Kaimu Mkurugenzi wa
Utafiti na Mafunzo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Hassan Mruttu amesema
wafugaji wakifuga kisasa kwa kunenepesha na kuvuna mifugo yao ni rahisi kupata
masoko ndani na nje ya nchi kwani watu wengi wanategemea bidhaa za ng'ombe.
Ameyasema hayo wakati
akiongea na wafugaji kwenye kijiji cha Nkerenge Wilaya ya Misenyi
Mkoani Kagera, (12/05/2020) Dkt. Mruttu amesema faida kuu za kufuga kwa mkakati
ni pamoja na kupata masoko ya uhakika kutokana na ng'ombe atakuwa
akijiuza na sio kutafuta mnunuzi kwani muonekano wake tuu utamvutia
mnunuzi.
" Biashara ya
mifugo ni nzuri na inafaida sana kwani mfugaji hawezi kulala njaa hata siku
moja, inamuwezesha mfugaji kuvuna, kuuza na kufanya mambo ya maendeleo."
Amesema Dkt. Mruttu
Aidha Mtafiti
kutoka Taasisi ya Utafiti Tanzania (TALIRI) Bi. Neema Urassa amehimiza wafugaji
kuendelea kuwekeza kwenye lishe bora ya ng'ombe na kufuga kwa kufuata kanuni
bora za ufugaji ili kupata faida zaidi na kuwataka wafugaji wanaofuga kwa
kutumia mfumo huria kufuga ng'ombe katika eneo kwa kuzingatia uwiano wa idadi
ya ng'ombe na malisho.
" Hii itachochea
uwezo wa ng'ombe kuzalisha mazao bora ya Nyama, maziwa, ngozi na bidhaa
zitokanazo na usindikaji wa mazao hayo kupata soko la uhakika"
Amesema Bi Neema
Hata hivyo Bi. Neema
ameongeza kuwa ng'ombe ni kama kiwanda kwani ana uwezo wa kula na kutunza
chakula (nyasi na vyakula vingine) na kuvibadilisha kuwa nyama, maziwa, ngozi
na mbolea kwa ajili ya matumizi ya binadamu.
" Kinyesi cha
ng'ombe ni chanzo cha nishati ya bayogesi kwa matumizi mbalimbali ya nyumbani
na kuwa faida hizi zote zinampatia mfugaji uwezo wa kuongeza pato la kaya na kuchangia
katika ukuaji wa uchumi.
Naye Mtafiti kutoka
Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Atupele Mohammed amewapongeza wafugaji kwa
kukubali na kutumia fursa ya uhimilishaji kwani kwa kufanya hivyo kasi ya
uzalishaji wa mifugo yenye ubora itaongezeka.
"Wafugaji
mmeonyesha mfano mzuri kwa mamna mnavyozingatia kanuni za afya kwa kuwa, karibu
kila kaya imeweka maji na sabuni kwa ajili ya kusafisha mikoni kwa kila mtu
anayeingia na kutoka katika maboma yenu." Amesema Bi. Atupele
Pia Bi Atupele
amewaeleza kwamba Wizara ya Mifugo na Uvuvi inajali afya na suala zima la
kujikinga na maambukizi ya virusi vya korona hivyo imetoa vitakasa mikono kwa
kila kaya iliyoshiriki katika mafunzo.
Aidha Mfugaji wa
kijiji cha Nkerenge Wilaya ya Misenyi Mkoani Kagera ambaye pia amepata fursa ya
kuhimilisha ng'ombe zaidi ya sitini ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi
na Serikali kwa kuona umuhimu wa kupeleka huduma hiyo kijijini kwao
na kuiomba Wizara hiyo kuwasaidia kupata madawa na chanjo kwa wakati, kupatiwa
elimu, wataalam wa malisho, na kuanzisha utaratibu wa kopa ng'ombe lipa
ng'ombe ambao utamsaidia Mfugaji kupata maziwa, kuuza na kuweza kuendesha
maisha yake.
Zoezi la Uhamasishaji na uelimishaji wa wafugaji
ukiendelea kwenye boma la Bw. Majid Kayondo Kata ya Mtukula kutoka kwa
watafiti wa wizara ya mifugo na Uvuvi leo Mkoani Kagera. (12/05/2020)
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni