Nav bar

Jumanne, 24 Mei 2022

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatarajia kuanza kutumia mfumo wa usimamizi wa utoaji vibali mbalimbali vya kusafirisha mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi unaojulikana kama “ Mifugo Management Information System (MIMIS)” ambao unalenga kuboresha mazingira ya ufanyaji wa biashara za Mifugo, kukata na kuhuisha leseni za wataalam wa Mifugo na vibali vinavyohusu uingizaji, uzalishaji na uuzaji  wa vyakula vya samaki.


Hayo yamebainishwa leo na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia sekta ya Mifugo Dkt. Charles Mhina alipokuwa akifungua mafunzo ya matumizi ya mfumo huo kwa wadau na wataalam kutoka sekta za  Mifugo na Uvuvi yaliyofanyika leo (18.05.2022) kwenye hoteli ya Royal Village jijini Dodoma.


“Uwepo wa mfumo huu utatusaidia kuokoa muda wa kushughulikia vibali lakini pia utaongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kuokoa fedha za Serikali  kwa sababu “Control Number” itazalishwa pale mtu anapofanya maombi tofauti na sasa ambapo mtu anaweza kukimbia  na kitabu cha kukusanyia mapato na baadae kuendelea kukitumia kwa manufaa yake binafsi” Amesema Dkt. Mhina.


Dkt. Mhina amepongeza namna mfumo huo unavyoweza kuchakata taratibu zote zinazohusu vibali kwa wakati mmoja tofauti na ilivyokuwa awali ambapo kila hatua ilikuwa na mfumo wake hali iliyokuwa ikisababisha usumbufu kwa watumiaji na kusababisha kuchelewesha upatikanaji wa vibali hivyo.


“Kupitia mfumo huu sasa hatutahitaji kujua zilipo karatasi zake za kibali ila tutaangalia tutahitaji tu kufahamu namba ya kibali chake ambayo ni lazima itaonekana kwenye mfumo lakini pia kwa mdau anayenunua ng’ombe wake wakati anawaweka kwenye zizi anaweza kuanza taratibu za kuomba kibali cha kuwasafirisha kupitia mtandao na ndani ya muda mfupi atakuwa ameshapata kibali chake” Ameongeza Dkt. Mhina.


Dkt. Mhina amezipongeza pande zote zilizoshiriki kutengeneza mfumo huo kwa kuziwezesha simu ndogo za mkononi kutumika kwenye mfumo huo jambo ambalo amebainisha kuwa litawawezesha wadau wengi zaidi kuutumia.


Akizungumzia hali ilivyokuwa kabla ya kuanza utekelezaji wa mfumo huo, Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia afya ya jamii ya veterinari, udhibiti wa pembejeo, mifugo na mazao yake Dkt. Stanford Ndibalema amesema kuwa hapo awali mfanyabiashara yoyote aliyekuwa anataka kusafirisha mazao ya mifugo alilazimika kuiandikia Wizara barua na mchakato wote ulichukua muda usiopungua wiki mbili.


Naye Mkurugenzi wa kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa upande wa sekta ya Mifugo, Baltazari Kibola ameainisha maeneo ambayo mfumo huo utayaangazia kuwa ni pamoja na eneo la usafirishaji wa mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi, utoaji wa vibali kwa wafanyabiashara wa vyakula vya mifugo na usajili wa wadau waliopo chini ya bodi za nyama na maziwa.


“Lakini pia mfumo huu sasa utaanza kuwasajili kwa njia ya mtandao wataalam wa vitu vinavyohusika na utoaji wa huduma za mifugo kama vile maabara au kliniki za mifugo ambazo zinaratibiwa na Baraza la Veterinari nchini na ikumbukwe hapo awali wataalam hawa walikuwa wanalazimika kupeleka maombi yao Wizarani ndipo mchakato wa kuyashughulikia uanze” Ameongeza Kibola.


Kwa upande wake Mtaalam wa mifumo kutoka kampuni iliyoratibu utengenezwaji wa mfumo huo inayojulikana kama “Trade Mark East Africa” (TMEA) James Temu amesema kuwa kukamilika kwa mfumo huo kutawafanya wadau wote waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya Mifugo na Uvuvi kupata huduma zote stahiki popote walipo ndani ya muda mfupi.

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Charles Mhina (kulia) akifafanua umuhimu wa Mfumo wa usimamizi wa utoaji vibali mbalimbali vya kusafirisha mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi unaojulikana kama “ Mifugo Management Information System (MIMIS)” wakati akifungua mafunzo ya mfumo huo kwa wadau na wataalam kutoka sekta za  Mifugo na Uvuvi yaliyofanyika leo (18.05.2022) kwenye hoteli ya Royal Village jijini Dodoma. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa upande wa sekta ya Mifugo, Baltazari Kibola.


Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo nchini Prof. Hezron Nonga (kushoto) na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji (Maji baridi) Dkt. Iman Kapinga wakinukuu sehemu ya hotuba ya   Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Charles Mhina (hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo ya mfumo wa usimamizi wa utoaji vibali mbalimbali vya kusafirisha mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi unaojulikana kama “ Mifugo Management Information System (MIMIS)”   kwa wadau na wataalam kutoka sekta za  Mifugo na Uvuvi yaliyofanyika leo (18.05.2022) kwenye hoteli ya Royal Village jijini Dodoma.


Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya mfumo wa usimamizi wa utoaji vibali mbalimbali vya kusafirisha mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi unaojulikana kama “ Mifugo Management Information System (MIMIS)” wakimsikiliza Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Charles Mhina (hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo ya mfumo huo leo (18.05.2022) kwenye hoteli ya Royal Village jijini Dodoma.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni