Ijumaa, 30 Septemba 2022
WAWEKEZAJI WASIOLIPA KODI, KUFUGA KISASA TUTAWAONDOA-NZUNDA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya Mifugo Bw. Tixon Nzunda amesema kuwa Serikali itawaondoa kwenye ranchi zake wawekezaji wote wasiofuga kisasa au kulipa kodi ya vitalu walivyokodishwa.
Nzunda amesema hayo leo (28.09.2022) mara baada ya kufika na kukagua baadhi ya vitalu vilivyopo kwenye ranchi ya Mkata iliyopo Mkoani Morogoro ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kuzitembelea ranchi zilizopo chini ya Kampuni ya ranchi za Taifa (NARCO).
“Serikali haitaruhusu ufugaji huu wa kienyeji ndani ya ranchi zake kwa sababu tunataka kuwa na ranchi zinazofanana na ranchi na kwa maneno mengine tungependa kuona wapangaji wetu waliopo kwenye ranchi zetu zote nchini wanakuja na mpango wa kufuga kisasa na kwa kuzingatia mipango ya biashara waliyonayo na kama hamuwezi kuzingatia mipango hiyo tutaomba mtupishe ili tubaki na wale wenye nia ya kufuga kisasa” Amesisitiza Nzunda.
Nzunda ameongeza kuwa kwa muda mrefu Tanzania imekuwa hainufaiki na rasilimali ya mifugo iliyopo nchini kutokana na kutofuata njia za ufugaji wa kisasa hivyo dhamira ya Wizara yake kupitia Sekta ya Mifugo ni kuhakikisha inaunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuhakikisha sekta ya Mifugo inatoa mchango wa kutosha kwa mfugaji mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Nzunda ametoa muda wa mwezi mmoja kuanzia leo kuhakikisha wawekezaji wote waliokodishwa vitalu kwenye ranchi za Taifa wanalipa madeni ya kodi wanazodaiwa ambapo amesisitiza kuwa watakaoshindwa kufanya hivyo wataondolewa.
“Wawekezaji wamelalamika hapa kuwa sababu ya kutolipa kodi hiyo ni ukubwa wa kodi kutoka shilingi 1,500 kwa ekari waliyokuwa wakilipa mwanzoni hadi 7,500 iliyoongezeka tangu mwaka 2018 hivyo niwaagize NARCO waende wakarekebishe hilo na wadaiwa wote walipe shilingi 3,500 kwa kila ekari waliyokuwa wamependekeza afu baada ya hapo tufanye tathmini kwa ambao hawatalipa ndani ya mwezi mmoja kuanzia leo tuwaondoe” Ameongeza Nzunda.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ranchi za Taifa (NARCO) Prof. Peter Msoffe mbali na kukiri kupokea maelekezo hayo, ameahidi kuyawasilisha kwenye Bodi ya kampuni hiyo ili waweze kufanya tathmini ya madeni ya kila mwekezaji kwa kiwango kilichoelekezwa ndipo waanze kulipa.
Mbali na kutembelea baadhi ya vitalu vilivyopo kwenye ranchi ya Mkata, Nzunda amefanya kikao na baadhi ya wawekezaji waliopo kwenye ranchi hiyo ambapo amewasisitiza kufanya shughuli zao kwa kufuata miongozo inayotolewa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Tixon Nzunda (kushoto) akitoa maelekezo ya namna ya kujenga birika la kunyweshea mifugo kwenye moja ya mabwawa yaliyochimbwa na wakandarasi wa mradi wa treni za mwendokasi ndani ya ranchi ya Mkata iliyopo Mkoani Morogoro leo (28.09.2022). Katikati ni Mkurugenzi Mkuu wa Ranchi za Taifa (NARCO), Prof. Peter Msoffe na katikati ni Meneja wa Ranchi ya Mkata Bw. Oscar Mengele.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Prof. Peter Msoffe (kushoto) akimkagua mmoja wa mbuzi waliopo kwenye ranchi ya Mkata wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Tixon Nzunda (kulia) iliyofanyika kwenye ranchi hiyo leo (28.09.2022) mkoani Morogoro.
PROGRAMU YA SAUTI KULETA MABADILIKO KWENYE SEKTA YA MIFUGO
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema kuwa Programu ya Samia Ufugaji kwa Tija (SAUTI) inakwenda kuleta mabadiliko makubwa kwenye Sekta ya Mifugo.
Waziri
Ndaki ameyasema hayo leo (28.09.2022) wakati anazungumza na vijana
waliochaguliwa kujiunga kwenye vituo atamizi kwa ajili ya mafunzo ya
unenepeshaji mifugo katika Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Kanda ya Mashariki na
Chuo cha Mafunzo ya Mifugo (LITA) – Buhuri.
Programu
ya SAUTI lengo lake ni kuanza kubadilisha fikra za vijana ili waweze kufuga
kisasa na kibiashara na kuona kuwa ufugaji unaweza kuwaletea maendeleo makubwa
kiuchumi. Aidha, Waziri Ndaki amemshukuru Rais Samia kwa kuiwezesha Wizara
kutekeleza Programu hiyo yenye kuleta mabadiliko makubwa katika Sekta ya Mifugo.
Akiwa
katika kituo cha TALIRI Kanda ya Mashariki, Waziri Ndaki amewataka watafiti
kuhakikisha matokeo ya tafiti wanazozifanya zinawafikia wafugaji ili kuweza
kuwabadilisha na kuwafanya waanze kufuga kisasa na kibiashara.
Aidha,
baada ya kutembelea vitalu vya majani ambayo tayari yameshafanyiwa utafiti,
amewasihi wafugaji kutembelea vituo vya utafiti wa mifugo kwa lengo la
kujifunza shughuli mbalimbali za ufugaji ikiwemo ya kilimo cha malisho. Lakini
pia amewasihi wafugaji kuanza kulima malisho na kuyahifadhi ili yaweze
kuwasaidia wakati wa kipindi cha ukame.
Naye
Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya
Mashariki, Dkt. Zabron Nziku amesema kuwa TALIRI imekuwa ikifanya tafiti nyingi
kwa lengo la kuhakikisha Sekta ya Mifugo inakua na wafugaji wananufaika
kiuchumi.
Akizungumza
kwa niaba ya vijana waliochaguliwa, Bi. Magesa ambaye ni mshiriki wa mafunzo
kutoka wilayani Muheza mkoani Tanga ameishukuru serikali kwa kuanzisha vituo
atamizi kwa kuwa vitawasaidia kupata elimu ya ufugaji kwa vitendo na hivyo
kuwawezesha kufuga kisasa na kwa tija.
ULEGA ATAKA VIJANA WAWEZESHWE KUJIAJIRI SEKTA YA UVUVI
Na Mbaraka Kambona,
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi una fursa nyingi za kiuchumi hivyo ni muhimu vijana kufundishwa namna ya kutumia fursa hizo kujiajiri ili kujiongezea kipato.
Naibu Waziri Ulega alitoa kauli hiyo wakati akiongea na Uongozi wa Shirikisho la Kimataifa linaloshughulika na programu ya uendelezaji wa pwani na uvuvi wa bahari (IUCN) walipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam Septemba 28, 2022.
Alisema kuwa katika ukanda wa pwani wa bahari kuanzia Moa mpaka Msimbati kuna fursa nyingi za ukuzaji viumbe maji ikiwemo ukulima wa mwani, ufugaji majongoo bahari na kaa na tayari kuna jitihada mbalimbali zimeshaanza kuchukuliwa na serikali kuhakikisha fursa hizo za uchumi wa buluu zinawasaidia wananchi hususan vijana na kinamama.
“Sasa hivi tuna shilingi bilioni tatu (3) za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajli ya ukulima wa mwani, zitatumika kununulia vifaa vya kulimia mwani ikiwemo Kamba, Taitai na Mbegu,”alisema
Aliongeza kwa kuwataka wadau hao kushirikiana na serikali kikamilifu kuwapatia ujuzi stahiki vijana ili waweze kutumia fursa hizo zilizopo katika ukanda wa pwani kujiongezea fursa za ajira na kipato.
“Leo IUCN mmekuja na hili jambo la kumuunga mkono Mhe. Rais Samia la kutengeneza fursa za ajira kupitia uchumi wa buluu, tafadhali, tuwafundishe hawa watu wetu wafuge,”alihimiza
Aidha, Mhe. Ulega aliwataka viongozi hao wa IUCN kuandaa mpango utakaoonesha namna watakavyoshirikiana na serikali katika kuwasaidia vijana kujiajiri kupitia fursa za uchumi wa buluu zilizopo nchini.
Kwa upande wake, Meneja wa Programu, Shirikisho la Kimataifa linaloshughulika na programu ya uendelezaji wa pwani na uvuvi wa bahari (IUCN), Dkt. Elinasi Monga alisema kuwa wao wapo tayari kushirikiana na serikali katika kuwezesha vijana kutumia fursa za uchumi wa buluu ili kujiajiri na kwa sasa wameshaanza kuwezesha baadhi ya vijana mkoani Tanga.
Halikadhalika alisema kuwa maelekezo aliyoyatoa Waziri Ulega watayafanyia kazi huku akiongeza kuwa ushirikiano wao na serikali utasaidia kufikia malengo waliyokusudia.
IDARA YA MASOKO TVLA YAKABIDHIWA GARI
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi amekabidhi Gari jipya aina ya HINO litakalokuwa linatumika kusafirisha Chanjo za Mifugo kutoka kituo cha uzalishaji (TVI) kilichopo Kibaha Mkoa wa Pwani na kuzisambaza kwa wateja maeneo mbalimbali hapa nchini.
Akikabidhi gari hilo kwa Mkurugenzi wa Huduma Saidizi siku ya tarehe 28/09/2022 Makao Makuu ya ofisi za Wakala zilizopo Temeke jijini Dar es salaam alisema kuwa, Wakala imefanikiwa kununua gari la kutunza baridi ambalo ni mahususi kwa ajili ya kusafirishia chanjo kutoka kituo cha uzalishaji chanjo kibaha na kuzisambaza kwa wateja wote nchini.
“Gari hili limenunuliwa kutokana na fedha za ruzuku ya maendeleo, nachukua fursa hii kuishukuru Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kutenga bajeti ya maendeleo ambayo imetuwezesha kununua chombo hiki cha usafiri ambacho kitasaidia kuwafikishia wafugaji chanjo kwa wakati.” Alisema Dkt. Bitanyi
Dkt Bitanyi aliongeza kuwa kwa mwaka huu wa fedha 2022 wakala imetenga bajeti ya kununua gari jingine kama hilo litakalotumika kwa ajili ya kusafirisha chanjo maeneno mbalimbali nchini kwa kusaidiana na gari lililopo.
“Nalikabidhi gari hili kwa Mkurugenzi wa Huduma saidizi ambaye ndie msimamizi wa shughuli za Wakala, na natoa rai kwa watakaokabidhiwa gari hili kulitunza kwa kuhakikisha linafanyiwa marekebisho (Services) kwa wakati ili liendelee kuwepo na kufanya kazi kwa ufanisi na kutokwamisha shughuli za usafirishaji na usambazaji wa chanjo.” Alisema Dkt. Bitanyi
Akipokea Gari hilo Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania Ndg Henry S. Mwaijega, amemshukuru Mtendaji mkuu kwa kuwakabidhi gari la usafirishaji wa chanjo kwani litasaidia katika kuboresha na kupanua huduma zinazotolewa na Wakala, vilevile ameahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa.
“Tuzingatie yale yote yaliyoagizwa na Mtendaji Mkuu kwani Serikali imeamua kutenga fedha kununua chombo hiki ili kurahisisha utekelezaji wa shughuli za usafirishaji chanjo, na kila atakaepewa dhamana ya kulitumia ahakikishe analitunza ikiwa ni pamoja na kufanya shughuli zilizokusudiwa” alisema Ndg. Mwaijega.
Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania-TVLA ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi inayojishughurisha na Uchunguzi wa Magonjwa ya Wanyama, Uzalishaji wa Chanjo za Mifugo, Uhakiki wa Ubora wa Vyakula vya Mifugo, Uhakiki wa ubora wa viuatilifu vya Mifugo, Utafiti wa magonjwa ya Wanyama pamoja na Huduma za ushauri.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Gari jipya aina ya HINO litakalokuwa linatumika kusafirisha Chanjo za Mifugo kutoka kituo cha uzalishaji (TVI) kilichopo Kibaha Mkoa wa Pwani na kuzisambaza kwa wateja maeneo mbalimbali hapa nchini leo tarehe 28/09/2022 Makao Makuu ya ofisi za Wakala zilizopo Temeke jijini Dar es salaam kulia kwake ni Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa Wakala Ndg Henry S. Mwaijega.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi akipata maelezo ya namna ya kulitumia Gari jipya la kusafirisha Chanjo za Mifugo kutoka kwa dereva wa gari Ndg. Salim Mbalazi leo tarehe 28/09/2022 Makao Makuu ya ofisi za Wakala zilizopo Temeke jijini Dar es salaam ambapo gari hilo litakuwa linasafirisha chanjo kutoka kituo cha uzalishaji (TVI) kilichopo Kibaha Mkoa wa Pwani na kuzisambaza kwa wateja maeneo mbalimbali hapa nchini ajili ya kutumika
WAZIRI NDAKI AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA TANZANIA NCHINI MISRI
Picha ya Pamoja ya Ujumbe wa Kampuni ya Evergreen Kutoka Nchini Misri ikiongozwa na Balozi wa Tanzania toka nchini Misri Dkt. Emmanuel Nchimbi wa tano toka (kushoto) na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh..Mashimba Ndaki wa nne toka kulia,Mwenyekiti wa Kampuni ya Evergreen Dkt.Adel Mosalamany wa tatu toka kulia, Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah, wa kwanza toka kushoto,mara baada ya Kikao cha Wajumbe hao na wataalam wa Uvuvi wakiongozwa na Waziri Mashimba Ndaki cha Kubaini fursa za maeneo ya kuwekeza katika Uvuvi kwa Kampuni ya Evergreen toka nchini Misri.Picha imechuliwa katika Ofisi za Wizara Mji wa Serikali Mtumba Dodoma, (27.09.2022)
ELIMU YA UDHIBITI WA UGONJWA WA KICHAA CHA MBWA YATOLEWA SHULENI
NDAKI AHIMIZA UWEPO WA MFUMO IMARA WA USIMAMIZI WA RASILIMALI ZA UVUVI AFRIKA
Na Mbaraka Kambona,
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewahimiza Wadau wa Sekta ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika (AU) kuhakikisha wanakuwa na mpango madhubuti wa pamoja wa usimamizi na uendelezaji wa rasilimali hizo ili mchango wake uwe na manufaa makubwa zaidi kwao.
Aliyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha kurasimisha mpango wa kusimamia rasilimali za Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji wa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo unaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 26-28, 2022.
Alisema ni wakati sasa nchi za Afrika kuwa na utaratibu wa pamoja wa kuratibu usimamizi wa uendelezaji wa rasilimali za uvuvi utakaosaidia kulinda ubora, usalama, kuimarisha ushirikiano kwa lengo la kukuza soko la mazao hayo ndani na nje ya Jumuiya hiyo.
"Nimewasisitiza wadau hawa walioshiriki kikao hiki kuwa ni muhimu kutoka na maazimio yatakayosaidia kuratibu vyema uendelezaji wa rasilimali za uvuvi kuliko ilivyo hivi sasa ambapo kila nchi ina namna yake ya kuendesha shughuli hizo", alisema
Aliongeza kwa kusema kuwa nchi hizo pia ziendelee kuelimisha wananchi wao juu ya uvuvi endelevu kwa kuzingatia Sheria na kanuni zilizopo katika maeneo yao.
Kuhusu changamoto za masoko, Waziri Ndaki alisema ni muhimu wanajumuiya hao kuona namna watakavyo zitafutia majawabu ili mazao ya uvuvi yaweze kupata soko kubwa zaidi katika nchi za nje ikiwemo ulaya na china ili nchi za Afrika ziweze kufaidika zaidi na rasilimali zake.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya kimataifa inayoshughulika na usimamizi wa rasilimali za mifugo (AU-IBAR), Bi. Francisca Gonah(katikati) muda mfupi kabla ya kufungua kikao kazi cha kurasimisha mpango wa usimamizi wa rasilimali za Uvuvi na Ufugaji wa Viumbe Maji kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika unaofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 26-28, 2022. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Uvuvi Tanzania, Bw. Emmanuel Bulayi.
Pichani ni sehemu ya washiriki wa kikao kazi cha kurasimisha mpango wa usimamizi wa rasilimali za Uvuvi na Ufugaji wa Viumbe Maji utakaotumiwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika unaofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku tatu kuanzia Septemba 26-28, 2022.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiongea na Washiriki wa kikao kazi kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika (hawapo pichani) cha kurasimisha mpango wa usimamizi wa rasilimali za Uvuvi na Ufugaji wa Viumbe Maji unaofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 26-28, 2022.
TALIRI YATAKIWA KUTOA MAFUNZO YA MALISHO YA MIFUGO KWA JAMII
Na. Edward Kondela
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Tixon Nzunda ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), kuongeza uvunaji wa malisho ya mifugo katika vituo vyake vyote nchini ili jamii inayowazunguka iweze kujifunza juu ya ulimaji wa malisho.
