Na. Daudi Nyingo – Iringa
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede, ameongoza zoezi la utambuzi na uchanjaji wa mifugo mkoani Iringa, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Utoaji Chanjo na Utambuzi wa Mifugo iliyozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipokuwa mkoani Simiyu hivi karibuni.
Akizungumza Julai 3, 2025, mkoani Iringa, Dkt. Mhede alisema kuwa kampeni hiyo ya miaka mitano inalenga kuchanja mifugo yote nchini kama sehemu ya uwekezaji katika sekta ya mifugo, unaowaletea faida wafugaji na kukuza uchumi wa taifa.
“Tunalenga kuchanja ng’ombe wapatao 400,000 hapa Iringa. Tayari tumejiridhisha kuwa chanjo zipo za kutosha, na tumeanza kutembelea maeneo mbalimbali kama Kalenga na shamba la mifugo la Kibete, linalomilikiwa na Richard Philips, kuhakikisha zoezi linaenda vizuri,” alisema Dkt. Mhede.
Mbali na ng’ombe, Dkt. Mhede alibainisha kuwa chanjo pia zitatolewa kwa kuku, na aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kwani huduma hiyo inatolewa kwa gharama nafuu kutokana na ruzuku ya serikali.
Aidha, Dkt. Mhede alisema kuwa utekelezaji wa kampeni hii unakwenda sambamba na juhudi za serikali za kufungua masoko ya nje kwa mifugo na mazao yake.
Kwa upande wake, Afisa Mifugo wa Mkoa wa Iringa, Hamadi Mwansasu, alisema kuwa mkoa umepokea chanjo dhidi ya homa ya mapafu kwa ng’ombe, pamoja na chanjo za kuku dhidi ya kideri, mafua, na ndui. Alibainisha kuwa tayari timu ya wataalamu ipo kazini kuhakikisha zoezi linafanyika kwa ufanisi katika halmashauri zote za Mkoa wa Iringa.
Kwa mujibu wa Mwansasu, matarajio ni kwamba tija ya uzalishaji wa mifugo itaongezeka, na hivyo kuwasaidia wafugaji kupata kipato zaidi na kuboresha maisha yao.
Naye Katibu wa Wafugaji Mkoa wa Iringa, Felix Sanga, aliipongeza serikali kwa kuona umuhimu wa kutoa chanjo dhidi ya homa ya mapafu kwa mifugo, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza vifo vya mifugo na kuongeza uzalishaji.
“Sisi kama viongozi tulifanya kampeni ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa chanjo, na tunashukuru zoezi hili limepokelewa kwa mikono miwili,” alisema Sanga.
Mkurugenzi wa Shamba la Mifugo la Philps, Bw. Richard Philips, alisema kuwa shamba lake limeshiriki kikamilifu katika zoezi hilo na kuwataka wafugaji wengine wachangamkie fursa hiyo. Aliongeza kuwa serikali imeahidi kuongeza aina zaidi za chanjo kwa lengo la kulinda afya ya mifugo.
Miongoni mwa wafugaji walionufaika na zoezi hilo ni Donard Luhavi kutoka Kijiji cha Kalenga, ambaye alisema kuwa mpango huo utaimarisha afya ya mifugo na kuongeza thamani ya mauzo yao.
“Gharama ya chanjo imepunguzwa kutoka shilingi 1,000 hadi 500 kwa kila ng’ombe. Hii imetupa motisha zaidi ya kushiriki kikamilifu katika zoezi hili,” alisema Luhavi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni