Nav bar

Jumamosi, 27 Mei 2023

VITUO ATAMIZI VYA MIFUGO VITATUE CHANGAMOTO YA AJIRA KWA VIJANA- Dkt. Mhina

Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) imetakiwa  kuwasimamia vizuri vijana 240 wanaoendelea kupatiwa mafunzo ya unenepeshaji mifugo  katika vituo atamizi 8 chini ya LITA ikiwa ni mpango wa Serikali kusaidia vijana hao kujiajiri na  kujikwamua kiuchumi.

Wito huo umetolewa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu ambaye ni  Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina wakati wa kikao cha baraza la wafanyakazi wa LITA kilichofanyika mkoani Arusha Mei 26, 2023.

Dkt. Mhina alisema Serikali imeanza kutekeleza mradi huo katika mwaka huu wa fedha baada ya kubaini wataalamu wanaotoka katika vyuo hivyo wanayo nafasi ya kupatiwa ujuzi zaidi ya kuzalisha kupitia vituo atamizi ili watakaporejea mitaani waweze kuwa na uwezo wa kuwekeza zaidi.

“Tunatengeneza wataalam ambao ni wawekezaji wao wenyewe watakapoweza kuzalisha ndivyo ambavyo tutaweza kuzalisha malighafi zaidi kwenye viwanda vyetu, kwahiyo hatutarajii wakitoka hapa wakategemee kuajiriwa ndio maana tunawaweka kwenye vituo atamizi ili wafanye kwa vitendo na kufanya kibiashara zaidi” amesema

Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene alifafanua kuwa mradi huo kwa kuanzia utatekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja ambapo utagawanywa kwa awamu 4 ambapo vijana hao watahudumia mifugo kwa kunenepesha ndani ya miezi 3.

Alisema katika kila kituo kuna  vijana wasiopungua 30 ambapo kila mmoja anahudumia ng’ombe 10 kwa kuwanenepesha kwa kipindi cha miezi mitatu na kufanya wahudumia ngombe 40 kwa mwaka mzima

“ kila kijana kwa mzunguko moja amepewa ng’ombe 10 wa kunenepesha kwa hiyo kwa mwaka mzima atanenepesha ngombe 40  na tunategemea faida itakayotokana na hao Ng’ombe watakao uzwa mnadani ni mtaji kwa kijana kwa ajili ya kwenda kuanzisha mradi wake baada ya kumaliza mwaka mmoja” amesema

Aliongeza kuwa mradi huo utakuwa fursa nzuri kwa vijana kufuga kibiashara kwa sababu licha ya kuanza kutekeleza mradi huo mwezi Aprili mwaka huu tayari wameanza kupokea oda ya kuhitaji ng’ombe hao.


Mwakilishi wa katibu Mkuu, ambae ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi,  Dkt. Charles Mhina akiongea wakati wa kufungua kikao cha baraza la wafanyakazi wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) kilichofanyika Tengeru LITA mkoani Arusha, Mei 26,2023 

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene (kulia) akieleza namna wakala hiyo inavyotekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa vitendo ili kuwaandaa vijana kujiajiri, kwa Mwakilishi wa Katibu Mkuu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina  wakati alipoenda kufungua kikao cha baraza la wafanyakazi LITA kilichofanyika Tengeru mkoani Arusha Mei 26,2023. 


Mwanafunzi anayejikita kwenye eneo la Afya ya Mnyama na Uzalishaji Bw. Julius Mmbando akionyesha namna taarifa /majibu ya vipimo vya magonjwa mbalimbali ya mnyama yanavyotoka kwenye mashine ya kupimia magonjwa hayo ya mifugo kwa Mwakilishi wa Katibu Mkuu Dkt. Charles Mhina alifika chuoni hapo Tengeru Mkoani Arusha Mei 26,2023. 

 

Ijumaa, 19 Mei 2023

UVUNAJI MALISHO NARCO WASHIKA KASI

 


WIKI YA MAZIWA 2023

 




SAUTI YETU WIKI HII

 


TUTAJENGA VITUO ATAMIZI NCHI NZIMA-SILINDE

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde amesema kuwa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaweka programu ya atamizi katika mikoa yote nchini kwa mwaka ujao wa fedha.

Mhe. Silinde ameyasema hayo Mei 18, 2023 wakati akitoa salamu za Wizara yake kwenye mwendelezo wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango aliyoifanya eneo la Ngaramtoni mkoani Arusha.

"Mhe. Makamu wa Rais, sasa hv wewe pamoja na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mmejikita katika kubadilisha maisha ya Watanzania kupitia sekta za uzalishaji na mmefanya hivyo kwenye Wizara za Kilimo na Mifugo na Uvuvi na kwa upande wa Wizara yetu mnataka Tanzania ibadilike kwenda kwenye ufugaji wa kisasa" Amesema Mhe. Silinde.

Mhe. Silinde ameongeza kuwa moja ya njia ambazo Serikali inatarajia kutekeleza azma hiyo ni kupitia programu ya unenepeshaji wa Mifugo ambapo imetoa fedha za kujenga vituo Atamizi nchi nzima.

"Lengo ni tuongeze tija, tuongeze na kuimarisha soko la ndani na nje ya nchi ili pato la Taifa linalotokana na sekta za Mifugo na Uvuvi lionekane kama ilivyo kwa nchi ya Namibia ambao wana mifugo milioni 4 tu lakini inachangia zaidi ya asilimia 54 kwenye pato la Taifa" Amesisitiza Mhe. Silinde.

Aidha Mhe. Silinde amesema kuwa kwa upande wa sekta ya Uvuvi serikali inakusudia kubadilisha maisha ya wavuvi nchini kwa kuongeza tija kwenye aina ya mavuvi yanayofanyika kwenye vyanzo mbalimbali vya asili na upande wa ufugaji wa samaki.

"Katika kufanikisha hilo, Serikali imetoa mkopo wa boti 160 usio na riba kwa wavuvi ili waweze kutekeleza shughuli zao kwa ufanisi" Amehitimisha Mhe. Silinde.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde ni miongoni mwa mawaziri wa kisekta waliopo kwenye ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayoifanya katika mikoa ya Arusha na Manyara kwa lengo la kukagua na kutatua changamoto mbalimbali za wananchi wa mikoa hiyo.



Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde akiwasalimia wananchi wa Loliondo muda mfupi baada ya kuwasili wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango (hayupo pichani) ambapo alizungumza na wafugaji wa eneo hilo Mei 17, 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango (kushoto) akisalimiana na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde muda mfupi baada ya kufika kwenye Uwanja wa ndege wa mkoa wa Arusha Mei 17,2023 ambako pamoja na mambo mengine alitembelea na kukagua shughuli za ufugaji mkoani humo na Manyara.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwa kwenye mavazi ya kiongozi wa kabila la wasonjo mara baada ya kuvikwa nafasi hiyo na wafugaji waliopo eneo hilo wakati wa Ziara yake aliyoifanya kijiji cha Longido Mei 17, 2023.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (katikati) akijibu hoja mbalimbali  za wafugaji wa kijiji cha Loliondo wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango (hayupo pichani) iliyofanyika kijijini hapo Meo 17, 2023.

WATAALAM WA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI WAMTEMBELEA MFUGAJI BW. JEREMIAH TEMU JIJINI DODOMA


 Mfugaji Bw. Jeremiah Temu akionyesha namna ya kukata malisho kwa kutumia mashine nyumbani kwake Mpamaa jijini Dodoma kwa wadau na wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi walipoenda kujifunza, Mei 17,2023

Mkurugenzi Msaidizi wa Maeneo ya Malisho kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Gabriel Bura (kulia) akisambaza malisho  ambayo yamekatwa kwa kutumia mashine kwenye eneo lililoandaliwa  kwa ajili ya kutengeneza saileji nyumbani kwa mfugaji  Bw. Jeremiah Temu Mpamaa jijini Dodoma,  Mei 17,2023

Sehemu ya vijana wakishindilia malisho yanayoandaliwa kwa ajili ya kutengeneza saileji kwa kutumia pipa la maji kwenye eneo lililoandaliwa ikiwa ni hatua moja wapo ya maandalizi nyumbani kwa mfugaji Mpamaa jijini Dodoma,  Mei 17,2023.

Mkurugenzi Msaidizi wa Maeneo ya Malisho kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Gabriel Bura  (kushoto) akionyesha sehemu malisho yanapoanzia kukatwa na umuhimu wake kwa watendaji kutoka Wizara hiyo wakati walipotembelea shamba la mfugaji Bw. Jeremiah Temu lililopo Mpamaa jijini Dodoma Mei 17,2023

Mfugaji Bw. Jeremiah Temu (wa nne kutoka kulia) akitoa maelezo kwa wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi walipomtembelea nyumbani kwake kwa lengo la kujifunza namna ya kupanda malisho na kutengeneza saileji kwa ajili ya mifugo Mpamaa jijini Dodoma Mei 17,2023

Sehemu ya malisho aina ya junkao yaliyopandwa nyumbani kwa mfugaji Bw.  Jeremiah Temu  Mei 17,2023 Mpamaa jijini Dodoma.

Mfugaji Bw. Jeremia Temu (kushoto) akitoa maelezo ya maana ya saileji na faida yake kwa mifugo, kwa wadau na wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi  waliomtembelea nyumbani kwake Mpamaa jijini Dodoma kwa lengo la kujifunza, Mei 17,2023


WIKI YA MAZIWA 2023

 




KIKAO CHA USHIRIKIANO BAINA YA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA KIMEFANYIKA WILAYANI CHAMWINO MKOANI DODOMA

 

Mkuu wa Tawi la Utawala Jeshi la Kujenga Taifa, Brigedia Generali Hassan Mabena akiongea wakati wa kufungua kikao cha ushirikiano wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Jeshi la Kujenga Taifa kilichofanyika kwenye ukumbi wa Jeshi hilo Wilayani Chamwino jijini Dodoma,  Mei 16,2023.


Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Angello Mwilawa akichangia hoja wakati wa kikao kifupi cha ushirikiano wa Wizara hiyo na jeshi la kujenga Taifa chanye lengo la kuwainua vijana kiuchumi kupitia sekta ya mifugo kilichofanyika kwenye Wilaya ya Chamwino jijini Dodoma Mei 16,2023.


Mkurugenzi wa Kilimo, mifugo na Uvuvi kutoka Jeshi la Kujenga Taifa,  Kanali Peter Lushika akieleza  namna wanavyowajenga vijana wao kuweza kujikwamua kiuchumi na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo wakati wa kikao kifupi kilichofanyika kwenye ukumbi wa jeshi hilo Chamwino jijini Dodoma,  Mei 16,2023


Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Daudi Mayeji akiongea wakati wa kufunga kikao cha ushirikiano wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Jeshi la kujenga Taifa chenye lengo la kuwainua vijana kiuchumi kupitia  Sekta ya Mifugo kilichofanyika Chamwino Jijini Dodoma, Mei 16,2023.



Mkuu wa Tawi la Utawala Jeshi la Kujenga Taifa Brigedia  Generali Hassan Mabena (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na watendaji kutoka jeshi la kujenga Taifa mara baada ya kikao kifupi cha ushirikiano wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Jeshi na Kujenga Taifa katika suala zima la kuwainua vijana kupitia  Sekta ya Mifugo, kilichofanyika Chamwino jijini Dodoma  Mei 16,2023.

WIKI YA MAZIWA 2023

 




SAUTI YETU WIKI HII

 


UIMARISHWAJI WA TVLA UNAENDA KUSAIDIA KUIMARIKA KWA MIFUGO NCHINI KUWEZA KUPATA MASOKO NJE YA NCHI-PROF.SHEMDOE

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe amefanya ziara kutembelea Maabara za Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kufahamu na kujionea kazi ambazo zinafanywa na Wakala hiyo.

 

Akizungumza wakati wa Ziara yake leo Mei 12, 2023 Jijini Dar es Salaam, Prof. Shemdoe amesema uimarishwaji wa TVLA unaenda kusaidia kuimarika kwa mifugo nchini na kuweza kupata masoko mengi nje ya nchi.

 

Amesema TVLA wamekuwa wakifanya maandalizi ya utengenezaji wa chanjo mbalimbali za mifugo ambazo zinasaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia maambukizi ya magonjwa mbalimbali kwenye mifugo.

 

"Miaka michache iliyopita tulikuwa tunapeleka nyama nje ya nchi tani elfu moja, lakini sasa mwaka huu ambao tunamalizia mwaka wa fedha tayari tumeshavuka tani elfu 12, kwahiyo tunapoelekea ni mahala pazuri". Amesema Prof. Shemdoe.

 

Aidha amewapongeza TVLA kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya ikiwemo kutambua magonjwa ya mifugo ambayo yapo nchini ili kuweza kuyazuia na kuyatokomeza.

 

Pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha ambazo zimesaidia kuimarisha TVLA na kuweza kufanya kazi kwa weledi mkubwa katika kuhakikisha wanadhibiti magonjwa ya mifugo.

 

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi amesema kuwa wanategemea kwa kiasi kikubwa ziara ya Katibu Mkuu kuzaa matunda kwani ameona ni kwa namna gani TVLA wamekuwa wakijtahidi kuhakikisha inafanya vizuri katika kutekeleza majukumu yake.

 


 Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (kushoto) akipata ufafanuzi kuhusiana na shughuli za kiuchunguzi wa magonjwa yanayoambukizwa na Bioteknolojia kutoka kwa Meneja wa kituo cha Uchunguzi wa Magonjwa yanayoambukiza na Bioteknolojia (CIDB) Dkt Jelly Senyagwa Chang'a aliptembelea Maabara hiyo Mei 12, 2023 Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujionea shughuli mbalimbali za Kimaabara.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (kushoto) akipata maelezo kuhusiana na namna Maabara ya utambuzi wa magonjwa ya virusi vya mlipuko (CIDB) inavyofanya kazi kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi alipombelea Ofisi ya TVLA Mei 12, 2023 Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kufahamu kazi zinazofanywa na TVLA pamoja na kujionea shughuli mbalimbali za Kimaabara.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (wa pili Kulia) akimsikiliza kwa umakini Meneja wa Maabara Kuu ya Mifugo (CVL) Dkt. Geofrey Omarch alipokuwa akitoa maelezo jinsi Maabara kuu ya Mifugo kitengo cha upimaji wa Ubora wa Vyakula vya Mifugo inavyofanya kazi alipombelea Ofisi ya TVLA Mei 12, 2023 Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kufahamu kazi zinazofanywa na TVLA pamoja na kujionea shughuli mbalimbali za Kimaabara.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (kulia) akipata maelezo wa namna ya upimaji wa vyakula vya Mifugo kutoka kwa Mkuu wa Idara ya Maabara ya Vyakula vya Mifugo wa TVLA Dkt. Scholastica Dotto alipombelea Ofisi ya TVLA Mei 12, 2023 Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kufahamu kazi zinazofanywa na TVLA pamoja na kujionea shughuli mbalimbali za Kimaabara.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (kulia) akipata maelezo kuhusiana na namna Kitengo cha Uthibiti wa Ubora wa Chanjo kinavyofanya uhakiki wa taarifa zilizochapishwa kwenye Chanjo kama ziko sahihi kabla Chanjo hazijaruhusiwa kupelekwa sokoni. Maelezo hayo aliyapata  kutoka kwa Fundi Sanifu Maabara Bi. Shukuru Joseph Nganga wa Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI - Kibaha),  alipotembelea Taasisi hiyo iliyopo Kibaha Mkoa wa Pwani Mei 12, 2023 kwa lengo la kufahamu kazi zinazofanywa na Taasisi hiyo hususan utafiti na uzalishaji wa Chanjo.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (wa pili kutoka kushoto) akipata maelezo kuhusiana na namna Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI Kibaha) inavyofanya kazi zake kutoka kwa Meneja wa Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) Dkt. Charles Mayenga alipotembelea Taasisi hiyo iliyopo Kibaha Mkoa wa Pwani Mei 12, 2023 kwa lengo la kufahamu kazi zinazofanywa na Taasisi hiyo na Uwekezaji wa Serikali katika Uboreshaji wa Miundombinu ya majengo na vifaa.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (Kushoto) akipata maelezo kuhusiana na majukumu yanayofanywa na Wakala kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi (kulia) alipombelea Ofisi ya TVLA Mei 12, 2023 Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kufahamu kazi zinazofanywa na TVLA pamoja na kujionea shughuli mbalimbali za Kimaabara.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (kulia) akiongea na vyombo vya Habari mbele ya baadhi ya watumishi wa Makao Makao Makuu ya Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kuhusiana na ziara aliyoifanya Mei 12, 2023 Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kufahamu kazi zinazofanywa na TVLA pamoja na kujionea shughuli mbalimbali za Kimaabara.

​SERIKALI YAJA NA MPANGO ENDELEVU WA UNYWAJI MAZIWA SHULENI

 SERIKALI YAJA NA MPANGO ENDELEVU WA UNYWAJI MAZIWA SHULENI 


 

Na. Edward Kondela

 


Serikali iko kwenye mkakati wa kukamilisha mpango kazi wa unywaji maziwa shuleni, ili kuhakikisha wanafunzi wanakunywa maziwa ili kuimarisha afya zao.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe, amebainisha hayo leo (11.05.2023) mara baada ya kufungua rasmi kikao cha mapitio ya mwisho ya mpango kazi wa unywaji maziwa shuleni, kilichofanyika jijini Dodoma.


Prof. Shemdoe amesema kumekuwa na changamoto ya unywaji maziwa nchini kutokana na takwimu za Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ambapo mtu mmoja kwa mwaka anatakiwa kunywa wastani wa lita 200 ila kwa sasa mtu mmoja kwa mwaka anakunywa lita 62 pekee.


“Kama Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambao ndiyo wazalishaii  wa maziwa kwenye mnyororo wa thamani tunaanza sisi huko kwenye mifugo tumeona ni vyema kwa kushirikiana wadau wakiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa Linalohudumia Watoto (UNICEF) na FAO kuhakikisha watoto shuleni wanapata maziwa.” Amesema Prof. Shemdoe


Ameongeza kuwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali mpango kazi huo utaielekeza serikali na sekta binafsi namna ya kuutekeleza katika kuchangia upatikanaji wa maziwa shuleni ili kuongeza idadi ya shule ambazo zimekuwa zikipata maziwa kupitia mpango huo.


Kwa upande wake Mkuu wa Lishe kutoka UNICEF – Tanzania, Bw. Patrick Codjia amesema huu ni mpango mzuri wa wizara katika kuweka msisitizo wa kuimarisha lishe hususan kwa wanafunzi ili kuimarisha afya zao kupitia unywaji maziwa pamoja na kuhamasisha wanafunzi kunywa au kula vitu ambavyo ni muhimu kwao afya zao.


Bw. Codjia amebainisha kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeonyesha nia na jitihada madhubuti katika kuhahikisha inaboresha afya ya watoto kwa kupata lishe bora kupitia unywaji wa maziwa.


Naye Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) Dkt. George Msalya amefafanua kuwa mpango wa unywaji maziwa shuleni umekuwa ukitekelezwa hapa nchini kwenye shule mbalimbali ambapo kuna wakati ulifika shule 113 na kufikia wanafunzi Elfu 90.


Aidha amesema mpango kazi huo ambao unatarajiwa kuzinduliwa rasmi Tarehe 1 Mwezi Juni Mwaka 2023 kwenye siku ya kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Maziwa Duniani ambapo utawezesha watekelezaji wa mpango kuona namna nzuri ya utekelezaji wa unywaji maziwa shuleni kwa kushirikiana na UNICEF ambapo Bodi ya Maziwa iliwashirikisha wadau mbalimbali kuandika mpango huo.


Nao baadhi ya washiriki wa kikao hicho wamesema mpango wa unywaji maziwa shuleni ni muhimu katika kuimarisha afya za watoto na kuleta chachu kwa wasindikaji wa maziwa kuwa na vifungashio vya bei nafuu ambavyo mzazi anaweza kumudu kwa ajili ya kumnunulia mwanaye maziwa.


Kikao cha mpango kazi wa unywaji maziwa shuleni kilichofanyika jijini Dodoma kimeshirikisha wizara za kisekta, taasisi za serikali, vyuo vikuu, wadau kutoka sekta binafsi, wazalishaji wa maziwa, wasindikaji wa maziwa, shule zinazotekeleza mpango wa unywaji maziwa, taasisi za kifedha na wadau wa maendeleo.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe akizungumza jijini Dodoma wakati akifungua rasmi kikao cha mapitio ya mwisho ya mpango kazi wa unywaji maziwa shuleni, ambapo amesema serikali iko kwenye mkakati wa kukamilisha mpango huo ili kuhakikisha wanafunzi wanakunywa maziwa na kuimarisha afya zao. (11.05.2023)

Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Michael akizungumzia juu ya mpango wa unywaji maziwa shuleni na namna serikali ilivyopitia hatua mbalimbali katika kuuandaa, wakati wa kikao cha mapitio ya mwisho ya mpango huo kwenye kikao kilichofanyika jijini Dodoma. (11.05.2023)

Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Dkt. George Msalya akifafanua kwa washiriki juu ya mpango wa unywaji maziwa shuleni katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma, ikiwa ni mapitio ya mwisho kabla ya mpango huo kuzinduliwa rasmi Tarehe 1 Mwezi Juni Mwaka 2023 kwenye siku ya kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Maziwa Duniani. (11.05.2023)

Mkuu wa Lishe kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa Linalohudumia Watoto (UNICEF) – Tanzania, Bw. Patrick Codjia akifafanua juu ya umuhimu wa lishe bora kwa watoto wakati wa kikao cha mapitio ya mwisho ya mpango wa unywaji maziwa shuleni. Kikao hicho kimefanyika jijini Dodoma. (11.05.2023)

Washiriki wa kikao cha mpango kazi wa unywaji maziwa shuleni kilichofanyika jijini Dodoma kutoka wizara za kisekta, taasisi za serikali, vyuo vikuu, wadau kutoka sekta binafsi, wazalishaji wa maziwa, wasindikaji wa maziwa, shule zinazotekeleza mpango wa unywaji maziwa, taasisi za kifedha na wadau wa maendeleo. (11.05.2023)

BIL. 4.6 KUWANUFAISHA WAVUVI TANGA NA PEMBA.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na nchi ya Ireland wameanza utekelezaji wa mradi wa "Bahari Mali" wenye thamani ya shilingi Bil.4.6 ambao utavinufaisha vikundi 19 vya wanawake na vijana waliopo mkoa wa Tanga na Pemba.


Akizungumza katika hafla fupi ya uzinduzi wa mradi huo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo ni ishara tosha ya namna Serikali ya Rais Dkt. Samia na Dkt. Hussein Ally Mwinyi zilivyodhamiria kukuza uchumi wa pande zote mbili kupitia sekta ya Uvuvi 


"Katika utekelezaji wa mradi huu, kila kikundi kitapewa mafunzo ya ujasiriamali bure kabisa na baada ya kumaliza mafunzo hayo kila kikundi kitawezeshwa mtaji wa shilingi milioni 32 hivyo ni lazima tukubaliane kuwa mama amedhamiria kubadilisha maisha ya watanzania kupitia fursa mbalimbali anazozipata kwa sababu sote tunakubaliana hakuna Serikali inaweza kukupa mtaji wa hela zote hizo bure kabisa" Ameongeza Mhe. Silinde.


Mhe. Silinde amebainisha kuwa lengo la mradi huo linaenda sambamba na malengo ya Serikali ambayo ni kuboresha uchumi wa wananchi hasa kupitia kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Waziri Kindamba amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo utaongeza utalii endelevu baina ya Tanga na Pemba na kukuza mazingira ya utawala bora ya mkoa huo wakati wote wa usimamizi wake.


"Lakini pia kwa kuzingatia kuwa utajiri wetu upo baharini, tutakuwa na jukumu muhimu la kukuza uchumi wa buluu kwa hapa mkoani kwetu kwa sababu kile kinachofanywa kule Zanzibar ni lazima na hapa Tanga kifanyike kwa utaratibu ule ule hivyo ninawahamasisha wananchi wa hapa tutumie fursa hii ipasavyo" Amesisitiza Mhe. Kindamba.


Kwa upande wake mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu kutoka Zanzibar Bw. Omar Mohamed amesema kuwa uchumi wa nchi yao unategemea shughuli za uvuvi kwa zaidi ya asilimia 60 hivyo mradi huo ni chachu ya kuendeleza jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukuza uchumi wa nchi hiyo.


Akielezea utekelezaji wake,  Mratibu wa mradi huo Dkt. Elinas Monga amesema kuwa mradi huo utatekelezwa  kwa  kipindi cha miaka 3 (2022-2025) katika Wilaya za Mkinga na Pangani (Tanga) na Micheweni na Mkoani (Pemba).


Mbali na utoaji wa mafunzo na fedha kwa ajili ya ukuzaji viumbe maji bahari, mradi huo unalenga kutunza na kuhifadhi rasilimali za bahari na Pwani, kuboresha uelewa na maarifa kwa wadau wanaohusika na ulinzi wa rasilimali hizo kuendeleza huduma za kiikolojia kwenye maeneo ya Tanga na Pemba.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (kushoto) akipokea maelezo kuhusu unenepeshaji wa kaa (aliyemshika) muda mfupi baada ya kuzindua mradi wa "Bahari Mali" kwenye hafla fupi iliyofanyika jijini Tanga Mei 10, 2023.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (aliyeshika kipaza sauti) akikabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shiingi milioni 192 kwa vikundi vya ujasiriamali wa uchumi wa buluu vya Tanga na Pemba muda mfupi baada ya kuzindua mradi wa "Bahari Mali" tukio lililofanyika Mei 10, 2023. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Waziri Kindamba na kulia kwake ni Naibu balozi wa Ireland nchini Bi. Mags Gaynor.

WAZIRI ULEGA AFANYA KIKAO NA VIONGOZI WA CHAMA CHA WAFUGAJI TANZANIA

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kulia) akimpa maagizo Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Bw. Evance Ntiyalunduwa  kwenye kikao cha  Waziri na Viongozi wa Chama cha wafugaji Tanzania (CCWT) (hawapo pichani) ambapo Viongozi hao walimtembelea Waziri kwa lengo la kujadiliana mambo mbalimbali yanayohusu ufugaji,  kikao hicho kilifanyika katika ofisi za wizara zilizopo jengo la NBC, Dodoma, Tarehe 10.05.2023.

Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango Bw. Evance Ntiyalundura(wapili kulia) akitoa maelezo kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega(wakwanza kulia) kwenye kikao cha Waziri na viongozi wa chama cha Wafugaji Tanzania ambao walimtembelea Waziri kwa lengo la kujadiliana mambo mbalimbali yanayohusu Mifugo, kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa ofisi za Wizara zilizopo jengo la NBC,  Jijini Dodoma.  Tarehe 10.05.2023.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akiongea jambo kwenye kikao na Wadau wa sekta ya Uvuvi kutoka Ziwa Tanganyika na Wataalamu wa Wizara. (Hawapo pichani) ambapo wadau hao waliwasilisha hoja zao na waziri amezipokea na kuagiza Wataalamu wa Wizara kumpatia taarifa za maboresho ya kiutafiti ambazo zilifanywa na TAFIRI ya mwaka 2020. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa ofisi za Wizara hiyo zilizopo,jengo la NBC, Dodoma. 10 Mei 2023.

Wadau wa sekta ya uvuvi kutoka ziwa Tanganyika na Wataalamu wa sekta Uvuvi kutoka Wizarani wakimsikilliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) (wakwanza kulia)alipokuwa akitoa maelekezo 10.05.2023, kwenye kikao ambacho kilifanyika kwa lengo la kutoa hoja na kuzitolea ufafanua kuhusu Uvuvi  wa Ziwa Tanganyika, kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa ofisi za Wizara zilizopo jengo la NBC, Dodoma.