Nav bar

Jumanne, 30 Septemba 2025

TANZANIA YAZINDUA RASMI MRADI WA STOSAR II: KUBORESHA USALAMA NA UBORA WA CHAKULA

Tanzania kung’aa masoko ya kimataifa

Na Daudi Nyingo-Dar Es Salaam

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Ulaya (EU), na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), imezindua rasmi Mradi wa STOSAR II unaolenga kuimarisha mifumo ya Sanitary and Phytosanitary (SPS) katika ukanda wa SADC ili kuwezesha biashara salama, ushindani na uendelevu wa mazao ya kilimo na vyakula.

Akizindua mradi huo tarehe 1 Septemba 2025 katika Hoteli ya Four Points by Sheraton jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede, alisema mradi huo utashughulikia maeneo muhimu yakiwemo afya ya wanyama, afya ya mimea, lishe na maendeleo ya minyororo ya thamani, hususan katika nyanja za uchunguzi na ufuatiliaji wa magonjwa, udhibiti wa ubora, na upatikanaji wa masoko ya kikanda na kimataifa.

“Mkutano huu ni tukio mahususi la kuzindua mradi huu wa kikanda ambao Tanzania ni miongoni mwa wanufaika. Mradi huu unalenga kuimarisha mifumo ya usafi na usalama wa chakula. Ninaposema chakula, simaanishi tu vyakula vya kawaida, bali pia mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, kwa kuzingatia afya na usalama wa walaji. Kwa lugha ya kitaalamu, tunasema Sanitary and Phytosanitary Measures (SPS).” alisema Dkt. Mhede.

Akizungumzia utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huo uliyoanza mwaka 2018, Dkt. Mhede alieleza kuwa zaidi ya wataalamu 150 wa Tanzania tayari wamenufaika kwa kupata mafunzo, ingawa utekelezaji ulikumbwa na changamoto kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO-19 (COVID-19).

“Lengo kuu la awamu ya pili ni kujenga mfumo imara ambapo taarifa za usalama na ubora wa chakula zinapatikana kwa wakati na kuwasilishwa kwa wadau ili kufanya maamuzi sahihi yanayozingatia ushahidi wa kisayansi. Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi na washirika wa maendeleo itaendelea kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa mafanikio.” aliongeza Dkt. Mhede.

Kwa upande wake, Mkuu wa Rasilimali Asilia katika Ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania  (EU), Bw. Lamine Diallo, alisema Umoja wa Ulaya umekuwa mshirika wa kudumu katika kilimo cha kanda hii kwani kwa miaka mingi wamefanya kazi kwa karibu na Tanzania kupitia programu mbalimbali za kuongeza uzalishaji, kukuza mbinu za kilimo zinazoangalia mabadiliko ya tabianchi, kuboresha afya ya mimea, na kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha na masoko ya kikanda na kimataifa. 

“Awamu hii mpya inajenga juu ya mafanikio makubwa ya STOSAR I, ambayo ilikamilika mwaka 2024. Awamu ya kwanza iliweka msingi muhimu kwa kuimarisha mifumo ya taarifa za kilimo, kuongeza uwezo wa kiufundi, na kuboresha usalama wa chakula na lishe katika kanda nzima. Kupitia STOSAR II, maono yetu ya pamoja ni kutoka kwenye hatua ya kuweka misingi hadi kufanikisha matokeo dhahiri, na kutekeleza kikamilifu sera ya kilimo ya kikanda ya SADC ili kutoa manufaa halisi kwa wananchi wa Afrika Mashariki na Kusini.” alisema Bw. Diallo.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa upande wa Tanzania, Dkt. Nyabenyi Tito Tipo, alisema kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, maendeleo makubwa yametokea katika utekelezaji wa mifumo ya Usafi na Usalama wa Chakula (SPS) nchini Tanzania, licha ya changamoto nyingi ambazo zinaweza kuwa kikwazo katika kuingia kwenye masoko ya kimataifa kama Umoja wa Ulaya (EU), Asia, na masoko mengine.

“Katika kipindi hiki, zaidi ya wakulima 200 wa parachichi wamefanikiwa kuuza mazao yao nje ya nchi, hasa kwenda Afrika Kusini na India. Washirika wa mafunzo pia wamelihakikishia kutokuwepo kwa virusi vya mafua hatari ya ndege (highly pathogenic avian influenza) nchini, pamoja na kutokuwepo kwa ugonjwa wa Fusarium wilt (ugonjwa wa ndizi), jambo ambalo limeimarisha usalama wa mimea. Aidha, kampeni ya chanjo ya Peste des Petits Ruminants (PPR) ilitekelezwa kwa mafanikio, ikiongeza nguvu katika mifumo ya afya ya wanyama. Msingi pia umewekwa ili kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya kuuza nje, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuuza bidhaa kwenda Mauritius.” alisema Dkt. Tipo.








MIFUGO NA UVUVI YAANZA KIBABE SHIMIWI 2025

◼️ Yawararua Maadili 2-0 Kamba Wanaume

◼️Yatwaa Magoli 40 na pointi 2 Mpira wa pete baada ya Maendeleo ya Jamii kutokomea kusikojulikana

Timu za mchezo wa Kamba upande wa Wanaume na Mpira wa pete kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi zimeanza vema kampeni ya kuwania ubingwa wa michuano ya SHIMIWI 2025 baada ya kuibuka na ushindi kwenye michezo yao ya leo Septemba 01,2025 iliyofanyika jijini Mwanza.

Nyota njema kwa Timu hizo ambazo zimekuwa gumzo jijini Mwanza tangu zilipoingia ilianza kwa upande wa mchezo wa kuvuta Kamba Wanaume ambapo walipimana ubavu na timu ya Tume ya Maadili na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mivuto yote miwili.

Baada ya ushindi huo kikosi cha wachezaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kilielekea kwenye uwanja wa CCM Kirumba kulikofanyika mchezo wa mpira wa Pete baina yao na timu ya Maendeleo ya jamii ambayo ilipotea ghafla na kumlazimu mwamuzi wa mchezo huo kuipa timu ya Mifugo na Uvuvi ushindi wa magoli 40-0 na pointi 2.

Kampeni ya kusaka ubingwa wa Michuano hiyo kwa Upande wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaendelea kesho ambapo timu ya soka itachuana na timu ya Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, kamba wanawake wakimenyana na timu ya Ofisi ya Makamu wa Rais, kamba wanaume wakichuana na UCSAF  na mpira wa pete kivumbi kitakuwa baina yao na timu ya Tume ya Utumishi.




MIKATABA YA UBORESHAJI KITUO CHA UKUZAJI VIUMBE MAJI KINGOLWIRA YASAINIWA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena ameongoza zoezi la utiaji sani baina ya serikali na wakandarasi watakaotekeleza miradi ya ukarabati wa vitotoreshi ya vifaranga, ujezi wa  mifumo ya hewa kwenye mabwawa ya kufugia samaki, uchimbaji wa visima vya maji eneo la Kingolwira mkoani Morogoro na ujenzi wa Soko la Samaki  Kipumbwi katika wilaya ya Pangani mkoa wa Tanga  na kuwataka wakandarasi hao kukamilisha miradi hiyo kwa wakati na kuzingatia viwango vya ubora kama mkataba unavyoelekeza. 

Bi. Meena amesema hayo leo Agosti 29, 2025 katika ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo mji wa serikali Mtumba Jijini Dodoma mara baada kusaini mikataba minne na wakandarasi hao ambapo aliwasisitiza kuzingatia muda na ubora wa miradi kulingana na makubaliano ya Mkataba.

"Miradi hii ni ya kimkakati kwa wizara yetu na kama mnavyojua inawagusa moja kwa moja wananchi hivyo mtekeleze  kwa kuzingatia muda na ubora wa miktaba ili uwanufaishe wananchi wetu." Alisema, Bi. Meena.

Kwa upande wao wakandarasi  wa miradi hiyo wameahidi kutekeleza mikataba yao kwa wakati na kuzingatia ubora ili ianze kufanya kazi kwa wakati.

Mikataba iliyosaini ni pamoja na Mkataba wa  kuchimba visima viwili vya maji eneo la Kingolwira Mkoani Morogoro unaotekelezwa na Kampuni ya EF. IMER CONSTRUCTION CO. LTD, Mkataba wa ujezi mifumo ya hewa Katika Mabwawa ya kufugia samaki  Kingolwira unaotekelezwa na kampuni ya Kanuta Engineering and Supply Limited.

Mikataba mingine ni ile ya ujenzi wa vitotoreshi vya Vifaranga vya samaki Kingolwira Morogoro, unaotekelezwa na Kampuni KPM investment LTD na Ujenzi wa Soko la Samaki eneo la ujenzi wa soko la samaki Kipumbwi pangani Tanga ambao unatekelezwa na Kampuni itwayo WCEC LIMITED kutoka  Dar es salaam.