Nav bar

Jumamosi, 24 Oktoba 2020

DKT. TAMATAMAH AKABIDHI INJINI ZA BOTI KWA VYAMA VYA USHIRIKA VYA WAVUVI KANDA YA ZIWA VICTORIA.

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kulia) akikabidhi Injini ya Boti kwa Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wa Wavuvi Zilagula, Bi. Agness Mbasha katika hafla fupi ya kugawa Injini za Boti kwa Vyama vya Ushirika vya Wavuvi Kanda ya Ziwa Victoria iliyofanyika katika Wilaya ya Muleba, Mkoani Kagera. (23.10.2020)

Pichani ni Injini za Boti (4) aina ya Yamaha ambazo Wizara ya Mifugo na Uvuvi imezikabidhi kwa Vyama vinne (4) vya Ushirika vya Wavuvi Kanda ya Ziwa Victoria katika hafla fupi iliyofanyika Wilayani Muleba, Mkoani Kagera. (23.10.2020)

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kulia) akijadiliana jambo na Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Utafiti na Mafunzo ya Uvuvi, Dkt. Erastus Mosha (kushoto) muda mfupi kabla ya kukabidhi Injini za Boti kwa Vyama vya Ushirika vya Wavuvi Kanda ya Ziwa Victoria katika hafla fupi iliyofanyika Wilayani Muleba, Mkoani Kagera. (23.10.2020)

Mkurugenzi Msaidizi, Kitengo cha Huduma za Ugani za Uvuvi, Anthony Dadu akifafanua jambo katika hafla fupi ya kukabidhi Injini za Boti kwa Vyama vya Ushirika vya Wavuvi Kanda ya Ziwa Victoria iliyofanyika Wilayani Muleba, Mkoani Kagera. (23.10.2020)

Mkazi wa Kasenyi, Ikuza, Wilayani Muleba, Mkoani Kagera, Edgar Katunzi akiuliza swali kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (hayupo pichani) katika hafla fupi ya kugawa Injini za Boti kwa Vyama vya Ushirika vya Wavuvi Kanda ya Ziwa Victoria iliyofanyika Wilayani Muleba, Mkoani Kagera. Wengine katika picha ni Sehemu ya Wananchi wanaofanya shughuli za Uvuvi Mkoani humo. (23.10.2020)

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Bw. Omary Mchengule akizungumza katika hafla fupi ya kugawa Injini za Boti kwa Vyama vya Ushirika vya Wavuvi Kanda ya Ziwa Victoria iliyofanyika Wilayani Muleba, Mkoani Kagera. Kulia kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah na kushoto kwake ni Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Uvuvi, Stephen Lukanga. (23.10.2020)

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi na Wawakilishi wa Vyama vya Ushirika vya Wavuvi Kanda ya Ziwa Victoria muda mfupi baada ya kukabidhi Injini za Boti kwa Vyama (4) vya Ushirika wa Wavuvi wilayani Muleba, Mkoani Kagera. Kutoka kulia waliokaa ni Mkurugenzi Msaidizi, Kitengo cha Huduma za Ugani za Uvuvi, Anthony Dadu akifuatiwa na Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Utafiti na Mafunzo ya Uvuvi, Dkt. Erastus Mosha. Kutoka kushoto ni Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Omary Mchengule akifuatiwa na Kaimu Mwenyekiti Chama cha Ushirika cha Wavuvi Zilagula, Bi. Agness Mbasha. (23.10.2020)



PROF. GABRIEL AFUNGA MAFUNZO YA SIKU MBILI YA WAKAGUZI WA VYAKULA VYA MIFUGO

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Uendelezaji Maeneo ya Malisho na Rasilimali za vyakula vya Mifugo (WMUV), Bw. Rodgers Shengoto akitoa maelezo mafupi kwa Mgeni Rasmi kuhusu mada zilizowasilishwa katika mafunzo hayo ya siku mbili ya wakaguzi wa vyakula vya Mifugo kwa Kanda ya Mashariki na Kati, yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) mkoani Morogoro. (23.10.2020)

Washiriki wa mafunzo ya ukaguzi wa vyakula vya Mifugo wakisikiliza kwa makini mgeni rasmi ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (hayupo pichani) wakati akifunga mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), mkoani Morogoro. (23.10.2020)

Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo (WMUV), Dkt. Asimwe Rwiguza akitoa taarifa fupi kwa mgeni rasmi kuhusu mafunzo ya siku mbili ya wakaguzi wa Vyakula vya Mifugo wakati wa kufunga mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) mkoani Morogoro. (23.10.2020)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa hotuba ya kufunga mafunzo ya siku mbili ya wakaguzi wa vyakula vya Mifugo Kanda za Mashariki na Kati, yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Kilimo Sokoine (SUA) mkoani Morogoro. (23.10.2020)

Mshiriki wa mafunzo ya siku mbili ya wakaguzi wa vyakula vya Mifugo Kanda ya Mashariki na Kati, Bi. Odetha Mchunguzi akitoa neno la shukrani kwa Mgeni Rasmi kwa niaba ya wenzake, wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo, yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) mkoani Mororgoro. (23.10.2020)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akimvalisha kitambulisho mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya siku mbili ya wakaguzi wa Vyakula vya Mifugo kwa Kanda ya Mashariki na Kati yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) mkoani Morogoro. (23.10.2020)






 

Ijumaa, 23 Oktoba 2020

SAUTI YETU WIKI HII


 

WATUMISHI WATAKIWA KUZIFAHAMU SHERIA NA TARATIBU ZA UTUMISHI WA UMMA.

 Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Zachariyya Kera amewataka watumishi wa umma kujijengea tabia ya kusoma katiba na sheria za kiutumishi ili kuzifahamu sheria na haki zao za msingi.

 

Akiongea wakati alipotembelea ofisi za Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) (20.10.2020) zilizopo Mkoani Pwani, akiambatana na baadhi ya viongozi waandamizi wa wizara hiyo sekta ya mifugo, Bw. Kera ametoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwataka  wafanyakazi kujua haki zao za msingi na kufuatilia kwa wakati.

 

"Watumishi waelimishwe kuhusu haki zao na wapate stahiki zao kwa wakati na kujijengea tabia ya kusoma sheria na taratibu za kiutumishi ili wasipitwe na mambo mengi." alisema Bw. Kera.

 

Katika ziara hiyo ya baadhi ya viongozi waandamizi wa Wizara ya Mifugo na uvuvi sekta ya mifugo, walipata pia fursa ya kutembelea kituo cha uhimilishaji kanda ya mashariki (kibaha) kilichopo Mkoani humo na Shamba la Malisho Vikuge kujifunza shughuli mbalimbali zinazofanywa na kituo pamoja na shamba hilo.

 

Meneja wa Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI), Dkt. Stella Bitanyi amesema chanjo ni muhimu sana kwa mifugo kwani huboresha afya za mifugo na mfugo ukiwa na afya nzuri hata afya ya binadamu huimarika pale atumiapo, chanjo zinaongeza pato la taifa kwani huzalishwa na kuuzwa.

 

Aidha, Dkt. Bitanyi ametumia nafasi hiyo kuwaeleza watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na upungufu wa vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi kwani wanatumia teknolojia ya chini sana katika utendaji wao wa kazi.

 

Hata hivyo ameshauri kuwe na utaratibu wa kutoa elimu kwa wataalam ya namna ya kutumia Chanjo kwani wengi hukosea na kuchanja maeneo yasiyostahili.

 

"Elimu ya uchanjaji inahitajika kwa wingi kwa wataalam wetu kwani wanachanja shingoni badala ya kuchanja nyuma ya kwapa kwenye ngozi." Alisisitiza Dkt. Stella.

 

 Mkuu wa kituo cha uhimilishaji kanda ya Mashariki (Kibaha), Bw. Anzigary Kasanga Balaka ameeleza kazi wanazofanya ikiwa ni pamoja na kuzalisha mbegu bora za madume na kuuza, kutoa ushauri kwa wafugaji na kuboresha mifugo yao kwa uhimilishaji, kuratibu Mafunzo ya uhimilishaji na kuuza vitendea kazi vya uhimilishaji kama mitungi ya gesi.

 

Aidha, Viongozi wa TVI, Kituo cha Uhimilishaji na Shamba la Malisho Vikuge waliishukuru serikali ya awamu ya tano kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuendelea kuona umuhimu wa shughuli wanazofanya na kuwatembelea kujionea mazingira ya watumishi wao na changamoto wanazopitia katika maeneo yao ya kazi na kuzitafutia ufumbizi.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu (WMUV), Bw. Zachariyya Kera (kulia) akitoa ufafanuzi wa hatua na namna mtumishi anavyopandishwa cheo kwa watumishi wa Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) walipotembelea kituo hicho wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani. (20/10/2020)

Mkurugenzi wa Manunuzi na Ugavi (WMUV), Bw. Emanuel Mayage akipata ufafanuzi wa namna ya kutengeneza chanjo mbalimbali kutoka kwa Meneja wa Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI), Dkt. Stella Bitanyi walipotembelea Taasisi hiyo mkoani Pwani. (20.10.2020)

Meneja wa Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI), Dkt. Stella Bitanyi akitoa taarifa ya Taasisi hiyo kwa watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) juu ya namna wanavyofanya kazi na mafanikio waliyopata hadi sasa walipotembelea Taasisi hiyo mkoani Pwani. (20.10.2020)





Jumanne, 20 Oktoba 2020

DKT. TAMATAMAH AKABIDHI VIPANDE VYA KAMBA 700,000 KWA WAKULIMA WA MWANI

 Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah amekabidhi vipande vya kamba za manila 700,000 kwa wakulima wa mwani katika Kijiji cha Songosongo, wilayani Kilwa, mkoa wa Lindi.

 

Akizungumza na wananchi wa Songosongo jana (19/10/2020) Dkt. Tamatamah amesema serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) imetoa kamba hizo ili kuwawezesha wakulima wa mwani kwani kamba ilikuwa ni moja ya changamoto waliyokuwa wakikabiliana nayo.

 

Kamba hizi za manila (ambazo kila moja ina urefu wa mita 10) katika kilimo cha mwani, hufungwa katika vigingi na hutumika kwa ajili ya kuoteshea mwani ambapo mwani hufungwa katika kamba hizo zinazosaidia pia mwani kutochukuliwa na maji ya bahari pale panapokuwepo na wimbi.

 

Dkt. Tamatamah amesema duniani kote kwa sasa mwani unalimwa kibiashara, hivyo mwani ni moja ya zao linalopewa kipaumbele katika wizara. Katika kilimo cha mwani wakulima wanakutana na changamoto mbalimbali zikiwemo za ukosefu wa mitaji na masoko.

 

“Wizara kupitia sekta ya uvuvi imeanza kutoa kamba ambazo ni moja ya pembejeo muhimu kwa wakulima wa mwani ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha wakulima hao kwa kuwapunguzia sehemu ya gharama za uzalishaji ili baadae waweze kusimama wenyewe,” alisema Dkt. Tamatamah.

 

Pia amesema kuwa kama wakulima watalima vizuri katika kamba moja ya mita kumi katika bamvua nne (miezi miwili) wanaweza kupata kati ya kilo 8-10, na kamba hizo walizopewa zinaweza kutumika kwa mwaka mzima. Lengo la wizara ni kusambaza kamba hizi kwa wakulima wa mwani maeneo yote Tanzania Bara.

 

Dkt. Tamatamah amesema kuwa ipo changamoto ya soko la mwani hasa kwenye bei kwani kwa sasa asilimia 90 ya mwani inauzwa nje ikiwa ghafi na ni asilimia 10 tu ndio inayotumika hapa nchini.

 

Hivyo wizara kwa sasa inawahamasisha wakulima kujiunga katika vikundi na kuwaunganisha na taasisi za kifedha ili waweze kukopesheka na waweze kuanzisha viwanda vidogo vya kuchakata mwani ili kuuongezea thamani. Hii itasaidia kupunguza kiasi cha asilimia ya mwani inayokwenda nje ya nji ikiwa ghafi na kusaidia kuongeza ajira.

 

Aidha, Katibu Mkuu Tamatamah amesema zao la mwani linazo faida kubwa ikiwa ni pamoja na kuongeza kipato katika jamii za maeneo ya pwani hasa kwa akina mama, inaodoa umaskini lakini pia linaingiza fedha za kigeni.

 

Naye mkulima wa mwani, Bi. Mbimbisa Omary amemshukuru Katibu Mkuu Tamatamah kwa kuwaletea vitendea kazi kwa ajili ya kilimo cha mwani. Bi. Mbimbisa amesema kilimo cha mwani kinawasaidia mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuwasomesha Watoto, kununua chakula pamoja na ujenzi wa nyumba.

 

Bi. Jaka Farahani ambaye ni mkulima wa mwani amesema changamoto ya masoko inawasumbua sana hasa pale wanunuzi wanaowategemea wasiponunua hivyo ameiomba wizara kuwasaidia kutatua changamoto hiyo. Lakini pia amemuomba Katibu Mkuu kuendelea kuwapelekea kamba nyingi zaidi kwa kuwa eneo la kulima ni kubwa na wakulima wapo wengi.

 

Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji (WMUV), Dkt. Nazael Madalla amesema wizara kupitia idara yake inaendelea kuhamasisha kampuni kuendelea kuchukua leseni kwa ajili ya kununua mwani na mpaka sasa zipo kampuni 7. Lengo la kuwa na kampuni nyingi ni kuongeza ushindani hivyo kampuni zinahamasishwa kujisajili ili zitambulike na ziweze kufanya biashara ya mwani.

 

Zao la mwani hapa nchini Tanzania lilianza kulimwa miaka ya 1980 na lilianzishwa katika kisiwa cha Zanzibar. Baada ya kufanikiwa katika kipindi cha majaribio, miaka ya 1990 mpaka 2000 Tanzania hususani Zanzibar ilikuwa ni nchi ya kwanza duniani kwa uzalishaji wa mwani. Lakini kutokana na changamoto mbalimbali kwa sasa Tanzania ni nchi ya tatu kwa uzalishaji wa mwani ambapo nchi ya kwanza ni Ufilipino ikifuatiwa na Indonesia.

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akiongozana na baadhi ya wakulima wa mwani baada ya kumaliza kutembelea moja ya shamba katika kijiji cha Songosongo, wilayani Kilwa. (19.10.2020)

Bi. Mbimbisa Omary ambaye ni mkulima wa mwani akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wakulima wa mwani wa kijiji cha Songosongo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (aliyevaa tisheti nyeusi) kutokana na wakulima hao kupatiwa kamba 700,000 na Wizara ya Mifugo na Uvuvi - Sekta ya Uvuvi. (19.10.2020)

Bi. Mbimbisa Omary ambaye ni mkulima wa mwani akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wakulima wa mwani wa kijiji cha Songosongo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (aliyevaa tisheti nyeusi) kutokana na wakulima hao kupatiwa kamba 700,000 na Wizara ya Mifugo na Uvuvi - Sekta ya Uvuvi. (19.10.2020)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akizungumza na wakulima wa mwani pamoja na wananchi wa kijiji cha Songosongo wilayani Kilwa (hawapo pichani) wakati alipokwenda kukabidhi kamba kwa wakulima hao. (19.10.2020)

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Songosongo waliofika kwenye mkutano kumsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah wakati alipotembelea Kijiji hicho kwa ajili ya kugawa kamba kwa wakulima wa mwani. (19.10.2020)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kulia) akimkabidhi kamba kwa ajili ya wakulima wa mwani Mwenyekiti wa kijiji cha Songosongo, Bw. Swaluya Sadi (kushoto). Dkt. Tamatamah amekabidhi jumla ya kamba 700,000 zoezi lililofanyika katika kijiji cha Songosongo, wilayani Kilwa. Katikati ni Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji (WMUV), Dkt. Nazael Madalla. (19/10/2020)

Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji (WMUV), Dkt. Nazael Madalla, akizungumza na baadhi ya akina mama wakulima wa mwani, baada ya zoezi la Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) kukabidhi kamba 700,000 kwa wakulima hao katika kijiji cha Songosongo, wilayani Kilwa. (19.10.2020)







 

Jumapili, 11 Oktoba 2020

SEKTA YA UVUVI INATOA ASILIMIA 30 YA PROTINI KWENYE LISHE - DKT. TAMATAMAH

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah amewataka wafugaji na wavuvi nchini kuacha kufanya kazi zao kwa mazoea na badala yake watumie njia za kisasa na kitaalam katika utekelezaji wa shughuli hizo.

 

Dkt. Tamatamah aliyasema hayo alipokuwa akiwasilisha taarifa za Sekta za Mifugo na Uvuvi wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula duniani uliofanyika leo (10.10.2020) mkoani Njombe.

 

Katika taarifa yake Dkt. Tamatamah alisema Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatambua umuhimu wa lishe bora kwa wananchi hususan wazee na watoto hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa nyama na samaki ni vyakula vinavyotoa protini kwa wingi zaidi ukilinganisha na vyakula vingine.

 

"Mhe. Mgeni rasmi sekta ya uvuvi inachangia asilimia 30 ya protini inayotokana na wanyama huku ikichangia ajira kwa Watanzania takribani Milioni 4.5 katika shughuli mbalimbali za sekta hiyo" Alisema Dkt.Tamatamah.

 

Aidha aliongeza kuwa uzalishaji wa samaki kwa upande wa maji ya asili umefikia kiasi cha takribani tani 497,567 huku kwa upande wa uzalishaji viumbe maji ukifikia kiasi cha takribani tani 18,716.36.

 

Kwa upande wa Mifugo Dkt. Tamatamah alisema kuwa sekta hiyo imechangia ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia lishe bora, ajira, kipato cha mtu mmoja mmoja na fedha za kigeni ambapo kwa mwaka 2019/20 ilichangia pato la taifa kwa asilimia 7.4 na kukua kwa asilimia 5 ikilinganishwa na asilimia 4.9 kwa mwaka 2018/19.

 

"Nihitimishe taarifa yangu kwa kutoa rai kwa wananchi kuongeza ulaji wa bidhaa zitokanazo na mifugo na uvuvi ili kufikia kiwango kilichosimikwa na shirika la chakula la duniani (FAO)" Alimalizia Dkt. Tamatamah.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akiwasilisha taarifa ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye uzinduzi wa Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani uliofanyika Mkoani Njombe. (10.10.2020)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt.Rashid Tamatamah (kulia) akifafanua jambo kwenye banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mgeni rasmi ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba (kushoto) alipotembelea banda la wizara hiyo kwenye  uzinduzi  wa Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula duniani. (10.10.2020)

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Dkt. Elifatio Towo (kulia) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba (kushoto) alipotembelea banda la taasisi hiyo kwenye Uzinduzi wa Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani. Katikati ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt.Rashid Tamatamah. (10.10.2020). 

Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Mhe. Andrea Tsere (wa pili kutoka kulia) akielezea jambo mbele ya Mgeni rasmi – Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba (kushoto) na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt.Rashid Tamatamah (wa tatu kutoka kulia) walipofika kwenye banda la Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwenye Uzinduzi wa Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani. (10.10.2020).


 




PROF. GABRIEL: OGESHENI MIFUGO YENU ILI KUIKINGA NA MAGONJWA

Wafugaji hapa nchini wametakiwa kuogesha mifugo yao ili kuikinga na magonjwa yaenezwayo na kupe.

 

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel jana tarehe 10.10.2020 wakati akizindua awamu ya tatu ya kampeni ya uogeshaji mifugo iliyofanyika katika Kijiji cha Bahi Sokoni, wilayani Bahi, mkoani Dodoma.

 

Prof. Gabriel amesema lengo kuu la kampeni hizi ni kuhamasisha wafugaji wote nchini kuunga mkono juhudi za serikali katika kuongeza tija ya ufugaji kwa kuwa na mifugo yenye afya njema, mifugo isiyo na magonjwa ambayo itazalisha mazao zaidi na yenye ubora wa kiwango cha kitaifa na kimatifa.

 

“Lengo la uogeshaji ni kudhibiti magonjwa yaenezwayo na kupe hususani Ndigana kali (East Coast Fever – ECF), Ndigana Baridi (Anaplasmosis), Mkojo Mwekundu (Babesiosis) na Maji Moyo (Heart Water) ambayo yamekuwa yakiathiri mifugo na kusababisha hasara kubwa kwa mfugaji,” alisema Peof. Gabriel.

 

Magonjwa yaenezwayo na kupe yasipodhibitiwa ipasavyo huchangia asilimia 72 ya vifo vyote vya ng’ombe hapa nchini. Kati ya magonjwa hayo, ugonjwa wa Ndigana Kali huchangia vifo kwa kiwango kikubwa cha asilimia 44. Hasara inayotokana na magonjwa yaenezwayo na kupe inakadiriwa kuwa ni dola za kimarekani milioni 64.7 kwa mwaka sawa na takribani shilingi bilioni 145. Hasara nyingine ni pamoja na kupunguza uzalishaji wa maziwa, kupungua kwa nyama kutokana na kukonda, kushuka thamani ya Ngozi, kupoteza wanayama kazi na udumavu wa ndama.

 

Prof. Gabriel amesema serikali imenunua dawa za kuogesha mifugo aina ya Paranex, Paratop na Amitrax kiasi cha lita 15,579 zenye thamani ya shilingi 592,822,375 ambazo zinatosheleza majosho 1,983 katika halmashauri 162 na matarajio ni kifikia jumla ya michovyo 405,000,000 ya mifugo yote itakayoogeshwa.

 

Kupitia kampeni hizi, serikali imekuwa ikitoa dawa zenye ruzuku na bei elekezo za kuogeshea mifugo ambapo kwa ng’ombe ni shilingi 50, mbuzi na kondoo shilingi 10 kwa mchovyo mmoja, wafugaji wamehamasika sana kuogesha mifugo yao.

 

Pia serikali kuu, halmashauri na wadau wengine wamejenga majosho 101, kukarabati majosho 578 pamoja na kuunda kamati 1,036 zinazosimamia shughuli za uogeshaji wa mifugo katika ngazi ya josho. Vilevile imeunda timu 12 ambazo huzunguka nchi nzima kwa ajili ya kuhamasisha shughuli za uogeshaji mifugo na ufuatiliaji wa miundombinu ya mifugo.

 

Katika kudhibiti magonjwa yaenezwayo na kupe, serikali imetunga Kanuni ya Uogeshaji na Matumizi ya Viuatilifu vya Mifugo (Acaricide Applications and Management Regulations, 2019). Kanuni hii inamlazimisha mfugaji kuogesha mifugo yake mara mbili kwa mwezi na serikali itasimamia zoezi la uogeshaji kwa ujumla.

 

Katika uzinduzi huo, Prof. Gabriel alitoa maelekezo kwa wafugaji wote nchini kuhakikisha wanaogesha mifugo yao ili kuikinga na magonjwa, halmashauri zote nchini kusimamia kanuni ya uogeshaji ili wafugaji waifuate maana majosho yapo na dawa zimeshatolewa, halmashauri zote nchini kwa kushirikiana na wafugaji na wadau ziendelee kukarabati majosho yake na miundombinu mingine ya mifugo na halmashauri kuhamasisha wafugaji kuunda vi vitakavyosimamia uendeshaji endelevu wa majosho ikiwa ni pamoja na kufungua akaunti benki kwa ajili ya kuhifadhi fedha zinazokusanywa wakati wa uogeshaji mifugo.

 

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Dkt. Fatuma R. Mganga amesema mifugo katika wilaya ya Bahi imekuwa ikichangia zaidi ya asilimia 55 ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa mwaka. Lakini mifugo imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya magonjwa kama Ndigana Kali, Ndigana Baridi, Ugonjwa wa Mapafu ya ng’ombe na mbuzi na kideri cha kuku. Halmashauri imekuwa ikidhibiti magonjwa haya kwa kuogesha na kunyunyizia mifugo viuatilifu, kutoa chanjo na kutoa ushauri wa kitaalam kupitia maafisa ugani waliopo katika kata na vijiji.

 

Nao wafugaji walioleta mifugo yao kwa ajili ya kuiogesha katika uzinduzi wa kampeni hiyo ya awamu ya tatu wilayani Bahi wameishukuru serikali kwa kufufua majosho na kujenga mengine mapya pamoja na kutoa ruzuku ya madawa ya kuogeshea mifugo kwani kwa kufanya hivyo wanaimani mifugo yao hatakufa tena kutokana na magonjwa yanayosababishwa na kupe.

 

Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga amesema kuwa awamu ya kwanza ya kampeni hii ilizinduliwa tarehe 16/12/2018 wilayani Chato na awamu ya pili uzinduzi wake ulifanyika tarehe 29/10/2019 katika halmashauri ya Mpimbwe mkoani Katavi.

 

Prof. Nonga amesema katika kampeni awamu ya kwanza na awamu ya pili serikali ilinunua jumla ya lita 21,373.06 za dawa zenye thamani ya 740,714,750 kwa lengo la kuhamasisha wananchi kuogesha mifugo yao. Katika awamu zote mbili kumekuwa na jumla ya michovyo 254,375,555 ya mifugo yote ikiwemo ng’ombe 176,320,815, mbuzi 58,012,461, kondoo 20,039,594 na punda 2,685.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (mwenye koti jeupe katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Kampeni ya Uogeshaji Mifugo Kitaifa awamu ya tatu katika kijiji cha Bahi Sokoni, wilayani Bahi, mkoani Dodoma. (10.10.2020)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel akiwahutubia wananchi wa wilaya ya Bahi (hawapo pichani) kwenye uzinduzi wa Kampeni ya Uogeshaji Mifugo Kitaifa uliofanyika katika kijiji cha Bahi Sokoni, wilayani Bahi, mkoani Dodoma. (10.10.2020)

Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo (WMUV), Prof. Hezron Nonga akitoa taarifa fupi ya Kampeni ya Kitaifa ya Uogeshaji Mifugo hapa nchini kwa mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa awamu ya tatu ya Kampeni hiyo uliofanyika katika kijiji cha Bahi Sokoni, wilayani Bahi, mkoani Dodoma. (10.10.2020)

Katibu Mkuu Wizara Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyemshika ng'ombe) akishirikiana na wafugaji katika zoezi la uzinduzi wa kuogesha Mifugo Kitaifa awamu ya tatu lililofanyika katika kijiji cha Bahi Sokoni, wilayani Bahi, mkoani Dodoma. (10.10.2020)

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Dkt. Fatima Mganga (mwenye kilembe) akipokea madawa ya ruzuku ya kuogeshea Mifugo kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel kwa niaba ya wakurugenzi wa Halmashauri zote hapa nchini wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Uogeshaji Mifugo Kitaifa awamu ya tatu uliofanyika katika kijiji cha Bahi Sokoni, wilayani Bahi, mkoani Dodoma. (10.10.2020)






IDARA YA UVUVI YAHAKIKISHA RASILIMALI ZA BAHARI ZINALINUFAISHA TAIFA KIUCHUMI

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesema ukusanyaji wa takwimu za sekta ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi unalenga kutoa tathmini ya hali ya uvuvi katika ukanda huo na kuhakikisha rasilimali za bahari zinaendelea kuleta manufaa na kuchangia katika uchumi wa nchi.


Akizungumza jijini Dar es Salaam (09.10.2020) wakati wa kufunga mafunzo ya siku mbili ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani yanayohusisha maafisa uvuvi na viongozi kutoka Vikundi vya Kusimamia Rasilimali ya Uvuvi Mwaloni (BMU), kutoka Mikoa ya Dar es Salaam katika Wilaya za Kinondoni, Kigamboni na Ilala pamoja na Mkoa wa Pwani ukihusisha Wilaya za Bagamoyo na Chalinze, Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi Bw. Emmanuel Bulayi amesema maendeleo ya wananchi katika eneo hilo yanategemea sana shughuli za uvuvi.


“Kwa hiyo suala la kuchukua takwimu na kujua rasilimali ikoje kila wakati na kila muda ni suala la msingi sana ni ukweli uliowazi maendeleo ya wananchi katika hili eneo yanategemea sana shughuli za uvuvi, hivyo ni muhimu sana halmashauri na wananchi wanakuwa katika mstari wa mbele katika kuhakikisha tunaendelea na uchumi endelevu katika Ukanda wa Pwani kwa manufaa yetu na vizazi vijavyo.” Amebainisha Bw. Bulayi


Aidha, amesema taarifa zinazochukuliwa wakati wa kukusanya takwimu kwa njia ya mfumo wa kieletroniki ni pamoja na kufahamu kiwango cha samaki wanaovuliwa kwa kilo, kwa boti na kwa siku, ni suala la msingi ili baadae serikali iweze kufahamu kiasi gani cha samaki kinachovuliwa na kuweka mipango itakayosaidia mikakati mbalimbali ya maendeleo.


Pia, Bw. Bulayi amewataka wakusanya takwimu kuhakikisha wanakusanya takwimu halisia kwani bila kuzingatia hilo watalidanganya taifa, hivyo wanapaswa wafahamu jukumu kubwa walilonalo kwa ajili ya kuitumikia sekta ya uvuvi nchini.


“Takwimu ndiyo hasa tunasema ni msingi wa sekta ya uvuvi katika kuhakikisha wavuvi wanaendelea, lakini pia sekta inaendelea, lakini pia sekta tunanufaika nayo kwa hiyo bila takwimu hakuna la kuongea.” Amefafanua Bw. Bulayi


Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Emmanuel Bulayi, amewakumbusha pia washiriki wa mafunzo ya siku mbili ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani kuwa, ukusanyaji wa takwimu ya sekta ya uvuvi ni takwa la kidunia kupitia Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), lakini pia ni takwa la nchi hivyo washiriki wa mafunzo hayo wana jukumu kubwa katika ukusanyaji wa takwimu sahihi.


Amesema mafunzo ya namna hiyo yanatarajia pia kuendelea kwenye halmashauri 15 katika Ukanda wa Bahari ya Hindi, hivyo kutaka uwepo ushirikiano wa kutosha kati ya maafisa uvuvi na wadau wa sekta ya uvuvi ili kuhakikisha rasilimali za bahari zinalinufaisha taifa.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uratibu wa Sekta kutoka Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Yusuf Semuguruka, ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuandaa mafunzo hayo kwa kuwa serikali inaangalia uwepo wa Vikundi vya Kusimamia Rasilimali ya Uvuvi Mwaloni (BMU) katika kusaidia kutafuta taarifa sahihi kwa ajili ya maandalizi ya sera mbalimbali.


Bw. Semuguruka amesema TAMISEMI itafuatilia kuangalia mafunzo hayo namna yanavyowasaidia maafisa uvuvi na viongozi wa BMU katika kukusanya takwimu sahihi.


Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo ambao wamekuwa wakituma taarifa za takwimu kwa kutumia mfumo maalum wa njia ya simu ya mkononi katika ofisi za makao makuu ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), wakizungumza kabla ya kuahirishwa kwa mafunzo hayo wakiwa kwenye mwalo wa samaki katika soko la Kunduchi jijini Dar es salaam wamesema wamenufaika na mafunzo hayo yakiwemo ya namna ya kupata takwimu kwa usahihi.


Mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani yamefanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga na baadaye yatafanyika katika Mkoa wa Mtwara kwa maafisa uvuvi na Vikundi vya Kusimamia Rasilimali ya Uvuvi Mwaloni (BMU), ambao wamekuwa wakikusanya takwimu hizo.


Mafunzo hayo yamehusisha ukusanyaji wa takwimu kwa kutumia sampuli za wingi wa samaki, idadi ya uchaguzi wa aina ya vyombo na zana za uvuvi, njia za ukusanyaji takwimu ikiwemo ya kutumia mfumo wa simu ya mkononi, namna ya kupata wastani wa uzito wa samaki pamoja na kufahamishwa umuhimu wa takwimu za uvuvi nchini.


Washiriki wa mafunzo hayo wamepatiwa vifaa mbalimbali vya kukusanyia takwimu katika maeneo ya kazi zikiwemo simu za mkononi, mizani, makoti ya mvua na mabuti.


Mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani yameandaliwa kupitia mradi wa usimamizi wa samaki wanaopatikana katika tabaka la maji la juu na kati unaotekelezwa kwa ushirikiano na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO).

Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Emmanuel Bulayi akizungumza na washiriki wa mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani yaliyofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam na kusisitiza umuhimu wa kupata takwimu sahihi ili kulinda rasilimali za bahari na kuhakikisha zinakuza uchumi wa taifa. (09.10.2020)

Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Emmanuel Bulayi akionesha vifaa mbalimbali zikiwemo simu za mkononi, makoti ya mvua, mizani na mabuti ambavyo wamekabidhiwa washiriki (hawapo pichani) wa mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za sekta ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani baada ya kuhitimu mafunzo ya siku mbili jijini Dar es Salaam. (09.10.2020)

Mkurugenzi wa Uratibu wa Sekta kutoka Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Yusuf Semuguruka, akizungumza na washiriki (hawapo pichani) wa mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani yaliyofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam na kubainisha kuwa TAMISEMI itahakikisha inafuatilia ili kufahamu namna mafunzo hayo yanavyoleta tija kwa maafisa uvuvi na viongozi wa BMU’s. (09.10.2020)

Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Emmanuel Bulayi na Mkurugenzi wa Uratibu wa Sekta kutoka Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Yusuf Semuguruka wakikabidhi vifaa vya kukusanyia takwimu kwa washiriki zikiwemo simu za mkononi, mizani, makoti ya mvua na mabuti. (09.10.2020)

Afisa Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani Bi. Antonia Mpemba, akionesha na kuwaelezea washiriki wenzake (hawapo pichani) wa mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani namna mfumo wa kukusanya taarifa kwa kutumia simu ya mkononi unavyofanya kazi. (09.10.2020)

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani wakipima uzito wa samaki kama sehemu ya mafunzo waliyopata, wakati walipotembelea soko la samaki katika mwalo wa Kunduchi jijini Dar es Salaam. (09.10.2020)

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani walipata fursa ya kufanya mahojiano na wavuvi waliokuwa wakitoka baharani kuvua samaki kama sehemu ya mafunzo waliyopata ya kufahamu mahali ambapo mvuvi amevua samaki na muda aliotumia kuwa baharini, wakati walipotembelea soko la samaki katika mwalo wa Kunduchi jijini Dar es Salaam. (09.10.2020)

Picha ya pamoja ya washiriki wa mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani wakiwa na baadhi ya maafisa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, mara baada ya kumaliza masomo ya vitendo katika mwalo wa Kunduchi jijini Dar es Salaam. (09.10.2020)










Ijumaa, 9 Oktoba 2020

SAUTI YETU WIKI HII


 

TAKWIMU SAHIHI ZA UVUVI, CHANZO KIKUU CHA KUTUNGA SERA NA MIPANGO YA MAENDELEO NCHINI

Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Idara ya Maendeleo ya Uvuvi imesema ni muhimu kuwa na watu wenye uelewa wa kukusanya takwimu za uvuvi ili kuhakikisha watunga sera wanakuwa na vigezo mbalimbali vya kutunga sera na mipango ya maendeleo nchini.

 

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo (08.10.2020) katika mafunzo ya siku mbili ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani yanayohusisha maafisa uvuvi na viongozi kutoka Vikundi vya Kusimamia Rasilimali ya Uvuvi Mwaloni (BMU), kutoka Mikoa ya Dar es Salaam katika Wilaya za Kinondoni, Kigamboni na Ilala pamoja na Mkoa wa Pwani ukihusisha Wilaya za Bagamoyo na Chalinze, Afisa Uvuvi Mwandamizi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Upendo Hamidu amesema kusipokuwa na takwimu sahihi za uvuvi ni vigumu kutunga sera pamoja na kuweka mipango ya maendeleo.

 

“Ili kuhakikisha kwamba takwimu za uvuvi zinakusanywa na zinatoa yale matunda ambayo yanategemewa na wizara inayatimiza, katika suala la takwimu kama hauna watu wenye uelewa wa kuzikusanya maana yake hauwezi kuzipata takwimu, lakini kama pia hakuna vifaa vya kukusanyia takwimu bado hauwezi kukusanya takwimu kwa ufasaha, mafunzo haya yamelenga katika uelewa wa kukusanya takwimu.” Amefafanua Bi. Hamidu.

 

Aidha, amesema mafunzo hayo yamelenga kujenga uelewa wa ukusanyaji takwimu lakini pia kupitia mafunzo hayo washiriki watapata fursa ya kupatiwa vifaa vitakavyowasaidia kukusanya takwimu halisi.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uratibu wa Sekta kutoka Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Yusuf Semuguruka, amesema siku za nyuma takwimu hazikuwa sahihi kutokana na utaratibu wa ukusanyaji wa taarifa na kutaka kuwepo na uhalisia katika ukusanyaji wa takwimu za uvuvi kwa kutumia vifaa sahihi.

 

Bw. Semuguruka amesema ofisi yake ina wajibu wa kuwasimamia viongozi wa serikali za mitaa wakiwemo viongozi wa ngazi za chini BMU’s, ambapo amefafanua wakati wa kutunga sera ni muhimu kuwa na takwimu sahihi na zisizo za kufikiria bali zinazofanana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ili kuwezesha taifa kuwa na taarifa sahihi kwa kutumia vifaa vinavyokubalika katika ukusanyaji wa taarifa.

 

Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani, ambao wamekuwa wakituma taarifa za takwimu kwa kutumia mfumo maalum wa njia ya simu ya mkononi katika Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), wamesema mafunzo yamekuwa na umuhimu mkubwa katika kuhakikisha wanaboresha njia mbalimbali za ukusanyaji wa taarifa.

 

Mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani yanafanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga na baadaye yatafanyika katika Mkoa wa Mtwara kwa maafisa uvuvi na Vikundi vya Kusimamia Rasilimali ya Uvuvi Mwaloni (BMU), ambao wamekuwa wakikusanya takwimu hizo.

 

Mafunzo hayo yanahusisha ukusanyaji wa takwimu kwa kutumia sampuli za wingi wa samaki, idadi ya uchaguzi wa aina ya vyombo na zana za uvuvi, njia za ukusanyaji takwimu ikiwemo ya kutumia mfumo wa simu ya mkononi, namna ya kupata wastani wa uzito wa samaki pamoja na kufahamishwa umuhimu wa takwimu za uvuvi nchini.

 

Mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani yameandaliwa kupitia mradi wa usimamizi wa samaki wanaopatikana katika tabaka la maji la juu na kati unaotekelezwa kwa ushirikiano na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO).

Afisa Uvuvi Mwandamizi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Upendo Hamidu akifafanua umuhimu wa takwimu za uvuvi kwa washiriki wa mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani yanayofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam. (08.10.2020)

Mkurugenzi wa Uratibu wa Sekta kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Bw. Yusuf Semuguruka, akiwaeleza washiriki wa mafunzo (hawapo pichani) namna TAMISEMI inavyowasimamia viongozi wa serikali za mitaa na wale wa BMU’s ili kuhakikisha wanakusanya takwimu sahihi. Mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani yanafanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam. (08.10.2020)

Washiriki wa mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani, wakiwemo maafisa uvuvi na viongozi kutoka Vikundi vya Kusimamia Rasilimali ya Uvuvi Mwaloni (BMU), katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani wakifuatilia mada mbalimbali juu ya ukusanyaji takwimu na umuhimu wa takwimu za uvuvi nchini. (08.10.2020)

Mchambuzi wa mifumo ya kompyuta kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Bw. Innocent Sailale akiwaelezea washiriki wa mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani, namna taasisi hiyo inavyokusanya taarifa za takwimu kupitia mfumo wa kompyuta kutoka katika simu za mkononi. (08.10.2020)





Alhamisi, 8 Oktoba 2020

MAAFISA UGANI WA SINGIDA NA DODOMA WAPATIWA MAFUNZO REJEA KUHUSU UFUGAJI WENYE TIJA.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa mafunzo rejea kwa maafisa ugani kutoka mikoa ya Singida na Dodoma ili kuwawezesha wagani hao kwenda kutoa elimu kwa wafugaji.

 

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani, Dkt. Angello Mwilawa amesema wizara imekua ikitekeleza mikakati muhimu katika sekta ya mifugo ili kuweza kumsaidia mfugaji kufuga kisasa na kibiashara.

 

Mikakati hiyo ni pamoja na Uboreshaji wa Koosafu za mifugo nchini, Udhibiti wa magonjwa, Upatikanaji wa uhakika wa malisho na maji katika maeneo yaliyo na mifugo, Kuboresha uzalishaji ulio wa kibiashara na ustawishaji wa ndege wafugwao, Kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa migogoro ya ardhi, Kuhamasisha na kuanzisha vyama vya ushirika vya wafugaji na Kudhibiti upotevu wa mapato yatokanayo na mifugo pamoja na mazao yake.

 

Dkt. Mwilawa amesema katika kutekeleza mikakati hiyo wizara imekua ikipata changamoto nyingi ambazo ni ukosefu wa maarifa kwa wafugaji na ndio maana wizara imeamua kutoa mafunzo rejea kwa maafisa ugani ili waweze kwenda kuwaelimisha wafugaji walioko katika mikoa yao.

 

Katika kutekeleza mikakati hiyo maafisa ugani wametakiwa kwenda kushirikiana na sekta na wadau wengine waliopo katika maeneo yao ili kuhakikisha wafugaji wanapata elimu hii na kuweza kufuga kwa tija.

 

Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo na  Mshauri wa mifugo kutoka sekretarieti ya mkoa wa Singida, Dkt. David Mluma  ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kutoa mafunzo  rejea kwa kuwapatia ujuzi katika sekta ya mifugo.

 

Dkt. Mluma amesema mafunzo haya yamekuja muda mzuri kwani serikali kwa sasa inaendelea kuhamasisha wafugaji kuboresha koosafu za mifugo ili wafugaji waweze kuzalisha kwa tija. Lakini pia wamekumbushwa suala la udhibiti wa magonjwa ambalo usimamizi wake unasaidia mazao ya mifugo kuuzwa ndani na nje ya nchi.

 

Afisa Mifugo kutoka Halmashauri ya Kondoa Mji, Semeni Mwakasege amesema mafunzo haya yamemsaidia kutambua sheria mbalimbali ambazo hapo awali hakudhani kama zinawahusu, hivyo ameahidi kwenda kuwaelimisha wataalamu wenzake pamoja na viongozi wa halmashauri ili wote kwa pamoja waweze kuzisimamia.

 

Pia ametoa wito kwa washiriki wenzake kuhakikisha kila mmoja anakwenda kutoa elimu waliyoipata kwa wataalam wenzao na wafugaji. Vilevile ameiomba wizara ya Mifugo na Uvuvi na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kuongeza wigo wa mafunzo haya ili wataalam wengi wa mifugo waweze kupata mafunzo haya ambayo yatasaidia kusambaza elimu hii kwa wafugaji wengi zaidi.

 

Mafunzo haya yametolewa kwa maafisa ugani 20 kutoka mikoa ya Singida na Dodoma na yamefanyika katika ukumbi wa chuo cha Mipango jijini Dodoma. Katika mafunzo hayo washiriki wameweza kupitishwa katika mada za Sheria Kanuni na Miongozo ya sekta ya mifugo, Udhibiti wa Magonjwa na matumizi ya dawa na viwatilifu, Sumukuvu, Madhara na namna ya kudhibiti, Mashamba darasa ya malisho na ustawishaji wa matunzo ya nyanda za malisho pamoja na uboreshaji wa koosafu za mifugo kwa ufugaji endelevu na tija.