Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Idara ya Maendeleo ya Uvuvi imesema ni muhimu kuwa na watu wenye uelewa wa kukusanya takwimu za uvuvi ili kuhakikisha watunga sera wanakuwa na vigezo mbalimbali vya kutunga sera na mipango ya maendeleo nchini.
Akizungumza jijini Dar es
Salaam leo (08.10.2020) katika mafunzo ya siku mbili ya ukusanyaji wa takwimu
za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani yanayohusisha maafisa
uvuvi na viongozi kutoka Vikundi vya Kusimamia Rasilimali ya Uvuvi Mwaloni
(BMU), kutoka Mikoa ya Dar es Salaam katika Wilaya za Kinondoni, Kigamboni na
Ilala pamoja na Mkoa wa Pwani ukihusisha Wilaya za Bagamoyo na Chalinze, Afisa
Uvuvi Mwandamizi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Upendo Hamidu amesema
kusipokuwa na takwimu sahihi za uvuvi ni vigumu kutunga sera pamoja na kuweka
mipango ya maendeleo.
“Ili kuhakikisha kwamba
takwimu za uvuvi zinakusanywa na zinatoa yale matunda ambayo yanategemewa na
wizara inayatimiza, katika suala la takwimu kama hauna watu wenye uelewa wa
kuzikusanya maana yake hauwezi kuzipata takwimu, lakini kama pia hakuna vifaa
vya kukusanyia takwimu bado hauwezi kukusanya takwimu kwa ufasaha, mafunzo haya
yamelenga katika uelewa wa kukusanya takwimu.” Amefafanua Bi. Hamidu.
Aidha, amesema mafunzo hayo
yamelenga kujenga uelewa wa ukusanyaji takwimu lakini pia kupitia mafunzo hayo
washiriki watapata fursa ya kupatiwa vifaa vitakavyowasaidia kukusanya takwimu
halisi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Uratibu wa Sekta kutoka Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Yusuf Semuguruka, amesema siku za nyuma
takwimu hazikuwa sahihi kutokana na utaratibu wa ukusanyaji wa taarifa na
kutaka kuwepo na uhalisia katika ukusanyaji wa takwimu za uvuvi kwa kutumia
vifaa sahihi.
Bw. Semuguruka amesema ofisi
yake ina wajibu wa kuwasimamia viongozi wa serikali za mitaa wakiwemo viongozi
wa ngazi za chini BMU’s, ambapo amefafanua wakati wa kutunga sera ni muhimu
kuwa na takwimu sahihi na zisizo za kufikiria bali zinazofanana na Ofisi ya
Taifa ya Takwimu (NBS) ili kuwezesha taifa kuwa na taarifa sahihi kwa kutumia
vifaa vinavyokubalika katika ukusanyaji wa taarifa.
Kwa upande wao baadhi ya
washiriki wa mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi
katika Ukanda wa Pwani, ambao wamekuwa wakituma taarifa za takwimu kwa kutumia
mfumo maalum wa njia ya simu ya mkononi katika Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi
Tanzania (TAFIRI), wamesema mafunzo yamekuwa na umuhimu mkubwa katika
kuhakikisha wanaboresha njia mbalimbali za ukusanyaji wa taarifa.
Mafunzo ya ukusanyaji wa
takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani yanafanyika
katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga na baadaye yatafanyika katika
Mkoa wa Mtwara kwa maafisa uvuvi na Vikundi vya Kusimamia Rasilimali ya Uvuvi Mwaloni
(BMU), ambao wamekuwa wakikusanya takwimu hizo.
Mafunzo hayo yanahusisha
ukusanyaji wa takwimu kwa kutumia sampuli za wingi wa samaki, idadi ya uchaguzi
wa aina ya vyombo na zana za uvuvi, njia za ukusanyaji takwimu ikiwemo ya
kutumia mfumo wa simu ya mkononi, namna ya kupata wastani wa uzito wa samaki
pamoja na kufahamishwa umuhimu wa takwimu za uvuvi nchini.
Mafunzo ya ukusanyaji wa
takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani yameandaliwa
kupitia mradi wa usimamizi wa samaki wanaopatikana katika tabaka la maji la juu
na kati unaotekelezwa kwa ushirikiano na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani
(FAO).
Afisa Uvuvi Mwandamizi kutoka
Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Upendo Hamidu akifafanua umuhimu wa takwimu za
uvuvi kwa washiriki wa mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao
ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani yanayofanyika kwa siku mbili jijini Dar es
Salaam. (08.10.2020)
Mkurugenzi wa Uratibu wa
Sekta kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Bw. Yusuf Semuguruka, akiwaeleza
washiriki wa mafunzo (hawapo pichani) namna TAMISEMI inavyowasimamia viongozi
wa serikali za mitaa na wale wa BMU’s ili kuhakikisha wanakusanya takwimu
sahihi. Mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika
Ukanda wa Pwani yanafanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam. (08.10.2020)
Washiriki wa mafunzo ya
ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani,
wakiwemo maafisa uvuvi na viongozi kutoka Vikundi vya Kusimamia Rasilimali ya
Uvuvi Mwaloni (BMU), katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani wakifuatilia mada
mbalimbali juu ya ukusanyaji takwimu na umuhimu wa takwimu za uvuvi nchini.
(08.10.2020)
Mchambuzi wa mifumo ya
kompyuta kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Bw. Innocent
Sailale akiwaelezea washiriki wa mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji
wa mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Pwani, namna taasisi hiyo inavyokusanya
taarifa za takwimu kupitia mfumo wa kompyuta kutoka katika simu za mkononi.
(08.10.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni