Nav bar

Jumatano, 27 Aprili 2022

MWONGOZO WA CHAKULA BORA CHA SAMAKI NJIANI KULETA TIJA KWA WAFUGAJI*

 

Na. Edward Kondela

Serikali imesema imeandaa mwongozo wa uandaaji wa chakula bora cha samaki na kwamba itahakikisha mwongozo huo unafuatwa na watengenezaji wa chakula hicho ili kuleta tija kwa wafugaji wa samaki ambao wamekuwa wakipata changamoto ya kutopata chakula bora cha samaki hapa nchini.

Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Nazael Madalla, amebainisha hayo (21.03.2022) Mjini Songea, katika Mkoa wa Ruvuma, kando ya mafunzo rejea kwa maafisa ugani kutoka halmashauri za mikoa ya Mbeya, Songwe, Katavi, Kigoma na Ruvuma ambao wamealikwa kwa ajili ya kujifunza na kukumbushwa njia bora za ufugaji samaki, ili kuhamasisha wananchi kufuga samaki.

Dkt. Madalla amesema licha ya serikali kufanya juhudi mbalimbali zikiwemo za kuhakikisha upatikanaji wa vifaranga vingi vya samaki, kwa sasa serikali inaweka nguvu zaidi katika kuhakikisha vyakula bora vya samaki vinazalishwa hapa nchini ili kuwapunguzia gharama wafugaji wa samaki kwa kuwa vyakula vingi vya samaki vinatoka nje ya nchi  na kwamba vinagharimu fedha nyingi.

Akifungua mafunzo hayo ya siku nne Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Bw. Emmanuel Kisongo amesema, anaamini maafisa ugani hao watakuwa chachu ya maendeleo na kufanya ufugaji wa samaki uwe endelevu.

Bw. Kisongo amesema ni wakati sasa maafisa ugani kuhamasisha, kuendeleza na kusimamia shughuli za uendelezaji ukuzaji viumbe maji ili wananchi waingie katika uchumi wa buluu kwa kufuga samaki na kuongeza uzalishaji wa samaki kupitia njia mbadala.

Nao baadhi ya wadau wa  ufugaji wa samaki kutoka Mkoani Ruvuma wameiomba serikali kujenga  kiwanda cha kusindika chakula bora  cha samaki ili kuweza kuwasaidia kutatua changamoto ya upatikanaji wa chakula ili ufugaji wao uwe na tija.

Mmoja wa wadau hao Bw. Kevin Chale mwenye mabwawa 11 ambapo kwa mwaka anavuna samaki aina ya sato tani 2 hadi 3 amesema kutokana na uhaba wa chakula bora cha samaki inakuwa ni changamoto kwao  katika kuongeza tija za ufugaji samaki kwa wingi.

Ameongeza kuwa changamoto ya upatikanaji vifaranga vya samaki tayari serikali imetatua, ambapo wanapata kwa wingi katika Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji Ruhila kilichopo Mkoani Ruvuma.

Naye Bw. Christopher Ndunguru  mdau mkubwa wa samaki katika Manispaa ya Songea amesema alianza kufuga Mwaka 2014 kwa kuanza na bwawa moja na sasa anamiliki  mabwawa 20, anafuga samaki ambao hawazaliani ili waweze  kukua na kuongezeka ukubwa ambapo kwa utafiti mdogo aliofanya amebaini kuwa wanaongezeka kwa hadi gram 50 -200 kwa mwezi.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji, inafanya mafunzo rejea ya siku nne Mjini Songea katika Mkoa wa Ruvuma yanayohusisha maafisa ugani kutoka mikoa ya Mbeya, Songwe, Katavi, Kigoma na Ruvuma ambao wamealikwa kwa ajili ya kujifunza na kukumbushwa njia bora za ufugaji samaki, ili kuhamasisha wananchi kufuga samaki.


Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Bw. Emmanuel Kisongo akifungua kikao cha mafunzo rejea ya ufugaji samaki kwa maafisa ugani (hawapo pichani) kutoka halmashauri za mikoa ya Mbeya, Songwe, Katavi, Kigoma na Ruvuma na kuwataka maafisa hao kuwa chachu ya kuhamasisha ufugaji samaki kwa wananchi. Mafunzo hayo yameandaliwa na Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na yanafanyika kwa siku nne Mjini Songea. (21.03.2022)* 

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Imani Kapinga (wa pili kutoka kushoto), akiwaongoza maafisa ugani kutoka halmashauri za mikoa ya Mbeya, Songwe, Katavi, Kigoma na Ruvuma kutembelea Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji Ruhila kilichopo katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma mara baada ya kumaliza siku ya kwanza ya mafunzo rejea ya ufugaji bora wa samaki ili kuhamasisha wananchi kufuga samaki. (21.03.2022)* 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni