Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa mafunzo na kuwakabidhi majukumu wakaguzi wa ngozi 33, kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria ili kuhakikisha ngozi inayozalishwa nchini inakuwa bora.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe, kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Gabriel Bura, aliyasema hayo wakati wa kufunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wakaguzi wa ngozi yaliyofanyika jijini Mwanza Mei 5, 2021.
Alisema, wakaguzi wa ngozi waliopatiwa mafunzo kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara na Simiyu wanatakiwa kuongeza usimamizi wa sheria ya biashara ya ngozi.
“Hii ni kutokana na kati ya asilimia 100 ya ngozi zinazopelekwa viwandani, asilimia 10 ndizo zinafaa kusindikwa na kutengenezea bidhaa huku asilimia 90 hazifai kutokana na kukosa ubora unaotakiwa, ambapo jambo hilo limekuwa likisababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara na wenye viwanda.” Alisema
Aliongeza kuwa watahakikisha uzalishaji wa ngozi unakuwa bora kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya viwanda, kwani kumekuwa na changamoto ya ubora hafifu wa ngozi zinazozalishwa hapa nchini hasa kwenye maeneo ya machinjio, wakati wa usafirishaji na mfugaji mwenyewe.
Bw. Bura alisema ili kukabiliana na changamoto hiyo Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliamua kuteua wakaguzi na kuwakabidhi majukumu ili waweze kusimamia ngozi kwenye machinjio, inazalishwa kwa kuhakikisha hazitobolewi na zinahifadhiwa vizuri kwa njia ile inayokubalika ya kutumia chumvi na zinaposafirishwa vibali vitolewe na zifike kwenye viwanda vilivyopo na vinavyofanya kazi ili kuepusha changamoto ya ngozi kutokufika kiwandani.
"Kuwepo kwa wakaguzi kutasaidia kujua ngozi imetolewa lini na kwa kiasi gani na zinatarajiwa kufika wapi, ndiyo sababu ya mafunzo haya, tunatarajia baada ya mafunzo ubora wa ngozi utaongezeka.
"Mwanzo viwanda vilikuwa vinapata asilimia 10 pekee ya ngozi bora lakini tunaamini ubora wa ngozi utaongezeka kutoka asilimia 10 sasa hadi kufikia asilimia 80 mwaka 2022, kuwa zikifika kiwandani zinaweza kusindikwa na kutengenezea bidhaa," Alisema Bw. Bura.
Sambamba na hayo alisema ubora wa ngozi unachangiwa na afya ya mnyama mwenyewe na kama ameathiriwa na magonjwa hata ngozi itakuwa haina ubora unaotakiwa kwa hiyo kwa kutoa chanjo watakuwa wamedhibiti magonjwa ambapo kwa kumuogesha mnyama watakuwa wamesaidia asishambuliwe na wadudu mfano ng'ombe akiwa ameshambuliwa na kupe katika kusindika ngozi alama za kupe au michirizi itaonekana kwenye ile bidhaa itakayokuwa imezalishwa hivyo bidhaa hiyo haitauzwa kwa bei inayotakiwa.
Kwa upande wake afisa wa ngozi mstaafu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, mkufunzi wa mafunzo hayo Bw. Emmanuel Muyinga alisema, moja ya maeneo ambayo amewasisitiza wakaguzi wa ngozi ni kusimamia wachunaji wa ngozi katika machinjio kwa sababu ndipo ngozi zinapozalishwa katika changamoto yote ya mnyororo wa thamani tatizo la uharibifu wa ngozi katika machinjio linachangia kwa kiwango kikubwa sana.
Bw. Muyinga alisema, ngozi ikishatobolewa inapunguza thamani, hivyo amesisitiza namna ya kuhifadhi ngozi baada ya kuchuna ambapo ngozi inatakiwa isikae zaidi ya saa nne katika machinjio baada ya kuchunwa ili iweze kufika katika mkondo wa biashara kabla ya kuanza kuoza.
Hata hivyo amewasisitiza Wakaguzi hao wakasimamie madaraja ya ngozi hali itakayosaidia kila mmoja katika eneo lake pindi wanapofanya uchambuzi wa madaraja kuzingatia na kuona ni madhara gani yanaathiri ngozi hivyo watatayarisha mpango kazi wa kuweza kutatua changamoto katika eneo husika linalokabili uzalishaji wa ngozi.
Naye Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Emmily Kasagala, amewaasa washiriki wa mafunzo hayo kujiepusha na vitendo vya ukosefu wa maadili na uonevu na badala yake wajenge mazingira rafiki kwa wadau kufanya biashara.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo Usalama wa Chakula na Lishe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Gabriel Bura akiongea na wakaguzi wa ngozi (hawapo pichani) walioudhuria mafunzo ya kuwajengea uwezo wakaguzi hao kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa yaliyofanyika Mkoani Mwanza. 05.05.2021)
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Bw. Emmily Kasagala akizungumza kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo wakaguzi wa ngozi kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa yaliyofanyika Mkoani Mwanza. (05.05.2021)
Mkufunzi wa mafunzo, Bw. Emmanuel Muyinga akitoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wakaguzi wa ngozi (hawapo pichani) kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa yaliyofanyika Mkoani Mwanza. (05.05.2021)
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Gabriel Bura (waliokaa katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya ngozi mara baada ya mafunzo hayo yaliyofanyika Mkoani Mwanza. (05.05.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni