WAFUGAJI wa Tanzania kupitia
Mradi wa Utafiti wa uboreshaji na utunzaji wa Mbari za ng’ombe aina ya Sahiwal
wako nchini Kenya kwa ziara ya mafunzo yaliyoratibiwa na Taasisi ya Utafiti wa
Mifugo Tanzania (TALIRI) kwa ufadhili wa Shirika la Kimataifa la AU-IBAR.
Wafugaji hao kutoka Umoja wa
Wafugaji wa Sahiwal Longido (UWASALO) wamekutana na wafugaji wa Transmara
nchini Kenya wanaonufaika na ufugaji kwa kutumia teknolojia ya uhimilishaji na
kuhifadhi na uendeleza nyanda za malisho ya mifugo.
Akizungumza mara baada ya
kutembelea wafugaji wa ng’ombe aina ya Sahiwal katika eneo la Kilgoris -
Transmara, nchini Kenya, Mratibu wa Mradi huo wa Sahiwal kutoka Tanzania, Dk.
Zebron Nziku amesema ziara hiyo imekuwa na tija kubwa kwa wafugaji wa Tanzania
hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali inafanya mageuzi makubwa katika
uboreshaji Koosafu za Mifugo.
Dk. Nziku amesema mradi huo
tayari umeendesha mafunzo yaliyohusisha wataalam na wafugaji kutoka Halmashauri
ya Longido nchini Tanzania kwa ushirikiano na wafugaji wa Transmara nchini
Kenya juu ya mbinu bora za uzalishaji na utunzaji wa Sahiwal.
Alisema lengo la ziara hiyo
ni kutoa fursa kwa wafugaji wa Sahiwal kutoka Halmashauri ya Longido nchini
Tanzania ambapo mradi huo umetekelezwa kwenda kuona na kujifunza kwa wafugaji
wenzao waliofanikiwa kufuga ng’ombe wa aina hiyo kwa muda mrefu nchini Kenya
ili kubadilishana uzoefu hasa katika eneo la uzalishaji kwa njia ya
uhimilishaji.
Alisema mradi huo
umetekelezwa kwa ushirikiano wa nchi za Tanzania na Kenya kwa lengo la
kuelimisha wafugaji, namna bora na rahisi ya kuzalisha na kutunza wa ng’ombe wa
Sahiwal kwa ajili ya kuongeza tija kwenye uzalishaji
Dkt. Nziku alisema Sahiwal ni
ng’ombe wanaopatikana kwenye nchi zote ndani ya Afrika Mashariki (transboundary
breed) na wana uwezo wa kutoa nyama nyingi na maziwa kati ya lita 14-16 kwa
siku, hivyo mradi umelenga kuboresha, kuendeleza na kutunza Mbari (breed) za
ng’ombe wa Sahiwal ili kuboresha maisha ya wafugaji kupitia mifugo hiyo.
Aliongeza kuwa kwa upande wa
Tanzania mradi huu umefanikiwa kununua Madume bora Matatu ya Mbegu za Sahiwal
ambayo kwa sasa yamehifadhiwa kwenye Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji NAIC -
Arusha kwa ajili ya kutoa mbegu zitakazo wanufaisha wafugaji wengi zaidi
nchini.
Wafugaji wa Tanzania na Kenya wakijadiliana kwa pamoja namna bora ya kuboresha ufugaji wao wakiwa kwenye mafunzo katika chuo cha Uchakataji Maziwa
(DTI), Naivasha Kenya.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni