Nav bar

Jumanne, 26 Januari 2021

NGURUWE WENYE THAMANI YA MILIONI 370 WAMEKUFA KWA HOMA, SERIKALI YAWEKA MIKAKATI KUDHIBITI

Na Mbaraka Kambona,


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha ugonjwa wa homa ya Nguruwe ulioikumba Mikoa ya Kanda ya Ziwa hivi karibuni unadhibitiwa, huku akisema kuwa tangu ugonjwa huo uanze mpaka sasa umeshasababisha vifo vya Nguruwe 1500 wenye thamani ya shilingi milioni 375.


Ndaki aliyasema hayo Januari 23, 2021 jijini Dodoma alipokuwa akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kuudhibiti ugonjwa huo uliokumba Mikoa ya Kanda ya Ziwa. 


Alisema kuwa vifo hivyo vimesababisha hasara ya moja kwa moja kwa wafugaji kwa sababu kipato hicho kilichopotea ilikuwa wakipate wafugaji huku akiwataka wafugaji hao kuwa watulivu na kufuata maelekezo ya serikali ili ugonjwa huo uweze kudhibitiwa kwa haraka.


Aliongeza kuwa  ugonjwa huo unaosababishwa na virusi unahama kutoka kwa nguruwe pori na  Ngiri na unasambaa kupitia  njia ya Maji, Damu au Kinyesi.


Ndaki alisema kuwa Halmashauri zilizoathirika mpaka sasa ni Mbogwe, Kyerwa, Geita, Sengerema, Kahama na Misungwi na alibainisha kuwa serikali imeshachukua hatua kadhaa za kudhibiti ugonjwa huo.


Alisema kuwa mpaka sasa serikali imeshachukua hatua mbalimbali za kuhakikisha ugonjwa huo unadhibitiwa ikiwemo kuweka karantini za mifugo hiyo ili kudhibiti ugonjwa huo usisambae zaidi.


“Tumeongeza Wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wakala ya Maabara ya Veterinari (TVLA), Wataalamu kutoka Chuo cha Sokoine (SUA) na Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) kwenda kuungana na wataalamu wa Halmashauri ili kuongeza nguvu ya kudhibiti ugonjwa huo,” alisema Ndaki

Ndaki alisisitiza kuwa ugonjwa huo hauna chanjo wala tiba huku akiwahimiza wananchi kuhakikisha wanazingatia maelekezo wanayopewa na wataalamu ikiwemo kupulizia dawa za kuua wadudu Kupe katika mabanda ili kuzuia ugonjwa huo usisambae zaidi.


“Niwaombe wananchi waache kula nyama ya Nguruwe, hatua hizi tunazochukua lengo lake ni kudhibiti ugonjwa usiendelee kuleta madhara zaidi katika maeneo mengine,”alisema Ndaki


Aidha, Ndaki amewataka Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi katika maeneo yaliyoathirika kuhakikikisha wanasimamia kikamilifu karantini zilizowekwa na wataalamu ili ugonjwa huo kuzuiwa kusambaa katika maeneo mengine  huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano ili hatua hizo zinazochukuliwa na serikali ziweze kuzaa matunda.


Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga alisema kuwa ili ugonjwa huo usisambae zaidi ni muhimu wafugaji kuhakikisha kuwa mifugo yao inakuwa katika mabanda wakati wote na kuacha kusafirisha mifugo na mazao yake kutoka sehemu moja kwenda nyingine kabla ya kupimwa na Daktari. 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki akiongea na Waandishi wa Habari (hawapo pichani)  kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kudhibiti ugonjwa wa homa ya Nguruwe kwenye Mkutano uliofanyika jijini Dodoma Januari 23, 2021.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakichukua matukio katika Mkutano wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (hayupo pichani) kuhusu ugonjwa wa homa ya Nguruwe uliofanyika jijini Dodoma Januari 23, 2021.
Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga (kushoto) akifafanua jambo kwa  Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu ugonjwa wa homa ya Nguruwe katika Mkutano uliofanyika jijini Dodoma Januari 23, 2021. Kulia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni