Nav bar

Jumatatu, 26 Mei 2025

PROF. SHEMDOE AITAKA FETA KUZALISHA WANAOJIAJIRI NA KUAJIRI WENGINE

Na. Maria Mtambalike - FETA 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe ameitaka Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi nchini (FETA) kuandaa wahitimu watakaoweza kujiajiri na kuajiri wengine badala ya kusubiri kuajiriwa kama ilivyo hivi sasa.

Prof. Shemdoe ametoa kauli hiyo wakati akifungua kikao kilichokutanisha wadau kujadili rasimu ya mitaala 5 inayohuishwa na mitaala 12 mipya iliyoandaliwa na Wakala hiyo 26 Mei, 2025 Mkoani Morogoro.

“Ni lazima tubadilike katika utoaji wetu wa elimu ili kuzingatia mafunzo yanayojikita kwenye ujuzi wa vitendo zaidi ili wahitimu wetu waweze kujiajiri na baadae waajiri wengine” Amesema Prof. Shemdoe.

Aidha Prof. Shemdoe ameielekeza Wakala hiyo kutengeneza mitaala itakayozalisha wataalam wanaozingatia mabadiliko ya tabia nchi kwenye utekelezaji wa shughuli za Uvuvi na ukuzaji Viumbe Maji.

“Mitaala hii pia izingatie teknolojia za kisasa ikiwa ni pamoja na matumizi ya zana mpya za Uvuvi, Ukuzaji viumbe Maji lakini mwisho mitaala hii lazima izingatie matumizi ya Akili Mnemba kwa sababu tusipoliangali hili tunaweza kujikuta siku za usoni tunasahihisha kazi iliyofanywa kutokana na matumizi ya teknolojia hiyo” Ameongeza Prof. Shemdoe.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mtendaji Mkuu wa FETA Dkt, Semvua Mzighani amesema kuwa Mitaala inayotarajiwa kuanzishwa itasaidia kutengeneza wataalamu waliobobea katika sekta ya uvuvi ambao watasaidia katika kukuza uchumi wa buluu.

"Serikali inakamilisha  ujenzi wa Bandari za Uvuvi za Kilwa na Bagamoyo hivyo tunataka wataalamu watakaozalishwa kutokana na mitaaala hii mipya waende kusaidia katika usimamizi wa  Bandari hizi" Ameongeza Dkt Mzighani.

Kikao hicho cha kuhuisha mitaala ya zamani na kuanzisha mitaala mipya kitafanyika kwa muda wa siku 10 ambapo kimeshirikisha wadau kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Wizara ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Sekretarieti ya Ajira na Shirika lisilo la Serikali la Sustainable Agriculture Tanzania (SAT).








BUNGE LAIDHINISHA BAJETI YA TSH. BIL.476.6 WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI

 BAJETI ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewasilishwa bungeni huku mafanikio lukuki yaliyopatikana kwenye  sekta za mifugo na uvuvi ndani ya kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita  yakibainishwa na hatua kadhaa zikitajwa kuchukuliwa na wizara kwa lengo la kuziwezesha sekta hizo muhimu kuendelea kuwa na mchango zaidi kwenye Pato la Taifa (GDP).

Akiwasilisha bajeti hiyo yenye muelekeo wa kuongeza uzalishaji na kukuza masoko ya mazao ya mifugo na uvuvi, bungeni jijini Dodoma Mei 23, 2025, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amebainisha mafanikio kadhaa ambayo sekta za mifugo na uvuvi zimeyapata.

Dkt. Kijaji akihutubia bunge hilo alisema kuwa moja ya mafanikio makubwa ambayo wizara yake  imeyapata ndani ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuongezeka kwa bajeti ya wizara kutoka Shilingi Bilioni 295.5 Mwaka 2023/2024 hadi Shilingi Bilioni 476.6 Mwaka 2025/2026 hatua ambayo inatafsiri kinagaubaga dhamira ya dhati ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha sekta za mifugo na uvuvi  zinaendelea kuwa chachu ya uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja.

Ameongeza kwa kusema kuwa utekelezaji wa Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) imewezesha jumla ya vikundi 20 vyenye vijana 106 kupatiwa ekari 1,761 katika Ranchi ya Kagoma na kupewa mkopo usio na riba wa jumla ya shilingi 934,231,000 kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa ajili ya kuendesha shughuli za unenepeshaji ng’ombe. Vijana hao walianza kazi ya unenepeshaji wa ng’ombe Januari, 2025 ambapo hadi kufikia Aprili, 2025 jumla ya ng’ombe 627 wenye thamani ya shilingi 451,440,000 walinunuliwa na kunenepeshwa kwa wastani wa shilingi 720,000 kwa kila ng’ombe, na kati ya ng’ombe hao,  452 waliuzwa kwa wastani wa shilingi 890,000 kwa kila ng’ombe na kupatikana kwa faida ya shilingi 76,840,000  ikiwa ni wastani wa shilingi 170,000 kwa kila ng’ombe.

Ameendelea kufafanua kuwa, hatua ya kupumzisha shughuli za uvuvi Ziwa Tanganyika umepelekea mavuno ya samaki kuongezeka katika ziwa hilo kufikia tani 38,999.82, zenye thamani ya shilingi 324,845,566,002.38 katika kipindi cha miezi minne (4) baada ya kufungua Ziwa kati ya Mwezi Septemba hadi Desemba, 2024 ikilinganishwa na tani 25,113.43, zenye thamani ya shilingi 166,476,911,002.19 kwa kipindi kama hicho Mwaka 2023 kabla ya kupumzisha Ziwa. Kutokana na ongezeko hilo imepelekea kiasi cha mazao ya uvuvi yaliyouzwa nje ya nchi kutoka Ziwa Tanganyika kwa Mwaka 2024 kuongezeka kufikia tani 1,227.21 zenye thamani ya shilingi 180,684,608,011.64 ikilinganishwa na tani 664.11 zenye thamani ya shilingi 97,036,183,747.23 Mwaka 2023, ikiwa ni ongezeko la asilimia 84.79.

Mafanikio mengine ambayo Dkt. Kijaji ameyataja ni kuondoa uvuvi haramu wa kutumia vilipuzi (blast fishing) katika Ukanda wa Bahari ya Hindi ambapo kwa sasa hali hiyo imedhibitiwa kuanzia vyanzo, wasambazaji na watumiaji wa vilipuzi na kwa zaidi ya mwaka hakuna matukio ya uvuvi huo kwa ukanda wote wa Bahari ya Hindi.

Ameongeza kwa kusema kuwa wizara yake imeweka mifumo madhubuti ya ufuatiliaji ili uhalifu huo usiendelee siku zijazo huku akibainisha kuwa kwa upande wa Maziwa Makuu wizara yake inaendelea na kazi ya kusafisha na kuondoa zana  haramu za uvuvi jambo ambalo limesaidia kugundua na kunasa mtandao mpana wa uingizaji wa nyavu haramu. Mafanikio yote yanayopatikana yanatokana na ushirikishwaji thabiti wa wadau mbalimbali wa Sekta ya Uvuvi wakiwemo Viongozi wa Ofisi za Wakuu wa Mikoa,  Mamlaka za Serikali za Mitaa, Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi  na Asasi Zisizo za Kiserikali (NGO).

Katika hatua ya kuhakikisha kunakuwa na usalama wa chakula na lishe, Dkt. Kijaji amesema katika kipindi cha miaka minne wizara yake imeendelea kupandikiza vifaranga vya samaki katika maeneo mbalimbali nchini ambapo hadi sasa jumla ya vifaranga 2,699,630 vya samaki, vyenye thamani ya Shilingi 269,963,000 vimepandikizwa katika Ziwa Ikimba (2,000,000) - Bukoba na mabwawa mawili (2) yaliyopo - Mufindi – Bwawa la asili la Nzivi (300,000) na Bwawa la Kihanga (300,000); Igunga - Bwawa la Mwamapuli (13,830); Ngara (1,000), na Lushoto - Bwawa la Gereza la Lushoto (60,000); Shule ya Irente (3,000); Sekondari ya Magamba (1,800) na Bwawa la kikundi cha Ngulwi (20,000).

Aidha, Dkt. Kijaji amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne, wizara yake imeendelea na utekelezaji wa mradi wa kutoa mikopo isiyo na riba na yenye masharti nafuu wa kuwezesha wananchi vizimba vya kufugia samaki na pembejeo zake katika mikoa ya Mara, Simiyu, Mwanza, Kagera, Geita, Katavi, Rukwa na Kigoma huku akibainisha kuwa hadi kufikia Aprili 2025 vizimba 480 vimekopeshwa kwa wanufaika 1,338 na jumla ya tani 216.68 za samaki zenye thamani ya Shilingi 1,576,132,969.36 zimevunwa kwenye vizimba 157 vya vikundi 32 na kufanya marejesho ya Shilingi 1,528,734,615.66.

Pia, Dkt. Kijaji ameongeza kuwa kwa mara ya kwanzaSerikali inakwenda kuzindua na kutekeleza Kampeni ya kitaifa ya chanjo na utambuzi wa mifugo nchi nzima lengo likiwa ni kuboresha afya ya mifugo na kuiongezea thamani ili iweze kuuzika kwenye masoko ya kimataifa.

Dkt. Kijaji ameendelea kuweka wazi kuwa Wizara yake kupitia Bodi ya Nyama imeendelea kutekeleza mkakati wa kukuza mauzo ya nyama nje ya nchi kwa ajili ya kuongeza fedha za kigeni huku akibainisha kuwa hadi kufikia Aprili 2025, jumla ya tani 9,863.41 za nyama zenye thamani ya Shilingi Trilioni 3.7 zimeuzwa sawa na asilimia 89.9 ya lengo la kuuza tani 10,971    ikilinganishwa na tani 9,326.3 zenye thamani ya Shilingi Trilioni 3.4 zilizouzwa kipindi kama hicho katika Mwaka 2023/2024.  Ongezeko hili  ni sawa asilimia 5.75 Hii ni kutokana na jitihada zinazofanywa Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuongeza ushirikiano na fursa za kibiashara nje ya nchi iliyopelekea masoko ya nyama kuendelea kuongezeka kufikia nchi 11 ambazo ni Bahrain, Comoro, Hong Kong, Jordan, Kenya, Kuwait, Oman, Qatar, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Vietnam.

VilevileDkt. Kijaji hakusita kueleza hatua za ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko ambao wizara yake unaendelea kuutekeleza na kuweka wazi kuwa hadi kufikia mwezi Aprili, 2025 ujenzi huo umefikia asilimia 81.9na kwamba katika hatua hizo za ujenzi umeshatoa ajira kwa wananchi takriban 570, na utakapokamilika unatarajiwa kuajiri zaidi ya watu 30,000.

Mafanikio mengine aliyoeleza Dkt. Kijaji ni kuongezeka kwa ulaji wa nyama, mayai na maziwa kwa wananchi kutokana na   kuimarika kwa biashara ya mazao ya mifugo nchini kwa Mwaka 2024/2025Akifafanua, Dkt. Kijaji amesema kiwango cha unywaji wa maziwa kwa mtu mmoja kimeongezeka kutoka wastani wa lita 67.5 Mwaka 2023/2024 hadi lita 68.1 Mwaka 2024/2025, ulaji wa nyama kutoka kilo 16 Mwaka 2023/2024 hadi kilo 17.6 Mwaka 2024/2025 na ulaji wa mayai kutoka 107 Mwaka 2023/2024 hadi 119 Mwaka 2024/2025. Aidha, ameongeza kuwa pamoja na ongezeko hilo, ulaji wa mazao hayo kwa mtu mmoja mmoja bado haujafikia viwango vinavyopendekezwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ambavyo ni lita 200 za maziwa, kilo 50 za nyama na mayai 300.

Hatua nyingine ya muhimu ambayo Dkt. Kijaji amebainisha ni kudhibitiwa kwa magonjwa yaenezwayo na kupe, mbung’o na wadudu wengine kwa kuratibu uogeshaji wa mifugo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa huku akisema kuwa hadi kufikia Aprili 2025, jumla ya michovyo 1,337,306,118 ya mifugo ikijumuisha ng’ombe 619,731,619, mbuzi 497,805,601, kondoo 198,572,994 na punda 21,195,904. Aidha, amefafanua kuwa uogeshaji huo wa mifugo umesaidia kupunguza matukio ya vifo vya mifugo nchini kutoka asilimia 48 ya vifo vyote katika Mwaka 2023/2024 hadi asilimia 45 kufikia Aprili, 2025.

Kama hiyo haitoshi, Dkt. Kijaji ametaja  vipaumbele vinne (4) ambavyo wizara yake imekusudia kuvitekeleza ili kuendeleza  mapinduzi makubwa katika sekta za mifugo na uvuvi, vipaumbele hivyo ni pamoja na kuongeza uzalishaji, thamani, na masoko ya mazao ya  mifugo na uvuvi, Kuimarisha ulinzi na usimamizi wa rasilimali za mifugo na uvuviKuhamasisha uwekezaji kwenye Sekta za Mifugo na Uvuvi, na Kuimarisha utafiti, mafunzo na huduma kwa sekta za Mifugo na Uvuvi.

Aidha, Dkt. Kijaji alitumia hotuba yake ya bajeti kupongeza jitihada binafsi zinazofanywa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kuziwezesha sekta za mifugo na uvuvi kuongeza tija katika uzalishaji  na kukuza masoko ili  kuifanya wizara kuwa na mwelekeo wa kibiashara zaidi ili kufanya wingi wa rasilimali zilizopo ziendane na mchango sawia katika pato la taifa.



Jumatano, 21 Mei 2025

WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI YAZINDUA RASMI ZOEZI LA KULINDA MAZALIA YA SAMAKI ZIWA VICTORIA

Na. Stanley Brayton, WMUV

◼️ Maboya 32 yawekwa katika mipaka ya Makulia ya Samaki 

◼️ Vifaranga vya Samaki 10,000 vya pandikizwa kwenye Mwalo wa Shadi Ziwa Victoria. 

Nyamagana, Mwanza 

Mei 20, 2025

Serikali, kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), imezindua Rasmi zoezi la kulinda Mazalia ya Samaki kwa kuweka maboya 32 kwenye mipaka ya maeneo maalumu yaliotengwa, kama alama ya kubainisha maeneo ya mazalia na makulia ya Samaki ambayo wavuvi wataweza kubaini maeneo hayo ambayo hayaruhusiwi kuvua, ikiwa ni moja ya njia ya kudhibiti Uvuvi haramu kwenye maeneo hayo maalumu yaliotengwa katika Ziwa hilo.

Akizungumza katika hafla ya Uzinduzi wa Uwekaji Maboya katika Mazalia na Makulia ya Samaki yaliyotengwa, leo Mei 20, 2025 Wilayani Nyamagana Mkoani Mwanza, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Edwin Mhede amesema swala la kuweka alama katika maeneo mahususi yaliobainishwa kwa ajili ya mazalia na makulia ya samaki ni takwa la kikanuni, na maeneo haya yamebainishwa kwa kushirikiana na Maafisa wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na wadau wa Sekta ya Uvuvi.

“Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Ashatu Kijaji amenituma kuja kuweka alama za maboya kwenye maeneo yalioainishwa kama mazalia ya Samaki na vilevile kuja kupandikiza vifaranga vya samaki 10,000 katika mwalo wa Shadi, hapa Ziwa Victoria, japo tayari tulishapandikiza Vifaranga 1,231,000 katika Ziwa Ikimba mkoani Kagera” ameseama Dkt. Mhede

Aidha, Dkt. Mhede amesema hategemei kuona wavuvi wakiharibu au kuvua Samaki katika maeneo haya yaliyobainishwa kwa ajili ya mazalia na makulia ya samaki, na kuwataka Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) kusimamia na kutoa taarifa pamoja na kuwaelimisha wavuvi kutofika sehemu hizo kwani swala la kulinda Rasilimali za uvuvi ni la kila mwananchi.

Vilevile, Dkt. Mhede amesema Sekta ya Uvuvi inatoa fursa ya uvuvi kwa mwananchi, na kuna takribani mahitaji ya samaki tani laki saba kwa mwaka, ambayo inahitaji wadau wajitokeze katika kuwekeza na kuzalisha ili kuweza kufikia lengo ili tusiwe chini kwa ajili ya kuongeza pato la mtu moja na pato la Taifa kiujumla.

Dkt. Mhede amesema Serikali ina mpango kabambe wa miaka kumi ulioanzishwa mwaka 2022 na utaenda mpaka mwaka 2037 kuhakikisha Sekta ya Uvuvi inachochea mapinduzi ya uchumi wa Buluu nchini.

Naye, Mkurugenzi wa Uvuvi Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Mohamed Sheikh amesema mkakati wa kulinda mazalia ya Samaki ni mkubwa kwa sababu katika maeneo ya ziwa na bahari kuna changamoto nyingi ikiwemo mambo ya athari za tabia ya nchi na ongezeko la watu linalopelekea mahitaji ya samaki kuongezeka na samaki kupungua, ndio maana Wizara imeamua kuchukua hatua katika kulinda rasilimali za uvuvi kwa kulinda mazalia ya samaki.

Pia, Prof. Sheikh, amesema huu ni mkakati endelevu, kwani kuna maeneo zaidi ya mia ambayo ni mazalia ya samaki ambayo yanahitaji kuwekewa maboya, na uwekaji huu umekuwa shirikishi kwa kuwashirikisha wadau wa uvuvi na wamekubali kulinda maeneo haya ya mazalia.

Halikadhalika, Prof. Sheikh amebainisha kuwa maboya haya yana ubora mkubwa na yana uwezo wa kuishi kwa miaka 80 kama yakitunzwa vizuri na yametengenezwa na Chuo kikuu cha Dar es Salaam, ili kusaidia katika uzalishaji wa samaki katika Ziwa Victoria.

Kwa Upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Nassoro Mkilagi ameshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji kwa kuleta maboya katika Ziwa Victoria ambayo yatasaidia katika Uzalishaji wa Samaki na kukuza shughuli za Uchumi Mwanza pamoja na Tanzania na kupungua shughuli za Uvuvi haramu nchini.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Edwin Mhede, akikata utepe kama ishara ya kuruhusu uwekaji wa Maboya katika Ziwa Victoria, wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Uwekaji Maboya katika Mazalia na Makulia ya Samaki yaliyotengwa katika Ziwa Victoria na Upandikizaji wa Vifaranga vya Samaki, Mei 20, 2025, Kata ya Luchelele Mwalo wa Shadi, Nyamagana - Mwanza.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Edwin Mhede, akizungumza na wavuvi wa Ziwa Victoria na wadau wa Sekta ya Uvuvi, wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Uwekaji Maboya katika Mazalia na Makulia ya Samaki yaliyotengwa katika Ziwa Victoria na Upandikizaji wa Vifaranga vya Samaki, Mei 20, 2025, Kata ya Luchelele Mwalo wa Shadi, Nyamagana - Mwanza.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Nassoro Mkilagi, akitoa neno la shukrani kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kabla ya kumkaribisha Naibu Katibu Mkuu (Uvuvi), wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Uwekaji Maboya katika Mazalia na Makulia ya Samaki yaliyotengwa katika Ziwa Victoria na Upandikizaji wa Vifaranga vya Samaki, Mei 20, 2025, Kata ya Luchelele Mwalo wa Shadi, Nyamagana - Mwanza.

Mkurugenzi wa Uvuvi Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Mohamed Sheikh, akielezea lengo la kuweka maboya katika Mazalia na Makulia ya Samaki katika Ziwa Victoria, wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Uwekaji Maboya katika Mazalia na Makulia ya Samaki yaliyotengwa katika Ziwa Victoria na Upandikizaji wa Vifaranga vya Samaki, Mei 20, 2025, Kata ya Luchelele Mwalo wa Shadi, Nyamagana - Mwanza.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Edwin Mhede, akipandikiza Vifaranga vya Samaki katika Ziwa Victoria, wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Uwekaji Maboya katika Mazalia na Makulia ya Samaki yaliyotengwa katika Ziwa Victoria na Upandikizaji wa Vifaranga vya Samaki, Mei 20, 2025, Kata ya Luchelele Mwalo wa Shadi, Nyamagana - Mwanza.

Wadau wa Sekta ya Uvuvi wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Uwekaji Maboya katika Mazalia na Makulia ya Samaki yaliyotengwa katika Ziwa Victoria na Upandikizaji wa Vifaranga vya Samaki, Mei 20, 2025, Kata ya Luchelele Mwalo wa Shadi, Nyamagana - Mwanza.

Picha ni muonekano wa Maboya yaliyopandikizwa katika Ziwa Victoria, wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Uwekaji Maboya katika Mazalia na Makulia ya Samaki yaliyotengwa katika Ziwa Victoria na Upandikizaji wa Vifaranga vya Samaki, Mei 20, 2025, Kata ya Luchelele Mwalo wa Shadi, Nyamagana - Mwanza.

Picha ni muonekano wa Boya lililopandikizwa katika Ziwa Victoria, wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Uwekaji Maboya katika Mazalia na Makulia ya Samaki yaliyotengwa katika Ziwa Victoria na Upandikizaji wa Vifaranga vya Samaki, Mei 20, 2025, Kata ya Luchelele Mwalo wa Shadi, Nyamagana - Mwanza.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Edwin Mhede (katikati), akiwa kwenye Boti tayari  kwa kwenda kuweka Maboya na kupandikiza Vifaranga vya Samaki katika Ziwa Victoria, wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Uwekaji Maboya katika Mazalia na Makulia ya Samaki yaliyotengwa katika Ziwa Victoria na Upandikizaji wa Vifaranga vya Samaki, Mei 20, 2025, Kata ya Luchelele Mwalo wa Shadi, Nyamagana - Mwanza, wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Uvuvi, Prof. Mohamed Sheikh na kushoto ni Mtendaji Mkuu wa FETA, Dkt. Semvua Mzighani.



Jumanne, 20 Mei 2025

FETA YAZINDUA MAFUNZO YA KOZI FUPI KADA YA UJUZI WA UVUVI

Na. Stanley Brayton, WMUV

◼️ Vifaranga vya Samaki 35,000 vya pandikizwa kwenye vizimba na bwawa 

Rorya, Mara 

Mei 20, 2025

Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kupitia Wakala wa Elimu  na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), imezindua Mafunzo ya Kozi fupi za Uvuvi na kuboresha Miundombinu ya Kampasi hiyo ya Gabimori, ikiwa ni pamoja na kujenga Madarasa mawili kwa ajili ya Mafunzo, Miundombinu ya msingi ya vitotoleshi vya Vifaranga vya Samaki, Vizimba viwili vya kufugia Samaki, Recirculating Aquaculture System (RAS), na Birika la kunyweshea Mifugo.

Akizungumza wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Miundombinu na Upandikizaji wa vifaranga vya samaki kwa ajili ya kuanza kutoa mafunzo katika Kampasi ya FETA Gabimori, leo Mei 20, 2025 Rorya - Mara, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Edwin Mhede amesema kuwa FETA inaanzisha Rasmi Mafunzo ya Kozi fupi katika Kampasi ya Gabimori ili wananchi waweze kujifunza jinsi ya kufuga Samaki kwa njia ya Vizimba na mabwawa.

“Leo tunazindua Programu za Mafunzo ya Kozi fupi hapa FETA Gabimori ili ianze kuwanufaisha wanajamii wanaozunguka eneo hili na wengine kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo nje na Mkoa wa Mara ili waweze kujifunza shughuli za Uvuvi na ukuzaji viumbe maji. ameseama Dkt. Mhede

Dkt. Mhede amesema kuwa Vifaranga vilivyopandikiza ni 35,000, ambapo vifaranga 4,000 vimepandikizwa kwenye vizimba viwili vya mafunzo ya vitendo, na kwenye bwawa (lambo) vimepandikizwa vifaranga 31,000 vyenye gramu kumi mpaka kumi na tano katika bwawa lenye ujazo wa waji lita milioni kumi.

Vilevile, Dkt. Mhede amesema kuwa vifaranga  vya samaki vitakuwa vinazalishwa FETA Kampasi ya Gabimori ili wale watakaokuwa wameanzisha vikundi vya miradi ya Ufugaji samaki kwa njia ya vizimba waweze kupata vifaranga kwa gharama himilivu.

Dkt. Mhede amesema kinachofanyika ni muendelezo wa Muongozo wa Serikali katika namna ya kutumia rasilimali za maji ili kuongeza kipato zaidi kwa jamii na uchumi wa nchi nzima ambapo Serikali ina mpango wa kupandikiza Vifaranga vya Samaki kwenye vyanzo mbalimbali vya maji nchi nzima.

Aidha, Dkt. Mhede amebainisha kuwa, FETA Gabimori kuna mradi unganishi ambao unahudumia pia Mifugo ambapo kuna Birika la kunyweshea Mifugo na Miundombinu ya Uvuvi.

Naye, Mtendaji Mkuu wa FETA, Dkt. Semvua Mzighani, amesema kuwa miundombinu ambayo imejengwa itasaidia Kampasi ya Gabimori kutoa Mafunzo ya Muda mfupi na ya muda mrefu (pale ambapo miundombinu yote ya chuo itakuwa imekamilika).

Dkt. Mzighani amesema kuwa FETA Gabimori itajikita katika kuwafundisha wananchi uzalishaji wa samaki kuanzia kwenye vifaranga mpaka pale samaki anapofika sokoni au kwenda kuliwa.

Halikadhalika, Dkt. Mzighani amebainisha kuwa wananchi watajifunza mbinu zote za uzalishaji wa vifaranga vya samaki pamoja na chakula bora cha samaki, na jinsi ya kuwatunza samaki pamoja na kupima ubora wa samaki ikiwemo jinsi ya kupata masoko na kuchakata samaki. 

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Mara, ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji, Mhandisi Mwita Chacha Okayo, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kuwataka wananchi wajitokeze kwa wingi ili waweze kupata mafunzo ya Ufugaji Samaki katika Chuo cha FETA Kampasi ya Gabimori.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Edwin Mhede (wa pili kulia), akizungumza na wadau wa Sekta ya Uvuvi (hawapo pichani), wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Miundombinu na Upandikizaji wa vifaranga vya samaki kwa ajili ya kuanza kutoa mafunzo katika Chuo cha Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Kampasi  ya Gabimori, Mei 20, 2025 Rorya - Mara, wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Uvuvi Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Mohamed Sheikh na wa pili kushoto ni Mtendaji Mkuu FETA, Dkt. Semvua Mzighani.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Edwin Mhede (wa pili kushoto), akisalimiana na Mkuu wa Wilaya  ya Rorya, Dkt. Khalfany Haule (wa Kwanza kulia), mara baada  ya kuwasili kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya huyo, wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Miundombinu na Upandikizaji wa vifaranga vya samaki kwa ajili ya kuanza kutoa mafunzo katika Chuo cha Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Kampasi ya Gabimori, Mei 20, 2025 Rorya - Mara, wa kwanza kushoto ni Mtendaji Mkuu wa FETA, Dkt. Semvua Mzighani.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Edwin Mhede (wa pili kushoto), akizungumza na Mkuu wa Wilaya  ya Rorya, Dkt. Khalfany Haule (wa Kwanza kulia), na kumuelezea lengo na dhumuni la ujio wake katika Wilaya hiyo, wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Miundombinu na Upandikizaji wa vifaranga vya samaki kwa ajili ya kuanza kutoa mafunzo katika Chuo cha Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Kampasi ya Gabimori, Mei 20, 2025 Rorya - Mara, wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Uvuvi Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Mohamed Sheikh.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Edwin Mhede (wa pili kushoto), akipandikiza Vifaranga vya Samaki katika kizimba kilichopo Chuo cha FETA Kampasi ya Gabimori, wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Miundombinu na Upandikizaji wa vifaranga vya samaki kwa ajili ya kuanza kutoa mafunzo katika Kampasi hiyo, Mei 20, 2025 Rorya - Mara.

Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Mara, ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji, Mhandisi Mwita Okayo (wa pili kulia), akipandikiza Vifaranga vya Samaki katika kizimba kilichopo Chuo cha FETA Kampasi yaGabimori, wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Miundombinu na Upandikizaji wa vifaranga vya samaki kwa ajili ya kuanza kutoa mafunzo katika Kampasi hiyo, Mei 20, 2025 Rorya - Mara.

Mkufunzi Chuo cha Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Kampasi ya Nyegezi, Bi. Anitha Lobina (wa kwanza kushoto), akipandikiza Vifaranga vya Samaki katika Bwawa lililopo Chuo cha FETA Kampasi ya Gabimori, wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Miundombinu na Upandikizaji wa vifaranga vya samaki kwa ajili ya kuanza kutoa mafunzo katika Kampasi hiyo, Mei 20, 2025 Rorya - Mara.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Edwin Mhede (wa pili kulia), akikagua Ubora wa Birika la kunyweshea Mifugo katika Chuo cha FETA Kampasi ya Gabimori, wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Miundombinu na Upandikizaji wa vifaranga vya samaki kwa ajili ya kuanza kutoa mafunzo katika Kampasi hiyo, Mei 20, 2025 Rorya - Mara.

Picha ni muonekano wa Vizimba wiwili na Bwawa Moja lililopo FETA Kampasi ya Gabimori, yaliyopandikizwa Vifaranga vya Samaki na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Edwin Mhede, wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Miundombinu na Upandikizaji wa vifaranga vya samaki kwa ajili ya kuanza kutoa mafunzo katika Kampasi hiyo, Mei 20, 2025 Rorya - Mara.


WATAALAMU KUTOKA NIGERIA KUJIFUNZA UCHUMI WA BULUU TANZANIA

Na. Hamisi Hussein - WMUV, Dodoma

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Abdul Mhinte, amesema kuwa Tanzania inaendelea kutekeleza sera ya kukuza Uchumi wa Buluu kwa kutumia rasilimali zake nyingi ambazo zimekuwa chachu ya maendeleo ya uchumi huo.

Bw. Mhinte ameyasema hayo leo, Mei 20, 2025, alipokuwa akiikaribisha kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara, Prof. Riziki Shemdoe,  timu ya wataalamu kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Sera na Mipango Kitaifa ya Nigeria (NIPSS), ambayo imewasili nchini kwa ziara ya mafunzo juu ya masuala ya Uchumi wa Buluu.

“Nchi yetu ina rasilimali nyingi zinazochochea maendeleo ya Uchumi wa Buluu, zikiwemo bahari, maziwa na mito, ambazo zimekuwa zikitumika kukuza na kuendeleza sekta hii muhimu,” amesema Bw. Mhinte.

Ameeleza kuwa sekta ya uvuvi inatoa fursa nyingi, na kusisitiza utayari wa Wizara kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuendeleza sekta hiyo kama sehemu ya mpango mpana wa kukuza Uchumi wa Buluu.

Kwa upande wake, Kiongozi wa msafara huo ambaye ni Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu kutoka Nigeria, Bw. Leye Oyebade, ameishukuru Wizara kwa juhudi inazoendelea kuzifanya katika kukuza Uchumi wa Buluu kupitia sekta ya uvuvi.

Timu hiyo ya wataalamu kutoka NIPSS imeanza ziara yao nchini Tanzania kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu katika masuala ya uchumi wa buluu.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ( Mifugo) Bw. Abdul Mhinte (Kulia) akipokea Zawadi Kutoka Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu kutoka Nchini Nigeria (Kushoto) walipofika Ofisi za Wizara kwa ajili ya Ziara ya kujifunza juu ya masuala ya uchumi wa Buluu Mei 20, 2025 , Mtumba Jijini Dodoma

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ( Mifugo) Bw. Abdul Mhinte (Kulia) akisisitiza Jambo wakati akiongea na Timu ya Watalaamu Kutoka Nigeria (haipo Pichani) iliyokuja Nchini kwa Ziara ya kujifunza masuala ya Uchumi wa Buluu, Mei 20, 2025 , Mtumba Jijini Dodoma

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ( Mifugo) Bw. Abdul Mhinte (Katikati) Kwa Niaba ya Katibu Mkuu akizungumza na timu ya wataalamu kutoka nchini Nigeria walipofika Ofisi za Wizara kwa ajili ya Ziara ya kujifunza juu ya masuala ya uchumi wa Buluu Mei 20, 2025 , Mtumba Jijini Dodoma

Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu Nchini Nigeria Bw. Leye Oyebade akizungumza na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ( Mifugo) Bw. Abdul Mhinte wakati wa timu ya wataalamu kutoka nchini humo walipofika Ofisi za Wizara kwa ajili ya Ziara ya kujifunza juu ya masuala ya uchumi wa Buluu Mei 20, 2025 , Mtumba Jijini Dodoma

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ( Mifugo) Bw. Abdul Mhinte ( wa Tano, Kulia) akiwa kwenye Picha ya Pamoja na timu ya Wataalamu kutoka nchini Nigeria walipofika Ofisi za Wizara kwa ajili ya Ziara ya kujifunza juu ya masuala ya Uchumi wa Buluu Mei 20, 2025 , Mtumba Jijini Dodoma

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ( Mifugo) Bw. Abdul Mhinte (Katikati) akiwa kwenye Picha ya Pamoja na timu ya wataalamu kutoka nchini Nigeria walipofika Ofisi za Wizara kwa ajili ya Ziara ya kujifunza juu ya masuala ya uchumi wa Buluu Mei 20, 2025 , Mtumba Jijini Dodoma


Jumatatu, 19 Mei 2025

BARAZA JIPYA LA WAFANYAKAZI LA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI LAUNDWA

 Na. Chiku Makwai – WMUV

Baraza jipya la wafanyakazi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi limeundwa kwa lengo la kuwashirikisha wafanyakazi wa Wizara hiyo katika utekelezaji wa shughuli za Serikali na ushirikiano, kuishauri Wizara juu ya ufanisi wa kazi na hatua zinazofaa kuchukuliwa ili kuimarisha utoaji huduma.

Akizungumza katika mkutano uliofanyika leo Mei 19, 2025 katika ukumbi wa Mabeyo – Complex jijini Dodoma Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema baraza hilo linapaswa kushauri Wizara juu ya mambo muhimu yanayohusu Haki, Wajibu na Maslahi ya wafanyakazi ili kuleta ufanisi na tija katika utekelezaji wa malengo ya Wizara hiyo.

“tunapaswa kulitumia baraza hili kama jukwaa muhimu la kutolea maoni, kujadili masuala yanayowahusu wafanyakazi na kutafuta suluhu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili Wizara yetu” 

Ameongeza kuwa katika mwaka wa Fedha 2025/2026 Wizara imejiwekea vipaumbele ambavyo ni Kuimarisha afya ya mifugo na viumbe maji, mifumo ya utambuzi wa mifugo, kuimarisha uongezaji thamani na masoko,pamoja na biashara ya mazao ya mifugo na uvuvi.

Pia Kuimarisha ulinzi na usimamizi wa rasilimali za Mifugo na Uvuvi kwa kuanzisha vyombo maalum vya utendaji kwa ajili ya kusimamia na kulinda rasilimali za wizara hiyo na kuboresha vituo vya ulinzi na usimamizi wa rasilimali zake na Kuimarisha utafiti, mafunzo na huduma za ugani katika sekta hiyo kuimarisha uwezo wa Taasisi za Utafiti na Mafunzo ya Mifugo na Uvuvi. 

Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambaye ni mwenyekiti wa baraza hilo Prof. Riziki Shemdoe amesema baraza hilo linaridhaa ya watumishi wote wa Sekta hiyo na kutakuwa na mjadiliano ya ajenda ikiwemo na ajenda ya bajeti.

Baraza la kwanza la fungu 99 limeundwa baada ya muunganiko wa sekta hizo mbili kwa kuzingatia kanuni na sheria ya mashauriano katika utumishi wa umma ya mwaka 2003 (the Public Service Negotiating Machinery, Act 2003).







Jumapili, 18 Mei 2025

WAFUGAJI WAHIMIZWA KUMTUNZA MNYAMA PUNDA

Na. Chiku Makwai - WMUV

Naibu  Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Abdul Mhinte amesema ni wajibu wa kila mfugaji punda kumtunza mnyama huyo kwani anahaki kama ilivyo kwa wanyama wengine, ikiwemo haki ya kutolala njaa, kutopata maumivu, kupata maji safi na kuwa huru dhidi ya magonjwa na kazi zinazozidi uwezo wake.

Bw. Mhinte ameyasema hayo Mei 17, 2025 kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt Ashatu Kijaji wakati wa maadhimisho ya Siku ya Punda Duniani yaliyofanyika katika Kijiji cha Chambalo, Wilaya ya Chemba, mkoani Dodoma. 

Aidha, Bw. Mhinte aliwasisitiza wafugaji kuhusu umuhimu wa kutambua mchango wa mnyama huyo katika maendeleo ya kiuchumi.

“Punda ana haki ya kutopata majeraha au mateso wakati wa kazi, kupata mapumziko ya kutosha na kupewa hifadhi stahiki,” alisema Mhinte, 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo, Dkt. Benezeth Lutege, amesema biashara ya punda na mazao yake ilisababisha kutoweka kwa wanyama hao barani Afrika  hivyo nchi za Afrika zilikubaliana kusitisha biashara hiyo kwa miaka 15.

Katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa INADES-Formation Tanzania Mbarwa Kivuyo, amebainisha kwamba  wamesambaza elimu ya matunzo bora ya punda kwa wafugaji elimu hiyo imejumuisha umuhimu wa lishe bora, upole wakati wa kazi, matumizi ya matandiko ili kuzuia majeraha.







Jumamosi, 17 Mei 2025

MAFUNZO YA WATAALAMU WA AFYA YA MIFUGO KIMATAIFA, YAZINDULIWA

Na. Chiku MAKWAI - WMUV

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imezindua rasmi mradi wa mafunzo kwa wataalamu wa afya ya mifugo, yanayofanyika katika nchi nne za Tanzania, Botswana, Zambia na Malawi.

Akizungumza leo (Mei 17, 2025) wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mafunzo maalum kwa wataalam hao  uliofanyika katika Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema mafunzo hayo yamelenga kuwapa ujuzi wa kisasa vijana, hususan wahadhiri ili waendane na hali halisi ya sekta ya ufugaji ndani na nje ya nchi.

Akizungumzia juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Prof. Shemdoe amesema Serikali iinaanzisha Kampeni ya Chanjo Kitaifa kwa ajili ya magonjwa 13 sugu ya mifugo itakayozinduliwa mwaka huu.

“Kampeni hiyo itaanza na magonjwa matatu, ambapo ng’ombe milioni 19, mbuzi na kondoo milioni 17, pamoja na kuku milioni 40 wanatarajiwa kuchanjwa nchi nzima. ” amesema Prof. Shemdoe.

Aidha, amebainisha kuwa kampeni hiyo itaambatana na mpango wa utambuzi wa mifugo kwa kuweka hereni kwa mifugo ili kutambua waliopata  chanjo na mahali walipo.

“Hii itamsaidia mfugaji kwenye ufuatiliaji wa afya ya mifugo wake na pia kufungua fursa katika masoko ya kimataifa,” ameongeza Prof. Shemdoe.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene,  amesema baadhi ya wahadhiri  watapatiwa mafunzo ndani ya nchi, huku wengine wakipewa fursa ya kwenda Hungary, Slovakia na Ubelgiji kwa ajili ya mafunzo ya juu na utaalamu katika maeneo yanayohusiana na afya ya mifugo.

Washiriki wa mafunzo haya ni pamoja na wataalamu kutoka halmashauri za wilaya, manispaa na majiji, pamoja na wahadhiri na wanafunz i wa LITA. 

Mafunzo haya yameandaliwa kupitia mradi wa EDVET unaosimamiwa na Shirika la MIOUT, kwa kushirikiana na wataalamu kutoka nchi za Hungary, Finland na Slovakia.