Nav bar

Jumatano, 31 Agosti 2022

SERIKALI KUTOA MIKOPO KWA WAVUVI NA WAKUZAJI VIUMBE MAJI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema kuwa serikali imeandaa mpango wa kuwawezesha wavuvi na wakuzaji viumbe maji kwa kuwapatia mitaji ili waweze kuboresha shughuli zao.

 

Waziri Ndaki ameyasema hayo leo (30.08.2022) kwenye hafla ya kusaini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa ununuzi wa boti za uvuvi na vizimba vya kufugia samaki kati ya wizara ya mifugo na uvuvi (sekta ya uvuvi) na benki ya maendeleo ya kilimo tanzania – TADB, hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Mzee uliopo katika Makao Makuu ya Jeshi la Magereza – Msalato Jijini Dodoma.

 

Mpango huu ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani katika hotuba yake aliyoitoa tarehe 07.01.2022 katika kilele cha Matembezi ya Miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo alisisitiza kutumika kwa fursa zilizopo katika kukuza Uchumi wa Buluu ikiwemo uvuvi na ukuzaji viumbe maji. Aidha, wakati akifunga Maonesho ya Sherehe za Wakulima (NANENANE), Mheshimiwa Rais aliagiza Wizara kuhakikisha kuwa uzalishaji wa Samaki unaongezeka kutoka tani 497,567 na kufikia tani 600,000 ifikapo mwaka 2025.

 

Katika utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeandaa Mpango wa kuwawezesha wavuvi na wakuzaji viumbe maji kwa kutoa mikopo isiyo na riba kwa vyama vya ushirika, vikundi vya wavuvi, wakuzaji viumbe maji, wavuvi binafsi na makampuni ya wavuvi. Mikopo hiyo itahusisha zana za kisasa za uvuvi ikiwemo boti, nyavu, injini, vizimba, vifaranga vya samaki, chakula cha samaki na pembejeo za ukulima wa mwani.

 

Waziri Ndaki ametoa wito kwa wavuvi na wakuzaji viumbe maji kuchangamkia fursa hiyo ya mikopo ili iweze kuwanufaisha. Aidha, amezisihi Halmashauri katika maeneo ya mradi kwenda kuwahamasisha wananchi wake ili waweze kuitumia kuitumia fursa hii ipasavyo.

 

Aidha, amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha shilingi bilioni 60 kwa ajili ya kuendeleza Sekta ya Uvuvi, fedha ambazo zipo katika bajeti ya mwaka 2022/2023. Waziri Ndaki amesema endapo zikitumika vizuri upo uwezekano mwaka ujao wa fedha fedha hizo zikaongezeka.

 

Waziri Ndaki amesema kama viongozi watahakikisha wanawasimamia wataalam wa Wizara kwa kuwa mradi huu unatakiwa kutakelezwa kwa muda maalum, hivyo ifikapo Juni 30, 2023 utekelezaji wa mradi huu uwe umekamilika.

 

Naye Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa kasi ya utoaji mikopo kwa wavuvi kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo ni ndogo, kwani mahitaji ya watanzani, kasi ya kuwafiki na urahisi wa upataji mikopo bado ni mdogo. Hivyo TADB inayo kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha kwamba mikopo inafika kwa walengwa, kwani watu wengi wamehangaika kupata mikopo hasa wavuvi wadogo na kusababisha kukata tamaa na kuacha kufanya shughuli za uvuvi.

 

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma amesema kuwa Kamati imefurahishwa sana na mpango wa serikali wa kutoa mikopo isiyo na riba inayokwenda kuwasaidia wavuvi na wakuzaji viumbe maji. Mradi huu utakwenda kusaidia kuongeza uzalishaji wa samaki utakaokwenda kukidhi mahitaji makubwa yaliyopo.

 

Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah amesema kuwa boti hizo zina urefu wa mita 7 hadi 14 zikiwa na injini zenye uwezo wa nguvu za farasi 9.9 hadi 60. Pia boti hizo zitakuwa na uwezo wa kubeba wavuvi 620, kubeba Samaki tani 1.5, mtambo wa kufuatilia/kutambua uwepo wa Samaki (Fish finder), kifaa cha kuongoza boti (GPS), vifaa vya kuokolea Maisha na zana za uvuvi zikijumuisha mishipi na nyavu. Jumla ya shilingi Bilioni 11.5 zimetengwa kwa ajili ya kukopeshwa na mkopo huo utalipwa kwa muda wa miaka mitano (5) bila Riba.

 

Wizara pia itatoa mkopo kwa Wafugaji Samaki kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kujenga jumla ya vizimba 831 ambapo kila kizimba kimoja kitakuwa na ukubwa wa mita za ujazo 144 M3 – 256 M3. Vilevile, itatoa jumla ya vifaranga 4,080,000 na chakula cha Samaki tani 3,482.5.

 

Aidha, mkataba huo uliosainiwa leo utahusisha wakulima wa mwani ambapo jumla ya wakulima 821 watakopeshwa kamba 108,372, tai tai 7,152,552 pamoja na mbegu za mwani. Kwa ujumla kiasi cha shilingi Bilioni 21 zitatumika kwa ajili ya vizimba na zao la mwani.

 

Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania, Frank Nyabudenge amesema kuwa benki hiyo ni taasisi ya kifedha ambayo ni benki ya serikali iliyojikita kwenye sekta ya kilimo. Moja ya malengo makubwa ya kuanzishwa kwake ni kuchangia utoshelevu wa chakula na usalama endelevu wa chakula nchini ambapo ni pamoja na utoaji lishe bora.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (wa pili kushoto) na Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo Tanzania, Frank Nyabudenge (wa pili kulia wakisaini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa ununuzi wa boti za Uvuvi na vizimba vya kufugia samaki kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB). (30.08.2022)


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akihutubia wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa ununuzi wa boti za Uvuvi na vizimba vya kufugia samaki kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ambapo amesema kuwa Wizara imeandaa Mpango wa kuwawezesha wavuvi na wakuzaji viumbe maji kwa kutoa mikopo isiyo na riba kwa vyama vya ushirika, vikundi vya wavuvi, wakuzaji viumbe maji, wavuvi binafsi na makampuni ya wavuvi. Hafla hii imefanyika kwenye ukumbi wa Mzee uliopo Makao Makuu ya Jeshi la Magereza - Msalato Jijini Dodoma. (30.08.2022)


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akitoa salam wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa ununuzi wa boti za Uvuvi na vizimba vya kufugia samaki kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ambapo amesema kuwa kasi ya utoaji mikopo kwa wavuvi kupitia TADB ni ndogo, kwani mahitaji ya watanzani, kasi ya kuwafiki na urahisi wa upataji mikopo bado ni mdogo, hivyo TADB inayo kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha kwamba mikopo inawafikia walengwa kwa wakati. Hafla hii imefanyika kwenye ukumbi wa Mzee uliopo Makao Makuu ya Jeshi la Magereza - Msalato Jijini Dodoma. (30,08,2022)


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma (Mb) akitoa salam za kamati wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa ununuzi wa boti za Uvuvi na vizimba vya kufugia samaki kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) amesema kuwa Kamati imefurahishwa sana na mradi huu wa kuwakopesha wavuvi na wakuzaji viumbe maji kwa kuwa utawasaidia kuongeza uzalisha na hivyo kuongeza upatikanaji wa samaki. Aidha, amesema kuwa Kamati itaendelea kuisimamia Wizara ili kuhakikisha maendeleo kwenye Sekta ya Uvuvi yanapatikana. Hafla hii imefanyika kwenye ukumbi wa Mzee uliopo Makao Makuu ya Jeshi la Magereza - Msalato Jijini Dodoma. (30.08.2022)


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akitoa neno la utangulizi wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa ununuzi wa boti za Uvuvi na vizimba vya kufugia samaki kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) amesema kuwa jumla ya wakulima 821 watakopeshwa kamba 108,372, tai tai 7,152,552 pamoja na mbegu za mwani. Kwa ujumla kiasi cha shilingi Bilioni 21 zitatumika kwa ajili ya vizimba na zao la mwani. Hafla hii imefanyika kwenye ukumbi wa Mzee uliopo Makao Makuu ya Jeshi la Magereza - Msalato Jijini Dodoma. (30.08.2022)


Naibu Katibu Mkuu, OR TAMISEMI (Afya), Dkt. Grace Magembe akitoa salam wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa ununuzi wa boti za Uvuvi na vizimba vya kufugia samaki kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) amemuhakikishia Waziri kuwa TAMISEMI itashiriki kikamilifu kwenye mkakati huo kwa kuwa tayari wanayo mifumo ambayo ilikuwa ikitumika kwenye utoaji wa fedha. Hivyo watashirikiana na wataalam kutoka Sekta ya Uvuvi kuangalia ni wapi wanafanya vizuri na kama kutakuwa na changamoto ziweze kutatuliwa ili mradi huu uweze kuleta tija na matokeo yaliyotarajiwa. Hafla hii imefanyika kwenye ukumbi wa Mzee uliopo Makao Makuu ya Jeshi la Magereza - Msalato Jijini Dodoma. (30.08.2022)


Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania, Frank Nyabudenge akitoa salam za TADB wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa ununuzi wa boti za Uvuvi na vizimba vya kufugia samaki kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) amesema kuwa watahakikisha mikopo hiyo inawafikia walengwa nakutoa matokeo chanya ya kuongeza mazao yatokanayo na uvuvi. Hafla hii imefanyika kwenye ukumbi wa Mzee uliopo Makao Makuu ya Jeshi la Magereza - Msalato Jijini Dodoma. (30.08.2022)


Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania, Frank Nyabudenge akitoa salam za TADB wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa ununuzi wa boti za Uvuvi na vizimba vya kufugia samaki kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) amesema kuwa watahakikisha mikopo hiyo inawafikia walengwa nakutoa matokeo chanya ya kuongeza mazao yatokanayo na uvuvi. Hafla hii imefanyika kwenye ukumbi wa Mzee uliopo Makao Makuu ya Jeshi la Magereza - Msalato Jijini Dodoma. (30.08.2022)


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (wa pili kushoto) na Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo Tanzania, Frank Nyabudenge (kulia) wakionyesha mikataba ya utekelezaji wa mradi wa ununuzi wa boti za Uvuvi na vizimba vya kufugia samaki kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) mara baada ya kumaliza kusaini mikataba hiyo. (30.08.2022)


Picha ya pamoja ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma (Mb), Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah na Wakurugenzi na Wakuu wa Vitenge wa Wizara hiyo mara baada ya kumalizika kwa hafla ya kusaini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa ununuzi wa boti za Uvuvi na vizimba vya kufugia samaki kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) iliyofanyika kwenye ukumbi wa Mzee uliopo Makao Makuu ya Jeshi la Magereza - Msalato Jijini Dodoma. (30.08.2022)


Picha ya pamoja ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma (Mb), Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah na Kamati ya maandalizi mara baada ya kumalizika kwa hafla ya kusaini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa ununuzi wa boti za Uvuvi na vizimba vya kufugia samaki kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) iliyofanyika kwenye ukumbi wa Mzee uliopo Makao Makuu ya Jeshi la Magereza - Msalato Jijini Dodoma. (30.08.2022)

Jumanne, 30 Agosti 2022

WADAU TASNIA YA KUKU WAKUTANA KUJADILI CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI

Na Mbaraka Kambona, Arusha


Wadau wa tasnia ya kuku wamekutana kujadili changamoto zinazokabili mnyororo wa thamani wa tasnia ya kuku na kuweka vipaumbele vya uwekezaji kwa lengo la kuifanya tasnia hiyo kuwa na mchango mkubwa zaidi katika pato la taifa.


Wadau hao kutoka serikalini na sekta binafsi walikutana jijini Arusha Agosti 29, 2022.


Akifungua mkutano huo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki alisema pamoja na jitihada zinazoendelea kufanywa kukuza tasnia ya kuku bado tasnia hiyo inaonekana ni ndogo, hivyo aliwataka wadau hao kujadili kwa kina ni namna gani wafanye ili tasnia hiyo iwe na mchango unaotarajiwa.


"Kwa hiyo taarifa ya mnyororo wa thamani wa tasnia ya kuku mtakayoijadili leo mtaweza kuwa na majibu ya changamoto zilizopo katika kuifanya tasnia hii inakwama hasa katika eneo la afya ya kuku, biashara na masoko na kutafutia ufumbuzi changamoto hizo", alisema


Aliongeza kwa kusema kuwa pamoja na tasnia hiyo kuendelea kutoa mchango wake katika lishe na kipato bado wadau wanajukumu kubwa la kuhakikisha wanaongeza uzalishaji wa kuku na mayai ili kukidhi soko lililopo ndani na nje ya nchi.


Aidha, alisema kuwa serikali ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea na itaendelea kuweke mazingira wezeshi kwa ajili ya tasnia ya kuku kukua huku akiwataka wadau hao kuendelee kutumia fursa hiyo kuimarisha mnyororo wa thamani wa tasnia hiyo kwa maslahi mapana ya taifa.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) akimueleza jambo Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika(afDB), Bw. Salum Ramadhani (wa tatu kutoka kushoto) muda mfupi baada ya kufungua mkutano wa kujadili changamoto zinazokabili mnyororo wa thamani wa tasnia ya kuku na kuweka vipaumbele vya uwekezaji uliofanyika jijini Arusha Agosti 29, 2022.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiongea na wadau wa tasnia ya kuku (hawapo pichani) wakati akifungua mkutano wa kujadili changamoto zinazokabili mnyororo wa thamani wa tasnia ya kuku na kuweka vipaumbele vya uwekezaji uliofanyika jijini Arusha Agosti 29, 2022.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Wadau wa tasnia ya kuku muda mfupi mara baada ya kufungua mkutano wa kujadili changamoto zinazokabili mnyororo wa thamani wa tasnia ya kuku na kuweka vipaumbele vya uwekezaji uliofanyika jijini Arusha Agosti 29, 2022.

SEKTA YA MIFUGO YAFANYA MAZUNGUMZO NA MAKAMPUNI MAKUBWA YA NCHINI UINGEREZA

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia Sekta ya Mifugo amesema kuwa wameanza kufanya mazungumzo na Makampuni makubwa yanayojishughulisha na shughuli za mifugo ya nchini Uingereza.

 

Katibu Mkuu Nzunda ameyasema hayo leo (29.08.2022) baada ya kumalizika kwa mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao uliowashirikisha Viongozi kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania, baadhi ya Wadau wa Sekta ya Mifugo waliopo nchini Uingereza pamoja na Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo wa Sekta ya Mifugo, mkutano ambao ulifanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Wizara uliyopo kwenye Mji wa Serikali – Mtumba Jijini Dodoma.

 

Mkutano huo ulijadili namna wadau hao kutoka nchini Uingereza wanavyoweza kuja kushirikiana na wadau wa Sekta ya Mifugo hapa nchini hasa wafuga ili kuikuza zaidi sekta hiyo.

 

Lengo hasa la mkutano huo ni kuona ni namna gani makampuni hayo yanaweza kusaidia kuimarisha mfumo wa ufugaji nchini kwa kutumia teknolojia rahisi za malisho ya mifugo, mbegu za mifugo na uchakataji wa mazao ya mifugo.

 

Katika mkutano huo makampuni hayo yameonyesha baadhi ya teknolojia za uchakataji wa malisho, ngozi, nyama na maziwa. Serikali imeyakaribisha makampuni hayo kwa ajili ya kuja kuleta teknolojia rahisi na yenye bei nafuu ili kuwezesha wafugaji wadogo na wa kati kumudu gharama za vifaa na kuzalisha kwa tija.

 

Lakini pia kupitia teknolojia hizi, zitasaidia kujenga uwezo wa Wizara katika kutambua teknolojia mbalimbali zinazotumika na nchi zilizoendelea kama Uingereza kwa ajili ya kuendeleza Sekta ya Mifugo.

 

Naye Mshauri Biashara kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania, Godfrey Lwakatare amesema kuwa lengo la kufika Wizarani ni kuiunganisha Sekta ya Mifugo na Makampuni makubwa kutoka nchini Uingereza yanayojishughulisha na sekta ya mifugo. Matarajio yao ni kuwa Sekta ya Mifugo hapa nchini itaweza kukua kupitia ushirikiano huo na Sekta Binafsi.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda akifungua mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao uliowashirikisha Viongozi kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania, baadhi ya Wadau wa Sekta ya Mifugo waliopo nchini Uingereza pamoja na Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo wa Sekta ya Mifugo ambao ulijadili namna wadau hao kutoka nchini Uingereza wanaweza kuja kushirikiana na wadau wa Sekta ya Mifugo hapa nchini hasa wafuga ili kuikuza zaidi sekta. Kushoto ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu (Mifugo), Dkt. Charles Mhina na kulia ni Mshauri Biashara kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania, Godfrey Lwakatare. Mkutano huo umefanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Wizara iliyopo kwenye Mji wa Serikali – Mtumba Jijini Dodoma. (29.08.2022)


Baadhi ya Viongozi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) na Viongozi kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa kwenye mkutano uliowashirikisha wadau wa Sekta ya Mifugo nchini Uingereza, ulijadili namna wadau hao kutoka nchini Uingereza wanaweza kuja kushirikiana na wadau wa Sekta ya Mifugo hapa nchini hasa wafuga ili kuikuza zaidi Sekta hiyo. Mkutano huo umefanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Wizara uliyopo kwenye Mji wa Serikali – Mtumba Jijini Dodoma. (29.08.2022)

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Sera na Mipango, Bw. Mbaraka Stambuli akiwasilisha mada ya fursa zilizopo kwenye Sekta ya Mifugo wakati wa mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao ulijadili namna wadau wa Sekta ya Mifugo kutoka nchini Uingereza wanaweza kuja kushirikiana na wadau wa Sekta ya Mifugo hapa nchini hasa wafuga ili kuikuza zaidi sekta hiyo. Mkutano huo umefanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Wizara uliyopo kwenye Mji wa Serikali – Mtumba Jijini Dodoma. (29.08.2022)


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda (kushoto) akimuelezea Waziri wa Nchi, Umwagiliaji na Nyanda za Chini, Mhe. Dkt. Birhanu Megersa kutoka nchini Ethiopia (hayupo pichani) namna Sekta ya Mifugo ilivyojipanga kuhakikisha mchango wa sekta hiyo kwa wafugaji na pato la Taifa unakua. Mazungumzo hayo yalifanyika kwenye Ofisi za Wizara zilizopo kwenye Mji wa Serikali - Mtumba Jijini Dodoma. (29.08.2022)


Waziri wa Nchi, Umwagiliaji na Nyanda za Chini, Mhe. Dkt. Birhanu Megersa kutoka nchini Ethiopia akielezea mambo mbalimbali aliyojifunza kwenye ziara yake ya kujifunza namna Tanzania ilivyojipanga kwenye matumizi na uendelezaji wa maeneo ya wafugaji wa asili. Mazungumzo hayo yalifanyika kwenye Ofisi za Wizara zilizopo kwenye Mji wa Serikali - Mtumba Jijini Dodoma. (29.08.2022)


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda akizungumza na Viongozi na Wataalam kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hiyo, Dkt. Jimmy Smith (wa pili kulia) walipofika ofisini kwake kwa lengo la kuona ni namna gani Taasisi wanazofanya nazo kazi zinafanikiwa, changamoto na kama kuna maeneo ambayo baadae yatahitaji kufanyiwa tafiti. Mazungumzo hayo yalifanyika kwenye Ofisi za Wizara zilizopo kwenye Mji wa Serikali - Mtumba Jijini Dodoma. (29.08.2022)


Picha ya pamoja ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda (wa nne kutoka kulia) akipokea zawadi kutoka kwa Viongozi na Wataalam wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo mara baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika kwenye Ofisi za Wizara zilizopo kwenye Mji wa Serikali - Mtumba Jijini Dodoma. (29.08.2022)

Jumapili, 28 Agosti 2022

SAUTI YETU WIKI HII

 


LITA KIKULULA YATAKIWA KUENDELEA KUSAIDIA WANANCHI

Na Mbaraka Kambona, 


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki ameipongeza Wakala ya Mafunzo ya Mifugo, Kampasi ya Kikulula (LITA-Kikulula) iliyopo Wilayani Karagwe Mkoani Kagera kwa kazi nzuri ya kuwawezesha wananchi ujuzi wa kufuga kisasa huku akiwataka kuendelea kuwasaidia wananchi kufanya ufugaji wa kisasa, wenye tija zaidi kwao na Taifa kwa ujumla.


Waziri Ndaki alitoa kauli hiyo Agosti 26, 2022 wakati wa ziara yake aliyoifanya katika kampasi hiyo kwa lengo la kukagua shughuli wanazozifanya.


"Napenda kuipongeza Kampasi hii ya LITA Kikulula kwa juhudi kubwa wanazofanya katika kazi zao, ukijaribu kuangalia rasilimali walizonazo na kile wanachokitoa utaona kwamba ni juhudi kubwa wanafanya ili kuwa na matokeo haya wanayoyapata," alisema


Alisema kuwa kampasi hiyo imeendelea kupata matokea hayo kwa sababu wanafundisha kwa vitendo zaidi kuliko maneno na ndio maana alipokutana na wanafunzi wa katika kampasi hiyo walimueleza Waziri huyo kuwa kutokana na Mafunzo wanayoyapata wapo tayari kujiajiri.


"Ni vizuri muendelee kuwa na muelekeo wa namna hiyo kwa sababu vyuo hivi vilianzishwa kwa lengo la kuzalisha wananchi watakaokuwa wafugaji wa kisasa, wanaofanya ufugaji wa tija, wafugaji ambao watakuwa wanajua kwamba kuwa na Ng'ombe ni utajiri", alisisitiza


Naye Kaimu Mkuu wa Kampasi hiyo ya Kikulula, Bw. Said Mohamed alimueleza Waziri huyo kuwa katika Kampasi hiyo wana programu ya kuwatembelea wafugaji kwa ajili ya kuwasaidia kutatua changamoto za mifugo zinazowakabili na kuwashauri namna bora ya ufugaji ila wanakabiliwa na changamoto ya usafiri kwa ajili ya wanafunzi hao.


Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kihanga, Bw. Rwamhangi Mugasha aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kupeleka Kampasi hiyo Kikulula kwa sababu kupitia Kampasi hiyo  wafugaji wengi wamebadilika, wanafuga kisasa na matunda ya ufugaji wameanza kuyaona.


"Mhe. Waziri naomba nikuambie kuwa wanafunzi hawa wamekuwa msaada mkubwa sana kwa wafugaji wetu hapa Kikulula, hata ile changamoto ya upungufu wa Wataalamu wa Mifugo kwenye Kata yetu kwa kweli haipo, hawa vijana wanasaidia sana, na  wanatembea kwa miguu kuwafikia wafugaji wetu, kwa kweli tunashukuru",  alisema Diwani huyo


Aidha, alisema kuwa katika Kata hiyo kwa sasa kumekuwa na wafugaji wengi wa kisasa na hivyo alimuomba Waziri Ndaki  kuona uwezekano wa kuwa na shamba darasa ili wafugaji waweze kujifunza zaidi ufugaji wa kisasa na waweze kubadilisha maisha yao.

Kaimu Mkuu wa Kampasi ya Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA -Kikulula), Bw. Said Mohamed  akimuonesha Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) mifugo iliyopo katika kampasi hiyo alipotembelea Agosti 26, 2022.

SERIKALI KUSHIRIKISHA WADAU BEI ELEKEZI ZA MIFUGO

Na Mbaraka Kambona, Chato


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema Serikali ipo kwenye mchakato wa kushirikisha wadau wa sekta ya mifugo kupanga bei elekezi za kuuzia mifugo katika minada ili kuwawezesha wafugaji na  wafanyabiashara kuuza mifugo yao kwa bei ambayo wao watakuwa wameshiriki kuipanga.


Alitoa kauli hiyo wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mnada wa Kimataifa  wa Buzirayombo unaojengwa Wilayani Chato, Mkoani Geita Agosti 26, 2022.


Alisema suala la kuwa na bei elekezi, Serikali inalifanyia kazi na tayari Wataalam walishaandaa na hatua iliyopo sasa ni ya kuwashirikisha wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo ili kwa pamoja waweze kukubaliana na kuja na bei ambayo itakuwa imeridhiwa na pande zote.


"Bei elekezi ikitoka ndio itakuwa mahali pa kuanzia na kwenda juu, hivyo tunalifanyia kazi suala hilo na muda sio mrefu tutato muelekeo wa jambo hilo", alisema


Aliongeza kwa kusema kuwa sambamba na bei elekezi Serikali inataka sasa mifugo yote nchini ianze kupimwa kwa kilo kama ambavyo mifugo itapimwa kwa kilo katika mnada huo wa kisasa wa Buzirayombo.


"Minada yetu yote tutakayoizindua safari hii tunataka iwe na mizani ya kupimia uzito wa mifugo na hili tunataka lifanyike pia katika minada yote ya awali inayomilikiwa na Halmashauri zetu hapa nchi ili tuondokane na vitendo vya kuwapunja wafugaji wetu", aliongeza 


Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Chato, Mhe. Medard Kalemani aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kujenga mnada huo wa kimataifa Wilayani humo huku akiongeza kwa kuiomba  kuhakikisha mradi huo unamalizika haraka ili wananchi wa Kanda ya Ziwa na maeneo mengine waanze kuona matunda yake.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kushoto) akimueleza jambo Mbunge wa Jimbo la Chato, Mhe. Medard Kalemani (kulia) alipotembelea mradi wa ujenzi wa mnada wa kisasa wa Buzirayombo unaofanyika Wilayani Chato, Mkoani Geita Agosti 26, 2022.

Kaimu Afisa Mfawidhi wa ufugaji wa samaki, Kanda ya Ziwa, Rubambagwe, Bilali Banali (katikati) akitoa maelezo kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kushoto) kuhusu maendeleo ya ujenzi wa mnada wa kisasa wa Buzirayombo. Waziri Ndaki alitembelea mradi huo Agosti 26, 2022.

Pichani ni muonekano wa jengo la mnada wa kisasa wa Buzirayombo unaojengwa Wilayani Chato, Mkoani Geita.

Ijumaa, 26 Agosti 2022

WAWEKEZAJI WAZAWA WAHIMIZWA KUWEKEZA SEKTA YA MIFUGO

Na Mbaraka Kambona, Kagera


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewahimiza wawekeza kutoka Sekta binafsi nchini kuwekeza katika sekta ya mifugo kwa sababu kuna fursa kubwa ya kukuza mitaji yao na kupata faida.


Alitoa wito huo alipotembelea na kukagua maendeleo ya kiwanda cha kuchakata maziwa na chakula cha mifugo cha Kahama Fresh kilichopo Wilayani Karagwe, Mkoani Kagera Agosti 25, 2022. 


Waziri Ndaki aliwahimiza wawekezaji wa sekta binafsi kuwekeza katika sekta ya mifugo nchini kwa sababu inawezekana  akitolea mfano muwekezaji huyo wa Kahama Fresh ambaye alianza uwekezaji katika shamba alilopewa na serikali na mpaka sasa amefungua kiwanda cha kuchakata maziwa na chakula cha mifugo.


"Niseme tu kwamba sisi Wizara ya Mifugo tuko tayari kumuunga mkono mwekezaji yeyote atakayeweza kufanya uwekezaji mahiri kama alivyofanya Kahama Fresh ili  shughuli ya ufugaji iwe ya  kibiashara zaidi na kuleta tija kwao binafsi na Taifa kwa ujumla," alisema


Aliongeza kwa kusema kuwa wawekezaji hao binafsi wakiwekeza katika sekta ya mifugo na kufanya ufugaji wa kibiashara watasaidia kuongeza fursa za ajira kwa wananchi lakini pia watakuza pato la taifa.


Aidha, alisisitiza kuwa kupitia uwekezaji wao watasaidia Wafugaji wengine ambao wanafanya ufugaji wa kujikimu kujifunza kupitia kwao na kufanya ufugaji wenye tija kubwa zaidi.


Kwa upande wake Mwekezaji wa Kiwanda cha Kahama Fresh, Josam Mtangeki alisema kuwa wamekuwa wakipata changamoto ya maji na chakula cha mifugo hasa wakati wa kiangazi hivyo aliiomba Wizara kumuongezea eneo la lisilopungua hekta 2000 ili aweze kulima malisho kwa ajili ya mifugo yake na malisho mengine atawakopesha wafugaji wadogowadogo ambao wanamuuzia maziwa kwa ajili ya kuyachakata kiwandani hapo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Albert Chalamila (wa pili kutoka kulia) muda mfupi mara baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa huyo Mkoani Kagera Agosti 25, 2022.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) akiangalia chakula cha mifugo alipotembelea shamba la mifugo la Kampuni ya Kahama Fresh lililopo Wilayani Karagwe, Mkoani Kagera Agosti 25, 2022. kushoto ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Kahama Fresh, Bw. Josam Mtangeki.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Albert Chalamila (kulia) akimueleza jambo Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kushoto) alipokutana na Waziri huyo ofisini kwake Mkoani Kagera Agosti 25, 2022. Waziri Ndaki alikuwa Mkoani humo kwa ziara ya siku moja kwa ajili ya kukagua shughuli mbalimbali zinazohusu Sekta ya Mifugo na Uvuvi.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Kahama Fresh, Bw. Josam Mtangeki (kushoto) akitoa maelezo kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) kuhusu mitambo iliyofungwa katika kiwanda cha kuchakata maziwa na chakula cha mifugo cha Kahama Fresh namna itakavyofanya kazi alipotembelea kukagua maendeleo ya kiwanda hicho kipya kilichopo Wilayani Karagwe, Mkoani Kagera Agosti 25, 2022.

MPANGO WA KUWEZESHA VIJANA KUJIAJIRI WAIVA

 Na Mbaraka Kambona,

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeandaa vituo atamizi vinne kwa ajili ya kuwafundisha vijana unenepeshaji wa mifugo ili waweze kujiajiri na kujiongezea kipato kupitia Sekta ya Mifugo.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki Agosti 24, 2022 wakati akitoa taarifa kwa umma ya kuwataka vijana kujitokeza kuomba nafasi za kujiunga katika Vituo Atamizi vilivyoandaliwa Mkoani Tanga, Mwanza na Kagera.

Alisema Mhe. Rais Samia anataka kuona vijana wanawezeshwa kujiajiri kupitia Sekta ya Mifugo kwani fursa zilizopo katika sekta hiyo ni nyingi ambazo zinaweza kuwasaidia vijana kujiongezea kipato na kukuza uchumi wa taifa.

Aliongeza kwa kusema kuwa wanaanzisha vituo hivyo kuwafunza vijana kufanya ufugaji kwa njia ya vitendo ili waweze kutumia ujuzi huo kujiajiri na kujiongezea kipato.

“Hawa vijana 240 watakaokuwa katika vituo hivyo vilivyoandaliwa wataelimishwa namna ya kufanya ufugaji wa kibiashara ili waweze kusaidia kuwabadilisha wafugaji wengine kufanya ufugaji wa kisasa na wenye tija na kuondokana na ufugaji wa kujikimu”, alisema

Halikadhalika, alisema kuwa ufugaji wa kibiashara watakaofanya vijana hao utasaidia kuongeza uhakika wa kupatikana kwa malighafi katika viwanda lakini pia kuvitumia vituo hivyo kuleta mageuzi katika sekta ya ufugaji.

Aidha, Waziri Ndaki alisema kuwa vijana wataokuwa tayari kujiunga na vituo hivyo nafasi zimeshatangazwa kupitia tovuti ya Wizara na fomu zinapatikana humo, hivyo wafanye hima kwani mwisho wa maombi hayo kupokelewa ni Septemba 7, 2022.

Sifa za muombaji awe raia wa Tanzania, awe ni mhitimu wa mafunzo ya mifugo katika ngazi ya Astashahada, Stashahada au Shahada kutoka vyuo vinavyotambuliwa na serikali na awe na umri kati ya miaka 18-30.

Jitihada hizo za Wizara ni sehemu ya utekelezaji maagizo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa Agosti 8, 2022 ambapo aliielekeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha inashirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kuwawezesha vijana kujiajiri ili kujiongezea kipato kupitia Sekta ya Mifugo.



​ULEGA: VIJANA CHANGAMKIENI FURSA UCHUMI WA BULUU

Na Mbaraka Kambona, Mwanza


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewahimiza vijana wa Kanda ya Ziwa Viktoria kufuga samaki ili kujiongezea kipato na kuongeza fursa za ajira nchini.


Waziri Ulega alitoa wito huo kwa nyakati tofauti akiwa ziarani katika Wilaya za Ukerewe na Ilemela zilizopo mkoani Mwanza Agosti 20, 2022.


Alisema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kutumia fursa za uchumi wa buluu zilizopo ndani ya Ziwa Viktoria kuwawezesha vijana kufuga samaki kwa kutumia vizimba na kuuza samaki hao ndani na nje ya nchi ili kujiongezea kipato.


"Rais Samia ametoa bilioni 20 kwa ajili ya kuwezesha vijana kufuga samaki katika vizimba, hivyo ni wakati sasa wa kujipanga ili pesa hizo zitakapokuja tuweze kuzitumia vizuri kufanya uzalishaji wa samaki kwa wingi ili tuweze kuuza na kupata kipato", alisema


Aliongeza kwa kusema kuwa samaki aina ya sato wanahitajika sana ndani na nje ya nchi, uhitaji ni mkubwa hivyo vijana wajipange vizuri ili waweze kutumia fursa hiyo kujiinua kimaisha.


Kwa upande wa vijana wanaojishughulisha na ufugaji wa samaki, Bw. Bahati Paul kutoka Ilemela na Peter Emmanuel kutoka Ukerewe kwa nyakati tofauti walisema kuwa mpango huo wa Serikali wa kuwawezesha vijana utasaidia sana vijana kujiajiri na kuondokana na changamoto ya ukosefu wa ajira.


Aidha, vijana hao waliiomba Serikali kutatua changamoto ya chakula cha samaki kwani imekuwa ikichangia kuongezeka kwa gharama za uzalishaji wa samaki nchini. 


Katika hatua nyingine, Waziri Ulega alisema mwaka huu pia Serikali itawakopesha wavuvi nchini kote boti za kisasa zaidi ya 150 ili wavuvi waweze kuboresha shughuli zao na kuongeza uzalishaji wa samaki.


Aliongeza kwa kusema kuwa boti hizo zitafungamanishwa na teknolojia za kisasa zitakazomsaidia mvuvi kurahisisha shughuli za uvuvi.


Waziri Ulega aliendelea kufafanua kuwa mkopo huo wa masharti nafuu unalenga kuwawezesha wavuvi kuboresha uvuvi wao kwa sababu nia ya  Mhe. Rais Samia ni kuwatoa wavuvi katika uvuvi wa kuwinda na kufanya uvuvi wa kisasa wa uhakika.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) akipatiwa maelezo na mmoja wa vijana wanaofanya miradi ya ufugaji wa samaki alipotembelea miradi hiyo Wilayani Ilemela, Mkoani Mwanza Agosti 20, 2022.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kulia) akikagua moja ya  kizimba katika miradi ya ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba inayofanywa na Vikundi vya vijana vya Chapakazi na Catfish alipotembelea miradi hiyo Wilayani Ilemela, Mkoani Mwanza Agosti 20, 2022.

WAZIRI NDAKI ATAKA AGIZO LA RAIS SAMIA JUU YA MAENEO YA WAFUGAJI KUTEKELEZWA

Na. Edward Kondela

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) amezitaka halmashauri na mamlaka za serikali za mikoa kuhakikisha zinatekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan la kutenga maeneo kwa ajili ya wafugaji ili kukuza sekta hiyo na kuepusha migogoro ya matumizi bora ya ardhi.


Waziri Ndaki amebainisha hayo (19.08.2022) alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro na kuzungumza na wakulima na wafugaji katika vijiji vya Tanga na Njiwa, ambapo amesema serikali ina nia nzuri ya kuendeleza Sekta ya Mifugo na kuzitaka halmashauri hizo na mamlaka za serikali za mikoa kutekeleza agizo hilo huku akiwataka wafugaji kutolisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima.


Ameongeza kuwa serikali pia imeelekeza maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho kuanzia ngazi ya kijiji ambayo hayajasajiliwa, yanatakiwa kutambuliwa rasmi na kusajiliwa pamoja na kulindwa na kuhakikisha yanatumika kama ilivyopangwa kwa ajili ya kulishia mifugo pekee pamoja na kuwataka wafugaji kutoingiza mifugo yao kwenye maeneo ya hifadhi na mapori tengefu.


 “Halmashauri na mamlaka za serikali za mikoa zinapaswa kuyalinda maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wafugaji, kama yapo maeneo yaliyotengwa na kijiji au kata kwa ajili ya malisho hayo maeneo yasajiliwe rasmi kuzuia migogoro.” Amesema Mhe Ndaki.


Aidha amewaarifu wafugaji kuwa kufuatia taarifa zilizotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), wizara inatoa tahadhari kwa wafugaji za taarifa zinazoonesha kumekuwepo na vipindi virefu vya ukavu vilivyojitokeza katika kipindi cha Mwezi Machi na Aprili mwaka 2022 hali ambayo inatishia upungufu wa malisho ya mifugo pamoja na maji.  


Amesema kufuatia hali hiyo wafugaji wategemee ukame hivyo wawe na tahadhari ya kuvuna mifugo na kubakiza ile inayoweza kutunzwa vizuri kutokana na kiasi cha malisho alichonacho mfugaji pamoja na maji.


“Tuchukue tahadhari ya kuvuna mifugo yetu tusije kukutana na ukame halafu tukaanza kulalamika mifugo imeanza kuwa dhaifu au kufa huku tulikuwa tukijua ni vizuri ukapunguza kwa kuvuna mifugo yako na kubaki na ile itakayotosheleza malisho uliyonayo pamoja na maji.” Amesema Mhe. Ndaki


Katika ziara hiyo ya kikazi ya siku moja ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Mathayo Maselle amezungumzia skimu ya umwagiliaji iliyopo Kijiji cha Njiwa na Itete ambayo imetengwa maalum kwa ajili ya kilimo imekuwa na changamoto ya wafugaji kuingiza mifugo yao katika eneo hilo jambo ambalo limekuwa likisababisha migogoro.


Hata hivyo kufuatia changamoto hiyo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ameutaka uongozi wa wilaya kwa kushirikiana na wakulima na wafugaji kutengeneza mfereji utakaosafirisha maji kutoka kwenye skimu hiyo hadi eneo lingine watakalolitenga kwa ajili ya kunyweshea mifugo maji badala ya mifugo hiyo kupita kwenye mashamba ya wakulima kwenda kunywa maji.


Nao baadhi ya wananchi waliohudhuria ziara ya Mhe. Waziri Ndaki wametoa maoni kadhaa yakiwemo ya utatuzi wa migogoro ya wakulima na wafugaji kutokana na matumizi bora ya ardhi pamoja na kuomba uwepo wa mpaka maalum wa skimu ya umwagiliaji ya vijiji vya Itete na Njiwa ili wakulima waweze kufanya shughuli zao hali kadhalika wafugaji wapate huduma ya maji ya mifugo yao bila kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro na kuzungumza na wakulima na wafugaji ambapo amesema baadhi ya kero serikali inaendelea kuzifanyia kazi ili kuhakikisha inaondoa migogoro kati yao na kuwahamasisha wafugaji kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika Jumanne ijayo Tarehe 23 Mwezi Agosti.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akizungumza na wakuu wa idara na vitengo wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro, kabla ya kuwatembelea baadhi ya wakulima na wafugaji wa wilaya hiyo, ambapo katika kikao hicho amepokea taarifa ya maendeleo ya sekta za mifugo na uvuvi na kutaka zoezi la uwekaji hereni za kieletroniki kwa mifugo lifanyike kwa amri kama sheria inavyotamka na siyo hiari. (19.08.2022)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), (kushoto) akipokewa na Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro Mhe. Mathayo Maselle (kushoto kwake), mara baada ya Waziri Ndaki kufika katika ofisi za wilaya hiyo kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku moja kwa kukutana na wakulima na wafugaji. (19.08.2022)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), akizungumza na baadhi ya wakulima na wafugaji waliohudhuria mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Tanga kilichopo Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro ambapo Waziri Ndaki amezitaka halmashauri na mamlaka za serikali za mikoa kutekeleza agizo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kutenga maeneo kwa ajili ya malisho ya mifugo pamoja na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho ambayo hayajatambuliwa, yatambuliwe rasmi na kusajiliwa ili kuepusha migogoro ya matumizi bora ya ardhi. (19.08.2022)

Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro Mhe. Mathayo Maselle, akizungumza kwenye kikao cha hadhara katika Kijiji cha Njiwa, ambapo mgeni rasmi ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), katika mkutano huo Mhe. Maselle ameelezea uwepo wa mgogoro wa matumizi ya skimu ya umwagiliaji iliyopo katika vijiji vya Njiwa na Itete ambapo Waziri Ndaki ameutaka uongozi wa wilaya hiyo kushirikiana na wakulima na wafugaji kutengeneza mfereji wa kusafirisha maji kwa ajili ya kunyweshea mifugo kwenye eneo watakalotenga ili kuepusha migogoro. (19.08.2022)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), akizungumza na baadhi ya wakulima na wafugaji waliohudhuria mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Njiwa kilichopo Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro, ambapo amewaarifu wafugaji kuwa kufuatia taarifa zilizotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), wizara inatoa tahadhari kwa wafugaji za taarifa zinazoonesha kumekuwepo na vipindi virefu vya ukavu vilivyojitokeza katika kipindi cha Mwezi Machi na Aprili mwaka 2022 hali ambayo inatishia upungufu wa malisho ya mifugo pamoja na maji hivyo wafugaji wategemee ukame na kuwaasa kuvuna mifugo na kubakiza ile inayoweza kutunzwa vizuri kutokana kiasi cha malisho alichonacho mfugaji pamoja na maji.(19.08.2022)

SPIKA MSTAAFU MSEKWA APONGEZA UCHUMI WA BULUU WA SERIKALI YA RAIS SAMIA

Na Mbaraka Kambona, Mwanza


Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Pius Msekwa ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za kuwezesha vijana kufuga samaki ili wanufaike kupitia uchumi wa buluu.


Mzee Msekwa alibainisha hayo alipotembelewa  nyumbani kwake Wilayani Ukerewe na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega wakati wa  ziara yake aliyoifanya Wilayani humo, Mkoani Mwanza Agosti 19, 2022.


Alisema kuwa mambo ambayo yanafanywa na Serikali ya awamu ya sita hususan ya kuwezesha vijana kujiajiri ni mambo ambayo Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere alitamani sana kuyafanya na hivyo kama angekuwa hai mpaka leo angefurahi sana.


"Haya yote uliyoyasema Mwl. Nyerere alitamani kuyafanya wakati wa uhai wake, kama angekuwepo leo angefurahi sana kwa sababu yale yote aliyoyataka kuyafanya Rais Samia anayaendeleza kwa kasi kubwa, hongereni sana",  alisema


Awali, akitoa taarifa ya fupi kuhusu ziara yake Mkoani Mwanza, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega alimueleza Spika Mstaafu Mzee Msekwa kuwa  Mhe. Rais Samia ametoka shilingi bilioni 20 kuwawezesha  watanzania hususan vijana kufuga samaki katika vizimba katika Ziwa Viktoria hivyo lengo la ziara yake hiyo ni kuhamasisha vijana na makundi mengine kuchangamkia fursa hiyo adhimu.


Katika hatua nyingine, Waziri Ulega alisema mwaka huu pia Serikali itawakopesha wavuvi nchini kote boti za kisasa zaidi ya 150 ili wavuvi waweze kuboresha shughuli zao na kuongeza uzalishaji wa samaki.


Aliongeza kwa kusema kuwa boti hizo zitafungamanishwa na teknolojia za kisasa zitakazomsaidia mvuvi kurahisisha shughuli za uvuvi.


Waziri Ulega aliendelea kufafanua kuwa Mhe. Rais Samia anataka kuwatoa wavuvi katika uvuvi wa kuwinda na kufanya ufugaji wa kisasa wa uhakika.



MKUTANO NA WAWEKEZAJI WA KAMPUNI YA BLUE CHELE CHELE KUTOKA NCHI YA SHELISHELI

 


Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi Bw. Magese Bulayi (katikati) akiongoza mkutano na wawekezaji wa Kampuni ya BLUE CHELE CHELE kutoka nchi ya Shelisheli hawapo pichani. Lengo la mkutano huo ni kujadili na kukubaliana maeneo ambayo wanaweza kuwekeza katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari  na Mwambao wa Bahari ya Hindi katika  Sekta ya Uvuvi. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Viumbe Maji Bw. Nazaeli Madala na Kushoto ni Muwakilishi kutoka Mamlaka ya Uvuvu wa Bahari Kuu (DSFA) BW. Peter Shunula. Mkutano huo umefanyika MVUVI HOUSE - Dsm,  (18.08.2022)


Balozi wa Heshima kutoka Jamhuri ya Shelisheli Bi. Màryvonne Pool (kushoto) akiongoza msafara huo wa wawekezaji kutoka SheliSheli amefuatana na Muwekezaji kutoka  Kampuni ya BLUE CHELE CHELE Bw. Danny Lowman (katikati)na Mshauri Muelekezi Bi. Sheryl Vangadasamy katika mkutano huo. (18.08.2022)


Kikao na Wawekezaji kutoka SheliSheli kimehudhuriwa na Wataalamu kutoka Idara ya Uvuvi (HQ), TAFIRI, MPRU, DSFA, TAFICO na Maafisa Wafawidhi wa Kanda Kuu ya Pwani na Mashariki. (18.08/2022)


Picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi Bw. Magese Bulayi(wa tatu kulia) akifuatiwa na Balozi wa Heshima Bi. Martvonne Pool,  akifuatiwa na Mshauri Muelekezi Bi Sheryl Vangadasam kutoka Jamhuri ya Shelisheli, Kaimu Mkurugenzi wa TAFICO Bi. Ester Mndeme, Mkurugenzi  Idara ya Ukuzaji wa Viumbe Bw. Nazael Madala na Muwekezaji kutoka Kampuni ya BLUR CHELE CHELE Bw. Danny Lowman. Kulia ni Mkurugenzi TAFIRI Bw. Eshmael Kimirei na Bi. Anita Kutoka MPRU, mara baada ya kumaliza kikao na wawekezaji katika Sekta Ya Uvuvi hapa nchini (18.08.2022)