Nav bar

Alhamisi, 24 Juni 2021

WANAWAKE WANAOJIHUSISHA NA UVUVI WATAKIWA KUWA WABUNIFU


Wanawake wanaojihusisha na  shughuli za uvuvi wametakiwa kuwa wabunifu ikiwa ni pamoja na kujengeana uwezo Ili kukuza biashara zao huku wakikumbushwa   kujilinda dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi.

Ushauri huo umetolewa (24.06.2021)  na Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mara, Bi. Neema Ibamba katika warsha ya siku tatu ya wadau hao Mjini Musoma Mkoani Mara.

Ibamba amesema kuwa  biashara yoyote inahitaji ubunifu  na kwamba wadau hao kutoka Mikoa ya Kanda ya ziwa lazima waende na wakati.

Aliongeza kuwa ubunifu unaotakiwa ni pamoja na kuwa na vifungashio vizuri  vya kisasa kwa ajili ya bidhaa zao pamoja na kuangalia fursa nyingine za masoko zinazowagusa.

Aidha katika kukuza kipato cha familia, Ibamba amewataka wanawake kuendelea kushirikiana na waume zao badala ya kuwadharau kutokana na kipato wanachopata.

"Biashara ama kupata kipato kisiwe kigezo cha kufanya dharau kwa wanaume wenu kwa kuwa mna pesa, hakikisheni kile mnachokipata mnakiweka mezani ili kiwasaidie," alisema Ibamba.

Aidha Ibamba amewataka wanawake hao kujua mbinu mbalimbali za kuweza kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi hususani katika mialo ya kuuzia samaki na  dagaa na kuwaasa kuendelea kushikamana kwa umoja wao Ili waweze kupiga hatua kwenye biashara zao kwa sasa na siku zijazo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji  wa Shirika la  Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo   (EMEDO), Bi.Editrudith Lukanga amesema kuwa ushirikiano ndiyo njia pekee ya kuwafikisha wanawake katika mafanikio.

Lukanga amewataka wanawake hao  kuendelea kushirikiana na waume zao Ili kulinda ndoa zao badala ya kuwa chanzo cha migogoro katika ndoa hizo.

Ameongeza kuwa shirika lao limekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha Umoja wa Wanawake wanaojihusisha na Uvuvi (TAWFA) unazidi kuimarika na kuhusisha kundi kubwa.

Kwa upande wake, Afisa Uvuvi Mwandamizi ambaye pia ni mratibu wa dawati la jinsia la Uvuvi la Wizara kutoka Wizara ya Mifugo na Uvivi, Bi. Upendo Hamidu  amesema kuwa Wizara hiyo itahakikisha inaweka mipango imara Ili kuwasaidia wanawake katika shughuli zao.

Warsha hiyo ya siku tatu imeandaliwa na  Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Shirika la EMEDO na kufanyika  mjini Musoma mkoani Mara.


Mgeni Rasmi ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya jamii Mkoa wa Mara, Bi. Neema Ibamba akiongea na washiriki wa warsha ya wanawake wanaojihusisha na Uvuvi (TAWFA) Kanda ya ziwa (hawapo pichani) kwenye warsha hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa John Ludini Mwembeni Complex Musoma. 24/06/2021.

Mteknolojia wa samaki Mwandamizi,  Bw. Masui Munda akiwasihi washiriki wa washra ya wanawake wanaojihusisha na Uvuvi (TAWFA) Kanda ya ziwa  kushirikiana kwa kushikana mikono Ili kuweza kupata maendeleo  zaidi Mkoani Mara. (24/06/2021)

Afisa Uvuvi Mwandamizi na Mratibu wa dawati la jinsia la Uvuvi la WMUV, Bi. Upendo Hamidu (picha ya juu), Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO), Bi. Editrudith Lukanga (kushoto) na Mwenyekiti wa NTT, Mr. Yahya Mgawe wakiongea na washiriki wa warsha ya wanawake wanaojihusisha na Uvuvi (TAWFA) hawapo pichani wakati wa warsha hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa John Ludini Mwembeni Complex Musoma. (24/06/2021)

Mgeni rasmi ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya jamii Mkoa wa Mara, Bi. Neema Ibamba (katikati waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa warsha mara baada ya warsha ya wanawake wanaojihusisha na Uvuvi (TAWFA) Kanda ya ziwa iliyofanyika kwenye ukumbi wa John Ludini Mwembeni Complex Musoma (24/06/2021.)


Jumapili, 20 Juni 2021

KAMATI YARIDHISHWA NA ELIMU YA UVUVI HARAMU BWAWA LA MTERA

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imeridhishwa na elimu iliyotolewa kuhusu uvuvi haramu kwa wavuvi wa bwawa la Mtera.

 

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dkt. Christine Ishengoma ameyasema hayo leo (19.06.2021) baada ya kamati kumaliza ziara yake kwenye kijiji cha Misisiri wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma na kijiji cha Mnadani wilaya ya Iringa ambapo walizungumza na wavuvi na wananchi wa maeneo hayo.

 

Dkt. Ishengoma amesema katika vijiji vyote walivyopita wamekuta wavuvi na wananchi kwa ujumla wanayo elimu kuhusu uvuvi haramu na wanashiriki katika kudhibiti kwa kukamata nyavu haramu na kuziteketeza.

 

Wavuvi wametakiwa kuendelea kudhibiti uvuvi haramu katika bwawa hilo ambalo kwa sasa samaki wamepungua katika baadhi ya maeneo kutokana na Uvuvi haramu.

 

Dkt. Ishengoma amewaahidi wananchi wa kijiji cha Mnadani kuwa atalifikisha tatizo la wingi wa viboko katika bwawa hilo kwa Waziri wa Maliasili na Utalii ili aweze kulishighulikia.

 

Naye Katibu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah amesema kuwa wizara imekuwa ikitoa elimu kuhusu uvuvi haramu na madhara yake kwa wavuvi na wananchi wanaolizunguka bwawa la Mtera ambapo kwa sasa wananchi hao wamekuwa wakishirikiana na serikali kudhibiti na kuteketeza nyavu zisizofaa zilizokamtwa.

 

Dkt. Tamatamah amewaahidi wavuvi wa kijiji cha Miseseri kuwaletea injini moja ya boti mwezi Julai, 2021 ambayo pamoja na shughuli za uvuvi itawasaidia katika kufanya doria za kudhibiti uvuvi haramu.

 

Pia amewaahidi wananchi hao kuwa atawatuma wataalam wa  utafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) kuja kuangalia kutafiti Kama upo uwezekano wa kuweka mbegu ya samaki ili kusaidia kuongeza wingi wa samaki katika bwawa.

 

Dkt. Tamatamah amewasisitiza wavuvi kujiunga kwenye vyama vya ushirika ili waweze kukopesheka na kuweza kupata zana sahihi za uvuvi ambazo mara nyingine hutolewa na wizara.

 

Mkazi wa kijiji cha Mnadani kata ya Izazi wilayani Iringa, Bw. Amiri ameieleza kamagi hiyo kuwa viboko katika bwawa hilo wameongezeka na wamekuwa wakijeruhi na hata kuwauwa wavuvi na hivyo kusababisha wavuvi kutokwenda kuvua. Tatizo hili limefanya samaki kuwa wachache katika masoko na kuwafanya wavuvi kutafuta shughuli nyingine za kuwaingizia kipato na hivyo ameiomba kamati kuwasaidia kulitatua tatizo hilo.

 

Wananchi katika vijiji vyote viwili wameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge na wizara kwa kuwatembele na kusikiliza matatizo waliyonayo na wanaomani kuwa matatizo yao yatatafutiwa ufumbuzi.


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Dkt. Christina Ishengoma akizungumza na wananchi wa kijiji cha Msisiri Kata ya Chipogolo wilayani Mpwapwa wakati kamati hiyo ilipotembelea kijijini hicho kusikiliza changamoto za wavuvi na wananchi kuhusu maendeleo ya Bwawa la Mtera. (19.06.2021)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akijibu maswali ya wananchi wa kijiji cha Msisiri (hawapo pichani) kilichopo Kata ya Chipogolo wilayani Mpwapwa wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ilipotembelea kijiji hicho na kusikiliza kero za wavuvi pamoja na wananchi kuhusu maendeleo ya Bwawa la Mtera. (19.06.2021)

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ambaye pia ni Mbunge wa Mvumi, Livingstone Lusinde akitoa mapendekezo yake kwa wananchi wa kijiji cha Msisiri kilichopo wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma mara baada kamati hiyo kutembelea kijiji hicho kuhusu Maendeleo ya Bwawa la Mtera. (19.06.2021)


Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Msisiri wakifatilia majibu na maelekezo yaliyokuwa yakitolewa na viongozi wakati wa mkutano wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji walipofika kuzungumza na wananchi wa kijiji hicho kilichopo Kata ya Chipogolo wilayani Mpwapwa  kuhusu za maendeleo ya Bwawa la Mtera. (19.06.2021)


Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Dkt. Christina Ishengoma akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mnadani Kata ya Izazi wilayani Iringa, Mkoani Iringa baada ya kamati hiyo kufanya ziara na kuzungumza na kuwasikiliza wananchi hao kuhusu maendeleo ya Bwawa la Mtera. (19.06.2021)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akitoa ufafanuzi kwa wananchi wa kijiji cha Mnadani Kata ya Izazi wilayani Iringa Mkoani Iringa wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji iliyosikiliza maoni na kero za wananchi kuhusu maendeleo ya Bwawa la Mtera. (19.06.2021)

Mvuvi wa Samaki, Amir Kiselo akitoa maoni yake kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ilipotembelea kijiji cha Mnadani Kata ya Izazi wilayani Iringa Mkoani Iringa kuhusu Maendeleo ya Bwawa la Mtera. (19.06.2021)


Afisa Uvuvi Kata ya Izazi, Onesmo Peter akielezea changamoto wanazozipata wavuvi katika Bwawa la Mtera wakati ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ilipotembelea kijiji hapo wilayani Iringa kwa lengo la kujua Maendeleo ya Bwawa la Mtera. (19.06.2021)


Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mnadani wakifatilia majibu na maelekezo yaliyokuwa yakitolewa na viongozi (hawapo pichani) wakati wa mkutano wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji walipofika kuzungumza na wananchi wa kijiji hicho kilichopo Kata ya Izazi wilayani Iringa kuhusu za maendeleo ya Bwawa la Mtera. (19.06.2021)




Alhamisi, 17 Juni 2021

TAASISI ZA BIMA NA ZA FEDHA ZATAKIWA KUWA MKOMBOZI WA WAFUGAJI NA WAVUVI

Taasisi za bima na za kifedha zimetakiwa kuwa mkombozi kwa wafugaji na wavuvi kwa kuhakikisha wanakuwa na uwezo wa kuwa na bima ya mifugo na samaki itakayowasaidia kuwa na ulinzi wa uwekezaji wao na kuweza kukopesheka.

 

Haya yamesemwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega leo Juni 17, 2021 wakati akifungua kikao cha Wadau wa Dawati la Sekta Binafsi ambalo lipo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye ukumbi mdogo wa wizara uliopo kwenye ofisi za NBC jijini Dodoma.

 

Ulega amesema kuwa wafugaji na wavuvi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya kutokopesheka kirahisi na taasisi za kifedha na hivyo kuwafanya washindwe kuitumia fursa ya mikopo ambayo ipo ili kukuza mitaji yao na hatimaye kuongeza mitaji na kipato pia.

 

“Kutokana na changamoto hii, wizara imeona ni vema kuwakutanisha wadau wanaohusika ili wote kwa pamoja tujadili tatizo nini na nini kifanyike ili tutakapotoka hapa tuwe na suluhisho ambalo litajibu tatizo la wafugaji na wakulima kuhusu bima na mikopo,” alisema Ulega.

 

 

Ulega amesema kuwa mifugo na samaki ni uwekezaji na ni bishara kubwa hivyo taasisi hizi za bima na fedha lazima ziwe na mtazamo huo na kwamba kufanya kazi na wafugaji na wavuvi kutawaletea tija na wao wenyewe.

 

Lengo la wizara ni kuhakikisha uwekezaji na biashara kwenye sekta za mifugo na uvuvi zinakua na mchango wake katika kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla kinaongezeka. Vilevile amezishauri taasisi za fedha kuangalia uwezekano wa kupunguza riba kwenye mikopo ili wafugaji na wavuvi waweze kukopesheka kirahisi.

 

Vilevile amesisitiza kwa wataalam na wadau walioshiriki kikao hicho kuendelea kutoa elimu kwa wafugaji na wavuvi ili watambue kuwa mifugo na samaki walionao ni uwekezaji. Pia amesema biashara na uwekezaji ukishamiri na kukiwa na mazingira mazuri kila mtu atataka kuwekeza na kufanya biashara ya mifugo na samaki pamoja na mazao yake.

 

Naye Kaimu Katibu Mkuu anayeshughulikia sekta ya mifugo, Dkt. Bedan Masuruli amesema kuwa sekta za mifugo na uvuvi zinahitaji kuendelezwa na moja kitu kinachotakiwa ni mitaji hivyo kupitia kikao hicho anaamini kuwa tatizo la upatikikanaji mitaji litapatiwa majibu.

 

Mratibu wa Dawati la Sekta Binafsi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Stephen Michael amesema dawati lilifuatilia upatikanaji wa bima kwa wafugaji ili kuweza kuwasaidia wafugaji na wavuvi kupata mikopo. Shirika la Bima la Taifa (NIC), limetoa bima kwa vyama vya ushirika vya wafugaji vitatu na vyama vya ushirika vya wavuvi vitatu.

 

Kaimu Mkurugenzi wa Mipango, Utafiti, na Maendeleo ya Masoko ya Bima Tanzania, Bw. Muyengi Zakaria amesema kuwa wameshazielekeza kampuni zote za bima nchini waandae bidhaa ambazo zinakidhi mahitaji ya wafugaji na wavuvi. Lakini pia ni lazima kuwepo na muongozo ambao utawasaidia wafugaji na wavuvi kuhakikisha wanakata bima itakayowasaidia wakati wanapopatwa na majanga.

 

Kikao hicho cha wadau kilihudhuriwa na wawakilishi wa taasisi na kampuni za bima, taasisi za kifedha, wawakilishi wa vyama vya ushirika vya wafugaji na wavuvi pamoja na viongozi na wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akifungua kikao cha wadau wa bima kwa ajili ya mifugo na uvuvi (hawapo pichani) ambapo amezisisitiza kampuni za bima na taasisi za kifedha kuwasaidia wafugaji na wavuvi. Kikao hicho kimefanyika kwenye ukumbi mdogo wa wizara ulipo kwenye jengo la NBC jijini Dodoma. 17.06.2021)


Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Bedan Masuruli akizungumza wakati wa kikao cha wadau wa bima kwa ajili ya mifugo na uvuvi kilichofanyika kwenye ukumbi mdogo wa wizara ulipo kwenye jengo la NBC jijini Dodoma. Kushoto ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega. (17.06.2021)


Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Masiko na Mratibu wa Dawati la Sekta Binafsi, Bw. Stephen Michael akielezea kazi inayofanywa na dawati wakati wa kikao cha wadau wa bima kwa ajili ya mifugo na uvuvi kilichofanyika kwenye ukumbi mdogo wa wizara ulipo kwenye jengo la NBC jijini Dodoma. (17.06.2021)

Baadhi ya washiriki wa kikao cha wadau wa bima kwa ajili ya mifugo na uvuvi wakifatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (hayupo pichani) kilichofanyika kwenye ukumbi mdogo wa wizara ulipo kwenye jengo la NBC jijini Dodoma. (17.06.2021)


Jumanne, 15 Juni 2021

MAAFISA UVUVI 11 WAKABIDHIWA VITAMBULISHO VYA UKAGUZI WA MAZINGIRA

Maafisa Uvuvi kumi na moja (11) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wamekabidhiwa vitambulisho vitakavyowawezesha kufanya ukaguzi wa mazingira katika shughuli zote zinazofanyika katika maeneo ya uvuvi nchini.  

Maafisa hao walikabidhiwa vitambulisho hivyo baada ya kupatiwa mafunzo ya ukaguzi wa mazingira na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) yaliyofanyika  Julai 20 hadi 22, 2020 jijini Dar es Salaam.

Wakati akikabidhi vitambulisho hivyo, Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Bw. Magesa Bulayi katika tukio lililofanyika jijini Dodoma Julai 14, 2021, alisema kuwa anawakabidhi vitambulisho hivyo na ni imani yake kuwa  wataalamu hao  wa ukaguzi wataweza kusaidia kutatua vikwazo vinavyorudisha nyuma juhudi za Wizara katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira katika maeneo ya uvuvi.

Alisema sekta imekuwa ikikabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi na uharibifu wa mazingira unaotokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu zikiwemo shughuli zinazofanywa na wavuvi wenyewe.

“Niwapongeze watumishi walioshiriki mafunzo haya kwani utaalamu wao ndani ya sekta utapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto za kimazingira ambazo sekta imekuwa ikipambana nazo,” alisema Bulayi

Aliongeza kuwa, uhifadhi wa mazingira ni muhimu sana katika ustawi na uendelevu wa rasilimali za uvuvi hapa nchini kwani huchangia katika kutoa ajira kwa wananchi, lishe, kipato pamoja na kuliingizia taifa fedha za kigeni.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwapongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usalama wa Mazingira (NEMC) kwa kukubali kutoa mafunzo ambayo yamekuwa chachu na kuamsha ari ya kusimamia, kudhibiti na kuhifadhi mazingira ndani ya sekta huku akiongeza kuwa  mafunzo hayo yamekuwa kiungo kati ya sekta ya Uvuvi, NEMC na taasisi nyingine na kwa pamoja watashirikiana kikamilifu kupunguza changamoto za kimazingira katika utunzaji  rasilimali za uvuvi.

Bulayi alitoa wito  kwa Mkuu wa Kitengo cha Mazingira, Melton Kalinga kuendelea kuratibu mafunzo hayo kadiri fedha zitakapopatikana ili kuwa na wakaguzi katika kanda zote na mafunzo ya awamu ya pili yaguse pia idara ya ukuzaji viumbe maji.

“Natambua kitengo kina changamoto ya ufinyu wa bajeti, hata hivyo sekta itajitahidi kutafuta vyanzo vingine vya fedha ili kitengo kiweze kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa,” aliongeza Bulayi

Aliendelea kusisitiza kuwa sekta inawategemea katika masuala ya usimamizi wa mazingira hivyo wakafanye kazi kwa weledi, na watumie ujuzi waliopata ili kuongeza ufanisi katika utendaji wao.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Mazingira, Bw. Melton Kalinga aliomba mafunzo hayo yatengewe fedha za kutosha ili kuongeza idadi ya wataalamu wa ukaguzi wa mazingira kwa kuwa mahitaji bado ni makubwa.

Afisa Uvuvi Mkuu, Bw. Jerome Fundi aliwaasa washiriki wenzake kuwa vitambulisho walivyopata ni dhamana ambayo imetolewa na Serikali hivyo wavitumie kama ilivyokusudiwa na sio vinginevyo.


Kaimu Katibu Mkuu ((WMUV), Sekta ya Uvuvi, Bw. Magesa Bulayi akiongea na Maafisa Uvuvi (hawapo pichani) kabla ya kuwakabidhi vitambulisho vya ukaguzi wa mazingira kwenye ukumbi wa Wizara uliopo kwenye mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma. (14.06.2021)


Mkuu wa kitengo cha Mazingira kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Melton Kalinga akiongea na Maafisa Uvuvi wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vitambulisho vya wakaguzi wa mazingira Sekta ya Uvuvi iliyofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Wizara katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma. (14.06.2021)


Kaimu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Bw. Magesa Bulayi akimkabidhi Afisa Uvuvi Mwamdamizi, Bi. Emmanuela Xavier kitambulisho cha ukaguzi wa mazingira wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vitambulisho vya wakaguzi wa mazingira Sekta ya Uvuvi Jijini Dodoma. (14.06.2021)


Afisa Uvuvi Mwandamizi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Bw. Jerome Fundi akitoa neno la shukrani kwa Kaimu Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi, Bw. Magesa Bulayi (hayupo pichani) mara baada ya kukabidhiwa vitambulisho vya ukaguzi wa mazingira kwenye ukumbi wa Wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma. (14/06/2021.)


Kaimu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) (wa pili kutoka kulia mbele), Bw. Magesa Bulayi akiwa kwenye picha ya pamoja na maafisa uvuvi mara baada ya hafla fupi ya kukabidhi vitambulisho vya wakaguzi wa mazingira, kwenye ukumbi wa wizara hiyo jijini Dodoma. (14/06/2021)

Jumamosi, 12 Juni 2021

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE KILIMO, MIFUGO NA MAJI YAPEWA SEMINA KUHUSU NARCO

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imepewa semina kuhusu Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kwa malengo ya kujua majukumu yake, muundo wake, utekelezaji wa bajeti, mafanikio, changamoto na mikakati ya kutatua changamoto hizo.

 

Kamati imepatiwa semina hiyo leo (11.06.2021) katika ukumbi wa Msekwa D uliopo ndani ya Viwanja vya Bunge Jijini Dodoma ambapo viongozi wa Wizara waliongozwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega.

 

Akizungumza kuhusu semina hiyo Mhe. Ulega amesema kuwa wizara imeona ni wakati muafaka kufanya semina kuhusu NARCO ili wajumbe wa kamati hiyo waweze kuielewa na kutoa maoni yao ambayo yatasaidia sana katika kuhakikisha kampuni hiyo inaendelea kuimarika kwa kuongeza uzalishaji wa mitamba, nyama na kuzidi kuchangia kwenye pato la taifa.

 

Mhe. Ulega amesema kuwa Kampuni hiyo ya Ranchi za Taifa ilipita katika kipindi kigumu na hivyo kushindwa kujiendesha lakini kutokana na jitihada mbalimbali zilizofanywa na wizara kwa sasa Kampuni hiyo inajiendesha yenyewe.

 

Katika taarifa iliyowasilishwa kwenye Kamati hiyo, imeainisha mafanikio yaliyopatikana, mipango iliyopo ya kuongeza uzalishaji na maeneo ya vipaumbele yaliyopo katika bajeti ya mwaka 2020/2021. Maeneo hayo ni Kuboresha Ranchi tano (5) za Kongwa, Ruvu, Kalambo, Missenyi na West Kilimanjaro ili kuongeza tija katika mnyororo wa thamani wa mazao ya Mifugo, Kuongeza uzalishaji wa ng’ombe kwa njia ya Uhimilishaji (AI) - kwa kutumia mbegu bora za ng’ombe wa nyama kama vile Boran na Simental.

 

Maeneo mengine ni Kudhibiti vifo vya mifugo kwa kiwango kisichozidi 2% ya wastani wa mifugo, Kuongeza na kuboresha nyanda za malisho kwa kudhibiti na kuondoa vichaka na  kuimarisha vyanzo vya maji na Kuweka alama za kuonekana katika mipaka ya ranchi, kuondoa wavamizi na  kuimarisha ulinzi wa mipaka.

 

Naye Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Dkt. Christina Ishengoma amesema sasa ni wakati muafaka kwa Ranchi za Taifa kuanza kuzalisha malisho kwa ajili ya mifugo ambayo yataweza kuwasaidia hata wafugaji wanaozizunguka ranchi hizo. Vilevile ameshauri ranchi hizo ziweze kutumika kama mashamba darasa ambapo wafugaji hasa wa maeneo ya jirani wataweza kupata elimu juu ya ufugaji bora.

 

Akichangia baada ya taarifa kuwasilishwa mjumbe wa kamati hiyo, Mhe. Prof. Patrick Ndakidemi amesema kuwa ni wakati muafaka kwa kamati kuisaidia NARCO. Prof. Ndakidemi amesema kwa kuwa tayari kampuni hiyo imeshaandaa andiko mradi, ni vema wajumbe hao wakalisoma hilo andiko na kuona ni maeneo yapi kamati inaweza kuisaidia kampuni hiyo. Vilevile amewasihi NARCO kuendelea kuyatunza na kuyalinda maeneo yao kwani yanawasaidia wafugaji wenye changamoto ya maeneo ya malisho kwa kuwakodishia.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akizungumza wakati wa Semina ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu majukumu, muundo, mafanikio, changamoto na mikakati ya kutatua changamoto zinazoikabili Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) iliyofanyika kwenye ukumbi wa Msekwa D uliopo katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma. Wa pili kutoka kushoto ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai akifuatiwa na Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma. (11.06.2021)


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akifafanua jambo wakati wa Semina ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu majukumu, muundo, mafanikio, changamoto na mikakati ya kutatua changamoto zinazoikabili Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) iliyofanyika kwenye ukumbi wa Msekwa D uliopo katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma. (11.06.2021)


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Viongozi na Wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakifuatilia mada iliyokuwa ikiwasilishwa kuhusu Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) wakati wa semina iliyofanyika kwenye ukumbi wa Msekwa D uliopo katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma. (11.06.2021)

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakitoa maoni na kuuliza maswali mara baada ya kumalizika kwa uwasilishaji wa taarifa kuhusu Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) wakati wa semina iliyofanyika kwenye ukumbi wa Msekwa D uliopo katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma. (11.06.2021)



MENEJA MACHINJIO YA DODOMA APEWA MIEZI 3 KUBORESHA MIUNDOMBINU

Na Mbaraka Kambona, Dodoma

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega ametoa miezi mitatu (3) kwa Meneja wa Machinjio ya Dodoma, Victor Mwita kufanya maboresho ya miundombinu iliyopo katika machinjio hayo ili iweze kutoa huduma inayostahiki na kuchangia ipasavyo katika pato la taifa.

 

Waziri Ulega alitoa maelekezo hayo wakati alipofanya ziara ya kukagua machinjio hayo yaliyopo jijini Dodoma Juni 8, 2021 ambapo pamoja na mambo mengine alimtaka meneja huyo kutumia vyema mapato wanayokusanya ili kuboresha miundombinu ya machinjio hiyo.

 

“Natoa miezi mitatu (3) ya kuboresha miundombinu ya machinjio hii, na mimi nitakuwa nakuja hapa kila mwezi kuangalia ni maboresho gani mmeyafanya, madhumuni yetu machinjio hii iweze kutoa mchango unaohitajika kwa taifa,” alisema Ulega

 

Alisema kuwa lengo la Serikali ya awamu ya sita ni kuona machinjio hiyo inafanya kazi katika uwezo wake uliosimikwa ili mchango wa sekta ya mifugo katika pato la taifa uweze kuonekana.

 

Aidha, alitumia nafasi hiyo pia kuwakumbusha maafisa wanaohusika katika kukusanya mapato katika machinjio na maeneo mengine kuwa hawatamvumilia mtu yeyote asiyekusanya mapato ya Serikali.

 

“Tuko imara sana katika ukusanyaji wa mapato, afisa yeyote asiyekusanya mapato ya serikali tutamtoa mara moja, tunataka tuhakikishe watu wanakusanya kwa haki na huduma inayotolewa pia itolewe kwa haki, hili jambo tunataka kulisimamia bila muhali,” aliongeza Ulega

 

Aliendelea kusema kuwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali yaende sambamba na uboreshaji wa mazingira mazuri ya biashara ili kumfanya anayelipa ushuru aone ni haki na ni halali kulipa, kwani kwa kufanya hivyo biashara ya mifugo itashamiri zaidi.

 

Naye, Meneja wa Machinjio hiyo, Victor Mwita alisema kuwa wamepokea maelekezo yote ya Naibu Waziri huyo na aliahidi kuyatekeleza yote ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

 

Alisema mkakati watakaoanza nao ni kuhakikisha wanabana matumizi ili waweze kutumia vizuri mapato watakayoyapata kuboresha miundo mbinu ya machinjio hayo ili iweze kuleta tija zaidi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (katikati) akikagua miundombinu ya Machinjio ya Dodoma alipotembelea machinjio hayo yaliyopo jijini Dodoma Juni 8, 2021. Wa kwanza kushoto ni  Meneja wa Machinjio hayo, Victor Mwita.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akiongea na Waandishi wa Habari hawapo pichani alipofanya ziara ya kukagua Machinjio ya Dodoma yaliyopo jijini Dodoma Juni 8, 2021. Akiwa katika Machinjio hayo alishuhudia shehena ya nyama za Mbuzi zikipakiwa katika gari maalum la kubebea nyama hizo kwa ajili ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kuuzwa.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akiangalia Ng'ombe waliopelekwa katika Machinjio ya Dodoma kwa ajili ya kuchinjwa. Waziri Ulega alifanya ziara ya kukagua Machinjio hiyo Juni 8, 2021.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (wa pili kutoka kushoto) akishuhudia shehena ya nyama za Mbuzi zinazopakizwa katika gari maalum la kubebea nyama hizo kwa ajili ya kusafirishwa na kuuzwa nje ya nchi alipotembelea machinjio ya Dodoma yaliyopo jijini Dodoma Juni 8, 2021. Kulia ni Mmiliki wa shehena hiyo, Muhamad Azim.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (kulia) akiongea na Mfanyabiashara wa nyama za Mbuzi, Muhamad Azim alipokutana nae katika Machinjio ya Dodoma yaliyopo jijini Dodoma Juni 8,  2021. Waziri Ulega alifanya ziara ya kukagua Machinjio hayo na amemtaka Meneja wa machinjio hayo kufanya uboreshaji wa miundombinu ili iweze kutoa huduma stahiki.



Alhamisi, 10 Juni 2021

SERIKALI KUFUTA KODI YA ONGEZEKO LA THAMANI KWENYE VIFAA VYA UVUVI

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalla Ulega amesema Serikali imefuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye vifaa vingi vya uvuvi ikiwemo injini za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu, nyavu za uvuvi na vifungashio ili kuwasaidia wavuvi kupata zana za uvuvi kwa bei nafuu.

Mhe. Ulega aliyasema hayo Juni 09, 2021, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti maalum, Mhe. Sylivia Sigula ambaye alitaka kufahamu mpango wa Serikali katika kuwawezesha wavuvi wa Ziwa Tanganyika wavue kisasa ili kupata kipato Zaidi na kutoa ajira kwa vijana.

"Kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2011 na Sheria ya Mamlaka ya Mapato ya mwaka 2014, Serikali imefuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye vifaa vingi vya uvuvi ikiwemo injini za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu, nyavu za uvuvi na vifungashio ili kuwasaidia wavuvi kupata zana za uvuvi kwa bei nafuu," alisema Mhe. Ulega

Alisema kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri ili wavuvi wapate mikopo ya masharti na riba nafuu kutoka katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB) na kupitia Dirisha la Kilimo katika Benki ya Rasilimali (TIB). 

Aliongeza kuwa Wizara kupitia Dawati la Sekta Binafsi imeviunganisha vyama vya ushirika vya wavuvi na taasisi za fedha ambapo mikopo iliyoombwa na kupitishwa ni shilingi bilioni 2.6 na mikopo iliyotolewa ni shilingi milioni 560.7. 

“Wizara imehamasisha Benki ya Posta (TPB) kuanzisha na kuzindua Akaunti ya Wavuvi (Wavuvi account) kwa ajili ya mikopo na bima mahususi kwa wavuvi hususan wavuvi wadogo. “ Alisema Mhe. Ulega 

Aidha, Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wavuvi kufanya uvuvi wenye tija na kuwahimiza wavuvi kujiunga katika vikundi na kuanzisha vyama vya ushirika vya msingi, Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) na VICOBA ili waweze kukopesheka kwa urahisi na taasisi za fedha na hivyo kujikwamua kiuchumi.  

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti maalum, Mhe. Sylivia Sigula aliyetaka kufahamu kauli ya Serikali kwa vijana ambao wamejiunga kwenye vikundi na wamekidhi vigezo lakini hawajapatiwa vifaa vya kuvulia na mikopo, Mhe Ulega alisema juu ya mafunzo na uwezeshaji wa vijana yaliyokwisha kuanzishwa, kuna chuo cha uvuvi kilichopo kigoma mjini, tutahakikisha chuo kile kinafikia makundi yote  na aliomba Mhe. amuwasilishie vikundi vya ziwa Tanganyika kimoja baada ya kingine ili kuweza kuvifikia na kuviwezesha.

Aliongeza kuwa, Serikali hususan Wizara ya Mifugo na Uvuvi, tulifanya jitihada za makusudi za kuanzisha dawati la sekta binafsi na sasa limefanya kazi kubwa na kabla ya kuanzishwa kwa dawati idara ya uvuvi ilipata mikopo sawa na asilimia sifuri kwa wavuvi wadogo na baada ya kuanzishwa tumeipandisha hadi kufikia milioni mia tano na sitini.

Mkakati wetu ni kuhakikisha tunaimarisha Zaidi dawati la sekta binafsi kimkakati kwa ajili ya kuiwezesha sekta hii kupata pesa Zaidi.

“maandiko ya vikundi hivi vya wavuvi wetu tutayapitia na kuwawezesha waweze kuwashawishi benki kuweka pesa Zaidi." Alisema Mhe. Ulega.

Aliongeza kuwa dawati la sekta binafsi limefika pazuri na shirika la bima la Taifa linakwenda kutupelekea kupata bima ya wavuvi na bima ya mifugo ili mabenki yaweze kuwa na hamu ya kutoa pesa Zaidi.

Jumatano, 9 Juni 2021

SERIKALI KUENDELEA KUIMARISHA UVUVI BAHARI KUU - ULEGA

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema Serikali inaendelea na juhudi za Kuimarisha uvuvi wa bahari kuu kwa kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) ili kuiwezesha nchi kunufaika na rasilimali za uvuvi hususan zile zilizopo katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari na Bahari Kuu.

Mhe. Ulega aliyasema hayo Juni 07, 2021 wakati akijbu swali la Mbunge wa Kawe, Mhe. Askofu Josephat Gwajima ambaye alitaka kufahamu mpango madhubuti wa kutumia Bahari kwa programu za uvuvi wa Bahari Kuu na michezo ya bahari ili kutengeneza ajira kwa vijana wa Jimbo la Kawe hasa ikizingatiwa nusu ya Jimbo hilo  lipo mwambao wa Bahari ya Hindi.

Alisema hadi sasa Serikali ina mpango wa kununua meli tano (5) za uvuvi ambazo zitavua katika maji ya kitaifa, bahari kuu, pamoja na kutoa leseni kwa meli kubwa zinazomilikiwa na Sekta Binafsi.  

Aliongeza kuwa Serikali ina mpango wa Kujenga Bandari ya Uvuvi katika Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi ambapo uwepo wa Bandari hiyo utawezesha meli za uvuvi zinazovua katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari ya Tanzania na Bahari kuu, kutia nanga, kushusha Mazao ya Uvuvi na kupata huduma mbalimbali zikiwemo mafuta na chakula ambapo meli hizo zitachangia kutoa ajira kwa wananchi, wakiwemo wa Jimbo la Kawe. 

“Serikali inaendelea kuboresha mazingira na usalama wa fukwe ya Bahari ya Hindi ili kuwavutia wawekezaji kuwekeza katika shughuli mbalimbali za michezo katika fukwe hizo," Alisema Mhe. Ulega.

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kawe aliyetaka kufahamu siku ambayo Serikali italeta boti kwa ajili ya kuokoa inapotokea madhara na kujua siku serikali itatoa mikopo kwa wavuvi wadogo wadogo wanaotumia mitumbwi ili kuboresha uvuvi wao, Mhe. Ulega alisema Serikali kwa pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi , Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi kupitia polisi marine  na ofisi ya Waziri Mkuu zote zinafanya kazi kwa pamoja.

Alisema kwa sasa wana mkakati wa kuhakikisha kwamba panapatikana chombo au vyombo ambavyo vitakuwa vikifanya kazi hiyo ya doria na kazi hiyo itaratibiwa na ofisi ya Waziri Mkuu kwa hivyo na wananchi wa kawe wapo katika mpango wa namna hiyo. 

Aliongeza kuwa tumejipanga vyema katika bajeti yetu ya 2021/2022, Serikali ya awamu ya sita ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga vyema huku alitumia fursa hiyo kumkaribisha kwa ajili ya kuhakikisha vikundi na vijana wa pale kawe waweze kupata mashine za boti na waweze kujiunga kwenye vikundi  vitakavyo wasaidia  kutengeneza vichanja vya ukaushaji wa samaki na hata kutengeneza mashine za kuzalisha barafu wauziane wenyewe ili  kukomesha tatizo la upotevu wa mazao.

 

Jumamosi, 5 Juni 2021

SEKTA ZA MIFUGO TANZANIA BARA NA ZANZIBAR ZAIMARISHA USHIRIKIANO.

 

Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar zimekubaliana kuendeleza ushirikiano kiutendaji katika ngazi za idara na taasisi zikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Zanzibar (ZALIRI) 

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi  Prof. Elisante Ole Gabriel alisema hayo wakati wa mapitio ya taarifa ya kikao cha wataalam wa sekta ya Mifugo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kilichofanyika Juni 04, 2021 Jijini Dar es salaam.

Alisema utaandaliwa mkakati wa pamoja wa mawasiliano katika sekta hizo za pande mbili ili wadau pia watambue ushirikiano huo ambao umelenga kukuza uzalishaji katika sekta ya Mifugo hapa nchini.

Alisema pamoja na mambo mengine wataangalia namna ya kuwepo kwa urahisi wa utekelezaji wa vibali vya mazao ya mifugo ili vibali ambavyo vimetolewa Zanzibar vitambulike bara na vilivyotolewa bara vitambulike Zanzibar.

"Utaandaliwa mkakati wa pamoja wa mawasiliano katika sekta hizi za pande mbili ili wadau pia watambue ushirikiano huo ambao umelenga kukuza uzalishaji katika sekta ya Mifugo  nchini pamoja na kuwepo kwa urahisi wa utekelezaji wa vibali vya mazao ya mifugo" alisema Prof. Elisante

Aliongeza kuwa uamuzi huo umekusudia kuboresha mazingira ya kufanyia biashara ili kuleta manufaa ya kiuchumi kwa muungano na kwamba utaratibu na kukuza ubora wa wataalam wa mifugo.

Kadhalika alibainisha suala la tozo ya maziwa yaliyokuwa yakitoka Zanzibar (maziwa ya unga) ambapo mnufaika wa nafuu ya tozo hiyo ni Azam kwa makubaliano ya kuhakikisha anawezesha wazalishaji wa maziwa Zanzibar kuendelea na waliazimia aendelee na tozo iliyoazimiwa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar Maryam Juma Sadalla alisema matayarisho ya sheria ya mifugo ni muhimu lifanyike kwa wakati kama walivyokubaliana ili kukuza sekta ya mifugo  Nchini.

Alisema kukamilika kwa sheria hiyo kutasaidi kuwepo kwa udhibiti wa magonjwa ya mlipuko ambayo yamekuwa yakisumbua mifugo hasa homa ya mafua ya ndege ambayo imekuwa changamoto kubwa kwa upande wa Zanzibar

“Nashukuru hatua iliyochukuliwa kuendeleza sekta yetu ya kilimo ambayo imeleta faraja kwa kutuongezea ajira kwa vijana ambao wamepata fursa ya kuzalisha vifaranga kupitia vibali maalum kwa sababu ya changamoto ya mafua ya  ndege” alisema Bi. Maryam.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akiongea na wataalam wa Sekta ya Mifugo wa Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kupitia taarifa ya kikao cha wataalam wa Sekta ya Mifugo kilichofanyika kwenye ukumbi wa TVLA Jijini Dar es, (04/06/2021)


Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Umwagiliaji Maliasili na Mifugo Zanzibar Bi. Maryam Juma Saadalla akiongea wakati wa kufunga kikao cha  ushirikiano cha wataalam wa Sekta ya Mifugo wa Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kilichofanyika kwenye ukumbi wa TVLA Jijini Dar es Salaam. (04//06/2021)


Baadhi ya washiriki wa kikao cha ushirikiano kati ya Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ngazi ya wataalam wakimsikiliza kwa makini Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (hayupo pichani) wakati wa kupitia taarifa ya kikao  cha kiutendaji kati ya Serikali hizo mbili ili kuzipatia ufumbuzi kwa maendeleo ya sekta ya mifugo kilichofanyika kwenye ukumbi wa TVLA Jijini Dar es Salaam (04/06/2021)* 

 



Makatibu Wakuu wa Sekta ya Mifugo (wa pili kutoka kushoto mbele ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel, na wa tatu kutoka kushoto ni Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo Umwagiliaji Maliasili na Mifugo Zanzibar Bi. Maryam Juma Saadalla wakiwa kwenye picha ya pamoja na wataalam wa Sekta hiyo mara baada ya kikao  cha ushirikiano Kati ya Serikali hizo mbili kilichofanyika kwenye ukumbi wa TVLA Jijini Dar es Salaam (04/06/2021).