Jumatatu, 29 Juni 2020
HALMASHAURI ZASHAURIWA KUIGA MACHINJIO YA ILALA.
Katibu Mkuu wa Wizara
ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Elisante Ole Gabriel amezishauri Halmashauri zote
nchini ambazo zinafanya shughuli za ufugaji kuiga mfano wa Machinjio ya
kisasa ya Ilala ili nao waone haja ya kuwa na machinjio ya kisasa
yatakayosaidia kuboresha biashara ya machinjio na kuongeza pato la halmashauri
zao.
Profesa Ole Gabriel
alitoa rai hiyo ofisini kwake jijini Dodoma Juni 26, 2020 alipokutana na Timu
ya Wataalamu kutoka Manispaa ya Ilala waliokuja kutembelea Machinjio ya Dodoma
ili kujifunza namna ambavyo machinjio hayo yanavyoendeshwa.
Akiongea na Wataalamu
hao, Prof. Ole Gabriel alisema itapendeza kama kila halmashauri ikawa na
machinjio ya kisasa kwani yatasaidia kuongeza mapato ya halmashauri hizo na
kuachana na kukimbizana kila siku na waendeshaji wa machinjio yaliyopo sasa
ambayo hayana viwango ambavyo vinatakiwa.
“Niwaombe Makatibu
Tawala wa Mikoa waliangalie hili, waone uwezekano wa kujenga machinjio ya
kisasa yatakayosaidia kuboresha mazingira ya biashara yatakayochagiza kuongezeka
kwa mapato ya Halmashauri,”alisema
Aliongeza kuwa sio
lazima Halmashauri zijenge Machinjio wao wenyewe, wanaweza kuingia ubia na
sekta binafsi na wakajenga machinjio ya kisasa wakawa wanauza nyama katika soko
la ndani na nje ya nchi, kodi ya Serikali ikawa inalipwa na wateja wakaendelea
kupata huduma nzuri.
Prof. Ole Gabriel
aliendelea kusema kuwa biashara ya nyama sio ndogo huku akifafanua kuwa kwa sasa wastani
wa kilo milioni 2.6 za nyama zinaliwa nchini kila siku na hivyo aliwahimiza
maafisa biashara kuelimisha jamii kuhusu zao la nyama ili watu wale nyama kwa
wingi.
“Kwa mujibu wa Shirika
la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) mahitaji ya kidunia kwa mtu mmoja anatakiwa
kula kilo 50 kwa mwaka, lakini sisi Watanzania bado wastani wetu wa kula nyama
kwa mtu bado upo chini sana, kwa sasa tumefikia kilo 15 kwa mwaka, bado kiasi
ni kidogo sana,” alieleza
“Maafisa biashara
tumieni taaluma zenu kuelimisha umma kuhusu zao la nyama ili watu wale
nyama, watu wakila nyama kwa wingi itachagiza biashara ya machinjio na ndipo
hasa uwekezaji pia utakwenda vizuri,” alisisitiza
Aidha, aliipongeza
Halmashauri ya Bahi kwa jitihada wanazoendelea nazo za kujenga machinjio ya
kisasa jambo ambalo litaboresha biashara ya machinjio na kuongeza pato la
Halmashauri hiyo.
Akielezea kuhusu
machinjio ya Dodoma, Prof. Ole Gabriel alisema kabla machinjio hayo
hayajachukuliwa na Serikali ng’ombe waliokuwa wanachinjwa kwa siku ni kati ya
40 mpaka 50 lakini toka machinjio hiyo irudishwe serikalini namba ya ng’ombe wanaochinjwa imepanda
kufikia 150.
Aliendelea kueleza
kuwa mikakati waliyonayo kuhusu machinjio hayo ni kuendelea kuiboresha kufikia
kuwa Machinjio ya Mfano kwa Afrika Mashariki, Ukanda wa Nchi za SADC na hata
ikiwezekana Afrika.
Aidha, Prof. Ole
Gabriel alisema kuwa anaamini ziara hiyo ni katika kutambua jitihada za
Wizara na hivyo aliwahakikishia wataalamu hayo kuwa Wizara ipo tayari
kushirikiana na Manispaa ya Ilala kuhakikisha mipango yao inafanikiwa na
machinjio hiyo iweze kufanya kazi zake kama walivyokusudia.
Naye Afisa Masoko wa
Manispaa ya Ilala, ambaye pia ndiye alikuwa kiongozi wa timu hiyo ya Wataalamu,
Ando Mwankuga alisema machinjio ya Ilala ni mradi wa kimkakati katika kuboresha
mazingira ya biashara ya machinjio ambayo itawawezesha kuwa na nyama za viwango
zitakazouzika hata nje ya nchi.
“Lengo la mradi ni
kuongeza mapato ya Manispaa, tunaamini mradi ukikamilika na kuanza kazi
tutapunguza utegemezi kwa Serikali,” alisema
Alisema machinjio hiyo
ambayo ni kubwa na ya kisasa inategemewa kuanza kufanya kazi Disemba, 2020
na watakuwa wanachinja ng’ombe 1500 na mbuzi 1000 kila siku.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof.
Elisante Ole Gabriel (katikati) akisisitiza jambo wakati akiongea na timu ya
wataalam kutoka manispaa ya Ilala (hawapo pichani) waliokuja kumtembelea
ofisini kwake jijini Dodoma Juni 26,2020. Kulia ni Afisa Mipango wa Manispaa ya
Ilala, Ando Mwankuga, kushoto niKaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji Mifugo
na Masoko wa Wizara ya mifugo na Uvuvi Bw. Abdallah Temba.
Afisa Mipango wa
Manispaa ya Ilala, Ando Mwankuga akieleza lengo la Ziara yao kwa Katibu Mkuu wa
Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) walipomtembelea
ofisini kwake mapema Juni 26,2020.
Baadhi ya wajumbe kutoka Manispaa ya Ilala
wakiwa katika kikao wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,
Prof. Elisante Ole Gabriel (hayupo pichani) walipomtembelea ofisini kwake
jijini Dodoma. Juni 26,2020.
Ijumaa, 26 Juni 2020
MADAKTARI WA MIFUGO WATAKIWA KUHUISHA TAARIFA ZAO.
Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania, Dkt.Bedan Masuruli
amewataka Madaktari wa Mifugo nchini kuhuisha majina yao kwenye daftari la
usajili wa madaktari wa mifugo kabla ya Julai 1, 2020.
Wakati akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma Juni 26,
2020, Dkt. Masuruli amesema ni muhimu wataalam kuhuisha majina yao ili baraza
liweze kufahamu wako wapi, wanafanya nini na wanatoa huduma gani.
"Nasisitiza madaktari wote wa mifugo ambao hawajahuisha
taarifa zao kwenye daftari la usajili wa madaktari wafanye hivyo kuanzia leo
hadi kufikia Juni 30, 2020 kwani kuanzia Julai mosi tunaanza kusimamia
Sheria" amesema Dkt. Masuruli.
Hata hivyo Dkt. Masuruli amesema wanafanya haya yote ili kuboresha
huduma kwa wafugaji wote nchini na watatoa vitambulisho kwa wataalam wote ili
wafugaji waweze kuwatambua.
Amesema kuwa wamejipanga kusambaza wataalamu wa mifugo
kwenye ngazi za msingi ili kuwa karibu na wananchi na kuwashauri namna ya
kuipatia kinga mifugo hiyo na kuleta tija katika ufugaji wao.
Aliongeza kuwa ili kufikia adhima hiyo ni lazima
wataalamu wote wa ngazi ya msingi kusajiliwa, kujiandikisha na kujiorodhesha
katika daftari ili kusaidia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kujua ubora wa wataalamu
walionao katika maeneo yote na kusaidia wananchi kuongeza tija
katika sekta ya ufugaji.
Tumeongeza muda ili wataalum waweze kuhuisha majina yao kwenye
daftari la usajili wa madaktari kabla ya Julai 1 wawe tayari wamejisajili, na
kwa ambaye hata fanya hivyo sheria za usajili zitachukua mkondo
wake,alisisitiza
“Baada ya kuhuisha taarifa zao, wataalamu watapatiwa
vitambulisho maalum ili kusaidia wafugaji na wananchi kutambua kuwa ni mtaalamu
aliyekidhi viwango hivyo, mwananchi anaweza kupatiwa huduma kwa kupata ushauri,
kinga na namna ya kuboresha ufugaji ili kufikia mafaniko makubwa, aliongeza
Dkt.Masuruli amesema kuwa Wataalamu hao watatakiwa
kuwasilisha Wizarani taarifa za magonjwa ya mifugo inayosumbua katika maeneo
yao ili kusaidia serikali kuandaa mpango kazi wa kutatua changamoto
zilizoshindikana kutatuliwa na wataalaum hao.
Aidha, amesisitiza kuwa lengo kuu la kusogeza huduma hizo kwa
wananchi ni kutaka kuhakikisha wanapatiwa huduma bora zinazokidhi viwango na
itasaidia kubaini magonjwa yanayojitokeza katika mifungo ya wananchi wanao
wahudumia na kuwasaidia kwa ukaribu.
“Natoa wito kwa vituo vyote vya afya ya wanyama kuanzia Julai
Mosi, 2020 kuweka mpango wa muda wa miezi mitatu kupata hadubini katika vituo
hivyo ili kusaidia kujua magonjwa katika mifugo ya wananchi wao wanao
wahudumia, alifafanua.
Dkt.Masuruli ameongeza kuwa ili wananchi waweze
kunufaika na ufugaji wanahitaji wataalamu wa mifugo kuwa karibu na wafugaji ili
kuwasaidia kuwapatia huduma bora itakayokidhi viwango na kuleta tija kwa
asilimia kubwa na kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Jumanne, 23 Juni 2020
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI MHE. LUHAGA MPINA AFANYA UTEUZI.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina amemteua Prof. Malongo Richard Mlozi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala ya Vyuo vya Mifugo Tanzania(LITA) na amewateua wafuatao kuwa Wajumbe wa Bodi ya LITA. Kupata orodha ya wajumbe walioteuliwa bofya hapa
MAGUFULI APONGEZA MAFANIKIO YALIYOPATIKANA SEKTA YA MIFUGO NA UVUVI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Magufuli
ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa jitihada kubwa ilizozichukua katika
kipindi cha miaka mitano ya Uongozi wake ambazo zimesaidia kuboresha na kukuza
uchumi wa nchi.
Akizungumza wakati akitoa hotuba yake ya kulifunga Bunge la kumi
na moja (11) la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Juni 16, 2020 jijini Dodoma,
Rais Magufuli alisema kuwa katika kipindi hiki cha miaka mitano ya uongozi wake
Wizara ya mifugo imechukua hatua kadhaa ambazo zimesaidia nchi kufikia
mafanikio makubwa.
Rais Magufuli akitaja baadhi ya maeneo ambayo Wizara
imeyashughulikia na kupata mafanikio, alisema kuwa katika kipindi hicho
serikali iliongeza eneo la ufugaji kutoka hekta milioni 1.4 mwaka 2005 hadi
kufikia hekta milioni 5 mwaka 2020. Jambo ambalo amelitaja kuwa limechangia kwa
kiasi kikubwa kupunguza migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, Serikali kupitia Wizara imejenga
mabwawa mapya ya kuogeshea ng’ombe 104, imesambaza chanjo na dawa za Mifugo
nchi nzima, huku idadi ya ng’ombe waliohimilishwa imeongezeka kutoka laki moja
na elfu tano (105,000) mwaka 2015 hadi kufikia laki tano kumi na nne elfu na
mia saba (514,700).
Aliongeza kuwa serikali imeimarisha ulinzi na usimamizi wa
rasilimali za uvuvi, kwa kuanzisha kanda kuu tatu (3) za Ziwa Victoria,
Tanganyika na Pwani ikiwa ni pamoja na kudhibiti zana haramu za uvuvi.
“Nakumbuka kuna wakati nilimuona Mhe. Mpina alikuwa anatembea na
rula kwenye Migahawa kupima urefu wa Samaki, hiyo ilikuwa ni katika hatua za
kuhakikisha tunapata mafanikio haya ambayo tumeyapata”, alisema Rais Magufuli.
Aliendelea kusema kuwa Wizara imehamasisha na kufanikiwa
kuongeza idadi ya Wafugaji wa Samaki kutoka laki moja themanini elfu na mia
nane arobaini na tatu (180,843) mwaka 2015 hadi kufikia laki mbili sitini elfu
mia nne sabini na nne (260,474) mwaka 2020.
“Katika kipindi hiki tumeongeza idadi ya Mabwawa kutoka 220,545
hadi kufikia 260,445 na kuongeza vizimba vya samaki kutoka 109 hadi 431, na
uzalishaji wa Vifaranga vya Samaki vimeongezeka kutoka milioni nane na tisini
elfu (8,090,000) hadi Vifaranga milioni kumi na nne laki tano thelathini na
moja elfu mia nne themanini na saba (14,531,487)”, aliongeza Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa sambamba na mafanikio hayo
serikali imeongezea mtaji kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kiasi cha
Shilingi Bilioni Mia Mbili na nane kupitia Mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya
Afrika. Pia serikali imeipatia TADB Dola za Kimarekani Milioni 25 sawa na
Shilingi Bilioni 57.8 ili kuendesha Mfuko wa dhamana.
“Hii ina maana kuwa kwa miaka mitano iliyopita Serikali imeipa
TADB Shilingi Bilioni 324.8 kuiwezesha Benki hiyo kutoa mikopo ya moja kwa moja
kwa wakulima, wafugaji na wavuvi yenye thamani ya kiasi cha shilingi bilioni
166.9 kwa Riba nafuu”, aliongeza Rais Magufuli
Kutokana na hatua hizo, Rais Magufuli alisema kuwa mafanikio
makubwa yamepatikana ambapo Sangara kwenye ziwa Victoria wameongezeka kutoka
tani 417,936 mwaka 2016 hadi kufikia tani 816,964 mwaka 2020.
“Kufuatia hatua hizo, urefu wa Sangara umeongezeka kutoka
wastani wa sentimeta 16 hadi kufikia sentimeta 25.2 jambo ambalo limefanya
samaki wetu kuanza kuhitajika kwa kiasi kikubwa katika soko la Ulaya na nyinyi
ni mashahidi Waheshimiwa Wabunge ndege zimeanza kuja Mwanza na kubeba Samaki
wetu kwa ajili ya kupeleka nje ya nchi”, alisisitiza Rais Magufuli.
“Kwa kuzingatia hilo mauzo ya samaki nje ya nchi
yameongezeka kutoka wastani wa shilingi bilioni 379 mwaka 2015 hadi bilioni 692
mwaka 2019”, alieleza Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli alisisitiza kuwa mafanikio hayo sio mambo
madogo ni hatua muhimu katika kukuza uchumi wa nchi ambao kwa sasa upo katika
hatua nzuri ya kufikia uchumi wa kati ifikipo mwaka 2025.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Magufuli Akizungumza
wakati akitoa hotuba yake ya kulifunga Bunge la kumi na moja (11) la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Juni 16, 2020 jijini Dodoma.
|
MHE. MPINA ATEUWA WAJUMBE WA BARAZA LA VETERINARI TANZANIA.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina (mb) kwa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 4(1) cha sheria ya veterinari Na.16 ya mwaka 2003 amewateuwa wajumbe wa Baraza la Veterinari Tanzania. kwa kuona majina ya wajumbe waliochaguliwa, bofya hapa
Jumatatu, 22 Juni 2020
UHUISHAJI WA MAJINA YA MADAKTARI KWENYE DAFTARI LA USAJILI.
Madaktari wafuatao wanatakiwa kuhuisha majina yao kwenye daftari la usajili wa madaktari wa mifugo kabla ya tarehe 25/06/2020. kupata orodha ya madaktari ambao hawajahuisha majina yao, bofya hapa
Ijumaa, 19 Juni 2020
WADAU WA TASNIA YA NDEGE WAFUGWAO WAIPONGEZA SERIKALI KWA KUTATUA KERO ZAO.
Wadau wa tasnia ndogo ya ndege wanaofugwa wameipongeza Serikali kwa
kutatua kero za kisera ambazo zilikuwa zikidumaza tasnia hiyo.
Hayo yamesemwa na Katibu wa chama Kikuu cha Wadau wa Tasnia ya
Kuku (PAT), Manase Mrindwa katika kikao cha Wadau wa tasnia ya kuku kilichofanyika
jijini Dodoma Juni 18,2020.
Akiongea kwenye kikao hicho Mrindwa alisema kuwa bajeti
ya Serikali ya mwaka 2020/2021 imetoa majibu kwa kero zao kwa
kuondoa kodi kwenye mayai ya kutotolesha vifaranga yanayotoka nje ya nchi, imepunguza
tozo kwenye vyakula vya mifugo vinavyosafirishwa nje ya nchi na kupunguza
tozo kwenye mayai yanayosafirishwa nje ya nchi.
“Unafuu huu wa tozo tunategemea utaiinua tasnia hii ya ndege
wanaofugwa hapa Tanzania, alisema Mrindwa.
Pamoja na pongezi hizo Mrindwa alieleza changamoto zilizowakumba
kufuatia mlipuko wa maradhi ya Korona ambazo zimechangia kupungua kwa
ulaji wa bidhaa za kuku kutokana na mdororo wa biashara uliopelekea kufungwa
kwa baadhi ya shughuli za biashara ikiwemo mahoteli, migahawa, vyuo, shule na
kusitishwa kwa shughuli zinazoleta mikusanyiko ya watu.
"Kudumaa kwa biashara zinazohitaji mazao ya kuku, kupungua
kufuga kuliathiri viwanda vinavyozalisha vyakula vya mifugo, uingizaji wa
bidhaa za kuku kutoka nje zilisitishwa, wafugaji waliokopa kwenye taasisi
mbalimbali za kifedha walipata shida katika marejesho." Aliongeza Mrindwa
Aidha, Mrindwa alisema kuwa kufuatia kupungua kwa
changamoto ya mlipuko wa maradhi ya Korona shughuli za kibiashara
zimeanza kurejea katika hali yake jambo ambalo litasaidia kuimarisha biashara
hiyo huku akitaja shughuli ambazo zimeshaanza kurejea kama vile usafiri wa
anga, utalii, uzalishaji katika viwanda, mashamba ya kuku wazazi ambayo
yameanza kupokea vifaranga vya kuku na kuanza kuingia nchini virutubisho vya
kutengenezea vyakula vya mifugo.
Aliongeza kuwa kwa sasa wafugaji wameanza kuongeza
na kuimarisha shughuli zao za ufugaji hivyo kupelekea kuwa na changamoto
ya ongezeko la mahitaji ya vifaranga wa nyama na wa mayai.
"Serikali iendelee kujadiliana na nchi jirani hususani
Kenya na Zambia ili shughuli za mipakani ziweze kufanyika kama awali na
usumbufu wa madereva na ucheleweshwaji wa mizigo uishe ili kurahisisha
upatikanaji wa bidhaa za mifugo ili biashara iweze kuimarika zaidi, alisisitiza
Mrindwa.
Katika hatua nyingine, Wadau hao wamekiri kujifunza namna ya
kuweka mkakati wa kuimairisha ulaji wa nyama ya kuku na mayai hapa
nchini, kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vya kutengeneza dawa za kuku na
uwekezaji katika maghala na kuiomba serikali kuendelea na mchakato wa kuzalisha
soya ya kutosha kwa mahitaji ya vyakula vya mifugo.
"Hivi sasa kwa wastani Mtanzania mmoja anakula mayai 75 kwa
mwaka wakati kiwango cha FAO ni kula mayai 200 kwa mwaka, pia Mtanzania anakula
kilo 15 za nyama kwa mwaka wakati FAO inapendekeza kula kilo 45 kwa
mwaka." Alifafanua Mrindwa.
Wadau wa tasnia ndogo ya ndege wanaofugwa wameipongeza Serikali kwa
kutatua kero za kisera ambazo zilikuwa zikidumaza tasnia hiyo.
Hayo yamesemwa na Katibu wa chama Kikuu cha Wadau wa Tasnia ya
Kuku (PAT), Manase Mrindwa katika kikao cha Wadau wa tasnia ya kuku kilichofanyika
jijini Dodoma Juni 18,2020.
Akiongea kwenye kikao hicho Mrindwa alisema kuwa bajeti
ya Serikali ya mwaka 2020/2021 imetoa majibu kwa kero zao kwa
kuondoa kodi kwenye mayai ya kutotolesha vifaranga yanayotoka nje ya nchi, imepunguza
tozo kwenye vyakula vya mifugo vinavyosafirishwa nje ya nchi na kupunguza
tozo kwenye mayai yanayosafirishwa nje ya nchi.
“Unafuu huu wa tozo tunategemea utaiinua tasnia hii ya ndege
wanaofugwa hapa Tanzania, alisema Mrindwa.
Pamoja na pongezi hizo Mrindwa alieleza changamoto zilizowakumba
kufuatia mlipuko wa maradhi ya Korona ambazo zimechangia kupungua kwa
ulaji wa bidhaa za kuku kutokana na mdororo wa biashara uliopelekea kufungwa
kwa baadhi ya shughuli za biashara ikiwemo mahoteli, migahawa, vyuo, shule na
kusitishwa kwa shughuli zinazoleta mikusanyiko ya watu.
"Kudumaa kwa biashara zinazohitaji mazao ya kuku, kupungua
kufuga kuliathiri viwanda vinavyozalisha vyakula vya mifugo, uingizaji wa
bidhaa za kuku kutoka nje zilisitishwa, wafugaji waliokopa kwenye taasisi
mbalimbali za kifedha walipata shida katika marejesho." Aliongeza Mrindwa
Aidha, Mrindwa alisema kuwa kufuatia kupungua kwa
changamoto ya mlipuko wa maradhi ya Korona shughuli za kibiashara
zimeanza kurejea katika hali yake jambo ambalo litasaidia kuimarisha biashara
hiyo huku akitaja shughuli ambazo zimeshaanza kurejea kama vile usafiri wa
anga, utalii, uzalishaji katika viwanda, mashamba ya kuku wazazi ambayo
yameanza kupokea vifaranga vya kuku na kuanza kuingia nchini virutubisho vya
kutengenezea vyakula vya mifugo.
Aliongeza kuwa kwa sasa wafugaji wameanza kuongeza
na kuimarisha shughuli zao za ufugaji hivyo kupelekea kuwa na changamoto
ya ongezeko la mahitaji ya vifaranga wa nyama na wa mayai.
"Serikali iendelee kujadiliana na nchi jirani hususani
Kenya na Zambia ili shughuli za mipakani ziweze kufanyika kama awali na
usumbufu wa madereva na ucheleweshwaji wa mizigo uishe ili kurahisisha
upatikanaji wa bidhaa za mifugo ili biashara iweze kuimarika zaidi, alisisitiza
Mrindwa.
Katika hatua nyingine, Wadau hao wamekiri kujifunza namna ya
kuweka mkakati wa kuimairisha ulaji wa nyama ya kuku na mayai hapa
nchini, kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vya kutengeneza dawa za kuku na
uwekezaji katika maghala na kuiomba serikali kuendelea na mchakato wa kuzalisha
soya ya kutosha kwa mahitaji ya vyakula vya mifugo.
"Hivi sasa kwa wastani Mtanzania mmoja anakula mayai 75 kwa
mwaka wakati kiwango cha FAO ni kula mayai 200 kwa mwaka, pia Mtanzania anakula
kilo 15 za nyama kwa mwaka wakati FAO inapendekeza kula kilo 45 kwa
mwaka." Alifafanua Mrindwa.
WATUMISHI WA SEKTA YA UVUVI WAASWA KUWA NA UADILIFU KATIKA UTUMISHI WA UMMA.
Watumishi wa sekta ya Uvuvi wameaswa
kuwa na uadilifu katika utumishi wa Umma hasa katika kuzingatia sheria,Kanuni
na Taratibu za Nchi.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Uvuvi,
Dkt. Rashid Tamatamah alipokua akifungua kikao cha Mafunzo ya maadili ya
Utumishi wa Umma, yaliyofanyika katika ukumbi wa St. Gasper leo tarehe
18/06/2020.
Dkt. Tamatamah amewasisitiza
watumishi kuwa wazalendo katika kazi na kufuata maelekezo yote ya utumishi wa
umma na sheria za Nchi.
Lengo la mafunzo hayo ni
kuwakumbusha watumishi kutambua majukumu yao ya kiutumishi pamoja na maadili ya
utumishi wa umma.
"Mtumishi anapaswa kujua
misingi yake ya kazi katika utumishi na kuepuka kuchukua na kupokea rushwa
katika kuwaudumia wananchi," alisema Dkt. Tamatamah.
Naye Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma
Bwana kutoka TAKUKURU, Joseph Kasongwa Mwaiselo amewaeleza watumishi madhara ya
rushwa kwa serikali, na kwamba baadhi ya watumishi wamekuwa wakikumbatia rushwa
na kudhani kuwa itawaongezea kipato.
Mwaiselo amesema madhara ya rushwa
serikalini ni pamoja na kupunguza ukuaji wa uchumi kwa sababu ina haribu
uwekezaji katika uchumi na pia rushwa inapunguza uwezo wa serikali kugharamia
huduma za kijamii ikiwamo Afya na Elimu.
Aidha, akinukuu maneno ya Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa alipo
wasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya
Mapato na Matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 2016/2017, Mwaiselo
amesema "Hatutaweza kufikia uchumi wa kati unaoendeshwa kwa viwanda kama
tutaendelea kulea uzembe, uvivu, na kukwepa wajibu wetu".
Watumishi wametakiwa kuacha rushwa
kwani rushwa ni adui wa haki na watumushi wanapaswa kupendana na kuacha majungu
ambayo yanasababisha kukosekana kwa haki.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali
Watu, Alex Mfundo amewasihi watumishi kuhakikisha wanafuata maadili ya utumishi
wa umma na amewapongeza watumishi kwa kuitikia wito katika mafunzo hayo.
Katika mafunzo hayo, watumishi
wameelekezwa juu ya masuala ya maadili ya utumishi wa umma pamoja na mwongozo
kuhusu ushiriki wa watumishi wa umma katika uchaguzi mkuu mwezi Oktoba, 2020.
Katibu Mkuu wa wizara
ya Mifugo na Uvuvi, sekta ya uvuvi (aliyekaa katikati) Dkt Rashid Tamatamah
akipata picha ya pamoja na watumishi wa sekta ya uvuvi mara baada ya kufungua
kikao cha mafunzo ya maadili ya utumishi wa umma, Nje ya ukumbi wa St. Gasper mjini
Dodoma leo tarehe 18/06/2020.
Mkurugenzi wa Elimu
kwa Umma Bwana Joseph Kasongwa Mwaiselo kutoka ofisi ya Takukuru, akitoa
mafunzo kwa watumishi wa sekta ya uvuvi na kuonyesha Madhara ya rushwa kwa
serikali, katika kikao cha mafunzo ya maadili ya utumishi wa Umma
kilichofanyika katika ukumbi wa St. Gasper mjini Dodoma leo tarehe
18/06/2020.
Ijumaa, 5 Juni 2020
BARAZA LA VETERINARI LAONYA MADAKTARI ‘FEKI’ KUHUDUMIA MIFUGO
Baraza
la Veterinari nchini Tanzania limewataka watu wote ambao hawana sifa za
Udaktari wa Mifugo kuacha mara moja kuhudumia na kutibu Mifugo huku likionya
kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa watakao kwenda kinyume na Sheria.
Onyo
hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Veterinari, Profesa Rudovick Kazwala
katika Mkutano wa 45 wa Baraza hilo ulilofanyika jijini Dodoma Mei 4, 2020.
Akiongea
na Vyombo vya Habari mara baada ya Mkutano huo, Profesa Kazwala alisema kuwa
kutokana na fani hiyo ya Udaktari wa Mifugo kuingiliwa na watu wasiokuwa na
sifa Baraza limeamua kuandaa vitambulisho na beji vitakavyowatambulisha
Madaktari hao pindi wanapokwenda kutoa huduma kwa wafugaji.
“Wale
wote wanaojiingiza katika fani hii bila kuwa na vyeti vya kitaaluma wajue kuwa
kuna sheria namba 16 ya Veterinari ya mwaka 2003 ambayo inakataza mtu ambaye
hajasomea taaluma ya Udaktari wa mifugo kufanya kazi ya kuhudumia na kutibu
mifugo, atakayekutwa na kosa hilo sheria itachukua mkondo wake” alisema Profesa Kazwala
Alisisitiza
kuwa kuanzia sasa wafugaji wanapaswa kujua kuwa wataalamu wa mifugo watakuwa na
vitambulisho vitakavyokuwa vinatolewa na Baraza hilo na kuwataka kuwakataa watu
watakaokuwa wanakwenda kutaka kutibu mifugo yao bila kitambulisho.
“Huko
nyuma hatukuwa na vitambulisho, kukosekana kwa vitambulisho kulipelekea watu
wasio na sifa kujiingiza katika kazi ya tiba ya mifugo na kuchafua sifa za fani
yetu”,alisema Profesa alifafanua
Kufuatia
changamoto hiyo, Profesa Kazwala alisema mkutano huo umekubaliana na kupitisha
maamuzi kuwa wataalamu wa mifugo wawe na vitambulisho ambavyo vitasaidia kuzuia na kuwaondoa watu wasio na sifa ya
udaktari wa mifugo.
Aliongeza
kuwa watahakikisha wakaguzi wa mifugo wanapita kila mara kwa wafugaji kukagua
mifugo yao na kufuatilia kama kuna watu kama hao ambao wanaendelea kuvunja
sheria.
Profesa
Kazwala ametoa wito kwa wafugaji na wananchi kwa ujumla kushirikiana na Baraza
hilo kuwakataa watu hao wasio na vitambulisho huku akiwasisitiza hata hao
madaktari watakaokuwa na vitambulisho wanapokwenda kutibu mifugo yao kuweka
kumbukumbu zao vizuri ikiwemo namba ya usajili ya mtaalamu huyo ili kama
likitokea tatizo lolote litakalo sababishwa na mtaalamu huyo iwe rahisi
kumtambua.
Aidha,
Profesa Kazwala amewaeleza wananchi kuwa huduma za mifugo zinaendelea
kuboreshwa nchini na kuanzia sasa vituo vyote vinavyotoa matibabu ya wanyama
lazima viwe na vifaa vya kuchunguza mifugo kwa
maana ya Darubini ili kutoa vipimo sahihi vya Sampuli zitakazokuwa
zinachukuliwa kutoka kwa mifugo.
Mwenyekiti
wa Baraza la Veterinari Tanzania, Prof. Rudovick Kazwala akiongea na waandishi
wa habari muda mfupi baada ya kumaliza mkutano wa 45 wa Baraza la Veterinari
Tanzania uliofanyika jijini Dodoma. (04/06/2020)
Mkurugenzi
wa Huduma za Mifugo, Prof. Hezron Nonga akifafanua jambo mbele ya vyombo vya
habari katika mkutano wa 45 wa Baraza la Veterinari Tanzania uliofanyika jijini
Dodoma. (04/06/2020)
Mwenyekiti wa Baraza la Veterinari, Profesa Rudovick Kazwala (aliyekaa katikati) akiwa kwenye picha Picha ya pamoja na wajumbe wa baraza hilo mara baada ya kumaliza Mkutano wa 45 wa Baraza la Veterinari uliofanyika jijini Dodoma Mei 4, 2020 |
Jumatano, 3 Juni 2020
NAIBU WAZIRI ULEGA AAGIZA KUKAMILIKA KANUNI, KUSIMAMIA SHERIA YA UVUVI WA BAHARI KUU
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Abdallah Ulega, amewataka watendaji wa Mamlaka ya
Usimamizi wa Uvuvi wa Bahari Kuu kufanya maandalizi ya kupata kanuni bora za
kusimamia Sheria ya Uvuvi wa Bahari Kuu iliyopitishwa hivi karibuni na Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza na watendaji wa mamlaka hiyo Mjini Unguja Visiwani
Zanzibar akifuatana na Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili na Mifugo, Dkt. Makame
Ali Ussi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Ulega aliwataka watendaji hao
kuunda kanuni bora zitakazoenda sambamba na mfumo wa biashara kwa kuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli anataka kuona namna ukanda
wa bahari unavyosaidia kuinua uchumi wa taifa.
“Jumla ya vipengele vyote vya sheria takriban 104 tumevifanyia
kazi na vipengele kama 23 ambavyo havijaguswa lakini vingine vyote vimeguswa
kuendana na uchumi wa bahari ili kuwa na mchango kwa mtu mmoja mmoja na taifa
kwa ujumla katika kufanya maboresho ya uvuvi na bahari kuu, rai yangu kwa
mamlaka mmefanya kazi nzuri kwa utengenezaji wa sheria lazima kwenda mbio sasa
ndani ya miezi miwili tuwe tumepata kanuni zitakazoenda sambamba na biashara ya
leo bila kuathiri maslahi mapana ya taifa letu.” Alisema Ulega
Aliongeza kuwa matumizi ya sheria hiyo yatakayoenda sambamba na
kanuni bora za utekelezaji wake zitakuwa chachu ya kuvutia uwekezaji kwa raia
kutoka nje ya nchi kuja na meli zao hapa nchini na kufanya shughuli za uvuvi na
wengine kuwekeza katika viwanda vya uchakataji wa samaki kwa kuwa Ukanda wa
Pwani ya Bahari Hindi bado hakuna uwekezaji wa kutosha wa viwanda hivyo.
Aidha, aliipongeza serikali ya awamu ya tano inayoongozwa
na Rais Dkt. John Magufuli ilivyoboresha mazingira kwenye maziwa na mito hali
iliyopelekea ndege za mizigo kubeba minofu ya samaki kutoka katika uwanja wa
ndege wa Mwanza na kusafirisha kwenda nje ya nchi.
Pia, Naibu Waziri Ulega alifafanua kuwa wakati watendaji
wa Mamlaka ya Usimamizi wa Uvuvi wa Bahari Kuu wanaandaa kanuni za kusimamia
sheria hiyo watambue kuwa ushirikiano ni muhimu katika utekezaji huo na
kutokuwa na mvutano wowote kwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Magufuli na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Ali Mohamed
Shein wanataka kuona mapinduzi makubwa katika sekta ya uvuvi.
“Lazima mfanye kazi pamoja mshirikiane msiwe na aina
yoyote ya mvutano, lazima mfanye kazi nzuri ya kushirikiana lazima taifa letu
linufaike, Tanzania kwanza, tunaenda kufungua uvuvi wa bahari kuu tunaenda
kufungua uchumi wa bluu tunataka uvuvi utoke kuchangia Asilimia 1.9 katika pato
la taifa kusiwe na jambo la kunyoosheana vidole.” Alifafanua Ulega
Ulega akizungumza katika kikao hicho alisema ni muda muafaka kwa
wavuvi hapa nchini kuondakana na uvuvi wa kuwinda bali uendane na teknolojia ya
kisasa kufahamu maeneo mahsusi kwa ajili ya uvuvi ili kupunguza gharama kwa
kutengwa vituo maalum vya kutolea taarifa ya maeneo yenye samaki na umbali wa
kufikia maeneo hayo.
Alibainisha kuwa ni lazima uwepo mfumo wa kitaaalamu kwenye
vyombo vyao vya uvuvi ili mvuvi anapotoka pwani kwenda baharini kuvua awe na
uhakika wa mahali anapokwenda kuvua samaki na kuwataka watendaji hao kulifanyia
kazi suala hilo haraka ili kufikia malengo ya wavuvi kunufaika zaidi kupitia
sekta hiyo.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Abdallah Ulega, akiwa katika ziara
maalum visiwani Zanzibar alitembelea kituo cha utotoaji wa vifaranga vya
samaki, majongoo na kaa eneo la Maruhubi Mjini Unguja, ambapo alisema ipo
miradi midogomidogo itakayoweza kutumika ikiwemo ya uvuvi wa samaki, majongoo
na kaa ambayo ina soko kubwa duniani.
Ulega alisema uzalishaji wa bahari ndio nguzo kuu ya kukuza
uchumi kwa wakaazi wa Ukanda wa Pwani wa Bahari ya Tanzania baada ya kufanikiwa
katika ukuzaji viumbe maji kwenye maji baridi hivyo mapinduzi makubwa
yanaelekezwa katika ukuzaji viumbe maji kwenye bahari.
“Serikali imeamua kwa dhati bahari yetu iweze kutunufaisha
na kuwa na mchango chanya wakati wa kuhamia katika uvuvi wa bahari kuu na jamii
iweze kufuga na kukuza kipato katika viumbe ambavyo vinauzika na kuhitajika
duniani kama kaa na majongoo bahari ambao wanahitajika katika mataifa ya nje ya
nchi yetu na wamekuwa wakiuzwa kwa bei kubwa.”
Ulega alisema, juhudi hizo zinaendana na mikakati ya serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa
kufanya mapinduzi katika sekta ya kilimo itakayoinua jamii ya Ukanda wa Pwani
kupitia miradi hiyo midogo.
"Tunafanya haya yote kwa ajili tunapata vyanzo vingi vya
mapato vitakavyosaidia uchumi wa nchi pamoja na wananchi ambayo itatusaidia
Tanzania kukuza maendeleo yake kwa haraka, kama ni utalii tunapongeza viongozi
wetu wakuu kwa kusimamia haya na elimu hii iende mbali zaidi uzalishaji viumbe
maji kwenye bahari unaweza kusababisha kuinuka kama taifa na kufanya vizuri
zaidi kiuchumi na kuinua pato la taifa.”
Aliongeza kuwa licha ya kuelekea mpango wa uvuvi katika bahari
kuu tayari miradi kama hiyo imeleta mageuzi makubwa katika maji baridi kwa
maana ya maeneo ya maziwa na mito kwa upande wa Tanzania Bara.
Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili na Mifugo, Dkt. Makame
Ali Ussi, alisema, Zanzibar inaendelea na mpango wa uchumi wa bahari, kwa kuwa
una nafasi kubwa ya kuingiza mapato ya haraka pamoja na kuwanufaisha wananchi
wengi.
“Tunaelekea kwenye uchumi wa bluu unaohitaji kutunza mazingira
ya bahari, ninawashauri watanzania sehemu zote za pwani watunze maeneo ya
bahari kwa kutunza maeneo ya mazalia ya samaki yakiwemo matumbawe.” Alisema
Ussi
Pamoja na hayo, alisema kuwa miradi hiyo ya uzalishaji wa samaki
imekuwa na nafasi kubwa katika kukuza mazingira ya bahari ambayo tayari sehemu
kubwa ya maeneo yanayotegemewa kwa uvuvi yameshaathirika.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Abdallah Ulega, amefanya ziara ya kikazi ya siku moja
visiwani Zanzibar ikiwa ni moja ya mikakati ya serikali kuhakikisha sekta ya
uvuvi inazidi kunufaisha zaidi taifa na mvuvi mmoja mmoja na kuongeza
ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Visiwani pamoja na kubadilishana uzoefu
katika sekta hiyo.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega (kushoto) akiwa ameshika
jongoo bahari alipotembelea kituo cha utotoleshaji vifaranga vya samaki, majongoo
bahari na kaa mjini Unguja, wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja Visiwani
Zanzibar. Aliyevaa tai nyekundu ni Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili na Uvuvi wa SMZ Dkt. Makame Ali Ussi. (02.06.2020) |
Naibu Waziri wa Mifugo
na Uvuvi Abdallah Ulega (wa kwanza kulia) akishuhudia kaa, alipotembelea kituo
cha utotoleshaji vifaranga vya samaki, majongoo bahari na kaa mjini Unguja,
wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja Visiwani Zanzibar.
Akiambatana na
Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili na Uvuvi wa SMZ Dkt. Makame Ali Ussi
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega (aliyevaa
koti jeusi) akipata maelezo ya ufuatiliaji wa meli zinazoingia katika maji ya
Tanzania kwenye Bahari ya Hindi mara baada ya kutembelea ofisi za Mamlaka
ya Usimamizi wa Uvuvi wa Bahari Kuu visiwani Zanzibar. (02.06.2020)
Naibu Waziri wa Mifugo
na Uvuvi Abdallah Ulega (aliyesimama) akizungumza na watendaji wa Mamlaka ya
Usimamizi wa Uvuvi wa Bahari Kuu (hawapo pichani) katika ofisi za mamlaka hiyo
Visiwani Zanzibar, aliyekaa kulia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili na Uvuvi
wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Makame Ali Ussi. (02.06.2020)
Jisajili kwenye:
Machapisho (Atom)