Nav bar

Ijumaa, 31 Mei 2024

MRADI WA MAZIWA FAIDA KUBORESHA MIUNDOMBINU MBALIMBALI

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe akishuhudiwa na Balozi Ireland Tanzania Mhe. Mary O’Neill amezindua miundombinu iliyojengwa kupitia mradi wa maziwa faida unaotekelezwa na kituo cha TALIRI Tanga kwa udhamini wa ubalozi wa Ireland chini ya Taasisi ya Teagacs.

Akiongea katika uzinduzi huo Shemdoe amesema Mradi wa maziwa faida mbali na kuboresha miundombinu mbalimbali lakini pia umekiwezesha kituo hicho kupata vifaa bora vya maabara kwa ajili ya kufanyia tafiti mbalimbali za mifugo na malisho bora.

Shemdoe ameendelea kueleza kuwa lengo la mradi wa maziwa faida ambao umegharimu zaidi ya Bilioni 7 ni kuboresha mnyororo wa thamani wa maziwa kwa wafugaji ambapo kituo cha TALIRI Tanga kimekuwa kikiendelea kutoa mafunzo kwa vitendo juu ya ufugaji wenye tija sambamba na kufanya tafiti mbalimbali za mifugo.

Sambamba na hayo, Shemdoe ametoa wito kwa jamii kuendelea kuzalisha na kutumia maziwa kwa wingi kwani tafiti zinaonesha kuwa watanzania tunapaswa kutumia lita 200 za maziwa kwa mwaka lakini ni kiasi cha lita 50 pekee kinatumika kwa kunywa kwa mwaka kwa watanzania wote.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Prof. Erick Komba akimshukuru Rais wa awamu ya sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha mahusiano ya kidemokrasia yaliyopelekea uwepo wa mradi huu muhimu kwa Taifa wenye kuongeza tija kwa wafugaji amesema TALIRI imejipanga vyema kuhakikisha mradi wa maziwa faida unaleta manufaa kwa wafugaji na watumiaji wa mazao ya mifugo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki, TALIRI Tanga Dkt. Zabroni Nziku akielezea mafanikio ya mradi wa maziwa faida amesema Kituo cha TALIRI Tanga kimefanikiwa kutathmini na kujua aina ya malisho bora, kuendelea kufanya tafiti za kupata ng’ombe bora, kuanzisha shamba la mfano la malisho, kuwajengea uwezo watafiti, maafisa ugani na wafugaji ambapo wadau zaidi ya 1000 wamefikiwa na kupatiwa elimu ya ufugaji bora.

Nae balozi wa Ireland Tanzania Mhe. Mary O’Neill ameipongeza TALIRI Tanga kwa namna inavyoendesha mradi huo na kuweza kufikia wadau wengi hususani wafugaji kitendo ambacho kimeleta mabadiliko makubwa kwa wafugaji hao juu ya ufugaji wenye tija.



Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi  Prof. Riziki Shemdoe (wa kwanza kulia) jana tarehe 29/05/2024 akiwa na Viongozi wa Chama na Serikali  wa Mkoa wa Tanga pamoja na Balozi wa Ireland  nchini Tanzania, amezindua Miondombinu ya majengo na vifaa vya maabara kwenye mradi wa Maziwa Faida Katika Kampasi ya TALIRI mkoani Tanga,

Alhamisi, 30 Mei 2024

MNADA WA MHUNZE KUFANYIWA UTAFITI WA KINA UWEPO WA TOPE MAJI - PROF. MUSHI

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza mchakato wa kufanya Utafiti wa kina juu ya chanzo cha tope maji yatokayo katika ardhi ndani ya mnada wa Mhunze Wilayani Kishapu ikiwa ni njia mojawapo ya kujua athari zinazoweza kujitokeza kutokana na uwepo wa hali hiyo katika eneo la ujenzi ambao unaendelea katika Mnada huo ili kuweza kutafuta suluhisho. Hii ni kufuatia hali hii kuleta taharuki kwa wafugaji na wauzaji wa mifugo kwenye mnada huo.

Akizungumza, leo Mei 29, 2024 Wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga wakati akienda kukagua hali ya eneo la mnada wa Mhunze, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Daniel Mushi amesema Wizara imeamua kufanya Utafiti wa kina ili kujiridhisha kama hali ya mnada wa Mhunze ni salama na kukabiliana na uwepo wa tope kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa watu na mifugo kwenye mnada huo.

"Leo tumekuja na wataalam kutoka Taasisi ya madini Tanzania kwa ajili ya kupima kilichotokea na kutupa taarifa, ambapo mpaka sasa wameshafanya uchunguzi wa awali na wametueleza kisayansi ni kitu gani kina sababisha matope haya na kutuhakikishia kwamba mradi wa ujenzi wa ukuta unaozunguka eneo hili na maboresho mengine yanaweza kuendelea", amesema Prof. Mushi.

Aidha, Prof. Mushi alisema Wataalamu watakapofanya uchunguzi wa kina wataeleza namna ya kukabiliana na suala hili ili yasijitokeze madhara na wataalamu wameihakikishia Wizara kuwa hakuna madhara yanayoweza kusababisha maafa katika mnada huo wa Mhunze.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Joseph Mkude amesema mbali na utafiti huo lakini pia yapo marekebisho na maboresho yanayotarajiwa kufanywa kwenye eneo hilo la mnada na maeneo ya pembezoni ili kujihakikishia usalama wa wananchi na mifugo.

Vilevile Mhe. Mkude ameishukuru sana Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuja kwa wakati na watafiti ili kufanya utafiti  baada ya kusikia jambo hili la kufurika kwa tope katika mnada wa Mhunze.

Akitoa ufafanuzi juu ya suala hilo la kufurika kwa tope katika mnada wa Mhunze, Mjiolojia kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa madini Tanzania, Bw. Sudian Chilagwile amesema, sababu iliyofanya waitwe na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuja kufanya uchunguzi kwenye eneo la mnada wa Mhunze ni uwepo wa  chemchem ya maji tope na udongo uliojaa matope ukitoka chini ya ardhi.

Bw. Chilagwile, ameweka bayana kuwa wao kama watafiti watafanya kazi ya Utafiti katika eneo hilo la mnada ili kubaini chanzo, japo utafiti wa awali wa kisayansi unaonyesha sababu ya yote ni uwepo wa mvua nyingi ambazo zimeleta athari katika miamba iliyopo aridhini ambayo imesababisha uwepo wa tope hilo, na kubainisha kuwa jambo hili haliwezi kuathiri shughuli za mnada huo kuendelea, ila watatoa ushauri kwa Wizara na wakandarasi juu ya ukarabati wa eneo hilo.


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Daniel Mushi, akizungumza katika kikao kifupi na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Joseph Mkude (hayupo pichani), baada ya kufika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, kwa ajili ya kujitambulisha na kuelezea nia na dhumuni la kufika kwake na ujio wake na Timu ya maafisa toka Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na wanajiolojia kwa ajili ya kufanya Utafiti juu ya uwepo wa tope maji katika mnada wa Mhunze, kikao kimefanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, leo Mei 29, 2024, Shinyanga.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Daniel Mushi (katikati), akimuahidi Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Joseph Mkude (kushoto), kushirikiana nae bega kwa bega katika kutatua changamoto iliyopo na kufuata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa watafiti, wakati alipofika katika mnada wa Mhunze Wilayani Kishapu kujionea hali ilivyo, leo Mei 29, 2024, Shinyanga.


Pichani ni sehemu eneo la mnada wa Mhunze lililo athiriwa na tope maji, Wilayani Kishapu - Shinyanga

VIJANA WATENGEWA BIL. 10.5 KWA AJILI YA MIRADI


Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetenga zaidi ya Shilingi Bilioni 10.5 kwa ajili ya mitaji ya miradi ya vijana ili kuwainua kiuchumi.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi amebainisha hayo (24.05.2024) jijini Mwanza, wakati wa kuhitimisha mafunzo kwa vitendo ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji awamu ya pili kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT – LIFE) ambayo imewejenga katika kujiajiri kupitia Sekta ya Uvuvi.

Mhe. Katambi amempongeza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) pamoja na viongozi wengine wa wizara kwa kusimamia vyema maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza ajira kwa vijana kupitia sekta za mifugo na uvuvi.

Ameongeza kuwa ni wakati sasa kwa vijana kutumia vyema fursa zitokanazo na sekta hizo ili kujipatia ajira na utajiri pamoja na kufuga kisasa na kuuza mazao ya mifugo na uvuvi yakiwa katika ubora unaotakiwa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema zaidi ya vijana 300 wamenufaika kupitia mafunzo hayo ya miezi mitatu kupitia vituo mbalimbali.

Prof. Shemdoe ameongeza kuwa lango la mafunzo hayo ni kuwezesha vijana kuwa wajisiriamali na wawekezaji kwenye shughuli za uvuvi na ukuzaji viumbe maji kwa kuwajengea ujuzi utakaowawezesha kubuni miradi na kuanzisha vikundi au kampuni ili waweze kujiajiri na kutoa fursa za ajira kwa wenzao.

Amebainisha kuwa awamu ya pili ya wigo wa mafunzo hayo imeongezeka tofauti ya awamu ya kwanza ambapo yalipokelewa maombi zaidi ya 1,200 ambapo inaashiria vijana wana ari ya kujiunga katika mafunzo hayo ya vitendo ambapo Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu) zinahitaji kuweka nguvu zaidi katika kuwawezesha vijana kujiajiri.

Kwa upande wake mmoja wa wanufaika wa BBT – LIFE akisoma risala kwa niaba ya vijana wenzake Bw. Muhsin Mussa amesema katika mafunzo hayo wamejifunza namna ya utunzaji wa fedha, kuunda na kusajili vikundi, maandiko ya miradi na namna ya kuiendesha pamoja na mafunzo ya vitendo kwa vijana wa Tanzania Bara na Visiwani.

Aidha, amesema mafunzo hayo wanaamini yataenda kupunguza wingi wa vijana wasio na ajira ambapo sasa wataweza kujishughulisha na uvuvi pamoja na ukuzaji viumbe maji kibiashara.


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi (mwenye tai nyekundu) akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (kulia kwake) wakiangalia moja ya vizimba vya kufugia samaki, wakati wa kuhitimisha mafunzo kwa vitendo ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji awamu ya pili jijini Mwanza kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT – LIFE). (24.05.2024)

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi (mwenye tai nyekundu) akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (kulia kwake) wakiangalia moja ya vizimba vyenye uwezo wa kufuga samaki takriban 100 na kisichogharimu zaidi ya Shilingi Laki Moja kwa ajili ya matengenezo yake, wakati wa kuhitimisha mafunzo kwa vitendo ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji awamu ya pili jijini Mwanza kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT – LIFE). (24.05.2024)


WAVUVI WATAKIWA KUTUMIA TEKNOLOJIA KUKABILIANA NA UPOTEVU WA MAZAO YA UVUVI


Naibu Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi Dkt. Edwin Mhede amewataka wadau wa uvuvi kuhakikisha wanatumia teknolojia za kisasa ambazo ni rahisi zitakazowezesha kukabiliana na changamoto ya upotevu wa mazao ya Uvuvi.

Ameyasema hayo Mei 28, 2024 wakati akifungua mkutano wa Uzinduzi wa mradi wa Asia -Africa BlueTech Superhighway ambao utachukua takribani miaka 7 (2024-2030) wenye lengo la kusaidia juhudi za Serikali katika kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi.

Mkutano huo ambao umezikutanisha nchi nne Afrika, Dkt. Edwin Mhede amesema wamejielekeza kuhakikisha wanufaika wa mradi huo wanakuwa ni wavuvi wenyewe.

Pia amesema eneo ambalo wanalifanyia kazi kwa kushirikiana na Worldfish pamoja na Taasisi za ndani  ni kuhakikisha wanakabiliana na changamoto za upotevu wa mazao ya uvuvi, pamoja na uharibifu mbalimbali unaojitokeza kwenye mnyororo wa thamani wakati watu wakivua, wakisafirisha, wakiuza na kununua samaki.

"Katika kutathimini fikra mpya za nini kifanyike zaidi ya hiki, tumejielekeza kuyagusa matatizo ya wavuvi na kujielekeza katika kufanya hivyo kuhakikisha kwamba mradi huu wanaofaidika ni wavuvi wenyewe"

"Ni matumaini yangu baada ya siku kadhaa tutakuja kuwa na kitu kikubwa sana kuweza kutusaidia kuyafikia maisha ya wengi ambayo ndiyo maelekezo lakini pia ndiyo maono ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha tunaenda kuyakuta mahitaji ya watu na tunayafanyia kazi" amesema

Dkt. Mhede amesema changamoto nyingine zinazowakabili wavuvi hao, ni pamoja na uduni wa Teknolojia , upatikanaji masoko, upatikanaji wa mitaji ya kifedha na maarifa lakini pia miundombinu

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Mohamed Sheikh, amesema Afrika ikiwemo Tanzania kunatatizo kubwa la upotevu wa mazao ya uvuvi ambapo inakisiwa kati ya asilimia 30-40 ya upotevu wa mazao hayo yanatokana na mabadiliko ya tabianchi

"Katika kipindi cha mvua inakua ni changamoto kubwa kwa wavuvi wetu hasa wale ambao wanachataka na wanasafirisha mfano, wavuvi wa dagaa wanavua na kuchakata, wanahitaji pia teknolojia mpya kwa ajili ya kusafirisha mazao yao ya uvuvi" amesema Prof. Sheikh.

Prof. Sheikh amesema Serikali ya awamu ya sita imeendelea na jitihada za kuhakikisha wanaongeza uzalishaji wa mazao hivyo amewaomba wadau mbalimbali kuweka mbinu bora ambazo zitawasaidia wavuvi kuweza kuhifadhi mazao yao ambayo yatakubalika ndani na nje ya nchi.

Naye Kiongozi wa Mawasiliano ya Kimataifa wa Taasisi ya WorldFish, Rajita Majumdar amesema kuwa zaidi ya tani 21.3 za samaki zimepotea kutokana na changamoto ya uhifadhi wa mazao hayo baada ya kuvuliwa ambapo wameona ni vyema kuja nchini kuungana na  Serikali na wavuvi kwa lengo la kupunguza upotevu huo ambao unafifisha uchumi.

"Nadhani inahitajika matumizi ya teknolojia nafuu inayoweza kufikiwa ili kuongeza umahiri katika kushughulikia mnyororo wa usambazaji wa chakula ambapo itasaidia kuondokana na uharibifu mkubwa"amesema

Aditya Parmar ambaye ametoka kwenye Taasisi ya WorldFish, amesema mradi huo umejikita katika  vipengele vinne ambavyo ni  usambazaji wa samaki, uuzaji, utunzaji, uhifadhi na usafirishaji ambapo itasaidia kwa kiasi kikubwa kutunza thamani ya ubora wa chakula kwa lengo la kuhakikisha lishe bora kwa jamii ya Pwani.

"Tunataka kuona jumuiya ya Pwani jinsi gani inaweza kuongeza mapato, tunataka kushirikisha wanawake na vijana kutekeleza mradi huu ambao tunatarajia utabadilisha maisha yao baada ya miaka michache ijayo "amesema

Mkutano huo unafuatiwa na mkutano ambao utafanyika Tarehe 5-7 mwezi Juni  mwaka huu katika ukumbi wa Mikutano Mlimani city Jijini Dar es Salaam ambao unazungumzia mahsusi wavuvi wadogo wanaochangia kwa asilimia 95.


Naibu katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede akiongea wakati wa kufungua mkutano wa  uzinduzi wa mradi wa Asia -Africa BlueTech Superhighway ambao utachukua takribani miaka 7  wenye lengo la kusaidia juhudi za serikali katika   upotevu wa mazao ya uvuvi., Mkutano huo umefanyika kwenye ukumbi wa hotel ya Ramada jijini Dar es Salaam Mei 28,2024

Mkurugenzi wa Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohamed Sheikh akiongea wakati wa  uzinduzi wa mradi wa Asia -Africa BlueTech Superhighway ambao utachukua takribani miaka 7  wenye lengo la kusaidia juhudi za serikali katika   upotevu wa mazao ya uvuvi., Mkutano huo umefanyika kwenye ukumbi wa hotel ya Ramada jijini Dar es Salaam Mei 28,2024

Mwakilishi kutoka kwenye Taasisi ya WorldFish Bw. Aditya Parmar akiwasilisha mada wakati wa mkutano wa uzinduzi wa mradi wa Asia -Africa BlueTech Superhighway   na kuelezea vipengele vinne ambavyo mradi huo umejikita  ikiwa ni pamoja na  usambazaji wa samaki, uuzaji, utunzaji, uhifadhi na usafirishaji ambapo itasaidia kwa kiasi kikubwa kutunza thamani ya ubora wa chakula kwa lengo la kuhakikisha lishe bora kwa jamii, Mei 28,2024 jijini Dar es salaam.

Naibu katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi Dkt. Edwin Mhede akiwa kwenye picha ya pamoja na sehemu ya wadau wa Sekta ya Uvuvi walioudhuria mkutano wa  uzinduzi wa mradi wa Asia -Africa BlueTech Superhighway ambao utachukua takribani miaka 7  wenye lengo la kusaidia juhudi za serikali katika   upotevu wa mazao ya uvuvi., Mkutano huo umefanyika kwenye ukumbi wa hotel ya Ramada jijini Dar es Salaam Mei 28,2024


VIJANA WA BBT – LIFE WAONESHWA VITALU, RAIS SAMIA ATAJWA KWA MCHANGO WAKE MKUBWA KWENYE SEKTA YA MIFUGO


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka historia ya kutafsiri ndoto halisi ya wingi wa mifugo nchini katika kubadilisha mfumo wa maisha kwa watanzania kupitia sekta hiyo.

Akizungumza (21.05.2024) wakati wa hafla fupi ya kuwaonesha vijana wanaohitimu mafunzo ya unenepeshaji mifugo kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT – LIFE), inayosimamiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, vitalu watakavyopatiwa kwa ajili ya ufugaji katika Ranchi za Kagoma na Kitengule zinazosimamaiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mhe. Julius Laizer amesema Mhe. Rais ameweza kuirasimisha rasmi biashara ya mazao ya mifugo kwa kuwa Sekta ya Mifugo ni muhimu katika maisha ya binadamu.

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Laizer amesema ni vigumu kutenganisha biashara yoyote inayohusu chakula cha binadamu isifanikiwe, hivyo kuwataka vijana wa BBT – LIFE kusimamia vyema ndoto na maono ya Mhe. Rais kwa kuwa wapo sehemu sahihi katika kujifunza na kufuga mifugo kibiashara.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Daniel Mushi amesema wizara inawaangalia vijana hao kama waleta mapinduzi kwenye Sekta ya Mifugo hivyo imeamua kuwaunganisha na baadhi ya benki zilizopo nchini kupata fursa za mikopo.

Ameongeza kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alianzisha programu hiyo kwa kwa kuitambua Sekta ya Mifugo kama sekta rasmi na kuwaingiza vijana kwenye ufugaji na uvuvi wa kibiashara na kwamba kila mwaka takriban vijana 1,600 wanahitimu kwenye vyuo mbalimbali vya mifugo hivyo serikali imeona haiwezi kuwaacha bila ajira bali wajifunze ufugaji kibiashara.

Aidha, amesema Mhe. Rais katika diplomasia ya kiuchumi amekuwa akizunguka nchi mbalimbali kutafuta masoko ya mazao ya mifugo na uvuvi ambapo kwa sasa nchi inahitaji wawekezaji wakubwa katika sekta hizo ili kuvipatia viwanda vilivyopo nchini mifugo kwa ajili ya kuchakatwa na kuhudumia masoko ya kimataifa, ambapo pia vijana wa BBT - LIFE wanatakiwa kuwa wawekezaji wakubwa katika Sekta ya Mifugo.

Pia, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) Bw. Bwire Mujarubi amesema kwa mujibu wa mwongozo kampuni hiyo imepewa majukumu ya kutenga vitalu kwa vijana wa BBT - LIFE, kupanga vijana hao kwenye vitalu, kuwapatia mikataba wafugaji katika ranchi za NARCO na kuwa miongoni mwa wateja wa mifugo kutoka kwa vijana wa BBT - LIFE watakaopatiwa vitalu katika ranchi hizo.

Amesema licha ya awamu ya kwanza ya BBT - LIFE kuelekea mwishoni ifikapo Tarehe 30 Mwezi Juni mwaka huu, NARCO itaendelea kuwalea vijana hao 161 ambapo kila mmoja atapatiwa hekari 10 bila kulipa gharama za upangaji katika kipindi cha miaka mitano kwenye ranchi za Kagoma hekta 311 na Kitengule hekta 2,000 zilizopo Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) Dkt. Pius Mwambene amesema kwa kipindi cha miaka miwili ambacho vijana wa BBT – LIFE wamekuwa wakipata mafunzo katika wakala hiyo wamepata uzoefu mkubwa wa kuandaa miundombinu ya mifugo pamoja na biashara ya mifugo.

Ameongeza kuwa vijana hao wakianza rasmi ufugaji hawataangaika na kwamba watakuwa wakishirikiana na wawekezaji wakubwa waliopo kwenye ranchi za NARCO, huku akibainisha kuwa wakati wa mafunzo vijana hao wamekuwa wakiuza mifugo ndani ya nchi pamoja na nchi za jirani.

Pia, amesema amesema lengo la programu hiyo ni kukuza ufugaji wa mifugo wenye tija kwa kuandaa vijana kuwa wawekezaji wakubwa kwenye sekta hiyo na kwamba programu hiyo kwa sasa itapelekwa kwenye ngazi za serikali za mikoa ili kuwanufaisha vijana wengi zaidi.

Mmoja wa vijana wanaonufaika na programu ya BBT - LIFE Bw. Posper Mugalula amesema wanashukuru kwa kupata fursa ya kushiriki mafunzo ya unenepeshaji mifugo hususan ng’ombe baada ya kumaliza elimu ya vyuo na wapo tayari kuingia rasmi katika ufugaji wa kisasa baada ya kupatiwa vitalu kwenye ranchi za NARCO.

Amewaomba vijana wenzake kushirikiana ili kufikia malengo ambayo serikali imekusudia na kuwa chachu ya vijana wengine kujiunga na mafunzo kwa awamu ya pili na kufuga kibiashara kwa kuwa Sekta ya Mifugo ina soko kubwa ndani na nje ya nchi.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikiendesha mafunzo ya unenepeshaji mifugo katika vituo vya Wakala ya Mifugo nchini (LITA) na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT – LIFE) ili kufikia maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha vijana kufanya ufugaji wenye tija katika sekta za mifugo na uvuvi.


Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kagera, wakati wa hafla fupi iliyofanyika katika Ranchi ya Kagoma iliyopo Wilaya ya Karagwe mkoani humo ya kuwaonesha vijana wanaohitimu mafunzo ya unenepeshaji mifugo kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT – LIFE), baadhi ya maeneo watakayopatiwa kwa ajili ya vitalu vya kufugia mifugo, Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mhe. Julius Laizer amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka historia ya kutafsiri ndoto halisi ya wingi wa mifugo nchini katika kubadilisha mfumo wa maisha kwa watanzania kupitia sekta hiyo. (21.05.2024)

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Daniel Mushi akizungumza na kuwaonesha baadhi ya vijana wanaohitimu mafunzo ya unenepeshaji mifugo awamu ya kwanza kupitia Programu ya Jenga kesho Iliyo Bora (BBT – LIFE), vitalu watakavyogaiwa kufanya ufugaji katika Ranchi za Kagoma na Kitengule ambazo ziko chini ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) katika Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera, ambapo katika kipindi cha miaka mitano hawatatozwa malipo ya upangaji katika ranchi hizo. (21.05.2024)

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Daniel Mushi (mwenye kofia nyeusi) akizungumza na baadhi ya wadau na vijana wanaohitimu mafunzo ya unenepeshaji mifugo awamu ya kwanza kupitia Programu ya Jenga kesho Iliyo Bora (BBT – LIFE), wakati vijana hao wakioneshwa vitalu watakavyogaiwa kufanya ufugaji katika Ranchi za Kagoma na Kitengule ambazo ziko chini ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) katika Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera, ambapo jumla ya vijana 161 watapatiwa vitalu ambapo kila mmoja atapatiwa hekari 10. (21.05.2024)



WAKAGUZI MIFUGO, MAZAO YAKE WAPIGWA MSASA


Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi leo Mei 22, 2024 imeanza kutoa mafunzo ya siku 3 kwa Wakaguzi wa mifugo na mazao yake waliopo kwenye vituo mbalimbali vya ukaguzi ikiwa ni pamoja na vile vilivyopo kwenye mipaka yote nchini zoezi litakalofanyika mkoani Morogoro.

Akifungua Mafunzo hayo Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo nchini Dkt. Benezeth Lutege amewataka wataalam hao mbali na kutumia vema taaluma zao, wazingatie weledi na watende haki wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuomba ushauri pale wanapopata changamoto.

“Tunapokuwa kule kwenye vituo vyetu vya ukaguzi tunapaswa kujua sisi ndio sura ya Wizara kwa hiyo tunavyowapokea wageni, tunavyoongea nao na tunavyotoa huduma zetu kuna athari kubwa sana kwa viongozi wetu wanaotusimamia hivyo tunaweza kuwachafua au kuwajengea sifa njema” Ameongeza Dkt. Lutege.

Aidha Dkt. Lutege ametoa angalizo kwa vijana hao kuacha kutanguliza mbele maslahi yao wakati wakitekeleza majukumu vituoni ili kuendelea kujenga dhana ya uaminifu na uadilifu jambo litakalolinda taswira ya Wizara na Serikali kwa ujumla.

“Akifika Mteja umemkamata, unatakiwa kumueleza makossa yake kwa moyo mweupe kabisa na kwa lugha stahiki bila kutumia nguvu au lugha chafu kisha na yeye umpe nafasi akueleze sababu zake na baada ya hapo upime kwa taaluma yako uone kama alichofanya ni kosa la kukusudia au la ndipo ufanye maamuzi” Amesisitiza Dkt. Lutege.

Kwa Upande wake Mratibu wa  Mradi wa Mfumo wa Usalama wa Wanyama, Mimea na Chakula ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia, Habari na Mawasiliano kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Baltazar Kibola amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wataalam hao kufahamu kuhusu Afya  ya wanyama na mazao yake kabla hawajatoa vibali kupitia mfumo wa utoaji vibali vya Mifugo na Mzao yake kielektroniki (MIMIS).

Naye Mratibu wa Mradi huo kutoka Shirika la “TradeMark Africa” ambao ndio wafadhili wakuu wa Mafunzo hayo Bi. Kezia Mbwambo ameeleza kuwa Shirika lake liliona umuhimu wa wataalam hao kujengewa uwezo kuhusu masuala ya usalama wa mifugo na mazao yake ili kulinda afya za Mifugo na watumiaji wa mifugo hiyo kwa ujumla.

Akizungumza kwa niaba ya wataalam wenzake, Afisa Mfawidhi wa kituo cha Ukaguzi wa Mifugo na Mazao yake Wilaya ya Temeke Bi. Mwajuma Chaurembo amelishukuru Shirika hilo kwa kuwajengea uwezo kupitia mafunzo hayo ambapo ameahidi kufanyia kazi kwa vitendo yote watakayojifunza kwa siku zote tatu.

Mafunzo hayo yanafuatia mafunzo ya awali yaliyodhaminiwa na Shirika la “TradeMark Afrika” na kuratibiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Kitego chake cha  Teknolojia, Habari na Mawasiliano ambayo yalihusu mfumo wa utoaji wa Vibali vya Mifugo na Mazao yake kielektroniki (MIMIS).


Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo nchini Dkt. Benezeth Lutege (kulia) akifungua mafunzo ya wakaguzi wa Mifugo na Mazao yake vituoni na mipakani Mei 22, 2024 mkoani Morogoro. Katikati ni Mratibu wa Mradi unaosimamia Mafunzo hayo kutoka Shirika la "Trade Africa" Bi. Kezia Mbwambo na kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Bw. Baltazar Kibola.

Pichani ni wakaguzi wa Mifugo na Mazao yake vituoni na mipakani wakiwa kwenye Mafunzo yanayohusu afya ya wanyama na mazao yake Mei 22, 2024 mkoani Morogoro.


Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo nchini Dkt. Benezeth Lutege (wa nne kutoka kulia mbele) na baadhi ya Viongozi na wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakiwa kwenye picha ya pamoja na wakaguzi wa Mifugo na mazao yake vituoni na mipakani mara baada ya kufungua mafunzo kwa wakaguzi hao Mei 22, 2024 mkoani Morogoro.


TUPAZE SAUTI KUOKOA PUNDA-MNYETI

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti amewataka wadau wote wanaosimamia ustawi na haki za wanyama kukemea vikali vitendo vitakavyosababisha kutoweka kwa Punda ili wanyama hao waendelee kuwasaidia wananchi katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Mhe. Mnyeti ametoa rai hiyo Mei 17, 2024 alipokuwa akifunga Maadhimisho ya siku ya Punda Afrika Mashariki ambayo kitaifa yamefanyika mkoani Dodoma yakitanguliwa na shughuli mbalimbali ikiwemo mijadala iliyolenga kuchukua hatua mbalimbali za kunusuru kutoweka kwa mnyama huyo.

“Punda wamekuwa wakifanya kazi kubwa na muhimu sana katika sekta za kiuchumi ambapo  katika shughuli za usafiri hivi sasa wamekuwa wakitumika mpaka kubeba vifaa vya ujenzi na siku za hivi karibuni tumeshuhudia wakibeba madini katika migodi mbalimali nchini” Ameongeza Mhe. Mnyeti.

Aidha Mhe. Mnyeti amebainisha kuwa kutokana na umuhimu wa ngozi na viungo vingine vya mnyama huyo ongezeko la uchinjaji wa wanyama hao lilikuwa kubwa hali iliyosababisha tishio la kutoweka kwao Afrika na ulimwenguni kwa ujumla.

“Serikali imechukua hatua mbalimbali ili kudhibiti kutoweka kwa wanyama hawa ikiwa ni pamoja na kusitisha shughuli za uchinjaji wake na biashara ya ngozi zake zilizokuwa zikiendeshwa kwa leseni ya muda ya kampuni ya Fan-Hu kutoka China na kama tungekiacha kiwanda hiki kiendelee kufanya kazi kwa miaka miwili basi kusingekuwa na punda hata mmoja hapa nchini” Amesisitiza Mhe. Mnyeti.

Kwa upande wake Mtaalam wa Mifugo na mmoja wa watetezi wa haki za Punda Dkt. Bedarn Masuruli ameipongeza Serikali kwa hatua zake mbalimbali za kuhakikisha mnyama huyo hatoweki huku pia akitoa rai kwa Serikali kuwazingatia wanyama hao katika Sera na Mipango inayohusiana na Mifugo.

“Wadau wamepongeza hatua ya Serikali kuungana na Taasisi zilizo chini ya Umoja wa Afrika kuandaa mkutano wa kwanza wa Afrika kuhusu Punda  uliozaa azimio la Dar Es Salaam ambalo linasema “Punda Afrika Sasa na katika Siku zijazo” Amesema Dkt. Masuruli.

Kwa upande wake Mkurugenzi msaidizi wa Huduma za ukaguzi na ustawi wa wanyama kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Anette Kitambi ameitaka jamii kushirikiana na Serikali kuwalinda Punda kwani mfumo wa uzazi  ni tofauti na wanyama wengine ambapo anaweza kuzaa mara moja au asizae kabisa na muda wake wa kubeba mimba huwa ni kati ya miezi 12 hadi 14.

“Na maajabu mengine ya punda kama akiona mazingira sio rafiki anaweza kuahirisha kuzaa hivyo ni mnyama mwenye sifa za tofauti kabisa ukiinganisha na wengine na ndio maana kutokana na umuhimu huo kati ya wanyama wote ni yeye tu ndo aliandaliwa siku yake kitaifa” Amebainisha Dkt. Kitambi.

 

Maadhimisho ya Siku ya Punda duniani hufanyika Mei 08 ya kila mwaka na kwa Afrika Mashariki huwa ni Mei 17 huku Serikali, wataalam na wadau mbalimbali wakitumia siku hiyo kujadili hatma ya mnyama huyo na ustawi wake kwa ujumla.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti (katikati) akikata keki kuashiria miaka 90 ya Shirika la kutetea haki za wanyama linaloitwa "BROOKE" wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Punda Afrika Mashariki Mei 17, 2024 jijini Dodoma, Wanaoshuhudia Kulia kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Riziki Shemdoe na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za ukaguzi na ustawi wa wanyama Dkt. Anette Kitambi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (kulia) akipokea zawadi kutoka kwa Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la kutetea haki za wanyama (ASPA) Bw. Livingstone Masija wakati wa maadhimisho ya Afrika Mashariki ya  siku ya Punda yaliyofanyika jijini Dodoma Mei 17, 2024.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti (katikati waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na wataalam na wadau mbalimbali wa kutetea haki za mnyama Punda wakati wa Maadhimisho ya Siku ya mnyama huyo Afrika Mashariki yaliyofanyika Mei 17, 2024 jijini Dodoma.


warsha ya kujenga uelewa kwa wadau kuhusu mkakati wa kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi,

 

Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia uthibiti wa ubora na masoko ya mazao ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Lukanga (wa tatu kutoka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau  wa uvuvi mara baada ya kushiriki warsha ya kujenga uelewa kwa wadau hao kuhusu mkakati wa kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi (MDS STATEGY) na kupitia mkakati wa masoko wa zao la dagaa, Warsha hiyo imefanyika kwenye ukumbi hoteli ya Flomi mkoani Morogoro Mei16, 2024

Afisa Uvuvi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Upendo Hamidu akichangia hoja wakati wa warsha ya kujenga uelewa kwa wadau kuhusu mkakati wa kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi na kupitia mkakati wa masoko wa zao la dagaa,  Mei 16,2024 mkoani Morogoro.

Mratibu wa Mradi unaofadhiliwa na shirika la maendeleo la Norway kupitia Shirika la chakula na kilimo (FAO) Bw. Joseph Lomba akieleza lengo la kufanya utafiti wa kutathmini hali ya upotevu wa rasilimali  ya uvuvi aina ya dagaa wakati wa warsha ya kujenga uelewa kwa wadau kuhusu mkakati wa kupunguza upotevu wa mazao hayo, warsha hiyo imefanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Flomi mkoani Morogoro,  Mei 16,2024

4

Mtaalam elekezi wa Mradi wa upunguzaji wa uaribifu wa dagaa nchini Bw. Yahaya Mgawe akiongoza warsha ya kujenga uelewa kwa wadau kuhusu mkakati wa kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi, warsha hiyo imefanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Flomi mkoani Morogoro,  Mei 16,2024

Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia uthibiti wa ubora na masoko ya mazao ya uvuvi, Bw. Stephen Lukanga akitoa neno la shukrani mara baada ya ufunguzi wa warsha ya kujenga uelewa kwa wadau kuhusu mkakati wa kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi na kupitia mkakati wa masoko wa zao la dagaa mkoani Morogoro Mei 16,2024.


shughuli mbalimbali zilizofanyika kwenye Wiki ya Protini iliyofanyika kwenye viwanja vya Bunge Mkoa wa Dodoma Mei 14, 2024.

 

Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe. Anjelina Mabula (kushoto) akipata maelezo kuhusiana na matumizi mbalimbali ya mazao ya Uvuvi yatokanayo na Samaki aina ya Jodar kutoka Mtaalam wa Utafiti wa mazao hayo wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) Bi. Siwema Luvanda alipotembelea Mabanda ya maonesho ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kujionea shughuli mbalimbali zinazofanyika kwenye Wiki ya Protini iliyofanyika kwenye viwanja vya Bunge Mkoa wa Dodoma Mei 14, 2024.

Mbunge wa Isimani Mhe. Wiliam Lukuvi (kulia) akikabidhiwa nyama aina ya Kongwa Beef kutoka kwa Bi. Beatrice Mhina (kushoto) mtaalamu kutoka Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) mara baada ya kuridhishwa na ubora wake alipotembelea Mabanda ya maonesho ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kujionea shughuli mbalimbali zinazofanyika kwenye Wiki ya Protini iliyofanyika kwenye viwanja vya Bunge Mkoa wa Dodoma Mei 14, 2024.

Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Halima Mdee (kulia) akipata maelezo kuhusiana na matumizi sahihi ya Chanjo ya Mdondo (Kideli) kwa kuku kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt Stella Bitanyi (kushoto) alipotembelea Mabanda ya maonesho ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kujionea shughuli mbalimbali zinazofanyika kwenye Wiki ya Protini iliyofanyika kwenye viwanja vya Bunge Mkoa wa Dodoma Mei 14, 2024.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (wa pili kushoto) akipata elimu kuhusina matumizi ya vifaa vya uokoaji majini kutoka kwa Meneja Mradi wa kampuni ya EMEDO Bw. Arthur Mugema (wa pili kutoka kulia) alipotembelea Mabanda ya maonesho ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kujionea shughuli zinazofanyika kwenye Wiki ya Protini iliyofanyika kwenye viwanja vya Bunge Mkoa wa Dodoma Mei 14, 2024.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (wa pili kushoto) akipata huduma ya mshikaki unaotokana na mazao ya Samaki alipotembelea Mabanda ya maonesho ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kujionea shughuli mbalimbali zinazofanyika kwenye Wiki ya Protini iliyofanyika kwenye viwanja vya Bunge Mkoa wa Dodoma Mei 14, 2024. Aliesimama kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt Edwin Mhede na aliesimama kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) Dkt. Ismael Kimirei.

Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (wa pili kutoka kushoto) akipata elimu kuhusiana na uzalishaji bidhaa za mazao yatakanayo na Maziwa kutoka kwa Mkurugenzi wa kampuni ya ASAS Bw. Fuad Jeffer (wa tatu kutoka kushoto) alipotembelea Mabanda ya maonesho ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kujionea shughuli mbalimbali zinazofanyika kwenye Wiki ya Protini iliyofanyika kwenye viwanja vya Bunge Mkoa wa Dodoma Mei 14, 2024.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (wa pili kutoka kulia) akipata elimu kuhusiana na uzalishaji wa dawa za kuogeshea Mifugo kutoka kwa Mtaalamu wa kampuni ya FARMBASE Dkt. Nasib Mtoi alipotembelea Mabanda ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi  kujionea shughuli mbalimbali zinazofanyika kwenye Wiki ya Protini iliyofanyika kwenye viwanja vya Bunge Mkoa wa Dodoma Mei 14, 2024. Aliesimama katikati ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Daniel Mushi.


WAZIRI MKUU AZINDUA KITUO CHA UFUGAJI MBUZI, KONGWA


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Mei 13, 2024 amezindua na kushuhudia makabidhiano ya Kituo Atamizi cha Ufugaji wa Kibiashara kwa Vijana, baina ya Taasisi ya PASS TRUST na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI)kilichopo Kongwa mkoani Dodoma.

Akizungumza baada ya makabidhiano ya kituo hicho, ambacho kinathamani ya shilingi bilioni 1.63 ikijumuisha uwekezaji wa vifaa na mindombinu, Mheshimiwa Majaliwa ameagiza uwekezaji utunzwe ili taifa liweze kunufaika kupitia uwezeshwaji wa vijana.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa lengo la mradi huo ni kuwapatia vijana ujuzi kwa vitendo ikiwemo elimu ya ujenzi wa mabanda, ulishaji, matibabu na usimamizi wa mbuzi lakini pia kutoa mafunzo ya biashara ili vijana waweze kuwa wajasiriamali na kuendeleza biashara ya unenepeshaji mbuzi.

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa hadi kufikia Aprili 2024, ongezeko la mauzo ya nyama nje ya nchi limefikia takribani shilingi bilioni 100 ambapo nyama ya mbuzi imeendelea kuongoza kwa kuchangia asilimia 70.1 ya mauzo yote, hivyo kituo hicho cha unenepeshaji wa mbuzi kitaendelea kuchaguza kwenye biashara ya nyama kupitia shughuli ya unenepeshaji wa mbuzi utakaokuwa ukifanywa na vijana hao.

 Aliongeza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepanga kukifanya  Kituo Atamizi cha Ufugaji kilichopo Kongwa kuwa kituo kikubwa kwa ajili ya ufugaji na unenepeshaji wa mbuzi nchini.

 Kituo hicho kilichokuwa kikisimamiwa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya PASS kimekabidhiwa kwa Serikali na kitakuwa chini ya uangalizi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI).





WATUMISHI WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI WATAKIWA KUWAJIBIKA NA KUWA WAADILIFU

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti amewataka watumishi wa wizara hiyo kuwa na uwajibikaji na uadilifu katika makujumu yao ya kuwatumikia wananchi.

Mhe. Mnyeti amebainisha hayo leo (10.05.2024) jijini Dodoma, wakati alipokuwa akihutubia wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kufafanua kuwa ana imani kubwa na watumishi wa wizara hiyo na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuwa na uzalendo.

Ameongeza kuwa katika uwajibikaji na uadilifu watumishi wa wizara hiyo wanatakiwa kutojiingiza kwenye matukio ya matumizi mabaya ya ofisi na kuhakikisha wanazidi kuwatumikia wananchi kwa kiwango kikubwa hususan wafugaji na wavuvi ambao wengi wao wanaishi vijijini.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe ambaye pia ni mwenyekiti wa baraza hilo, amesema kikao hicho kimetoka na maazimio tisa ambapo pia wajumbe wameridhia Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2023/2024 na Mpango wa Bajeti ya Mwaka 2024/2025 kusomwa bungeni.

Aidha, Prof. Shemdoe akijibu hoja mbalimbali kutoka kwa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la wizara hiyo, amesema uongozi unaendelea kutatua changamoto mbalimbali mahali pa kazi ikiwemo kuongeza vitendea kazi.

Pia, amesema wizara itaendelea kuboresha maslahi ya watumishi na kuwajengea mazingira bora zaidi ya kufanyia kazi kwa kuwa wamekuwa wakitumia muda mwingi kuwa kazini.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede amewataka watumishi wa wizara hiyo kuwa tayari kuwajibika na kutekeleza bajeti ya wizara mara baada ya kusomwa na kupitishwa bungeni.

Akisoma taarifa ya hoja na maoni ya watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) – Tawi la wizara hiyo Bw. Silas William, ameomba uongozi wa wizara kuangalia kwa ukaribu baadhi ya changamoto zinazowapata watumishi waliopo kazini na ambao wanastaafu ili kuondokana na usumbufu ambao umekuwa ukijitokeza.

Bw. William amesema watumishi wa wizara wataendelea kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kila siku kwa kuwahudumia wananchi kwa miongozo ya sheria na kanuni za utumishi wa umma ili waweze kufikia malengo ya serikali ya kukuza sekta za mifugo na uvuvi.

Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Mifugo na Uvuvi walipata pia fursa ya kuuliza maswali na kuchangia hoja mbalimbali na wote kwa pamoja kukubaliana na maazimio tisa kwa ajili ya kufikia malengo ya baraza hilo.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti akiwahutubia wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kufafanua kuwa ana imani kubwa na watumishi wa wizara hiyo na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuwa na uzalendo. Kikao hicho kimefanyika jijini Dodoma na kukubaliana maazimio tisa likiwemo la kuridhia Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2023/2024 na Mpango wa Bajeti ya Mwaka 2024/2025 kusomwa bungeni. (10.05.2024)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la wizara hiyo, akifafanua hoja mbalimbali na kutoa taarifa ya maazimio tisa kwenye kikao cha baraza kilichofanyika jijini Dodoma. (10.05.2024)

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede amewataka watumishi wa wizara hiyo kuwa tayari kuwajibika na kutekeleza bajeti ya wizara ya mwaka 2024/2025 mara baada ya kusomwa na kupitishwa bungeni. Dkt. Mhede amebainisha hayo jijini Dodoma wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi la wizara hiyo. (10.05.2024)



UPUMZISHWAJI ZIWA TANGANYIKA WAUNGWA MKONO

Wananchi wanaojishughulisha na uvuvi katika ukanda wa Ziwa Tanganyika wameunga mkono hatua ya serikali ya kupumzisha shughuli za uvuvi katika ziwa Tanganyika ili kulipa nafasi ziwa kuongeza kiwango chake cha uzalishaji wa samaki.

Wananchi hao waliunga mkono hatua hiyo wakati wa hafla ya kukabidhi vizimba vya kufugia samaki, boti za kisasa za uvuvi na doria na pia kupata elimu na uelewa kuhusu upumzishaji wa shughuli za Uvuvi Ziwa Tanganyika iliyofanyika katika Mwalo wa Katonga, mkoani Kigoma Mei 9, 2024.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wawakilishi wa wananchi, akiwemo Mbunge wa Kigoma Mjini, Mhe. Kilumbe Ng’enda alisema kuwa muda ambao umepangwa ziwa kupumzishwa ni muafaka kwa sababu kipindi hicho ni maarufu kwa jina la ‘kilimia’ ambapo ziwa huwa linajifunga lenyewe na kufanya kupungua kwa Mazao ya samaki.

Aliongeza kwa kueleza kuwa, kwa muda mrefu sasa wavuvi wamekuwa wakitumia vifaa vyao na mafuta kwenda mbali bila mafanikio yoyote kwa sababu samaki wamepungua sana ziwani, hivyo kupumzisha ziwa kutasaidia samaki kuongezeka na hivyo wavuvi wataweza kupata mavuno mengi zaidi baada ya ziwa kufunguliwa.

Naye, Mbunge wa Kigoma Kusini, Mhe. Nashon Bidyanguze alisema kuwa mwanzoni walikuwa wanapinga kufungwa kwa ziwa kwa sababu wananchi walikuwa hawana elimu ya kufungwa kwa ziwa lakini sasa hawawezi kuendelea kupinga kwa sababu tayari serikali imepeleka boti na vizimba kwa ajili ya wananchi kutumia kufuga samaki katika kipindi ambacho ziwa litakuwa limefungwa.

Wakati akikabidhi boti na vizimba kwa wanufaika wanaofanya shughuli zao katika Ziwa Tanganyika, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa Mhe. Rais, Dkt. Samia  Suluhu Hassan ametoa Boti na Vizimba hivyo ili wananchi watumie kufugia samaki kama njia mbadala ya kujipatia kipato katika kipindi ambacho ziwa litakuwa limepumzishwa.

Aidha, Waziri Ulega amewataka wanufaika wa boti hizo na wengine wote wanaoendesha shughuli za Uvuvi Ziwa Tanganyika na Nyasa kutumia zana hizo kwa malengo yaliyokusudiwa, huku akiwaelekeza maafisa uvuvi wa ukanda wa ziwa Tanganyika kutotumia kipindi hicho kuwasumbua wavuvi hususani wavuvi wadogo badala yake waendelee kuwaelimisha ili waweze kutoa ushirikiano wa kutosha wakati wote wa zoezi hilo.

Katika hafla hiyo, Waziri Ulega amekabidhi vizimba 29  kwa vikundi sita na watu binafsi 16 na Boti 6 kwa ajili ya uvuvi na doria katika mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa.





ULEGA: TUMEJIPANGA KUIMARISHA BIASHARA YA MAZAO YA MIFUGO


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema wizara yake imejipanga kuyasimamia vyema mazao ya mifugo hususan maziwa, nyama na ngozi ili yazalishwe kwa ubora na kushamirisha biashara kwa lengo la kuyafanya mazao hayo kuwa na mchango mkubwa zaidi kwenye pato la Taifa.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na Wajumbe wa Bodi ya Nyama na Bodi ya Maziwa kwenye kikao kilichofanyika jijini Dodoma Mei 7, 2024, ambapo alipokea taarifa za utekelezaji wa bodi hizo ambazo kwa sasa zimeunganishwa na kuundwa taasisi moja itakayosimamia mazao hayo ya mifugo.

“Tuko katika uundaji wa taasisi nyingine ya usimamizi wa mazao kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, tunakwenda kuunda taasisi nzuri, makini, imara, itakayokwenda kuongeza tija na kushamilisha biashara. Wadau msiwe na wasiwasi, tunatambua juhudi kubwa mnazozifanya, tumejipanga kufanya kazi kwa pamoja kuleta maendeleo ya Tasnia hizi mbili na Sekta ya Mifugo kwa ujumla”, alisema

“Niwaahidi kuwa tutajitahidi kwa upande wetu kama serikali kuyasimamia mazao haya, kuhakikisha biashara zinakuwa rasmi, na kuchangia zaidi kwa uchumi, lishe, na ajira”, aliongeza

Aidha, alitumia nafasi hiyo pia kuwaomba wananchi kuendelea kunywa maziwa na kula nyama kwa wingi kwani kwa  kufanya hivyo watachangia kuinua tasnia za maziwa na nyama na kukuza uchumi wa Taifa.

Katika hatua nyingine, Waziri Ulega  amewahimiza Wafugaji kuzalisha zaidi maziwa na nyama zenye ubora kwani bado mahitaji ya bidhaa hizo ni makubwa ndani na nje ya nchi.


Katibu Mkuu, Wizara Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mhe. Waziri kuzungumza na wajumbe wa Bodi ya Nyama na Bodi ya Maziwa katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma Mei 7, 2024.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akizungumza na Wajumbe wa Bodi ya Nyama na Bodi ya Maziwa (hawapo pichani) wakati wa kikao kilichofanyika jijini Dodoma Mei 7, 2024, ambapo alipokea taarifa za utekelezaji wa bodi hizo ambazo kwa sasa zimeunganishwa na kuundwa taasisi moja itakayosimamia mazao hayo ya mifugo.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (katikati waliokaa)akiwa katika picha za pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Nyama na Bodi ya Maziwa muda mfupi baada ya kumaliza kuzungumza nao katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma Mei 7, 2024.