Katibu Mkuu Nzunda amebainisha hayo (23.09.2022) wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika kituo cha TALIRI kilichopo Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma pamoja na kampasi ya Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA).
Ameongeza kuwa sambamba na jamii inayoishi karibu na vituo vya TALIRI kujifunza juu ya ulimaji wa malisho ya mifugo, jamii hiyo inapaswa pia kujifunza juu ya teknolojia rahisi ya uvunaji wa malisho pamoja na kufahamishwa utaratibu wa ulimaji wa malisho ukiwemo wa undaaji wa mashamba na uvunaji wa mbegu.
Ameiasa sekta binafsi kujikita katika biashara ya malisho ya mifugo kwa kuwekeza kwenye vifaa vya uvunaji wa malisho hususan malisho ya asili ambayo kwa sasa ni biashara yenye faida kubwa ambapo robota moja linauzwa kuanzia Shilingi Elfu Nne pamoja na kuwekeza kwenye uzalishaji wa mbegu za malisho ambazo zinahitajika kwa wingi.
Aidha, amewataka vijana hususan wasomi kuchangamkia fursa ya ulimaji wa malisho ya mifugo kwa kupata elimu juu ya ulimaji bora wa malisho kupitia TALIRI na hatimaye kuwekeza kulingana na maelekezo watakayopata ili walime kwa faida.
Akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa TALIRI pamoja na LITA amewataka kubadilika na kufanya kazi kutokana na mabadiliko ya mazingira ya sasa na kutofanya kazi kwa mazoea pamoja na kuacha kufanya kazi kwa malalamiko na kusubiri kila kitu kutoka serikalini, badala yake wafanye kazi kutokana na rasilimali inayopatikana kwa wakati huo na kuzidi kuboresha utendaji wao wa kazi.
Akiwa katika ziara hiyo Katibu Mkuu Nzunda ameambatana na Mwenyekiti wa bodi ya TALIRI Prof. Sebastian Chenyambuga, Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo Prof. Erick Komba, Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angello Mwilawa pamoja na viongozi wengine wa TALIRI na LITA, ametembelea pia ujenzi wa bweni la wanafunzi la LITA na kuutaka uongozi wa kampasi hiyo kuhakikisha jengo hilo linakamilika ifikapo tarehe 30 Mwezi Oktoba mwaka huu ili lianze kutumika.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Tixon Nzunda (wa tatu kutoka kulia), akitoa maelekezo kwa uongozi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), kuongeza uvunaji wa malisho ya mifugo katika vituo vyake vyote nchini ili jamii inayowazunguka iweze kujifunza juu ya ulimaji wa malisho. Bw. Nzunda amebainisha hayo wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika kituo cha TALIRI kilichopo Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma pamoja na kampasi ya Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA). (23.09.2022)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Tixon Nzunda akikagua ng’ombe aina ya Mpwapwa wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma na kuitaka TALIRI kuongeza tija katika uzalishaji wa mifugo bora na kuhakikisha inazifikia jamii ili ziweze kuboresha mifugo yao. (23.09.2022)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Tixon Nzunda (wa nne kutoka kushoto) akikagua josho la kuogeshea mifugo lililopo Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma, ambalo ni josho la kwanza Afrika Mashariki lililojengwa na wajerumani Mwaka 1905. Katibu Mkuu Nzunda ameshuhudia josho hilo alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika taasisi hiyo. (23.09.2022)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Tixon Nzunda (wa nne kutoka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mwenyekiti wa bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Prof. Sebastian Chenyambuga, Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo Prof. Erick Komba, Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angello Mwilawa pamoja na viongozi wa TALIRI na Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) Kampasi ya Mpwapwa Mkoani Dodoma, wakati Katibu Mkuu Nzunda alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja na kushuhudia uimara wa josho la kuogeshea mifugo lililojengwa na wajerumani Mwaka 1905. (23.09.2022)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Tixon Nzunda akizungumza na baadhi ya wafanyakazi (hawapo pichani) wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) pamoja na Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma, ambapo amewataka kubadilika na kufanya kazi kutokana na mabadiliko ya mazingira ya sasa na kutofanya kazi kwa mazoea pamoja na kuacha kufanya kazi kwa malalamiko na kusubiri kila kitu kutoka serikalini, badala yake wafanye kazi kutokana na rasilimali inayopatikana kwa wakati huo na kuzidi kuboresha utendaji wao wa kazi. (23.09.2022)
Baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) pamoja na Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Tixon Nzunda (hayupo pichani) wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma ambapo walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali na kutoa ushauri. (23.09.2022)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Tixon Nzunda (wa kwanza) akitoka kwenye jengo la bweni la wanafunzi wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) ili kushuhudia maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma, ambapo ameutaka uongozi wa kampasi hiyo kuhakikisha jingo linakamilika ifikapo tarehe 30 Mwezi Oktoba mwaka huu ili lianze kutumiwa na wanafunzi. (23.09.2022)
SEKTA YA UVUVI YAWEKA SAINI HATI YA USHIRIKIANO WA PROGRAMU YA UKUZAJI VIUMBE MAJI
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kushoto) na Mkurugenzi wa programu ya ukuzaji viumbe maji kutoka Shirika la Gatsby Africa, Bw. Ben Gimson (wa pili kutoka kushoto) wakiweka saini kwenye hati ya ushirikiano kati ya Shirika hilo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) yenye lengo la kuweka mazingira mazuri ya kisera kwa kuwezesha ukuaji wa tasnia ya Ukuzaji Viumbe Maji, kutoa msaada wa kiufundi kwa wafugaji samaki kibiashara ili kuongeza uzalishaji na tija na kuwezesha mpango wa matumizi bora ya Ziwa Victoria katika muktadha wa ufugaji samaki kwa vizimba. Septemba 23,2022 Jijini dar es salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Programu ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Shirika la Gatsby Africa, Bw. Ben Gimson (wa pili kutoka kushoto) na watendaji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi mara baada ya kuweka Saini kwenye hati ya ushirikiano baina ya Shirika hilo na Wizara, lengo likiwa ni pamoja na kuweka mazingira mazuri ya kisera kwa kuwezesha ukuaji wa tasnia ya Ukuzaji Viumbe Maji, kutoa msaada wa kiufundi kwa wafugaji samaki kibiashara ili kuongeza uzalishaji na tija na kuwezesha mpango wa matumizi bora ya Ziwa Victoria katika muktadha wa ufugaji samaki kwa vizimba. Septemba 23,2022 Jijini dar es salaam.
WAZIRI NDAKI AKUTANA NA UJUMBE KUTOKA BENKI YA DUNIA
ULEGA AMALIZA MKWAMO WA UTEKELEZAJI WA MRADI WA CHAMA CHA USHIRIKA CHA BUKASIGA
Na Martha Mbena.
Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amemaliza mkwamo wa utekelezaji wa mradi wa ukaushaji dagaa wa chama cha Ushirika cha BUKASIGA uliopo katika kisiwa cha Ghana, Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe.
Mhe. Ulega alifanikiwa kuumaliza mkwamo huo wakati alipokuwa akiendesha kikao kazi cha kujadiliana namna bora ya kukubaliana kati ya chama cha Ushirika cha BUKASIGA, Sokoine University Graduates Entreprenuers Cooperative" (SUGECO) na Benki ya maendeleo ya Kilimo (TADB) kilichofanyika katika ukumbi wa mkutano, Jengo la Nbc,Dodoma. 22 Septemba 2022.
Mhe. Ulega amesema pande zote mbili wamefikia mahali pazuri na mwanga umeonekana na watu wamekubaliana kule ambapo wamepakusudia.
"Nawapongeza sana kwasababu washirika hawa wameitika wito wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwakuweza kufanya kazi kwa bidii kuweza kujenga uchumi wa nchi yetu" Amesema Mhe. Ulega.
Pia Mhe. Ulega ameagiza chama cha ushirika cha BUKASIGA na watu wa SUGECO Kuandika mkataba wa makubaliano ambao utaeleza namna ya uendeshaji wa mradi na watu wa SUGECO, na kufikia makubaliano ambapo Wizara itasimamia makubaliano hayo, na ameagiza mwisho wa kuandaliwa mkataba huo utakuwa tarehe 06 Oktoba 2022.
Naye Mbunge wa Ukerewe, Mhe. Joseph Mkundi amemshukuru Mhe. Naibu Waziri kwa kuweza kuitisha kikao cha makubaliano na kuweza kuondoa mkwamo huo wa utekelezaji mradi wa ukaushaji dagaa,
Mhe.Mkundi ameongezea kwa kusema anatamani kuona Bukasiga wanaendelea na mradi huo kwani waliweza kuhamasisha na vyama vidogovidogo kwenye zao la dagaa.