Nav bar

Jumatano, 31 Oktoba 2018

SERIKALI IPIME MAENEO YA WAFUGAJI ILI WAMILIKISHWE KISHERIA
Wafugaji wa Halimashauri ya Wilaya ya Hai, Mkoani Kilimanjaro wamewalalamikia watendaji wa Serikali na kwamba wao ndio wanao chochea Migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Hai.

Malalamiko hayo yametolewa jana na wafugaji wa kijiji cha Sanya Station, katika kata ya Kia, katika Halmashauri ya Wilaya Hai, walipokuwa wakitoa kero zao kwa Katibu Mkuu Mifugo, Prof.Elisante Ole Gabriel, aliyefika katika kijiji hicho kusikiliza kero za wafugaji hao kwa Niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe .Luhaga Joelson Mpina.

“Sisi Wafugaji na Wakulima natuna tatizo kabisa, Shida kubwa iko kwa hao Mgambo, ambao wanatumwa na watendaji wa Serikali waje wakamate Ngombe wetu bila kosa lolote na kufanya mradi wao wa kuwaingizia fedha;.alisikika Mfugaji akilalamika.

Aidha watumishi waliopo katika taasisi za Umma za NARCO na TALIRI ,West Kilimanjaro nao wamelalamikiwa na wafugaji hao kuwa ni vinara wa kuchukua rushwa hasa Ngombe wa wafugaji wanapokamatwa wakiwa katika maeneo ya Taasisi hizo wakipata Malisho.

Aidha,Wafugaji wa kijiji cha Sanya Station wamemweleza katibu Mkuu kuwa, changamoto kubwa waliyonayo kwa sasa katika kijiji hicho ni pamoja na, uhaba wa maeneo ya Malisho, Mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda wa miaka 30, ambapo mamlaka ya kiwanja cha ndege ya KIA wananataka kuwapora ardhi waliyoridhishwa na Mababu zao ,Eneo halali lenye kubwa wa Hekta Elfu 11, lenye wakazi zaidi ya Elfu ishirini na nne (24,000) katika kata ya Kia.

Changamoto nyingine waliyotaja ni pamoja na ubovu wa miundombinu ya Majosho ,ukosefu wa visima virefu vya kunyweshea Maji Mifugo na kukosekana kwa Mnada katika Eneo hilo.

Kwa upande wake Katibu wa chama cha Wafugaji Taifa Bw. Magembe Makoye, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe John Pombe Magufuli kwa Kuwateua Viongozi waandamizi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ukianzia na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Joelson Mpina, Katibu Mkuu Mifugo, Prof.Elisante Ole Gabriel ambao kwa asili wote ni wafugaji.

Makoye amewaasa Wafugaji kufuata kanuni, Taratibu na sheria za nchi ili waendelee
kuheshimika, kwani wafugaji wanajitosheleza kwa kila kitu ndio maana hawajawahi kuomba chakula Serikalini na wanasomesha watoto wao bila tatizo lolote.

Tunaomba Serikali ipime maeneo ya wafugaji ili wamilikishwe kisheria,  Sasahivi kila hifadhi
imeanzisha Mahabusu ya Mifugo, Ngombe wakikamatwa ndani ya hifadhi anapigwa faini ya
Tsh.100,000/= kwa ngombe mmoja. Hii ni rasimu ya sheria ambayo ilikuja kwa wadau tuliikataa, cha kushangaza watu wa Maliasili wanaitumia, hii ni sheria kandamizi ;alisema.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Hai Bw.Lengai Ole Sabaya amepiga Marufuku kwa watendaji wa Vijiji na Vitongoji kupokea fedha yoyote ya Migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji. Mhe Sabaya amesema kuwa Migogoro mingi inayotokea ni kwa sababu wananchi wa kifugaji hawashirikishwi  katika ngazi za maamuzi.

Akifanya Majumuisho ya Mkutano huo, Katibu Mkuu Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel ameishukuru kamati ya Ulinzi na Usalama ya Halmashauri ya Wilaya ya Hai kwa kutatua Migogoro iliyopo kwa Weledi Mkubwa.

Ole Gabriel amesema kuwa Serikali inatambua haki za Wafugaji,katika nchi hii wafugaji ni
wawekezaji, Lakini ni lazima wafugaji wazingatie sheria, kwani wanamchango mkubwa sana katika Uchumi wa Viwanda.

Rais Magufuli anawapenda wafugaji lakini pia yeye mwenyewe ni Mfugaji, ndio maana katika ilani ya Chama cha Mapinduzi Ibara ya 25 yote inaongelea Wafugaji na namna Bora ya kuweza kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Prof.Gabriel amesema kuwa changamoto mbalimbali walizozieleza Wafugaji hao zinafanyiwa kazi kwani Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Sikivu.

Pia Katibu Mkuu Mifugo aliwakumbusha wafugaji kuachana na kufuga kwa mazoea, amewambia wakati umefika sasa kubadilika na kuanza kufuga Kisasa na Kibiashara.Katibu Mkuu Mifugo na Mbunge wa Siha Dr. Mollel wakifurahia jambo mara baada ya Mzee wa jamii ya kimasai kuja kuwasalimia mara baada ya mkutano kumalizika.

Katibu Mkuu akiongea na wafugaji


Jumatatu, 29 Oktoba 2018

SERIKALI YATEKETEZA NYAVU ZA WAVUVI HARAMU NYUMBA YA MUNGU


Serikali imepiga marufuku uvuvi haramu na kuteketeza nyavu aina ya makokoro 35 , makila 6 na nyavu za zenia 25 zilizokuwa zikitumiwa na wavuvi haramu katika bwawa la Nyumba ya Mungu lililopo Mkoani Kilimanjaro

Naibu Waziri wa mifugo na Uvuvi Abdalah Ulega akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kagongo kata Lang’ata leo amesema serikali haitamwonea huruma mtu yeyote atakayekamatwa akijihusisha na uvuvi haramu kwani serikali imekua ikipoteza kiasi kikubwa cha mapato kutokana na uvuvi huo.

“Hatuna utani na mtu asiye na huruma na rasilimali za nchi hii, Tanzania ndio nchi yenye sehemu kubwa yenye maji kuliko sehemu nyingine lakini bado tunaagiza samaki kutoka nchini china, tumeagiza sato., perege hadi kibua wa kichina, tusipotokomeza leo bwawa litakuwa historia kwa vizazi vijavyo” amesema Ulega

Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira alisema uwepo wa bwawa hilo
umekuwa msaada mkubwa kwa wananchi katika eneo hilo na sasa ni wakati wa wananchi kuwa walinzi kwa kila mmoja ili kutokomeza uvuvi haramu.

“Hebu leo amueni kabisa kwamba biashara ya samaki ndio mfumo wa maisha yenu, Ninyi mkifanya
hivyo sisi hatutahitaji kufunga hili bwawa , wakati wote tutahitaji kuongeza kizazi cha samaki na kuleta wataalamu kupima kiwango cha samaki tulichonacho” alisema Mghwira

Kwa upande wake Dismas Gondwe mkazi wa kijiji cha kigongo kata ya Lang’ata amesema uvuvi haramu katika bwawa hilo unatokana na kukosekana kwa utaratibu maalumu unaowaelekeza wavuvi kuendesha shughuli zao katika bwawa hilo.

Gondwe ameiomba serikali kuwawezesha wavuvi wa bwawa la Nyumba ya Mungu zana harali ambazo serikali inazitambua.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akizungumza na wavuvi wa kijiji cha Kagongo kata ya Langata mkoani Kilimanjaro juu ya serikali kutokumuonea huruma mtu yoyote ambaye anajiusisha na shughuli za uvuvi haramu 
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega (wa kwanza kulia) kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro , Anna Mghwira na  Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Aatron  Mbogho wakiteketeza zana haramu zilizokuwa zikitumika katika uvuvi haramu kwenye Bwawa la Nyumba  ya Mungu.UZINDUZI WA BODI YA KAMPUNI YA RANCHI ZA TAIFA (NARCO)*Bodi ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) imezinduliwa rasmi  tarehe 27/10/2018 na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Joelson Mpina.

Ninawashukuru wote kwa kukubali uteuzi huu kwa sababu natambua hakuna kazi iliyo nyepesi - Waziri Mpina

Namshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uteuzi huu kwani ametambua uwezo na uzalendo wenu, Nchi hii inapaswa kuendelezwa na wananchi wazalendo watakaowezesha Nchi kusonga mbele - Mhe. Mpina

Ni matarajio yangu kuwa; Bodi hii itaweza kufikia Mikakati tuliojiwekea na ndani ya Wiki mbili zijazo lazima kikao cha Bodi kiitishwe ili kuanza utekelezaji wa mikakati tutakayojiwekea - Waziri Mpina

Sekta ya Mifugo ina mchango mkubwa katika ujenzi wa taifa letu ambapo mpaka sasa jumla ya Mifugo tuliyonayo ni mil 57 na tunazalisha Lita Bil 2.4 za Maziwa - Waziri Mpina.

Tunahitaji mpaka mwakani tuongeze idadi kubwa ya Mifugo kwa sasa, tuna Ngombe milioni 30.5, mbuzi 18.8 mil, kondoo Mil. 5.3, nguruwe Mil. 1.9, Kuku wa kienyeji Mil. 38.2, na wa kisasa ni Mil. 36.6.

Mpaka sasa idadi ya mifugo inayouzwa Nje ya Nchi kwa njia haramu na halali ni asilimia 70 na mifugo michache tuliobaki nayo ni asilimia 30 - Waziri Mpina.

 Mazao mengi yanaingia Nchini bila kufuata taratibu na Mifugo inatoroshwa kwakuwa hatuna Viwanda vya uhakika hapa Nchini, tuna viwanda 32 lakini ni machinjio- Waziri Mpina.

Ifike mahali kwenye Taasisi za Serikali ikiwemo na NARCO Kuwe na viwanda vya uhakika Itakuwa ni mfano na kielelezo kwa Sekta binafsi - Waziri Mpina.

 Tumepandisha tozo kuanzia 1000 hadi 10,000 ili kila mmoja aweze kumiliki eneo ambalo anauwezo
nalo - Waziri Mpina.

Shirika lifike mahali linatoa nyama ya ng’ombe ndani na Nje ya Nchi na kutengenza bidhaa zitokananzo na ngozi - Waziri Mpina

Naitaka Bodi na timu nzima  kuhakikisha mnaandaa mpango kazi na wa biashara kwa kushirikiana
na Dawati la Sekta Binafsi - Waziri Mpina

 kwa mashirika yangu yote kabla ya tarehe 30/11/2018 lazima tuandae gawio letu kwa Serikali - Waziri Mpina

Ni lazima kila mmoja afahamu wajibu wake ili tuweze kufikia mafanikio tuliyojipangia - Waziri Mpina

Watendaji wa Wizara yangu mtakuwa na kazi ya kusimamia mikakati tuliojiwekea inatekelezaa hadi
kufikia tarehe 30/11/2018 nipatiwe mikakati hiyo - Waziri Mpina.

Naimani pamoja na magumu haya mageuzi lazima yafanyike “ penye nia Pana njia” - Waziri Mpina.

Bodi inayozinduliwa leo iko kisheria kwa mujibu wa Mashirika ya Umma na. 2 ya mwaka 1992 kifungu cha 9 (1). Natangaza rasmi uzinduzi wa Bodi hii - Waziri Mpina.

 Naamini kuzinduliwa kwa Bodi hii kutaleta mapinduzi Makubwa na ni matumaini tutalinda rasilimali za Nchi yetu - KM Prof Ole Gabriel.

Bodi hii imesheheni wataalam wanaoaminika,tunaamini wataenda kuondoa changamoto mbalimbali
zinazolikabili shirika hili - Katibu Mkuu, Prof Ole Gabriel.

Tanzania ni Nchi ya 2 kuwa na ng’ombe wengi lakini hatufanyi vizuri kwenye eneo hili ila naimani
wajumbe hawa watafanya kazi ambayo wameiandaa kuifanya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Kilimo, Mifugo, na Maji, Mhe. M. Mgimwa.

 Tunataka mwakani tuwe na idadi kubwa ya ng’ombe ambapo tukijidhatiti kukuza Ranchi zetu na
kuhusisha Sekta binafsi tunauwezo wa kupata wadau nje na ndani ya Nchi. - Mhe M. Mgimwa .

Namshkuru Rais Dkt. Magufuli kwa uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi hii, kwani najua umezingatia mengi pamoja na utendaji wako wa kazi na uzoefu wa kuitumikia nchi ya Tanzania pia tunaamini ni chaguo sahihi kwa wakati sahihi - Katibu Mkuu Mifugo Prof. Ole Gabriel.

Namshukuru Mhe. Rais kwa kuniteua naahidi mimi na wajumbe tuna uwezo wa kuifanya kazi hii -
Mwenyekiti wa Bw. Bodi Paul Kimiti.

Tutajenga timu ya kufanya kazi kwani uzoefu uliopo katika vichwa vya wajumbe hawa utakua ni
rasilimali ya kubwa katika utendaji wetu - Mwenyekiti wa Bodi Bw. Paul Kimiti

Tayari tumeanza kuweka malengo na mikakati ya utendaji kazi itakayorudisha imani ya shirika la
NARCO - Mwenyekiti wa Bodi Bw. Paul Kimiti.
Mhe Waziri akimpongeza  Mwenyekiti wa Bodi ya NARCO Bw. Paul Kimiti baada ya kuteuliwa na Mhe. Raisi.

Mhe. Waziri akisalimiana na Katibu Mkuu Mifugo

Picha ya pamoja Mhe. Waziri akiwa na Bodi ya NARCO iliyoteuliwa, Waheshimiwa Wabunge, Wakurugenzi na Watumishi wa Baraza wakati wa uzinduzi wa Bodi , Jijini Dodoma.

Alhamisi, 25 Oktoba 2018

KATIBU MKUU MIFUGO, PROFESA ELISANTE OLE GABRIEL AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA OMAN MHE. ALI A. AL MAHRUQI NCHINI TANZANIA JUU YA KUTAFUTA SOKO LA NYAMA NCHINI OMAN.Katibu Mkuu ( mwenye suti nyeusi ) na Balozi wa Oman wakiwa kwenye picha ya pamoja na maafisa kutoka Wizara ya mambo ya nje na wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Katibu Mkuu Mifugo, Profesa Elisante Ole Gabriel akisema jambo kwenye kikao kifupi mapema leo  jijini Dar es salaam.
Katibu Mkuu Profesa Elisante Ole Gabriel akijadili jambo na Balozi wa Oman Mhe. Ali A. Al Mahruqi mapema leo jijini Dar es salaam.

Jumatatu, 15 Oktoba 2018

KATIBU MKUU MIFUGO AFANYA UKAGUZI MINADA YA SHANWA MASWA NA MWANUZI MEATU
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof.Elisante Ole Gabriel leo amefanya ukaguzi mnada ya Awali wa Shanwa uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa na Mwanuzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu.

Akiongea na Katibu Mkuu, Dkt. Gabriel Bura kutoka Wizarani ambaye pia ni mmoja wa timu Nzagamba, Dkt. Bura,amemweleza Katibu Mkuu kuwa tangu wamewasili hapo, kazi zinaenda vizuri bila shida yoyote.

Katibu Mkuu tangu timu Nzagamba imeanza kutekeleza majumu yake,katika mnada wa Senai timu ilifanikiwa kukusanya jumla ya Tsh.7,028,000/= ukilinganisha na Tsh.756,000/= zilizokuwa zinakusanywa kabla ya Nzagamba kuanza kutekeleza Majukumu yake. alisema.

Aidha Bura amesema kuwa wafanyabiashara wameanza kuelewa mabadiliko ya tozo mpya,isipokuwa bado kuna changamoto chache, baadhi ya wafanyabiashara wanafanya biashara nje Minada kinyume cha sheria ili kukwepa kwa Makusudi kulipa tozo zilizowekwe kisheria.

Wakati huo huo baadhi ya wafugaji waliokuwepo katika mnada wa Shanwa Maswa walitoa baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni pamoja na kupigwa faini pale Ngombe wanapofika pungufu katika mnada wa Kizota au Pugu hata kama atakuwa amekufa njiani kwa kukanyagwa na wenzake.

Akijibu baadhi ya changamoto zilizotolewa na wafugaji na Wafanyabiashara hao, Katibu Mkuu Mifugo Prof. Ole Gabriel aliwambia wafugaji/Wafanyabiashara hao kuwa ni vyema kufuata taratibu na kanuni zilizowekwa kwa mujibu wa sheria ili waweze kufanya biashara zao za mifugo bila bugudha yoyote.

Katika hatua nyingine Dkt. Benezeth Lutege akiwa katika Mnada wa awali wa Mwanuzi Halmashauri ya Wilaya ya Meatu,amemwambia Katibu Mkuu kuwa zoezi la ukusanyaji ushuru kwa kutumia tozo mpya liliingia dosari baada ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kugoma kukusanya ushuru huo kwa kutumia tozo mpya kwa kisingizio cha kutokupata Taarifa hizo Mapema.

Mkuu nililazimika kutumia nguvu kuwatangazia wafugaji na Wafanyabiashara kuwa wanatakiwa kulipa viwango vipya vya tozo vilivyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwaka huu wa fedha na sio vya Mwaka jana. ;alisema.

Katibu Mkuu akimsikiliza kwa makini Bw. Adam Noti, Afisa Mifugo katika Halmashauri ya Wilaya ya MASWA (Aliyenyoosha mkono)

Katibu Mkuu akiwa na badhi ya Wafugaji na wafanyabiashara wa Mifugo katika Mnada wa Shanwa Halmashauri ya Wilaya ya MASWA.

Katibu Mkuu Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika Mnada wa Shanwa katika Halmashauri ya Wilaya ya MASWA

Katibu Mkuu akiongea na baadhi ya wafanyabiashara waliopanga foleni wakisubiri kulipia tozo mbalimbali.


ULEGA AFUNGUA RASMI MAONESHO YA NNE YA NDEGE WAFUGWAO
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Mbunge wa Mkuranga Abdallah Ulega amezindua rasmi maonesho ya nne ya ndege wafugwao katika viwanja vya maonesho (sabasaba) jijini Dar es salaam.


Akizungumza katika uzinduzi huo Ulega ameeleza kuwa maonesho ya mwaka huu yamehusisha makampuni mengi ya ndani na nje ya nchi kama Kenya, Poland na China na amewakaribisha kuwekeza nchini kutokana na kuwepo kwa fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali.


Aidha ametoa pongezi kwa vyama vyote vya wadau wa ndege wafugwao chini ya chama mama cha Tanzania Poultry show (TPS) kwa kutoa kipaumbele katika suala la ufugaji wa kuku.


Pia amewataka kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja na wao kama serikali wapo pamoja kama walezi wao, katika kuhakikisha wanasonga mbele zaidi na amewapongeza kwa ushirikiano wao kupitia vyama vyao.


Ulega amesema kuwa Rais Magufuli ameendelea kusimamia maendeleo ambapo hadi sasa tozo zilizokuwa kero kwa wafugaji, wakulima na wavuvi zimeondolewa ili kuweza kuendeleza shughuli hizo.


 Kuhusiana na changamoto zilizotolewa na wafugaji hao hasa katika mashudu na soya ambazo huagizwa kutoka nje Ulega amesema kuwa maandalizi yameanza katika nyanda za juu kusini ambako soya zimelimwa na wanavutia uwekezaji katika usindikaji ili kuweza kuvutia uwekezaji wa kuchakata soya na kupunguza gharama za kuagiza bidhaa hizo kutoka nje.


Kuhusiana na machinjio zinazochinja kuku Ulega amesema kuwa sehemu hizo zimekuwa na ubora wa chini sana na amewataka wahakikishe wanaboresha machinjio hayo yanayosimamiwa na halmashauri na manispaa hasa kwa kuzingatia wanaweka  sehemu ya machinjio ya kuku ili kuleta thamani.


Mwenyekiti wa chama cha ndege wafugwao Harko Bhaghat amemshukuru Naibu Waziri na Wizara kwa ujumla kwa kutoa kipaumbele kwa wafugaji na kusema kuwa hadi sasa wamepata mafanikio makubwa na kubwa zaidi ni baada ya serikali kuondoa tozo katika bidhaa za mifugo.


Bhaghati amewataka wafugaji kujisajili ili waweze kupata fursa mbalimbali za kuendeleza soko la ndege wafugwao hasa kuku.


Mtaalamu na Mshauri wa Mifugo kutoka kampuni ya Hill Poultry Feed akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega kuhusu uzalishaji na utunzaji wa mifugo unaofanywa

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi ,Abdallah Ulega akizungumza na wafugaji wa ndege wafugwao katika ufunguzi wa maonesho ya nne ya ndege wafugwao nchini jijini  Dar es salaam.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akitembelea mabanda mbalimbali katika viwanja vya sabasaba jijini Dar es salaam