Nav bar

Jumatano, 30 Julai 2025

BI. MEENA AWATAKA WAFUGAJI NA WAFANYABIASHARA WA MIFUGO KUPELEKA MIFUGO KARANTINI KABLA YA KUUZA NJE YA NCHI

Na. Stanley Brayton, WMUV

Kibaha, Pwani 

Julai 30, 2025

⬛  Ataka Kituo cha Karantini ya Mifugo Kwala na Kampuni ya NARCO kuweka alama kwenye mipaka ya maeneo yao.

⬛ Ataka Dawati la Ndege Wafugwao kuanzisha Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) ya Kuku

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena amewataka Wafugaji na Wafanyabiashara za Mifugo kupeleka Mifugo yao kwenye kituo cha Karantini ya Mifugo ili kufanyiwa Uchunguzi wa Magonjwa kabla ya kuuza Mifugo hiyo nchi za nje, ikiwa ni njia moja wapo ya kukuza Biashara hiyo Kimataifa.

Akizungumza wakati alipotembelea Kituo cha Karantini ya Mifugo Kwala, Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Shamba la Kuku la Kampuni ya Tanzania Sunshine na Kampuni ya Mkuza Chicks, leo Julai 30, 2025 Mkoani Pwani, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena amesema uwepo wa Kituo cha Karantini ya Mifugo ni fursa ya kimkakati katika kuyafikia masoko ya mifugo na mazao yake ya ndani na nje ya nchi.

“Kituo hiki ni muhimu sana, na kimekaa Kimkakati, hivyo kinatakiwa kifanye kazi ipasavyo ili wafugaji waone umuhimu wake na kuweza kunufaika nacho Kibiashara, kwani kinasaidia kuwahakikishia usalama wa mifugo na mazao yake hasa katika Masoko ya nje ya nchi.” amesema Bi. Meena

Aidha, Bi. Meena ameitaka Idara ya Huduma za Mifugo kuweka utaratibu wa kila Mfugaji au Mfanyabiashara ya Mifugo kupitisha Mifugo yao katika karantini kabla ya kwenda kuuza nje ya nchi, na ameielekeza idara kuangalia namna bora ya  kuboresha Miundombinu ya Kituo hicho ili kiweze kutoa huduma Bora zaidi.

Vilevile, Bi. Meena amesisitiza kuwa Karantini ina maslahi mapana Kitaifa na hivyo wananchi kuvamia na kufanya shughuli zao katika eneo hilo inasababisha karantini hiyo kupoteza sifa yake kimataifa. 

Pia, amekitaka Kituo cha Karantini ya Mifugo Kwala na Kampuni ya NARCO kuhakikisha inapima na kuweka alama kwenye mipaka ili kuepusha uvamizi katika maeneo yao.

Katibu Mkuu amelitaka Dawati la Ndege wafugwao kuanzisha Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) ya Kuku na kuwapa vijana elimu juu ya Ufugaji bora wa kuku ili waweze kupata ajira, kujikwamua kiuchumi na kuongeza tija na Pato la Taifa kiujumla.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena (wa kwanza kushoto), akizungumza na Watendaji wa Wizara hiyo, juu ya Uboreshaji wa Miundombinu ya Kituo cha Karantini ya Mifugo Kwala, mara baada ya kutembelea na kufanya kikao kifupi na Watendaji wa Kituo hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Julai 30, 2025 Pwani.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena (wa kwanza kushoto), akizungumza na Watendaji wa Wizara hiyo, mara ya baada ya kusikiliza changamoto na Kero za Kituo cha Karantini ya Mifugo Kwala, wakati alipotembelea na kufanya kikao kifupi na Watendaji wa Kituo hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Julai 30, 2025 Pwani.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena (wa pili kushoto), akisalimiana na Watendaji wa Wizara hiyo, mara baada ya kutembelea Kituo cha Karantini ya Mifugo Kwala kabla ya kufanya kikao kifupi na Watendaji wa Kituo hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Julai 30, 2025 Pwani.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena (wa pili kushoto), akizungumza na Watendaji wa Wizara hiyo, mara baada ya kutembelea Shamba la kuku la Kampuni ya Tanzania Sunshine kabla ya kufanya nao kikao kifupi na Watendaji wa Kampuni hiyo iliyopo Wilayani Kibaha, Julai 30, 2025 Pwani.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena (wa sita kushoto), akimsikiliza Mtendaji wa Kampuni ya Mkuza Chicks akielezea Mchakato mzima wanaoufanya katika kuzalisha nyama ya Kuku, mara baada ya kutembelea Shamba la kuku la Kampuni ya hiyo kabla ya kufanya nao kikao kifupi na Watendaji wa Kampuni hiyo iliyopo Wilayani Kibaha, Julai 30, 2025 Pwani.


Alhamisi, 24 Julai 2025

DKT. MHEDE: TAASISI ZA FEDHA ZITOE MIKOPO YENYE RIBA NAFUU KWA WAFUGAJI

Na. Martha Mbena,  Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa rai na ushauri kwa taasisi za fedha nchini, hasa benki, kutoa masuluhisho ya kifedha na mikopo yenye riba himilifu kwa wafugaji na wadau wa mnyororo wa thamani wa sekta ya mifugo ili waweze kufanya biashara shindani ya mifugo na mazao yake na kuinua uchumi wao na Taifa kwa ujumla.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede, leo Julai 23, 2025 katika Hoteli ya Gerwill Jijini Dodoma wakati akifungua Kongamano la kujadili fursa za sekta ya Mifugo na ngozi ulioandaliwa na Serikali kwa kushirikiana na benki ya Equity Tanzania Ltd.

"Watu wetu watakapokuja kukopa nawaomba sana tuzingatie kutokwenda zaidi ya ukomo wa riba uliowekwa na mdhibiti wa sekta ya fedha (Benki Kuu ya Tanzania). Tufanye kama vile ambavyo kiongozi wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alivyothubutu kuweka fedha ya umma kwenye afua mbalimbali ili kuwasaidia wafugaji wetu", amesema Dkt. Mhede.

Pia, ameipongeza Benki ya Equity Tanzania Ltd kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuandaa kongamano hilo muhimu, na kuonesha utayari wa kushirikiana na Serikali katika kuwezesha mitaji, kuboresha biashara za wafugaji, kutoa mafunzo, pamoja na kuimarisha minyororo ya thamani katika sekta ya Mifugo na mazao yake, hususani sekta ya ngozi na bidhaa za ngozi.

“Kongamano hili ni fursa ya kipekee ya kufanya tathmini ya kina kuhusu hali ya sekta ya Mifugo. Kupitia jukwaa hili, tunaweza kuona fursa zilizopo na changamoto zinazoikabili sekta, ili kwa pamoja tuweze kuchukua hatua sahihi za kimaendeleo katika safari yetu ya Mpango Kabambe wa Mageuzi ya Sekta ya Mifugo ili kuinua uchumi wa wafugaji na wadau wote wa sekta ya mifugo na ngozi,” ameeleza 

Aidha, amesisitiza kuwa sekta ya Mifugo ni uti wa mgongo kwa mamilioni ya Watanzania, hivyo ushirikiano wa karibu na taasisi kama Benki ya  Equity Tanzania Ltd ni msingi imara wa mageuzi chanya katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Vile vile, Dkt. Mhede, ametoa wito kwa wadau wengine kutoka sekta mbalimbali kuiga mfano wa Benki ya Equity Tanzania Ltd kwa kuwekeza katika sekta ya Mifugo, kwa kuwa ina fursa nyingi ambazo hazijatumika kikamilifu, hasa kwenye maeneo ya uzalishaji wa ngozi bora, usindikaji wa mazao ya mifugo, na upatikanaji wa masoko ya uhakika na yenye thamani stahiki.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Equity Tanzania Ltd, Dkt.Florens Turuka, amesema kuwa benki hiyo imeona fursa nyingi katika sekta ya Ngozi, hali iliyowasukuma kuwekeza moja kwa moja katika sekta hiyo ili kusaidia wafugaji kufikia maendeleo.

“Fursa zilizopo kwenye sekta ndogo ya ngozi ni nyingi, hivyo wafugaji wanapaswa kujitokeza kushirikiana nasi ili waendelee kukuza biashara yao,” amesema Dkt. Turuka.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity Tanzania Ltd, Bi. Isabela Maganga, amesema kuwa benki hiyo imejipanga kushirikiana na serikali katika kuwekeza kwenye sekta ya Mifugo, hasa zao la Ngozi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupanua wigo wa biashara na kusaidia wananchi.

Ukuaji wa sekta ya Ngozi nchini Tanzania umeendelea kuimarika ambapo mwaka 2020/2021 jumla ya vipande million 11.7 vilizalishwa ikilinganishwa na vipande milioni 15.2 vya Ngozi mwaka 2024/2025 (sawa na ongezeko la asilimia 29.9), hivyo ushirikiano wa Serikali na wadau wengine kupitia mjadala ulioandaliwa na benki ya Equity utasaidia kuweka mikakati ya pamoja ya kukuza sekta ya Ngozi nchini na kuongeza mchango wake kwenye Pato la Taifa na mtu mmoja mmoja kwenye mnyororo wa thamani wa kisekta.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk.Edwin Mhede, akizungumza wakati akifungua  kongamano la ngazi ya juu kuhusu kufungua fursa za minyororo ya thamani ya mifugo na ngozi nchini Tanzania lililoandaliwa na Benki ya Equity lililofanyika leo Julai 23.2025 jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Equity, Dkt.Florens Turuka, akizungumza wakati wa  kongamano la ngazi ya juu kuhusu kufungua fursa za minyororo ya thamani ya mifugo na ngozi nchini Tanzania lililoandaliwa na Benki ya Equity lililofanyika leo Julai 23.2025 jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity, Bi. Isabela Maganga, (aliyesimama)  akizungumza wakati wa  kongamano la ngazi ya juu kuhusu kufungua fursa za minyororo ya thamani ya mifugo na ngozi nchini Tanzania lililoandaliwa na Benki ya Equity lililofanyika leo Julai 23,2025 jijini Dodoma.





SERIKALI YAANZA KUPANDIKIZA SAMAKI ZIWA HAUBI KONDOA DC

Na. Hamis Hussein

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Edwin Mhede amezindua rasmi upandikizaji wa vifaranga vya samaki aina sato katika ziwa Haubi lililopo halmashauri ya Wilaya ya Kondoa ili kuongeza aina ya samaki wanaopatika kwenye ziwa hilo.

Dkt. Mhede amezindua upandikizaji huo julai 21, 2025 katika kijiji cha Haubi ambapo amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi itatuma wataalam kwa ajili kufanya tathmini ya namna ya kulinda ikolojia ya ziwa hilo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kufanya upandikizaji wa vifaranga vya samaki.

Amesema ili kuongeza aina ya samaki wanaopatikana kwenye ziwa hilo  wizara itashirikiana na wananchi wa kijiji hicho ambao ndio wamiliki wa asili wa ziwa hilo na watalam watatoa  elimu ya jinsi ya kupandikiza  samaki aina ya sato tofauti na Kambare wanaopatikana kwa sasa ambao wamesababisha wananchi wa kijiji cha Haubi kuwa na mavuno ya samaki ya msimu.

Kwa upande kwake mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Bi. Mwasiti Juma amesema ziwa hilo  limekuwa likitumika kuwapatia wananchi mahitaji ya madogo madogo ya nyumbani hususani protini kutokana na samaki lakini changamoto ni uwepo wa samaki aina moja  jambo linalosababisha kuwa na mavuno kidogo na ya msimu.






BI. MEENA AONGOZA KIKAO CHA KAMATI YA UONGOZI WA MRADI WA C - SDTP JIJINI DODOMA

Na. Hamis Hussein

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena ameongoza Kikao cha kamati ya uongozi wa mradi wa mageuzi katika tasnia ya maziwa kwa kuzingatia mabadiliko ya tabia nchi leo Julai 22, 2025 katika hoteli ya Rafiki jijini Dodoma.

Kikao hicho kimelenga Kutambulisha mradi huo wa mageuzi ya tasnia ya maziwa  kwa kuzingatia mabadiliko ya tabia ya nchi kwa kamati ya uongozi ili kamati iweze kupitia na kuuidhinisha mpango kazi wa mradi na manunuzi kwa mwaka 2025/ 2026.







CHANJO YA MIFUGO ITAONGEZA THAMANI YA MIFUGO YETU - DKT. MHEDE

Na. Hamisi Hussein, Kondoa

Uamuzi wa Serikali wa kuwekeza kwenye sekta ya mifugo kwa kutoa ruzuku ya chanjo na utambuzi wa mifugo utasaidia kupatikana kwa  ithibati kutoka Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH) ya kufanya biashara ya mifugo na mazao yake kwenye masoko ya ndani na ya kimataifa jambo litakaloinua uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

Hayo yamefahamika wakati Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede akikagua utekelezaji wa Kampeni ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo  katika kijiji cha Soera wilayani  Kondoa mkoani Dodoma leo Julai 21, 2025.  

" Leo tumekabidhi pikipiki 31 kwa maafisa ugani ili waweze kutekeleza kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo, serikali imetoa ruzuku ya chanjo ya asilimia 50 kwa ng'ombe, mbuzi na kondoo na asilimi 100 (bure) kwa chanjo ya kuku kwahiyo chanjo  hii itaongeza thamani ya mifugo yetu" amesema Dkt. Mhede.

Kuhusu utambuzi Dkt. Mhede amesema zoezi la chanjo ya mifugo linaenda sambamba na utambuzi ili  kutengenisha  mifugo iliyochanjwa na ambayo bado haijachanjwa na kudhibiti wizi wa mifugo na kutoa wito kwa wataalam wanaoenda kutekeleza kampeni hiyo kutumia na kuvitunza vifaa vya chanjo  ili viwahudumie wafugaji kama ilivyokusudiwa.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Bi. Mwasiti  Juma ameishukuru serikali kwa kutoa chanjo hiyo kwani itawainua wafugaji kiuchumi kutokana na kwamba sekta ya mifugo ni sehemu muhimu katika uchumi wa Kondoa.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa Shabani Millao amekiri kuipokea kampeni hiyo na kuahidi kuwasimamia wataalam wa chanjo na utambuzi wa Mifugo kutekeleza kampeni hiyo kwa wafugaji wote wa Wilaya hiyo.

Naye Daktari wa Mifugo Wilaya Kondoa ambaye ndiye mratibu wa kampeni ya chanjo na utambuzi Wilayani hapo Dkt. Chritian Mwiga amesema wilaya hiyo itachanja ng'ombe 200,000 mbuzi na kondoo 280,000 na kuku 460,000 huku akitoa wito kwa wafugaji kupeleka mifugo katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya chanjo.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Edwin Mhede (kushoto) akitoa chanjo ya mdondoo wa Kuku kama ishara ya kuanza kwa utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo kwa Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma Julai 21, 2025.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Edwin Mhede (kushoto) akimkabidhi Pikipiki Afisa Ugani Kata ya Itololo Bi. Thereza Luoga  kwa ajili ya utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo kwa Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma Julai 21, 2025.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Edwin Mhede (wa pili kulia) akimwekea  ng'ombe hereni ya kielekitroniki kwa ajili ya utambuzi baada  ya kumpatia chanjo ya homa ya mapafu ikiwa ni utekelezaji wa kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo kwa Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma Julai 21, 2025.


Jumatatu, 21 Julai 2025

DKT. MHEDE AZITAKA TAASISI ZINAZOFANYA KAZI MPAKANI NAMANGA KUFANYA KAZI KWA USHIRIKIANO ILI KULETA TIJA

 Na. Stanley Brayton, WMUV 

 Longido 

 Julai 20, 2025 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Edwin Mhede, amezitaka Taasisi zinazofanya kazi katika mpaka wa Namanga kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuleta tija katika Uzalishaji na kutekeleza majukumu yao na kuleta matokeo chanya. 

Akizungumza leo Julai 20, 2025 alipotembelea Kituo cha Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (FRP), Mnada wa Upili na Idara ya Huduma za Mifugo vilivyoko katika mpaka wa Namanga, Wilaya ya Longido, kwa lengo la kufanya ufuatiliaji wa shughuli za Uvuvi na Mifugo katika eneo hilo na kuongea na Watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi walioko katika Kituo hicho ili kubaini changamoto zinazowakabaili maafisa katika kutekeleza majukumu yao, Dkt. Mhede amesema ni muhimu kushirikiana kati ya Taasisi na Taasisi katika kuleta tija na kuongeza uzalishaji pamoja na Maendeleo nchini.

Vilevile, Dkt. Mhede amesema ni vyema Wataalam wa Sekta zote kushirikiana na wadau kwa kukaa nao vikao vya pamoja ili kubaini changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Aidha, Dkt. Mhede ameelekeza Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kufanya maandalizi kwa ajili ya kupandikiza vifaranga vya samaki katika Mabwawa ya Manyara, Eda Chini na Eyasi ili kuongeza Uzalishaji wa zao hilo la Samaki katika Mabwawa hayo na kuleta tija katika Sekta hiyo.

Pia, Dkt. Mhede, amitaka Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kufuatilia Mabwawa ya asili ambayo yapo Mikoani, hususani katika Mkoa wa Arusha na Manyara kwa ajili ya kupandikiza vifaranga ili kuongeza uzalishaji nchini.

       

UWEZESHAJI WAVUVI WAONGEZA MAVUNO YA SAMAKI KUFIKIA TANI ZAIDI YA LAKI 5 KWA MWAKA

Na. Hamisi Hussein, Lindi

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesema Programu ya utoaji wa boti za kisasa za uvuvi pamoja na programu nyingine zimelenga  kuwawezesha wavuvi wadogo kunufaika na shughuli za uvuvi hapa nchini.

Akikabidhi boti za kisasa za uvuvi na vifaa vyake awamu ya pili kwa mikoa ya Lindi na Mtwara, hafla iliyofanyika katika Bandari ya Lindi leo Julai 18, 2025,  Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena amesema uwezeshwaji wa wavuvi wadogo umeongeza tija katika sekta ya uvuvi ambapo kiwango cha samaki kinachovunwa kwa mwaka kimeongezeka zaidi  baada ya uwezeshaji huo.

"Zoezi la ugawaji wa boti za kisasa za uvuvi na Vifaa vyake lililozinduliwa na Mhe. Rais ni sehemu ya juhudi za serikali kuwawezesha wavuvi wadogo kunufaika na sekta ya uvuvi, na juhudi hizi zimeongeza kiwango cha samaki wanaovunwa kutoka tani 387,542.56 zenye thamani ya Shilingi trilioni 1.74 mwaka 2017/2018 hadi kufikia tani 529,668.01 zenye thamani ya Shilingi trilioni 4.5 mwaka 2024/2025" alisema

Bi. Meena aliongeza kwa kusema kuwa ongezeko hilo pia limeonekana kwenye mauzo ya mazao ya uvuvi nje ya nchi ambapo yameongezeka kutoka tani 44.939.79 hadi tani 59,746.41 sawa na ongezeko la tani 14,806.7.

Katika hatua nyingine, Bi. Meena amewataka Wananchi waliokabidhiwa boti za kisasa za uvuvi  kukemea na kukataa vitendo vya Uvuvi haramu kwani serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza kutumia teknolojia ya kisasa ya kudhibiti uvuvi haramu katika eneo la bahari kuu na maziwa ili kulinda rasilimali za uvuvi nchini.

 "Ni matumaini yangu kuwa ninyi mnaokabidhiwa boti hizi hivi leo mtakuwa mstari wa mbele katika kukemea na kukataza vitendo vya uvuvi haramu.  Pia nitoe rai kwa wavuvi wote nchini kuendelea kupinga vitendo hivi viovu, kwa pamoja tulinde rasilimali zetu kwa kizazi cha sasa na kijacho"

Aidha, alibainisha kuwa Idadi ya watu wanaojipatia kipato kupitia shughuli za uvuvi nchini imeongezeka kutoka watu milioni 4 mwaka 2020 hadi kufikia zaidi ya watu milioni 6 mwaka 2025, hii ni kutokana na uwezeshwaji wa wavuvi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya sekta ya uvuvi unaofanywa na serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Akisoma taarifa ya mradi huo Mkurugenzi wa Uvuvi Prof. Mohamed Sheikh amesema jumla ya boti 10 za uvuvi zilizokabidhiwa kwa mkoa wa Lindi na Mtwara zitawanufaisha wanufaika 427 kati ya hayo wanaume 391 wanwake 36.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi Bw. Nathalis Linuma amesema katika kuhakikisha wavuvi wanaunganishwa na taasisi za fedha, Mkoa huo umeendelea kufanya usajili  wa vikundi ili viweze kupatiwa mikopo ambapo hadi sasa jumla ya vikundi 8 vya ushirika wa wavuvi vimesajiliwa.

Nao baadhi ya wanufaika wa Boti hizo wameishukuru  Serikali kwa kupatiwa  vifaa hivyo kwani vitasaidia kuwa na uhakika wa samaki jambo litakaloongeza tija katika sekta ya uvuvi.

Katibu Mkuu wa. Wizara  ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena (kushoto) akikabidhi Boti za kisasa za uvuvi na vifaa vyake  kwa wawakilishi wa vikundi vya mikoa ya Lindi na Mtwara muda mfupi baada ya uzinduzi wa zoezi hilo Julai 18, 2025 Mkoani Lindi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena  akizungumza na wavuvi ambao ni wanufaika wa mikopo ya boti za kisasa za Uvuvi kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara  wakati wa Hafla ya ugawaji boti hizo za Uvuvi awamu ya pili iliyofanyika Julai 18, 2025 mkoani Lindi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena (Kulia) akikabidhi cheti kwa mwakilishi wa kikundi cha wanufaika wa mikopo ya boti za kisasa za Uvuvi kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara  wakati wa Hafla ya ugawaji boti hizo za Uvuvi awamu ya pili iliyofanyika Julai 18, 2025 mkoani Lindi.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi Nathalis Linuma akizungumzia hali ya sekta ya Uvuvi kwa Mkoa wa Lindi wakati wa Hafla ya ugawaji boti hizo za Uvuvi awamu ya pili iliyofanyika Julai 18, 2025 mkoani Lindi.

Sehemu ya Boti 10 za Kisasa za Uvuvi zilizokabidhiwa kwa wanufaika wa mikoa ya Lindi na Mtwara wakati wa Hafla ya ugawaji Boti hizo awamu ya pili iliyofanyika Julai 18, 2025 Mkoani Lindi.


Alhamisi, 17 Julai 2025

DKT. MHEDE AHITIMISHA MKUTANO WA WADAU WA TASNIA YA KUKU

Na. Hamis Hussein

Naibu Katibu Mkuu  Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Edwin Mhede amehitimisha  mkutano wa wadau wa tasnia ya kuku ujulikanao  (National Poultry Delivery Lab), uliofanyika kwa siku mbili katika Hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam. 

Akizungumza leo Julai 16, 2025 katika hafla ya kufunga Mkutano huo Dkt. Mhede amesisitiza kuundwa haraka kwa kamati ndogo ya kiufundi itakayoratibu na kufuatilia maazimio ya mkutano huo na kuahidi kushirikiana nayo  ili kuhakikisha kuwa  Wizara kwa kushirikiana na wadau, inakamilisha na kuzindua  Mkakati wa Tasnia ya Kuku.

Aidha, Dkt. Mhede amewapongeza wadau wa tasnia ya kuku walivyobainisha na kujadili changamoto na fursa za tasnia hiyo na kutoa mikakati ya kuinua tasnia hiyo , ikiwa ni hatua muhimu ya kuanisha masuala ya kuzingatia katika uandaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Tasnia ya Kuku Nchini.

Katika hatua nyingine Dkt. Mhede amesisitiza kuongeza wigo wa ushiriki wa wadau wengine katika mnyororo wa thamani ili kuhakikisha masuala yote ya kimkakati yanaingia katika  mapendekezo hayo.



DKT. KIJAJI AKABIDHI BOTI ZA UVUVI ZENYE THAMANI YA BIL.2

Na. Omary Mtamike

◼️Ni sehemu ya Boti 120 zinazotolewa na Serikali kwenye awamu ya pili

◼️Wavuvi 205 kunufaika

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amekabidhi boti 13 za Uvuvi zenye thamani ya takribani shilingi Bil. 2 kwa Vikundi vya mikoa ya Pwani na Dar-es-salaam ambazo zinatarajiwa kuwanufaisha zaidi ya Wavuvi 205  wa mikoa hiyo.

Mhe. Dkt. Kijaji amekabidhi boti hizo Julai 16, 2025 kwenye ufukwe wa Shirika la Uvuvi nchini (TAFICO) ambapo mkoa wa Pwani umekabidhiwa Boti 8 huku mkoa wa Dar-es-Salaam ukikabidhiwa boti 5 zote jumla zikiwa na uretu wa mita 12 na 14 ambazo zinajumuisha vifaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Nyavu, kamba, maboya, nyuzi, kitafuta samaki na boti saidizi maarufu kama dingi.

“Boti mlizopokea leo zimefanyiwa maboresho yote yaliyotokana na maoni mliyotoa kutoka kwenye boti za awamu ya kwanza na sisi kama Serikali tunatamani kuona mnaendelea mnafanikiwa kupitia boti hizo” Ameongeza Mhe. Dkt. Kijaji

Aidha Mhe. Dkt. Kijaji amebainisha kuwa ugawaji wa boti hizo ni sehemu ya mkakati wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan uliolenga kuboresha sekta ya Uvuvi nchini ambapo wanufaika wanajumuisha makundi manne ambavyo ni watu binafsi, makampuni na vikundi vya Wavuvi.

“Boti hizi zimechangia ongezeko la idadi ya watu wanaonufaika kutokana na Sekta ya Uvuvi ambapo mpaka zaidi zaidi ya Watu Milioni 6 wanapata vipato vyao kupitia sekta hii hivyo niwaombe wote mliopatiwa mikopo hii muirejeshe kwa wakati ili tuwawezeshe na wengine kukopeshwa “ Amesema Mhe. Dkt. Kijaji.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-Salaam Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe. Mikaya Dalmia amesema kuwa awamu ya kwanza ya mkopo wa boti hizo za Uvuvi iliufanya mkoa huo kuvuna takribani tani 18892 za samaki hivyo aliwataka wanufaika wa awamu ya pili kutumia vema fursa hiyo ili wavune zaidi ya kiwango hicho cha awamu iliyopita.

Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Shaib Ndemanga mbali na kuishukuru Serikali kwa boti hizo zinazotolewa kwa mkopo wenye masharti nafuu, amesema kuwa zitaboresha maisha ya wananchi wa mkoa huo ambao kwa kiasi kikubwa wanajishughulisha na shughuli za Uvuvi kwa ajili ya mahitaji ya Chakula na kukuza uchumi wao.

Boti hizo zilizotolewa leo ni sehemu ya Boti 120 zinazotarajiwa kutolewa kwenye awamu ya pili ya Mkopo huo wenye masharti nafuu ambapo mpaka kukamilika kwa awamu zote mbili jumla ya Boti 280 zinatarajiwa kukopeshwa kwa Wavuvi nchini.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (katikati), Viongozi na Watendaji wa Wizara na mikoa ya Pwani na Dar-es-Salaam wakikabidhi mfano wa ufunguo wa boti ya Uvuvi ikiwa ni ishara ya kukabidhi boti za kisasa za Uvuvi kwa Vikundi vya mikoa hiyo (kulia) Julai 16, 2025 jijini Dar-es-Salaam.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (kushoto) akikabidhi cheti kwa mwakilishi wa kikundi cha “Survival Women) kutoka Bagamoyo wakati wa Hafla ya ugawaji Boti za kisasa za Uvuvi awamu ya pili iliyofanyika Julai 16, 2025 jijini Dar-es-Salaam.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (katikati) akikabidhi zana za Uvuvi kwa wawakilishi wa vikundi vya mikoa ya Pwani na Dar-es-Salaam muda mfupi baada ya kuwakabidhi boti za kisasa za Uvuvi Julai 16, 2025 jijini Dar-es-Salaam.





Jumatano, 16 Julai 2025

DKT. MHEDE AFUNGUA MKUTANO WA WADAU WA TASNIA YA KUKU

Na. Hamis Hussein 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede amefungua Mkutano wa tasnia ya Kuku (National Poultry Delivery Lab) unaofanyika  katika Hoteli ya Serena, Jijini Dar-es-salaam kuanzia leo Julai 15-16, 2025. 

Mkutano huo umelenga kuwakutanisha wadau wa tasnia ya kuku ili kuchambua, kujadili na kutoa suluhisho ya namna ya kukabiliana na changamoto zinazopunguza ufanisi na ushindani wa tasnia ya Kuku nchini.

Akifungua Mkutano huo,  Dkt. Mhede alielezea kuwa tasnia ya kuku  imeajiri asilimia 65 ya vijana na asilimia 51 ya wanawake nchini

 "Tasnia ya Kuku inachagiza ukuaji wa sekta nyingine ikiwemo Kilimo kutokana na mahitaji makubwa  ya vyakula vya Kuku vinavyotokana na mahindi na soya  ambayo vimeifanya tasnia hii  ya kuku kuwa ya kimkakati nchini" alisema Dkt. Mhede.

Aidha, Dkt Mhede amewahimiza Washiriki wa mkutano huo kutumia jukwaa hilo kuchambua na kuanisha maeneo ya kimkakati ambayo yatatatua changamoto zinazoikabili tasnia hiyo pamoja na  kujenga uwezo kwa wafugaji  na wafanyabiashara  wa tasnia ya kuku ndani ya nchi ili waweze kuzalisha kwa tija na kuyafikia masoko.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede akifungua Mkutano wa tasnia ya Kuku (National Poultry Delivery Lab) unaofanyika  katika Hoteli ya Serena, Jijini Dar-es-salaam kuanzia leo Julai 15-16, 2025.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede, akiwa katika picha ya pamoja na Washiriki mara baada ya uzinduzi  wa Mkutano wa National Poultry Delivery Lab  unaofanyika katika hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam kuanzia Julai 15-16, 2025.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede akiwa katika mazungumzo na wadau kutoka Benki ya Dunia,  SAGCOT, pamoja na Shirika la IFAD kando ya Mkutano wa National Poultry Delivery Lab unaofanyika katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam kuanzia Julai 15- 16, 2025.


UTEKELEZAJI KAMPENI YA CHANJO: MIFUGO MILIONI 6 YACHANJWA NDANI YA WIKI 2

Na. Omary Mtamike

◼️Zoezi sasa kuendelea kwa miezi 2

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amebainisha kuwa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo imefanyika kwa mafanikio ambapo takribani Mifugo Milioni 6 imechanjwa na kutambuliwa tangu kuanza kwa kampeni hiyo Julai 02,2025 hadi sasa. 

Mhe. Dkt. Kijaji asema hayo wakati wa tukio la kuanza kwa kampeni hiyo mkoani Dodoma lililofanyika Wilaya ya Bahi Julai 15, 2025 ambapo ametoa shukrani kwa wafugaji kote nchini kwa namna walivyojitokeza tangu kuanza kwa zoezi hilo ambapo amewaomba kuendelea kufanya hivyo kwa kipindi chote cha miezi miwili ya utekelezaji wake.

“Mhe. Rais amedhamiria kutekeleza kampeni hii kwa wafugaji wote bila kumuacha hata mmoja na ndio maana amewawezesha maafisa Mifugo kwenye kata zote pikipiki na mafuta yake ili waweze kuwafikia wafugaji wote hivyo sitegemei kuona mtaalam yoyote wa Mifugo akiwa ofisini wakati wa utekelezaji wa kampeni hii” Ameongeza Mhe. Dkt. Kijaji

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa huo kwenye tukio hilo ambaye pia Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Joachim Nyingo amesema kuwa utekelezaji wa kampeni hiyo una manufaa kwa Watanzania wote ambapo wengi watanufaika kupitia mzunguko wa fedha zitakazotokana na kuuzwa kwa Mifugo hiyo kwenye masoko ya nje.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji kanda ya kati Bw. Saramba Mataji amewataka wafugaji wote kwenye kanda hiyo kuchangamkia fursa hiyo iliyotolewa na Serikali ili waweze kuondokana na changamoto ya upotevu wa Mifugo yao ambayo imekuwa ikiwasumbua kwa muda mrefu.

Kampeni hiyo ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo itaendelea kote nchini kwa kipindi cha miezi Miwili ambapo kwa mwaka huu ambapo Serikali imeshatoa takribani Shilingi Bilioni 69.2 kwa ajili ya utekelezaji wake.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (katikati) akitoa chanjo ya mdondo wa kuku kama ishara ya kuanza kwa utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo mkoani Dodoma Julai 15,2025. Kulia ni Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa huo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Joachim Nyingo na kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Bi. Albina Mtumbuka.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, Viongozi na Watendaji mbalimbali wa mkoa wa Dodoma (kushoto) wakishuhudia zoezi la uchanjaji linavyofanyika wakati wa hafla ya kuanza kwa Kampeni ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo Wilaya iliyofanyika Wilaya ya Bahi Julai 15, 2025.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akivalishwa skafu na vijana wa skauti mara baada ya kuwasili Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma Julai 15, 2025 ambako aliongoza Hafla ya kuanza kwa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo mkoani humo.


Jumanne, 15 Julai 2025

CHANJO NA UTAMBUZI NI MAPINDUZI YA SEKTA YA MIFUGO NCHINI-DKT.KIJAJI

Na. Omary Mtamike

◼️Serikali yadhamiria kuondokana na homa ya Mapafu ya Ng’ombe ifikapo 2030

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo itakuwa ni chachu ya mapinduzi wa sekta ya Mifugo nchini.

Mhe. Kijaji amesema hayo wakati wa ziara yake ya Ukaguzi wa utekelezaji wa kampeni hiyo Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro Julai 10, 2025 ambapo amebainisha kuwa kufanyika kwa kampeni hiyo kunaweka ukomo wa kutorosha mifugo katika nchi jirani ambako wafugaji walikuwa wanaenda kutafuta masoko kwenye nchi zilizopata ithibati ya Shirika la kimataifa la Afya ya wanyama (WOAH).

“Kwa hivi sasa baada ya kutangaza tu kuanza kwa kampeni hii tayari masoko ya kimataifa yameonesha dhamira ya kuhitaji Mifugo yetu hai na mazao yake na ninatamani itakapomalizika miaka 5 ya utekelezaji wa kampeni hii turejee kwa Mhe. Rais na kumuonesha namna alivyofanikiwa kubadili sekta yetu ya Mifugo” Ameongeza Mhe. Dkt. Kijaji.

Akielezea ubora wa hereni za kielektroniki zinazotumika kwenye zoezi la Utambuzi wa Mifugo, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo nchini Dkt. Benezeth Lutege amesema kuwa hereni hizo zimetengenezwa kwa kuzingatia ustawi wa wanyama ikiwa ni pamoja na kuwekewa kifaa maalum kinachoziwezesha kuzunguka sikioni pindi mnyama anapotembea.

“Lakini pia hereni hizi mbali na kuwa na gamba gumu lisiloweza kuvunijika, maandishi yake yameandikwa kwa mionzi mikali na hivyo kutoweza kufutika hata yakikwanguliwa na kifaa chenye ncha kali” Ameongeza Dkt. Lutege.

Akizungumza kwa niaba ya wafugaji wa Mkoa wa Morogoro, Kiongozi wa kimila wa mikoa ya kanda ya Mashariki Chifu Kashu Moreto amesema kuwa chanjo hizo na hereni zinafuta fikra potofu waliyokuwa nayo wafugaji hapo awali ambapo waliamini mifugo inachanjwa na kutambuliwa ili itaifishwe na Serikali.

“Kwa bahati nzuri Rais wetu mpendwa ameongea maneno mazuri kwa kusema hereni zitatolewa bure hivyo mimi kwa kuwa ni kiongozi wa takribani mikoa 7 hivyo nitapiga kelele kwa wafugaji wenzangu wote tukachanje ila naomba Serikali iendelee kusimamia vema zoezi hili ili chanjo hizo ziendelee kuwa salama kwa Mifugo yetu” Amesema Chifu Kashu.

Ziara hiyo ya Mhe. Dkt. Kijaji iliyolenga kukagua utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo iliyozinduliwa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu Juni 16, 2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inatarajiwa kuhitimishwa katika Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (katikati) akitoa chanjo ya mdondo wa kuku kama ishara ya kuanza kwa utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo mkoani Morogoro Julai 10, 2025. Kushoto Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa huo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Doto Maulid na kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Japhary Kubecha.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji na baadhi ya Viongozi wa Wilaya ya Mvomero na wale wa wafugaji (kulia) wakishuhudia namna zoezi la utoaji wa chanjo za Mifugo linavyofanyika mara baada ya kuanza kwa utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo mkoani Morogoro Julai 10,2025.





PWANI KUCHANJA NA KUTAMBUA MIFUGO YOTE KWA SIKU 30

Na. Omary Mtamike

Uongozi wa mkoa wa Pwani umesema kuwa utatumia siku 30 pekee kuchanja na kutambuaMifugo yake badala ya miezi 2 iliyopangwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutekeleza zoezi hilo.

Ahadi hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Shaib Ndemanga ambaye pia alimwakilisha mkuu wa Mkoa huo kwenye ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji iliyolenga kukagua Utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo kwenye kwenye kijiji cha Miono Wilaya ya Chalinze.

“Tunajua nyie kama Wizara mmepanga kutekeleza awamu ya kwanza ya zoezi hili kwa miezi miwili lakini nikuhakikishie Mhe. Waziri mkoa wa Pwani kwa furaha tuliyonayo na namna tulivyopokea zoezi hili tutahakikisha tunamaliza ndani ya siku 30” Amesema Mhe. Ndemanga.

Akizungumza mara baada ya kushuhudia kuanza kwa utekelezaji wa kampeni hiyo mkoani Pwani, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ameupongeza mkoa huo kwa namna walivyopokea zoezi hilo alilolitaja kama sehemu ya maono makubwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa upande wa sekta ya Mifugo na wafugaji kwa ujumla.

“Tumeshaanza majadiliano na nchi 5 wanaohitaji kuchukua mifugo yetu ikiwa hai na hiyo inamaanisha kwa sasa soko la Mifugo yetu limeonekana na kwa hapa Pwani tuna kiwanda kikubwa cha kusindika nyama ambacho kitaweza kufikia asilimia 100 za uwezo wake tofauti na ilivyo sasa ambapo kinafanya kazi kwa asilimia 50 ya uwezo wake” Ameongeza Mhe. Dkt. Kijaji.

Naye Mwenyekiti wa chama cha Wafugaji mkoani humo Bw. Ngobere Msamau mbali na kuishukuru Serikali kutokana na chanjo hizo amemhakikishia Mhe. Dkt. Kijaji kuwa wataendelea kutekeleza ushauri na maelekezo yote wanayopewa na Serikali baada ya tija kubwa waliyoanza kuipata hivi sasa.

Ziara hiyo ya Mhe. Dkt. Kijaji iliyolenga kukagua utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo iliyozinduliwa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu Juni 16, 2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea katika mkoa wa Morogoro Julai 10, 2025.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (kushoto) akitoa chanjo ya mdondo wa kuku kama ishara ya kuanza kwa utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo mkoani Pwani Julai 09, 2025. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mhe. Petro Magoti.

Mkurugenzi wa huduma za Mifugo nchini Dkt. Benezeth Lutege (kushoto) akimweleza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, Viongozi na Watendaji mbalimbali wa Wizara hiyo na mkoa wa Pwani sifa za hereni za kielektroniki zitakazotumika kwenye zoezi la Utambuzi wa Mifugo wakati wa hafla ya kuanza kwa utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo mkoani humo Julai 09, 2025.

Wakuu wa Wilaya ya Bagamoyo na Kisarawe Mhe. Petro Magoti na Shaib Ndemanga wakielezwa namna mfumo wa utambuzi wa Mifugo kwa kutumia hereni za kielektroniki unavyofanya kazi wakati wa hafla ya kuanza kwa utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo mkoani Pwani Julai 09, 2025. Kushoto anayeshuhudia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji na Viongozi mbalimbali wa mkoa wa Pwani (kulia) wakishuhudia zoezi la uchanjaji linavyofanyika Kwenye kijiji cha Miono mkoani humo Julai 09, 2025.