Nav bar

Jumatano, 31 Mei 2023

ASILIMIA 90 YA MAZIWA YANAYOZALISHWA NCHINI YAPO NJE YA MFUMO-DKT. MUSHI

◼️ AWAMWAGIA SIFA ASAS KWA MCHANGO WAO KWENYE JAMII INAYOWAZUNGUKA 


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Daniel Mushi ameitaka Bodi ya Maziwa nchini kwa kushirikiana na wadau wote waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa bidhaa hiyo kufanya tathmini ya kina juu ya kiwango cha maziwa yanayozalishwa na kupotea kabla hayajaingia kwenye mfumo rasmi wa uchakataji.


Dkt. Mushi amesema hayo Mei 31,2023 wakati akifungua kongamano la wadau wa tasnia ya maziwa lililofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambapo amebainisha kuwa ni asilimia 10 pekee ya maziwa yanayozalishwa ndio yanayoingia kwenye mfumo rasmi huku asilimia 90 ikiwa haijulikani ilipo.


“Kwanza ni lazima tukubali kuwa kiwango cha maziwa cha lita Bil.3.6 kwa mwaka ni kidogo sana ukilinganisha na idadi ya mifugo tuliyonayo lakini pia tungetamani tufike mahali tujitosheleze kwenye matumizi ya maziwa yanayozalishwa hapa nchini kwa sababu kwa  sasa tunatumia maziwa mengi yanayoagizwa kutoka nje” Ameongeza Dkt. Mushi.


Dkt. Mushi amesema kuwa viwanda vilivyopo hapa nchini vina uwezo wa kuchakata lita 865,000 lakini mpaka sasa viwanda hivyo vinachakata asilimia 25 tu ya uwezo wake jambo ambalo amebainisha kuwa linarudisha nyuma jitihada za wasindikaji hao katika kukuza uchumi wa taifa kwa ujumla.


Katika hatua nyingine Dkt. Mushi ameipongeza kampuni ya ASAS kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kukuza tasnia ya maziwa na ustawi wa jamii inayoizunguka kupitia shughuli zake za usindikaji wa maziwa.


“Kwa kweli ASAS wamefanya kazi kubwa sana kiukweli ningetamani tuwe na kina ASAS wengi zaidi hapa nchini kwa sababu naamini hilo lingepeleka mbali sana maendeleo ya tasnia ya maziwa hivyo nitoe wito kwa wasindikaji na wadau wengine wa maziwa tuachane na mashindano na badala yake tushirikiane kutumia fursa nyingi sana zilizopo kwenye tasnia kwa sababu hata wakiwepo kina ASAS 20 bado hawatatosha” Amesisitiza Dkt. Mushi.


Kongamano la wadau wa Tasnia ya maziwa hufanyika kila mwaka kwa lengo la kujadili na kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili wadau wote waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa maziwa.

KIKAO KAZI CHA KITAIFA KINACHORATIBU MWONGOZO WA KUENDELEZA UVUVI MDOGO NCHINI CHAFANYIKA MKOANI MOROGORO

 

Mwenyekiti wa kikosi kazi cha kitaifa kinachoratibu Mwongozo wa kuendeleza Uvuvi mdogo Nchini (NTT) Bw. Yahya Mgawe akiongea jambo na  viongozi wanawake wanaojihusisha na shughuli za Uvuvi Tanzania (TAWFA) wa mikoa yote Nchini (hawapo pichani) kwenye Warsha ya mafunzo ya Uongozi na Usimamizi kwa wananwake hao  iliyofanyika katika Ukumbi wa Edema Hotel, Morogoro, iliyoanza leo 30 Mei  hadi 02 Juni 2023.

Mkurugenzi Msaidizi kitengo cha Uendelezaji wa Rasilimali za Uvuvi (FRD) Bi. Merisia Mparazo akiongea na wanawake viongozi waliohudhuria warsha ya mafunzo ya Uongozi na Usimamizi kwa Viongozi wanawake wanaojihusisha na shughuli za uvuvi Tanzania (TAWFA) (hawapo pichani) Katika ukumbi wa Edema Hotel, Morogoro, (30.05.2023.)

Afisa Uvuvi Mkuu, ambaye pia ni Mratibu wa mwongozo wa mradi wa kuendeleza uvuvi mdogo Bi. Lilian Ibengwe akiwasilisha mada kuhusu Mchakato na Mafanikio katika Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi,  kwenye Warsha ya mafunzo ya Uongozi na Usimamizi kwa Viongozi wanawake wanaojihusisha na shughuli za uvuvi Tanzania (TAWFA), iliyofanyika katika ukumbi wa Edema Hotel, Morogoro, 30 Mei 2023.

Afisa Uvuvi Mwandamizi ambaye pia ni mratibu wa dawati la jinsia kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Upendo Hamidu akiwasilisha katiba ya  "Tanzania Women Fish Workers Association" (TAWFA) ambayo Viongozi hao wataanza kuitumia katika shughuli zote za Uvuvi. Kwenye Warsha ya mafunzo ya Uongozi na Usimamizi kwa Viongozi, katika ukumbi wa Edema Hotel,  Morogoro,  30 Mei 2023.

Afisa Uvuvi Mwandamizi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Grace Kakama akiwasilisha malengo na Utaratibu wa Warsha ya mafunzo ya Uongozi na Usimamizi kwa viongozi wanawake wanaojihusisha na shughuli za uvuvi Tanzania (TAWFA) wa mikoa yote Nchini,(hawapo pichani) mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Edema Hotel, Morogoro, 30 Mei 2023.

Katibu wa TAWFA Maji bahari (COWOFO) kutoka Mkoa wa Lindi Wilaya ya Kilwa, Bi. Pili Mkemi ambaye ni mmoja wa wanawake viongozi wanaopata mfunzo ya uongozi na usimamizi kwa viongozi wa TAWFA, Akichangia mada  katika majadiliano katika warsha hiyo,  iliyofanyika katika ukumbi wa Edema Hotel,  Morogoro,  30 Mei 2023.

Sehemu ya washiriki wa warsha ya Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi kwa Viongozi wanawake wanaojihusisha na shughuli za uvuvi Tanzania (TAWFA) wa mikoa yote Nchini, ambayo mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Edema Hotel,  Morogoro, 30 Mei 2023.

MAZIWA YASIYO SALAMA NI HATARI KWA MLAJI-SILINDE

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde ameonya kuwa matumizi ya maziwa yasiyo salama huhatarisha maisha ya mlaji kutokana na kutumika kama njia ya kusafirisha  magonjwa ya mifugo kwenda binadamu.


Mhe. Silinde amesema hayo kwenye sherehe za ufunguzi wa Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya unywaji maziwa duniani iliyofanyika Mei 30, 2023 kwenye viwanja vya Chipukizi mkoani Tabora.


“Mwaka huu maadhimisho haya ya Wiki ya unywaji Maziwa kitaifa tumeyaelekeza kwenye kusisitiza matumizi ya maziwa salama kwa sababu kumekuwepo na magonjwa mengi sana yanayosababishwa na maziwa yasiyo salama, mfano ugonjwa wa kutupa mimba ambapo mtu akinywa maziwa yanayotokana na ng’ombe anayeumwa ugonjwa huo naye huanza kuathiriwa  na tatizo hilo hapo hapo” Ameongeza Mhe. Silinde.


Mhe. Slinde amewataka Wananchi wote waliopo karibu na mkoa wa Tabora kufika kwenye maonesho hayo ili wapate elimu ya kutosha kuhusu sheria namba 8 ya maziwa ambayo inaanisha kila kitu kuhusu maziwa salama.


“Lakini pia tunatambua moja ya changamoto nyingine kubwa inayowakabili watumiaji wengi wa maziwa ni uchakachuaji wa maziwa hayo, kwanza huo ni wizi kwa sababu mlaji anatoa pesa ilia pate maziwa bora sio yale yaliyoongezwa maji lakini pili tumewaelekeza Bodi ya Maziwa kuhakikisha wanafikisha elimu ya uuzaji wa maziwa bora kwa wasambazaji na wauzaji wote wa bidhaa hiyo na baada ya hapo wale ambao watashindwa kukubaliana na elimu hiyo  tutawachukulia hatua kupitia sheria yetu ya maziwa” Amesisitiza Mhe. Silinde.


Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Dkt. George Msalya ametoa rai kwa wadau wote waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa maziwa kuzingatia sheria ili kuhakikisha mlaji anapata maziwa yaliyo salama.


“Maziwa ni chakula bora sana na kiburudisho poa kwa watu wa rika zote wakati wote hivyo ni lazima sisi kama wenye dhamana ya kusimamia usalama wa bidhaa hii tunatekeleza wajibu wetu katika kuhakikisha mlaji haathiriki kutokana na matumizi ya zao hili la mifugo” Amesema Dkt. Msalya.


Akizungumzia hali ya uzalishaji na matumizi ya maziwa kwa mkoa wa Tabora, Kaimu Mkuu wa Mkoa huo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mhe. Naitapwaki Tukai amesema kuwa mkoa huo ndio unaoongoza kwa wingi wa ng’ombe hapa nchini hali inayowafanya gharama za maziwa kuwa chini ukilinganisha na maeneo mengine.


“Kwetu sisi wamasai maziwa ni chakula na ndio maana wengi tuna afya njema hivyo nitoe rai kwa wananchi wa mkoa wa Tabora tutumie fursa hii ya upatikanaji wa maziwa mengi mkoani kwetu kuboresha afya zetu na uchumi wetu kwa ujumla” Ameongeza Mhe. Tukai


Maadhimisho hayo ya kitaifa ya Wiki ya unywaji maziwa huambatana na shughuli mbalimbali zinazolenga kuhamasisha matumizi ya maziwa na huanza Mei 29 ya kila mwaka na kufikia tamati Juni 1  ambapo kwa mwaka huu yanatarajiwa kuhitimishwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (katikati) akishiriki kwenye tukio la unywaji maziwa kwa lengo la kuhamasisha wananchi kutumia bidhaa hiyo wakati wa  ufunguzi wa maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya unywaji maziwa  uliofanyika kwenye viwanja vya Chipukizi mkoani Tabora Mei 30, 2023.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (katikati) akiongoza wadau wanaoshiriki Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya Unywaji Maziwa kukata utepe kuashiria ufunguzi wa Maadhimisho hayo uliofanyika Mei 30, 2023 kwenye Viwanja vya Chipukizi Mkoani Tabora. Kushoto kwake ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Naitapwaki Tukai akifuatiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Bodi ya Maziwa nchini Prof. Zackaria Masanyiwa. Wa pili kutoka kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Mhe. Kemirembe Lwota.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (kushoto) akiangalia mashine ya kukamua maziwa muda mfupi baada ya kufika kwenye Viwanja vya Chipukizi Mkoani Tabora yanakofanyika Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya Unywaji Maziwa Duniani, Mei 30, 2023.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde akimuangalia "Panya Mweupe" ambaye hutumiwa na Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA)  kwenye utambuzi wa magonjwa ya mifugo muda mfupi baada ya kufika kwenye Viwanja vya Chipukizi ambako amefungua Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya Unywaji Maziwa duniani Mei 30, 2023.

​VIJANA WANUFAIKA MAFUNZO YA UVUVI KUPEWA KIPAUMBELE KATIKA MIKOPO

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewahakikishia vijana walionufaika na mafunzo atamizi ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji na ambao wameshaandaa maandiko ya miradi kuwa watapewa kipaumbele katika kupata mikopo ili waweze kuendeleza miradi yao.

Waziri Ulega alitoa kauli hiyo wakati akifunga mafunzo atamizi ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji katika hafla fupi iliyofanyika mkoani Mwanza Mei 29, 2023.

Alisema kuwa Wizara yake inatambua changamoto ya upatikanaji wa mitaji kwa wawekezaji katika sekta ya uvuvi hivyo kupitia programu hiyo wizara imejipanga kuwasaidia wanufaika wa mafunzo hayo kupata mitaji ya kuanzisha miradi iliyobuniwa kutokana na maandiko waliyowasilisha wizarani.

"Juhudi hizi za kutafuta mitaji ni pamoja na ruzuku na mikopo kutoka serikalini, taasisi za kifedha na washirika wa maendeleo. Nipende kusisitiza kuwa uanzishwaji wa vikundi, ushirika au kampuni ni fursa ya kuweza kufikiwa kirahisi na serikali sambamba na kupata fursa za mikopo yenye masharti nafuu kutoka serikalini na taasisi mbalimbali za kifedha,"alisema

Aliongeza kuwa programu hiyo ya atamizi inaendana na azma ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yenye nia ya kuwajengea uwezo vijana katika fani ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji ili waweze kujiajiri, kuongeza tija na kuongeza kipato kwa mtu na Taifa kwa ujumla.

Aidha, aliwaeleza vijana hao kuwa hatua walizoanza kuchukua za mchakato wa kuunda vikundi au kampuni kwa nia ya kuanzisha miradi ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji zitasaidia kwa kiasi kikubwa juhudi ya serikali ya kuongeza fursa za ajira kupitia sekta ya uvuvi; na kuchangia ukuaji wa sekta kutoka asilimia 2.5 ya sasa hadi kufikia asilimia 8.4 ifikapo mwaka 2025/2026.

Kwa upande wao vijana 197 walionufaika na mafunzo hayo walimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa fursa ya kujifunza kwa vitendo ufugaji wa samaki wakisema kuwa fursa hiyo itawawezesha kujiajiri, kukuza kipato chao na Taifa kwa ujumla.
#MifugoNaUvuviNiUtajiri

HEKARI 5,520 ZA NARCO ZAKABIDHIWA KWA WANANCHI

Na. Edward Kondela

 

Serikali imekabidhi hekari 5,520 za Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kwa wananchi wa wilaya za Bagamoyo, Chalinze na Kibaha Mkoani Pwani ili ziendelezwe kwa shughuli mbalimbali za kijamii zikiwemo za mifugo na kilimo.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (Mb), amebainisha hayo (26.05.2023) katika Ranchi ya Ruvu iliyopo Wilaya ya Kibaha, ambapo amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeridhia kukabidhi hekari 5,520 kwa vijiji 19 vilivyokuwa vimevamia sehemu ya eneo la ranchi na kuwataka wananchi ambao wapo ndani ya mipaka mipya ya Ranchi ya Ruvu kuondoka mara moja.


Mhe. Silinde amesema serikali imeridhia kukabidhi hekari hizo baada ya timu iliyoundwa mwaka wa fedha 2019/20 kutoa mapendekezo juu ya vijiji vilivyozunguka Ranchi ya Ruvu ambavyo vilivamia eneo la ranchi hiyo.


Ameongeza kuwa kufuatia uamuzi huo wa serikali, amewataka viongozi wa maeneo hayo kupanga mipango bora ya ardhi ili kuondokana na migogoro ya ardhi baina ya wafugaji na wakulima na kuwataka wananchi kutovamia tena mipaka mipya iliyopo kati ya Ranchi ya Ruvu na vijiji vinavyozunguka ranchi hiyo.


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Aboubakar Kunenge amesema kufuatia makabidhiano ya ardhi hiyo kwa wananchi kutoka NARCO, ni dhahiri serikali imeamua kutafuta suluhu kwa wananchi wake kwa kuwapatia eneo ambalo wataweza kufanya shughuli zao baada ya kukaa kwa muda mrefu katika eneo hilo ambalo walikuwa hawalimiliki.


Mhe. Kunenge amewataka wananchi kuendelea kuiamini serikali na kuwataka kutoa ushirikiano kwa viongozi wao badala ya kujichukulia maamuzi ambayo baadae yanasababisha kutoa hisia tofauti kuwa serikali haiwajali wananchi wake na kukemea vitendo vya uvamizi wa maeneo ya serikali.


Nao baadhi ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo fupi wamepongeza maamuzi ya serikali ya kuwakabidhi ardhi ambayo wamekuwa wakiitumia na kuahidi kuzidi kutoa ushirikiano kwa serikali na kuipongeza kwa kuwapatia ardhi hiyo ambayo wataiendeleza kwa shughuli zao na kuwa walinzi wa mipaka ya Ranchi ya Ruvu ambayo wanaiuzunguka.


Serikali imekabidhi hekari 3,720 kwa Wilaya ya Chalinze, hekari 300 Wilaya ya Bagamoyo na hekari 1,500 Wilaya ya Kibaha ambazo zilikuwa zikimilikiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) katika Ranchi ya Ruvu ambayo wananchi walikuwa wamevamia sehemu ya ranchi hiyo.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (Mb) akizungumza juu ya maamuzi ya serikali kutoa hekari 5,520 za Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kutoka katika Ranchi ya Ruvu kwa ajili ya wilaya za Bagamoyo, Chalinze na Kibaha Mkoani Pwani kwa vijiji 19 vinavyozunguka ranchi hiyo ambavyo vilikuwa vimevamia eneo la ranchi na kuwataka wananchi waliovamia mipaka mipya ya ranchi kuondoka mara moja. Naibu Waziri Silinde amezungumza hayo katika hafla fupi iliyofanyika katika Ranchi ya Ruvu iliyopo Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani. (26.05.2023)


Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Aboubakar Kunenge akibainisha namna serikali ilivyoamua kutafuta suluhu kwa wananchi wake kwa kuwapatia maeneo ambayo wataweza kufanya shughuli zao baada ya kukaa kwa muda mrefu kwenye maeneo hayo ambayo walikuwa hawamiliki. Mhe. Kunenge amebainisha hayo katika hafla fupi iliyofanyika katika Ranchi ya Ruvu iliyopo Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani, ambapo serikali imekabidhi hekari 5,520 za Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kutoka katika Ranchi ya Ruvu kwa ajili ya wilaya za Bagamoyo, Chalinze na Kibaha Mkoani Pwani kwa vijiji 19 vinavyozunguka ranchi hiyo. (26.05.2023)

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) Prof. Peter Msoffe (aliyekaa kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Chalinze Bw. Ramadhan Possi wakitia saini makabidhiano ya eneo la hekari 3,720 lililokuwa linalomilikiwa na NARCO kutoka katika Ranchi ya Ruvu baada ya serikali kuamua kukabidhi eneo hilo kwa wananchi waliokuwa wamevamia eneo hilo. Wanaoshuhudia utiaji saini huo ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Aboubakar Kunenge, katika hafla fupi iliyofika kwenye Ranchi ya Ruvu. (26.05.2023)

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) Prof. Peter Msoffe akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Kibaha Bi. Butamo Ndalahwa hati ya makabidhiano ya eneo la hekari 1,500 lililokuwa linamilikiwa na NARCO kutoka katika Ranchi ya Ruvu baada ya serikali kuamua kukabidhi eneo hilo lililokuwa limevamiwa na wananchi. Hafla hiyo fupi imefanyika kwenye Ranchi ya Ruvu iliyopo Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani. (26.05.2023)

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) Prof. Peter Msoffe akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Bagamoyo Bw. Shauri Selenda hati ya makabidhiano ya eneo la hekari 300 lililokuwa linamilikiwa na NARCO kutoka katika Ranchi ya Ruvu baada ya serikali kuamua kukabidhi eneo hilo kwa wananchi waliokuwa wamelivamia. Hafla hiyo fupi imefanyika kwenye Ranchi ya Ruvu iliyopo Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani na kushuhudiwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Aboubakar Kunenge. (26.05.2023)

VITUO ATAMIZI VYA MIFUGO VITATUE CHANGAMOTO YA AJIRA KWA VIJANA

Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) imetakiwa  kuwasimamia vizuri vijana 240 wanaoendelea kupatiwa mafunzo ya unenepeshaji mifugo  katika vituo atamizi 8 chini ya LITA ikiwa ni mpango wa Serikali kusaidia vijana hao kujiajiri na  kujikwamua kiuchumi.


Wito huo umetolewa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu ambaye ni  Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina wakati wa kikao cha baraza la wafanyakazi wa LITA kilichofanyika mkoani Arusha Mei 26, 2023.


Dkt. Mhina alisema Serikali imeanza kutekeleza mradi huo katika mwaka huu wa fedha baada ya kubaini wataalamu wanaotoka katika vyuo hivyo wanayo nafasi ya kupatiwa ujuzi zaidi ya kuzalisha kupitia vituo atamizi ili watakaporejea mitaani waweze kuwa na uwezo wa kuwekeza zaidi.


“Tunatengeneza wataalam ambao ni wawekezaji wao wenyewe watakapoweza kuzalisha ndivyo ambavyo tutaweza kuzalisha malighafi zaidi kwenye viwanda vyetu, kwahiyo hatutarajii wakitoka hapa wakategemee kuajiriwa ndio maana tunawaweka kwenye vituo atamizi ili wafanye kwa vitendo na kufanya kibiashara zaidi” amesema


Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene alifafanua kuwa mradi huo kwa kuanzia utatekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja ambapo utagawanywa kwa awamu 4 ambapo vijana hao watahudumia mifugo kwa kunenepesha ndani ya miezi 3.


Alisema katika kila kituo kuna  vijana wasiopungua 30 ambapo kila mmoja anahudumia ng’ombe 10 kwa kuwanenepesha kwa kipindi cha miezi mitatu na kufanya wahudumia ngombe 40 kwa mwaka mzima


“ kila kijana kwa mzunguko moja amepewa ng’ombe 10 wa kunenepesha kwa hiyo kwa mwaka mzima atanenepesha ngombe 40  na tunategemea faida itakayotokana na hao Ng’ombe watakao uzwa mnadani ni mtaji kwa kijana kwa ajili ya kwenda kuanzisha mradi wake baada ya kumaliza mwaka mmoja” amesema


Aliongeza kuwa mradi huo utakuwa fursa nzuri kwa vijana kufuga kibiashara kwa sababu licha ya kuanza kutekeleza mradi huo mwezi Aprili mwaka huu tayari wameanza kupokea oda ya kuhitaji ng’ombe hao.


Mwakilishi wa katibu Mkuu, ambae ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi,  Dkt. Charles Mhina akiongea wakati wa kufungua kikao cha baraza la wafanyakazi wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) kilichofanyika Tengeru LITA mkoani Arusha, Mei 26,2023


Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Plus Mwambene (kulia) akieleza namna wakala hiyo inavyotekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa vitendo ili kuwaandaa vijana kujiajiri, kwa Mwakilishi wa Katibu Mkuu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina  wakati alipoenda kufungua kikao cha baraza la wafanyakazi LITA kilichofanyika Tengeru mkoani Arusha Mei 26,2023.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Mhina (kulia) akimsikiliza kwa makini mkuu wa chuo cha Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) Tengeru, Dkt.  Flora Kajuna (kushoto) wakati alipotembelea maabara chuoni hapo alipoenda kufungua kikao cha baraza la wafanyakazi LITA Mei 26, 2023 Mkoani Arusha.

Mwanafunzi anayejikita kwenye eneo la Afya ya Mnyama na Uzalishaji Bw. Julius Mmbando akionyesha namna taarifa /majibu ya vipimo vya magonjwa mbalimbali ya mnyama yanavyotoka kwenye mashine ya kupimia magonjwa hayo ya mifugo kwa Mwakilishi wa Katibu Mkuu Dkt. Charles Mhina alifika chuoni hapo Tengeru Mkoani Arusha Mei 26,2023.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu ambae pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa baraza hilo mara baada ya kikao kifupi kilichofanyika kwenye ukumbi wa chuo cha Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) Tengeru mkoani Arusha,  Mei 26, 2023 wa pili kutoka kulia ni Mtendaji mkuu wa Wakala hiyo Dkt. Pius Mwambene.

KIKAO CHA MAPITIO YA RASIMU YA MTAALA WA AFYA YA WANYAMA NA UZALISHAJI CHAFANYIKA MKOANI DODOMA

 

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (Ugani) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Samwel Mdachi, akifungua kikao cha mapitio ya rasimu ya mtaala wa afya ya wanyama na uzalishaji ili kuingiza masuala ya sumu kuvu kilichofanyika jijini Dodoma kikiwashirikisha washiriki kutoka idara za wizara hiyo sekta ya mifugo pamoja na taasisi zilizo chini ya wizara. (25.05.2023)

Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Nyanda za Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Asimwe Rweguza akifafanua jambo juu ya rasimu ya mtaala wa afya ya wanyama na uzalishaji pamoja na umuhimu wa malisho ya mifugo wakati wa kikao cha mapitio ya rasimu ya mtaala wa afya ya wanyama na uzalishaji ili kuingiza masuala ya sumu kuvu kilichofanyika jijini Dodoma kikiwashirikisha washiriki kutoka idara za wizara hiyo sekta ya mifugo pamoja na taasisi zilizo chini ya wizara. (25.05.2023)

Afisa Mifugo Msaidizi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Sebastian Shilangalila akizungumza wakati wa maandalizi na kupitia mada mbalimbali wakati wa kuanza kwa kikao cha mapitio ya rasimu ya mtaala wa afya ya wanyama na uzalishaji ili kuingiza masuala ya sumu kuvu kilichofanyika jijini Dodoma kikiwashirikisha washiriki kutoka idara za wizara hiyo sekta ya mifugo pamoja na taasisi zilizo chini ya wizara. (25.05.2023)

Picha ya pamoja ya washiriki wa kikao cha mapitio ya rasimu ya mtaala wa afya ya wanyama na uzalishaji ili kuingiza masuala ya sumu kuvu kilichofanyika jijini Dodoma kikiwashirikisha washiriki kutoka idara za wizara hiyo sekta ya mifugo pamoja na taasisi zilizo chini ya wizara. (25.05.2023)

TUKUTANE TABORA

 


WIZARA, SUA ZATEKELEZA MAAGIZO YA MHE. RAIS, DKT. SAMIA

Kufuatia maelekezo aliyoyatoa Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi ishirikiane na Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo (SUA) kuwawezesha vijana kujiajiri yaanza kutekelezwa baada ya pande hizo mbili kusaini makubaliano ya ushirikiano kuinua sekta za mifugo na Uvuvi.


Akiongea muda mfupi baada ya kushuhudia tukio la kusaini makubaliano lililofanyika mkoani Morogoro katika Siku ya Kumbukizi ya 18 ya Hayati Edward Moringe Sokoine Mei 23, 2023 , Waziri wa Mifugo na Uvuvi alisema tukio hilo ni utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais, Dkt Samia aliyotoa katika kilele cha Maadhimisho ya NaneNane yaliyofanyika Mkoani Mbeya Agosti 8, 2022.

Alisema kuwa Dkt Samia anataka kuona mabadiliko katika sekta za uzalishaji, hivyo fursa zilizopo katika sekta za uzalishaji zikitumika vizuri manufaa makubwa yatapatikana ikiwemo kulia kwa uchumi wa Taifa na mtu mmoja mmoja.

Aidha, Waziri Ulega alimshukuru, Mhe. Rais, Dkt. Samia kwa jitihada zake za kuhamasisha vijana na wanawake kushiriki kwenye kilimo kupitia progamu mbalimbali.

Alisema kuwa Mifugo na Uvuvi ni utajiri kwa sababu matokeo yake ni ya haraka na biashara yake ni ya haraka pia.

Pia, alitoe wito kwa sekta binafsi na washirika wa maendeleo kuendelea kujitokeza na kuunga mkono jitihada hizo ili vijana waweze kushiriki katika shughuli za uzalishaji kupitia nyanja za kilimo, mifugo na uvuvi.

"Nitoe rai kwa Wadau wa sekta Binafsi na Wadau wa maendeleo kuunga mkono jitihada za Mhe, Rais kwa kutoa mitaji ya fedha, vitendea kazi, mafunzo, na teknolojia
zitakazowezesha vijana kushiriki katika kilimo, mifugo na uvuvi kwa tija na ufanisi zaidi", alisema.

SAUTI YETU WIKI HII 

TUKUTANE TABORA

 
SEKTA YA UVUVI KUENDELEZA USHIRIKIANO NA SHIRIKA LA MAENDELEO LA KIMATAIFA LA JAPAN (JICA)

 

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ismael Kimirei akiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (Sekta ya Uvuvi) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh pamoja na viongozi wengine wa TAFIRI na wizara hiyo, kwenye mazungumzo ya kuendeleza ushirikiano katika Sekta ya Uvuvi kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA), ambapo baadhi ya maafisa waandamizi wa shirika hilo hapa nchini walifika katika ofisi za makao makuu ya TAFIRI jijini Dar es Salaam ili kupata taarifa mbalimbali za TAFIRI na maeneo ya kushirikiana. (19.05.2023).


Maafisa waandamizi kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) hapa nchini, wakiwa kwenye mazungumzo na uongozi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) na baadhi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, mara baada ya maafisa hao kutoka JICA kufika makao makuu ya TAFIRI jijini Dar es Salaam ili kujadili maeneo ya kushirikiana katika Sekta ya Uvuvi na kupata taarifa mbalimbali juu ya taasisi hiyo. (19.05.2023).


Maafisa waandamizi kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) hapa nchini, mara baada ya mazungumzo na uongozi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) na baadhi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye makao makuu ya TAFIRI jijini Dar es Salaam, juu ya kuendeleza ushirikiano katika Sekta ya Uvuvi walipata fursa ya kujionea baadhi ya vifaa vya utafiti wa uvuvi (19.05.2023).


Picha ya pamoja ya Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ismael Kimirei (wa tatu kutoka kulia) akiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (Sekta ya Uvuvi) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh (wa pili kutoka kulia) na baadhi ya maafisa kutoka TAFIRI na wizara hiyo pamoja na maafisa waandamizi kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) hapa nchini, mara baada ya mazungumzo na uongozi wa TAFIRI na baadhi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi juu ya maeneo ya ushirikiano katika Sekta ya Uvuvi yaliyofanyika katika makao makuu ya TAFIRI jijini Dar es Salaam. (19.05.2023)


TUKUTANE TABORA

 
SERIKALI YAJA NA MPANGO MAALUM WA MAFUNZO YA UFUGAJI SAMAKI

Na. Edward Kondela


Serikali kuanza kutoa mafunzo maalum ya muda mfupi kwa wafugaji wa samaki kote nchini ili kukuza tasnia hiyo na kuleta tija kwa nchi na wananchi kwa ujumla.


Hayo yamebainishwa (19.05.2023) jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (Sekta ya Uvuvi) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh, mara baada ya wizara hiyo kuingia hati ya makubaliano kupitia Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA) na Chama Kikuu cha Wakuza Viumbe Maji Tanzania (AAT) ili wakala hiyo kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wafuga samaki na watu wanaotaka kuingia katika tasnia hiyo kupitia Mradi wa Kikanda wa Ukuzaji Viumbe Maji (EAC TRUEFISH PROJECT).


Prof. Sheikh amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo kwenye sekta za uzalishaji ikiwemo uvuvi kwa kuweka fedha nyingi kwenye ukuzaji viumbe maji hususan ufugaji wa samaki, hivyo kuna haja ya kuweka mafunzo maalum katika ufugaji wa viumbe maji.


“Huu ni ushirikiano kati ya wizara kupitia chuo cha FETA, kwa kuwa serikali imeweka fedha nyingi katika ufugaji viumbe maji, kuwa na mafunzo ya namna hii ya ufugaji wa samaki na kutengenza mitaala inayokubalika kwa Afrika Mashariki ni suala la msingi ili kufuga kwa tija.” Amesema Prof. Sheikh


Ameongeza kuwa lengo la makubaliano hayo ni kuwa na wanufaika wengi ambapo kwa sasa wataanza na wachache ambao wanategemewa kwenda kufundisha wengine baada ya kuhitimu mafunzo hayo ili kuwa na ufugaji wa tija.


Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA) Dkt. Semvua Mzighani amesema mafunzo ya ufugaji samaki yatatolewa kwa muda wa wiki moja hadi mbili kwa kuanzia katika Kampasi ya FETA iliyopo Nyegezi jijini Mwanza, ambapo kwa sasa walengwa wakubwa ni katika Bonde la Ziwa Victoria ambao tayari wameanza kufuga samaki ili kuwapatia maarifa ya ufugaji bora.


Dkt. Mzighani amefafanua kuwa masomo yatakayofundishwa katika kozi hizo ni namna ya kupata vifaranga bora vya samaki, vyakula bora vya samaki na namna ya kuwafuga samaki ili wakue wakiwa salama na wenye afya njema kabla ya kuwafikisha sokoni.


Aidha, amesema mafunzo hayo yatakuwa na mbinu mpya na aina nzuri ya ufugaji ambayo itampa faida mfugaji kwa sababu ufugaji ni biashara na kwamba wananchi ambao pia bado hawajaanza ufugaji samaki wanaruhusiwa pia kufika katika Kampasi ya FETA Nyegezi jijini Mwanza ili kupatiwa utaratibu wa kupata mafunzo hayo.  


Naye Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Wakuzaji Viumbe Maji Tanzania (AAT) Dkt. Charles Mahika amesema mafunzo hayo ni muhimu kwao hususan katika kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa chakula bora cha samaki, mafunzo ya kuzalisha vifaranga bora vya samaki pamoja na upatikanaji wa masoko ya samaki.


Dkt. Mahika ameongeza kuwa wao kama chama kazi yao kubwa ni kuwaunganisha wafugaji wa samaki kote nchini kupata mafunzo hayo kutoka FETA ambapo wanaamini ufugaji wa samaki utakuwa na tija zaidi kwa kuzingatia kumekuwa na ongezeko la ufugaji kwa kutumia vizimba.


Hati ya makubaliano hayo iliyotiwa saini kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA) na Chama Kikuu cha Wakuzaji Viumbe Maji Tanzania (AAT) kwa ajili ya kutoa mafunzo ya muda mfupi ya ufugaji samaki yanafadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kupitia Mradi wa Kikanda wa Ukuzaji Viumbe Maji (EAC TRUEFISH PROJECT).

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA) Dkt. Semvua Mzighani (kushoto) na Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Wakuza Viumbe Maji Tanzania (AAT) Dkt. Charles Mahika (kulia), wakitia saini hati ya makubaliano kati ya FETA na AAT ili wafuga samaki kupatiwa mafunzo ya muda mfupi na FETA kupitia Mradi wa Kikanda wa Ukuzaji Viumbe Maji (EAC TRUEFISH PROJECT) unaofadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO). Wanaoshuhudia utiaji saini huo ni baadhi ya maafisa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na FAO. (19.05.2023)

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA) Dkt. Semvua Mzighani (kushoto) na Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Wakuza Viumbe Maji Tanzania (AAT) Dkt. Charles Mahika (kulia), wakibadilishana hati ya makubaliano kati ya FETA na AAT ili wafuga samaki kupatiwa mafunzo ya muda mfupi na FETA kupitia Mradi wa Kikanda wa Ukuzaji Viumbe Maji (EAC TRUEFISH PROJECT) unaofadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO). Wanaoshuhudia utiaji saini huo ni baadhi ya maafisa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na FAO. (19.05.2023)

Kabla ya utiaji saini wa hati ya makubaliano ya mafunzo ya muda mfupi ya ufugaji samaki kati ya Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA) na Chama Kikuu cha Wakuza Viumbe Maji Tanzania (AAT) ili wafuga samaki kupatiwa mafunzo ya muda mfupi na FETA kupitia Mradi wa Kikanda wa Ukuzaji Viumbe Maji (EAC TRUEFISH PROJECT) unaofadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO). Washirki walipata fursa ya kupitia makubaliano hayo kabla ya kusainiwa rasmi kwa ajili ya kuanza utekelezaji. (19.05.2023)