Nav bar

Alhamisi, 14 Januari 2021

KIKAO KAZI CHA KUANDAA MWONGOZO WA KUSIMAMIA RASILIMALI ZA UVUVI KWENYE MAJI MADOGO NA MAENEO OEVU NCHINI


Kaimu Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi, Bw. Amosi Machilika akisoma hotuba kwa niaba ya Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah wakati wa kikao kazi cha kuandaa mwongozo wa kusimamia Rasilimali za Uvuvi kwenye maji madogo na maeneo oevu nchini kwenye ukumbi wa Chuo cha mipango jijini Dodoma. 14/01/2021


Kaimu Mkurugenzi wa Uvuvi, Bi. Merisia Sebastian Mparaza akieleza lengo la kuandaa mwongozo wa kusimamia Rasilimali za Uvuvi kwenye maji madogo na maeneo oevu nchini wakati wa kikao hichi kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi leo kwenye ukumbi wa Chuo cha mipango jijini Dodoma. 14/01/2021

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Dkt. Ismail Kimirei akichangia mada wakati wa kikao cha kuandaa mwongozo wa kusimamia Rasilimali za Uvuvi kwenye maji madogo na maeneo oevu nchini wakati wa kikao hichi jijini Dodoma. 14/01/2021

 


Mkurugenzi wa Idara  ya Utafiti, Mafunzo na Ugani  Sekta ya Uvuvi, Dkt. Erastus Mosha akichangia hoja kwenye kikao kazi cha kuandaa mwongozo wa kusimamia Rasilimali za Uvuvi kwenye ukumbi wa Chuo cha mipango jijini Dodoma leo 14/01/2021


Kaimu Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi, Bw. Amosi Machilika ( wa pili kutoka kulia mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa kikao cha kuandaa mwongozo wa kusimamia Rasilimali za Uvuvi kwenye maji madogo na maeneo oevu nchini mara baada ya kikao hichi kwenye ukumbi wa  Chuo cha mipango jijini Dodoma. (14/01/2021)


WALIOKAIDI MKATABA WA NARCO KIKAANGONI NDANI YA SIKU KUMI

Na. Edward Kondela


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ametoa siku kumi kwa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kubaini na kuwanyang’anya maeneo, wawekezaji waliopatiwa vitalu katika ranchi za taifa ambao wamebadili matumizi ya ardhi kinyume na makubaliano ya mikataba yao.


Waziri Ndaki amebainisha hayo jana (12.01.2021) wakati alipotembelea Ranchi ya Usangu iliyopo Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya alipokuwa kwenye ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo na kufanya mkutano wa hadhara na baadhi ya wawekezaji, wakulima na wafugaji, ambao wanafanya shughuli zao katika ranchi hiyo na kubaini kuwa baadhi ya wawekezaji waliopatiwa vitalu na NARCO kwa ajili ya kufuga na kulima malisho ya mifugo wamekuwa wakikodisha maeneo hayo kwa wakulima na wafugaji kinyume na mkatabata.


“NARCO siku kumi nadhani zinawatosha kubaini watu wanaojiita wawekezaji, waliobadilisha matumizi ya ardhi ambayo siyo kufuga wala malisho wanyang’anywe maeneo kwa kuwa wameenda kinyume na utaratibu wa mkataba kati yao na NARCO, na mimi nitafuatilia nitapenda kupata taarifa mmepata wangapi na wangapi wamenyang’anywa kwa kuwa wameenda kinyume na utaratibu waliokubaliana.” Amesema Mhe. Ndaki


Waziri Ndaki amelazimika kutoa kauli hiyo baada ya kupata taarifa kutoka kwa baadhi ya wakulima na wafugaji wa Wilaya ya Mbarali kuwa wamekuwa wakikodishwa maeneo ya ranchi hiyo na wawekezaji kwa shilingi elfu ishirini kwa hekari moja kwa ajili ya kilimo na madebe kumi ya nafaka baada ya mavuno kwa kila hekari moja, huku wafugaji wakilipa takriban shilingi milioni mbili kwa hekari moja katika kipindi cha miezi minne kwa ajili ya kulisha mifugo yao kwenye maeneo ya wawekezaji ambao wamepatiwa vitalu na NARCO kwa mkataba wa kufuga au kulima malisho ya mifugo.


Amefafanua kuwa mkataba wa NARCO na wawekezaji kwa ajili ya kufugia mifugo na kulima malisho hauruhusu wawekezaji kukodisha eneo kwa mtu mwingine kwa ajili ya shughuli zozote kwa kuwa maeneo ya ranchi za taifa ni mali ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO).


Kuhusu deni la zaidi ya Shilingi Bilioni Sita ambalo NARCO inawadai wawekezaji waliopatiwa vitalu katika ranchi za taifa zilizopo kwenye maeneo mbalimbali nchini, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ameutaka uongozi wa NARCO kufikia Tarehe 15 Mwezi Februari Mwaka 2021 saa saba mchana awe amepata taarifa ya wawekezaji waliolipa madeni yao pamoja na ambao bado hawajalipa, kabla ya kuchukuliwa kwa hatua zaidi.


“Wawekezaji wote ambao tunawadai hapa Usangu na kwenye ranchi zingine wote walipe pesa ya NARCO tulipokubaliana kwenye mkataba tulikubaliana mtalipa pesa, mlipe madeni yenu ifikapo tarehe 15 mwezi februari saa saba mchana muwe mmelipa madeni yenu tunataka NARCO ijiendeshe kibiashara, lakini sioni tukielekea kwenye kujiendesha kibiashara na moja ya matatizo yanayotufanya tusifike huko ni kulea watu wa namna hii.” Amefafanua Mhe. Ndaki.


Ameongeza kuwa wale ambao hawatakuwa wamelipa hadi kufikia muda huo wanyang’anywe maeneo hayo ili wapatiwe watu wengine ambao wataweza kulipa kwa mujibu wa mkataba ili NARCO iweze kufikia malengo yake na kulalamika kuwa NARCO imechelewa kuchukua hatua kwa watu ambao wamekuwa na madeni ya siku nyingi.    


Amesema kuwa wizara imefanya tathmini juu ya madeni hayo na kuagiza yalipwe katika viwango na tozo mpya zilizowekwa kwa sababu imejiridhisha kwamba kwa gharama hizo NARCO itaweza kujiendesha na kuhudumia vizuri ranchi zake.


Kwa mujibu wa taarifa ya NARCO iliyotolewa na Kaimu Meneja Mkuu wa kampuni hiyo Bw. Masele Mipawa, maeneo ya vitalu katika ranchi za taifa yanayokodishwa kwa wawekezaji yamegawanywa katika viwango vitatu, ambapo kiwango cha chini ni Shilingi 3,500/= kwa hekari moja kuanzia eneo lenye hekta 1 hadi 2000, kiwango cha kati ni Shilingi 5,500/= kwa hekari moja kuanzia eneo lenye hekta kuanzia hekta 2001 hadi 5000 na kiwango cha juu ni Shilingi 7,500/= kwa hekari moja kuanzia eneo lenye hekta zaidi ya 5001.


Aidha Waziri Ndaki, amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuangalia namna ya kukodisha maeneo ya ranchi za taifa kwa wakulima ambao wanaweza kulima malisho ya mifugo ili kuondokana na migogoro ya wakulima kupata maeneo kwa ajili ya kilimo ili kujikwamua kiuchumi.


Amesema ni muda muafaka kwa wizara kuangalia namna wananchi wanavyoweza kutumia maeneo hayo kwa ajili ya tija kwa taifa badala ya kusubiri wawekezaji ambao baadhi yao wamekuwa wakienda kinyume na makubaliano ya mikataba na kuwafanya wananchi wanaoishi karibu na ranchi za taifa kukosa maeneo kwa ajili ya kufanya shughuli zao za kiuchumi.


Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema atahakikisha anasimamia maelekeo yote yaliyotolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki likiwemo la wawekezaji kulipa madeni ya vitalu walivyokodishwa ili Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) inayomiliki maeneo hayo iweze kujiendesha kibiashara kama moja ya malengo ya kampuni hiyo kupitia maeneo yake.


Katika mkutano huo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki na baadhi ya wakulima, wafugaji na wawekezaji wanaofanya shughuli zao kwenye Ranchi ya Usangu iliyopo Wilaya ya Mbarali, Bibi Uliya Mahenge amemuomba Waziri Ndaki kuwapatia wakulima maeneo kwenye ranchi za taifa ili waweze kujikwamua kiuchumi kupitia kilimo huku wakilipa kodi ya serikali ya maeneo hayo watakayokidishwa kama ambavyo wafugaji wanavyopatiwa vitalu kwa ajili ya kufugia mifugo kwenye ranchi hizo.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amemaliza ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Mbeya ambapo katika ziara hiyo alikuwa na lengo la kufahamu changamoto zilizopo kwenye Ranchi ya Usangu ambayo ni moja ya ranchi zinazomilikiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ambayo ipo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (aliyesimama), akizungumza na baadhi ya wakulima na wafugaji wanaofanya shughuli zao kwenye Ranchi ya Usangu iliyopo Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya, pamoja na baadhi ya wawekezaji waliopatiwa vitalu katika ranchi hiyo wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo. Kulia kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel na kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Mhe. Reuben Mfune. (12.01.2021)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (kulia), akielekezwa jambo na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel wakati wa kikao na baadhi ya wakulima na wafugaji wanaofanya shughuli zao kwenye Ranchi ya Usangu iliyopo Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya, pamoja na baadhi ya wawekezaji waliopatiwa vitalu katika ranchi hiyo. Waziri Ndaki amefanya ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo ili kutambua changamoto zilizopo kwenye Ranchi ya Usangu na kuzitafutia ufumbuzi. (12.01.2021)

Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) Bw. Masele Mipawa akitoa taarifa ya madeni ya wawekezaji waliopatiwa vitalu kwenye ranchi za taifa zilizopo maeneo mbalimbali nchini wakati wa kikao cha Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki na baadhi ya wakulima na wafugaji wanaofanya shughuli zao kwenye Ranchi ya Usangu iliyopo Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya, pamoja na baadhi ya wawekezaji waliopatiwa vitalu katika ranchi hiyo. Bw. Mipawa amesema NARCO inawadai wawekezaji zaidi ya Shilingi Bilioni Sita. (12.01.2021)

Picha ya pamoja ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel na baadhi ya wakulima na wafugaji wanaofanya shughuli zao kwenye Ranchi ya Usangu iliyopo Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya, pamoja na baadhi ya wawekezaji waliopatiwa vitalu katika ranchi hiyo. Waziri Ndaki amemaliza ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Mbeya kwa kuwataka wawekezaji waliopatiwa vitalu katika ranchi za taifa kuheshimu mikataba waliyoingia na kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO). (12.01.2021) 

WAKAGUZI WA NGOZI WATAKIWA KUSIMAMIA UZALISHAJI WA NGOZI BORA

Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe, Bw. Gabriel Bura amewataka wakaguzi wa zao la Ngozi wa Kanda ya Mashariki kusimamia ubora wa Ngozi zinazozalishwa.

 

Bura ameyasema hayo leo (12.01.2021) wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya wakaguzi wa Ngozi wa Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam, Pwani na Morogoro) yanayofanyika katika ukumbi wa Mvuvi House jijini Dar es Salaam.

 

Wakaguzi hao wa Ngozi wametakiwa kusimamia uzalishaji wa zao hilo katika hatua zake zote ili kupata Ngozi zinazofaa kusindikwa katika viwanda.

 

Aidha, wakaguzi hao wametakiwa kutumia sheria namba 18 ya mwaka 2008 inayolenga kuboresha zao la ngozi ili wadau waweze kuzalisha ngozi bora inayokidhi mahitaji ya viwanda vyetu na hatimaye kuwa na tija ya uzalishaji wa zao hilo.

 

Bura amesema uzalishaji wa ngozi za ng’ombe na mbuzi kwa siku ni vipande 31,000 lakini ni asilimia 10 tu ya ngozi zinazopelekwa viwandani hufaa kwa ajili ya kusindikwa, na asilimia 90 hazifai kutokana na kukosa ubora unaofaa kwa ajili ya kusindikwa.

 

“Hivyo baada ya kupata mafunzo haya ni matarajio ya wizara kuwa mtakwenda kulisimamia nyema zao hili la Ngozi ili kuhakikisha Ngozi yote inayozalishwa inakuwa bora,” alisema Bura.

 

Hapa nchini vipo viwanda viwili tu vyenye uwezo wa kusindika ngozi hadi hatu ya mwisho ambavyo ni Moshi Leather Industry chenye uwezo wa kusindika futi za Mraba elfu 15,000 kwa siku na Himo Tannery and Planter Ltd chenye uwezo wa kusindika futi za mraba 10,000 kwa siku.

 

Uwezo wa usindikaji wa viwanda vyote viwili kwa siku ni sawa na vipande 1000 vya ngozi ya ng’ombe na 9000 vya ngozi ya mbuzi, hivyo bado kuna uhitaji wa viwanda vya kusindika Ngozi na vilivyopo kuongeza uwezo wake wa kusindika zao hilo.

Kaimu Mkurugenzi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe, Bw. Gabriel Bura (kulia aliyesimama) akifungua mafunzo ya siku mbili ya Wakaguzi wa Ngozi kutoka Hamashauri na Manispaa za Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam, Pwani na Morogoro) yenye lengo la kuwajengea uwez, yanayofanyika katika ukumbi Mvuvi Huose Jijini Dar es Salaam (12.01.2021)


Mshiriki wa Mafunzo ya wakaguzi wa ngozi, Bw. Severine Munishi kutoka Halmashauri ya Malinyi akichangia mada ya Sheria ya Ngozi katika mafunzo ya kikao cha wakaguzi wa Ngozi yanayofanyika katika ukumbi wa Mvuvi House Jijini Dar es salaam. (12.01.2021)

Picha ya pamoja ya Washiriki wa Mafunzo ya siku mbili ya Wakaguzi wa Ngozi na Wawezeshaji nje ya Jengo la Mvuvi House Jijini Dar es Salaam. (12.01.2021)

Mtaalam wa Ngozi Mstaafu, Bw. Emmanuel Muyinga akiwasilisha mada ya Sheria ya Ngozi namba 18 ya mwaka 2008 kwa Washiriki wa Mafunzo ya Ngozi ya siku Mbili toka Halmashauri na Manispaa za Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam, Pwani na Morogoro) yaliyofanyika katika ukumbi wa Mvuvi House Jijini Dar es Salaam. (12.01.2021)

Afisa Mifugo Mkuu kutoka Idara ya Uzalishaji na Masoko (WMUV), Bw. Edson Kilyenyi akitoa maelezo mafupi ya kuwakaribisha washiriki wa Mafunzo ya wakaguzi wa Ngozi kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi afungue mafunzo hayo, yanayofanyika katika ukimbi wa wa Mvuvi House Jijini Dar es Salaam. (12.01.2021)Jumanne, 12 Januari 2021

GEKUL ATEMBELEA WAKALA YA MAABARA YA VETERINARI KIBAHA MKOANI PWANI

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Wakala ya Maabara ya Veterinari (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi akimuonesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul moja ya chanjo wanazozalisha alipotembelea Kituo cha Wakala hiyo cha kutengeneza chanjo kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani Januari 11, 2021. Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Wakala ya Maabara ya Veterinari (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi akimuonesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul moja ya chanjo wanazozalisha alipotembelea Kituo cha Wakala hiyo cha kutengeneza chanjo kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani Januari 11, 2021.


Meneja Uzalishaji wa Kiwanda cha TANCHOICE, Selo Luwongo (kushoto) akimuonesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (wa tatu kutoka kushoto) mbuzi waliochinjwa na kuhifadhiwa katika chumba chenye baridi kali kwa ajili ya kusafirishwa kuuzwa nje ya nchi. Gekul alitembelea kiwanda hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani Januari 11, 2021.

Meneja Uzalishaji wa Kiwanda cha TANCHOICE, Selo Luwongo (wa pili kutoka kushoto) akimuonesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (wa pili kulia) maroli yaliyopakiwa minofu ya nyama ya mbuzi zaidi ya Tani 40 kwa ajili ya kuuzwa nje ya nchi alipotembelea Kiwanda hicho Januari 11, 2021. Kulia ni Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama, Imani Sichwale.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Wakala ya Maabara ya Veterinari (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi (kulia) akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (katikati) alipotembelea Kituo cha Wakala hiyo kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani Januari 11, 2021. Kushoto ni Kaimu Msajili, Bodi ya Nyama, Imani Sichwale.


 

Jumapili, 10 Januari 2021

FETA WATAKIWA KUONGEZA KASI YA KUZALISHA WATAALAM KUIMARISHA UVUVI WA BAHARI KUU

 Na Mbaraka Kambona,

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul ameitaka Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kuongeza kasi ya kuzalisha Wataalam watakaokuwa na uwezo wa kuendesha Meli za uvuvi wa bahari kuu zitakazonunuliwa na Serikali ili kuongeza ajira na kukuza uchumi wa nchi kupitia uchumi wa bluu.

 

Gekul alitoa kauli hiyo alipofanya ziara katika ofisi za Wakala hiyo zilizopo Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani mwishoni mwa wiki.

 

Alisema kuwa mpango wa serikali katika miaka hii mitano chini ya uongozi wa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ni kununua meli nane zitakazotumika kwenye shughuli za uvuvi wa bahari kuu, hivyo ni muhimu kuongeza kasi ya kutoa wataalam ambao wataweza kuziendesha meli hizo pindi zitakapofika.

                                   

Aliongeza kuwa mwishoni mwa mwaka huu meli ya kwanza itakuja, huku akisema kuwa haitapendeza kama vyombo hivyo vitakuja halafu pasiwepo na vijana watakaohusika na kuviendesha. 

 

“Nchi inawategemea mtoe wataalam watakaosaidia kuendesha meli hizo zitakazoletwa kwa ajili ya uvuvi wa bahari kuu, tunaomba mkatuzalishie wataalam ambao hatutapata upungufu wa wataalam wa kuendesha vyombo hivyo,” alisema Gekul

 

Awali akimkaribisha Naibu Waziri, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), Dkt. Semvua Mzighani alisema kuwa wameshaingia mkataba wa maridhiano wa viwango vya mafunzo na utoaji vyeti kwa wafanyakazi wa vyombo vya uvuvi wa mwaka 1995 na hivyo itasaidia kuweza kutoa vyeti kwa Manahodha wa Meli, Maafisa wa Meli, Mabaharia na Waangalizi wa Meli zitakazofanyakazi katika uvuvi wa bahari kuu.

 

“Huwezi kuajiriwa kule kama hauna cheti cha kukutambulisha, hivyo kupitia maridhiano haya sasa Mabahari watapatikana kutoka katika chuo hiki,” alisema Dkt. Mzighani

 

Dkt. Mzighani aliongeza kuwa kwa Afrika vyuo vinavyotoa mafunzo kwa Wataalam hao vipo Afrika ya Kusini na Misri, huku akisema ni wakati mzuri sasa kupitia mafunzo yatakayotolewa hapa nchini kuongeza ajira kwa vijana na kupata fedha za kigeni kupitia watu kutoka nchi nyingine watakaokuja kusoma katika chuo hicho.

 

Aidha, Dkt. Mzighani alisema pamoja na mipango na mikakati mizuri waliyonayo katika kuboresha huduma zao bado wanakabiliana na changamoto kubwa ya gharama za uendeshaji wa vyuo vya uvuvi, hivyo ameiomba serikali iwaongezee nguvu ili waweze kutoa wataalam wazuri watakaokwenda kulisaidia Taifa kukuza na kuimarisha uchumi wa bluu.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul akiwapa chakula Samaki alipotembelea Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), Kampasi ya Mbegani iliyopo Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani mwishoni mwa wiki. Kulia kwake ni Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Wakala hiyo, Dkt. Semvua Mzighani.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), Dkt. Semvua Mzighani (kushoto) akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kulia) alipotembelea Wakala hiyo iliyopo Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani mwishoni mwa wiki.

Nahodha Mkuu, Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), Kampasi ya Mbegani, Nikasi Mbandi (kulia) akimuonesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul ramani inayoonesha maeneo ya uvuvi na kina chake katika Bahari ya Hindi alipotembelea Wakala hiyo iliyopo Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani mwishoni mwa wiki.Jumamosi, 9 Januari 2021

GEKUL AMPA MKURUGENZI ILALA SIKU 7 KUMLIPA MKANDARASI

Na Mbaraka Kambona,

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kuhakikisha kuwa ndani ya siku 7 anamlipa Mkandarasi anayejenga Machinjio ya Vingunguti shilingi bilioni 5 anazodai ili aweze kukamilisha ujenzi huo.

 

Gekul alitoa agizo hilo alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa machinjio hayo yaliyopo jijini Dar es Salaam Januari 8, 2021.

 

Alisema kuwa hali za machinjio nyingi kwa sasa sio nzuri, Wanyama wanachinjwa katika mazingira machafu na sio salama kwa walaji huku akisema machinjio hayo ya Vingunguti yatakuwa mkombozi kwa wananchi wa Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla.

 

“Kwa hiyo Mkurugenzi hakikisha ndani ya siku 7 kuanzia leo tarehe 8 unamlipa Mkandarasi ili kazi hii ikamilike kama ambavyo Mhe. Rais, Dkt. John Magufuli alivyoagiza,” aliagiza Gekul

 

Gekul aliendelea kusisitiza kuwa kukamilika kwa ujenzi huo ni lazima uende sambamba na ununuzi wa magari kwa ajili ya kubebea nyama na kuzisambaza katika mabucha yaliyopo jijini Dar es Salaam kwani haitapendeza kuwepo kwa machinjio hayo mazuri halafu nyama ziwe zinabebwa kwenye pikipiki.

 

Aliongeza kuwa ili kuhakikisha machinjio hayo yanapata Wanyama wazuri na salama kwa ajili ya walaji, wataboresha mnada wa machinjio ya Pugu ili wanyama watakaokuwa wanapelekwa hapo wawe na viwango vya kuchakatwa katika machinjio hayo.

 

Aidha, aliwapongeza Mkurugenzi na Mkandarasi kwa jitihada kubwa wanazozifanya katika kukamilisha ujenzi huo na kuwataka kuongeza kasi ya ujenzi ili ukamilike kama inavyotarajiwa.

 

Naye, Msimamizi wa ujenzi huo kutoka Shirika la Nyumba la Taifa, Mhandisi, Efraim Phanuel alisema kuwa endapo watalipwa kiasi hicho cha pesa wanachodai kama alivyoagiza Naibu Waziri watakamilisha ujenzi huo mapema mwezi wa pili mwaka huu.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul (katikati) akikagua risiti ya mteja aliyemkuta akitoka na mbuzi katika mnada wa Pugu uliopo jijini Dar es Salaam alipotembelea mnada huyo Januari 8, 2021. Kulia ni Kaimu Msajili, Bodi ya Nyama, Imani Sichwale.


Mhandisi Efraim Phanuel akimuonesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul michoro inayoonesha muonekano wa  machinjio ya Vingunguti utakavyokuwa baada ya kukamilika kwake alipotembelea machinjio hayo Januari 8, 2021.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto) akimsikiliza Msimamizi wa Ujenzi wa Machinjio ya Vingunguti, Mhandisi EfraimPhanuel (hayupo pichani) alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa machinjio hayo Januari 8, 2021. Kulia ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Jumanne Shauri.


Ijumaa, 8 Januari 2021

SAUTI YETU WIKI HII


 

HALMASHAURI ZASHAURIWA KUTUMIA BMU KUKUSANYA MAPATO YA UVUVI

Na Mbaraka Kambona,

 

Mratibu wa Mradi wa Usimamizi wa Rasilimali za Bahari Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish), Dkt. Nichrous Mlalila ameziomba Halmashauri kuvitambua Vikundi vya Ulinzi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) na kuzipa uwezo wa kukusanya mapato yatokanayo na shughuli za uvuvi ili ziweze kusaidia vikundi hivyo kujiendesha na kuendeleza sekta ya uvuvi nchini.

 

Dkt. Mlalila alitoa rai hiyo katika ziara ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya BMU inayojengwa na Mradi wa SWIOFish katika Kata ya Dunda, Wilayani Bagamoyo Januari 7, 2021.

 

Kwa mujibu wa Dkt. Mlalila sehemu kubwa ya mapato yanayokusanywa kwa sasa na Halmashauri hayarudishwi kwa Jamii ya wavuvi kwa ajili ya kuendeleza shughuli za sekta na uchumi wa jamii husika.

 

Dkt. Mlalila alisema anatambua kuwa kuna changamoto ya kisheria ambayo baadhi ya Halmashauri zimetumia kuzizuia BMU kukusanya mapato yanayotokana na rasilimali za uvuvi.

 

“Tunahamasisha Halmashauri kuwapa uwezo BMU kukusanya mapato ili kuziwezesha kupata kipato cha uhakika cha kuendesha shughuli zao za kulinda rasilimali za Uvuvi lakini pia mapato hayo yatawezesha kuendeleza sekta ya uvuvi tofauti na ilivyo sasa,” alisema Dkt. Mlalila

 

Katika baadhi ya Halmashauri ambazo wamewapa kazi BMU ya kukusanya mapato kama vile Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Mkoani Tanga, Mapato yanayotokana na uvuvi yameongezeka kutoka shilingi milioni 9 kwa robo mwaka hadi milioni 51 na kutoka shilingi milioni 36 hadi milioni 256 kwa mwaka.

 

“Nazishauri Halmashauri nyingine zichukue mfano wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani kwa sababu sisi tumezipa mafunzo ya kina hizi BMU katika kusimamia fedha na ukusanyaji wa mapato, hivyo tunaamini hilo ni suala la mchakato na tumewasilisha andiko TAMISEMI ili kuangalia namna ya kuzifanya BMU kuendelea na shughuli zake hata pale ambapo mradi wa SWIOFish utakapokwisha muda wake,” aliongeza Dkt. Mlalila

 

Akizungumzia suala hilo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul alisema kuwa BMU ya kata ya Dunda na zingine zikajifunze Pangani kuona wao wanafanyaje na sisi kama Wizara tutaangalia kama kuna chanzo ambacho wataalam wa Halmashauri wanakusanya na hakifanyi vizuri na kuna BMU mahali inakusanya vizuri basi tutaibua hiyo hoja tuone tutafanyaje.

 

“Ukweli ni kwamba kwenye vyanzo hivi vya leseni na ushuru wa rasilimali za uvuvi katika halmashauri zetu nyingi hazifanyi vizuri na hivyo kuna haja ya kuviangalia vizuri hasa wataalam wetu wanaotumika kukusanya hayo mapato kwa sababu kuna baadhi yao wamefanya hapo ndio maeneo yao ya kupatia pesa zao,” alisema Gekul

 

Alisema Wakurugenzi wanaweza kuwa na nia njema kabisa lakini wale wanaotumwa kukusanya hayo mapato wanarudisha maduhuli hayo kama walivyotumwa? Kama kuna watu wanauwezo wa kukusanya zaidi ya wataalam wa Halmashauri sidhani kama kuna haja ya kuwa na kigugumizi cha kuwatoa hao watu ili kazi hiyo apewe anayeweza kukusanya vizuri.

 

“Kwa sababu mwisho wa siku sisi wananchi tunachotaka ni maendeleo hivyo nisingependa niseme moja kwa moja hapa kuwa BMU wapewe kazi hiyo isipokuwa Halmashauri ziangalie kama sheria inawaruhusu kuwatumia BMU kukusanya mapato,” aliongeza Gekul

 

Gekul alisema kuwa wao kama Wizara watawasiliana na TAMISEMI kuona maelekezo yakoje kwa sababu anasema kuna vyanzo Halmashauri zenyewe zinakusanya na vingine vinaruhusiwa kukusanywa na wakala na pale ambapo BMU itaonekana inafaa ipewe uwezo wa kukusanya.

 

Mradi wa SWIOFish unafadhiliwa na Benki ya Dunia kuhamasisha ulinzi na usimamizi wa rasilimali za bahari na ndio umeimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi wa rasilimali za bahari (BMU) kwa ajili ya kulinda na kuhamasisha uvunaji endelevu wa rasilimali za bahari katika Wilaya za Mkinga, Pangani, Bagamoyo, Lindi Vijijini na Tanga Jiji.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto) akitoa maelekezo kwa Mratibu wa Mradi wa Usimamizi wa Rasilimali za Bahari Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish), Dkt. Nichrous Mlalila (kulia) alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya Kikundi Cha Ulinzi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) katika kata ya Dunda, Wilayani Bagamoyo Januari 7, 2021.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Ulinzi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU), Kata ya Dunda, Wilayani Bagamoyo, Isihaka Hudi (kulia) akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto) alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi ya BMU hiyo Januari 7, 2021.

Mratibu wa Mradi wa Usimamizi wa Rasilimali za Bahari Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish), Dkt. Nichrous Mlalila akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto) alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya Kikundi cha Ulinzi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) inayojengwa katika Kata ya Dunda, Wilayani Bagamoyo Januari 7, 2021.

WASHIRIKI WA MAFUNZO YA UKAGUZI WA RASILIMALI YA VYAKULA VYA MIFUGO WAPEWA VITAMBULISHO.

Washiriki wa mafunzo ya ukaguzi wa rasilimali ya vyakula vya mifugo kutoka mikoa mbalimbali wakifuatilia kwa makini maelezo ya Afisa Mifugo Mtafiti Mkuu kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Bi. Wende Maulaga (kushoto) wakati akitoa mafunzo hayo kwenye Maabara ya TVLA jijini Dar es salaam. (07/01/2021) 

 

Afisa Mtafiti Mifugo Mwandamizi, kitengo cha Upimaji Ubora na Usalama kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Scholastica Doto akionyesha na kutoa elimu ya namna  mashine ya kupimia madini kwenye vyakula vya mifugo inavyofanya kazi kwa washiriki (hawapo pichani) wa mafunzo ya ukaguzi wa rasilimali ya vyakula vya mifugo walipotembea maabara ya TVLA jijini Dar es salaam. 07/01/2021.* 


Mgeni rasmi ambaye ni Mkurugenzi wa Utambuzi na Huduma za Uchunguzi kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Chanasa Mpelumbe akimvalisha kitambulisho mmoja wa washiriki wa mafunzo ya ukaguzi wa rasilimali ya vyakula vya mifugo kutoka Tanga  Bw. Mustafa Khalifan baada ya kufunga mafunzo hayo ya siku tatu yaliyofanyika kwenye ukumbi wa TVLA jijini Dar es salaam. 07/01/2021.*


*Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Idara ya Uendelezaji malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Rogers Shengoto akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi ambaye ni Mkurugenzi wa Utambuzi na Huduma za Uchunguzi kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Chanasa Mpelumbe na washiriki wote (hawapo pichani) wa mafunzo ya ukaguzi wa Rasilimali ya Vyakula vya Mifugo wakati wa kufunga mafunzo hayo ya siku tatu yaliyofanyika kwenye ukumbi wa TVLA jijini Dar es salaam. 07/01/2021*  Mkurugenzi wa Utambuzi na Huduma za Uchunguzi kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dr. Chanasa Mpelumbe (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wataalam waliotoa mafunzo ya ukaguzi wa Rasilimali ya Vyakula vya Mifugo pamoja na washiriki wa mafunzo  mara baada ya kuwakabidhi vitambulisho na kufunga mafunzo hayo kwenye ukumbi wa TVLA jijini Dar es salaam. 08/01/2021* 


Alhamisi, 7 Januari 2021

VIJANA WAHIMIZWA KUCHANGAMKIA FURSA UFUGAJI SAMAKI KATIKA MABWAWA

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul amewahimiza vijana kujihusisha na ufugaji wa samaki katika mabwawa huku akisema fursa hiyo itawaokoa vijana wengi kuondokana na kilio cha ukosefu wa ajira nchini.

 

Gekul aliyasema hayo alipotembelea Kampuni ya ufugaji wa Samaki inayojulikana kwa jina la Bigfish iliyopo Wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam Januari 6, 2021.

 

Alisema kuwa muelekeo wa Serikali kwa sasa ni kuimarisha ufugaji wa samaki katika mabwawa kwasababu uvuvi wa kutegemea maji ya asili umekuwa mkubwa na kupelekea kupungua kwa rasilimali za uvuvi, hivyo kimbilio pekee ambalo litawawezesha vijana wengi kupata ajira ni ufugaji wa samaki katika mabwawa.

 

Aliongeza kuwa Serikali ipo mbioni kuweka miongozo na kanuni za ufugaji huo ili kuwalinda na kuwawezesha wafugaji waweze kufuga vizuri na kwa kuzingatia taratibu zitakazowekwa.

 

“Serikali itawawezesha vijana kwa hali ya juu, kuwajengea mabwawa, kuwapatia mafunzo ya ufugaji bora wa samaki ili vijana wetu waweze kujikwamua na suala la ukosefu wa ajira,” alisema Gekul

 

Aliendelea kusema kuwa Rais, Dkt. John Magufuli aliahidi ajira zaidi ya milioni 8, moja ya sekta ambayo inategemewa kutengeneza ajira hizo ni ya uvuvi hivyo aliwahimiza vijana kuchangamkia fursa hiyo ili waweze kujikomboa kiuchumi.

 

Kuhusu uwezeshaji, Gekul aliziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatenga asilimia 10 katika mapato yao kwa ajili ya kuwawezesha vijana na watu wenye Ulemavu ili waweze kufanya ufugaji katika mabwawa na kujipatia ajira.

Aidha, Gekul alisema kuwa anafahamu changamoto zinazokabili ufugaji wa samaki wa mabwawa ni pamoja na uhaba wa vifaranga vya samaki na ukosefu wa chakula cha kutosha na cha uhakika kwa ajili ya samaki hivyo alitumia fursa hiyo kuiagiza Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) kutafuta muarobaini wa changamoto hizo ili kuwaondolea kero hiyo wafugaji.

 

Aliongeza kuwa ufugaji wa samaki katika mabwawa utasaidia kupunguza kilio cha uhaba wa malighafi unaokabili viwanda vingi nchini huku akiongeza kuwa ufugaji huo pia utasaidia kupunguza uvuvi haramu kwa sababu watu watakuwa na chanzo mbadala cha kujipatia kipato.


Kaimu Meneja Mkuu, Shirika la Uvuvi (TAFICO), Ester Mulyila (kulia) akimpokea Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto) alipotembelea Shirika hilo lililopo jijini Dar es Salaam Januari 6, 2021. 

Mshauri wa Uvuvi kutoka Japan, Koji Hase (kushoto) akimuonesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul(kulia) baadhi ya taarifa kuhusu uvuvi alipotembelea Shirika la Uvuvi la Tanzania (TAFICO) lililopo jijini Dar es Salaam Januari 6, 2021. 

Afisa Uzalishaji Vifaranga, Kampuni ya Bigfish, Pastory Aloyce (kushoto) akifafanua jambo kuhusu ufugaji wa samaki kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul alipotembelea eneo la ufugaji wa samaki la kampuni hiyo iliyopo Wilayani Kigamboni, jijini Dar es Salaam Januari 6, 2021. 

Mkurugenzi Mkuu, Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI), Dkt. Ismael Kimerei (kulia) akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul alipotembelea taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam Januari 6, 2021. Wa kwanza kushoto ni Mratibu wa Mradi wa SWIOFish, Dkt. Nichrous Mlalila. 

 


TVLA YAWATAKA WATAALAMU KUZINGATIA UBORA WA VYAKULA VYA MIFUGO


Wataalamu kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) wametakiwa kuzingatia mafunzo wanayopatiwa ili wazalishaji wa vyakula vya mifugo waweze kuzalisha vyakula vyenye ubora unaotakiwa.

 

Kaimu Mtendaji Mkuu wa TVLA Dkt. Stella Bitanyi amebainisha hayo jana (06.01.2021) wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya ukaguzi wa rasilimali ya vyakula vya mifugo yanayofanyika jijini Dar es Salaam na kubainisha kuwa wataalamu wataweza pia kutekeleza majukumu mapya ya kuzingatia zaidi ubora wa vyakula vya mifugo.

 

"Uwepo wenu kama wakaguzi utarahisisha huduma kwa wananchi, na upatikanaji kwa sampuli zaidi ili kupata uhakika wa ubora wa vyakula vya mifugo nchini" alisema Dkt. Bitanyi.

 

Aidha, Dkt. Bitanyi ameishukuru timu wa wataalamu wa idara ya uendelezaji wa malisho na masilimali za vyakula vya mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na afisa mifugo mtafiti mkuu kutoka TVLA kwa namna wanavyoshirikiana katika mafunzo hayo ambayo yanalenga kuboresha zaidi uwepo wa vyakula bora vya mifugo.

 

"Ni matarajio ya wakala kuwa kupitia mafunzo haya mtaongeza ufanisi katika kazi zenu pia kuongeza uwezo wa wakala katika jukumu zima la udhibiti wa uzalishaji holela wa vyakula vya mifugo na kuwezesha kuongeza tija katika sekta ya mifugo." Alisema Dkt. Bitanyi.

 

Kaimu Mtendaji Mkuu wa TVLA Dkt. Stella Bitanyi alisema mafunzo hayo ya siku tatu yatawawezesha wataalamu kufahamu sheria na kanuni za ukaguzi wa vyakula vya mifugo, uzalishaji sahihi wa vyakula vya mifugo, weledi katika kuchambua ubora wa rasilimali za vyakula vya mifugo wakati wa ukaguzi, ukaguzi wa maeneo ya utunzaji wa vyakula vya mifugo na namna bora ya uchakataji wa sampuli. 

 

Pia, amewasihi wataalamu kutumia muda uliopo kwenye mafunzo hayo kuhakikisha wanazingatia wanayofundishwa na kuweka katika mipango yao ya kazi hasa kutokana na ukweli kuwa, TVLA imeanzishwa ikiwa na majukumu ya kuchunguza magonjwa ya mifugo, uhakiki ubora wa vyakula vya mifugo, upimaji wa nguvu ya dawa za kuogeshea pamoja na  uzalishaji na usambazaji wa chanjo za mifugo.

 

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) ilianzishwa chini ya Sheria ya Wakala za Serikali ya Mwaka 2012 kwa lengo la kutoa huduma za uchunguzi, utambuzi na utafiti wa magonjwa, vimelea vya magonjwa ya wanyama na ubora wa bidhaa za mifugo.


Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi akieleza lengo na majukumu ya wataalamu (hawapo pichani) wakati wa kufungua mafunzo ya ukaguzi wa rasilimali ya vyakula vya mifugo yanayoendelea jijini Dar es salaam. (06.01.2021) 


Mkurugenzi wa Utawala na Biashara kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Bw. Richard Masanja akiwasisitiza wataalamu kuzingatia yote wanayofundishwa kabla ya kumkaribisha Kaimu Mtendaji Mkuu wa TVLA, Dkt. Stella Bitanyi kufungua mafunzo hayo jijini Dar es salaam. (06.01.2021)* 


Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya ukaguzi wa rasilimali ya vyakula vya mifugo kutoka mikoa mbalimbali wakifuatilia kwa makini maelezo ya Afisa Mifugo Mtafiti Mkuu kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinary Tanzania (TVLA), Bi. Wende Maulaga wakati akitoa mafunzo hayo kwenye ukumbi wa TVLA jijini Dar es salaam. (06.01.2021)*

 

Timu ya wataalam wanaotoa mafunzo ya ukaguzi wa rasilimali ya vyakula vya mifugo, (kushoto juu) ni Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali za Vyakula vya Mifugo kutoka Idara ya Uzalishaji Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo Bw. Rogers Shengoto, Afisa Mifugo Mtafiti Mkuu   Bi. Wende Maulaga (kulia) na Afisa Mifugo kitengo cha Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Bi. Theodata Salemma wakitoa elimu kwa baadhi ya washiriki wa mafunzo jijini Dar es salaam. (06.01.2021)* Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania ( TVLA), Dkt. Stella Bitanyi (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na  wakurugenzi pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi mara baada ya kufungua mafunzo ya siku tatu ya ukaguzi wa rasilimali ya vyakula vya mifugo kwenye ukumbi wa TVLA jijini Dar es salaam. (06.01.2021)*