Nav bar

Jumatano, 31 Mei 2023

MAZIWA YASIYO SALAMA NI HATARI KWA MLAJI-SILINDE

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde ameonya kuwa matumizi ya maziwa yasiyo salama huhatarisha maisha ya mlaji kutokana na kutumika kama njia ya kusafirisha  magonjwa ya mifugo kwenda binadamu.


Mhe. Silinde amesema hayo kwenye sherehe za ufunguzi wa Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya unywaji maziwa duniani iliyofanyika Mei 30, 2023 kwenye viwanja vya Chipukizi mkoani Tabora.


“Mwaka huu maadhimisho haya ya Wiki ya unywaji Maziwa kitaifa tumeyaelekeza kwenye kusisitiza matumizi ya maziwa salama kwa sababu kumekuwepo na magonjwa mengi sana yanayosababishwa na maziwa yasiyo salama, mfano ugonjwa wa kutupa mimba ambapo mtu akinywa maziwa yanayotokana na ng’ombe anayeumwa ugonjwa huo naye huanza kuathiriwa  na tatizo hilo hapo hapo” Ameongeza Mhe. Silinde.


Mhe. Slinde amewataka Wananchi wote waliopo karibu na mkoa wa Tabora kufika kwenye maonesho hayo ili wapate elimu ya kutosha kuhusu sheria namba 8 ya maziwa ambayo inaanisha kila kitu kuhusu maziwa salama.


“Lakini pia tunatambua moja ya changamoto nyingine kubwa inayowakabili watumiaji wengi wa maziwa ni uchakachuaji wa maziwa hayo, kwanza huo ni wizi kwa sababu mlaji anatoa pesa ilia pate maziwa bora sio yale yaliyoongezwa maji lakini pili tumewaelekeza Bodi ya Maziwa kuhakikisha wanafikisha elimu ya uuzaji wa maziwa bora kwa wasambazaji na wauzaji wote wa bidhaa hiyo na baada ya hapo wale ambao watashindwa kukubaliana na elimu hiyo  tutawachukulia hatua kupitia sheria yetu ya maziwa” Amesisitiza Mhe. Silinde.


Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Dkt. George Msalya ametoa rai kwa wadau wote waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa maziwa kuzingatia sheria ili kuhakikisha mlaji anapata maziwa yaliyo salama.


“Maziwa ni chakula bora sana na kiburudisho poa kwa watu wa rika zote wakati wote hivyo ni lazima sisi kama wenye dhamana ya kusimamia usalama wa bidhaa hii tunatekeleza wajibu wetu katika kuhakikisha mlaji haathiriki kutokana na matumizi ya zao hili la mifugo” Amesema Dkt. Msalya.


Akizungumzia hali ya uzalishaji na matumizi ya maziwa kwa mkoa wa Tabora, Kaimu Mkuu wa Mkoa huo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mhe. Naitapwaki Tukai amesema kuwa mkoa huo ndio unaoongoza kwa wingi wa ng’ombe hapa nchini hali inayowafanya gharama za maziwa kuwa chini ukilinganisha na maeneo mengine.


“Kwetu sisi wamasai maziwa ni chakula na ndio maana wengi tuna afya njema hivyo nitoe rai kwa wananchi wa mkoa wa Tabora tutumie fursa hii ya upatikanaji wa maziwa mengi mkoani kwetu kuboresha afya zetu na uchumi wetu kwa ujumla” Ameongeza Mhe. Tukai


Maadhimisho hayo ya kitaifa ya Wiki ya unywaji maziwa huambatana na shughuli mbalimbali zinazolenga kuhamasisha matumizi ya maziwa na huanza Mei 29 ya kila mwaka na kufikia tamati Juni 1  ambapo kwa mwaka huu yanatarajiwa kuhitimishwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (katikati) akishiriki kwenye tukio la unywaji maziwa kwa lengo la kuhamasisha wananchi kutumia bidhaa hiyo wakati wa  ufunguzi wa maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya unywaji maziwa  uliofanyika kwenye viwanja vya Chipukizi mkoani Tabora Mei 30, 2023.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (katikati) akiongoza wadau wanaoshiriki Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya Unywaji Maziwa kukata utepe kuashiria ufunguzi wa Maadhimisho hayo uliofanyika Mei 30, 2023 kwenye Viwanja vya Chipukizi Mkoani Tabora. Kushoto kwake ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Naitapwaki Tukai akifuatiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Bodi ya Maziwa nchini Prof. Zackaria Masanyiwa. Wa pili kutoka kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Mhe. Kemirembe Lwota.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (kushoto) akiangalia mashine ya kukamua maziwa muda mfupi baada ya kufika kwenye Viwanja vya Chipukizi Mkoani Tabora yanakofanyika Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya Unywaji Maziwa Duniani, Mei 30, 2023.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde akimuangalia "Panya Mweupe" ambaye hutumiwa na Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA)  kwenye utambuzi wa magonjwa ya mifugo muda mfupi baada ya kufika kwenye Viwanja vya Chipukizi ambako amefungua Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya Unywaji Maziwa duniani Mei 30, 2023.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni