresha shughuli za mifugo kwenye mkoa huo na kuondoa changamoto za migogoro ya wafugaji ambapo uongozi wa mkoa waliniambia juu ya mradi huu ambao utakuwa na msaada mkubwa sana kwa wakulima na wafugaji wa mkoa wa Morogoro na nchi kwa ujumla.” Amesema Prof. Gabriel.

 

Prof. Gabriel amebainisha kuwa mradi huo wa kipekee ambao mara baada ya kiwanda hicho kukamilika kitakuwa na uwezo wa kuchinja ng'ombe zaidi ya 200 na mbuzi zaidi ya 1,000 kwa siku, kumejengwa mabwawa makubwa ambayo yatakuwa yanakusanya maji yanayotoka kwenye machinjio, kisha kutibiwa kabla ya kutumika tena kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji.

 

“Mradi huu una jambo mahsusi kuliko mingine, maji haya ya mabwawa yatatumika kwa ajili ya umwagiliaji huu ni moja kati ya miradi ambapo wafugaji na wakulima watanufaika ili wote waone huu mradi ni wa kwao kwa ajili ya uchumi wetu.” Ameongeza Prof. Gabriel.

 

Aidha, amesema mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 25, ambao unashirikisha wabia mbalimbali ukiwemo Mfuko wa Pesheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), ni azma ya serikali katika kuzidi kuboresha mazingira ya uwekezaji hapa nchini kwenye sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Mifugo hivyo kuwataka wafugaji kuboresha mifugo yao kwa kufuga ng’ombe bora wa kisasa na kupitia miradi ya kunenepesha mifugo ili waweze kuuza mifugo yenye ubora katika viwanda vya kusindika mazao ya mifugo hapa nchini ili sekta izidi kukua na kuchangia pato la taifa kupitia uchumi wa viwanda.

 

Pia katibu mkuu huyo amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha Tanzania inakuwa na mifugo mingi na bora kwa kuhakikisha mifugo inaogeshwa ili kujikinga dhidi ya magonjwa na kuwataka wakurugenzi wa halmashauri kote nchini, kuhakikisha maeneo yao yana majosho ya kutosha kwa ajili ya kuogeshea mifugo na kuwataka wayafanyie ukarabati majosho ambayo hayafanyi kazi.

 

“Tufuge kisasa Namibia, Botswana wana ng’ombe wachache lakini wanauza kwa wingi nyama nje ya nchi, ndiyo maana tunaimarisha afya za mifugo, ndiyo maana nchi nzima tunashughulika na masuala ya uogeshaji niwatake wakurugenzi wa halmashauri wahakikishe kwenye maeneo yao kuna majosho ya kutosha na niwatake yale ambayo hayafanyi kazi vizuri yaboreshwe. Ameongeza Prof. Gabriel.

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amelitaka pia Dawati la Sekta Binafsi lililo chini ya wizara hiyo pamoja na Idara ya Uzalishaji na Masoko kwa kushirikiana na PSSSF kukutana haraka ili kujadili changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika mradi wa kiwanda cha nyama Nguru Hills ili mradi huo ukamilike kwa wakati.

 

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Bw. Hassan Chama Hassan amemwambia katibu mkuu huyo kuwa, mradi huo ukikamilika kwa wakati wafugaji watanufaika kwa kuwa wanakabiliana na changamoto ya kuuza mifugo yao kupitia minada ambapo wanakutana na madalali ambao wanafanya bei za mifugo kuwa chini, huku Meneja Ujenzi wa mradi huo kutoka PSSSF Mhandisi Grayson Bambaza akibainisha kuwa wafugaji watakuwa wanauza mifugo yao kwa kilo na siyo kwa kukadiria kulingana na umbo la mfugo.

 

Mradi wa kiwanda cha nyama katika Ranchi ya Nguru Hills unaotarajia kukamilika mwezi Aprili Mwaka 2021, unategemewa kutoa ajira kwa wafanyakazi 120 hadi 200 kulingana na uzalishaji.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel (wa kwanza kushoto) akizungumza na baadhi ya viongozi wa Ranchi ya Nguru Hills juu ya mradi wa kiwanda cha nyama kinachojengwa katika ranchi hiyo huku akiwataka wahakikishe mara baada ya kiwanda hicho kitakapoanza kufanya kazi, kitoe bidhaa bora ili kushindana na soko la kimataifa. Meneja Mkuu wa ranchi hiyo Bw. Paul Phillips (aliyesimama katikati) amemuhakikishia katibu mkuu huyo kuzingatia maelekezo yake. (28.11.2020)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akikagua mabwawa yanayojengwa katika Ranchi ya Nguru Hills, ambayo yatapokea maji yatakayokuwa yanatoka kwenye machinjio na kutibiwa kabla ya kutumika kwenye kilimo cha umwagiliaji. Prof. Gabriel ameambatana na viongozi wa ranchi, viongozi wa halmashauri ya Wilaya ya Mvomero na baadhi ya watumishi kutoka wizarani. (28.11.2020)

Muonekano wa moja ya mabwawa yanayojengwa katika Ranchi ya Nguru Hills, ambayo yatapokea maji yatakayokuwa yanatoka kwenye machinjio na kutibiwa kabla ya kutumika kwenye kilimo cha umwagiliaji. (28.11.2020)

Muonekano wa nje wa ujenzi wa kiwanda cha nyama Nguru Hills kinachotarajiwa kutoa ajira kati ya wafanyakazi 120 hadi 200 kulingana na uzalishaji. (28.11.2020)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akikagua ujenzi wa kiwanda cha nyama Nguru Hills huku akijihakikishia vipimo vilivyobainishwa katika mchoro wa jengo hilo. (28.11.2020)

Muonekano wa moja ya maeneo ya ndani ya kiwanda cha nyama Nguru Hills kitakachokuwa na uwezo wa kuchinja mbuzi zaidi ya 200 na ng’ombe zaidi ya 1,000 kwa siku. (28.11.2020)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa Ranchi ya Nguru Hills viongozi kutoka halmashauri ya Wilaya ya Mvomero na Wizara ya Mifugo na Uvuvi. (28.11.2020)







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni