Nav bar

Jumanne, 24 Mei 2022

BILIONI 5 KUTUMIKA KULINDA HIFADHI ZA BAHARI NCHINI

Na Mbaraka Kambona, 


Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) wamekubaliana kutekeleza Mradi wa kulinda na  kutunza baianuai ya ukanda wa Bahari ya Hindi katika Wilaya ya Mkinga iliyopo Mkoani Tanga.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki alibainisha hayo baada ya kufanya kikao kifupi na Mwakilishi wa shirika hilo nchini, Dkt. Katrina Bornemann kilichofanyika ofisini kwake  jijini Dodoma Mei 18, 2022.


Alisema lengo la mradi huo ambao utagharimu shilingi za kitanzania bilioni 5 ni kuhakikisha maeneo ya bahari pamoja na ukanda wa pwani Wilayani Mkinga yanalindwa na kuhifadhiwa ili yaweze kuwa endelevu na kuleta maendeleo kwa wananchi.


"GIZ wamekubali kutoka kiasi cha shilingi za kitanzania bilioni 5 kwa ajili ya kutunza mazalia ya samaki, maeneo tengefu na fukwe za bahari ili maeneo hayo yaweze kuwa na tija zaidi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla", alisema


Aliongeza kwa kusema kuwa  wameshakubaliana mradi huo utaanza mara moja na tayari shirika hilo limeshaidhinisha kiasi hicho cha pesa kitumike katika mradi huo utakaodumu kwa miaka 5.


"Tunalishukuru shirika hili la GIZ kwa kuamua kushirikiana nasi katika kutunza baianuai ya bahari nchini, ahadi yetu ni kuwa tutatekeleza mradi huu kwa ustadi na weledi mkubwa kuhakikisha kwamba matokeo yanayotarajiwa yanapatikana na yanaonekana hasa kwa wananchi wetu ambao wataguswa na mradi huu", alibainisha


Mwakilishi wa shirika hilo la GIZ hapa nchini, Dkt. Katrina Bornemann alifika jijini Dodoma kuonana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa lengo la kuutambulisha mradi huo ili uweze kuanza kutekelezwa mapema kama ilivyokusudiwa.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akipatiwa maelezo kuhusu mradi wa kutunza baianuai unaotarajiwa kutekelezwa hapa nchini na Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo kutoka nchini Ujerumani (GIZ), Dkt. Katrina Bornemann (kulia) walipokutana jijini Dodoma Mei 18, 2022. Kushoto ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ( Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akiagana na Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo kutoka nchini Ujerumani (GIZ), Dkt. Katrina Bornemann (kulia) muda mfupi baada ya kumaliza mazungumzo yao jijini Dodoma Mei 18, 2022. Kushoto ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni