Na, Edward Kondela
Serikali imeanza
utekelezaji wa ufugaji samaki kwa njia ya vizimba katika Ziwa Tanganyika baada
ya mpango huo kuonesha mafanikio makubwa katika Ziwa Victoria.
Akizungumza (11.01.2024)
katika Mwalo wa Kasanga uliopo Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa, Naibu Waziri wa
Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti amesema tayari wizara imeanza kutoa elimu
kwa wavuvi wa ukanda wa Ziwa Tanganyika kabla ya kufikisha vizimba hivyo na
mbegu bora za samaki.
Mhe.Mnyeti ameongeza kuwa
kwa sasa serikali imetenga Shilingi Bilioni 20 kwa ajili uwekaji vizimba katika
Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika kwa sababu ufugaji wa samaki unakua kwa kasi
maeneo mbalimbali duniani kutokana na upungufu wa samaki waliopo kwenye maji ya
asili yakiwemo mabonde, maziwa, mito na bahari kutokana na sababu mbalimbali
ikiwemo ya uharibifu wa mazingira, ongezeko la watu na uharibifu wa mazalia ya
samaki.
Ameongeza kuwa ili kunusuru
upungufu wa samaki katika masoko ya ndani na nje ya nchi serikali imeamua
kuanza kusambaza vizimba kwa wavuvi wa Ziwa Tanganyika ambavyo vitatolewa kwa
mkopo nafuu usio na riba.
Awali akiwa katika Ofisi za
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa alipokutana na mkuu wa mkoa huo Mhe. Charles Makongoro Nyerere
alimueleza azma ya serikali ya kulipumzisha Ziwa Tanganyika katika shughuli
zozote za uvuvi kwa kipindi cha miezi mitatu kila mwaka kwa miaka mitatu
mfululizo ambapo kwa mwaka huu litafungwa kuanzia tarahe 15 mwezi Mei hadi 15
mwezi Agosti 2024 ili kupisha samaki waweze kuzaliana.
Amesema kupumzishwa kwa
shughuli za uvuvi katika ziwa hilo ni utekelezaji wa Mkataba wa Kikanda wa
Usimamizi wa Uvuvi endelevu katika ziwa hilo na bonde lake ambapo nchi
wanachama wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika kwa maana ya Burundi, Jamhuri ya
Kidemokeasia ya Kongo, Tanzania na
Zambia zilitia saini mkataba huo Tarehe 9 Mwezi Desemba Mwaka 2021 kwenye
mkutano wa 9 wa mawaziri wa nchi hizo.
Amebainisha kuwa
kupumzishwa kwa ziwa hilo kutatoa fursa kwa wavuvi kujifunza namna bora ya
kufuga samaki pamoja na kuwa na njia nyingine za kujipatia kipato zikiwemo za
kufuga mifugo na kilimo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Rukwa
Mhe. Charles Makongoro amesema mpango wa serikali kuhamasisha kufuga samaki kwa
njia ya vizimba ni mzuri kwa kuwa wavuvi watapata fursa ya kujifunza namna
nyingine ya kuendeleza biashara ya samaki na kwamba mkoa utasimamia utekelezaji huo ili wananchi
waendelee kunufaika na mazao ya uvuvi.
Baadhi wananchi wanaofanya
shughuli za uvuvi katika Ziwa Tanganyika wakiwa kwenye mkutano wa hadhara
ulioandaliwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti katika
Kata ya Kasanga, wamepongeza juhudi za serikali kwa kuwatafutia njia mbadala ya
kuendeleza Sekta ya Uvuvi na kuiomba serikali kuzidi kutoa elimu zaidi juu ya ufugaji
kwa njia ya vizimba.
Aidha, wamekiri kwamba kwa
sasa mazao ya samaki yamepungua kwa kiasi kikubwa katika ziwa hilo na samaki
wanaopatikana ni wadogo ambao wanahitaji kubakia ziwani ili kukua.
Naibu Waziri Mnyeti amepata
pia fursa ya kushuhudia maendeleo ya ujenzi wa soko la samaki katika Kata ya
Kasanga linalogharimu Shilingi Bilioni 1.4 na kuwataka wananchi hao mara soko
litakapokamilika ni vyema wakaliendesha wao wenyewe na kulifanya la kisasa
zaidi.
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti akizungumza na wadau wa uvuvi kwenye mkutano wa
hadhara katika Kata ya Kasanga Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa, akibainisha juu
ya utekelezaji wa ufugaji samaki kwa njia ya vizimba katika Ziwa Tanganyika
baada ya mpango huko kufanya vizuri Ziwa Victoria. Serikali imetenga Shilingi
Bilioni 20 kwa ajili uwekaji vizimba katika Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika.
(11.01.2024)
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti (katikati) akikagua maendeleo ya ujenzi wa soko la
samaki katika Kata ya Kasanga Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa alipofanya ziara
ya kkazi ya siku moja kukagua maendeleo ya Sekta ya Uvuvi na kutaka mara soko
likikamilika wananchi wa eneo hilo waliendeshe kisasa ili liwe na tija kwako.
Soko hilo linagharimu Shilingi Bilioni 1.4 (11.01.2024)
Mkurugenzi Msaidizi wa
Undelezaji Rasilimali za Uvuvi Bi. Merisia Mparazo akizungumza na wananchi
wakati akimwakilisha Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi),
kwenye mkutano wa hadhara katika Mwalo wa Kasanga Wilaya ya Kalambo Mkoani
Rukwa akiwakumbusha juu ya shughuli za uvuvi zinazofuata sheria. (11.01.2024)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni