Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw.Tixon Nzunda amesisitiza wawekezaji wa Ranchi ya
Taifa ya kalambo kufuata taratibu na sheria ya mikataba waliyoingia na Ranchi hiyo.
Hayo ameyasema Februari 22, 2022 alipotembelea Ranchi hiyo
iliyopo mkoani Rukwa na kupata fursa ya kutembelea baadhi ya Vitalu vya Kalambo
Ranchi na kushuhudio ufugaji bora unaofanyika katika Ranchi hiyo.
"Fuateni taratibu
mlizokubaliana na Ranchi katika kuendesha shughuli zenu katika vitalu vyenu
mlivyopangishwa, kuanzia Vitalu vya muda mrefu mpaka vile vya Muda mfupi,
Mikataba yenu inaelekeza mlime malisho kwenye vitalu vyenu,mjenge majosho,
mchimbe Visima, nani kati yenu ametekeleza hayo??"Aliuliza Nzunda.
Aidha, Katibu Mkuu Mifugo
Bw.Tixon Nzunda amekemea vikali wawekezaji ambao hawataki kuchanja mifugo yao,
kuogesha au wanachanja mifugo michache na baadhi kuiacha bila kuchanja, amesema
kwa kufanya hivyo mifugo hiyo bado itaendelea kuambukizana magonjwa.
"Tunataka vitalu vyenu
viwe vya mfano kwa kuwa na mikakati endelevu ya Ufugaji, ogesheni, chanjeni
mifugo yenu ili maeneo haya yawe maeneo huru ya Magonjwa"
Pia, Nzunda ameelekeza
wafugaji hao kulima malisho katika Vitalu vyao, Kujenga Majosho, kuchimba
Malambo na Visima ili inapotokea ukame au uhaba wa Malisho wawe na malisho ya
kulisha mifugo yao.
Pia Katibu Mkuu Mifugo
Nzunda alipata fursa ya kutembelea ofisi
za Zonal Veterinary centre (ZVC), Tanzania Veterinary laboratory Agency (TVLA)
na kiwanda cha nyama cha SAAFI kilichopo Mjini sumbawanga na kukagua baadhi ya
Miundombinu ya kiwanda hicho.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Rukwa
Mhe. Joseph Mkirikiti amesema kuwa anafarijika sana kuona sasa Viongozi wa
Wizara ya Mifugo na Uvuvi wanasimama
kidete kusimamia na kutetea maslahi ya wafugaji ikiwemo kuhakikisha maeneo ya
malisho hayachukuliwi na wakulima.
Katika hatua nyingine
Meneja wa Kalambo Ranchi Bw. Noel Makawia amemweleza katibu Mkuu Mifugo kuwa
Ranchi ya Kalambo inaukubwa wa hekta
62,088.3 zenye uwezo wa kulisha ng'ombe Elfu ishirini mpaka ng'ombe Elfu
ishirini na tano (20,000 -25,000)
Makawia amesema kuwa Ranchi
hiyo imegawanyika katika sehemu kuu tatu ambapo ni eneo mama la Ranchi hiyo,
lenye ukubwa wa hekta 13,588.3 ambalo lina jumla ya ng'ombe 1,796 Kondoo 186,
Mbuzi 181 na farasi 11.
Makawia amebainisha kuwa eneo lingine ni la vitalu vya muda Mrefu ambalo linaukubwa wa Hekta 38,500 ambalo limetengwa katika vitalu 13 ambavyo vinaukubwa kati ya hekta 2,000-3,000 ambavyo vina jumla ya ng'ombe 14,036 mbuzi 1,103 kondoo 1,318 na Punda 85.
Eneo la tatu ni la vitalu
vidogo vidogo lenye ukubwa wa hekta 10,000 ambalo limetengwa katika Vitalu 20
ambapo linajumla ya ng'ombe 5,700.
Makawia amemweleza katibu
Mkuu Nzunda baadhi ya mipango yao ya baadaye ya kuhakikisha Ranchi hiyo
inaendelea kuwa na malisho ya kutosha ikiwa ni pamoja na kulima shamba la
malisho ekari 500 kutoka ekari 100 walizolima sasa, kuchimba bwawa kwa ajili ya
kuvuna Maji ya Mvua na kujenga Machinjio ya kisasa.
Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi Bw.Tixon Nzunda (Mwenye kaunda Suti ya Dark Blue) akikagua
majengo ya ZVC pamoja na TVLA sumbawanga yaliyokarabatiwa na Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Mifugo) leo tarehe 22/02/2022. Anayemwongo Katibu Mkuu Mwenye sharti
la Draft ni Dkt. Rajabu Mlekwa Meneja Mfawidhi TVLA.
Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi Bw.Tixon Nzunda (wa pili kutoka kushoto) akimsikiliza Meneja wa
Kiwanda cha nyama cha SAAFI Bw.James Michael (wa kwanza kushoto) akitoa maelezo
mafupi juu kiwanda hicho.Wengine ni Dkt.Anneth Kitambi, Mkurugenzi Msaidizi
huduma za Ukaguzi-Ustawi wa Wanyama na Utambuzi wa Mifugo, Bw.Salehe Msanda,
Katibu Tawala Msaidizi Seksheni ya Uchumi na Uzalishaji kutoka ofisi ya Mkuu wa
Mkoa na Watumishi wengine kutoka ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni