Nav bar

Jumamosi, 30 Septemba 2023

MIFUGO NA UVUVI YAIBAMIZA TUME YA UTUMISHI MPIRA WA PETE.

◾ Yatoa suluhu na Ofisi ya waziri Mkuu (Sera) upande wa mpira wa miguu. 


Timu ya mpira wa pete kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza vema mbio za kutwaa taji la mchezo huo kwenye michuano ya SHIMIWI inayoendelea mkoani Iringa mara baada ya kufanikiwa kuifunga timu ya Tume ya Utumishi kwa magoli 11-6 kwenye mchezo uliochezwa chuo kikuu cha Ruaha leo Septemba 29, 2023.


Timu hiyo ilianza kwa kasi ya chini kipindi cha kwanza ambapo hadi timu zinaenda mapumziko ilikuwa imeshakubali kichapo cha magoli 4-3 hali iliyomlazimu kocha wa timu hiyo Bi. Masele Shabani kufanya mabadiliko na kuiongezea kasi  timu hiyo hali iliyowafanya waibuke na ushindi huo mpaka mwisho wa mchezo.


Kwa upande mwingine katika mchezo uliochezwa mapema kabisa leo asubuhi, timu ya Wizara hiyo kwa upande wa mpira wa miguu imetoka suluhu na timu ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera) mara baada ya kuhitimishwa kwa mchezo uliokuwa na upinzani mkali kutoka pande zote mbili.


Timu hiyo inatarajia kutupa karata yake ya pili kesho (Septemba 30, 2029) kwenye mchezo baina yake na timu ya Mawasiliano utakaochezwa kwenye uwanja wa Mkwawa 2 kuanzia saa 08 kamili mchana.WAZALISHAJI WA VYAKULA VYA MIFUGO WATAKIWA KUHAKIKI UBORA WA SAMPULI ZAO

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega ametoa rai na kuwasisitiza wazalishaji wa vyakula vya mifugo wote nchini kuhakikisha wanapeleka sampuli za vyakula wanavyozalisha kwenye maabara ya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) ili kuhakiki ubora na viwango kwa kuzingatia matakwa ya sheria hiyo kabla ya kuanza kuwauzia wafugaji ndani ya nchi au kuvisafirisha nje ya nchi. 


Waziri Ulega alitoa rai hiyo wakati akifungua warsha kuhusu uzalishaji wa protini kwa ajili ya vyakula vya Mifugo na kupunguza ushindani iliyofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 29, 2023.


Alisema kuwa tasnia hiyo imepewa kipaumbele na umuhimu wa pekee kwa kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetunga sheria mahususi inayojulikana kwa jina la Sheria ya Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Wanyama (Sura Na.180) pamoja na Kanuni na Miongozo mbalimbali. Lengo la sheria hiyo ni kuhakikisha vyakula vinavyozalishwa vinakidhi ubora na viwango stahiki ili kuwezesha uzalishaji bora wa mifugo, samaki na mazao yatokanayo na mifugo na samaki. 


Aliendelea kufafanua kuwa pamoja na  Sheria hiyo, Wizara inayo Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) iliyopewa jukumu la kuhakiki na kupima ubora na viwango stahiki vya malighafi zinazotumika kwenye uzalishaji wa vyakula vya mifugo. 


"Hivyo, ninapenda kupitia warsha hii kutoa rai na msisitizo mkubwa kwa wazalishaji wa vyakula vya mifugo wote nchini kuhakikisha wanapeleka sampuli za vyakula wanavyozalisha kwenye maabara ya TVLA ili kuhakiki ubora na viwango kwa kuzingatia matakwa ya sheria hiyo kabla ya kuanza kuwauzia wafugaji wetu au kuvisafirisha nje ya nchi," alisema Waziri Ulega 


Aidha, aliitaka TVLA kuhakikisha inatembelea katika maeneo ya wazalishaji wa malighafi za kutengeneza vyakula vya Mifugo ili wakakague ubora wa malighafi hizo ili kuongeza tija na ufanisi wa kazi katika kulinda usalama wa chakula cha mifugo.


Sambamba na hilo, Waziri Ulega amewahimiza wafugaji wote wa mifugo na samaki na watumiaji wa rasilimali za vyakula vya mifugo, kuhakikisha wanatumia vyakula vinavyozalishwa kwenye viwanda vilivyosajiliwa na kutambuliwa rasmi na Wizara ya Mifugo na Uvuvi. 


