SERIKALI ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la
Maendeleo la NORAD, Norway imesaini mkataba wa uzalishaji samaki aina ya Sato
zaidi ya tani 100,000 kwa mwaka katika kipindi cha miaka 10 ijayo.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa
mradi huo kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, mhe.Luhaga Joelson Mpina, Katibu Mkuu wa sekta
ya Uvuvi Dk. Rashid Tamatamah amesema, mradi huo umekuja muda muafaka wakati nchi
ina mahitaji makubwa.
Amesema lengo la Serikali ni kuzalisha samaki kwa wingi
ambapo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kwenye mabwawa.
Amesema mradi huo umekuja kwa sababu ya kazi nzuri ya asasi
ya Norges Vel, Chama cha Ukuzaji Viumbe Maji Tanzania (AAT) na Wakala ya Elimu
na Mafunzo ya Uvuvi (FETA).
Aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka 20 sasa Tanzania
imekuwa haifanyi vizuri katika sekta ya uvuvi ambapo imekuwa ikizalisha samaki
tani 350,000 hadi 380,000 kwa mwaka."Samaki wanaozalishwa hivi sasa kwenye
vyanzo vya maji idadi yake imebaki kuwa vilevile haiongezeki kwa kasi hivyo
kuna kila haja ya kuongeza kasi ya uzalishaji,"alisema Tamatamah.
Amesema serikali ina nia ya dhati katika kuendeleza ufugaji
samaki japokuwa imekuwa ikikabiliwa na changamoto kadhaa.Tamatamah amesema fursa
zilizopo hapa nchini ni pamoja na vyanzo vya vya maji, hali ya hewa na
mazingira lakini wameshindwa kuzalisha tani za kutosha.
Amesema hadi sasa Tanzania imekuwa ikizalisha tani 16,000
wakati Norway inazalisha tani milioni 2.5 kwa mwaka."Hii ni fursa kwetu
kwakuwa wenzetu wana ujuzi wa uzalishaji samaki, itasaidia kutuongezea ujuzi na
sisi,"alisema Tamatamah.
Alibainisha kuwa Mradi huo utatekelezwa Kibaha mkoani Pwani
ambapo vijana watapata fursa ya elimu pamoja na kuzalisha samaki.
Amesema anaamini hakuna uzoefu mbadala kwa mbinu hiyo kwani
ni moja ya njia sahihi ya kupata ujuzi. Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya
Kibaha, Assumpter Mshama alisema mradi huo ni fursa na neema kwa wananchi wa
Kibaha.
Alisema anaamini mradi huo utaongeza idadi ya samaki
wanaozalishwa nchini pamoja naa kukuza uchumi wa nchi.
Naye, Balozi wa Norway nchini Tanzania, Elizabeth Jacobson
alisema, ana imani mradi huo utafungua fursa kwa vijana na kukuza uchumi wa
nchi.
Alisema mradi huo umeletwa ili kutokomeza changamoto zilizopo
za uhaba wa samaki pamoja na kufungua njia za ujasiriamali kwa wananchi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni