Nav bar

Jumanne, 7 Desemba 2021

FISH4ACP ITACHOCHEA ONGEZEKO LA PATO LA TAIFA KUPITIA SEKTA YA UVUVI-DKT. TAMATAMAH

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah amesema kuwa Mradi wa FISH4ACP utasaidia kuongeza nguvu kwenye maboresho ambayo sekta ya Uvuvi inaendelea kuyafanya hivi sasa  kwa ajili ya  kuongeza mchango wa sekta 

Dkt. Tamatamah ameyasema hayo  (06.12.2021) wakati akifungua warsha ya siku mbili ya ukamilishaji mpango wa maboresho ya mnyororo wa thamani wa dagaa na samaki aina ya mgebuka kutoka Ziwa Tanganyika iliyofanyika kwenye ukumbi wa “Kigoma Social Hall” uliopo Manispaa ya Kigoma.

“Lakini pia mradi huu utakuwa na mchango mkubwa katika kutoa ajira hasa kupitia maboresho ya mnyororo wa thamani ya mazao yanayotoka  Tanganyika, utapunguza umasikini miongoni mwa wavuvi na wadau wote watakaohusika kwenye mnyororo huo na kubwa zaidi utaongeza kiwango cha ulaji wa samaki ambao kwa mujibu wa Shirika la Kilimo na Chakula Uliwenguni (FAO) kila Mtanzania anakula kiasi cha kilo 8.5 kwa mwaka hivyo naamini mpaka kukamilika kwa mradi huu angalau kila Mtanzania atakuwa anakula kilo 10.5 kwa mwaka” Amesema Dkt. Tamatamah.

Dkt. Tamatamah ameongeza kuwa katika kuboresha shughuli za Uvuvi wa Ziwa Tanganyika Serikali kupitia kanuni ya Uvuvi ya mwaka 2020, Serikali ilipunguza viwango vya tozo ya usafirishaji wa dagaa inayoenda nje kutoka dola za Marekani 1.5 hadi 0.5 kwa kilo na kwa upande wa Migebuka kutoka Dola za Marekani 0.5 hadi 0.3  jambo ambalo anaamini litahamasisha sana biashara ya mazao hayo ya uvuvi katika masoko ya nje.

“Lakini pia kwa kutambua kuwa  uvuvi endelevu na ulinzi wa rasilimali za uvuvi unategemea uwepo wa taarifa sahihi zinazopatikana kwa wakati za idadi na mtawanyo wa samaki katika vyanzo husika na hapa niishukuru tena Serikali ya awamu ya sita kwa kutenga fedha za utafiti wa utambuzi wa wingi na mtawanyiko wa samaki katika bahari ya Hindi na Ziwa Tanganyika na huu ndo utakuwa utafiti wa kwanza kufanyika tangu nchi yetu ipate uhuru” Amesisitiza Dkt. Tamatamah.

Akizungumza kwa niaba ya Shirika la Chakula na Kilimo Ulimwenguni (FAO), Mwakilishi mkazi wa Shirika hilo kwa upande wa Afrika Mashariki Martin Van Der Knaap amepongeza kazi nzuri iliyofanywa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI) katika kusimamia hatua mbalimbali za utekelezaji wa mpango huo ambapo kwa niaba ya Shirika lake  ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wakati wote wa utekelezaji wa mpango huo.

“Miaka kadhaa iliyopita Umoja wa Ulaya uliomba miswada mbalimbali itakayolenga kwa undani kuhusu mnyororo wa thamani wa samaki na mazao mengine ya uvuvi katika maeneo mbalimbali na ni miswada 12 tu kati ya zaidi ya 40 ndo ilikubaliwa kuwezeshwa fedha kwa ajili ya utekelezaji ukiwemo huu unaohusu mradi wa FISH4ACP hivyo FAO tunaishukuru sana EU kwa kukubali kufadhili mradi huu ambao umeonekana kutekelezwa vizuri zaidi  Tanzania ukilinganisha na maeneo mengine” Amesema Martin.

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah amebainisha kuwa Serikali kupitia Wizara yake imejipanga kuelekeza nguvu katika uvuvi wa bahari kuu ambao unatarajiwa kuboresha uchumi wa mvuvi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

 “Kiukweli eneo ambalo kama sekta bado hatujaliwekea nguvu kubwa ni kwenye upande wa Uvuvi wa bahari na tumegundua moja ya changamoto kubwa zinazoikabili sekta ya Uvuvi ni uwekezaji mdogo kwenye upande wa Uvuvi wa bahari kuu hasa kutoka sekta binafsi hivyo kwa hivi sasa tumeleekeza nguvu yetu kwenye sera ya uendelezaji wa miundombinu ambapo jambo la kwanza ni ujenzi wa bandari za uvuvi na tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia shilingi bilioni 50.72 ambayo tutaanza kujengea bandari ya Uvuvi huko Kilwa Masoko” Amesema Dkt. Tamatamah.

Dkt. Tamatamah amesema kuwa Serikali imeamua kuwekeza zaidi kwenye uvuvi wa bahari kuu kwa sababu mabadiliko ya tabia nchi yanayoendelea hivi sasa yamesababisha samaki wengi kutopatikana kwenye ukanda wa pwani huku wengi  wakikimbilia katikati ya bahari (deep sea) hivyo ni lazima zifanyike jitihada za kuhakikisha uvuvi kwenye ukanda huo unaendelea.

“ Mbali na Ujenzi wa bandari, Serikali pia kupitia mpango wa tatu wa maendeleo ya Taifa , inatarajia kununua meli 4 za uvuvi ambazo zitasaidia kwa kiasi kikubwa suala la Uvuvi wa bahari kuu na kwa mwaka huu wa fedha kupitia Shirika la “IFARD” tutanunua meli mbili  na nyingine mbili tutanunua kabla ya mpango kukamilika mwaka 2025/2026” Amesisitiza Dkt. Tamatamah.

Katika kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wahisani mbalimbali wanaofadhili miradi ya sekta ya uvuvi, Serikali imetenga fedha zitakazotumika  kwa ajili ya utafiti wa wingi na mtawanyo wa rasilimali za Uvuvi kwa upande wa bahari ya Hindi na Ziwa Tanganyika ambapo kwa mwaka huu wa fedha jumla ya shilingi milioni 800 zimeshatolewa kwa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI) kwa ajili ya utekelezaji wa Utafiti huo.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah (kushoto) na Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI) Dkt. Ismail Kimirei wakifuatilia maoni ya mmoja wa wadau wa  Uvuvi wa Ziwa Tanganyika wakati wa  warsha ya siku mbili ya ukamilishaji mpango wa maboresho ya mnyororo wa thamani wa dagaa na samaki aina ya mgebuka kutoka Ziwa Tanganyika iliyofanyika kwenye ukumbi wa “Kigoma Social Hall” uliopo Manispaa ya Kigoma  (06.12.2021).



Sehemu ya wadau wa Uvuvi wa Ziwa Tanganyika wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah (hayupo pichani) wakati akifungua warsha ya siku mbili ya ukamilishaji mpango wa maboresho ya mnyororo wa thamani wa dagaa na samaki aina ya mgebuka kutoka Ziwa Tanganyika iliyofanyika kwenye ukumbi wa “Kigoma Social Hall” uliopo Manispaa ya Kigoma  (06.12.2021).

 

Jumapili, 5 Desemba 2021

WAFUGAJI WATAKIWA KUTUMIA MFUMO WA UTAMBUZI WA MIFUGO KIELEKTRONIKI

 

Serikali imewataka wafugaji Wilayani Mufindi kutumia vyema fursa iliyotolewa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi   ya utambuzi wa mifugo kwa mfumo wa kielektroniki ili kuondokana na changamoto ya wizi wa mifugo hiyo uliokuwa ukijitokeza mara kwa mara.

Rai hiyo ilitolewa Disemba 4, 2021 na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Bw. Saad Mtambule wakati wa uzinduzi wa zoezi la utambuzi, usajili na ufatiliaji mifugo kwa kuweka hereni maalum sikioni zenye namba zinazotolewa na Wizara.

Alisema katika kipindi cha hivi karibuni Wilaya hiyo ilikumbwa na wimbi la wizi wa Ng'ombe ambapo ilikuwa ni vigumu kutambua kutokana na kukosa Alama  maalum za kuwatambulisha.

"Tulikuwa na changamoto ya wizi wa mifugo kwa muda mrefu sana na ilikuwa ni jambo gumu kutambua mifugo ikipotea katika kijiji kimoja na kuipata katika kijiji kingine kwa hiyo kupitia utambuzi huu utakuwa umekomesha kabisa wizi kwa sababu mifugo yote itakua inatambulika" alisema

Akizungumzia mfumo huo wa utambuzi Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ukaguzi na ustawi wa Wanyama kutoka wizara ya mifugo na uvuvi (Mifugo), Dkt. Annette Kitambi alibanisha kuwa  hereni zitakazotumika zitakuwa za kisasa ambazo zitawekwa namba na hazitachubuka.

Alisema hereni hizo zitakuwa na namba 12 zikianzia na namba ya nchi, mkoa, wilaya na kata  husika inayopatikana mifugo hiyo ambapo pia zitawekwa taarifa zote muhimu ambazo zitasajiliwa katika mtandao.

"Huu mfumo hereni zitakuwa na namba 12 ambapo katika usajili tutapiga picha ya ng'ombe na namba zilizopo katika hereni kwa hiyo kutakuwa na picha mbili ambazo zitasaidia kutambua mifugo ni ya nani na hata ikitokea imeibiwa itakuwa rahisi kupatikana kwa sababu itaweza kufuatiliwa kama zinavyofuatiliwa simu zikiibiwa" alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji nchini, Jeremiah Wambura aliishukuru Wizara kwa kuanzisha mfumo huo ambao pamoja na kusaidia katika kudhibiti wizi wa mifugo pia utasaidia Serikali kujua idadi ya mifugo iliyopo na kupanga utaratibu mzuri  wa maeneo ya malisho kutokana na mahitaji ya mifugo iliyopo.


Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Bw. Saad Mtambule akiongea na wafugaji wa Halmashauri hiyo wakati wa uzinduzi wa mwongozo wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa Mifugo Disemba 04, 2021 Mkoani Iringa. 

Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ukaguzi na ustawi wa wanyama, Dkt. Annette Kitambi akisisitiza suala la uwekaji hereni Mifugo na umuhimu wa utambuzi usajili na ufuatiliaji wa mifugo  kwa wafugaji wa Wilaya ya Mufindi wakati wa  uzinduzi wa  mwongozo huo  Mkoani Iringa. Disemba 04, 2021. 

Mwenyekiti wa wafugaji Tanzania, Bw. Jeremiah Wambura akihamasisha wafugaji kupokea zoezi la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwani lina manufaa kwao na litasaidia kudhibiti wizi na upotevu wa Mifugo yao. Disemba 04,2021 Mkoani Iringa

 


Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Bw. Saad Mtambule avalisha hereni kwenye sikio la ng'ombe wa kwanza kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi mara baada ya uzinduzi wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa Mifugo Disemba 04, 2021 Mkoani Iringa.