Watumishi wa sekta ya Uvuvi wameaswa
kuwa na uadilifu katika utumishi wa Umma hasa katika kuzingatia sheria,Kanuni
na Taratibu za Nchi.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Uvuvi,
Dkt. Rashid Tamatamah alipokua akifungua kikao cha Mafunzo ya maadili ya
Utumishi wa Umma, yaliyofanyika katika ukumbi wa St. Gasper leo tarehe
18/06/2020.
Dkt. Tamatamah amewasisitiza
watumishi kuwa wazalendo katika kazi na kufuata maelekezo yote ya utumishi wa
umma na sheria za Nchi.
Lengo la mafunzo hayo ni
kuwakumbusha watumishi kutambua majukumu yao ya kiutumishi pamoja na maadili ya
utumishi wa umma.
"Mtumishi anapaswa kujua
misingi yake ya kazi katika utumishi na kuepuka kuchukua na kupokea rushwa
katika kuwaudumia wananchi," alisema Dkt. Tamatamah.
Naye Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma
Bwana kutoka TAKUKURU, Joseph Kasongwa Mwaiselo amewaeleza watumishi madhara ya
rushwa kwa serikali, na kwamba baadhi ya watumishi wamekuwa wakikumbatia rushwa
na kudhani kuwa itawaongezea kipato.
Mwaiselo amesema madhara ya rushwa
serikalini ni pamoja na kupunguza ukuaji wa uchumi kwa sababu ina haribu
uwekezaji katika uchumi na pia rushwa inapunguza uwezo wa serikali kugharamia
huduma za kijamii ikiwamo Afya na Elimu.
Aidha, akinukuu maneno ya Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa alipo
wasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya
Mapato na Matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 2016/2017, Mwaiselo
amesema "Hatutaweza kufikia uchumi wa kati unaoendeshwa kwa viwanda kama
tutaendelea kulea uzembe, uvivu, na kukwepa wajibu wetu".
Watumishi wametakiwa kuacha rushwa
kwani rushwa ni adui wa haki na watumushi wanapaswa kupendana na kuacha majungu
ambayo yanasababisha kukosekana kwa haki.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali
Watu, Alex Mfundo amewasihi watumishi kuhakikisha wanafuata maadili ya utumishi
wa umma na amewapongeza watumishi kwa kuitikia wito katika mafunzo hayo.
Katika mafunzo hayo, watumishi
wameelekezwa juu ya masuala ya maadili ya utumishi wa umma pamoja na mwongozo
kuhusu ushiriki wa watumishi wa umma katika uchaguzi mkuu mwezi Oktoba, 2020.
Katibu Mkuu wa wizara
ya Mifugo na Uvuvi, sekta ya uvuvi (aliyekaa katikati) Dkt Rashid Tamatamah
akipata picha ya pamoja na watumishi wa sekta ya uvuvi mara baada ya kufungua
kikao cha mafunzo ya maadili ya utumishi wa umma, Nje ya ukumbi wa St. Gasper mjini
Dodoma leo tarehe 18/06/2020.
Mkurugenzi wa Elimu
kwa Umma Bwana Joseph Kasongwa Mwaiselo kutoka ofisi ya Takukuru, akitoa
mafunzo kwa watumishi wa sekta ya uvuvi na kuonyesha Madhara ya rushwa kwa
serikali, katika kikao cha mafunzo ya maadili ya utumishi wa Umma
kilichofanyika katika ukumbi wa St. Gasper mjini Dodoma leo tarehe
18/06/2020.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni