Nav bar

Jumatatu, 27 Mei 2019

TANZANIA YASHIRIKI KONGAMANO LA MATUMIZI ENDELEVU YA RASILIMALI ZA BAHARI NCHINI MSUMBIJI




Nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi zikiwemo Tanzania, Kenya, Msumbiji na Afrika ya Kusini na Visiwa vya Ushelisheli zimepewa rai ya kuhakikisha zinafanya kila njia kulinda rasilimali za pamoja hususan zinazopakana na bahari ili ziweze kusaidia kukuza uchumi wa nchi hizo.

Rai hiyo imetolewa na Rais wa Msumbiji Mhe. Filipe Jacinto Nyusi wakati wa ufunguzi wa kongamano la kujadili matumizi endelevu ya rasilimali za bahari linaloendelea katika mji wa Maputo nchini humo.

Rais Nyusi amesema kongamano hilo la siku mbili lina umuhimu mkubwa kwa kuwa linafanyika wakati huu ambapo uvunaji holela na usiofuata utaratibu wa rasilimali za bahari umeshamiri katika nchi nyingi za bara la Afrika na Asia.

Akihutubia washiriki wa Kongamano hilo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ameelezea hatua mbalimbali ambazo nchi ya Tanzania imepiga katika kuhakikisha malengo ya milenia kuhusu uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za asili yanafikiwa.

Mhe. Ulega amezitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kupambana na uvuvi haramu na biashara haramu ya utoroshwaji wa mazao ya uvuvi, kudhibiti uvuvi wa mabomu katika pwani ya Bahari ya Hindi, kutekeleza miradi ya kuhifadhi mazingira ya bahari kwa lengo la kuinua maisha ya jamii za wavuvi, kulinda maeneo tengefu ya bahari, kufanya utafiti na kuzuia uharibifu wa bahari unaotokana na matumizi ya bidhaa za plastiki.

Aidha, Mhe. Ulega amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi za ukanda wa Bahari ya Hindi kuhakikisha rasilimali zilizopo zinalindwa na zinazinufaisha nchi wanachama.

Pamoja na mambo mengine mkutano huo umeangazia mchango wa sekta
zingine ambazo kwa pamoja zinachochea ukuaji wa uchumi wa bluu ambao
unahimiza matumizi ya bahari katika kukuza uchumi wa nchi.

Sekta hizo ni pamoja na usafirishaji, utalii wa bahari, uhifadhi wa mazingira, utafutaji na uchimbaji wa gesi, pamoja na usalama wa chakula na ajira.

Kwa pamoja washiriki wa kongamano hilo wamekubaliana katika kuimarisha ushirikiano, kuendelea kubadilishana uzoefu na kwamba juhudi za pamoja zinahitajika ili kulinda rasilimali za bahari kwa kuwa baadhi ya rasilimali hizo hazina mipaka kama ilivyo kwa samaki aina ya jodari ambao huhama kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine.

Kongamano hilo limeandaliwa na nchi ya Msumbiji kwa kushirikiana na Norway pamoja na mashirika mbalimbali ikiwemo Benki ya Dunia, ambapo zaidi ya washiriki 300 kutoka sehemu mbalimbali duniani wakiwemo wataalam wa sayansi za bahari, mazingira, usafirishaji majini, viongozi wa kisiasa, wakuu wa mashirika ya fedha na mashirika binafsi yanayojihusisha na uhifadhi wa rasilimali za bahari wanahudhuria kongamano hilo.

Tanzania, imewakilishwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega na wengine ni Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Mmanga Mjengo Mjawiri, Mkurugenzi wa Uvuvi Zanzibar Mussa Aboud Jumbe na maofisa kutoka Mamlaka ya Bahari ya Kuu nchini.



Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ( wa pili kutoka kulia) akifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa kwenye kongamano la matumizi endelevu ya rasilimali za bahari katika Mji wa Maputo, Nchini Msumbiji.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe, Abdallah Ulega akihutubia washiriki kwenye kongamano la matumizi endelevu ya rasilimali za bahari lililofanyika katika mji wa Maputo, Nchini Msumbiji


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (katikati) akiwa katika mazungumzo na maafisa kutoka SMZ ambao pia wameshiriki kwenye kongamano la matumizi endelevu ya rasilimali za bahari katika mji wa Maputo  Nchini Msumbiji.


Jumanne, 14 Mei 2019

KATIBU MKUU WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI (MIFUGO) AAHIDI KUBORESHA WIZARA KUWA YA MFANO KIUTENDAJI SERIKALINI



                                                                                                                                                               

                                                                                                                                                            
 Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo)   Prof. Elisante Ole  Gabriel amesema anataka wizara hiyo iwe ya mfano katika kumsaidia Rais Dkt. John Magufuli katika kutimiza majukumu na malengo ya nchi kwa kufanya kazi kwa bidii na ufanisi zaidi.

Prof. Gabriel amesema hayo leo (08.05.2019) ofisini kwake jijini Dodoma wakati akipokea taarifa ya ukaguzi wa utendaji kazi wa wizara hiyo katika idara ya utawala na rasilimali watu, na kupongeza utendaji kazi wa idara hiyo katika kusimamia matakwa ya mtumishi wa umma.

 "Nina dhamira ya dhati ya kuboresha wizara na mambo yote yaliyofanyiwa ukaguzi yatafanyiwa kazi na yanaendelea kufanyiwa kazi pamoja na kusaini fomu zote za likizo kwa wakati, kupandisha watumishi vyeo pamoja na kutoa elimu ya majukumu kwa waajiriwa wote." Alisema Prof. Gabriel.

Aidha Katibu Mkuu huyo akizungumza mbele ya wakaguzi kutoka katika tume hiyo wakiongozwa na bibi Kombe Shayo, ameshauri wakaguzi kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi zikiwemo TALIRI, TAFIRI, TVLA, FETA, Bodi ya Maziwa na Bozi ya Nyama kuona wanavyofanya shughuli zao, kuonyesha kiwango au hatua walizofikia tangu kuanza kwa ukaguzi.

Hali kadhalika Prof. Gabriel ameomba wakaguzi kutoa elimu ya ‘opras’ kwa watumishi wa wizara mwishoni mwa mwezi Mei au mwanzoni mwa mwezi Juni ili watumishi waelewe vizuri na  kupewa zaidi elimu ya nidhamu ya kazi pamoja na ufanyaji kazi mzuri, ulio bora na wenye tija.

Awali akiwasilisha taarifa kwa katibu mkuu huyo, Mkaguzi kutoka Tume ya Utumishi wa Umma Bibi Kombe Shayo amesema watumishi wanapaswa kupewa elimu juu ya kujaza fomu ya ‘opras’ na watu wa masijala wapate maelekezo ya jinsi ya kutunza fomu hizo pamoja na menejimenti ya wizara kuhakikisha inapandisha watumishi madaraja na kuwathibitisha kazini kwa wakati pamoja na watumishi kupata mgawanyo wa kazi.

"Watumishi wanaenda kwenye mafunzo na wanatoa taarifa pindi wakiwa masomoni na pindi wamalizapo ambalo ni jambo zuri  na pia ufadhili upo na watumishi wakasome mapema na wasisubiri umri usogee" alifafanua Bibi Shayo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Bw. Zakariyya Kera alipatiwa sifa za kipekee na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel pamoja na Mkaguzi wa Tume ya Utumishi wa Umma Bibi Kombe Shayo kwa kufanya kazi kwa umahiri mkubwa katika idara hiyo kutokana na kusimamia kwa ufanisi mkubwa mambo mbalimbali yahusuyo watumishi wa wizara hiyo.


Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Zakariyya Kera akimwagiwa sifa za utendaji na mkaguzi Bi. Kombe Shayo.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wakaguzi kutoka tume ya Utumishi wa Umma  pamoja na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara hiyo Bw. Zakariyya Kera (wa kwanza kushoto).


Jumatatu, 13 Mei 2019

SERIKALI ZA TANZANIA NA DENMARK ZAJA NA MPANGO WA KULINDA RASILIMALI ZA ZIWA TANGANYIKA.




SERIKALI ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Denmark kupitia Shirika la Misaada la Kimaendeleo (DANIDA) imesema kuna haja ya kuendeleza mapinduzi makubwa katika sekta ya uvuvi nchini ili kulinda rasilimali zipatikanazo katika maziwa, bahari na mito nchini.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa kupokea taarifa ya utafiti uliofanywa katika Ziwa Tanganyika lililopo Mkoani Kigoma, kutazama mabadiliko ya tabia nchi katika eneo la ziwa hilo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema utafiti huo umeonyesha wazi kuwa zipo athari zinazotokana na tabia nchi na sababu zingine kama idadi ya wavuvi kuongezeka na baadhi yao kutumia zana haramu za uvuvi na kuathiri mazingira ya ziwa na rasilimali zilizopo.

Mhe. Ulega amesema mambo yote ambayo yamefanyiwa utafiti yakijadiliwa vyema litatolewa tamko la Sera ambayo itakuwa ni ushauri wa kitaalam ambao utaiongoza serikali ikiwa inaendelea kufanya maboresho ya kanuni na sheria za uvuvi.

"Kitu hiki ni muhimu sana kwa sababu eneo la Ziwa Tanganyika watu wanatengemea sana kwa shughuli za kujipatia samaki na kuendesha maisha yao, ile rasilimali tusipoweza kuweka mkakati mzuri wa kuitunza na kuhakikisha kuwa inakuwa endelevu basi maana yake jamii ile kuna wakati ile rasilimali kama sasa hivi kiasi cha samaki kimepungua sio kama ilivyokuwa huko kipindi cha nyuma”. Alisema Mhe. Ulega

Amefafanua kuwa ni muhimu kuchukua hatua mbalimbali za kielimu kwa kuwaelimisha wavuvi, hatua za kusimamia kwa kutumia njia zilizo bora zaidi ili kupatikana kwa uendelevu wa rasilimali zilizopo katika Ziwa Tanganyika.

“Kinyume na hapo watu watakosa zile fursa na umasikini utajikita zaidi kwa hivyo ni muhimu kudhibiti na kuweza kuwa na mpangilio mzuri ili mradi ile rasilimali iweze kuwa endelevu”. Alifafanua Mhe. Ulega

Aidha Naibu Waziri Ulega amebainisha kuwa serikali na wananchi kwa ujumla ina jukumu la kudhibiti shughuli za   kibinadamu ziendane na utaratibu wa ulinzi wa mazingira ili kudhibiti athari za mazingira.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah amesema matokeo hayo ya utafiti yamekuja wakati muafaka kwa sababu baadhi ya majukumu ya kisera ambayo wameyaleta yanahusiana na zoezi ambalo linaendeshwa na wizara la kuboresha Sheria ya Uvuvi ya mwaka 2003 ili iendane na hali halisi ya sasa.

“Tumekusanya maoni kwa wadau nchi nzima na sasa tunachambua yale maoni tuangalie maendeleo yanayotakiwa, kwa hiyo na hawa katika ushauri wanaokuja nao na matamko ya kisera kuna maeneo vilevile kutokana na uchunguzi waliofanya wanaona ili tuendelee vizuri katika kujenga rasilimali za uvuvi katika Ziwa Tanganyika kuna vitu tunatakiwa tubadilishe kwenye sheria hivyo wamekuja muda muafaka na tumefurahi sana”. Alisema Dkt. Tamatamah

Hali kadhalika, Bw. Ismail Aron Kimbilei ambaye ni Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Mkoa wa Kigoma amesema wamependekeza Ziwa Tanganyika kupumzishwa kwa shughuli za uvuvi kila baada ya muda fulani ili kuongeza mazalia ya samaki.

“Naamini kwamba yatafanyiwa kazi na naamini utafiti wetu utakuwa  na faida kama watawahusisha wadau kwamba wavuvi wawekwe chini na waelezwe faida za kutunza ziwa na waelezwe hasara za kufanya kinyume na matarajio halafu waangalie na waamue  kwa pamoja na wanaweza kufanya kwa mfano tuu tuanze kwa kufunga miezi mitatu tuone matokeo yake kama dagaa na migebuka itakuwa imeongezeka na baada ya hapo wataamua cha msingi ni kushirikisha wadau.” Alisema Bw. Kimbilei


Naibu Waziri wa Wizara ya MIfugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega katika picha ya pamoja na Watafiti wa kutazama mabadiliko ya tabia nchi katika eneo la Ziwa Tanganyika na wawakilishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi jijini Dodoma.


WAFUGAJI KITETO WAKABIDHIWA HATI MILIKI YA NYANDA ZA MALISHO.




Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewezesha kupatiwa hati miliki ya kimila Nne (4) kwa kikundi cha wafugaji  cha Olengapa kupitia mradi wa Uendelezaji wa Nyanda za Malisho (SRMP).

Tukio hilo la kukabidhi hati miliki ya kimila kwa Kikundi cha Wafugaji lilifanyika katika Kijiji cha Lengatei Wilaya ya Kiteto Mkoa wa Manyara.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia mradi wa SRMP imeweza kutoa hati hiyo kwa kikundi cha wafugaji cha Olengapa vinavyoruhusu kutumia na kumiliki eneo la malisho kwa pamoja.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Sekta ya Mifugo,Prof Elisante Ole Gabriel, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Bw. Zakariyya Kera alisema, eneo hilo lililotengwa linaukubwa wa hekta 30,145.

Alisema pia, lengo ni kuwapatia  haki wafugaji ya uhakika wa kumiliki Ardhi kwa shughuli zao za kiuchumu na kijamii.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Bw. Manyara Alexanda Mnyeti, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Bw. Tumaini Magesa alisema, nashukuru wizara ya Mifugo na uvuvi kuheshimu ilani ya Chama cha mapinduzi kwasabau ni hitaji la chama tawala na hili limefanikiwa.




Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Bw. Zakariyya Kera akisoma hotuba kwa ufupi kwa niaba ya Katibu  Mkuu sekta ya Mifugo.



Mwenyekiti wa kikundi cha Olengapa Bw. Kilekeni Noongejeck akipokea hati miliki ya kimila kwa niaba ya kikundi kutoka kwa mgeni rasmi  Bw. Tumaini Magesa

WAFUGAJI WAASWA KUBADILIKA KIFIKRA NA KUFUATA SHERIA




SERIKALI imewataka wafugaji nchini kubadili fikra zao na kutambua umuhimu wa kufuata sheria, taratibu na kanuni za nchi ili kujiepusha na mkono wa sheria pindi wanapoingiza mifugo yao katika hifadhi na mapori ya akiba.

Akizungumza na baadhi ya wafugaji jana (20.04.2019) katika Wilaya ya Meatu, Mkoani Simiyu, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel amesema baadhi ya wafugaji wamekuwa wakiingiza mifugo yao katika hifadhi na mapori ya akiba, hivyo kusababisha kutokuwepo kwa mahusiano mazuri kati yao na wahifadhi kwa madai ya kuonewa ilhali wahifadhi hao wanatakeleza sheria za nchi.

“Tunatamani fikra za wafugaji wote nchini zibadilike na zianze kutambua umuhimu wa kufuata sheria, taratibu na kanuni, ndiyo msingi wa mafaniko. Niwaombe wafugaji wote nchini watambue kwamba Wizara ya Mifugo na Uvuvi itapenda wafugaji wafuate sheria, taratibu na kanuni, tukifanya hivyo tutakuwa marafiki wa wizara unapokuwa mhalifu unakuwa tena siyo mfugaji bali unakuwa mhalifu.” Alisema Prof. Gabriel.

Katibu mkuu huyo amelazimika kukutana na wafugaji hao kutokana na hivi karibuni ng’ombe kukamatwa katika Pori la Akiba la Maswa ambapo wamiliki wa ng’ombe hao wamekiri kufanya kosa na kulipa faini waliyotozwa na mahakama mara baada ya kukiri kosa na kutiwa hatiani.

“Hivi karibuni ng’ombe walikamatwa katika Pori la Akiba la Maswa, ndipo busara ikatumika kuona jambo hilo linafikia tamati ambapo wahusika wamekabidhiwa ng’ombe zao kwa kuwa busara imetumika na siyo kwamba wao wameshinda, kwa mujibu wa sheria wenzetu wa hifadhi wanachofanya ni kusimamia Sheria Namba Tano ya Mwaka 2009 ya Hifadhi ya Wanyamapori kwamba mifugo ikikamatwa inaweza kutaifishwa.” Alifafanua Prof. Gabriel.

Awali akizungumza na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kabla ya kuzungumza na wafugaji hao, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel amewashukuru madiwani wa halmshauri hiyo wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Mhe. Juma Issack Mpina kwa uelewa wa hali ya juu baada ya Meneja wa Pori la Akiba la Maswa Bw. Lusato Masinde kutoa elimu na sheria iliyotumika na maamuzi yaliyotolewa na mahakama kwa wafugaji waliyoingiza mifugo katika Pori la Akiba la Maswa.

Aidha amebainisha kuwa kunapaswa kuwepo kwa mawasiliano mazuri kati ya viongozi na jamii ya wafugaji katika maeneo yote nchini ili kujenga mahusiano mazuri na kuelewa majukumu ya wasimamizi wa hifadhi na mapori ya akiba ambao wamekuwa wakisimamia sheria na kwamba hawapo kwa ajili ya kumuonea mtu yeyote.

Katika kikao na wafugaji Prof. Gabriel amewataka pia wasijichukulie sheria mkononi hata wanapokuwa wamepishana kauli na wasimamizi wa sheria kama ambavyo imekuwa ikijitokeza katika maeneo mbalimbali nchini ambapo amebainisha kuwa kwa kufanya hivyo ni kosa kubwa kisheria, huku akiwapongeza wafugaji wa Wilaya ya Meatu kwa kuwa watulivu na kuonesha ushirikiano kwa maafisa wa Pori la Akiba la Maswa baada ya kuingiza mifugo yao katika pori hilo kinyume na sheria na kutii hatua za kisheria zilizochukuliwa dhidi yao.

Akizungumza na wafugaji Katika kuhakikisha sekta ya ufugaji inaboreka katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Wilaya ya Meatu, Mkoani Simiyu, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel amesema wizara inahakikisha kwa juhudi zote inaboresha sekta ya ufugaji nchini yakiwemo malisho bora kwa kuwepo kwa shamba darasa katika wilaya hiyo na maeneo mengine.

Pia Prof. Gabriel amewataka wafugaji kufuga kisasa kwa kuwa na ng’ombe wanaopatikana kwa njia ya uhimilishaji ambao wamekuwa na matokeo mazuri kwa kuwa na nyama nyingi na maziwa mengi yenye ubora.

“Ukifuga wa kisasa wa ng’ombe wanaopatikana kwa njia ya uhimilishaji hautajivunia idadi ya ng’ombe ulionao bali kwa kilo na wingi wa maziwa ambao ng’ombe hao wanatoa, ambapo ng’ombe mmoja anafikia hadi kilogram 800 na tumehakikisha kama wizara wafugaji wanapata mbegu za ng’ombe bora kwa bei isiyozidi Shilingi Elfu Tano.” Alisema Prof. Gabriel

Kwa upande wake Meneja wa Pori la Akiba la Maswa Bw. Lusato Masinde amesema wapo kwa ajili ya kuwasaidia wananchi na kwamba wataendelea kusimamia sheria.

“Sisi tutaendelea kutoa elimu ili wananchi wafahamu umuhimu wa sheria zilizopo nchini ikiwemo inayohusu maeneo ya hifadhi na mapori ya akiba ili wananchi wasifanye shughuli zinazokatazwa katika maeneo hayo.” Alisema Bw. Masinde.

Amefafanua wao kama maafisa wanaolinda Pori la Akiba la Maswa wanahitaji ushirikiano kutoka kwa wananchi hususan wafugaji wa Wilaya ya Meatu ili kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuwatia hatiani kwa kukiuka sheria za nchi ambazo wamepewa kuzisimamia.

Nao baadhi ya wafugaji walioshiriki kikao cha Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel wameomba kupata elimu zaidi juu ya uhimilishaji ili waweze kufuga ng’ombe kisasa na wenye tija kiuchumi.

Pamoja na hilo wamewaomba pia wafugaji wenzao kufuata sheria, taratibu na kanuni za nchi na kuwa karibu na viongozi wa wilaya hiyo ili waweze kufanya shughuli zao kwa kufuata maelekezo yao na kuwa na mawasiliano mazuri ambayo yatawaepusha kutojiingiza na ukiukwaji wa sheria kwa kuingiza mifugo kwenye maeneo wasiyoruhusiwa.



Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika matukio mbalimbali alipofanya kikao na wafugaji katika Wilaya ya Meatu, Mkoani Simiyu juu ya umuhimu wa kufuata sheria.

 


NORWAY YAISAIDIA SEKTA YA UVUVI NCHINI



SERIKALI ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la NORAD, Norway imesaini mkataba wa uzalishaji samaki aina ya Sato zaidi ya tani 100,000 kwa mwaka katika kipindi cha miaka 10 ijayo.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mradi huo kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi,  mhe.Luhaga Joelson Mpina, Katibu Mkuu wa sekta ya Uvuvi  Dk. Rashid Tamatamah amesema,  mradi huo umekuja muda muafaka wakati nchi ina mahitaji makubwa.

Amesema lengo la Serikali ni kuzalisha samaki kwa wingi ambapo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kwenye mabwawa.

Amesema mradi huo umekuja kwa sababu ya kazi nzuri ya asasi ya Norges Vel, Chama cha Ukuzaji Viumbe Maji Tanzania (AAT) na Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA).

Aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka 20 sasa Tanzania imekuwa haifanyi vizuri katika sekta ya uvuvi ambapo imekuwa ikizalisha samaki tani 350,000 hadi 380,000 kwa mwaka."Samaki wanaozalishwa hivi sasa kwenye vyanzo vya maji idadi yake imebaki kuwa vilevile haiongezeki kwa kasi hivyo kuna kila haja ya kuongeza kasi ya uzalishaji,"alisema Tamatamah.

Amesema serikali ina nia ya dhati katika kuendeleza ufugaji samaki japokuwa imekuwa ikikabiliwa na changamoto kadhaa.Tamatamah amesema fursa zilizopo hapa nchini ni pamoja na vyanzo vya vya maji, hali ya hewa na mazingira lakini wameshindwa kuzalisha tani za kutosha.

Amesema hadi sasa Tanzania imekuwa ikizalisha tani 16,000 wakati Norway inazalisha tani milioni 2.5 kwa mwaka."Hii ni fursa kwetu kwakuwa wenzetu wana ujuzi wa uzalishaji samaki, itasaidia kutuongezea ujuzi na sisi,"alisema Tamatamah.

Alibainisha kuwa Mradi huo utatekelezwa Kibaha mkoani Pwani ambapo vijana watapata fursa ya elimu pamoja na kuzalisha samaki.

Amesema anaamini hakuna uzoefu mbadala kwa mbinu hiyo kwani ni moja ya njia sahihi ya kupata ujuzi. Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama alisema mradi huo ni fursa na neema kwa wananchi wa Kibaha.

Alisema anaamini mradi huo utaongeza idadi ya samaki wanaozalishwa nchini pamoja naa kukuza uchumi wa nchi.

Naye, Balozi wa Norway nchini Tanzania, Elizabeth Jacobson alisema, ana imani mradi huo utafungua fursa kwa vijana na kukuza uchumi wa nchi.

Alisema mradi huo umeletwa ili kutokomeza changamoto zilizopo za uhaba wa samaki pamoja na kufungua njia za ujasiriamali kwa wananchi.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashidi Tamatamah, akihutubia kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Joelson Mpina kwenye hafla ya Uzinduzi wa Mradi wa Ufugaji wa Samaki iliyofanyika katika ofisi za Wizara jijini Dr es salaam.