Nav bar

Jumanne, 15 Juni 2021

MAAFISA UVUVI 11 WAKABIDHIWA VITAMBULISHO VYA UKAGUZI WA MAZINGIRA

Maafisa Uvuvi kumi na moja (11) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wamekabidhiwa vitambulisho vitakavyowawezesha kufanya ukaguzi wa mazingira katika shughuli zote zinazofanyika katika maeneo ya uvuvi nchini.  

Maafisa hao walikabidhiwa vitambulisho hivyo baada ya kupatiwa mafunzo ya ukaguzi wa mazingira na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) yaliyofanyika  Julai 20 hadi 22, 2020 jijini Dar es Salaam.

Wakati akikabidhi vitambulisho hivyo, Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Bw. Magesa Bulayi katika tukio lililofanyika jijini Dodoma Julai 14, 2021, alisema kuwa anawakabidhi vitambulisho hivyo na ni imani yake kuwa  wataalamu hao  wa ukaguzi wataweza kusaidia kutatua vikwazo vinavyorudisha nyuma juhudi za Wizara katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira katika maeneo ya uvuvi.

Alisema sekta imekuwa ikikabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi na uharibifu wa mazingira unaotokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu zikiwemo shughuli zinazofanywa na wavuvi wenyewe.

“Niwapongeze watumishi walioshiriki mafunzo haya kwani utaalamu wao ndani ya sekta utapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto za kimazingira ambazo sekta imekuwa ikipambana nazo,” alisema Bulayi

Aliongeza kuwa, uhifadhi wa mazingira ni muhimu sana katika ustawi na uendelevu wa rasilimali za uvuvi hapa nchini kwani huchangia katika kutoa ajira kwa wananchi, lishe, kipato pamoja na kuliingizia taifa fedha za kigeni.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwapongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usalama wa Mazingira (NEMC) kwa kukubali kutoa mafunzo ambayo yamekuwa chachu na kuamsha ari ya kusimamia, kudhibiti na kuhifadhi mazingira ndani ya sekta huku akiongeza kuwa  mafunzo hayo yamekuwa kiungo kati ya sekta ya Uvuvi, NEMC na taasisi nyingine na kwa pamoja watashirikiana kikamilifu kupunguza changamoto za kimazingira katika utunzaji  rasilimali za uvuvi.

Bulayi alitoa wito  kwa Mkuu wa Kitengo cha Mazingira, Melton Kalinga kuendelea kuratibu mafunzo hayo kadiri fedha zitakapopatikana ili kuwa na wakaguzi katika kanda zote na mafunzo ya awamu ya pili yaguse pia idara ya ukuzaji viumbe maji.

“Natambua kitengo kina changamoto ya ufinyu wa bajeti, hata hivyo sekta itajitahidi kutafuta vyanzo vingine vya fedha ili kitengo kiweze kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa,” aliongeza Bulayi

Aliendelea kusisitiza kuwa sekta inawategemea katika masuala ya usimamizi wa mazingira hivyo wakafanye kazi kwa weledi, na watumie ujuzi waliopata ili kuongeza ufanisi katika utendaji wao.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Mazingira, Bw. Melton Kalinga aliomba mafunzo hayo yatengewe fedha za kutosha ili kuongeza idadi ya wataalamu wa ukaguzi wa mazingira kwa kuwa mahitaji bado ni makubwa.

Afisa Uvuvi Mkuu, Bw. Jerome Fundi aliwaasa washiriki wenzake kuwa vitambulisho walivyopata ni dhamana ambayo imetolewa na Serikali hivyo wavitumie kama ilivyokusudiwa na sio vinginevyo.


Kaimu Katibu Mkuu ((WMUV), Sekta ya Uvuvi, Bw. Magesa Bulayi akiongea na Maafisa Uvuvi (hawapo pichani) kabla ya kuwakabidhi vitambulisho vya ukaguzi wa mazingira kwenye ukumbi wa Wizara uliopo kwenye mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma. (14.06.2021)


Mkuu wa kitengo cha Mazingira kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Melton Kalinga akiongea na Maafisa Uvuvi wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vitambulisho vya wakaguzi wa mazingira Sekta ya Uvuvi iliyofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Wizara katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma. (14.06.2021)


Kaimu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Bw. Magesa Bulayi akimkabidhi Afisa Uvuvi Mwamdamizi, Bi. Emmanuela Xavier kitambulisho cha ukaguzi wa mazingira wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vitambulisho vya wakaguzi wa mazingira Sekta ya Uvuvi Jijini Dodoma. (14.06.2021)


Afisa Uvuvi Mwandamizi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Bw. Jerome Fundi akitoa neno la shukrani kwa Kaimu Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi, Bw. Magesa Bulayi (hayupo pichani) mara baada ya kukabidhiwa vitambulisho vya ukaguzi wa mazingira kwenye ukumbi wa Wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma. (14/06/2021.)


Kaimu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) (wa pili kutoka kulia mbele), Bw. Magesa Bulayi akiwa kwenye picha ya pamoja na maafisa uvuvi mara baada ya hafla fupi ya kukabidhi vitambulisho vya wakaguzi wa mazingira, kwenye ukumbi wa wizara hiyo jijini Dodoma. (14/06/2021)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni