Wataalamu Wizara ya Mifugo na Uvuvi wamekutana kwa ajili ya kujadili Mifumo inayopendekezwa katika kuanzisha Kitengo cha Ufuatiliaji wa Taarifa za Masoko ya Mifugo na Mazao yake ikiwa ni njia mojawapo ya kuwasaidia wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo kujua nini kinatokea katika masoko, pamoja na kuisaidia serikali kufanya maamuzi kuhusiana na masoko ya mifugo.
Akizungumza, leo Septemba 04, 2024, mkoani Morogoro katika kikao cha kujadili Mifumo inayopendekezwa katika kuanzisha Kitengo cha Ufuatiliaji wa Taarifa za Masoko ya Mifugo na Mazao yake, Mkurugenzi Msaidizi Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe, Dkt. Nyamizi Bundala, amesema mafunzo haya yana lengo la kujengeana uwezo kuhusu taarifa za masoko ya mifugo na mazao yake ikiwemo, upatikanaji, uchakataji na uwasilishawaji wa taarifa hizo sambamba na uanzishwaji wa dawati/kitengo mahususi kitakacho shughulikia taarifa za masoko ya mifugo na mazao yake.
"Mafunzo haya yamekuja wakati muafaka na yanaendana na dhamira ya dhati ya Serikali katika kuhakikisha Sekta zetu za uzalishaji, hususani sekta za mifugo na uvuvi, zinachangia ipasavyo katika kuinua kipato cha wananchi katika mnyororo wa thamani, kuchangia katika Pato la Taifa, kuongeza pato la fedha za kigeni, na kuimarisha uhakika na usalama wa chakula na lishe nchini. Aidha, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu masoko na kuweka mazingira wezeshi ambayo yamechangia ongezeko la biashara la mifugo hai na mazao yake " amesema Dkt. BundalaAidha,
Dkt. Bundala amesema, katika kipindi cha miaka mitatu (2021/22-2023/24), Serikali imejenga minada 51 ya kisasa ya mifugo yenye thamani ya shilingi bilioni 17.5. Minada hii imewezesha ongezeko la biashara ya mifugo nchini ambapo, thamani ya mifugo iliyouzwa katika minada imeongezeka kutoka shilingi trilioni 1.5 mwaka 2021/22 hadi trilioni 3.4 mwaka 2023/24, na hii imeleta ongezeko la mauzo ya nyama nje ya nchi kutoka tani 1,774 mwaka hadi kufikia tani 14,701 mwaka. Hivyo kufanya jumla ya tani 40,635.48 zenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 164.8 zilizouzwa nje ya nchi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Dkt. Bundala amesema kuwa, suala la kuweka mifumo ya upatikanaji wa taarifa za masoko si geni, hapa nchini kwani lilianza zamani, katika miaka ya 90, Wizara ya iliyokuwa kuwa ikisimamia mifugo kupitia mradi wa TLMP ilianzisha mfumo wa LINKS (Livestock Information Network and Knowledge System) ambayo ilikuwa ikiratibu taarifa za masoko.
Vilevile, Dkt. Bundala alisema kwa kuzingatia maendeleo ya teknolojia yaliyopo, mageuzi ya uchumi, kukua kwa masoko ya ndani, kikanda na kimataifa na uwepo wa soko huria la biashara ya bidhaa mbalimbali duniani, upatikanaji wa taarifa za masoko ya hususani ya mifugo na mazao yake kwa wakati ni suala la muhimu, ili kuwawezesha wadau kutambua fursa za masoko na biashara zilizopo, kupenyeza katika masoko mapya, kuongeza wigo wa masoko na kufanya maamuzi sahihi ya kupanga bei, kuuza au kununua bidhaa hizo kulingana na ushahidi wa taarifa.
Naye, Mwakilishi wa Shirika la ASPIRES Tanzania, Bw. Emmanuel Domonko, amesema suala la kuandaa kitengo cha Ufuatiliaji wa Taarifa za Masoko ya Mifugo ni muhimu sana kwa wafugaji, wafanyabiashara na serikali kwa ujumla kwani kitasaidia kuongeza tija katika ufugaji, na faida kwa wafugaji na wafanyabiashara na mapato kwa taifa. Pamoja na hayo, taarifa za wakati za masoko zitasaidia Wizara kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati.
Pia, Bw. Domonko amesema wao kama ASPIRES wapo katika kusaidia kuboresha mifumo ikiwemo pamoja na maboresho ya Sera za kilimo pamoja na mifugo ili kuleta mabadiliko chanya katika Sekta ya Mifugo na Uvuvi.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko, ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe, Dkt. Nyamizi Bundala, akitoa hotuba kwa washiriki wa kikao cha kujadili Mifumo inayopendekezwa katika kuanzisha Kitengo cha Ufuatiliaji wa Taarifa za Masoko ya Mifugo na Mazao yake, kilichofanyika katika Ukumbi wa Edema, Septemba 04, 2024, Morogoro