Na. Martha Mbena.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema Serikali kupitia Wizara ya Mifugo imekuja na mageuzi kwa kufuga mifugo bora yenye tija kupitia Ng'ombe aina ya Borani ili kupata kilo nyingi, nyama nyingi na kuzalisha maziwa mengi jambo ambalo litachangia pato la Taifa.
Waziri Ndaki ameyasema hayo (21.11.2022) wakati akikabidhi madume 50 ya Ng'ombe aina ya Borani kwa makundi ya wafugaji wa Wilaya ya Maswa kwenye hafla fupi iliyofanyika kwenye kata ya Buchambi Mkoani Simiyu.
"Kiasi cha sh 915 milioni kilichotolewa na Serikali kimetumika kununua madume 336 ya Ng'ombe aina ya Borani ambayo yatakabidhiwa kwenye Wilaya 10 nchi nzima, Kwa hapa Wilaya ya Maswa tumekabidhi haya madume 50, Ombi langu muwatunze kwa kuwaosha mara kwa mara ili wasipate kupe wakapata ugonjwa wa Ndigana," Alisema Waziri Mashimba.
Mhe. Mashimba aliongeza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa Ng'ombe hao bure kwa vikundi vyote vya wafugaji na kila kikundi kitapata dume ambalo litapanda majike yasiyopungua 25 kwa mwaka, Lengo ni kuzalisha Ng'ombe wa kisasa na bora zaidi kwa ufugaji.
Alisema kuwa mpango wa Serikali ni kuhamasisha ufugaji wa kisasa wa mifugo michache na kipato kingi na kuongeza kuwa aina hiyo ya Ng'ombe ni tofauti na Ng'ombe wa kawaida na kufafanua kuwa Ng'ombe wa kienyeji wanne ni sawa na Ng'ombe mmoja wa aina ya Borani.
"Niwaambieni tu kuwa kwa madume haya Ng'ombe atakayezaliwa ana uwezo wa kutoa lita 5 mpaka 10 kwa siku lakini wa kienyeji akijitaidi sana anaweza kutoa lita 1 mpaka 5 kwa siku kwa hiyo Ng'ombe wa kienyeji anaingizia serikali pato dogo," Alisema Ndaki.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Maswa Aswege Kaminyonge amesema changomoto kubwa ni ukosefu wa pikipiki zitakazotumika katika mizunguko kwenye vijiji mbalimbali ili kufuatilia mradi huo usije ukakwama.
Vilevile mkuu huyo wa Wilaya aliwataka maafisa watendaji wa kata kufuatilia kwa ukaribu zaidi wafugaji wote waliokabidhiwa madume hayo ili yasidhulike kwa kukosa matunzo.
kwa upande wake Mmiliki wa Shamba la Mifugo Mkoani Kagera, Bw. Josam Ntangeki amesema madume hayo kati ya mwaka mmoja hadi miwili yamepatiwa huduma zote za chanjo na kuwaomba wafugaji kujitaidi kuwapatia Ng'ombe hao huduma zote ikiwapo kuwapatia na chanjo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni