Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema ugawaji wa madume ya bora ya ng’ombe ni utekelezaji wa mpango wa mabadiliko wa Sekta ya Mifugo.
Waziri
Ndaki ameyasema hayo leo (24.11.2022) wilayani Chamwino Mkoani Dodoma wakati
alipokuwa anagawa madume bora 50 ya ng’ombe aina ya boran ambapo kila mmoja ana
uwezo wa kupanda majike 25 kwa mwaka, kwa vikundi vya wafugaji kwa lengo la
kwenda kuboresha mifugo yao ambayo mingi ni ya asili.
“Mifugo
mingi iliyopo hapa nchini ni ya asili na uzalishaji wake wa nyama na maziwa kwa
mfugo ni ndogo, hivyo kwa kuanza kuboresha mifugo kwa kutumia madume haya
pamoja na njia ya uhimilishaji kutasaidia wafugaji kuwa na mifugo michache
ambayo itakuwa na uzalishaji mkubwa wa nyama na maziwa,” Alisema
Ng’ombe
wa asili huzalisha nyama kilo 80 -120 kwa ng’ombe wakati baada ya kuboreshwa kwa
kosaafu mfugaji anaweza kupata kilo 150 – 200 kwa ng’ombe. Lakini pia kwenye
upande wa maziwa ng’ombe hawa walioboreshwa kosaafu huwa na uwezo wa kutoa kati
ya lita 5 – 10 za maziwa na hivyo kumfanya mfugaji apate tija zaidi tofauti na
mfugaji wa ng’ombe wa asili.
Wafugaji
wametakiwa kuyatunza madume hayo kwa kufuata taratibu zote wanazoelekezwa na
wataalam wa mifugo. Lakini pia Waziri
Ndaki amevitaka vikundi ambavyo vimepatiwa madume hayo kuyatumia kwa
kushirikiana na wafugaji wengine ili kuhakikisha tija inapatikana kwa wafugaji
ndani ya Wilaya ya Chamwino.
Kaimu
Katibu Mkuu Sekta ya Mifugo, Dkt. Asimwe Rwiguza amesema Wizara inaendelea
kutekeleza mpango wa mabadiliko wa sekta hiyo ambapo licha ya kazi ya
uboreshaji wa kosaafu inayoendelea, wafugaji wanaendelea kupatiwa elimu kuhusu
malisho ya mifugo.
Wizara
inaendelea kuanzisha mashamba darasa ya malisho ya mifugo kwa lengo la kutoa
elimu ya kilimo cha malisho na namna ya kuyatunza malisho hayo pamoja na nyanda
za malisho ili malisho hayo yaweze kuwasaidia wakati wa kiangazi kikali.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Mhe. Gift Msuya amesema kuwa uongozi wa Wilaya utakwenda
kusimamia utekelezaji wa mpango wa mabadiliko wa sekta ya mifugo kwa
kuhakikisha madume hayo yaliyogawiwa kwenye vikundi yanatunzwa na kutumika ili
kuboresha kosaafu.
Mkurugenzi
wa Idara ya Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko kutoka Sekta ya Mifugo, Bw.
Stephen Michael amesema kuwa takribani asilimia 97 ya ng’ombe waliopo nchini ni
wa asili hivyo katika kutekeleza mpango wa mabadiliko wa sekta, Wizara imepanga
kununua mitamba 1,160,000 ambayo itapelekwa kwenye mashamba ya serikali. Hivyo
kutokana na uzalishaji wake wafugaji wataweza kupata ng’ombe bora hapa nchini
badala ya kutegemea kuagiza kutoka nje.
Aidha,
Wizara inaendelea na zoezi la uhimilishaji mifugo ambapo tayari imeshapanga
kuhimilisha takribani ng’ombe 373,000 katika mwaka wa fedha 2022/2023 kwenye
maeneo ambayo hawatapata madume hayo.
Mwakilishi
wa taasisi ya PASS Trust, Langelika Kalebi amesema kuwa taasisi hiyo ni
mwezeshaji ikichochea maendeleo kwenye kilimo (mifugo, uvuvi, mazao, na mazao
ya porini). Taasisi hiyo ipo nchi nzima ikichochea maendeleo kwenye upatikanaji
wa mitaji na elimu, hivyo wanaongezea dhamana katika kurahisisha upatikanaji wa
mitaji kwa mtu mmoja, vikundi, vyama vya ushirika.
Naye
mwenyekiti wa wafugaji Wilaya ya Chamwino, Bw. John Kochocho ameishukuru
serikali kupitia Sekta ya Mifugo kwa kuwapelekea wafugaji madume hayo ya
ng’ombe yatakayokwenda kuboresha kosaafu na hivyo kuwafanya wazalishe kwa tija
na kibiashara.
Serikali ya awamu ya sita ya Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imefanikiwa kununua jumla ya madume bora ya ng’ombe wa nyama 366 aina ya Boran kama sehemu ya jitihada za kuendelea kuboresha tija ya ng’ombe tulionao nchini.