Nav bar

Ijumaa, 29 Mei 2020

"WATANZANIA TUNYWE MAZIWA YA HAPA NCHINI"-ULEGA




Watanzania wametakiwa kuwa wazalendo kwa kunywa maziwa yanayotengenezwa hapa nchini ili kuendeleza uchumi wa viwanda na Taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega wakati akifungua maadhimisho ya 23 ya wiki ya maziwa  Mkoani Dodoma kwa njia ya kielectronic 

"Ninaomba Sana na ninawasisitiza watanzania lazima tuwe na wivu wa maendeleo kwa ajili ya Taifa letu, lazima tuwe na uzalendo wa Taifa letu" Ulega

Pia ameongezea na kusema kuwa Mhe. Raisi wetu Dr John Joseph Pombe Magufuli ametupa Ari kubwa Sana ya uzalendo kwa kupenda vya kwetu.

Imeelezwa kuwa sekta ya Mifugo katika Pato la Taifa hapa nchini inachangia kwa asilimia saba (7%) huku asilimia thelathini (30%) ikitokana na sekta ndogo ya maziwa hivyo asilimia 1.2% ya Pato zima la Taifa inatokana na sekta ya maziwa.

Mhe. Ulega amesema  Katika mwaka 2017/2018 kulikua na jumla ya viwanda (76,) lakini hivi Sasa tunajumla ya viwanda (99) kwa hivyo tunazidi  ongezeko la viwanda vidogo,vya Kati na vikubwa 20 katika Taifa letu.

Naye Kaimu msajili wa bodi ya maziwa Dr Sophia Mlote amesema bodi ya maziwa imefanya jitihada kubwa kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali katika kuhakikisha tasnia ya maziwa inakua kwa kiasi kikubwa

Maadhimisho ya wiki ya maziwa yanakwenda sambamba na kauli mbiu isemayo "wiki ya maziwa 2020 chagua viongozi Bora kwa maendeleo ya tasnia ya maziwa"


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Abdallah Ulega akifungua rasmi Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa Kielekitroniki 2020 yaliyofanyika kitaifa Mkoani Dodoma. Maadhimisho haya ni ya 23 kufanyika tangu kuanzishwa kwa Maadhimisho haya mwaka 1997 yakiwa na lengo la kuhamasisha unywaji wa maziwa nchini kutoka wastani wa Lita 49 kwa mtu kwa mwaka hadi kufika Lita 200 kwa mtu kwa mwaka. 


Kaimu msajili wa bodi ya maziwa bi Sophia Mlote akitoa Taarifa ya tasnia ya maziwa katika ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya maziwa, na wadau wakimsikiliza kwa makini,maadhimisho hayo yalifanyika katika ukumbi wa treasure square  tarehe 28/05/2020

Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko Dkt. Felix Nandonde kwa niaba ya Katibu Mkuu (M) akimkaribisha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Abdallah Ulega kwenye Ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa Kielekitroniki yaliyofanyika kitaifa Mkoani Dodoma. 


Katibu Tawala Mkoa Ndugu, Maduka  Kessy akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mh.Abdallah Ulega mara baada ya ufunguzi rasmi wa Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa kwa njia ya Kielekitroniki jijini Dodoma,

Jumanne, 26 Mei 2020

MAAZIMIO YA MKUTANO WA MAWAZIRI WA KILIMO, USALAMA WA CHAKULA, KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (SADC jijini Dsm, (22.05.2020)




* Mkutano umetoa miezi mitatu kwa kila mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kufanya tathmini ya madhara ya ugonjwa wa Covid - 19 katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.

* Mkutano umeweka mikakati ya usalama wa chakula na lishe katika ukanda wa SADC licha ya changamoto mbalimbali.

* Mkutano umeazimia mikakati ya kulinda magonjwa yanayovuka mipaka yanayohusu mimea na wanyama na kuathiri kilimo na mifugo.

* Mikakati imewekwa kutathmini namna wavuvi wanavyoathirika na ugonjwa wa Covid - 19.

* Mikakati imewekwa kwa shughuli za uvuvi katika ukuzaji viumbe kwenye maji hususan kwa nchi zizisizokuwa na maji ya asili (maziwa, bahari na mito).

* Mkutano umeweka mikakati ya nchi wanachama wa SADC kujilinda na ugonjwa wa covid - 19.



Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina (Mb) ambaye pia Mwenyekiti wa Mawaziri wa Kilimo, Usalama wa Chakula, Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) (kulia), akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel ambaye ni mwenyekiti wa maafisa waandamizi wa SADC katika sekta hizo, wakiimba wimbo wa taifa kabla ya kuanza kwa mkutano wa SADC kwa njia ya video 'video conference' jijini Dar es Salaam. (22.05.2020) 




Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina (Mb) ambaye pia Mwenyekiti wa Mawaziri wa Kilimo, Usalama wa Chakula, Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) akizungumza na mawaziri 11 kati ya 16 wakati wa mkutano wa SADC kwa njia ya video 'video conference' jijini Dar es Salaam. (22.05.2020) 



Baadhi ya maafisa waandamizi kutoka Tanzania, wakifuatilia mkutano wa mawaziri wa Kilimo, Usalama wa Chakula, Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa njia ya video 'video conference' jijini Dar es Salaam. (22.05.2020) 



Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina (Mb) ambaye pia Mwenyekiti wa Mawaziri wa Kilimo, Usalama wa Chakula, Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) akionyesha ishara ya kuwaaga mawaziri 11 kati ya 16 wa SADC (hawapo pichani) walioshiriki  mkutano wa SADC kwa njia ya video 'video conference'. (22.05.2020) 




Picha ya pamoja ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina (Mb) ambaye pia Mwenyekiti wa Mawaziri wa Kilimo, Usalama wa Chakula, Kilimo, Mifugo na Uvuvi akiwa na baadhi ya maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Wizara ya Kilimo ambao wamehudhuria mkutano wa SADC kwa njia ya video 'video conference' jijini Dar es Salaam. (22.05.2020) 



Ijumaa, 22 Mei 2020

WAFANYABIASHARA WATAKIWA KUTHAMINI SOKO LA NYAMA.






Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewataka wafanyabiashara wanaouza nyama nchini kutopandisha bei ya nyama kipindi hiki cha sikukuu ya Eid El Fitr  ili kuhakikisha kila mwananchi anapata kitoweo hicho.



Akizungumza (18.05.2020) jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri Mhe.Ulega amemtaka pia Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Bw. Jumanne Shauri ndani ya siku saba kuhakikisha wanawapeleka wafanyabiashara wanaofanya biashara katika machinjio ya vingunguti kujionea eneo jipya lililotengewa na Manispaa ya ilala.



Mhe. Ulega amebainisha hayo wakati akikagua ujenzi wa mradi wa machinjio ya kisasa katika eneo la vingunguti katika Manispaa ya Ilala, ambapo amesisitiza wafanyabiashara wa nyama wanapaswa kuuza nyama kwa bei ya kawaida kulingana na hali ilivyo ili kuhakikisha watu wote wanapata kitoweo hicho.



Aidha amesema imekuwa ni kawaida kwa wafanyabiashara wa Nyama kupandisha bei kipindi cha sikukuu kinapofika hali inayosababisha  wananchi kutopata nyama kulingana na bei kuwa juu.



"Serikali ya awamu ya tano inatengeneza uchumi endelevu hivyo katika kuhakikisha hili wafanyabiashara wa nyama wanatakiwa kuchangamkia fursa ya sikukuu ya Eid El kuuza nyama kwa bei ya kawaida na sio ya kuwaumiza wananchi," amesema Mhe. Ulega.



Kuhusu mradi wa machinjio ya kisasa ya vingunguti ambapo hadi sasa umefikia asilimia 85 ya ukamilikaji wake, Mhe. Ulega amesema mradi huo unaogharimu kiasi cha Sh.Billioni 12.4 ambao unalengo la kuhakikisha wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam, mikoa mingine na nchi za nje kupata nyama itakayokuwa bora na yenye kuandaliwa vizuri kutokana na jengo hilo.



"Wizara yangu ndiyo inashughulikia masuala ya mifugo natoa pongezi kwa serikali kwa hatua hii ya kufikisha jengo hili katika kiwango cha juu kwani kiwanda pekee kinachotusaidia kwa sasa kipo Mwanza, Chobo Investmest hivyo kupitia kiwanda hiki naamini tutaongeza nguvu katika uuzaji wa nyama." Ameongeza Mhe. Ulega



Hata hivyo Mhe. Ulega amesema uwekezaji wa mradi huu utailipa serikali katika hatua zote ikiwemo kiuchumi na kijamii pindi shughuli za mnada zitakapoanza kufanyika katika jengo hilo.



Naibu waziri huyo amesema Tanzania bado ina fursa nyingi katika mifugo na serikali tayari ina mikakati mizuri ya kuhakikisha sekta hii inazidi kukua siku hadi siku na kutoagiza nyama nje ya nchi.



"Bado tuna fursa nyingi katika kuhakikisha nyama inapatikana kwa wingi na tutaacha ununuaji wa nje ya nchi pindi mradi huu utakapokamilika na tutahakikisha sisi ndio tunawapelekea watu wa  nchi nyingine" amesema Mhe. Ulega



Amesema eneo hilo litachinja ng'ombe takriban 1,500 na mbuzi 1000 kwa siku moja pindi itakapokamilika hivyo upandishaji holela wa bei ya nyama kwa vipindi vya sikukuu hautakuwepo tena kutokana na nyama kupatikana kwa urahisi zaidi.



Pia amesema kwa wafanyabiashara wa machinjio hayo wanaofanya biashara, tayari wamepatiwa eneo ambalo watajengewa na kufanya shughuli zao karibu na eneo hilo kama kawaida.



"Najua kuna watu wanajiuliza kuhusu wakinamama na vijana wanaofanya kazi hapa, Manispaa ya Ilala imeshawatafutia eneo na ni zuri lipo karibu na machinjio haya ya kisasa litawapa fursa ya kuendelea kufanya shughuli zenu, ninamuagiza Mkurugenzi wa Manispaa kuwapeleka wafanyabiashara na kuliona hilo eneo." amesema Ulega



Wakati huo huo Mhe. Ulega amempongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa hotuba yake aliyotoa juzi ambapo wafugaji na wavuvi wamempongeza kwani bila kutoka kwao hawawezi kupata kipato.



Pia amesema maono ya Rais Magufuli ni ya kizalendo, Kiutu na kuwainua wananchi wake hivyo watendaji katika nyanja mbalimbali wanapaswa kutomuangusha ili kuifikisha nchi katika uchumi wa juu.



Kwa Upande wake Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama nchini, Bw. Imani Sichalwe amesema kupitia mradi huo wafugaji watapata masoko makubwa na kutoingiliwa na madalali ambao kwa asilimia kubwa walikuwa wanawapunja.



Amesema ni wakati wa wafugaji kujipanga na kuanza kufuga kisasa kwa kuongeza ubora na kuwaongezea thamani mifugo yao.


"Wafugaji wataunganishwa moja kwa moja na watu wa mradi hivyo hawatawatumia tena madalali, kinachotakiwa wafugaji wanenepeshe mifugo yao iwe tayari kwa kuuza," amesema Bw. Sichalwe





Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (wa pili kutoka kushoto) akisikiliza kwa makini maelekezo ya ramani ya jengo la machinjio ya Vingunguti Wilaya ya Ilala mkoani Dar es salaam. (18/05/2020) 
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (wa pili kutoka kushoto) atembelea machinjio ya Vingunguti Wilaya ya Ilala jijini dar es salaam. (18/05/2020) lengo likiwa ni pamoja na kuimiza ukamilishwaji wa mradi huo.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) atembelea machinjio mpya inayojengwa Vingunguti Wilaya ya Ilala Mkoani Dar es salaam.


UKIFUGA KISASA HUWEZI KULALA NJAA. - MRUTTU





Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Hassan Mruttu amesema wafugaji wakifuga kisasa kwa kunenepesha na kuvuna mifugo yao ni rahisi kupata masoko ndani na nje ya nchi kwani watu wengi wanategemea bidhaa za ng'ombe.



Ameyasema hayo wakati akiongea na  wafugaji kwenye kijiji cha Nkerenge Wilaya ya  Misenyi Mkoani Kagera, (12/05/2020) Dkt. Mruttu amesema faida kuu za kufuga kwa mkakati ni pamoja na kupata masoko ya uhakika kutokana na  ng'ombe atakuwa akijiuza na sio kutafuta mnunuzi kwani  muonekano wake tuu utamvutia mnunuzi.



" Biashara ya mifugo ni nzuri na inafaida sana kwani mfugaji hawezi kulala njaa hata siku moja, inamuwezesha mfugaji kuvuna, kuuza na kufanya mambo ya maendeleo." Amesema Dkt. Mruttu



Aidha Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti Tanzania (TALIRI) Bi. Neema Urassa amehimiza wafugaji kuendelea kuwekeza kwenye lishe bora ya ng'ombe na kufuga kwa kufuata kanuni bora za ufugaji ili kupata faida zaidi na kuwataka wafugaji wanaofuga kwa kutumia mfumo huria kufuga ng'ombe katika eneo kwa kuzingatia uwiano wa idadi ya ng'ombe na malisho.



" Hii itachochea uwezo wa ng'ombe kuzalisha mazao bora ya Nyama, maziwa, ngozi na bidhaa zitokanazo na usindikaji wa mazao hayo  kupata soko la uhakika" Amesema Bi Neema



Hata hivyo Bi. Neema ameongeza kuwa ng'ombe ni kama kiwanda kwani ana uwezo wa kula na kutunza chakula (nyasi na vyakula vingine) na kuvibadilisha kuwa nyama, maziwa, ngozi na mbolea kwa ajili ya matumizi ya binadamu.



" Kinyesi cha ng'ombe ni chanzo cha nishati ya bayogesi kwa matumizi mbalimbali ya nyumbani na kuwa faida hizi zote zinampatia mfugaji uwezo wa kuongeza pato la kaya na kuchangia katika ukuaji wa uchumi.



Naye Mtafiti kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Atupele Mohammed amewapongeza wafugaji kwa kukubali na kutumia fursa ya uhimilishaji kwani kwa kufanya hivyo kasi ya uzalishaji wa mifugo yenye ubora itaongezeka.



"Wafugaji mmeonyesha mfano mzuri kwa mamna mnavyozingatia kanuni za afya kwa kuwa, karibu kila kaya imeweka maji na sabuni kwa ajili ya kusafisha mikoni kwa kila mtu anayeingia na kutoka katika maboma yenu." Amesema Bi. Atupele



Pia Bi Atupele  amewaeleza kwamba Wizara ya Mifugo na Uvuvi inajali afya na suala zima la kujikinga na maambukizi ya virusi vya korona hivyo imetoa vitakasa mikono kwa kila kaya iliyoshiriki katika mafunzo.



Aidha Mfugaji wa  kijiji cha Nkerenge Wilaya ya Misenyi Mkoani Kagera ambaye pia amepata fursa ya kuhimilisha ng'ombe zaidi ya sitini  ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi na  Serikali kwa kuona umuhimu wa kupeleka huduma hiyo kijijini kwao na  kuiomba Wizara hiyo kuwasaidia kupata madawa na chanjo kwa wakati, kupatiwa elimu, wataalam wa malisho, na kuanzisha utaratibu wa kopa ng'ombe lipa  ng'ombe ambao utamsaidia Mfugaji kupata maziwa, kuuza na kuweza kuendesha maisha yake.

Mfugaji wa kijiji cha Nkerenge kata ya Mtukula Wilaya ya Misenyi Mkoani Kagera Bw. Majid Kayondo ambae pia alipata fursa ya kuhimilisha mifugo yake ameishukuru Wizara ya mifugo na Uvuvi na Serikali kwa ujumla kwa kuweza kuwafikia na kuwahamashisha juu ya ufugaji bora na wenye tija. Aidha ameiyomba serikali kuwajengea Barabara ya kuingia mnadani, kupatiwa madawa kwa wakati, kupatiwa elimu ya malisho na kurudisha utaratibu wa kopa ng'ombe lipa ng'ombe. (12/05/2020) 

Zoezi la Uhamasishaji na uelimishaji wa wafugaji ukiendelea kwenye boma la Bw. Majid Kayondo Kata ya Mtukula  kutoka kwa watafiti wa wizara ya mifugo na Uvuvi leo Mkoani Kagera. (12/05/2020) 




PROF. GABRIEL ATOA TAHADHARI YA CORONA KWA WAFANYAKAZI






Mwenyekiti wa baraza la Wafanyakazi Sekta ya Mifugo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel, amewataka watumishi wa Sekta ya Mifugo kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya virusi vya corona kwa kufuata maagizo yanayotolewa na wataalamu wa afya huku wakiendelea kuchapa kazi kwa bidii.



Akizungumza na wajumbe wa baraza la wafanyakazi kwenye kikao cha baraza la wafanyakazi kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya jiji la Dodoma leo,  Prof. Gabriel amesema 'Janga hili ni la kimataifa na kwa vyovyote vile mmesikia katika nchi mbalimbali."



Amesema "Kwa niaba ya sekta ya mifugo wafugaji wote wa Ng'ombe zaidi ya milioni 32.5 na Mbuzi ambao wako zaidi ya milioni 20 na kondoo zaidi ya milion 5.5, kuku zaidi ya milion 79 kwa kweli tunamshukuru sana Dkt. John Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchukua uamuzi mzito wa kutoipeleka nchi kwenye kufungiwa watu kukaa nyumbani (Lockdown).



Vilevile, amesema watumishi wanatakiwa kufanya mambo matatu, ya tahadhari, maombi ba na kuchapa kazi kwa bidii.



"Baadhi ya watu pengine hawafahamu, lakini kwenye sekta ya mifugo kuna athari ambayo tungeipata, sidhani hata kama tungeweza kuziba pengo hilo," Amesema Prof. Gabriel



"Hata hivyo kwenye sekta ya mifugo nyama zinazoliwa ni zaidi ya kilo za nyama  2,628,000 maana yake ingefanyika Lockdown na hizo nyama zisingeliwa na maziwa yanayonyweka ni lita 8,352,000 kwa maana pia maziwa hayo yasingenyweka.



Ameongezea kuwa fursa kubwa kwa wafugaji kufuga kisasa na kuwa na mifugo yenye tija na mahitaji yanapotokea ndani ya nchi huko duniani kunawezekana  kutumia hiyo kama fursa ya kuweza kupata mahitaji ya chakula.



Amewaasa pia watumishi kufanya kazi kwa uadilifu na watumishi wazembe, wavivu na wabadhilifu hawatakuwa na nafasi katika sekta ya mifugo, akawasihi watumishi kufuata sheria, taratibu na kanuni za nchi na kuendelea na ushirikiano maana ni jambo la muhimu sana.



Ameongeza kuwa watumishi wa sekta ya mifugo wasikubali wafugaji waonewe na kupondwa haki yao na mtu yoyote na kwa namna yoyote.



Kwa upande wa ufugaji, wafugaji kote nchini we wametakiwa kufuata sheria, taratibu na kanuni bila kukosea chochote na bila kujidanganya kwamba kuna watu wa kuwatetea pale wanapokiuka sheria kwa makusudi.



Mwenyekiti wa baraza la wafanyakazi sekta ya mifugo ambae pia ni Katibu Mkuu wizara ya Mifugo na Uvuvi(mifugo) Prof, Elisante Ole Gabriel, akiongea na wajumbe wa baraza hilo (hawapo pichani) Kuhusu mambo ya kiutendaji kazi katika kipindi hiki cha  maambukizi ya virusi vya  Corona, na kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Covid 19, katika kikao cha baraza la wafanyakazi kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya jiji l Dodoma leo tarehe 12/05/2020. 

Bwana Andrew Ponda, akitoa neno la shukrani mara baada ya kuchaguliwa kuwa Katibu wa baraza la wafanyakazi sekta ya Mifugo na Msaidizi wake Bi Suzan Silayo, leo  tarehe 12/05/2020 katika kikao cha baraza la wafanyakazi kilichofanyika Kwenye ukumbi wa Halamashauri ya jiji la Dodoma. 


Katibu Mkuu wa wizara ya mifugo na uvuvi, sekta ya mifugo katikati akiwa ni Mwenyekiti wa baraza la wafanyakazi Prof, Elisante Ole Gabriel kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza hilo , mara baada ya kumaliza kikao cha Baraza la wafanyakazi kilichifanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma leo tarehe 12/05/2020. 




WAFUGAJI WAELEZWA UMUHIMU WA UHIMILISHAJI.





Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Hassan Ally Mruttu ameongoza zoezi la utoaji mafunzo ya umuhimu wa uhimilishaji na faida ya zoezi hilo kwa  wafugaji Mkoani Kagera.



Akiongea wakati wa mafunzo elekezi ya uhamasishaji wa umuhimu wa uhimilishaji wa ng'ombe kwenye kijiji cha Kagenyi Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera Jana (10/05/2020) Dkt. Hassan Mruttu amesema lengo la mafunzo hayo ni kutaka wafugaji kufuga kwa kuongezea thamani ng'ombe wao.



"Ufugaji wa kisasa unawezesha mfugaji kupata ng'ombe wengi na bora wwnaokuwa kwa haraka na kutoa maziwa na nyama kwa wingi kuliko ng'ombe wasioboreshwa." Amesema Dkt. Mruttu.



Aidha ametoa wito kwa wafugaji kusaidiana na kupeana taarifa za upandikizaji wa mbegu bora za ng'ombe (uhimilishaji) ili wafugaji wengi waweze kufikiwa na huduma hiyo.



Naye mtafiti wa Mifugo, Bi. Neema Urassa kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) amewaelekeza  wafugaji kuwa pamoja na uhimilishaji wa ng'ombe kwa kutumia mbegu za ng'ombe walioboreshwa  ni muhimu wafugaji kubadili mtizamo na kukubali  kufuga kibiashara na kuzingatia uvunaji wa ng'ombe kwa msimu unaofaa.





Aliongeza kuwa uzalishaji wa ng'ombe bora na bidhaa zake utachangia katika kukidhi mahitaji ya lishe bora ya kaya na upatikanaji wa malighafi za viwanda.



Kwa upande wake afisa mifugo wa Wilaya ya kyerwa Mkoani Kagera Bw.  Fred Kija amewasihi wafugaji kuendelea kupeana taarifa za uhimilishaji ili kusaidia wafugaji wengi kuweza kufikiwa na kupata huduma iyo



Hata hivyo mwenyekiti wa wafugaji kijiji cha Kaitambuzi Bw. Charles Bwanakunu ameelezea changamoto wanazozipata ikiwa ni pamoja na serikali ya kijiji  kuchukua ardhi yao na kumuomba  Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina na  serikali kwa ujumla kuwasaidia kutatua changamoto hiyo ili wafugaji wa kyerwa waweze kupata haki yao na kufanya kazi zao bila usumbufu.



Aidha ameishukuru serikali kwa kuweza  kuona umuhimu wao kama wafugaji na kuwafikia kwa kuwapa elimu ya ufugaji wa kisasa, uhimilishaji, kuvuna na kufuga kibiashara na kuahidi kufanya kazi maarifa hayo yaliyoyapa.

Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (wa kwanza kulia) Dkt. Ally Hassan Mruttu akitoa elimu ya umuhimu na faida za uhimilishaji kwa wafugaji na wasaidizi wao kwenye shamba la KMC LTD linalosimamiwa na  Bw. Elias Leopold Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera. (10/05/2020) 

Mtafiti kutoka TALIRI Bi. Neema Urassa (wa pili kutoka kulia) akimuelimisha mfugaji faida ya  kuongeza thamani kwa mifugo,  kufuga kibiashara na kuvuna mifugo yake ili iweze kuwa na tija kwake na kumuongezea kipato jana katika Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera. (10/05/2020) 

Watafiti  kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakiangalia mifugo iliyotengwa kwa ajili ya  zoezi la uhimilishaji kwenye shamba la KMC LTD wilayani Kyerwa Mkoani Kagera. (10/05/2020)