Nav bar

Jumapili, 28 Agosti 2022

SERIKALI KUSHIRIKISHA WADAU BEI ELEKEZI ZA MIFUGO

Na Mbaraka Kambona, Chato


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema Serikali ipo kwenye mchakato wa kushirikisha wadau wa sekta ya mifugo kupanga bei elekezi za kuuzia mifugo katika minada ili kuwawezesha wafugaji na  wafanyabiashara kuuza mifugo yao kwa bei ambayo wao watakuwa wameshiriki kuipanga.


Alitoa kauli hiyo wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mnada wa Kimataifa  wa Buzirayombo unaojengwa Wilayani Chato, Mkoani Geita Agosti 26, 2022.


Alisema suala la kuwa na bei elekezi, Serikali inalifanyia kazi na tayari Wataalam walishaandaa na hatua iliyopo sasa ni ya kuwashirikisha wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo ili kwa pamoja waweze kukubaliana na kuja na bei ambayo itakuwa imeridhiwa na pande zote.


"Bei elekezi ikitoka ndio itakuwa mahali pa kuanzia na kwenda juu, hivyo tunalifanyia kazi suala hilo na muda sio mrefu tutato muelekeo wa jambo hilo", alisema


Aliongeza kwa kusema kuwa sambamba na bei elekezi Serikali inataka sasa mifugo yote nchini ianze kupimwa kwa kilo kama ambavyo mifugo itapimwa kwa kilo katika mnada huo wa kisasa wa Buzirayombo.


"Minada yetu yote tutakayoizindua safari hii tunataka iwe na mizani ya kupimia uzito wa mifugo na hili tunataka lifanyike pia katika minada yote ya awali inayomilikiwa na Halmashauri zetu hapa nchi ili tuondokane na vitendo vya kuwapunja wafugaji wetu", aliongeza 


Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Chato, Mhe. Medard Kalemani aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kujenga mnada huo wa kimataifa Wilayani humo huku akiongeza kwa kuiomba  kuhakikisha mradi huo unamalizika haraka ili wananchi wa Kanda ya Ziwa na maeneo mengine waanze kuona matunda yake.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kushoto) akimueleza jambo Mbunge wa Jimbo la Chato, Mhe. Medard Kalemani (kulia) alipotembelea mradi wa ujenzi wa mnada wa kisasa wa Buzirayombo unaofanyika Wilayani Chato, Mkoani Geita Agosti 26, 2022.

Kaimu Afisa Mfawidhi wa ufugaji wa samaki, Kanda ya Ziwa, Rubambagwe, Bilali Banali (katikati) akitoa maelezo kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kushoto) kuhusu maendeleo ya ujenzi wa mnada wa kisasa wa Buzirayombo. Waziri Ndaki alitembelea mradi huo Agosti 26, 2022.

Pichani ni muonekano wa jengo la mnada wa kisasa wa Buzirayombo unaojengwa Wilayani Chato, Mkoani Geita.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni