Nav bar

Ijumaa, 19 Julai 2019

WAFUGAJI WA TANZANIA KUPITIA MRADI WA SAHIWAL WAZURU NCHINI KENYAWAFUGAJI wa Tanzania kupitia Mradi wa Utafiti wa uboreshaji na utunzaji wa Mbari za ng’ombe aina ya Sahiwal wako nchini Kenya kwa ziara ya mafunzo yaliyoratibiwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kwa ufadhili wa Shirika la Kimataifa la AU-IBAR.

Wafugaji hao kutoka Umoja wa Wafugaji wa Sahiwal Longido (UWASALO) wamekutana na wafugaji wa Transmara nchini Kenya wanaonufaika na ufugaji kwa kutumia teknolojia ya uhimilishaji na kuhifadhi na uendeleza nyanda za malisho ya mifugo.

Akizungumza mara baada ya kutembelea wafugaji wa ng’ombe aina ya Sahiwal katika eneo la Kilgoris - Transmara, nchini Kenya, Mratibu wa Mradi huo wa Sahiwal kutoka Tanzania, Dk. Zebron Nziku amesema ziara hiyo imekuwa na tija kubwa kwa wafugaji wa Tanzania hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali inafanya mageuzi makubwa katika uboreshaji Koosafu za Mifugo.

Dk. Nziku amesema mradi huo tayari umeendesha mafunzo yaliyohusisha wataalam na wafugaji kutoka Halmashauri ya Longido nchini Tanzania kwa ushirikiano na wafugaji wa Transmara nchini Kenya juu ya mbinu bora za uzalishaji na utunzaji wa Sahiwal.

Alisema lengo la ziara hiyo ni kutoa fursa kwa wafugaji wa Sahiwal kutoka Halmashauri ya Longido nchini Tanzania ambapo mradi huo umetekelezwa kwenda kuona na kujifunza kwa wafugaji wenzao waliofanikiwa kufuga ng’ombe wa aina hiyo kwa muda mrefu nchini Kenya ili kubadilishana uzoefu hasa katika eneo la uzalishaji kwa njia ya uhimilishaji.

Alisema mradi huo umetekelezwa kwa ushirikiano wa nchi za Tanzania na Kenya kwa lengo la kuelimisha wafugaji, namna bora na rahisi ya kuzalisha na kutunza wa ng’ombe wa Sahiwal kwa ajili ya kuongeza tija kwenye uzalishaji

Dkt. Nziku alisema Sahiwal ni ng’ombe wanaopatikana kwenye nchi zote ndani ya Afrika Mashariki (transboundary breed) na wana uwezo wa kutoa nyama nyingi na maziwa kati ya lita 14-16 kwa siku, hivyo mradi umelenga kuboresha, kuendeleza na kutunza Mbari (breed) za ng’ombe wa Sahiwal ili kuboresha maisha ya wafugaji kupitia mifugo hiyo.

Aliongeza kuwa kwa upande wa Tanzania mradi huu umefanikiwa kununua Madume bora Matatu ya Mbegu za Sahiwal ambayo kwa sasa yamehifadhiwa kwenye Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji NAIC - Arusha kwa ajili ya kutoa mbegu zitakazo wanufaisha wafugaji wengi zaidi nchini.


Wafugaji wa Tanzania na Kenya wakijadiliana kwa pamoja namna bora ya kuboresha ufugaji wao wakiwa kwenye mafunzo katika chuo cha Uchakataji Maziwa 
(DTI), Naivasha Kenya.


Wafugaji wa Tanzania na Kenya walioko kwenye mafunzo nchini Kenya wakiwa katika picha ya pamoja na Mratibu wa Mradi wa Sahiwal , Dkt. Zabron Nziku na wataalamu wengine kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi mara baada ya kutembelea chuo hicho cha uchakataji Maziwa (DTI) Naivasha KenyaSHIRIKA LA KIMATAIFA LA AU-IBAR LAFADHILI MAFUNZO YA WAFUGAJI WA TANZANIA NA KENYA.SHIRIKA la Kimataifa la AU-IBAR linalofadhili Mradi wa Utafiti wa uboreshaji na utunzaji wa Mbari za ng’ombe aina ya Sahiwal limefanikiwa kuwapeleka wafugaji wa Tanzania nchini Kenya kujifunza mbinu bora za uboreshaji mifugo.

Mradi huo unaotelekezwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) umewezesha kunufaisha wafugaji wengi wa jamii ya Kimasai katika Wilaya ya Longido Mkoa wa Arusha kuanza uboreshaji mifugo yao kupitia njia ya uhimilishaji.

Akizungumza na wafugaji katika eneo la Kiligoris na Naivasha nchini wakati wa ziara ya mafunzo kwa wafugaji wa Tanzania, Mratibu Mwenza wa mradi huo kutoka TALIRI Makao Makuu Dodoma, Neema Urassa alisema mradi huo umeleta tija wafugaji wengi hasa katika Wilaya ya Longido.

Urassa alisema katika utekelezaji wa mradi huo wafugaji mia moja kutoka wilayani Longido mkoani Arusha wamenufaika kwa kujengewa uwezo kupitia mafunzo ya utunzaji bora wa ng’ombe na ufugaji wa kibiashara wenye tija utakaowezesha wafugaji kukidhi mahitaji ya lishe ya kaya, kutoa fursa za ajira na fursa za kujikwamua kiuchumi.

Aliongeza kuwa mradi huo pia ulitoa fursa kwa wafugaji hao wa Longido kufanya ziara ya mafunzo kwa vitendo katika Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji wa Mifugo Tanzania (NAIC) mkoani Arusha ili kuona madume bora yatakayotumika kutoa mbegu za Sahiwal na jinsi kazi hiyo inavyofanywa na wataalam kituoni hapo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Uhimilishaji NAIC Arusha Dkt. Paul Mollel amesema wafugaji watumie mbinu zilizofanyiwa utafiti na mbegu za Sahiwal ili kuboresha aina ya mifugo wanayofuga na kubadilishana uzoefu juu ya matumizi mbinu bora za ufugaji utakaoharakisha uzalishaji, Wafugaji mje kwa wingi katika kituo cha NAIC Arusha ili muweze kujipatia mbegu nzuri na bora za Sahiwal kwa ajili ya kupata ng”ombe bora na wazuri na mfuge kwa tija. Alisema Dkt. Paul Mollel


Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Masoko Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Abdalla Temba alisema Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa mbegu bora zinapatikana ili kuongeza uzalishaji wa nyama na maziwa.

Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wafugaji wa Sahiwal Longido (UWASALO), Peter Lengooya Ole Kipara amezishukuru Serikali za Tanzania na Kenya na wafugaji wa nchi hizo kwa umoja na ushirikiano mafunzo hayo yameongeza undugu kati yao na kwa umoja huu wameweza kujifunza kufuga kisasa na kuleta tija.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Wafugaji wa Sahiwal upande wa Kenya, David Ole Mosingo amesema mafunzo hayo yamewawezesha kuongeza uelewa na wamekubaliana na njia hiyo ili waweze kufuga kisasa na kwa manufaa zaidi.Mratibu Mwenza wa Mradi wa Sahiwal kutoka TALIRI Makao Makuu Dodoma, Bi. Neema Urassa pamoja na Mratibu wa Mradi huo Tanzania Dkt. Zabron Nziku wakiangalia mifugo bora iliyoboreshwa kupitia mradi huo kwa wafugaji wa Transmara nchini Kenya

Mratibu Mwenza wa Mradi wa Sahiwal, Bi. Neema Urassa, akichangia hoja katika mafunzo ya wafugaji wa ng'ombe katika ukumbi wa DTI Naivasha Nchini Kenya

Mratibu Mwenza wa Mradi wa Sahiwal kutoka Taasisi ya Utafiti wa mifugo (TALIRI) Makao Makuu Dodoma, Neema Urassa akizungumza na wafugaji wa Transmara nchini Kenya wakati wa ziara ya mafunzo ya wafugaji kutoka Tanzania waliotembelea wenzao wa Kenya kwenye mradi unaofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la AU-IBAR.

Mratibu Mwenza wa Mradi wa Sahiwal kutoka TALIRI Makao Makuu Dodoma, Bi. Neema Urassa akiwa katika picha ya pamoja na wafugaji kutoka Tanzania wakiwa nje ya ukumbi wa TDI Naivasha nchini Kenya .


Jumatano, 17 Julai 2019

DENI LA TSHS BIL. 7 LAWAWEKA PABAYA WADAIWA SUGU WA NARCO
Serikali imesema wadaiwa wote waliowekeza katika ranchi za taifa zinazomilikiwa na Kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO) walipe madeni yao kabla haijachukua hatua ya kuwanyang’anya maeneo na kuwafikisha mahakamani.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema hayo jijini Dodoma katika ofisi za makao makuu ya NARCO wakati akizungumza na wawekezaji waliopatiwa vitalu 111 katika ranchi za taifa zilizopo maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kulisha mifugo yao ambapo hadi sasa wanadaiwa Tshs Bilioni Saba.

“Lipeni bila shuruti, ahadi yangu kwenu mkifanya majukumu yenu ofisi yangu itawapatia ushirikiano wa kutosha, kama mheshimiwa rais akiendelea kuniacha hapa katika wizara hii wale ambao hawalipi watakuwa wamepoteza sifa za kuwa wawekezaji na siyo kwamba itaishia hapo tutachukua hatua za kisheria na watalipa deni ili kusudi watanzania wengine wawekeze ambao wanaweza kulipa hela ya serikali, hulipi nitakuondoa tena nitakufunga.” amesema Prof. Gabriel

Prof. Gabriel ameitaka NARCO kuhakikisha makampuni matano ambayo yanadaiwa fedha nyingi zaidi zinazokaribia tshs Bilioni Moja, yalipe fedha hizo ili kuiwezesha NARCO iweze kufanya shughuli zake na kuboresha ranchi inazozisimamia.

Katibu mkuu huyo ameitaka pia NARCO kuwekeza katika ranchi zake ili wawekezaji waweze kupata huduma mbalimbali muhimu kwa ajili ya mifugo yao yakiwemo maji na malisho pamoja na kuboreha njia za mawasaliano na wawekezaji, kutengeneza mpango wa uwekezaji na mikakati ya kiusalama.

Aidha Prof. Gabriel ameutaka uongozi wa Umoja wa Wawekezaji wa Ranchi za Taifa (UWARATA) kufanya kazi kwa kufuata misingi ya kisheria ikiwemo kusajili chama chao ili kiwe na nguvu ya kusimamia wanachama wao katika kuhakikisha wanafanya kazi kwa kufuata taratibu na sheria za nchi na kuwa daraja la mawasiliano kati ya Wizara ya mifugo na Uvuvi na NARCO.

Akizungumza kuhusu deni la tshs Bilioni Saba wanalowadai wawekezaji, kwa niaba ya Kaimu Meneja Mkuu wa Narco Prof. Philemon Wambura, Meneja Masoko wa NARCO Bw. Emmanuel Mzava amesema deni hilo limedumu kwa zaidi ya miaka miwili sasa na wamekuwa wakifanya juhudi mbalimbali za kuwasiliana na wawekezaji ili waweze kulipa na katika kikao hicho kuweka mkakati wa kulipwa deni hilo.

“Baada ya kufanya kikao na katibu mkuu sisi watendaji tuliobaki hapa pamoja na wawekezaji katika vitalu vilivyopo katika ranchi za taifa, miongoni mwa mambo tunayofanya ni kuwekeana sasa kama makubaliano madogo ambayo yameandaliwa kwamba mwekezaji tunamsomea deni lake na tunakubaliana lini analipa deni lake.” Amesema Bw. Mzava.

Nao baadhi ya wawekezaji waliofika katika kikao hicho wamesema kimekuwa na manufaa makubwa kwao ili waweze kutatua changamoto zinazowakabili na kuwa na misingi mizuri ya kuendelea kumiliki vitalu walivyopatiwa na kulisha mifugo yao kwa kufuata sheria za nchi.

Kikao cha katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel, uongozi wa Kampouni ya Ranchi ya Taifa (NARCO) na wanachama wa Umoja wa Wawekezaji wa Ranchi za Taifa (UWARATA), kimefanyika ikiwa ni siku chache baada ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina kuutaka uongozi wa NARCO kubadilika na kutumia maeneo yake kwa ajili ya kuwekeza na kupata faida ili iweze kujiendesha na kutoa gawio serikalini.

Wanachama hao walioshiriki kikao hicho wanatoka katika vitalu 111 vilivyopo katika ranchi za Kagoma, Kikulula, Mabale na Kitengule zilizopo Mkoani Kagera, ranchi zingine ni Uvinza, Usangu na Kalambo zilizopo Nyanda za juu Kusini na ranchi za Mkata, Mzeri, Dakawa zilizopo Mashariki na Pwani.Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa kwenye picha ya pamoja na wawekezaji katika ranchi za taifa waliohudhuria kikao kwenye makao makuu ya NARCO jana (15.07.2019) jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na wawekezaji katika ranchi za taifa kwenye makao makuu ya NARCO jana (15.07.2019) jijini Dodoma.Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Felix Nandonde akifuatilia kikao cha Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel wakati akizungumza na wawekezaji katika ranchi za taifa kwenye makao makuu ya NARCO jana (15.07.2019) jijini Dodoma.
ZIARA YA KATIBU MKUU UVUVI DKT. RASHID TAMATAMAH MKOANI RUKWA.

Dkt. Rashid Tamatamah amesema mikakati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi hasa kwenye Sekta ya Uvuvi ni kuendeleza ufugaji samaki na kuangalia fursa za kuwekeza katika ufugaji samaki.

Hayo yamebainishwa na katibu Mkuu Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah alipofanya ziara yake leo (15/07/2019) Mkoani rukwa ya kutembelea bwawa la Ilembo, Kiwanda cha kuchakata samaki cha Migebuka Fisheries, soko la Kasanga Pamoja na kuwatembelea Watumishi wa kituo cha Doria cha Kasanga.

FURSA ZA UWEKEZAJI KATIKA UFUGAJI SAMAKI.

Serikali ipo hapa na nia yetu ni kuja na kusikiliza changamoto zinazowakabili katika suala zima la ufugaji samaki.

Serikali ipo hapa na nia yetu ni kuangalia fursa ya kukuza Tasnia ya ukuzaji viumbe maji hasa ufugaji wa samaki na kuwekeza katika malambo ambapo yakitunzwa vizuri yanaweza kutoa samaki wengi kwa wananchi.

Katibu Mkuu Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amesema hayo leo alipopata fursa ya kutembelea bwawa la Ilembo na kuongea na Wananchi wa Kijiji cha Ilembo, Katika Wilaya ya Sumbawanga.

Lengo la ziara hii ni kuja kuangalia fursa ya maeneo ya kupandikiza samaki kwenye mabwawa,alisema Katibu Mkuu Uvuvi.

Malambo yanayoweka maji mwaka mzima tunataka kuyapandikiza samaki ili wananchi waendelee kupata samaki.

Vilevile kuangalia namna Wizara itakavyotoa mchango kwa Watanzania wanaopata changamoto ya kuingia katika ufugaji samaki.

Pia Dkt. Tamatamah alieleza kuwa, watu wahamasike kufuga samaki kwenye mabwawa na wasitegemee maziwa peke yake ili kujiongezea kipato.

UDHIBITI WA UTOROSHAJI SAMAKI, KULINDA VIWANDA VYA NDANI.

Katibu Mkuu Dkt. Rashid Tamatamah amesema nia ya Mh. Raisi Dkt. John Pombe Magufuli haitafikia ya Serikali ya viwanda kama malighafi yote inakimbizwa nchi za nje.

Alisema hayo leo wakati alipotembelea Kiwanda cha kuchakata samaki cha Migebuka Fisheries kilichopo Kasanga, Wilaya ya Kalambo.

Afisa Mfawidhi kituo cha Rukwa na Katavi Bw. Juma Makongororo amesema, Nguvu kazi ikiongezeka itasaidia kudhibiti uingizaji holela wa mazao ya Uvuvi na dhana haramu za uvuvi.

UIMARISHAJI WA SOKO LA KASANGA

Sisi kama Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kipaumbele chetu ni kuimarisha miundo mbinu ya masoko ya samaki.

Alisema hayo Katibu Mkuu Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah alipotembelea Soko la samaki la Kasanga, Wilaya ya Kalambo Leo na kuongea na uongozi wa eneo hilo la soko.

Kwa niaba ya Wizara napenda kuchukua nafasi hii kushukuru Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kwa juhudi ya kuendelea kuimarisha soko la Kasanga  alisema Katibu Mkuu.

Mara nyingi kuimarisha masoko ya ndani yanaongeza thamani ya samaki na kupata soko la nje na kusaidia kukuza uchumi wa nchi.

KIKAO KAZI KITUO CHA DORIA KASANGA
Katibu Mkuu Dkt. Rashid Tamatamah alipata wasaa wa kuongea na Watumishi wa kituo cha Doria cha Kasanga na kusikiliza changamoto za kazi zinazowakabili katika maeneo yao.katibu Mkuu Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah afanya ziara yake leo (15/07/2019) Mkoani rukwa ya kutembelea kiwanda cha kuchakata Samaki cha Migebuka Fisheries kilichopo Kasanga
  katibu Mkuu Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah leo (15/07/2019) akutana na kuongea na Watumishi wa Kituo cha Doria cha Kasanga, Mkoani Rukwa


Attachments area
katibu Mkuu Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah afanya ziara yake leo (15/07/2019) Mkoani rukwa ya kutembelea bwawa la Ilembo.


ZIARA YA JPM NAMIBIA, YAWAIBUA WAWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA MIFUGO NCHINI
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amemshukuru Rais Dkt. John Magufuli kufuatia ziara yake ya kikazi ya siku mbili aliyofanya nchini Namibia kuanzia Mei 27 hadi 28 Mwaka 2019, kuanza kuonesha mafanikio baada ya kupokea ugeni kutoka Kampuni ya Burmeister and Partners (PTY) Ltd inayomikili kiwanda cha kuchakata nyama nchini Namibia iliyoonesha nia ya kuwekeza hapa nchini.

Akizungumza (09.07.2019) ofisini kwake katika mji wa serikali eneo la Mtumba Jijini Dodoma na mmoja wa wakurugenzi katika kampuni hiyo Bw. Hendrick Boshoff, Prof. Gabriel amesema lengo la ziara yake ni kupata taarifa za awali, kutoka kwa wataalam wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili waweze kuwa na njia sahihi ya uwekezaji ambao utakuwa na tija kwa watanzania kupitia Sekta ya Mifugo.

“Mheshimiwa rais alifanya ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Namibia akiambatana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina na viongozi wengine, nichukue fursa hii kwa niaba ya wizara kumshukuru mheshimiwa rais kutuanzishia suala la soko la mazao ya mifugo hususan nyama, tumetembelewa na mmoja wa wakurugenzi wa Kampuni ya Burmeister and Partners (PTY) Ltd inayomiliki kiwanda cha kuchakata nyama nchini Namibia ili kukutana na wataalam baada ya rais kuonesha muelekeo na wao wakaitikia.” Amesema Prof. Gabriel

Katika mazungumzo hayo Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo, amesema wameuhakikishia ugeni huo kutoka Namibia kuwa wizara iko tayari kupitia Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina kwa kuhakikisha nia ya kampuni hiyo kuanzisha kiwanda kingine cha kuchakata nyama hapa nchini inafikia katika utekelezaji kufuatia ziara ya mheshimiwa rais nchini Namibia.

Prof. Gabriel amefafanua kuwa ujio wa ugeni huo unaratibiwa na wizara nne zikiwemo za Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Viwanda na Biashara, Ofisi ya Waziri Mkuu eneo la Uwekezaji na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika Sekta ya Mifugo ambapo Prof. Elisante Ole Gabriel ndiye Katibu Mkuu anayeshughulikia sekta hiyo na kwamba ameupokea ugeni wa mkurugenzi wa kampuni hiyo kutoka Namibia kwa niaba ya makatibu wakuu kutoka katika wizara nyingine tatu.

Aidha, ametoa wito kwa watanzania kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali hususan zinazolenga kuongeza masoko ya kutengeneza na kuuza bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.

“Viwanda kama hivi vikija ajira nyingi zitaongezeka na pia pato la taifa litaongezeka, bado tuko chini katika ulaji wa nyama takwimu zilizotolewa na Shirika la Chakula Duniani (FAO) zinaonesha walau mtu wa kawaida anatakiwa kula kilogramu 50 kwa mwaka, bado kwa watanzania tunakula kilogram 15 kwa mwaka mzima, tunaleta wenzetu waongeze bidii katika hilo ili wazalishe na soko la ndani liwepo tuuze na nje ya nchi.” Alifafanua Prof. Gabriel

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Burmeister and Partners (PTY) Ltd inayomikili kiwanda cha kuchakata nyama nchini Namibia Bw. Hendrick Boshoff amwemambia Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel kuwa, kampuni hiyo ilianza kuendesha shughuli zake miaka 40 iliyopita na wamekuja nchini Tanzania wakilenga zaidi uwekezaji wa kuyaongezea thamani mazao ya mifugo hususan nyama.

Akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Viwanda Vidogo na Kati (DSME) Dkt. Consolata Ishebabi, amesema ugeni huo utafahamishwa pia fursa mbalimbali zilizopo hapa nchini kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) ili kufahamu mazingira mbalimbali ya uwekezaji yakiwemo ya sekta binafsi.

Aidha, Dkt. Ishebabi amefafanua kuwa ugeni huo utafikishwa pia katika Kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO) ambapo watafikishwa katika Ranchi ya Kongwa ambayo ipo chini ya NARCO kuweza kuona aina ya mifugo iliyopo nchini na waweze kupata taarifa za jumla ambazo zitawapatia mwanzo mzuri wa kuwekeza hapa nchini katika Sekta ya Mifugo.

Kikao hicho kiliwahusisha wataalam kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akiagana na kupiga picha ya pamoja na mmoja wa wakurugenzi katika Kampuni ya Burmeister na Partners (PTY) Ltd inayomiliki kiwanda cha kuchakata nyama nchini humo Bw. Hendrick Boshoff pamoja na wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Viwanda na Biashara, Ofisi ya Waziri Mkuu eneo la Uwekezaji pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
 Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika mazungumzo ofisini kwake jijini Dodoma (09.07.2019) na mmoja wa wakurugenzi katika Kampuni ya Burmeister and Partners (PTY) Ltd ya nchini Naimibia inayolimiki kiwanda cha kuchakata nyama nchini humo Bw. Hendrick Boshoff (Picha ya kwanza juu kushoto) ambaye yupo nchini kwa ajili ya nia ya kampuni hiyo kuwekeza kufuatia ziara ya Mhe. Rais Dkt. John Magufuli nchini Namibia. Bw. Boshoff alisindikizwa na Dkt. Consolata Ishebabi Mkurugenzi wa Viwanda Vidogo na Kati (DSME) (Picha ya chini kushoto) kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara.


Jumanne, 2 Julai 2019

NARCO WATAKIWA KUJIENDESHA KWA FAIDA NA KUTOA GAWIO SERIKALINI
Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeitaka Kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO) kubadilika na kufanya shughuli zake kwa tija ili iweze kunufaika na rasilimali ardhi na mifugo inayomiliki.

Akizungumza wakati akitembelea na kujionea shughuli zinazofanywa katika ranchi za Ruvu iliyopo Mkoani Pwani na Mkata iliyopo Mkoani Morogoro jana (01.07.2019), Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amezitaka ranchi hizo zilizo chini ya NARCO kuhakikisha zinatumia vitu ardhi inazomiliki ili kufuga mifugo itakayoongeza tija kwa taifa.

Prof. Gariel akiwa katika Ranchi ya Ruvu amemuelekeza meneja wa ranchi hiyo Bw. Elisa Binamungu kuhakikisha ranchi hiyo inafuatilia pia madeni yote inayodai ili iweze kupata fedha na kujiendesha kwa kutumia fursa zilizopo za kuuza kwa tija mazao ya mifugo ikiwemo nyama na maziwa.

“Lengo la ziara yangu ni kuhakikisha mnatekeleza agizo alilolitoa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina June 15 mwaka huu, alipokutana na viongozi wa NARCO la kuwataka kubadilika kiutendaji na muweze kunufaika na ardhi na mifugo mnayomiliki hali kadhalika kuweza kutoa gawio serikalini.” Alisema Prof. Gabriel.

Akiwa katika Ranchi ya Mkata Prof. Gabriel amejionea ujenzi wa kisima kwa ajili ya kupata maji ya kunyweshea mifugo na kumuagiza meneja wa ranchi hiyo Bw. Iddy Athuman kuhakikisha kisima hicho kinakamilika katika mwaka wa fedha 2019/2020 kwa kuwa ranchi hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya maji kwa mifugo.

“Ni muhimu kisima hiki kikamilike kwa kuwa maji ni uchumi mtakapokuwa na maji mengi ndivyo mtakavyoweza kuwa na mifugo kulingana na uwepo wa maji, pia kuhusu wazo lenu la kuanza kufuga ng’ombe wa maziwa ni wazo zuri hususan kisima hiki kikianza kutumika na kuwa na maji ya kutosha.” Alifafanua Prof. Gabriel.

Wakiwa katika ranchi wanazozisimamia mameneja hao wamesema watatekeleza maagizo yote kwa wakati kama yalivyoelekezwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina ili ranchi hizo za Ruvu na Mkata ziweze kunufaika kupitia rasilimali ardhi na mifugo zinazomiliki.Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Ranchi ya Mkata mara baada ya kutembelea ranchi za Ruvu na Mkata kujionea utendaji kazi wa ranchi hizo. (01.07.2019)
 Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa na Meneja wa Ranchi ya Ruvu Bw. Elisa Binamungu (Picha ya kwanza juu) na Meneja wa Ranchi ya Mkata Bw. Iddy Athuman (Picha ya kwanza chini) wakati alipotembelea ranchi hizo na kujionea shughuli mbalimbali wanazofanya. (01.07.2019)


KATIBU MKUU UVUVI AFUNGA MAFUNZO YA UFUATILIAJI UBORA NA UNADHIFU WA MAJI
Katibu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah amewataka washiriki wa mafunzo ya siku sita ya uelewa wa ufuatiliaji wa ubora na unadhifu wa maji na mazingira kuzingatia mafunzo hayo ili yawe na tija katika ukanda wa Bahari ya Hindi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam (30.06.2019) wakati wa kufunga mafunzo hayo yaliyokuwa yakifanyika katika Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI) Dkt. Tamatamah amesema mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Serikali ya Watu wa China kupitia Sino-Africa Joint Research Centre (SAJOREC) na East African Great Lakes Urban Ecology (EAGLU) kwa kushirikiana na TAFIRI yanalenga kuboresha sekta ya uvuvi nchini pamoja na nchi zinazonufaika na Bahari ya Hindi pamoja na maziwa yaliyopo nchini.

Kuhusu mafunzo hayo katibu mkuu huyo Dkt. Tamatamah amesema washiriki walipata mafunzo kupitia mihadhara iliyotolewa na wakufunzi wabobezi kutoka China na Tanzania pamoja na kukusanya takwimu kutoka mito iliyopo Mkoani Dar es Salaam na kuchakata takwimu hizo katika maabara ya TAFIRI.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu TAFIRI Dkt. Semvua Mzighani amesema kupitia mafunzo hayo Serikali ya Watu wa China, SAJOREC na EAGLU wametoa vifaa vya utafiti vyenye thamani ya Tshs Milioni 70 ambavyo vitatumika kwa tafiti za kuangalia ubora na unadhifu wa maji na mazingira kwa ujumla.

Aidha Dkt. Mzighani amesema mafunzo hayo yalishirikisha washiriki kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Ethiopia pia walikuwepo waendesha mafunzo hayo kutoka China.Vifaa vyenye thamani ya Tshs Milioni 70 vilivyotolewa katika Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI) na Serikali ya Watu wa China kwa kushirikiana na Sino-Africa Joint Research Cente (SAJOREC) na East African Great Lakes Urban Ecology (EAGLU) wakati wa mafunzo ya ufuatiliaji ubora na unadhifu wa maji pamoja na mazingira yaliyofanyika TAFIRI kwa siku sita.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah wakati akifunga mafunzo ya siku sita ya ufuatiliaji ubora na unadhifu wa maji pamoja na mazingira yaliyofanyika katika Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI) ambapo pia aliwakabidhi pia washiriki vyeti vya ushiriki wa mafunzo hayo.


x

HABARI PICHAKaimu  Mkurugenzi  Msaidizi  wa  Mazao  ya  Mifugo, Usalama  wa  Chakula  na  Lishe  Bw. Gabriel  Bura  mwenye  shati  la  mistari  (kulia),  Bw. John  Chobo  kushoto  pamoja  na picha  ya  pamoja  na  Afisa  Mfawidhi  kituo  cha  Uchunguzi  wa  Magonjwa  ya  Mifugo Mwanza  Bi. Subira  Samwel,  na  wafanyakazi  wa  kiwanda  cha  nyama  cha  Chobo  walipoenda  kutembelea  kiwanda  hicho  kilichopo  katika  Wilaya ya  Misungwi  jijini Mwanza

Bw. Gabriel  Bura Kaimu  Mkurugenzi  Msaidizi  wa  Mazao  ya Mifugo  na  Usalama wa  Chakula  na  Lishe  akishuhudia  hatua  za  uchinjaji  wa  mbuzi  kuanzia mwanzo hadi kufikia hatua ya kuwekwa kwenye chumba cha baridi tayari kwa kusafirisha  kwa wateja katika kiwanda cha Chobo Investment  alipoenda kwenye ukaguzi  jijini  Mwanza. (25.6.2019)

Kaimu  Mkurugenzi  Msaidizi  wa  Mazao  ya  Mifugo,  Usalama  wa  Chakula na Lishe  Bw. Gabriel  Bura  katika  picha  mbalimbali  alipotembelea  chuo cha mafunzo  ( DIT) tawi la  Mwanza na kujionea shughuli na mafunzo yatolewayo chuoni hapo  jijini Mwanza.(25.6.2019)


Bw. Gabriel  Bura  Kaimu  Mkurugenzi  Msaidizi  wa  Mazao  ya  Mifugo  Usalama  wa Chakula  na  Lishe  akipata taarifa mbalimbali  kutoka  kwa  mmoja  wa  walimu  wa chuo  hicho Bw. William  Lohai  alipoenda  kutembelea  chuo  hicho  jijini  Mwanza.(25.6.2019)


Jumatatu, 1 Julai 2019

WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI YAPONGEZWA KWA NIA YA KUANZISHA USHIRIKA WA WAFUGAJI WA ASILI
Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepongezwa kwa jitihada zake za kuboresha mazingira ya wafugaji nchini, baada ya kuanzisha mchakato wa uanzishwaji wa chama cha ushirika wa wafugaji wa ng’ombe wa asili.

Akifungua semina iliyowahusisha wafugaji wa ng’ombe wa asili waliopo Wilayani Tunduru, Mkoani Ruvuma katibu tawala wa wilaya hiyo Bw. Ghaibu Lingo amesema ushirika huo utakapoanzishwa itakuwa rahisi kwa uongozi wa wilaya hiyo kutatua na kuwabaini wafugaji waliopo ili waweze kusaidiwa namna ya kukua kiuchumi na kuboreshewa mazingira ya maeneo ya ufugaji.

Bw. Lingo amesema kupitia ushirikia huo pia itakuwa rahisi kwa serikali ya wilaya kufahamu idadi halisi ya ng’ombe wa asili waliopo wilayani hapo na mahitaji yanayotakiwa yakiwemo ya majosho na madawa kwa ajili ya kuwahudumia mifugo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Ugani kutoka Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani Dkt. Pius Mwambene amesema kuanzishwa kwa chama cha ushirika wa wafugaji wa ng’ombe wa asili ni kati ya malengo saba ya wizara hiyo yanayolenga kuboresha sekta ya mifugo nchini.

Dkt. Mwambene amesema ushirika huo utaweza kuwasaidia wafugaji kujiinua kiuchumi na pia serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaweza kuwatambua rasmi wafugaji hao kupitia chama hicho na kuweza kuwasaidia kupitia chama chao.

Akitoa mada kuhusu malisho bora ya mifugo mara baada ya kufunguliwa kwa semina hiyo, Afisa Mifugo kutoka Idara ya Uendelezaji wa Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo Bw. Deogratius Nholope amewataka wafugaji kuwa na ufahamu juu ya malisho bora ya mifugo yao ili iweze kuwa na afya bora na kuweza kutoa mazao bora.

Bw. Nholope amesema kupitia kuanzishwa kwa chama cha ushirika cha wafugaji wa ng’ombe wa asili katika Wilaya ya Tunduru, wafugaji watapata fursa ya kufahamu namna ya kupata malisho bora na pia kupatiwa mbegu kwa ajili ya kupanda malisho.

Naye Afisa Ushirika kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Bi. Miriam Mahuwi amewafahamisha wafugaji hao umuhimu wa ushirika kwa kuwa utawajenga kiuchumi na hatimaye kuwa na ufugaji wenye mafanikio kupitia chama hicho.

Bi. Mahuwi amesema ili kuanzishwa kwa ushirika huo ni vyema wafugaji hao wakawa katika kikundi wanachoelewana na ambao wanafanya shughuli inayofanana na kujiwekea malengo na hatimaye chama hicho mara baada ya kuanzishwa kiweze kuwapatia mafanikio kiuchumi.

Semina hiyo imewahusisha wafugaji kutoka Wilaya ya Tunduru, Mkoani Ruvuma ambao wamepatiwa vitalu na Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ili waweze kulisha mifugo yao na kuondokana na tabia ya kuhamahama kutafuta malisho.Mkurugenzi Msaidizi wa Ugani, kutoka Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani Dkt. Pius Mwambene akitoa mada kwa wafugaji juu ya umuhimu wa kuanzishwa kwa chama cha wafugaji wa ng’ombe wa asili katika Wilaya ya Tunduru, Mkoani Ruvuma. (12.06.2019)
Afisa Mifugo kutoka Idara ya Uendelezaji wa Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo Bw. Deogratius Nholope akitoa mada kwa wafugaji juu ya umuhimu wa malisho bora ya mifugo kwa wafugaji waliohudhuria semina ya uanzishwaji wa chama cha ushirika wa wafugaji wa ng’ombe wa asili katika Wilaya ya Tunduru, Mkoani Ruvuma. (12.06.2019)
Afisa Ushirika kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Bi. Miriam Mahuwi akizungumzia faida na namna ya kuanzishwa kwa ushirika kwa wafugaji waliohudhuria semina yenye lengo la kuanzishwa kwa chama cha ushirika wa wafugaji wa ng’ombe wa asili katika Wilaya ya Tunduru, Mkoani Ruvuma. (12.06.2019)


SERIKALI YADHAMIRIA KUPUNGUZA UMASKINI KUPITIA ZAO LA NGOZI
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imedhamiria kupunguza umasikini kwa kuboresha kipato cha wafanyabiashara na kuongeza ajira kwa wananchi kupitia zao la ngozi hususan ngozi itokanayo na wanyama wafugwao hapa nchini.

Hayo yamesemwa  na Mkurugenzi wa Uzalishaji Mifugo na Masoko, Dkt.Felix Nandonde wakati akifungua mafunzo ya wachunaji wa ngozi wa machinjio ya Manispaa ya Morogoro mjini humo.

Dkt.Nandonde amesema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha kuwa washiriki wanaongeza utaalamu katika uchinjaji, uchunaji, ukaushaji, uhifadhi,usafirishaji na usindikaji ili kuzalisha ngozi bora itayokuwa na thamani zaidi.

Akiongelea mchango wa zao la ngozi kwenye pato la Taifa na la mtu mmoja, mmoja, Dkt.Nandonde alisema kuwa hadi mwezi Machi mwaka 2018/19 jumla ya sh.bil.5.2 zilikusanywa kutokana na usafirishaji ngozi na bidhaa zake nje ya nchi.

Akifafanua kuhusu sheria Na.18 ya Mwaka 2008, inayosimamia biashara ya ngozi nchini, Dkt.Nandonde alisema kuwa sheria hiyo inawataka wachunaji wote wa Ngozi kupata mafunzo na kupewa leseni za uchunaji ngozi.

Akihitimisha hotuba yake mgeni rasmi, Dkt.Nandonde alisema kuwa baada ya mafunzo hayo,Wizara ina mategemeo makubwa sana kuhusu mabadiliko ya ubora wa ngozi zinazozalishwa hapa nchini.

Naye Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw.Gabriel Bura aliwataka washiriki kuzingatia mafunzo hayo ya awali na kuahidi kuwa mafunzo mengine yataendelea kutolewa nchi nzima ikiwa ni kielelezo cha serikali kuitambua na kuithamini kada hiyo.

Kwa upande wa washiriki wa mafunzo hayo wakiongea kwa nyakati tofauti wameishukuru sana serikali ya awamu ya tano kwa kuitambua na kuonyesha nia ya kuinua sekta hiyo kwa vitendo.

Aidha washiriki hao wameiomba serikali pia kuangalia uwezekano wa kuwatafutia masoko ya uhakika ili kuinua vipato vyao na kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye pato la taifa.
Mgeni rasmi,Mkurugenzi wa Uzalishaji Mifugo na Masoko, Wizara ya  Mifugo na Uvuvi, Dkt.Felix Nandonde (kushoto) akiongea na Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro Bw.John Mgalula ofisini kwake leo kabla ya kufungua mafunzo ya wachunaji wa ngozi wa machinjio ya manispaa hiyo.Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Msaidizi wa mazao ya mifugo, usalama wa chakula na lishe, Bw.Gabriel Bura.

Washiriki wa mafunzo ya wachunaji wa ngozi wa machinjio ya Manispaa ya Morogoro wakimsikiliza mgeni rasmi Dkt.Felix Nandonde (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku moja yanayofanyika mjini Morogoro  (12.6.2019).Mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Uzalishaji Mifugo na Masoko, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt.Felix Nandonde (mwenye suti) kwenye picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa mafunzo ya wachunaji wa ngozi wa machinjio ya manispaa ya Morogoro mara baada ya ufunguzi rasmi wa mafunzo hayo mjini Morogoro.


UTAYARI WA MATAIFA YETU KATIKA KUPAMBANA NA MAGONJWA YA MIFUGO.
Kwa sasa nchi ya Tanzania inauwezo wa kutengeneza dawa ya kudhibiti baadhi ya magonjwa ya mlipuko katika taasisi ya TVLA iliyopo Kibaha jijini Dar es salam, ikiwemo dawa ya ugonjwa Wa kimeta ambayo imeonekana kuwa tishio kwa Mifugo ,wanyamapori na binadamu.

Alisema hayo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega kwenye ufunguzi wa zoezi la majaribio ya udhibiti Wa magonjwa ya milipuko katika eneo la mpaka Wa Namanga unaoinganisha nchi ya Tanzania na Kenya ,utakao endeshwa kwa siku nne na wanachama Wa jumuiya iliyofanyika Mpakani Namanga.

Alieleza kuwa ,Wizara yake imejipanga vizuri dhidi ya magonjwa ya mlipuko kwa mifugo, na zoezi hili linaloendelea lipo chini ya umoja Wa afrika mashariki lakini wanashirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha utayari Wa nchi wanachama unatekelezeka,hata sasa wamefanikiwa kudhibiti ugonjwa wa Kimeta ambao una athari kwa Mifugo,wanyamapori na binadamu

Alifafanua kuwa,kuna wataalamu wakutosha wanaoshughulikia magonjwa haya pindi yanapo tokea chini ya Ofisi ya Waziri mkuu inayohusika na maafa na kueleza kuwa Mifugo ya Tanzania ni salama kwani wanapatiwa chanjo Mara kwa Mara,lakini pia tuna wataalamu wetu katika vituo hivi vya pamoja (OSBP) na katika maeneo ya mkoani

Alidai kuwa Mifugo mingi ya Tanzania inauzwa Nchi Jirani ya Kenya nakuwataka wananchi jirani wa kenya kuondoa hofu juu ya Mifugo hiyo kwani kabla haijapelekwa huko kibiashara inafanyiwa Ukaguzi na vipimo mbali mbali na wataalamu ,na endapo Mifugo akibainika kuwa na ugonjwa hawezi kusafirishwa kibiashara kwenda nchi nyingine.

Magonjwa haya yanatoka kwa Mifugo kwenda kwa wanyamapori hadi kwa binadamu hususani kimeta,tumejipanga ipasavyo,tunayo taasisi inayojihusisha na utengenezaji wa dawa ya kimeta ikiwemo taasisi ya TVLA iliyopo kibaha; alisema UlegaNaibu waziri Abdallah Ulega akitoa hotuba yake kwa ufupi kabla ya uzinduzi.
Maongezi kati ya Mawaziri kutoka Tz mara baada ya zoezi hilo kufanyika  katika mpaka wa Tanzania na Kenya, Namanga


Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhe. Adan Mohamed akisalimiana na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega mara baada ya kiwasili mpakani Namanga.