Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Mhe. Abdallah Ulega amesema wizara yake imejipanga kuyasimamia vyema mazao ya
mifugo hususan maziwa, nyama na ngozi ili yazalishwe kwa ubora na kushamirisha
biashara kwa lengo la kuyafanya mazao hayo kuwa na mchango mkubwa zaidi kwenye
pato la Taifa.
Ameyasema hayo wakati
akizungumza na Wajumbe wa Bodi ya Nyama na Bodi ya Maziwa kwenye kikao
kilichofanyika jijini Dodoma Mei 7, 2024, ambapo alipokea taarifa za
utekelezaji wa bodi hizo ambazo kwa sasa zimeunganishwa na kuundwa taasisi moja
itakayosimamia mazao hayo ya mifugo.
“Tuko katika uundaji wa
taasisi nyingine ya usimamizi wa mazao kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt
Samia Suluhu Hassan, tunakwenda kuunda taasisi nzuri, makini, imara,
itakayokwenda kuongeza tija na kushamilisha biashara. Wadau msiwe na wasiwasi,
tunatambua juhudi kubwa mnazozifanya, tumejipanga kufanya kazi kwa pamoja
kuleta maendeleo ya Tasnia hizi mbili na Sekta ya Mifugo kwa ujumla”, alisema
“Niwaahidi kuwa
tutajitahidi kwa upande wetu kama serikali kuyasimamia mazao haya, kuhakikisha
biashara zinakuwa rasmi, na kuchangia zaidi kwa uchumi, lishe, na ajira”,
aliongeza
Aidha, alitumia nafasi hiyo
pia kuwaomba wananchi kuendelea kunywa maziwa na kula nyama kwa wingi kwani
kwa kufanya hivyo watachangia kuinua
tasnia za maziwa na nyama na kukuza uchumi wa Taifa.
Katika hatua nyingine,
Waziri Ulega amewahimiza Wafugaji
kuzalisha zaidi maziwa na nyama zenye ubora kwani bado mahitaji ya bidhaa hizo
ni makubwa ndani na nje ya nchi.
Katibu Mkuu, Wizara Mifugo
na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha
Mhe. Waziri kuzungumza na wajumbe wa Bodi ya Nyama na Bodi ya Maziwa katika
kikao kilichofanyika jijini Dodoma Mei 7, 2024.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Mhe. Abdallah Ulega akizungumza na Wajumbe wa Bodi ya Nyama na Bodi ya Maziwa
(hawapo pichani) wakati wa kikao kilichofanyika jijini Dodoma Mei 7, 2024,
ambapo alipokea taarifa za utekelezaji wa bodi hizo ambazo kwa sasa
zimeunganishwa na kuundwa taasisi moja itakayosimamia mazao hayo ya mifugo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Mhe. Abdallah Ulega (katikati waliokaa)akiwa katika picha za pamoja na Wajumbe
wa Bodi ya Nyama na Bodi ya Maziwa muda mfupi baada ya kumaliza kuzungumza nao
katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma Mei 7, 2024.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni