Nav bar

Jumatano, 16 Machi 2022

UJENZI WA BANDARI YA UVUVI MBIONI KUANZA


Na Saja Kigumbe

Serikali imeweka wazi kuwa mradi  wa ujenzi wa bandari ya uvuvi  unatarajia kuanza muda wowote kuanzia sasa baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu.

Bandari hiyo ambayo inatarajiwa kujengwa Wilayani Kilwa Masoko, Mkoani Lindi inatarajiwa kuwa chachu ya kuimarika kwa uchumi wa buluu nchini.

Hayo yalibainishwa Machi 16, 2022 Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti  na Mafunzo ya uvuvi, Dkt. Erastus Mosha wakati wa mkutano wa wadau uliolenga kupitia rasimu ya taarifa ya upembuzi yakinifu wa mradi huo wa kimkakati.

Alisema bandari hiyo itaiwezesha nchi kupata mapato kupitia  meli za uvuvi na bidhaa zinazotokana na uvuvi zitauzwa hapa ndani  na nje ya nchi.

Dkt. Mosha alisema Serikali tayari imetenga fedha za kufanikisha ujenzi huo ambao unatarajiwa kufanyika katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa.

“Tanzania hatujawahi kuwa na bandari ya uvuvi na hili limesababisha tumeshindwa kunufaika vya kutosha kupitia rasilimali za uvuvi kwa maana kwamba meli kubwa zinazovua kwenye ukanda wa uchumi wa bahari kushindwa kuja kwetu kutoa mizigo yao.

“Kutokana na  mazingira hayo tumeishia kupata tozo ya leseni ya hizo meli pekee, tukiacha mizigo yote wanayopata na shughuli zote zinazohusu uvuvi na bandari zinaenda kufanyika katika nchi nyingine tungekuwa na bandari, meli zingeweza kuja kwetu,” alisema Dkt. Mosha.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uvuvi Bi. Merisia Mparazo alisema utekelezaji wa mradi huo utaiwezesha nchi kuvuna rasilimali zilizopo kwenye ukanda wa uchumi wa bahari hususani kwenye kina kirefu.

Alisema uwepo wa bandari hiyo utapanua wigo wa kiuchumu katika mkoa wa Lindi ambapo licha ya shughuli za bandari utawezesha kuanzishwa kwa viwanda vya kuchakata samaki watakaovuliwa, biashara ya mafuta ya meli na utengenezaji wa vyombo hivyo vya uvivu.

“Kama kuna bandari ya uvuvi lazima zitakuwepo shughuli nyingine zinazoendana na hiyo, mfano zile meli zitahitaji mafuta au marekebisho madogo madogo tunategemea huduma za aina hii zitapatikana pale.

"Kana kwamba hiyo haitoshi kama samaki hao wakubwa watakuja kwenye bandari yetu lazima uchakataji utafanyika hapa nchini hivyo kutakuwa na viwanda vya kuchakata minofu ya samaki, bado biashara ya vyakula na hoteli itachukua nafasi hivyo vyote vitazidi kuuchangamsha mkoa mzima wa Lindi,” alisema Merisia.

 

Kwa upande wake mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi, Bw. Ramadhani Hatibu amesema Mkoa huo umepokea vizuri mradi huo kutokana na kuwa na tija kwa taifa na jamii kwa ujumla.

Amesema kutokana na mradi huo kutasaidia kuvua samaki wenye ujazo mkubwa ambao utasaidia pato la Taifa.

Naye Mdau wa uvuvi Bw. Khalfan Shabani amesema ujenzi wa bandari hiyo ya Uvuvi utaleta maendeleo makubwa katika Sekta ya Uvuvi.

Aidha ameiyomba Serikali kuwakaribisha wawekezaji kwa ajili ya ujenzi wa karakana ya meli baada ya ujenzi wa bandari kukamilika.


Mkurugenzi Msaidizi Utafiti na Mafunzo ya uvuvi Sekta ya Uvuvi Dkt. Erastus Mosha (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau wa Sekta hiyo mara baada ya kikao kifupi kilichofanyika kwenye ukumbi wa millennium tower Jijini Dar es salaam lengo likiwa ni pamoja na kujadili taarifa ya upembuzi yakinifu ya ujenzi wa bandari ya Uvuvi Machi 16, 2022.

Mkurugenzi Msaidizi wa uendelezaji wa Uendelezaji wa Rasilimali za Uvuvi (Uvuvi), Bi. Merisia Parazo (kulia) akifungua kikao na kueleza lengo la kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa millennium tower Jijini Dar es salaam, Machi 16, 2022

Alhamisi, 10 Machi 2022

ULINZI WA RASILIMALI ZA UVUVI KUSTAWISHA UCHUMI WA BULUU - ULEGA

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewataka wataalam, wavuvi na wafugaji wa viumbe maji kulinda rasilimali za uvuvi ili kustawisha uchumi wa buluu.

Naibu Waziri Ulega ametoa kauli hiyo (07.03.2022) wakati alipokuwa akizungumza kwenye uzinduzi wa mwaka wa kimataifa wa uvuvi mdogo na ukuzaji viumbe maji – IYAFA 2022 uliofanyika kwenye uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza.

Amesema upo umuhimu wa kuanzisha chombo cha ulinzi wa rasiliamli za uvuvi chenye wataalam wa uvuvi na ulinzi ili kuhakikisha rasilimali hizo zinalindwa.

Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan imeweka malengo ya kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinalindwa ili kustawisha uchumi wa buluu utakaosaidia kukuza pato la wavuvi, wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi na taifa kwa ujumla.

Serikali kwa muda mrefu imekuwa ikisikia changamoto nyingi zinazowakabili wavuvi na rasilimali za uvuvi na kwamba sasa ni wakati muafaka wa kukabiliana na changamoto hizo.Hivyo aliwataka watumishi wa Wizara kwa  kushirikiana na  Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) ili waone ni namna gani wanaweza kusaidia sekta ya uvuvi kwa baadhi ya maeneo hususani changamoto zinazowakabili wavuvi wadogo nchini.

Naibu Waziri Ulega aliwataka wataalam wa Sekta ya Uvuvi kushirikiana na wawakilishi wa FAO kuandaa mradi kwa ajili ya matumizi bora ya Ziwa Victoria utakaosaidia katika kuepusha migogoro na wavuvi na utakaolinda rasilimali za uvuvi. Lakini pia wataalam waandae mradi utakaosaidia katika kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi kwa kuwa bado ipo changamoto ya upotevu wa mazao hayo.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa FAO hapa nchini, Charles Tulahi alisema Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limetangaza mwaka 2022 kuwa ni mwaka wa uvuvi mdogo na ufugaji viumbe maji kutokana na mchango mkubwa ambao sekta za uvuvi na ufugaji wa viumbe maji zinatoa katika kuimarisha lishe, kutokomeza umaskini na katika kuongeza ajira.

FAO imepewa jukumu la kuongoza maadhimisha ya mwaka huu wa uvuvi mdogo na ufugaji wa viumbe maji kwa kushirikiana na serikali mbalimbali duniani, mashirika pamoja na vyombo muhimu kwa wavuvi. Tulahi ameipongeza Tanzania kwa kuwa na Mpango kazi wa Kitaifa wa utekelezaji wa miongozo ya uvuvi nchini.

Kabla ya kuzindua maadhimisho hayo, Naibu Waziri Ulega alitembelea mwalo wa Kirumba ambapo aliwaeleza wavuvi kuwa Serikali inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan imepanga kuhakikisha tozo zote kichefuchefu zinaondolewa ili wavuvi na wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi waweze kufanya shughuli zao kwa uhuru na tija zaidi.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akiongea na wavuvi wadogo (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa mwaka wa kimataifa wa uvuvi mdogo na ukuzaji viumbe maji 2022 kwenye uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza, Machi 07, 2022. Mhe. Ulega amesema uvuvi ni kazi kama zilivyo kazi nyingine hivyo amewataka wataalam kufanya kazi zaidi ili kuiheshimisha kazi hiyo.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa Mwakilishi Msaidizi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Bw. Charles Tulaki (kulia) mara baada ya uzinduzi wa mwaka wa kimataifa wa uvuvi mdogo na ukuzaji viumbe maji 2022 uliofanyika kwenye uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza, Machi 07, 2022. Katikati ni Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi.

Mwakilishi wa wafugaji viumbe maji, Mhe. Said Sadiki akiongea na hadhara ya wavuvi walioshiriki kwenye uzinduzi wa mwaka wa kimataifa wa uvuvi mdogo na ukuzaji viumbe maji 2022 ambapo amesema kuwa ufugaji wa samaki una faida kubwa endapo wafugaji hao watafuata maelekezo wanayopewa na wataalam, Machi 07,2022

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (wa tatu kutoka kushoto) akipata maelezo kutoka kwa mvuvi, Bi. Elizabeth Mpuya (wa tatu kutoka kulia) wakati alipokuwa anatembelea mabanda ya baadhi ya wavuvi kwenye uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza, Machi 07, 2022. Wa pili kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi.

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (wa nne kutoka kushoto waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki mara baada ya kuzindua maadhimisho ya mwaka wa kimataifa wa uvuvi mdogo na ukuzaji viumbe maji 2022 kwenye uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza, Machi 07, 2022.

 Jumapili, 6 Machi 2022

SERIKALI YADHAMIRIA KUWAINUA WAVUVI WADOGO


Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi amesema Serikali imedhamiria  kuboresha Sekta ya Uvuvi  kwa kuwawezesha wavuvi wadogo wakiwemo wanawake ili waweze kunufaika na rasilimali za uvuvi zilizopo nchini.

Aliyasema hayo wakati wa hafla ya mashindano ya mbio za kuendesha mitumbwi kwa wavuvi wanawake kutoka mikoa ya Kanda ya ziwa iliyofanyika jijini Mwanza Machi 6, 2022.

“ Tumedhamiria kuwainua wavuvi wadogo na ndio maana tumeandaa mwongozo wa hiari na mpango mkakati kwa ajili ya kuendeleza uvuvi, rasilimali na mazao yake hapa nchini,” alisema Bulayi

Alisema lengo la Serikali la kuandaa Mwongozo huo kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) ni kukuza mchango wa sekta ya uvuvi mdogo kwa maslahi mapana ya wananchi kiuchumi, kijamii na kimazingira.

Aliongeza kwa kusema kuwa mwongozo huo ambao umekubaliwa na Jumuiya ya Kimataifa, unaamsha   misingi ya kusimamia na kuendeleza uvuvi mdogo kwa sababu asilimia 85 ya shughuli za uvuvi hapa nchini zinafanywa na wananchi wenye kipato cha chini.

Alifafanua kwamba Serikali inataka kuwainua wavuvi wadogo kwa kuwawezesha mikopo na  kuwapatia  mafunzo ili waweze kufanya uvuvi wenye tija kupitia vikundi vyao vya uvuvi na ushirika.

Kwa upande wake mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), Bw. Charles Tulahi aliishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) kwa kuwapa fursa ya kushiriki kwenye maandalizi ya mwongozo wa hiari wa kitaifa wa kutambua na kuendeleza  rasilimali za Uvuvi na kwamba hatua hiyo itasaidia katika kuboresha lishe na  ajira kwa jamii.

"Ni Imani yetu kuwa mpango kabambe huo wa Uvuvi utaleta mabadiliko makubwa katika Sekta ya Uvuvi Nchini hasa kwa wavuvi wadogo wanawake ", alisema

"Tumeshirikiana na Serikali ya Tanzania kuhakikisha mazingira ya mvuvi mdogo wa Tanzania yanakuwa bora zaidi kwa ajili ya kupata kipato lakini pia ustawi wa maisha yao" aliongeza

Alifafanua kuwa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) limeipatia Tanzania kiasi cha shilingi milioni 450 zilizotumika kuandaa mwongozo na shughuli za utawala katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

 

Naye, Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la EMEDO, Bi. Editrudith Lukanga alisema mchango wa mwanamke katika uvuvi ni mkubwa lakini bado mchango huo haujatambuliwa kikamilifu.

Aidha, aliishukuru Serikali kwa kuandaa Mwongozo huo ambao utawasaidia wanawake wavuvi kutambuliwa kwenye shughuli zao za uvuvi kwa kufanya uvuvi wenye tija utakaowaongezea kipato, ajira na lishe.


Washiriki wanawake wakiwa kwenye zoezi la kushindana kuendesha mitumbwi  ziwa victoria Jijini Mwanza. Machi 06, 2022. lengo likiwa ni pamoja na kuamasisha wanawake kushiriki katika zoezi la Uvuvi.

Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa mashindano ya wanawake ya  kuendesha mitumbwi na maafisa kutoka Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), EMEDO na maafisa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi mara baada ya mashindano hayo yaliyofanyika ziwa victoria  kamanga Jijini Mwanza. Machi 06, 2022. 

Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi (wa pili kutoka kushoto) akikabidhi zawadi ya fedha kiasi cha shilingi laki saba kwa washindi wa kwanza wa mashindano ya kupiga kasia kwa wanawake mara baada ya mashindano hayo yaliyofanyika  ziwa Victoria kamanga Mkoani mwanza Machi 06, 2022. 


Jumatano, 2 Machi 2022

RAIS SAMIA KUWAINUA WANANCHI KUPITIA UCHUMI WA BULUU-ULEGA


Na Mbaraka Kambona, Lindi

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amejipanga kuwainua wananchi kupitia fursa zinazopatikana katika Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi ili waweze kukuza kipato chao na kuchangia katika pato la taifa.

Ulega alitoa kauli hiyo Machi 1, 2022 alipotembelea vikundi vya ukulima wa mwani, ufugaji samaki na Kambakochi kwa lengo la kuhamasisha wananchi kuchangamkia fursa za ukuzaji viumbe maji zilizopo katika Mkoa wa Lindi.

“Nia ya Rais wetu, Mama Samia ni kuhakikisha mnakuwa na kipato kizuri wakati wote, mzunguko wenu wa kipato uimarike kupitia fursa hizi zinazopatikana katika uchumi wa buluu, uchumi wenu ukiimarika umasikini utapungua lakini vilevile mtaweza sasa kuchangia mapato katika Halmashauri zetu na taifa kwa ujumla”,alisema Mhe. Ulega

Alisema nia ya serikali ni kutaka kuwawezesha wananchi kujiunga katika vikundi ili waweze kukopesheka kirahisi huku akimuelekeza Mtendaji Mkuu, Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), Dkt. Semvua Mzighani kuhakikisha wanawasaidia vikundi vya ukuzaji viumbe maji  kwa kuwapa utaalam wa namna ya kuzalisha kwa tija  na kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao yao.

Aidha, katika ziara yake hiyo pia alizielekeza Halmashauri na Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB) kuhakikisha wanawapa maarifa ya kibiashara na kuwawezesha mitaji ili wananchi hao waweze kujikwamua kimaisha kupitia shughuli zao hizo.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack alimshukuru Mhe. Rais Samia kwa kufungua fursa za uchumi wa buluu na kusema kuwa Mkoa wa Lindi wapo tayari kuzitumia fursa hizo ili wananchi waweze kunufaika.

“Mhe. Naibu Waziri ninachotaka kukuthibitishia ni kwamba uchumi wa buluu tumeshauanza hapa mkoani Lindi na tuko tayari kwenda mbele tunachohitaji ni kuungwa mkono tu”, alisisitiza Mhe. Telack


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (katikati) akitoa maelekezo kwa Mtendaji Mkuu, Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), Dkt. Semvua Mzighani (kushoto)  alipotembelea vikundi vya ukulima wa mwani, ufugaji samaki na Kambakochi kwa lengo la kuhamasisha wananchi kuchangamkia fursa za ukuzaji viumbe maji zilizopo katika Mkoa wa Lindi Machi 1, 2022. 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega(katikati) akimueleza jambo Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack (kushoto) kuhusu ufugaji wa Samaki katika mabwawa walipotembelea kikundi cha ASM kinachoshughulika na ufugaji wa samaki katika mabwawa kwa kutumia maji ya hahari kilichopo Mkoani Lindi Machi 1, 2022. 

 


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (katikati) akimueleza jambo Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack (wa pili kutoka kulia) kuhusu ufugaji wa Samaki katika mabwawa kwa kutumia maji ya bahari walipotembelea kikundi cha ufugaji Samaki cha ASM kilichopo mkoani Lindi Machi 1, 2022. 

WASAIDIENI WANANCHI WANUFAIKE KUPITIA UCHUMI WA BULUU - ULEGA


Na Mbaraka Kambona, Lindi

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewataka Wataalam na Watendaji wa Serikali katika Mikoa ya Lindi na Mtwara kuwahamasisha Wananchi kutumia fursa zilizopo katika Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi hususan ufugaji wa  Majongoo Bahari, Kaa na Ukulima wa Mwani ili waweze kukuza kipato chao.

Naibu Waziri Ulega alitoa agizo hilo katika kikao kazi cha mkakati wa Kampeni ya Kuhamasisha Shughuli za Ukuzaji Viumbe Maji Bahari kwa Wataalam wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kilichofanyika Mkoani Lindi Februari 28, 2022.

"Uchumi wa buluu ni moja ya vipaumbele vya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake ya Awamu ya Sita, lakini namna gani tumetumia fursa hizo kulingana na uhitaji wa soko ili kuwainua watu katika uchumi wao na Taifa letu ndio kazi yetu sisi wataalam tuliopo hapa", alisema Mhe. Ulega

Alisema kuwa wataalam hao kuanzia Maafisa Ardhi, Maafisa Maendeleo na Ushirika, Maafisa Uvuvi na Maafisa Biashara wakishirikiana vyema watakuwa na mchango mkubwa katika kuwainua watu kiuchumi kupitia Rasilimali Bahari.

Aliongeza kwa kusema kuwa uchumi wa buluu una fursa kubwa ya biashara, hivyo ni lazima maafisa hao waweze kuwasaidia wananchi kuwaonesha fursa zinazopatikana humo ili waweze kuzalisha kwa wingi na kupelekea katika masoko makubwa na kukuza kipato chao.

Aidha, aliongeza kwa kuwataka wataalam hao kujipanga vyema na kwenda kuwajengea uwezo na kuwahamasisha Wananchi kutumia fursa hizo huku akifafanua kuwa wananchi wachache wakielewa fursa hizo kutashawishi watu wengi zaidi kuingia katika shughuli hizo.

"Ninaamini sisi Wataalam tukiwa na utayari wa kuwasaidia hawa wananchi kutumia fursa hizi vizuri basi tutaweza kuwaondoa katika hali ya uduni na wakawa na kipato cha uhakika", alisisitiza

Kuhusu mikakati ya Serikali kukuza Sekta ya Uvuvi ukanda wa kusini, Mhe. Ulega alisema katika Wilaya ya Kilwa Masoko panajengwa bandari kubwa ya Uvuvi itakayotoa fursa nyingi za kujiongezea kipato wananchi  lakini fursa hizo zote ili ziweze kuwa na tija ni muhimu timu ya wataalam hao ikapanga na kuwa na dhamira ya dhati ya kusaidia wananchi kunufaika na fursa hizo.

"Kwa kuanzia ni lazima muunde vikundi vya ushirika ambavyo vitakuwa na watu walio tayari ili Serikali itakapoleta pesa za kuwasaidia ikute vikundi hivyo vipo tayari", alifafanua


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiongea na Wataalam na Watendaji wa Serikali wa Mkoa wa Lindi na Mtwara wakati akifungua kikao kazi cha mkakati wa Kampeni ya Kuhamasisha Shughuli za Ukuzaji Viumbe Maji Bahari kwa Wataalam wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kilichofanyika Mkoani Lindi Februari 28, 2022.

Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mhe. Shaibu Ndemanga akitoa taarifa ya Mkoa kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (wa pili kutoka kushoto)  katika kikao kazi cha mkakati wa Kampeni ya Kuhamasisha Shughuli za Ukuzaji Viumbe Maji Bahari kwa Wataalam wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kilichofanyika Mkoani Lindi Februari 28, 2022. Katika kikao kazi hicho Mhe. Ndemanga alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack.
ULEGA AZIAGIZA HALMASHAURI KUWEZESHA VIKUNDI VYA USHIRIKA


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega ameziagiza Halmashauri za  Wilaya hususan zilizopo katika Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi kutoa asilimia 10 zinazotengwa na Serikali kwa ajili ya kuwezesha vijana na kuwapa vikundi vya ushirika vya Wafugaji jongoo bahari, kaa na Wakulima wa Mwani ili waweze kuongeza nguvu na kuendeleza shughuli zao za uzalishaji.

Ulega alitoa maelekezo hayo alipokuwa akiongea kwa nyakati tofauti na kikundi cha ufugaji jongoo bahari na kikundi cha wakulima wa mwani alipowatembelea kukagua shughuli wanazofanya Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani Februari 25, 2022.

Wakati akiongea na wanavikundi hao, Naibu Waziri Ulega alitumia nafasi hiyo kufikisha ujumbe kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kupitia Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo, Bw. Shauri Selenda kuwa asilimia 10 zinazotengwa na Serikali kwa ajili ya kuwezesha vijana  wapewe wanavikundi hao wanaofuga jongoo bahari, kaa na kilimo cha Mwani ili waweze kufanya uzalishaji mkubwa na wenye tija.

“Tunataka hii Pwani yetu yote kuanzia Moa kule Tanga Mpaka Msimbati itumike kwa ajili ya shughuli za uzalishaji, vijana na kina mama wawezeshwe kufanya shughuli hizi ili kuvutia watu wengine kufanya shughuli hizi na kuzalisha kwa tija zaidi”, alisisitiza Mhe. Ulega

Alisema lengo la kuwezesha vikundi hivyo ni kutaka wakue ili watoke katika uzalishaji mdogo na kuwa Kampuni na kuzalisha kwa wingi kitendo ambacho kitawaongezea kipato wao na taifa kwa ujumla.

“Haya mambo mnayofanya ya uzalishaji yameandikwa katika ilani ya Chama cha Mapinduzi, na hizo pesa tunazosema zitolewe ni utekelezaji wake chini ya maono ya Rais Samia Suluhu Hassan”, alifafanua

Aidha, Mhe. Ulega aliutaka uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kutembelea vikundi hivyo ili kujua changamoto zao na kuwaelekeza namna ya kufanya ili waweze kukopeshwa na benki hiyo.

“Lakini natoa maelekezo pia kwa watu wa benki ya kilimo, mtembelee hivi vikundi mpange vizuri na muwaongezee nguvu ili wapate mavuno ya uhakika, wewe Afisa Biashara kutoka Benki ya TADB, nakupa wiki moja urudi hapa ukutane na hawa wanavikundi, uweke nao mikakati na uwaelekeze namna ya kufanya ili waweze kupata hiyo mikopo”,alisema

Pamoja na hayo, aliwahimiza vijana kuendelea kuchangamkia fursa hizo za ufugaji wa majongoo bahari na ukulima wa mwani kwa sababu soko biashara hiyo ina manufaa makubwa na soko pana ambalo sio rahisi kulikidhi.

Katika hatua nyingine, Mhe. Ulega pia kuvipongeza vyombo vya habari kwa kazi nzuri wanayofanya ya kutangaza vyema fursa mbalimbali zinazopatikana katika uchumi wa buluu na hivyo aliendelea kuwaomba kuendelea na kazi hiyo ya kutangaza fursa hizo zinazopatikana nchini ili ziweze kuvutia wawekezaji wengi zaidi.

Lengo la ziara yake Mkoani Pwani ni kutathmini na kufanya kikao kazi cha kuweka Mikakati na kampeni ya kuhamasisha kutumia ipasavyo fursa za uchumi wa buluu huku akisisitiza  kuwa baada ya miezi 3 atarejea tena katika maeneo hayo ili kufanya ufuatiliaji wa maelekezo hayo.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiongea na Wanakikundi wa Kilimo cha Mwani kilichopo Kijiji cha Mlingotini, Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani Februari 25, 2022. Mhe. Ulega alitembelea kikundi hicho ikiwa Ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya siku mbili Mkoani Pwani ambayo lengo lake ni kutathmini na kufanya kikao kazi cha kuweka Mikakati na kampeni ya kuhamasisha kutumia ipasavyo fursa za uchumi wa buluu.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) akiwa amemshika Jongoo Bahari alipotembelea Kikundi cha kuzalisha Majongoo Bahari cha Kaole kilichopo Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani Februari 25, 2022. Mhe. Ulega alimuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kukiwezesha Kikundi hicho ili kiweze kuzalisha kwa tija.

 

ULEGA AHAMASISHA MIKOA YA PWANI KUCHANGAMKIA FURSA UCHUMI WA BULUU


Na Mbaraka Kambona, Pwani

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewahimiza Viongozi wa Mikoa iliyopo Pwani ya Bahari ya Hindi hususan Pwani na Dar es Salaam kuhamasisha wananchi wao kujiunga katika vikundi vya ushirika ili wawezeshwe na serikali kunufaika na fursa zinazopatikana katika uchumi wa buluu ikiwemo ufugaji wa kaa, majongoo bahari na kilimo cha mwani.

Ulega alitoa rai hiyo katika kikao kazi cha mkakati wa kampeni ya kuhamasisha shughuli za ukuzaji viumbe maji bahari kwa viongozi na wataalam wa mikoa ya Pwani na Dar es Salaam kilichofanyika Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani Februari 24, 2022.

Alisema ili wananchi waweze kunufaika na fursa hizo, suala la kuwa na ushirika ni muhimu sana huku akihimiza kila halmashauri kuhamasisha wananchi kujiunga katika vikundi na kuunda ushirika katika maeneo yao.

“Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hotuba yake aliyoitoa Januari 7, 2022 katika kilele cha Matembezi ya Miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar alisisitiza shughuli za ukuzaji viumbe maji hususani ufugaji wa kaa kuwa ni moja ya fursa za ajira kwa vijana”,alisema Mhe. Ulega

Alifafanua kwa kusema kuwa Ibara ya 43 (h) ya Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi inahimiza kuanzishwa vikundi vya ushirika vya wavuvi na wafugaji viumbe maji huku akiongeza kuwa  kukuza na kuimarisha uchumi wa buluu ni moja ya kipaumbele cha serikali ya awamu ya sita, hivyo ni muhimu kuwaanda wananchi na fursa pana iliyopo katika tasnia ya ukuzaji viumbe maji ili serikali inapoanza kuwawezesha wawe wako tayari.

Aidha, alisema Serikali inatambua changamoto mbalimbali zinazoikabili tasnia ya Ukuzaji Viumbe Maji katika kuzitumia fursa hizo zikiwemo mitaji midogo ya uwekezaji, upatikanaji wa pembejeo mbalimbali na masoko ya baadhi ya mazao yatokanayo na ukuzaji viumbe maji, katika kukabiliana na changamoto hizo,alisema, mwaka 2019, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilianzisha Dawati la Sekta Binafsi ili liwe kiunganishi au daraja kati ya Wizara, wawekezaji, masoko na taasisi za kifedha kama njia mojawapo ya ufumbuzi wa tatizo la mitaji, masoko na vitendea kazi kwa wavuvi, wakuzaji viumbe maji.

Lengo la ziara yake ni kutathmini na kufanya kikao kazi cha kuweka Mikakati na kampeni ya kuhamasisha kutumia ipasavyo fursa za uchumi wa buluu


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiongea na Viongozi na Wataalam wa Mikoa ya Pwani na Dar es Salaam katika Kikao Kazi cha Mikakati na Kampeni ya Kuhamasisha Shughuli za Ukuzaji Viumbe Maji Bahari kilichofanyika Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani Februari 24, 2022. Mhe. Ulega aliwahimiza Viongozi hao kuwahamasisha Wananchi wao kuchangamkia fursa zilizopo katika uchumi wa buluu ikiwemo  ufugaji wa Kaa, Majongoo Bahari, Kambakochi na ukulima wa Mwani.

Sehemu ya Viongozi na Wataalam wa Mikoa ya Pwani na Dar es Salaam walioshiriki katika Kikao Kazi cha Mikakati na Kampeni ya Kuhamasisha Shughuli za Ukuzaji Viumbe Maji Bahari kilichofanyika Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani Februari 24, 2022. Mhe. Ulega aliwahimiza Viongozi hao kuwahamasisha Wananchi wao kuchangamkia fursa zilizopo katika uchumi wa buluu ikiwemo  ufugaji wa Kaa, Majongoo Bahari, Kambakochi na ukulima wa Mwani.


NZUNDA ASISITIZA WATALAAM WA MIFUGO KUFANYA KAZI KWA WELEDI


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw.Tixon Nzunda amesisitiza watalaam wa Mifugo kufanya kazi zao kwa Weledi ili kusaidia Sekta ya Mifugo kusonga mbele.

Hayo ameyasema leo 23 feb 2022 alipokuwa akifungua kikao cha Watalaam wa Mifugo na Uvuvi kanda za nyanda za juu kusini na kusini Magharibi, mkoni Katavi.

"Watalaam fanyeni kazi zenu kwa Weledi ili wafugaji hawa wafaidike na huduma zenu, kila mtalaam awe na Register, ili mwisho wa siku aulizwe amehudumia wafugaji wangapi katika halmashauri yake, kata au kijiji.Lakini kama hiyo haitoshi kwa mwaka fedha 2023/2024 tutakuwa na mkataba wa utendaji kazi ili kupima utendaji kazi wa watalaam wetu" Alisema Nzunda.

Aidha, Nzunda amesema kuwa  Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kuwa na Mifugo mingi, asilimia 1.4 ya ng'ombe wote wako Tanzania na nchi yetu  ni ya pili barani Africa kwa uwingi wa Mifugo ikitanguliwa na Ethiopia, lakini bado tija hiyo ya kuwa na mifugo mingi kiasi hicho haionekani.

"Pamoja na kuwa Tanzania tuna ng'ombe 33 Milioni lakini bado inachangia kiasi kidogo sana katika pato la taifa, ni asilimia 7.1tu, tunazidiwa na Botswana yenye mifugo Milioni mbili lakini inachangia pato la taifa  zaidi ya asilimia 20."Alisema Nzunda.

Katibu Mkuu Mifugo amesema kuwa, sasa ni wakati mwafaka wa  kufanya mageuzi katika Sekta ya Mifugo kwa kila Mkoa wenye Mifugo/Halmashauri na kata kuandaa Mpango mkakati wa Sekta ya mifugo ili kuutekeleza Mpango huo ili Sekta iweze kusonga mbele na kuleta matokeo chanya na yenye tija kwa Taifa.

Pia, Bw. Nzunda amesisitiza kuwa suala la Uogeshaji Mifugo, Uchanjaji, Utambuzi na ufuatiliaji, ulimaji wa malisho sio suala la hiari tena,ni lazima kama tunataka mabadiliko katika Sekta, wafugaji wabadilike na waanze kufuga kwa tija.

Katika hatua nyingine katibu Mkuu mifugo ameweka jiwe la Msingi katika Ujenzi wa kiwanda cha usindikaji Maziwa cha MSS-Nsimbo Mkoani Katavi.

Mmiliki wa kiwanda hicho cha MSS-Nsimbo Bw. Marick Salum amesema kuwa kiwanda hicho kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kusindika Maziwa lita elfu mbili kwa saa. Pia amemwambia katibu Mkuu Mifugo kuwa mkoa wa Katavi una ng'ombe zaidi ya elfu moja hivyo upatikanaji wa Maziwa sio tatizo, pia uanzishwaji wa kiwanda hicho ni muhimu kwa sababu wafugaji watapata soko la kuuzia maziwa yao.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw.Tixon Nzunda akihutubia Watalaam wa Sekta ya Mifugo na Uvuvi(Hawapo pichani) wa kanda ya nyanda za juu kusini na kusini Magharibi leo tarehe 23/02/2022 Mkoani Katavi.Lengo la kikao hicho ni kubadilishana uzoefu katika utendaji kazi.Kulia ni Dkt.Samora Mshang'a,Daktari wa Mifugo kutoka mkoa wa Mbeya,kushoto ni Dkt.Anneth Kitambi, Mkurugnzi Msaidizi huduma za ukaguzi-Ustawi wa wanyama na utambuzi wa Mifugo.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw.Tixon Nzunda (Kushoto) akiweka jiwe la Msingi katika Ujenzi wa Kiwanda cha kusindika Maziwa cha MSS-Nsimbo Mkoani Katavi leo tarehe 23/02/2022.Kulia ni Bw.Marick Salum,Mmiliki wa Kiwanda cha MSS-Nsimbo.


KAIMU KATIBU MKUU WIZARA YA MIFUGO DKT. CHARLES MHINA AKIKAGUA MAENDELEO YA UJENZI WA JENGO LA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Charles Mhina ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu (Mifugo), (katikati), akitoa maagizo kwa mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa jengo la makao makuu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) pamoja na mshauri elekezi wa mradi huo Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA), kuhakikisha wanampatia taarifa ya kila wiki juu ya maendeleo ya mradi huo unaotekelezwa katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma. Kulia kwa kaimu katibu mkuu ni mbunifu wa majengo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Humphrey Killo anayesimamia mradi huo na kushoto kwa kaimu katibu mkuu ni mbunifu wa majengo kutoka TBA Bw. Weja Ng’olo. (23.02.2022)

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Charles Mhina ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu (Mifugo), (watatu kutoka kulia), akipatiwa maelezo ya ujenzi wa mradi wa jengo la makao makuu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoka kwa mmoja wa wasimamizi wa mradi huo unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma ambapo kaimu katibu mkuu huyo ameeleza kutoridhishwa na kasi ya ujenzi huo. (23.02.2022)

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Charles Mhina ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu (Mifugo), (katikati), akiwa ameambatana na baadhi ya watendaji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), wakati akikagua ujenzi wa mradi wa jengo la makao makuu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma baada ya kutoridhishwa na kasi ya ujenzi huo na kuagiza kuchukuliwa kwa hatua za haraka, ikiwemo ya muda wa kazi kuongezwa ili kukamilisha mradi huo katika muda wa miezi 24 kama ilivyoainishwa kwenye mkataba. (23.02.2022)

Muonekanao wa maendeleo ya ujenzi wa mradi wa jengo la makao makuu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) pamoja na mshauri elekezi wa mradi huo Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA), ambapo Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Charles Mhina ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu (Mifugo), ametembelea na kukagua mradi huo na kukataa ombi la NHC la kuongezewa muda wa zaidi ya miezi 24 nje ya mkataba ili kutekeleza mradi na kuagiza kuongezwa kwa muda wa saa za kazi, uwepo wa wafanyakazi zaidi pamoja na vifaa vya kutosha kwa ajili ya ujenzi. (23.02.2022)

 

NZUNDA ASISITIZA WAWEKEZAJI KUFUATA TARATIBU NA SHERIA YA MIKATABA YAO.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw.Tixon Nzunda amesisitiza wawekezaji wa Ranchi ya Taifa ya kalambo kufuata taratibu na sheria ya mikataba waliyoingia na  Ranchi hiyo.

Hayo ameyasema  Februari 22, 2022 alipotembelea Ranchi hiyo iliyopo mkoani Rukwa na kupata fursa ya kutembelea baadhi ya Vitalu vya Kalambo Ranchi na kushuhudio ufugaji bora unaofanyika katika Ranchi hiyo. 

"Fuateni taratibu mlizokubaliana na Ranchi katika kuendesha shughuli zenu katika vitalu vyenu mlivyopangishwa, kuanzia Vitalu vya muda mrefu mpaka vile vya Muda mfupi, Mikataba yenu inaelekeza mlime malisho kwenye vitalu vyenu,mjenge majosho, mchimbe Visima, nani kati yenu ametekeleza hayo??"Aliuliza Nzunda.

Aidha, Katibu Mkuu Mifugo Bw.Tixon Nzunda amekemea vikali wawekezaji ambao hawataki kuchanja mifugo yao, kuogesha au wanachanja mifugo michache na baadhi kuiacha bila kuchanja, amesema kwa kufanya hivyo mifugo hiyo bado itaendelea kuambukizana magonjwa.

"Tunataka vitalu vyenu viwe vya mfano kwa kuwa na mikakati endelevu ya Ufugaji, ogesheni, chanjeni mifugo yenu ili maeneo haya yawe maeneo huru ya Magonjwa"

Pia, Nzunda ameelekeza wafugaji hao kulima malisho katika Vitalu vyao, Kujenga Majosho, kuchimba Malambo na Visima ili inapotokea ukame au uhaba wa Malisho wawe na malisho ya kulisha mifugo yao.

Pia Katibu Mkuu Mifugo Nzunda alipata fursa ya kutembelea  ofisi za Zonal Veterinary centre (ZVC), Tanzania Veterinary laboratory Agency (TVLA) na kiwanda cha nyama cha SAAFI kilichopo Mjini sumbawanga na kukagua baadhi ya Miundombinu ya kiwanda hicho.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joseph Mkirikiti amesema kuwa anafarijika sana kuona sasa Viongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi  wanasimama kidete kusimamia na kutetea maslahi ya wafugaji ikiwemo kuhakikisha maeneo ya malisho hayachukuliwi na wakulima.

Katika hatua nyingine Meneja wa Kalambo Ranchi Bw. Noel Makawia amemweleza katibu Mkuu Mifugo kuwa Ranchi ya Kalambo inaukubwa  wa hekta 62,088.3 zenye uwezo wa kulisha ng'ombe Elfu ishirini mpaka ng'ombe Elfu ishirini na tano (20,000 -25,000)

Makawia amesema kuwa Ranchi hiyo imegawanyika katika sehemu kuu tatu ambapo ni eneo mama la Ranchi hiyo, lenye ukubwa wa hekta 13,588.3 ambalo lina jumla ya ng'ombe 1,796 Kondoo 186, Mbuzi 181 na farasi 11.

Makawia amebainisha kuwa eneo lingine ni la vitalu vya muda Mrefu ambalo linaukubwa wa Hekta 38,500 ambalo limetengwa katika vitalu 13 ambavyo vinaukubwa kati ya hekta 2,000-3,000 ambavyo vina jumla ya ng'ombe 14,036 mbuzi 1,103 kondoo 1,318 na Punda 85.

Eneo la tatu ni la vitalu vidogo vidogo lenye ukubwa wa hekta 10,000 ambalo limetengwa katika Vitalu 20 ambapo linajumla ya ng'ombe 5,700.

Makawia amemweleza katibu Mkuu Nzunda baadhi ya mipango yao ya baadaye ya kuhakikisha Ranchi hiyo inaendelea kuwa na malisho ya kutosha ikiwa ni pamoja na kulima shamba la malisho ekari 500 kutoka ekari 100 walizolima sasa, kuchimba bwawa kwa ajili ya kuvuna Maji ya Mvua na kujenga Machinjio ya kisasa.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw.Tixon Nzunda (Mwenye kaunda Suti ya Dark Blue) akikagua majengo ya ZVC pamoja na TVLA sumbawanga yaliyokarabatiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) leo tarehe 22/02/2022. Anayemwongo Katibu Mkuu Mwenye sharti la Draft ni Dkt. Rajabu Mlekwa Meneja Mfawidhi TVLA.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw.Tixon Nzunda (wa pili kutoka kushoto) akimsikiliza Meneja wa Kiwanda cha nyama cha SAAFI Bw.James Michael (wa kwanza kushoto) akitoa maelezo mafupi juu kiwanda hicho.Wengine ni Dkt.Anneth Kitambi, Mkurugenzi Msaidizi huduma za Ukaguzi-Ustawi wa Wanyama na Utambuzi wa Mifugo, Bw.Salehe Msanda, Katibu Tawala Msaidizi Seksheni ya Uchumi na Uzalishaji kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Watumishi wengine kutoka ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Rukwa.


 

Jumanne, 1 Machi 2022

Waziri wa mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki watembelea Ofisi za National Service Projects Organization ya Misri na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Misri

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) (wa tatu kutoka kushoto) na ujumbe kutoka Tanzania wakiwa kwenye kikao kifupi na wenyeji wao wa Misri  mara baada ya kuwasili Nchini humo lengo likiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu na kukuza ushirikiano katika Sekta ya Uvuvi. Februari 21, 2022.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kutoka kushoto) pamoja na ujumbe wake kutoka Tanzania walitembelea Ofisi za National Service Projects Organization ya Misri  na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Misri ukiongozwa na Naibu Waziri wa Ulinzi Jenerali Medhat El  Nahas, lengo likiwa ni pamoja na kueleza fursa za ushirikiano na uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Uvuvi Nchini Tanzania. Februari 21,2022

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) (kushoto meza kuu ) akiwa kwenye  picha ya pamoja na  Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Taifa ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji Misri, Jenerali Eslam Attia Rayan, wakiwa na  ujumbe kutoka Tanzania na ujumbe kutoka Misri wakati wa ziara rasmi nchini  humo, lengo likiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu na kukuza ushirikiano katika Sekta ya Uvuvi. Februari 21, 2022.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kushoto waliokaa) na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Taifa ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji Misri  Jenerali Eslam Attia Rayan wakitia saini kwenye  hati ya makubaliano ya ushirikiano Kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) na Kampuni ya Taifa ya NCFA. Februari 21, 2022 nchini Misri, lengo likiwa ni kukuza ushirikiano na uwekezaji katika minyororo ya thamani ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji pamoja na kukuza utaalam katika Sekta ya Uvuvi.

 

IDARA TA DGLF YATEMBELEA KIJIJI CHA OLOLOSOKWANI KUONA ENEO LILILOPENDEKEZWA KWA AJILI YA UJENZI WA JOSHO.

Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Dkt. Asimwe Rwiguza (wa kwanza kushoto) akiwa na Wataalam kutoka Sekta ya Mifugo na Uongozi wa Kijiji cha Ololosokwani wakati alipotembelea eneo lililopendekezwa kwa ajili ya ujenzi wa Josho. (15.02.2022)

Baadhi ya wafugaji wa Kijiji katika vijiji vya Ololosokwani na Soitsambu wilayani Ngorongoro mkoa wa Arusha wakisikiliza maelezo ya Wataalam kutoka Sekta ya Mifugo wakati walipotembelea vijiji hivyo kwa lengo la kutoa elimu kuhusu uboreshaji wa Kosaafu za Mifugo, Udhibiti wa magonjwa ya mifugo na Maeneo ya Malisho. (15.02.2022)

Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Dkt. Asimwe Rwiguza akiwasalimu wafugaji wa Kijiji cha Soitsambu wakati Wataalam wa Sekta ya Mifugo walipofika kijijini hapo kwa lengo la kutoa elimu kuhusu uboreshaji wa Kosaafu za Mifugo, Udhibiti wa magonjwa ya mifugo na Maeneo ya Malisho. (15.02.2022)

 

SUMU KUVU TISHIO LA USUGU WA DAWA KWA BINADAMU NA MIFUGO

 

Na. Edward Kondela

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imesema katika mwaka ujao wa fedha 2022/2023 inatarajia kuongeza wigo wa kufanya vipimo vya ubora wa vyakula vya mifugo ili kubaini aina za sumu kuvu ambazo zinaweza kusababisha madhara ya kiafya kwa binadamu na mifugo.

Mtendaji Mkuu wa TVLA Dkt. Stella Bitanyi amebainisha hayo ofisini kwake jijini Dar es Salaam, wakati wa zoezi la kuhakiki ubora wa vyakula vya mifugo vinavyozalishwa hapa nchini lililofanyika mwishoni mwa wiki, zoezi ambalo limefanywa katika wilaya za Temeke na Ubungo na wataalamu kutoka TVLA.

Dkt. Bitanyi amesema wakala hiyo inatarajia pia kupima mabaki ya ‘antibiotic’ na dawa nyingine za mifugo ndani ya vyakula vya mifugo ili kuhakikisha ubora wa vyakula vya mifugo kwa kutokuwa na mabaki ya dawa ambazo zinaweza kusababisha usugu wa dawa kwa mifugo pamoja na binadamu atakayetumia mazao yanayotokana na mifugo hiyo.

Katika hatua nyingine mtendaji mkuu huyo wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), ametoa wito kwa wazalishaji wa vyakula vya mifugo nchini pamoja na wafugaji kuhakikisha wanafikisha sampuli za vyakula katika maabara hiyo ili kupima ubora wa chakula ambacho kinastahili kutumiwa na mifugo pamoja na malighafi ambazo zitatumiwa katika kutengeneza vyakula hivyo.

Amebainisha kuwa matumizi ya vyakula sahihi vya mifugo ambavyo vina virutubisho vinavyostahili, vitamuwezesha mfugaji kufuga kwa tija kwa kuwa mifugo itakuwa katika muda unaotakiwa kitaalamu na kufikia kiwango cha uzito unaotakiwa sokoni.

Akizungumza wakati wa zoezi la kukagua ubora wa vyakula vya mifugo katika Wilaya za Temeke na Ubungo, Afisa Mtafiti wa Mifugo kutoka TVLA Dkt. Evaline Mfuru amesema uwiano sawa wa virutubisho vinavyotakiwa kwenye vyakula vya mifugo kwa kiasi kikubwa hupunguza gharama za uzalishaji pamoja na kudhibiti magonjwa ya mifugo.

Nao baadhi ya wafugaji na wazalishaji wa vyakula vya mifugo wamesema zoezi la uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo litakuwa na tija kwa kuhakikisha vinapatikana vyakula bora, ambavyo vitaleta tija kwa mfugaji pamoja na kuondoa sokoni vyakula vya mifugo ambavyo havikidhi vigezo.

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) ambayo iko chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikifanya uchunguzi wa ubora wa vyakula vya mifugo ili vyakula hivyo viwe katika viwango vinavyotakiwa kwa ajili ya matumizi ya mifugo na kuleta tija kwa mfugaji.


Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi, akizungumza ofisi kwake jijini Dar es Salaam, juu ya mipango ya TVLA katika mwaka ujao wa fedha 2022/2023 kuongeza wigo wa kufanya vipimo vya ubora wa vyakula vya mifugo ili kubaini aina za sumu kuvu ambazo zinaweza kusababisha madhara ya usugu wa dawa kwa binadamu na mifugo. (14.02.2022)

Kutoka kushoto ni Mkaguzi wa Vyakula vya Mifugo kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Temeke Bi. Theodora Baziwe, akifuatiwa na Fundi Sanifu Maabara kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Bw. Henry Mlundachuma, wakizungumza na mfugaji Bw. Erasto Mbise, walipomtembelea nyumbani kwake katika Wilaya ya Temeke Mkoani Dar es Salaam ili kujiona shughuli za ufugaji na vyakula vya mifugo anavyotumia ikiwa ni sehemu ya kuhakiki ubora wa vyakula vya mifugo zoezi lililofanywa katika wilaya za Temeke na Ubungo na wataalamu kutoka TVLA.  (14.02.2022)