Nav bar

Jumatatu, 17 Mei 2021

WAWEKEZAJI WATAKIWA KUGEUKIA FURSA YA KILIMO CHA MBEGU ZA MALISHO YA MIFUGO

Serikali imewataka wadau wa uwekezaji nchini kugeukia Sekta ya Mifugo hasa katika kutumia fursa ya changamoto ya uhaba wa mbegu za malisho ambayo mahitaji yake ni zaidi ya tani milioni 7 kulinganisha uzalishaji wa sasa wa tani 127 pekee.

Rai hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu  wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Elisante Ole Gabriel wakati akifungua warsha maalum ya wadau wa uzalishaji mbegu za malisho hapa nchini  Mkoani Morogoro 12, Mei 2021.

Alisema kuwa takwimu zinaonyesha kiwango cha uzalishaji wa mbegu ni mdogo ukilinganisha na mahitaji yake na kwamba kama wawekezaji wakigeuza changamoto hiyo kuwa fursa inasadia kwa kiasi kikubwa kuongeza uzalishaji.

“Mahitaji ya mbegu za malisho Tanzania ni tani milioni 7 lakini kiwango cha  mbegu kilichozalishwa kwa mwaka 2019/20 ni tani 127 maana yake ni kwamba kuna uhaba mkubwa sana ivyo changamoto hiyo tuichukulie kama fursa ya uwekezaji katika sekta hiyo” alisema Prof Gabriel.

Kadharika alisema Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi  itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo, makampuni na watu binafsi wenye nia ya kuzalisha mbegu bora za malisho, kufanya kazi hii kibiashara kwa kuwapa mwongozo unaostahili.

Alibainisha kuwa lengo ni kufanikisha juhudi hizi za Serikali hasa kujiletea faida za kiuchumi kupitia uwepo wa fursa ya wingi wa mifugo nchini na hata kuuza malisho katika mataifa mengine.

“Hii si tu kwamba itainua uchumi wa mtu binafsi bali italipatia Taifa fedha za kigeni, hasa tukizingatia kuwa wananchi wanaweza kutumia fursa ya ardhi iliyopo kuzalisha malisho kibiashara kama wanavyo zalisha mazao ya chakula”. alisema Prof. Gabriel

Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya Utafiti Mafunzo na huduma za Ugani, Dkt. Angello Mwilawa alisema lengo la warsha hiyo ni kuhakikisha tafiti zilizofanyika kubaini mbegu bora za malisho zinawafikia wafugaji wadogo kwenye mashamba yao.

Alisema zipo mbegu ambazo zimekuwa rahisi kuwafikia wafugaji kama mbegu aina ya Nyasi, mikunde inayotaambaa na mikunde jamii ya miti malisho ambazo zipo katika makundu tofauti ambazo pia mahitaji ya msingi katika mashamba ya malisho.

“Tunaona kuna fursa kubwa ya uzalishaji wa mbegu endelevu na hapa tunazungumzia mbegu mafungu matatu ambazo hizo tunaangalia ni namna gani tunaongeza uzalishaji hapa nchini” alisema Dkt. Mwilawa.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akifungua warsha ya wadau wa uzalishaji wa mbegu za malisho kwenye ukumbi wa Cate hotel Mkoani Morogoro (12.05.2021)

 


Mkurugenzi wa Utafiti Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Angello Mwilawa akimkaribisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Elisante Ole Gabriel (hayupo pichani), kufungua warsha ya uzalishaji wa mbegu za malisho kwenye ukumbi wa Cate hotel Mkoani Morogoro. (12.05.2021)


Mhadhiri mstaafu chuo kikuu cha Sokoine na Mwenyekiti mstaafu wa chama cha nyanda za malisho Tanzania, Prof. Ephraim Mtengeti akimshukuru Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (hayupo pichani) kwa kuweza kushiriki nao na kufungua warsha ya uzalishaji wa mbegu za malisho kwenye ukumbi wa Cate hotel Mkoani Morogoro 12.05.2021


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (waliokaa katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau walioudhuria warsha ya uzalishaji wa mbegu za malisho mara baada ya kufungua warsha hiyo kwenye ukumbi wa Cate hotel Mkoani Morogoro.  (12.05.2021)

Jumapili, 16 Mei 2021

KIKAO CHA MAKATIBU WAKUU WA NCHI ZA JUMUIYA YA MAENDELEO YA NCHI ZA KUSINI MWA AFRIKA (SADC) WENYE DHAMANA YA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah (katikati) akiongoza ujumbe wa Tanzania katika kikao cha makatibu wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wenye dhamana ya  kilimo, mifugo na uvuvi. Kulia kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Andrew Massawe na Katibu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel wakiwa kwenye maandalizi ya mkutano wa mawaziri wa SADC utakaofanyika Tarehe 07 Mei 2021. Mkutano huo umefanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma. Mkutano huo unafanyika kwa njia ya video na kuhudhuriwa na nchi wanachama wa SADC. (05.05.2021)

Wajumbe kutoka Tanzania wakiwa katika kikao cha makatibu wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wenye dhamana ya  kilimo, mifugo na uvuvi, kwa ajili ya maandalizi ya mkutano wa mawaziri wa SADC utakaofanyika Tarehe 07 Mei 2021. Ujumbe wa Tanzania umehudhuria mkutano huo kwenye ukumbi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma. Mkutano huo unafanyika kwa njia ya video na kuhudhuriwa na nchi wanachama wa SADC. (05.05.2021)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah (kushoto) ambaye anaongoza ujumbe wa Tanzania katika kikao cha makatibu wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wenye dhamana ya  kilimo, mifugo na uvuvi, akibadilishana mawazo na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Andrew Massawe (katikati) na Katibu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel kwa ajili ya maandalizi ya mkutano wa mawaziri wa SADC utakaofanyika Tarehe 07 Mei 2021. Ujumbe wa Tanzania umehudhuria mkutano huo kwenye ukumbi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma. Mkutano huo unafanyika kwa njia ya video na kuhudhuriwa na nchi wanachama wa SADC. (05.05.2021)

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sera na Mipango kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Bw. Adam Mwaigoga (katikati), Afisa Uvuvi Mwandamizi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Didas Mtambalike (kulia) na Mkurugezi wa Idara ya Sera na Mipango kutoka Wizara ya Kilimo Bw. Obadiah Nyagiru wakibadilishana mawazo kabla ya kuanza kwa kikao cha maandalizi ya mkutano wa mawaziri wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wenye dhamana ya  kilimo, mifugo na uvuvi, utakaofanyika Tarehe 07 Mei 2021. Ujumbe wa Tanzania umehudhuria mkutano huo kwenye ukumbi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma. Mkutano huo unafanyika kwa njia ya video na kuhudhuriwa na nchi wanachama wa SADC. (05.05.2021)


Ijumaa, 7 Mei 2021

WAVUVI WAHIMIZWA KUJIUNGA KWENYE VYAMA VYA USHIRIKA

Serikali imeendelea kuhamasisha uanzishwaji na uimarishaji wa vikundi na vyama vya ushirika vya msingi vya  wavuvi  wadogo kwa lengo la kuwapatia mtaji, ujuzi, vifaa pamoja na dhana za uvuvi katika maeneo ya mwambao wa bahari ya hindi , maziwa, mabwawa na mito ili kuzalisha ajira na kipato. 

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), bungeni leo wakati akijibu swali la Mbunge wa Nyasa, Mhe. Eng. Stella Manyanya   ambaye alitaka kufahamu mikakati ya Serikali katika kuhakikisha mikopo inatolewa kwa mtu mmoja mmoja aliye tayari, kuliko kutoa kupitia vikundi jambo ambalo linachelewesha ukuaji wa sekta ya uvuvi.

Mhe. Ulega alisema kuwa katika kutekeleza ilani  kwa mwaka wa fedha 2020/2021 serikali iliadhimia kuhamasisha wavuvi na wakuzaji viumbe maji kujiunga kwenye vyama vya ushirika ili kuwa na sauti ya pamoja ikiwa ni rahisi kutatua changamoto zinazowakabili kwa pamoja na kuwa na usimamizi endelevu wa rasilimali za uvuvi.

Aidha Serikali iliwezesha vyama vya ushirika kwa kuvipatia elimu, dhana na vifaa bora vya uvuvi kama vile injini za boti, pamoja na kuviunganisha na taasisi za fedha ili kupata mikopo yenye riba na masharti nafuu kwa lengo la kufanya shughuli zao kwa tija.

"Mhe. Naibu Spika kutokana na ilani ya chama cha mapinduzi Serikali itaendelea kuvihamasisha na kuviendeleza vyama vya ushirika, aidha mtu mmoja mmoja anayo fursa ya kuomba injini za boti kupitia taasisi za kifedha nchini.” Alisema Mhe. Ulega

Ulega aliongezea kuwa Serikali imejipanga vyema katika kuhakikisha wavuvi wote nchini wanapata suluhu ya changamoto zinazo wakabili wakiwemo wavuvi wa ziwa Nyasa na ndio maana imejipanga pia kwenda kuhakikisha inajenga soko la kisasa katika eneo la mwambao wa ziwa Nyasa.

Akijibu swali la nyongeza la Mhe. Mwamtum Zodo, ambaye alitaka kufahamu mkakati wa Serikali wa kuwakwamua wavuvi wa pembezoni mwa bahari ya hindi, kwa mikoa ya Tanga, Dar- es- salaam, Pwani, Lindi na Mtwara katika kushiriki kwenye uchumi wa bluu, Mhe. Ulega alisema Serikali ya awamu ya sita inayo ongozwa  Mhe. Samia Suluhu Hassan, inayo mkakati madhubuti ya kuhakikisha inawasaidia wavuvi wa ukanda wa Pwani hasa kuendana na uchumi wa bluu kwa kuongeza uzalishaji kwa wavuvi kwa kuweka miamba ya kuvutia samaki na kutengeneza katika ukanda wote wa pwani

“Tutahakikisha kwamba tunatengeneza vichanja vya kukaushia samaki ili kusaidia kutopoteza mazao ya uvuvi wanayo zalisha, kwa kuoza na kuaribika, tunataka tuhakikishe samaki wote wanaozalishwa kwenye ukanda wa pwani hawaaribiki kwa sababu tutawaongezea thamani kwa kuwakausha lakini vilevile tutakwenda kuongeza uzalishaji wa barafu na kuwa na “cold rooms” za kutosha katika ukanda mzima wa pwani ili kuweza kuutumia vyema uchumi wa bluu na kuongeza kipato cha mvuvi mmoja mmoja na hatimae kuongeza kipato cha Serikali yetu. Alisema Ulega.

Hata hivyo ametoa wito kwa wabunge wote kuhimiza wavuvi na wakuzaji viumbe maji wa maeneo yao kujiunga kwenye vyama vya ushirika vya wavuvi kama chachu ya kuwaletea maendeleo.

WAKAGUZI WA NGOZI WATAKIWA KUHAKIKISHA UZALISHAJI WA NGOZI BORA*

  

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa mafunzo na kuwakabidhi majukumu wakaguzi wa ngozi 33, kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria ili kuhakikisha ngozi inayozalishwa nchini inakuwa bora.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe, kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw.  Gabriel Bura, aliyasema hayo wakati wa kufunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wakaguzi wa ngozi yaliyofanyika jijini Mwanza Mei 5, 2021.

Alisema, wakaguzi wa ngozi waliopatiwa mafunzo kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara na Simiyu wanatakiwa kuongeza usimamizi wa sheria ya biashara ya ngozi.

“Hii ni kutokana  na kati ya  asilimia 100 ya ngozi zinazopelekwa viwandani,  asilimia 10  ndizo zinafaa kusindikwa  na kutengenezea bidhaa huku asilimia 90 hazifai kutokana na kukosa ubora unaotakiwa, ambapo jambo hilo limekuwa likisababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara na wenye viwanda.” Alisema

Aliongeza kuwa watahakikisha uzalishaji wa ngozi unakuwa bora kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya viwanda, kwani kumekuwa na changamoto ya ubora hafifu wa ngozi zinazozalishwa hapa nchini hasa kwenye maeneo ya machinjio, wakati wa usafirishaji na mfugaji mwenyewe.

Bw. Bura alisema ili kukabiliana na changamoto hiyo Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliamua kuteua wakaguzi na kuwakabidhi majukumu ili waweze kusimamia ngozi kwenye machinjio, inazalishwa  kwa kuhakikisha hazitobolewi na zinahifadhiwa vizuri kwa njia ile inayokubalika ya kutumia chumvi na zinaposafirishwa vibali vitolewe na zifike kwenye viwanda vilivyopo na vinavyofanya kazi ili kuepusha changamoto ya ngozi kutokufika kiwandani.

"Kuwepo kwa wakaguzi kutasaidia kujua ngozi imetolewa lini na kwa kiasi gani na zinatarajiwa kufika wapi, ndiyo sababu ya mafunzo haya,  tunatarajia baada ya mafunzo ubora wa ngozi utaongezeka.

"Mwanzo viwanda vilikuwa vinapata asilimia 10 pekee ya ngozi bora lakini tunaamini ubora wa ngozi utaongezeka kutoka asilimia 10 sasa hadi kufikia asilimia 80 mwaka 2022, kuwa zikifika kiwandani zinaweza kusindikwa na kutengenezea bidhaa," Alisema Bw. Bura.

Sambamba na hayo alisema ubora wa ngozi unachangiwa na afya ya mnyama mwenyewe na kama ameathiriwa na magonjwa hata ngozi itakuwa haina ubora unaotakiwa kwa hiyo kwa kutoa chanjo watakuwa wamedhibiti magonjwa ambapo kwa kumuogesha mnyama watakuwa wamesaidia asishambuliwe na wadudu  mfano ng'ombe akiwa ameshambuliwa na kupe katika kusindika ngozi alama za kupe au michirizi itaonekana kwenye ile bidhaa itakayokuwa imezalishwa hivyo bidhaa hiyo haitauzwa kwa bei inayotakiwa.

Kwa upande wake afisa wa ngozi mstaafu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, mkufunzi wa mafunzo hayo Bw. Emmanuel Muyinga alisema, moja ya maeneo ambayo amewasisitiza wakaguzi wa ngozi ni kusimamia wachunaji wa ngozi katika machinjio kwa sababu ndipo ngozi zinapozalishwa katika changamoto yote ya mnyororo wa thamani tatizo la uharibifu wa ngozi katika machinjio linachangia kwa kiwango kikubwa sana.

Bw. Muyinga alisema, ngozi ikishatobolewa inapunguza thamani, hivyo amesisitiza namna ya kuhifadhi ngozi baada ya kuchuna ambapo ngozi inatakiwa isikae zaidi ya saa nne katika machinjio baada ya kuchunwa ili iweze kufika katika mkondo wa biashara kabla ya kuanza kuoza.

Hata hivyo amewasisitiza Wakaguzi hao wakasimamie madaraja ya ngozi hali itakayosaidia kila mmoja katika eneo lake pindi wanapofanya uchambuzi wa madaraja kuzingatia na kuona ni madhara gani yanaathiri ngozi hivyo watatayarisha mpango kazi wa kuweza kutatua changamoto katika eneo husika linalokabili uzalishaji wa ngozi.

Naye Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Emmily Kasagala, amewaasa washiriki wa mafunzo hayo kujiepusha na vitendo vya ukosefu wa maadili na uonevu na badala yake wajenge mazingira rafiki kwa wadau kufanya biashara.


Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo Usalama wa Chakula na Lishe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Gabriel Bura akiongea na wakaguzi wa ngozi (hawapo pichani) walioudhuria mafunzo ya kuwajengea uwezo wakaguzi hao kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa yaliyofanyika Mkoani Mwanza. 05.05.2021)


Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Bw. Emmily Kasagala akizungumza kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo wakaguzi wa ngozi kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa yaliyofanyika Mkoani Mwanza. (05.05.2021)


Mkufunzi wa mafunzo, Bw. Emmanuel Muyinga akitoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wakaguzi wa ngozi (hawapo pichani) kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa yaliyofanyika Mkoani Mwanza. (05.05.2021)Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Gabriel Bura (waliokaa katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya ngozi mara baada ya mafunzo hayo yaliyofanyika Mkoani Mwanza. (05.05.2021)

Jumamosi, 1 Mei 2021

SIKU YA WAFANYAKAZI DUNIANI


 

WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUPIMA AFYA ZAO MARA KWA MARA

 Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo),  Prof. Hezron Nonga, ametoa wito kwa  watumishi wa umma kupima afya zao mara kwa mara ili kutambua afya zao kama ambavyo muongozo wa kudhibiti virusi vya ukimwi (VVU), Ukimwi na magonjwa sugu yasiyo ambukiza mahala pa kazi unavyowataka.

 

Prof. Nonga, aliyasema hayo  wakati akifungua mafunzo pamoja na upimaji wa afya kwa watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi yaliyofanyika Jijini Dodoma Aprili 30, 2021.

 

Alisema kuwa upimaji wa afya kwa watumishi wa umma kwa mujibu wa muongozo huo wa mwaka 2014 ni jambo la lazima siyo hiyari.

 

“Kupima afya ni jambo la lazima na muhimu sana kwa mtumishi kwani itasaidia hata kuongeza tija katika taasisi baada ya kutambua afya yake” amesema Prof.Nonga.

 

Aidha amesema kuwa kwa kutambua afya za wafanyakazi kutamwezesha  mwajiri kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa jukumu mbalimbali.

 

“Kama mtumishi atakuwa na afya njema basi atasaidia kuongeza uzalishaji katika taasisi hivyo wafanyakazi wanatakiwa kupima afya zao kwa mujibu wa muongozo huo wa kudhibiti vvu, ukimwi, pamoja na magonjwa sugu yasiyoambukiza” alisisitiza Prof. Nonga.

 

Aliongeza  kuwa, kwa mtumishi ambaye atabainika mara baada ya vipimo kuwa ana maambukizi ya virusi vya ukimwi taratibu zinamtaka mwajiri wake kumpatia kiasi cha Sh. 100,000 kila mwezi.

 

Alisema kuwa mafunzo hayo kwa wafanyakazi, watapatiwa mada mbalimbali kutoka kwa watalaam wa masula ya afya.

 

“Wafanyakazi wanatakiwa pia kufanya mazoezi ili kuondokana na tatizo la uzito uliopitiliza pamoja na msongo wa mawazo” alisema.

 

Kwa upande wake mtoa mada katika mafunzo hayo Daktari Bingwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dkt. Garvin Kweka, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuongea na watumishi ili kuwasaidia kujenga tabia ya kutambua afya zao mara kwa mara.

 

“Leo nimekuja kuzungumza na watumishi hawa kwani tumekuwa tukipoteza nguvu kazi nyingi kutokana na magonjwa, asilimia 60 ya watumishi inaonyesha wana tatizo la uzito kupindukia pamoja na msongo wa mawazo kwa hiyo mafunzo haya yatawasaidia kutambua nini wafanye na kipi wasifanye ili kuwa na afya njema, ili kuendelea kuleta tija katika maeneo yao ya kazi”alisema Dk.Kweka.

 

Naye Mratibu wa Ukimwi, Vvu na magonjwa sungu yasiyoambukiza mahala pa kazi Sekta ya Mifugo Rachel Maliselo, amesema kuwa lengo la zoezi hilo ni kutoa fursa kwa wafanyakazi kupima afya zao kwa mujibu wa muongozo huo.

 

Alisema wafanyakazi wamefurahi sana kupata fursa hii kwani inawapa nafasi ya kutambua afya zao na kufanya kazi  kwa bidii na kuongeza tija katika maeneo yao ya  kazi.

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Hezron Nonga akizungumza na watumishi wa Wizara hiyo (hawapo pichani) wakati akifungua mafunzo pamoja na upimaji wa afya yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma Aprili 30, 2021.


Baadhi ya watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ( Mifugo) walioshiriki mafunzo pamoja na upimaji  afya yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma. Aprili 30, 2021.


Kaimu Mkurugenzi Idara ya Utawala na Rasilimali watu, Bw. Fraksed Mushi, akimkaribisha Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Hezron Nonga (hayupo pichani) kufungua mafunzo pamoja na upimaji wa afya yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma 31.04.2021.


Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Hezron Nonga akiongoza watumishi wa Wizara hiyo (hawapo pichani) kwenye zoezi la upimaji afya mtumba jijini Dodoma Aprili 30, 2021.


Daktari Bingwa wa magonjwa yasiyo ambukiza kutoka hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Garvin Kweka akieleza lengo la kutoa mafunzo  ikiwa ni pamoja na kuwasaidia watumishi  kujenga tabia  ya  kupima na kutambua afya zao mara kwa mara mtumba jijini Dodoma. Aprili 30, 2021.