 Aliongeza kwa kusema kuwa wafugaji wakitumia vyakula vinavyozalishwa kwenye Viwanda itasaidia kupunguza malalamiko ya udumavu wa mifugo kwa kulishwa vyakula visivyo na ubora na viwango stahiki na hivyo kumwongezea hasara na mara nyingine kusababisha hata vifo kwa mifugo na samaki."Kwa kufuata utaratibu huo, Wizara itaweza kufuatilia malalamiko yanayoweza kutokea kwa vile mfugaji atakuwa ana uhakika wa chanzo cha chakula alichotumia kimetoka kwa mzalishaji gani", alibainisha Waziri Ulega


Kwa upande wake, Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Mhe. Wieber de Boer alisema gharama za uzalishaji wa protini kwa ajili ya chakula cha mifugo ni kubwa hapa nchini hivyo wapo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutafuta njia mbadala ya kutatua changamoto hiyo ili sekta ya mifugo iweze kukua vizuri.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiongea na wadau wa sekta ya mifugo wakati akifungua warsha kuhusu uzalishaji wa protini kwa ajili ya vyakula vya Mifugo na kupunguza ushindani iliyofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 29, 2023.

Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Mhe. Wieber de Boer akitoa neno la utangulizi katika warsha kuhusu uzalishaji wa protini kwa ajili ya vyakula vya Mifugo na kupunguza ushindani iliyofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 29, 2023.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) akiteta jambo na Mkurugenzi wa Viumbe Maji, Dkt. Nazael Madalla katika warsha kuhusu uzalishaji wa protini kwa ajili ya vyakula vya Mifugo na kupunguza ushindani iliyofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 29, 2023.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akimueleza jambo Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Mhe. Wieber de Boer (kushoto) walipokutana mapema leo kando ya   warsha kuhusu uzalishaji wa protini kwa ajili ya vyakula vya Mifugo na kupunguza ushindani iliyofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 29, 2023. Kulia ni Mtendaji Mkuu wa Kituo cha SAGCOT, Bw. Geoffrey Kirenga.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Bw. Rogers Shengoto akiwa katika warsha kuhusu uzalishaji wa protini kwa ajili ya vyakula vya Mifugo na kupunguza ushindani iliyofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 29, 2023.

MIFUGO NA UVUVI YAIBUKA KIDEDEA KAMBA WANAUME

Timu ya Wanaume kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza vema mbio zake za kutwaa ubingwa wa kuvuta kamba mara baada ya kuibuka na ushindi wa mivuto yote miwili dhidi ya timu ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi kwenye  mchezo uliochezwa leo Septemba 29, 2023 kwenye viwanja vya Chuo kikuu cha Mkwawa mkoani Iringa.


Muda mfupi ujao Wizara itatupa karata yake kwa upande wa mpira wa miguu ambapo itamenyana na timu ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera) kwenye uwanja wa chuo kikuu cha Mkwawa.

Timu ya mchezo wa kamba upande wa wanaume kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikimenyana na timu ya Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Lindi leo Septemba 29, 2023 ambapo iliibuka na ushindi wa mivuto yote miwili, Kulia ni mhamasishaji wa timu hiyo Bi. Mary Kamtole akitekeleza wajibu wake.

Hiki ndio Kikosi cha mchezo wa Kamba kwa upande wa wanaume kilichoibuka na ushindi dhidi ya timu ya Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Lindi mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Chuo kikuu cha Mkwawa mkoani Iringa leo Septemba 29,2023 ikiwa ni sehemu ya michuano ya SHIMIWI inayoendelea mkoani hapa.

Pichani ni Kikosi cha timu ya mpira wa Pete kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kinachocheza na timu ya Tume ya Utumishi muda mfupi ujao kwenye uwanja wa Chuo kikuu cha Ruaha leo septemba 29,2023 ikiwa ni muendelezo wa michuano ya SHIMIWI inayofanyika mkoani Iringa.

ULEGA AKIWAHUTUBIA WANAJUMUIYA YA WAISLAMU WA SUNNI KATIKA TUKIO LA KUADHIMISHA SIKUKUU YA KUZALIWA BWANA MTUME MUHAMMAD (S.A.W)

 


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiwahutubia Wanajumuiya ya Waislamu wa Sunni katika tukio la kuadhimisha Sikukuu ya kuzaliwa Bwana Mtume Muhammad (S.A.W) liliyofanyika katika Msikiti wa Sunni jijini Dar es Salaam usiku wa Septemba 28, 2023. Katika tukio hilo, Waziri Ulega ndiye alikuwa mgeni rasmi akimuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (katikati) akiwa  na aliyewahi kuwa Shekhe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum (kulia) wakishuhudia matukio mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea katika sherehe ya maadhimisho ya Sikukuu ya kuzaliwa Bwana Mtume Muhammad (S.A.W) iliyofanyika katika Msikiti wa Sunni jijini Dar es Salaam usiku wa Septemba 28, 2023.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) akifurahia jambo na Mbunge wa Jimbo la Mpendae, Zanzibar, Mhe. Taufiq Turki walipokutana katika tukio la kuadhimisha Sikukuu ya kuzaliwa Bwana Mtume Muhammad (S.A.W) liliyofanyika katika Msikiti wa Sunni jijini Dar es Salaam usiku wa Septemba 28, 2023.

Sehemu ya Viongozi wa Jumuiya ya Waislamu wa Sunni wakiwa katika meza kuu katika tukio la kuadhimisha Sikukuu ya kuzaliwa Bwana Mtume Muhammad (S.A.W) liliyofanyika katika Msikiti wa Sunni jijini Dar es Salaam usiku wa Septemba 28, 2023.

MAADHIMISHO YA SIKU YA KICHAA CHA MBWA DUNIANI KITAIFA YAFANYIKA WILAYANI MPWAPWA

 

Mkurugenzi msaidizi Idara ya Huduma za Afya ya Mifugo Dkt.Stanford Ndibalema Mwakilishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika Madhimisho ya ya siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani  kitaifa Wilayani Mpwapwa akitoa Salamu za Wizara ambapo ameseama maadhimisho ya udhibiti wa Kichaa cha Mbwa nchini hufanyika kila mwaka kwa kushiikiana na Wizara ya Afya na wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kutoa elimu kwa jamii na wadau wa Mbwa na paka umuhimu wa kuchanja Mbwa ,(28.09.2023).

Wadau wa Mbwa na paka walioleta mbwa wao kwa ajili ya kuchanjwa wakimsikiliza mgeni rasmi  hayupo pichani akisoma hatuba ya maadhimisho ya siku ya  kichaa cha Mbwa duniani Wilayani Mpwapwa .(28.09.2023)

Mkurugenzi toka Wizara ya Afya Dkt.Rogati Kishimba akitoa salam za Wizara ya Afya kuhusu siku ya kichaa cha Mbwa duniani katika Madhimisho ya siku hiyo yaliyofanyika Wilayani Mpwapwa  leo ambapo amesema gharama za kutibu kichaa cha mbwa ni kubwa kuliko udhibi wa Ugonjwa huo hivyo jamii ihamasishwe kudhibiti ugonjwa huo.(28.09.2023).

Mgeni rasmi wa maadhimisho ya siku ya kichaa cha Mbwa Arb ogust Waryoba akitoa kadi kwa mbwa ambaye tayari amechanjwa kwa mwenye mbwa baada ya mbwa wake  kuchanjwa leo kwenye maadhimisho ya siku ya kichaa cha mbwa kitaifa Halmashauri ya Mpwapwa (28.09.2023)

Dkt. Wa Mifugo toka Halmashauri ya Mpwapwa Dkt.Emmanuel John akitoa chanjo kwa mmoja ya wafugaji w a Mbwa walioleta Mbwa wao kuchanjwa leo kwenye maadhimisho ya siku ya kichaa Mbwa kitaifa Wilayani Mpwapwa,(28.09.2023).

WAZIRI ULEGA AFANYA MAZUNGUMZO NA WATAALAM KUTOKA BENKI YA MAENDELEO YA AFRICA (AfDB)

 


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (katika) akiongea na timu ya Wataalam kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) (hawapo pichani) alipokutana nao mapema leo Septemba 27, 2023 jijini Dodoma kwa lengo la kufanya tathmini ya awali ya mradi wa Jenga Kesho Iliyobora (BBT) ambao Benki hiyo wanataka kuunga mkono. Kulia ni Katibu Mkuu, Prof. Riziki Shemdoe na kushoto ni Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Daniel Mushi. Mradi unatarajiwa kuanza Utekelezaji mapema mwezi Februari, 2024.


Kiongozi wa Mradi kutoka Taasisi ya Mabadiliko ya Kilimo Afrika (AATI), Bw. Marin VanDamme (kulia) akimuonesha jambo Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega wakati wa kikao kilichofanyika ofisini kwa Waziri huyo jijini Dodoma mapema leo Septemba 27, 2023. 

Lengo la kufika ofisini kwa Mhe. Waziri lilikuwa ni kuwasilisha hatua ya awali ya maandalizi ya Mpango Mkuu wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kupata maoni ya Mhe. Waziri kwa hatua iliyofikiwa kabla ya kuendelea hatua inayofuata.


Sehemu ya timu ya Wataalam kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na baadhi ya Wataalam kutoka Wizarani (pichani) wakifuatilia majadiliano wakati wa kikao baina yao na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega kilichofanyika leo Septemba 27, 2023 jijini Dodoma kwa lengo la kufanya tathmini ya awali ya mradi wa Jenga Kesho Iliyobora (BBT) ambao Benki hiyo wanataka kuunga mkono.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akieleza jambo wakati wa kikao baina yake na timu ya Wataalam kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) (hawapo pichani) alipokutana nao mapema leo Septemba 27, 2023 jijini Dodoma.

PROF. SHEMDOE AWAAGA WAWAKILISHI MICHUANO YA SHIMIWI

◾Waahidi Makubwa, Kuelekea Iringa kesho 


Katibu Mkuu Wizara ya Mfugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amewaaga wawakilishi wa wizara hiyo kwenye  michuano ya SHIMIWI ambapo amewataka wawakilishi hao kurejea na ushindi wa nafasi ya kwanza kwenye kila mchezo watakaoshiriki.


Katika tukio hilo lililofanyika Septemba 27, 2023 kwenye Ofisi ndogo za Wizara hiyo zilizopo jengo la NBC jijini Dodoma, Prof. Shemdoe amewataka wachezaji wote waliochaguliwa kushiriki kwenye michuano hiyo kujituma na kucheza kwa ushindani wakati wote wa michuano hiyo.


“Mimi mara zote nipo kwenye timu ya ushindi kwa hiyo hata huku naamini nimekuja kwenye timu ya ushindi na nina Imani sana na nyinyi kwa sababu ninafahamu kuwa kwenye mashindano ya mwaka huu tutakuwa na vikombe vingi zaidi ya vile tulivyoshinda mwaka jana” Ameongeza Prof. Shemdoe.


Akisisitiza suala la kudumisha  nidhamu , Prof Shemdoe amewataka wachezaji hao kutambua kuwa wao ni watumishi wa umma hivyo wanapaswa kufuata taratibu zote zinazowaongoza kulingana na nafasi zao wakati wote wakiwa kwenye mashindano hayo.


“Wale dada zangu ambao mmefanya vizuri msimu uliopita niwaombe mkafanye vizuri zaidi mwaka huu na ninajua tuna washiriki wengi wa mchezo wa Kamba,nina Imani safari hii tutashika nafasi ya kwanza inshaallah” Amebainisha Prof. Shemdoe.


Awali akitoa taarifa fupi ya maandalizi ya timu hizo yalivyokuwa Mwenyekiti wa SHIMIWI kutoka Wizarani hapo Bw. Ally Suru aliuhakikishia uongozi wa Wizara kufanya vizuri kwenye mashindano hayo kutokana na maandalizi mazuri waliyoyafanya.


"Naomba nitumie fursa hii kwa niaba ya viongozi wenzangu, makocha na wachezaji kuwashukuru Viongozi wa Wizara kwa ushirikiano mkubwa ambao wametupatia tangu tulipoanza maandalizi yetu na tunaomba muendelee kutuonesha ushirikiano huo ili tufanye vizuri zaidi kwenye mashindano huko Iringa" Aliongeza Bw. Suru.


Aidha Bw. Suru amewapongeza viongozi hao kwa uamuzi  wa kupeleka washiriki wa michezo yote inayoshindaniwa kwenye michuano hiyo jambo ambalo limekuwa ni kinyume kwa Taasisi nyingi kutokana na changamoto ya ufinyu wa bajeti.


Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wanamichezo wenzake, mwakilishi wa wachezaji hao Dkt. Aurelia Bundala amemuahidi Prof. Shemdoe kutekeleza yote aliyowaasa ambapo amemhakikishia kuwa wataibuka vinara kwenye kila mchezo watakaoshiriki.


Jumla ya wanamichezo 93 kutoka wanaoshiriki michezo ya Mpira wa miguu, mpira wa pete, kuvuta Kamba, mbio za baiskeli, riadha na kurusha vishale kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wataondoka Septemba 28, 2023 kuelekea  mkoani Iringa inakotarajiwa kufanyika Michuano ya SHIMIWI kuanzia Septemba 29, 2023.KONGAMANO LA WADAU WA MAZIWA LAFANYIKA MKOANI MWANZA

 


Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania Dkt. George Msalya akitoa neno la utangulizi kwenye Kongamano la Wadau wa Maziwa mkoa wa Mwanza lilifanyika Septemba 26, 2023 katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambapo ameelezea ukuaji wa Sekta ya Maziwa kwa ujumla hivyo amewataka wananchi wa Mwanza kuchangamkia fursa zilizopo kwenye Ufugaji hasa wa Ng'ombe wa Maziwa.


Mwakilishi wa Shirika la Heifer International Bw. Ndisha Joseph akijibu moja ya hoja iliyoibuka kwenye Kongamano la Wadau wa Maziwa lililofanyika Septemba 26, 2023 jijini Mwanza ambapo mmoja wa wajumbe alitaka kujua namna shirika hilo linavyoweza kuwasaidia wafugaji wadogo wadogo wa ng'ombe wa maziwa kupata elimu ili kufahamu faida ya kuwa katika vikundi vya Ushirika

Sehemu ya Washiriki wa Kongamano la Wadau wa Maziwa lililofanyika Septemba 26, 2023 Mkoani Mwanza wakifuatilia kwa makini mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa kwenye Kongamano hilo ambapo sehemu kubwa ya walioalikwa ni Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu wa shule za Jiji la Mwanza, pamoja na mambo Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania Dkt. George Msalya amewapitisha kwa ufupi Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni uliozinduliwa hivi karibuni na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega wakati wa Maadhimisho ya Wiki Ya Maziwa Juni 1, 2023 mkoani Tabora

KIKAO KAZI

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega(kulia) akiongea na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti katika kikao kazi kilichofanyika ofisini kwake jijini Dodoma mapema leo Septemba 26, 2023. Katika kikao hicho, pamoja na mambo mengine walijadiliana kuhusu dira na muelekeo wa utekelezaji wa majukumu na shughuli mbalimbali za kila siku za Wizara katika kuwahudumia wananchi na kutimiza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (katikati) akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti katika kikao kazi kilichofanyika ofisini kwake jijini Dodoma mapema leo Septemba 26, 2023. Katika kikao hicho pamoja na mambo mengine walijadiliana kuhusu dira na muelekeo wa utekelezaji wa majukumu na shughuli mbalimbali za kila siku za Wizara katika kuwahudumia wananchi na kutimiza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Wengine katika picha kutoka kulia ni Naibu Katibu Mkuu (Mifugo), Dkt. Daniel Mushi na wa pili kutoka kulia ni Naibu Katibu Mkuu (Uvuvi), Bi. Agnes Meena.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kulia) akimuonesha jambo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti wakati wa kikao kazi kilichofanyika ofisini kwake jijini Dodoma mapema leo Septemba 26, 2023.

BI. MEENA AFUNGUA KIKAO KILICHOJADILI MRADI WA TASFAM

 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Kisaka Meena, akifungua kikao cha Menejimenti cha kupitia nyaraka muhimu za Mradi wa TASFAM ulioudhuriwa na wakuu wa Idara, Vitengo na wajumbe wengine muda mfupi baada ya kufika kwenye ukumbi wa wizara Septemba 25, 2023.

Sehemu ya washiriki wa kikao cha Menejimenti cha kupitia nyaraka muhimu za Mradi wa TASFAM wakimsikiliza kwa makini Naibu Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi Bi. Agness Meena (hayupo pichani) wakati akifungua kikao hicho kwenye ukumbi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi mtumba jijini Dodoma  Septemba 25,2023.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Kisaka Meena (wa sita kutoka kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na Menejimenti ya Sekta ya Uvuvi iliyokutana kujadili nyaraka muhimu za Mradi wa TASFAM ulioudhuriwa na wakuu wa Idara, vitengo na wajumbe wengine katika ukumbi wa Wizara Septemba 25, 2023.

BOTI 4 ZENYE THAMANI YA 200M ZAKABIDHIWA KWA BMU's NKASI

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe leo tarehe 25 Sept 2023 amezindua na kukabidhi boti nne za doria zenye thamani ya 200M zilizotolewa msaada na taasisi ya The Nature Conservancy (TNC) kwa BMU's tisa zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa.


Akikabidhi boti hizo Prof.Shemdoe amesema kuwa boti hizo zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa, boti hizo ni kwaajili ya matumizi ya doria tu zisionekane tena  zinafanya kazi kinyume na malengo yaliyokusudiwa.


"Boti hizi nazizindua leo na kuwakabidhi, naomba sana zikatumike kwa ajili ya doria,zisionekane tena zinavua samaki huko ziwani, BMU's mnatakiwa kuwa waaminifu,mzitumie hizi boti kwa maslahi ya Jamii nzima inayowazunguka hapa". Alisema Prof.Shemdoe.


Aidha, Vijiji nufaika na Boti hizo ni pamoja na Kalungu, Mkinga, Kilando na Itete. Pia, Katibu Mkuu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dr. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali wa Wavuvi kote nchini, kwani katika Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa Rais ametoa jumla ya Boti 15 kwa ajili ya kukopesha vikundi vya Wavuvi kwa mkopo wa usiokuwa na riba.


Katika hatua nyingine, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Taasisi ya The Nature Conservancy Bw. Peter Limbu amemweleza Katibu Mkuu kuwa mradi wa Uhifadhi wa Ziwa Tanganyika ni moja ya miradi Mingi inayotekelezwa nchini Tanzania kupitia shirika la kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (TNC).


Aidha, Limbu amesema kuwa katika Wilaya ya Nkasi Taasisi ya TNC inashirikiana na Shirika la "Sustain Lake Tanganyika" pamoja na jamii chini ya uongozi thabiti wa Wilaya ya Nkasi katika kulinda, Kutunza na kuendeleza rasilimali za ziwa Tanganyika ili ziweze kunufaisha jamii kwa chakula, biashara na maendeleo katika kizazi hiki na kijacho.


Awali Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mhe. Peter Lijualikali amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali wananchi wa Wilaya ya Nkasi kwa kutoa Boti 15 kwa ajili ya kuwakopesha  Vikundi vya Wavuvi Wilayani Nkasi kwa mkopo usiokuwa na riba.


Vilevile Mhe.Lijualikali ameishukuru Taasisi ya The Nature Conservancy kwa kuwa mstali wa mbele wa kulinda na kuziendeleza rasilimali za Uvuvi katika ziwa Tan ganyika.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe  Pamoja na Mhe.Lijualikali, Mkuu wa Wilaya ya Nkasi,  wakikata utepe kuashiria kuzinduliwa kwa Boti 4 za doria ili ziweze kukabidhiwa kwa BMUs Katika Halmashauri ya Wilaya Nkasi.Wengine katika picha ni maafisa kutoka mkoa wa.Rukwa,  Halimshauri ya Wilaya ya Nkasi pamoja na wananchi.

Boti zilizokabidhiwa kwa  BMU's Katika Kijiji cha Kalungu Wilayani Nkasi kwa ajili ya Doria.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof.Riziki Shemdoe (wa tatu kutoka kushoto) akimsikiliza Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Bw. Gerald Kusaya (Katikati) akiongea mara baada ya kufika ofisini kwake kusaini Kitabu cha Wageni.Wengine katika Picha ni timu ya Wataalam kutoka Mkoa wa Rukwa.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe akisalimia na baadhi ya wanakijiji cha Kalungu mara baada ya kuwasili kijijini hapo kwa ajili kukabidhi boti za doria kwa BMUs.Kulia kwake ni Mhe.Peter Lijualikali,Mkuu wa Wilaya ya Nkasi.


ELIMU YA KUENDESHA KITUO CHA HUDUMA KWA WATEJA YATOLEWA

 

Bw. Imani Mwakalile kutoka Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), akitoa elimu ya namna ya kuendesha kituo cha huduma kwa wateja ambacho kinatarajia kuanzishwa kwa lengo la kuwahudumia wadau wa sekta ya Mifugo na Uvuvi, kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa NBC, Dodoma, 21.09.2023.

Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani Dkt. Angelo Mwilawa(aliyesimama) akifungua kikao cha kujadili namna ya kuendesha kituo cha huduma kwa wateja(Call Centre Service), ambacho kinatarajiwa kuanzishwa Wizarani, kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa NBC, Dodoma, 21.09.2023.

Wajumbe wa kikao cha kujadili namna ya kuendesha kituo cha huduma kwa wateja kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi,  wakimsikiliza mwezeshaji Bw.Imani Mwakalile, kutoka Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL- aliyesimama) katika ukumbi wa NBC, Dodoma 21.09.2023.

Mwakilishi kutoka Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) (katikati) Bw. Imani Mwakalile akiwa kwenye picha ya pamoja na wawakilishi kutoka wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambao wameshiriki kwenye kikao cha kujadili namna ya kuendesha kituo cha huduma kwa wateja (Call Centre Service) ambacho kinatarajia kuanzishwa kwa lengo la kuwahudumia wadau wa sekta ya uvuvi na Mifugo,  katika ukumbi wa NBC, Dodoma, 21.09.2023.

​RAIS, DKT. SAMIA AANDIKA HISTORIA MPYA SEKTA YA UVUVI

Leo Septemba 19, 2023, ni siku ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameandika historia mpya katika sekta ya uvuvi baada ya kuweka jiwe la msingi kuashiria uzinduzi wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko ambayo haijawahi kuwepo tangu nchi ya Tanzania ipate uhuru.


Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka  jiwe hilo la msingi la ujenzi wa bandari ya uvuvi ya Kilwa katika tukio lililofanyika Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika Mikoa ya Mtwara na Lindi.


Kukamilika kwa bandari hiyo kutawezesha meli za uvuvi zinazovua katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari ya Tanzania na Bahari Kuu kutia nanga na kushusha samaki wanaolengwa na wale wasiolengwa kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi. 


Pia, uwepo wa bandari ya uvuvi utachochea uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata samaki na miundombinu ya uhifadhi wa mazao ya uvuvi. Hivyo, uwekezaji huu, unaenda kuimarisha biashara ya mazao ya uvuvi kwenda nje ya nchi kutoka tani 40,721.53 zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 249.54 hadi tani   52,937.99 na kuchangia takriban asilimia 10 katika pato la Taifa ifikapo mwaka 2036.


Aidha, Bandari hiyo inatarajiwa kutengeneza ajira kwa watanzania takriban 30,000 huku katika hatua za awali za ujenzi, jumla ya ajira za muda mfupi 278 zimetolewa ambapo kati ya hizo ajira 106 sawa na asilimia 38 zimetolewa kwa wakazi wa wilaya za Mkoa wa Lindi.


Pamoja na uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa bandari ya Uvuvi, Rais Samia pia amegawa boti 34 kati ya boti 160 ambazo zinatolewa nchi nzima. Boti hizi kwa ukanda wa bahari ya Hindi zipo 92 zikihusisha wavuvi na wakulima wa mwani.


"Serikali imejipanga kuhakikisha mazingira ya wavuvi na wakuzaji viumbe maji yanaimarika ndio maana leo nimegawa boti za kisasa zikiwa na kifaa cha kuonyesha upatikanaji wa samaki na uhifadhi wa samaki", alisema Mhe. Dkt. Samia


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amemshukuru Rais Samia kwa namna ambavyo ameiwezesha sekta ya Mifugo na Uvuvi kwa kuiongezea bajeti.


Aidha, amemshukuru Rais Samia kwa kuamua kutekeleza ujenzi wa mradi huo ambao utakuwa na tija kwa wananchi wa Kilwa na Tanzania kwa ujumla.


Ulega amesema ujenzi huo wa bandari ambao unagharimu zaidi ya bilioni 266 unakwenda kujibu changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili wananchi, lakini pia kuleta fursa za ajira zisizopungua 30,000. Ujenzi huu utawezesha ujenzi wa Viwanda vya kuchakata samaki, karakana ya kutengeneza meli, sehemu ya kuhifadhi samaki na uzalishaji wa barafu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (kulia) akizindua rasmi uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa katika tukio lililofanyika Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi leo Septemba 19, 2023.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (kulia) akikata utepe kuashiria ugawaji wa maboti kwa wavuvi wilayani Kilwa wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa katika tukio lililofanyika Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi leo Septemba 19, 2023.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiongea na Wananchi wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa bandari ya Uvuvi ya Kilwa iliyofanyika Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi leo Septemba 19, 2023.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega  akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuongea na Wananchi waliojitokeza katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa bandari ya uvuvi ya Kilwa iliyofanyika Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi leo Septemba 19, 2023.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akitoa maelezo mafupi kuhusu ujenzi wa bandari ya Uvuvi ya Kilwa kwa  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan muda mfupi kabla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa bandari hiyo Wilayani Kilwa, mkoani Lindi Septemba 19, 2023.

Katibu Mkuu, Prof. Riziki Shemdoe akitoa neno la utambulisho wa Viongozi wa Wizara wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa bandari ya uvuvi inayojengwa Wilayani Kilwa, mkoani Lindi, tukio hilo limefanyika leo  Septemba 19, 2023.

Sehemu ya Wananchi waliojitokeza katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa iliyofanyika Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi leo Septemba 19, 2023.

HAFLA YA UWEKEAJI WA JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA BANDARI YA UVUVI NA UGAWAJI WA BOTI ZA UVUVI

 


BBT KUTATUA CHANGAMOTO YA BEI YA NYAMA MTWARA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa wizara yake imejipanga kutumia Shamba la Mifugo la Nangaramo lililopo Mkoani Mtwara kuanzisha programu ya BBT ili kuwapa fursa vijana wa Mikoa ya Kusini kunenepesha mifugo na kuuza nyama kwa bei nafuu tofauti na ilivyo sasa mkoani Mtwara bei ya kilo moja ya nyama inafika mpaka Shilingi Elfu Kumi (10000).


Waziri Ulega aliyasema hayo katika mkutano wa hadhara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Wananchi wa Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara leo Septemba 17, 2023.


Alisema pamoja na uwepo wa mifugo mingi katika Mkoa huo na Mikoa mingine ya jirani lakini bado upatikanaji wa nyama kwa bei nafuu umekuwa changamoto na ndio maana wamejipanga kuanzisha programu ya BBT itakayowawezesha vijana kunenepesha mifugo na kuuza nyama kwa bei ambayo wananchi walio wengi wataimudu.


Aliongeza kwa kusema kuwa kupitia programu hiyo vijana pia wataweza kunufaika na kuuza mifugo na nyama kwa nchi ya Comoro ambayo kwa kiasi kikubwa wanategemea biashara Mifugo na nyama kutoka nchini Tanzania.


Halikadhalika alisema kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi imejipanga pia kutumia maeneo yote yaliyopo katika mpango wa matumizi bora ya ardhi kuweka miundombinu ya kisasa ya mifugo ili kuwawezesha wafugaji kuzalisha kwa tija.


Aidha, Waziri Ulega alimshukuru Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake juu ya migogoro ya wakulima na wafugaji iliyopo katika Mikoa ya Kusini na kumuahidi  kwamba watasimamia vyema maelekezo yake huku akiongeza kwa kuwataka wafugaji kuhakikisha wanafanya ufugaji wao kwa kuzingatia Sheria za nchi na atakayeendelea kukiuka hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kulia) akifurahia jambo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Jerry Silaa alipokutana nae katika tukio la uzinduzi wa  Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini iliyozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Septemba 15, 2023.

Sehemu ya Wananchi mkoani Mtwara wakiwa wamejitokeza kumlaki Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa tukio la uzinduzi wa Barabara ya Mtwara – Mnivata (Kilometa 50) leo  Septemba 15, 2023.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Viongozi mbalimbali muda mfupi baada ya  kuwasili kwa ajili ya tukio la kukagua na kuona shughuli za uboreshaji wa Bandari ya Mtwara leo Septemba 15, 2023. Wa tatu kutoka kulia anayesalimiana nae ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na Viongozi wengine wakati wa tukio la kukata utepe kuashiria uzinduzi wa  Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini iliyozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Septemba 15, 2023. Wa tatu kutoka kulia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) akijadiliana jambo na Mbunge wa Mtwara Mjini, Mhe. Hassan Mtenga alipokutana nae katika Mkutano wa hadhara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan uliofanyika kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mkoani Mtwara Septemba 15, 2023.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) akiongea na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi  Taifa, Cde. Mohamed Kawaida alipokutana nae katika Mkutano wa hadhara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan uliofanyika kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mkoani Mtwara Septemba 15, 2023.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiongea na Wananchi wa Mkoa wa Mtwara katika Mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mkoani Mtwara Septemba 15, 2023. Wa kwanza kulia waliokaa ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega.