Nav bar

Jumatano, 27 Aprili 2022

KIKAO CHA MAFUNZO REJEA YA UFUGAJI SAMAKI KWA MAAFISA UGANI MJINI SONGEA



Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Bw. Emmanuel Kisongo akifungua kikao cha mafunzo rejea ya ufugaji samaki kwa maafisa ugani (hawapo pichani) kutoka halmashauri za mikoa ya Mbeya, Songwe, Katavi, Kigoma na Ruvuma na kuwataka maafisa hao kuwa chachu ya kuhamasisha ufugaji samaki kwa wananchi. Mafunzo hayo yameandaliwa na Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na yanafanyika kwa siku nne Mjini Songea. (21.03.2022)* 

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kulia aliyekaa) akiwa pamoja na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangyise (wa pili kutoka kushoto aliyekaa) wakisaini mkataba wa Makubaliano ya Kujenga, Kuanzisha na Kusimamia Kituo cha Taifa cha Ukuzaji Viumbe Maji bahari kati ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakati wa halfla fupi ya uwekaji saini mkataba huo iliyofanyika kwenye Shule Kuu ya Sayansi na Teknolojia ya Uvuvi - Kampasi ya Kunduchi Jijini Dar es Salaam. (22.03.2022)* 

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini Mkataba wa Makubaliano ya Kujenga, Kuanzisha na Kusimamia Kituo cha Taifa cha Ukuzaji Viumbe Maji bahari kati ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambapo amemtaka mkandarasi kumaliza kazi aliyopewa kwa wakati na kwa kuzingatia ubora. Kushoto ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye. Hafla hiyo imefanyika kwenye Shule Kuu ya Sayansi na Teknolojia ya Uvuvi - Kampasi ya Kunduchi Jijini Dar es Salaam. (22.03.2022)* 

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini Mkataba wa Makubaliano ya Kujenga, Kuanzisha na Kusimamia Kituo cha Taifa cha Ukuzaji Viumbe Maji bahari kati ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Hafla hiyo imefanyika kwenye Shule Kuu ya Sayansi na Teknolojia ya Uvuvi - Kampasi ya Kunduchi Jijini Dar es Salaam. (22.03.2022)*

Picha ya pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (wa saba kutoka kulia) na Viongozi na Wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Wizara ya Mifugo na Uvuvi mara baada ya kumalizika kwa hafla fupi ya utiaji saini Mkataba wa Makubaliano ya Kujenga, Kuanzisha na Kusimamia Kituo cha Taifa cha Ukuzaji Viumbe Maji bahari kati ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na Wizara ya Mifugo na Uvuvi. (22.03.2022)* 


 

MWONGOZO WA CHAKULA BORA CHA SAMAKI NJIANI KULETA TIJA KWA WAFUGAJI*

 

Na. Edward Kondela

Serikali imesema imeandaa mwongozo wa uandaaji wa chakula bora cha samaki na kwamba itahakikisha mwongozo huo unafuatwa na watengenezaji wa chakula hicho ili kuleta tija kwa wafugaji wa samaki ambao wamekuwa wakipata changamoto ya kutopata chakula bora cha samaki hapa nchini.

Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Nazael Madalla, amebainisha hayo (21.03.2022) Mjini Songea, katika Mkoa wa Ruvuma, kando ya mafunzo rejea kwa maafisa ugani kutoka halmashauri za mikoa ya Mbeya, Songwe, Katavi, Kigoma na Ruvuma ambao wamealikwa kwa ajili ya kujifunza na kukumbushwa njia bora za ufugaji samaki, ili kuhamasisha wananchi kufuga samaki.

Dkt. Madalla amesema licha ya serikali kufanya juhudi mbalimbali zikiwemo za kuhakikisha upatikanaji wa vifaranga vingi vya samaki, kwa sasa serikali inaweka nguvu zaidi katika kuhakikisha vyakula bora vya samaki vinazalishwa hapa nchini ili kuwapunguzia gharama wafugaji wa samaki kwa kuwa vyakula vingi vya samaki vinatoka nje ya nchi  na kwamba vinagharimu fedha nyingi.

Akifungua mafunzo hayo ya siku nne Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Bw. Emmanuel Kisongo amesema, anaamini maafisa ugani hao watakuwa chachu ya maendeleo na kufanya ufugaji wa samaki uwe endelevu.

Bw. Kisongo amesema ni wakati sasa maafisa ugani kuhamasisha, kuendeleza na kusimamia shughuli za uendelezaji ukuzaji viumbe maji ili wananchi waingie katika uchumi wa buluu kwa kufuga samaki na kuongeza uzalishaji wa samaki kupitia njia mbadala.

Nao baadhi ya wadau wa  ufugaji wa samaki kutoka Mkoani Ruvuma wameiomba serikali kujenga  kiwanda cha kusindika chakula bora  cha samaki ili kuweza kuwasaidia kutatua changamoto ya upatikanaji wa chakula ili ufugaji wao uwe na tija.

Mmoja wa wadau hao Bw. Kevin Chale mwenye mabwawa 11 ambapo kwa mwaka anavuna samaki aina ya sato tani 2 hadi 3 amesema kutokana na uhaba wa chakula bora cha samaki inakuwa ni changamoto kwao  katika kuongeza tija za ufugaji samaki kwa wingi.

Ameongeza kuwa changamoto ya upatikanaji vifaranga vya samaki tayari serikali imetatua, ambapo wanapata kwa wingi katika Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji Ruhila kilichopo Mkoani Ruvuma.

Naye Bw. Christopher Ndunguru  mdau mkubwa wa samaki katika Manispaa ya Songea amesema alianza kufuga Mwaka 2014 kwa kuanza na bwawa moja na sasa anamiliki  mabwawa 20, anafuga samaki ambao hawazaliani ili waweze  kukua na kuongezeka ukubwa ambapo kwa utafiti mdogo aliofanya amebaini kuwa wanaongezeka kwa hadi gram 50 -200 kwa mwezi.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji, inafanya mafunzo rejea ya siku nne Mjini Songea katika Mkoa wa Ruvuma yanayohusisha maafisa ugani kutoka mikoa ya Mbeya, Songwe, Katavi, Kigoma na Ruvuma ambao wamealikwa kwa ajili ya kujifunza na kukumbushwa njia bora za ufugaji samaki, ili kuhamasisha wananchi kufuga samaki.


Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Bw. Emmanuel Kisongo akifungua kikao cha mafunzo rejea ya ufugaji samaki kwa maafisa ugani (hawapo pichani) kutoka halmashauri za mikoa ya Mbeya, Songwe, Katavi, Kigoma na Ruvuma na kuwataka maafisa hao kuwa chachu ya kuhamasisha ufugaji samaki kwa wananchi. Mafunzo hayo yameandaliwa na Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na yanafanyika kwa siku nne Mjini Songea. (21.03.2022)* 

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Imani Kapinga (wa pili kutoka kushoto), akiwaongoza maafisa ugani kutoka halmashauri za mikoa ya Mbeya, Songwe, Katavi, Kigoma na Ruvuma kutembelea Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji Ruhila kilichopo katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma mara baada ya kumaliza siku ya kwanza ya mafunzo rejea ya ufugaji bora wa samaki ili kuhamasisha wananchi kufuga samaki. (21.03.2022)* 


WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI KUPOKEA MELI YA UVUVI YA WAWEKEZAJI JIJINI DAR ES SALAAM

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kushoto) akisalimiana na Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Suleiman Makame (wa pili kulia)baada ya kuwasili bandarini Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupokea meli ya Uvuvi ya Wawekezaji kutoka nchini Uhispania meli ambayo itakuwa inafanya kazi ya kuvua samaki katika bahari kuu. (21.03.2022)* 

 Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Suleiman Makame (kulia) akisalimiana na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Dkt. Christina Ishengoma (kushoto) wakati wakiwasili bandarini Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupokea meli ya Uvuvi ya Wawekezaji kutoka nchini Uhispania meli ambayo itakuwa inafanya kazi ya kuvua samaki katika bahari kuu. Katikati ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki. (21.03.2022)* 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) akimkabidhi Kibali cha kuvua nje ya mipaka ya Tanzania kwa Meneja wa Vyombo Vya Uvuvi vya Kampuni ya Albacora ya nchini Uhispania, Bw. Imanol Loinaz mara baada ya kuwasili kwa meli ya PACIFIC STAR itakayokuwa inafanya kazi ya uvuvi wa bahari kuu. Waziri Ndaki amekabidhi kibali hicho bandarini Jijini Dar es Salaam. Katikati ni Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Suleiman Makame na kushoto ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega. (21.03.2022)*  

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Mhe. Suleimani Makame (kulia) akimkabidhi Leseni ya uvuvi wa bahari kuu kwa Meneja wa Vyombo Vya Uvuvi vya Kampuni ya Albacora ya nchini Uhispania, Bw. Imanol Loinaz mara baada ya kuwasili kwa meli ya PACIFIC STAR itakayokuwa inafanya kazi ya uvuvi wa bahari kuu. Waziri Masoud amekabidhi kibali hicho bandarini Jijini Dar es Salaam. Katikati ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki na kushoto ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega. (21.03.2022)* 

Meli ya Uvuvi ya Wawekezaji wa Kampuni ya Albacora ya nchini Uhispania ikiwa imewasili kwenye bandari ya Dar es Salaam. (21.03.2022)* 


 

Jumatatu, 25 Aprili 2022

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KILIMO MIFUGO NA MAJI WAKIKAGUA UJENZI WA BWAWA LA KUNYWESHEA MAJI MIFUGO CHALINZE

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akitoa ufafanuzi kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakati ilipotembelea Kijiji cha Chamakweza wilayani Chalinze mkoa wa Pwani kukagua ujenzi wa Bwawa la kunyweshea Maji Mifugo. Kushoto ni Mhe. Dkt. Chistina Ishengoma ambaye ndio Mwenyekiti wa Kamati hiyo. (18.03.2022)* 
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiwa na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Viongozi, Wataalam na Wafugaji wakati walipokuwa wanatembelea kukagua Bwawa la kunyweshea Maji Mifugo la Chamakweza wilayani Chalinze mkoa Pwani. (18.03.2022)* 
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Dkt. Christina Ishengoma (wa pili kutoka kushoto) akijiridhisha kama maji yanatoka kwenye bomba wakati Kamati hiyo ilipofika kukagua ujenzi wa Bwawa la kunyweshea Maji Mifugo la Chamakweza wilayani Chalinze mkoa Pwani. Kulia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki. (18.03.2022)* 

*Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Dkt. Asimwe Rwiguza (kulia) akitoa maelezo mafupi juu ya ujenzi wa Bwawa la kunyweshea Maji Mifugo la Chamakweza wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ilipotembelea mradi huo. (18.03.2022)* 

 

NZUNDA AHIMIZA WELEDI, UWAJIBIKAJI*

 

Na Mbaraka Kambona, Morogoro

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda amewataka Watumishi wa Wizara hiyo, Sekta ya Mifugo kufanya kazi kwa weledi, uadilifu, uwajibikaji na usikivu kwa umma ili waweze kutoka huduma bora kwa jamii.

Nzunda alitoa wito huo alipokuwa akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi, Sekta ya Mifugo kilichofanyika Mkoani Morogoro Machi 18, 2022.

Wakati akizungumza na Watendaji na Watumishi wa Wizara hiyo aliwataka kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake waimarishe uwajibikaji ili waweze kuwaletea  maendeleo wananchi.

"Jukumu letu la kwanza ni kuhakikisha tunatoa huduma bora kwa umma kwa kiwango cha juu na zinazokidhi matarajio na matakwa ya wananchi", alisema Nzunda

Pia, aliwataka wajiandae kufanya mabadiliko makubwa katika Sekta hiyo huku akiwahimiza kuja na mikakati ya kupata rasilimali fedha nje ya bajeti ya Serikali.

"Ili tuweze kuleta mabadiliko hayo ni wajibu wetu kuwa wabunifu na kuwashirikisha Wadau kupata rasilimali na kuvutia wawekezaji kuwekeza katika sekta hii", aliongeza

Aliendelea kusema kuwa serikali itaendelea kuwawekea mazingira bora ya utendaji wa kazi ikiwemo kuwapatia rasilimali fedha na vifaa ili waweze kutoa huduma ambayo wananchi wanaitaka.

Aidha, aliwataka Watumishi hao kufanya kazi kwa kuzingatia matokeo chanya na kuachana na michakato isiyo na tija

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda akiongea na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Sekta ya Mifugo (hawapo pichani) wakati akifungua kikao cha baraza hilo kilichofanyika Mkoani Morogoro Machi 18, 2022. wakati akifungua kikao hicho, Bw. Nzunda aliwahimiza Watumishi kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi ili kuongeza tija na ufanisi wa kazi. 

 

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi, Sekta ya Mifugo muda mfupi baada kufungua kikao cha baraza hilo kilichofanyika Mkoani Morogoro Machi 18, 2022. 

UMUHIMU WA USHIRIKIANO BAINA YA VIONGOZI WA WILAYA YA MULEBA NA WAVUVI MKOANI KAGERA

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah akifafanua kwa wajumbe (hawapo pichani) katika kikao kilichomhusisha pia Mkuu wa Wilaya ya Muleba na maafisa wafawidhi wa Kanda ndogo za Bukoba na Muleba pamoja na vikosi vya ulinzi na usalama katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Kagera, juu ya umuhimu wa ushirikiano baina ya viongozi wa Wilaya ya Muleba na wavuvi pamoja na kuhakikisha halmashauri ya wilaya hiyo inatoa vibali maeneo ya visiwani ili kuwaondolea kero wavuvi kusafiri mwendo mrefu kufuata vibali hivyo pamoja na wavuvi kuruhusiwa kuuza mazao ya uvuvi mahali popote nchini kwa kuzingatia sheria za nchi. (15.03.2022)* 

Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Emmanuel Bulayi (aliyesimama) akifafanua vifungu mbalimbali vya Sheria ya Uvuvi, kwa wajumbe katika kilichofanyika kwenye Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Kagera, na kuwakutanisha Mkuu wa Wilaya ya Muleba na maafisa wafawidhi wa Kanda ndogo za Bukoba na Muleba pamoja na vikosi vya ulinzi na usalama, ambapo lengo la kikao hicho ni kuondoa kero zinazoihusu sekta ya uvuvi katika wilaya hiyo. (15.03.2022)* 

 

Picha ya pamoja ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Prof. Faustin Kamuzora, Mkuu wa wilaya ya Muleba Bw. Toba Nguvila, Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Emmanuel Bulayi, maafisa wafawidhi wa Kanda ndogo za Bukoba na Muleba pamoja na vikosi vya ulinzi na usalama, mara baada ya kumaliza kikao kilichohusu namna ya kutatua kero mbalimbali zinazohusu sekta ya uvuvi. Kikao hicho kimefanyika katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Kagera. (15.03.2022)* 


 Akiwa Mkoani Geita katika Soko la Kimataifa la Kasenda lililopo Wilayani Chato, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amezungumza na baadhi ya wadau wa sekta ya uvuvi na kuwajulisha namna uongozi wa wizara umefanya kikao na uongozi wa Mkoa wa Kagera na Wilaya ya Muleba na kukubaliana kuongeza ushirikiano na viongozi wa Mkoa wa Geita, Wilaya ya Chato pamoja na wadau wa sekta ya uvuvi ili wavuvi waweze kufanya shughuli zao bila kubughudhiwa na waruhusiwe kusafirisha mazao ya uvuvi popote nchini kwa kuzingatia sheria za nchi. (16.03.2022)*