Nav bar

Jumapili, 5 Desemba 2021

WAFUGAJI WATAKIWA KUTUMIA MFUMO WA UTAMBUZI WA MIFUGO KIELEKTRONIKI

 

Serikali imewataka wafugaji Wilayani Mufindi kutumia vyema fursa iliyotolewa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi   ya utambuzi wa mifugo kwa mfumo wa kielektroniki ili kuondokana na changamoto ya wizi wa mifugo hiyo uliokuwa ukijitokeza mara kwa mara.

Rai hiyo ilitolewa Disemba 4, 2021 na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Bw. Saad Mtambule wakati wa uzinduzi wa zoezi la utambuzi, usajili na ufatiliaji mifugo kwa kuweka hereni maalum sikioni zenye namba zinazotolewa na Wizara.

Alisema katika kipindi cha hivi karibuni Wilaya hiyo ilikumbwa na wimbi la wizi wa Ng'ombe ambapo ilikuwa ni vigumu kutambua kutokana na kukosa Alama  maalum za kuwatambulisha.

"Tulikuwa na changamoto ya wizi wa mifugo kwa muda mrefu sana na ilikuwa ni jambo gumu kutambua mifugo ikipotea katika kijiji kimoja na kuipata katika kijiji kingine kwa hiyo kupitia utambuzi huu utakuwa umekomesha kabisa wizi kwa sababu mifugo yote itakua inatambulika" alisema

Akizungumzia mfumo huo wa utambuzi Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ukaguzi na ustawi wa Wanyama kutoka wizara ya mifugo na uvuvi (Mifugo), Dkt. Annette Kitambi alibanisha kuwa  hereni zitakazotumika zitakuwa za kisasa ambazo zitawekwa namba na hazitachubuka.

Alisema hereni hizo zitakuwa na namba 12 zikianzia na namba ya nchi, mkoa, wilaya na kata  husika inayopatikana mifugo hiyo ambapo pia zitawekwa taarifa zote muhimu ambazo zitasajiliwa katika mtandao.

"Huu mfumo hereni zitakuwa na namba 12 ambapo katika usajili tutapiga picha ya ng'ombe na namba zilizopo katika hereni kwa hiyo kutakuwa na picha mbili ambazo zitasaidia kutambua mifugo ni ya nani na hata ikitokea imeibiwa itakuwa rahisi kupatikana kwa sababu itaweza kufuatiliwa kama zinavyofuatiliwa simu zikiibiwa" alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji nchini, Jeremiah Wambura aliishukuru Wizara kwa kuanzisha mfumo huo ambao pamoja na kusaidia katika kudhibiti wizi wa mifugo pia utasaidia Serikali kujua idadi ya mifugo iliyopo na kupanga utaratibu mzuri  wa maeneo ya malisho kutokana na mahitaji ya mifugo iliyopo.


Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Bw. Saad Mtambule akiongea na wafugaji wa Halmashauri hiyo wakati wa uzinduzi wa mwongozo wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa Mifugo Disemba 04, 2021 Mkoani Iringa. 

Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ukaguzi na ustawi wa wanyama, Dkt. Annette Kitambi akisisitiza suala la uwekaji hereni Mifugo na umuhimu wa utambuzi usajili na ufuatiliaji wa mifugo  kwa wafugaji wa Wilaya ya Mufindi wakati wa  uzinduzi wa  mwongozo huo  Mkoani Iringa. Disemba 04, 2021. 

Mwenyekiti wa wafugaji Tanzania, Bw. Jeremiah Wambura akihamasisha wafugaji kupokea zoezi la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwani lina manufaa kwao na litasaidia kudhibiti wizi na upotevu wa Mifugo yao. Disemba 04,2021 Mkoani Iringa

 


Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Bw. Saad Mtambule avalisha hereni kwenye sikio la ng'ombe wa kwanza kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi mara baada ya uzinduzi wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa Mifugo Disemba 04, 2021 Mkoani Iringa. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni