Nav bar

Jumatano, 22 Februari 2023

NZUNDA ATOA MAELEKEZO KWA WATAFITI WA MIFUGO

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda amewataka watafiti wa mifugo kufanya tafiti zinazozingatia maslai ya nchi.

 

Nzunda ameyasema hayo (20.02.2023) wakati akifungua Warsha ya Uzinduzi wa Mradi wa Utafiti wa Mifugo na Mazingira kwa lengo la kuchunguza utoaji wa jopo gesi (GHC) na kupunguza gharama za chakula katika mifumo ya wafugaji wadogo wa ng’ombe wa maziwa iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Panama mkoani Kilimanjaro.

 

Watafiti wametakiwa kuzingatia malengo ya nchi katika kuleta mabadiliko kwenye sekta ya mifugo katika tafiti wanazozifanya ili kuongeza tija katika uzalishaji na sio kutumia tafiti hizo kwa matakwa ya wafadhili au maslai yao binafsi.

 

Pia watafiti wametakiwa kuzingatia utaalam, misingi ya maadili, uwajibikaji unaotokana na matendo na matokeo ya tafiti wanazozifanya ukiwemo utafiti wa Mifugo na Mazingira kwa lengo la kuchunguza utoaji wa jopo gesi (GHC) na kupunguza gharama za chakula katika mifumo ya wafugaji wadogo wa ng’ombe wa maziwa.

 

Vilevile amewasihi watanzania kuziunga mkono taasisi za utafiti kwa kuwa sayansi huwa haisemi uongo, hivyo kupitia tafiti hizo mabadiliko kwenye sekta ya mifugo.

 

Nzunda amewataka maafisa ugani kuhakikisha wanayafikisha matokeo ya tafiti kwa wafugaji na kuhakikisha yanatumika. Aidha, maafisa ugani wametakiwa kuhakikisha wanawatembelea wafugaji na kutoa ushauri wao pale unapohitajika. Vilevile ameziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuweka utaratibu wa kuwapima maafisa hao ili kuhakikisha wafugaji wanatembelewa.

 

Akiuzungumzia mradi huo, Mratibu wa mradi wa ADGG na Mtafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Duniani (ILRI), Dkt. Eliamoni Lyatuu amesema kuwa taasisi hiyo ya utafiti imekuwa ikifanya tafiti mbalimbali hapa duniani kwa kushirikiana na taasisi za utafiti za nchi husika.

 

Katika mradi huo, wamelenga kufanya utafiti utakaosaidia kuangalia athari za mazingira zinazosababishwa na mifugo, lengo likiwa ni kuhakikisha kuna kuwa na ufugaji wa ng’ombe kwa gharama nafuu na usioathiri mazingira.

 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti Tanzania, Prof. Erick Komba alieleza malengo ya taasisi hiyo katika kuhakikisha wafugaji wananufaika na tafiti mbalimbali zinazofanyika ili waweze kufuga kwa tija. Katika utafiti huo wanaokwenda kuufanya wataangalia pia vyakula vinavyotumika kwenye mifugo kama navyo vinamchango katika kuathiri mazingira.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda akifungua Warsha ya Uzinduzi wa Mradi wa Utafiti wa Mifugo na Mazingira kwa lengo la kuchunguza utoaji wa gesi joto (GHC) na kupunguza gharama za chakula katika mifumo ya wafugaji wadogo wa ng’ombe wa maziwa iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Panama mkoani Kilimanjaro ambapo amewasihi watafiti hao kuzingatia malengo ya nchi katika kuleta mabadiliko kwenye sekta ya mifugo katika tafiti wanazozifanya ili kuongeza tija katika uzalishaji. (20.02.2023)


Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani, Dkt. Dkt. Angello Mwilawa akizungumza wakati wa Warsha ya Uzinduzi wa Mradi wa Utafiti wa Mifugo na Mazingira kwa lengo la kuchunguza utoaji wa gesi joto (GHC) na kupunguza gharama za chakula katika mifumo ya wafugaji wadogo wa ng’ombe wa maziwa iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Panama mkoani Kilimanjaro ambapo alielezea namna wizara inavyoshirikiana na taasisi za utafiti wa mifugo. (20.02.2023)


Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti Tanzania, Prof. Erick Komba akieleza malengo ya taasisi hiyo katika kuhakikisha wafugaji wananufaika na tafiti mbalimbali zinazofanyika ili waweze kufuga kwa tija wakati wa Warsha ya Uzinduzi wa Mradi wa Utafiti wa Mifugo na Mazingira kwa lengo la kuchunguza utoaji wa gesi joto (GHC) na kupunguza gharama za chakula katika mifumo ya wafugaji wadogo wa ng’ombe wa maziwa iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Panama mkoani Kilimanjaro. (20.02.2023)


Mratibu wa mradi wa ADGG na Mtafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Duniani, Dkt. Eliamoni Lyatuu akitoa maelezo kwa washiriki kabla ya kufanyika kwa kazi za makundi wakati wa Warsha ya Uzinduzi wa Mradi wa Utafiti wa Mifugo na Mazingira kwa lengo la kuchunguza utoaji wa gesi joto (GHC) na kupunguza gharama za chakula katika mifumo ya wafugaji wadogo wa ng’ombe wa maziwa iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Panama mkoani Kilimanjaro. (20.02.2023)


Mratibu wa mradi wa ADGG na Mtafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Duniani, Dkt. Eliamoni Lyatuu akitoa maelezo kwa washiriki kabla ya kufanyika kwa kazi za makundi wakati wa Warsha ya Uzinduzi wa Mradi wa Utafiti wa Mifugo na Mazingira kwa lengo la kuchunguza utoaji wa gesi joto (GHC) na kupunguza gharama za chakula katika mifumo ya wafugaji wadogo wa ng’ombe wa maziwa iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Panama mkoani Kilimanjaro. (20.02.2023)

Jumanne, 21 Februari 2023

KAZI YAZIDI KUENDELEA KUPITIA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI

 BIL 6.2 ZA MABWAWA KUNUFAISHA WAFUGAJI

Na. Edward Kondela


Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha kila sekta nchini ambapo imepanga kujenga mabwawa ya kunyweshea mifugo maji kote nchini.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akizungumza (17.02.2023) wakati alipofanya ziara ya kikazi kukagua maendeleo ya ujenzi wa bwawa la maji la Kwekinkwembe lililopo katika Wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga, amesema Rais Dkt. Samia katika bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2022/23 ameridhia kuipatia wizara Shilingi Bilioni 6.2 kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa hayo.


Naibu Waziri Ulega amefafanua kuwa kila sekta nchini imeguswa ikiwemo ya mifugo na kwamba hakuna iliyeachwa nyuma hivyo wafugaji watanufaika kwa kupata maji ya uhakika mara baada ya mradi wa ujenzi wa mabwawa ya kunyweshea mifugo maji kukamilika.


“Rais Mhe. Dkt. Samia hakuna aliyemuacha pembeni ndiyo maana amegusa wakulima mbegu za ruzuku, amegusa wafugaji mabwawa na majosho, hivyo hakuna aliyeachwa nyuma.” Amesema Mhe. Ulega.


Aidha amemtaka mkandarasi anayefanya shughuli za ujenzi wa bwawa hilo kuhakikisha anatoa taarifa ya kila hatua ya ujenzi na kuacha nakala wilayani hadi ngazi ya kijiji kunapojengwa bwawa hilo ili taarifa ziwe wazi na kumtaka kukamilisha ujenzi kwa wakati.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Mhe. Abel Busalama amewataka wananchi wa Kijiji cha Kwekinkwembe kuhakikisha bwawa hilo linalojengwa kwa thamani ya Shilingi Milioni 504 mara litakapokamilika walisimamie vyema ili liwe na tija kwao.


Amesema uongozi wa kijiji utapaswa kuweka utaratibu mzuri wa namna ya kulitumia na kuliongezea thamani kwa kuyafanyia pia maji hayo shughuli mbalimbali.


Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji nchini (CCWT) Wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga Bw. Merieki Long’oni amesema ni faraja kubwa kwao kwa namna serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali kuwasogezea huduma ya maji karibu kwa ajili ya mifugo yao kwa kuwa maji ni shida katika baadhi ya maeneo ya wilaya hiyo.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amehitimisha ziara ya kikazi ya siku tatu katika Mkoa wa Tanga ambapo amekagua na kushuhudia maendeleo ya miradi mbalimbali ya sekta za mifugo na uvuvi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), (katikati) akikagua maendeleo ya ujenzi wa bwawa la kunyweshea mifugo maji la Kwekinkwembe lililopo katika Wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga huku akimtaka mkandarasi kukamilisha ujenzi kwa wakati na kuwashirikisha viongozi wa eneo hilo. (17.02.2023)

Muonekano wa juu wa maendeleo ya ujenzi wa bwawa la kunyweshea mifugo maji la Kwekinkwembe lililopo katika Wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga ambapo ni moja mabwawa yanayojengwa maeneo mbalimbali nchini yatakayogharimu Shilingi Bilioni 6.2. (17.02.2023)

ULEGA: MSOMERA YAZIDI KUNG’ARA MIRADI YA WAFUGAJI YAPAA

Na. Edward Kondela


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amesema anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo serikali inahakikisha kila sekta inafikiwa katika maendeleo wakiwemo wafugaji na wavuvi.


Naibu Waziri Ulega amebainisha hayo (16.12.2023) wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Kijiji cha Msomera kilichopo Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga, kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali inayowahusu wafugaji, yakiwemo mabwawa ya maji, minada ya mifugo, majosho na malambo ili kusogeza huduma karibu kwa wakazi wa kijiji hicho.


Amesema mbali na wafugaji ambao serikali imekuwa ikiwafikia kwa kuwapatia huduma mbalimbali za miundombinu kwa ajili ya shughuli za mifugo, wavuvi na wafugaji wa samaki pia wanafikiwa.


“Hakuna lililosimama yote yanasonga mbele makandarasi waendelee kushirikisha vyema wenyeji ambao wanajua mazingira ya hapa na wenyeji kushirikiana na makandarasi na wenyewe kuwashirikisha viongozi kila hatua.” Amesema Mhe. Ulega


Ameongeza kuwa anaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa imetenga fedha Shilingi kwa mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji kwa wafugaji, ikiwemo minada takriban Shilingi Bilioni 5.9 kwa ajili ya kujenga minada mipya na kukarabati ya zamani na Shilingi Bilioni 5.9 kwa ajili ya kutengeneza majosho.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe. Albert Msando akitoa taarifa ya wilaya kwenye kikao cha Kijiji cha Msomera ambacho Naibu Waziri Ulega alikuwa mgeni rasmi, amesema hadi sasa serikali imeshajenga majosho saba kwa ajili ya kuoshea mifugo, miradi kwa ajili ya malisho ya mifugo ambapo maandalizi yamekamilika yakiwemo ya upatikanaji wa mbegu.


Mhe. Msando ameongeza kuwa idadi ya mifugo iliyopo katika kijiji hicho ni mingi kuliko idadi ya wakazi wake ambapo inafikia zaidi ya 86,234 ikiwemo ng’ombe 28,049 mbuzi 32,743 kondoo 24,795 na punda 647.


Nao baadhi ya wanakijiji cha Msomera katika kikao hicho walipata fursa ya kutoa maoni na maswali kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) ambapo moja ya maoni yao ni kuwepo kwa vikundi vinavyojumuisha wanakijiji hao ili wapatiwe mashamba darasa na ng’ombe wa maziwa ili wafuge kisasa, ambapo Naibu waziri Ulega ameielekeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) kufika katika kijiji hicho na kutoa elimu juu ya mikopo kwa wafugaji hao ili waweze kufuga kwa tija na kibiashara kwa kuwa wana makazi ya kudumu.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) yuko Mkoani Tanga kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kujionea namna maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya sekta za mifugo na uvuvi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akiendesha trekta mara baada ya kufika katika moja ya mashamba darasa ya malisho ya mifugo kwenye Kijiji cha Msomera Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga, katika ziara yake ya siku moja kwenye wilaya hiyo.  (16.02.2023)

BI. MWANGISA AFUNGA KIKAO CHA UZINDUZI WA MATAWI YA WANAWAKE WANAOJIHUSISHA NA SHUGHULI ZA UVUVI TANZANIA

 

Mkurugenzi msaidizi wa utawala na rasilimali watu Sekta ya uvuvi, Bi. Marry Mwangisa akitoa neno wakati wa kufunga kikao cha uzinduzi wa matawi ya wanawake wanaojihusisha na shughuli za uvuvi Tanzania (TAWFA) Kanda ya ziwa Nyasa na maji madogo kwa wanawake hao (hawapo pichani) na kuwahasa kushikamana na kuunda vikundi vitakavyowasaidia kujikwamua kiuchumi Mkoani Iringa Februari 16,2023

Mratibu wa mwongozo wa  Mradi wa kuendeleza Uvuvi mdogo Bi. Lilian Ibengwe akiwapongeza wanawake kwa ushiriki wao (hawapo pichani) na kuwasihi kuzingatia yale yote waliyoelimishwa  wakati wa  kikao cha kufunga  uzinduzi wa matawi ya TAWFA Kanda ya Ziwa Nyasa na maji madogo kilichofanyika kwenye ukumbi wa royal palm Mkoani Iringa, Februari 16,2023

Viongizi wa wanawake wanaojihusisha na shughuli za uvuvi Tanzania (TAWFA) Kanda ya ziwa Nyasa (picha ya juu) na viongizi wa maji madogo (picha ya chini) wakiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa NTT pamoja na watendaji kutoka Sekta uvuvi mara baada ya uchaguzi wa viongizi hao uliofanyika kwenye ukumbi wa royal palm Mkoani Iringa Februari 16,2023

SERIKALI KUTUMIA BILIONI 1.8 KWA AJILI YA MASHAMBA DARASA YA UFUGAJI SAMAKI

Serikali  ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt.Rais, Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewezesha Halmashauri kumi na nne (14) kwa kutoa fedha kiasi cha Tsh 1.8 Bilioni kwa ajili ya kujenga miradi ya mashamba darasa ya Ufugaji Samaki.


Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe maji, kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Eng.George Kwandu (16.02.2023) alipoenda kukagua moja ya miradi hiyo uliopo Kijiji cha Tubugwe,kata ya Chamkoroma, Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma.


Eng. Kwandu amesema mradi huo wa  kijiji cha Tubugwe umegharimu kiasi cha Tsh 128 milioni, kwa lengo la kuwasaidia vijana na wanawake nchini ambapo itaobgeza ajira kwa vijana, kuongeza kipato na kuongeza usalama wa chakula.


Aidha, Eng kwandu  amesema mradi huo unatakiwa kutekelezwa katika kipindi cha miezi mitatu, ambapo kutakuwa na Ujenzi wa mabwawa manne ambayo kwa kila moja ina mita za mraba 600, mfeleji wa kupitishia maji, ofisi na jengo la kufundishia ufugaji samaki.


 "Tunamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha mradi huu, na kwa niaba ya katibu Mkuu Uvuvi niwaombe wanufaika muulinde mradi huu", amesema Eng. Kwandu.


Pia, ameongezea kwa kusema mradi huo unasimamiwa na Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, ambapo matarajio ya wizara mradi utakapo kamilika utawezesha wakulima Mia moja (100) kila wilaya.


Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Tubugwe Kibaoni, Bw. Noel Makubi, amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan  kwa kuona vyema kuleta mabwawa ya shamba darasa katika kijiji hicho ambapo wanakijiji watapata fursa kama ajira na kujiongezea kipato.


Pia, Makubi amemshukuru Mkurugenzi wa Uvuvi kwa kushirikiana nao vizuri kwakufika eneo la mradi huo na kufuatilia Miundombinu ya kuleta maji na kuhakikisha mradi unaenda sawa.


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Dkt. Omary Nkulo(wa pili kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe maji Eng.GeorgeKwandu(wa pili kulia), wakati alipoenda kutembelea ofisini kwake na kumuelezea lengo la ujio huo ambapo ni kukagua mradi wa ujenzi wa mabwawa ya kufugia samaki kwa ajili ya Shamba darasa la ufugaji bora wa samaki katika kijiji cha Tubugwe kilichopo kata ya Chamkoroma, Wilayani hapo. Leo (16.02.2023.) na kushoto ni Afisa Uvuvi Mwandamizi Bw. John Mapunda.

Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe maji, Eng. George Kwandu (wapili kulia) akikagua cements ambazo zitatumika kujenga mradi wa mabwawa ya kufugia samaki kwa ajili ya Shamba darasa la ufugaji bora wa samaki, wakati alipoenda kutembelea mradi huo uliopo kijiji cha  Tubugwe, kata ya Chamkoroma, Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, (kushoto) ni  Afisa Uvuvi mwandamizi Bw. John Mapunda.16.02.2023.

Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe maji, Eng. George Kwandu (wapili kulia) akichukua vipimo vya mfeleji ambao utatumika kuchukulia maji na kupeleka kwenye mradi wa mabwawa ya kufugia samaki kwa ajili ya Shamba darasa la ufugaji bora wa samaki katika kijiji cha Tubugwe kilichopo kata ya Chamkoroma, Wilaya ya Kongwa. (16.02.2023)

Afisa Uvuvi mwandamizi Bw. John Mapunda (watatu kushoto) akielezea namna ya bwawa bora la kufugia samaki linavyopaswa kuwa na kuwaelezea mafundi wa ujenzi, sehemu ya kutolea maji inatakiwa iwe na kimo gani kitaalamu, wakati walipoenda kutembelea mradi wa ujenzi wa mabwawa ya kufugia samaki ambapo mradi huo utagharimu kiasi cha Tsh 128 milioni, katika kijiji cha Tubugwe kilichopo, Wilaya ya Kongwa. (16.02.2023).

MAONO YA DKT. SAMIA YAWAVUTIA VIJANA KUJIAJIRI KWENYE UFUGAJI

Na. Edward Kondela


Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeamua kukuza sekta ya mifugo kupitia unenepeshaji wa mifugo ili wananchi waweze kufuga kibiashara na kwa tija zaidi.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amebainisha hayo (15.02.2023) Mkoani Tanga, wakati alipotembelea vijana waliojiunga kwenye vituo atamizi vilivyopo Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) na Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) ili kupata mafunzo ya vitendo ya ufugaji kibiashara na unenepeshaji bora wa mifugo.


Mhe. Ulega amefafanua kuwa kupitia dira na maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia, serikali imeonelea kuichangamsha Sekta ya Mifugo, kupitia unenepeshaji na ufugaji wenye tija hivyo wizara kuja na programu ya Samia Ufugaji kwa Tija (SAUTI).                                                   


“Tunataka kutengeneza matokeo chanya kwa vijana katika maendeleo yao Rais Dkt. Samia anataka vijana wachakarikaji, wenye kasi ya maendeleo.” Amesema Mhe. Ulega 


Nao baadhi ya vijana ambao wanapata mafunzo hayo wamemwambia Naibu Waziri Ulega kuwa wamejiwekea mikakati ya kufanya ufugaji wenye tija mara wakapomaliza mafunzo yao ambayo yanadumu kwa mwaka mmoja.


Wamebainisha kuwa ni wakati wao saa kufikiria kujiajiri na hata kutoa mafunzo kwa wafugaji wengine wa asili ili wafuge kisasa na kuingia katika biashara ya unenepeshaji wa mifugo


Programu ya SAUTI ambayo imeanzishwa kutokana na maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyotoa wakati wa kuhitimisha sherehe za wakulima (Nanenane) Mwaka 2022, imelenga kuwabadilisha vijana kifikra kwa kuwapatia mbinu mbalimbali za ufugaji wa kisasa na kibiashara ikiwa ni pamoja na kuwaonyesha fursa zilizopo kupitia Sekta ya Mifugo.    

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvui Mhe. Abdallah Ulega (Mb (wa tatu kushoto) akizungumza na vijana waliojiunga mafunzo ya vitendo ya ufugaji kwa tija na biashara na kunenepesha mifugo, kwenye Kituo Atamizi kilichopo Wakala ya Elimu ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) Mkoani Tanga, kupitia programu ya Samia Ufugaji kwa Tija (SAUTI). (15.02.2023)

DKT. SAMIA AMWAGA MABILIONI KUINUA FURSA ZA UCHUMI WA BULUU.

Na. Edward Kondela


Serikali imeendelea kutekeleza bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 katika uwekezaji wa uchumi wa buluu kupitia maji ya Bahari ya Hindi, maziwa na mito ikiwemo kuhamasisha ufugaji wa viumbe maji.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amebainisha hayo (15.02.2023) wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi Mkoani Tanga ambapo katika siku ya kwanza ya ziara hiyo, kwenye Sekta ya Uvuvi ametembelea vikundi vya ushirika vya ukuzaji viumbe maji vya Jifute kinachonenepesha kaa pamoja na Mondura na Mchukuuni vinavyojishughulisha na ufugaji wa tango bahari ama kwa jina lingine la zamani jongoo bahari pamoja na ukulima wa mwani.


Ili kukuza uchumi wa buluu, Naibu Waziri Ulega amesema serikali imeweka Shilingi Bilioni 2.5 kwa ajili ya kuendeleza zao la mwani ambapo tayari Shilingi Milioni 447 zimeshatolewa kwa vikundi mbalimbali, Shilingi Bilioni 11.5 zimetengwa kwa ajili ya kutengeneza boti za kisasa za uvuvi na Shilingi Bilioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa vizimba vya kufugia samaki aina ya sato kwenye Ziwa Victoria.


Mhe. Ulega amesema serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejizatiti kuinua uchumi wa buluu kwa kutenga fedha nyingi huku wadau mbalimbali wa sekta hiyo wakikaribishwa kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia kuweka mazingira mazuri ya ukuzaji viumbe maji.


Aidha, amewataka wadau wa Sekta ya Uvuvi hususan vikundi vya ushirika vya wavuvi kuchangamkia fursa ambayo serikali imetoa fedha ili kuongeza mahitaji ya ukuzaji viumbe maji kutokana na masoko yaliyopo ndani na nje ya nchi.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Pangani Mhe. Zainabu Abdallah amesema anafurahishwa na namna Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inavyoweka juhudi za kuwasaidia vijana katika uwekezaji kwenye viumbe maji kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kutaka uwekezaji wa kisasa kwa kuongeza mnyoyoro wa thamani, huku akibainisha kuwa wilaya yake iko tayari kutenga maeneo mengi zaidi kwa ajili ya shughuli za ukuzaji viumbe maji.


Akisoma risala ya kikundi cha ushirika cha kilimo cha mwani na ufugaji tango bahari cha Mchukuuni kilichopo jijini Tanga, Bw. Abdallah Mtondo amelalamikia kitendo cha baadhi ya watu ambao siyo waaminifu kuiba matango bahari katika mashamba yao hususan nyakati ambapo maji yamefunika mashamba hayo.


Kutokana na hali hiyo wameiomba serikali kuwachukulia hatua za kisheria watu hao ambao wamekuwa wakiwarudisha nyuma katika shughuli za ufugaji ili kujiongezea tija jambo ambalo Naibu Waziri Ulega amelitolea kauli kali na kutaka mamlaka husika kuingilia kati jambo hilo huku akisisitiza wanunuzi wa mwani na tango bahari kununua mazao hayo kwenye vikundi vinavyotambulika na kusajiliwa.


Awali kabla ya kuanza ziara ya kikazi Mkoani Tanga, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amefika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Omary Mgumba na kufanya naye mazungumzo juu ya namna serikali kupitia wizara hiyo inavyofanya jitihda mbalimbali za kufungua fursa kwa wadau wa sekta za mifugo na uvuvi kwa kufuga na kuuza mazao yanayotoka katika sekta hizo.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), (wa nne kushoto) akiwa kwenye boti ya uvuvi iliyopewa jina la Mv. Blue Economy na kubainisha mambo kadhaa juu ya uwekezaji wa serikali kwenye Uchumi wa Buluu, mara baada ya kutembelea kikundi cha ushirika cha Mchukuuni kilichopo jijini Tanga ambacho kinajishughulisha na kilimo cha mwani na ufugaji tango bahari ama jina lingine la zamani jongoo bahari. (15.02.2023)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), (wa kwanza kushoto) akiwa kwenye kikundi cha ushirika cha unenepeshaji kaa kiitwacho Jifute kilichopo Wilaya ya Pangani, Mkoani Tanga kujionea namna wanavyojishughulisha na unenepeshaji wa kaa hao pamoja na vizimba vilivyojengwa mahsusi kwa ajili ya kufuga kaa 600 kwa wakati mmoja. (15.02.2023)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), (aliyesimama) akiwa kwenye mazungumzo mara baada ya kufika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Omary Mgumba (aliyekaa), kabla ya Naibu Waziri Ulega kuanza ziara ya kikazi mkoani humo. (15.02.2023)

KIKOSI KAZI KINACHORATIBU MWONGOZO WA KUENDELEZA UVUVI MDOGO NCHINI KIKIENDELEA NA KIKAO CHA KUZINDUA MATAWI YA WANAWAKE

 

Mwenyekiti wa kikosi kazi cha kitaifa kinachoratibu muongozo wa kuendeleza Uvuvi Mdogo nchini (NTT), Bw. Yahya Mgawe akiwasilisha mada wakati wa kikao cha uzinduzi wa matawi ya wanawake wanaojihusisha na shughuli za uvuvi Tanzania (TAWFA) Kanda ya ziwa Nyasa na maji madogo   kilichofanyika kwenye ukumbi wa royal palm Mkoani Iringa Februari 15,2023

Afisa Uvuvi Mwandamizi ambaye pia ni mratibu wa dawati la jinsia kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Bi. Upendo hamidu akichangia hoja wakati wa kikao cha uzinduzi wa matawi ya TAWFA Kanda ya ziwa Nyasa na maji madogo kilichofanyika kwenye ukumbi wa royal palm Mkoani Iringa Februari 15,2023

Mteknolojia wa samaki Mkuu, Bi. Flora Ruhanga akichangia hoja kwenye kikao cha uzinduzi wa matawi ya wanawake wanaojihusisha na shughuli za uvuvi Tanzania (TAWFA) Kanda ya ziwa Nyasa na maji madogo kilichofanyika kwenye ukumbi wa royal palm Mkoani Iringa Februari 15,2023

Mjumbe wa kikosi kazi cha kitaifa kinachoratibu muongozo wa kuendeleza Uvuvi Mdogo nchini (NTT), Bi. Leticia Bigeyo akifafanua jambo kwenye kikao cha uzinduzi wa matawi ya wanawake wanaojihusisha na shughuli za uvuvi Tanzania (TAWFA) Kanda ya ziwa Nyasa na maji madogo   kilichofanyika kwenye ukumbi wa royal palm Mkoani Iringa Februari 15,2023

Sehemu ya washiriki wa kikao cha uzinduzi wa matawi ya wanawake wanaojihusisha na shughuli za uvuvi Tanzania (TAWFA) Kanda ya ziwa Nyasa na maji madogo wakichangia hoja na kujibu waswali wakati wa kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa royal palm Mkoani Iringa Februari 15,2023

Mratibu wa mwongozo wa  Mradi wa kuendeleza Uvuvi mdogo Bi. Lilian Ibengwe akijibu maswali wakati wa kikao cha uzinduzi wa matawi ya TAWFA Kanda ya Ziwa Nyasa na maji madogo kilichofanyika kwenye ukumbi wa royal palm Mkoani Iringa, Februari 15,2023

Jumatatu, 20 Februari 2023

SERIKALI, WADAU KUIMARISHA USALAMA WA WAVUVI ZIWA VICTORIA

Na Mbaraka Kambona, Dodoma


Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Utunzaji wa Rasilimali za Uvuvi (EMEDO) chini ya Ufadhili wa Shirika la Royal National Lifeboat Institution(RNLI) linalojishughulisha na usalama kwenye maji na uokozi wanatekeleza mradi wa kuzuia wavuvi kuzama majini na kuhakikisha wanakuwa salama wakati wote wa shughuli zao katika Ziwa Victoria.


Mradi huo wa miaka 3 kuanzia 2022/2025 umelenga kuwaelimisha wavuvi hatua mbambali za kuchukua za kujizuia kuzama majini kabla ya kuingia kazini, lakini pia mradi utajikita katika kutoa mafunzo mbalimbali kwa jamii na wavuvi, BMU na watalamu wengine wa serikali wanaofanya kazi na wavuvi.


Pia, Mradi utashirikiana kwa karibu na taasisi za serikali zinazohusika moja kwa moja kwenye suala la usalama kwenye maji .


Lengo kuu la mradi huo ni kuhakikisha kuwa wadau wote wa sekta ya uvuvi kwa pamoja wanashirikiana kuchukua hatua mbalimbali za kuzuia matukio ya kuzama kwa wavuvi na wanakuwa salama wakiwa katika shughuli zao za kila siku.


Kwa mujibu wa Mkuu wa Programu wa shirika la RNLI nchini Tanzania, Rachel Roland, mwaka 2019 walifanya utafiti kuhusu usalama wa jamii za wavuvi wanaoishi kandokando ya ziwa viktoria  na walibaini kuwa asilimia 84 ya vifo vya wavuvi vinatokea wakiwa katika shughuli zao za kila siku za uvuvi katika ziwa.


Hivyo, mwaka 2022 RNLI na EMEDO walizindua mradi unaoitwa “Lake Victoria Drowning Prevention Project” kwa lengo la kufuatilia visa hatarishi vinavyochangia kusababisha kuzama kwa wavuvi katika ziwa hilo na kuchukua hatua za kupunguza vifo huku kauli mbiu ikiwa ni "Kuzama Kunazuilika, Chukua Tahadhari".


Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu(Sekta ya Uvuvi), Bw. Stephen Lukanga alisema kuwa mradi huo ni muhimu kwa ustawi wa maisha ya jamii za wavuvi hivyo utekelezaji wake unahitaji ushirikiano wa karibu baina ya serikali na wadau  katika kila hatua ili kuwe na uelewa wa pamoja wakati wote.


RNLI ni shirika la kimataifa lililoanzishwa mwaka 1824 kwa ajili ya kusaidia kuokoa maisha ya jamii zinazoishi kandokando ya bahari na ziwa nchini Uingereza na Ireland, lakini kwa sasa wamepanua wigo na kufanya kazi katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu (Sekta ya Uvuvi), Bw. Stephen Lukanga akisisitiza jambo wakati wa kikao cha  kuwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Mradi wa Lake Victoria Drowning Prevention Project katika kikao kilichowahusisha Wataalam kutoka Sekta ya Uvuvi na Wataalam kutoka Shirika la EMEDO na Shirika la RNLi kilichofanyika Mtumba, jijini Dodoma Februari 15, 2023.

Mkuu wa Programu wa Shirika la RNLI nchini Tanzania, Rachel Roland akitoa maelezo mafupi kuhusu shughughuli za shirika hilo muda mfupi kabla ya kuwasilisha taarifa yao ya Utekelezaji wa Mradi wa Lake Victoria Drowning Prevention Project katika kikao kilichowahusisha wao na Wataalam kutoka Sekta ya Uvuvi kilichofanyika Mtumba, jijini Dodoma Februari 15, 2023.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu(Sekta ya Uvuvi), Bw. Stephen Lukanga(wa pili kutoka kushoto mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa kikao cha kuwasilisha taarifa  ya Utekelezaji wa Mradi wa Lake Victoria Drowning Prevention Project kilichofanyika Mtumba jijini Dodoma Februari 15, 2023. Wa kwanza kushoto mstari wa mbele ni Mkuu wa Programu wa Shirika la RNLI nchini Tanzania, Rachel Roland na kulia ni Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Utunzaji wa Rasilimali za Uvuvi (EMEDO), Madam Editrudith.

SEKTA YA UVUVI YAZINDUA MATAWI YA TAWFA KANDA YA ZIWA NYASA NA MAJI MADOGO

 


Kaimu Mkurugenzi wa Uvuvi Bw. Stephen Lukanga akisoma Hotuba kwa Niaba ya Katibu Mkuu Sekta ya uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah wakati wa uzinduzi wa matawi ya TAWFA Kanda ya ziwa Nyasa na maji madogo kilichofanyika kwenye ukumbi wa royal palm Mkoani Iringa Februari 14,2023 lengo likiwa ni pamoja na kuwaunganisha wanawake wa  Tanzania nzima kupitia vikundi vyao Ili kuwezesha kuwa na sauti ya pamoja, kubadilishana mawazo na uzoefu katika kupata uhakika wa masoko.

Mkurugenzi msaidizi wa utawala na rasilimali watu Sekta ya uvuvi, Bi. Marry Mwagisa akitoa neno kwa wanawake wanaojihusisha na shughuli za uvuvi (hawapo pichani) wakati wa kikao cha uzinduzi wa matawi ya TAWFA Kanda ya ziwa Nyasa na maji madogo kilichofanyika kwenye ukumbi wa royal palm Mkoani Iringa Februari 14,2023

Mwenyekiti wa kikosi kazi cha kitaifa kinachoratibu muongozo wa kuendeleza Uvuvi Mdogo nchini (NTT), Bw. Yahya Mgawe akiongea na wanawake wanaojihusisha na shughuli za uvuvi Tanzania (TAWFA) wakati wa kikao cha uzinduzi wa matawi hayo Kanda ya ziwa Nyasa na maji madogo (hawapo pichani) kilichofanyika kwenye ukumbi wa royal palm Mkoani Iringa Februari 14,2023

Mwenyekiti wa TAWFA, Bi. Beatrice Mmbaga akieleza maana ya TAWFA na lengo lake hasa kwa wanawake (hawapo pichani)  wakati wa kikao cha uzinduzi wa matawi ya wanawake wanaojihusisha na shughuli za uvuvi Tanzania (TAWFA) Kanda ya ziwa Nyasa na maji madogo kilichofanyika kwenye ukumbi wa royal palm Mkoani Iringa Februari 14,2023

Afisa Uvuvi Mwandamizi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Bi. Upendo hamidu akiwasilisha mada kwa wanawake wanaojihusisha na shughuli za Uvuvi wakati wa kikao cha uzinduzi wa matawi ya TAWFA Kanda ya ziwa Nyasa na maji madogo kilichofanyika kwenye ukumbi wa royal palm Mkoani Iringa Februari 14,2023

Kaimu Mkurugenzi wa Uvuvi Bw. Stephen Lukanga (waliokaa katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa kikao cha uzinduzi wa matawi ya TAWFA Kanda ya ziwa Nyasa na maji madogo mara baada ya uzinduzi huo uliofanyika kwenye ukumbi wa royal palm Mkoani Iringa Februari 14,2023

Mratibu wa Mradi wa small Scale fisheries Guidelines Bi. Lilian Ibengwe akiwasilisha mada wakati wa kikao cha uzinduzi wa matawi ya TAWFA Kanda ya Ziwa Nyasa na maji madogo kilichofanyika kwenye ukumbi wa royal palm Mkoani Iringa, Februari 14,2023

WATAFITI NA WANASAYANSI KUTOKA NCHI 18 DUNIANI WAKUTANA JIJINI ARUSHA

WATAFITI na wanasayansi kutoka nchini 18 duniani, wamekutana jijini  Arusha kutafuta ufumbuzi wa kutokomeza ugonjwa wa  Ndorobo unaoenezwa na Mbung’o ambao umekuwa tishio kwa wanyama na binadamu kwa nchi za Afrika ikiwemo Tanzania.

Akiongea kwenye mkutano huo jana Jijini Arusha Mkurugenzi wa huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga alisema watafiti hao watakuja na jibu la pamoja la namna ya kutokomeza ugonjwa huo unaotishia soko la Nyama kimataifa.

Amesisitiza kuwa uwepo wa ugonjwa wa Ndorobo, Afrika inapata hasara ya takribani dola za kimarekani bilioni 1.2 kutokana na gharama za matibabu na mifugo kukataliwa kuchinjwa .

Amesema Tanzania imefanikiwa kudhibiti ugonjwa huo kwa kiasi kikubwa ambapo hadi sasa upo chini ya asilimia 1.5, lakini jitihada zaidi zinahitajika ili kuutokomeza kutokana na mbung’o wengi kuwepo maeneo yaliyo jirani na misitu na hifadhi za wanyama pori na hivyo kusababisha mifugo mingi kukondeana na hatimaye kufa kutokana na vimelea wanavyoambukizwa na Mbung’o. 

“Ng’ombe anapougua ugonjwa huo hukondeana kwa muda mrefu, afya yake huwa mbovu na hivyo hushindwa kuzalisha na nyama yake huwa mbovu haifai kuliwa na binadamu ndio maana watafiti wamekutana ili kubadilishana uzoefu ili kupata njia bora ya kutokomeza ugonjwa huo” amesema

Prof. Nonga amesema kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikifanya jitihada kubwa ya kupambana na ugonjwa huo kupitia majosho ya uogeshaji mifugo zaidi ya 3000 yaliyopo nchi nzima ili kuua wadudu kupe na mbung’o.

“Serikali imekuwa ikinunua dawa za kuogesha mifugo na kuzitoa kwa wafugaji ili wakaogeshe mifugo yao na kutokomeza magonjwa yaenezwayo na Mbung’o, Kupe na Mbu anayesambaza ugonjwa wa homa ya bonde la ufa” amesema Prof Nonga.

Aidha amesema hapa nchini kuna viwanda vya nyama zaidi ya 10 vinavyohitaji kuzalisha nyama iliyobora ili kuuza nje ya nchi, lakini vimeshindwa kukidhi mahitaji ya soko kutokana na changamoto ya nyama kunakosababishwa na ugonjwa wa mbung’o.

Ameongeza kuwa, pamoja na mambo mengine mkutano huo utakuja na majibu juu ya ufugaji bora wenye tija utakaokuwa na manufaa kwa mfugaji kuweza kutajirika na mifugo yake. Alitoa wito kwa wafugaji kuwatumia wataalamu wa mifugo pindi wanapoona uwepo wa dalili za magonjwa hayo.

Naye Dkt. Furaha Mramba ambaye ni mtafiti kiongozi kupitia mradi wa kudhibiti ugonjwa wa Ndorobo kwa njia ya kutumia dawa Tanzania, amesema kuwa wamefanikiwa kugundua aina saba za Ndorobo wenye uwezo wa kusambaza ugonjwa kwa mifugo na binadamu.

Dkt. Mramba ambaye pia ni Mkurugenzi wa kampuni ya kuzalisha chanjo za wanyama Tanzania, amesema maeneo ya uhifadhi wa wanyama pori ndio yenye Ndorobo wengi na hivyo aliwashauri wafugaji kuhakikisha wanafuata ushauri wanaopewa na wataalam wa mifugo ikiwa ni pamoja na uogeshaji mifugo ili pale wanapolisha maeneo jirani na hifadhi za Wanyama pori mifugo isiweze kuathiriwa na magonjwa hayo.

Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo, Prof. Hezron Nonga akifungua mkutano uliowakutanisha watafiti wa mifugo Africa kujadili namna ya kudhibiti ugonjwa wa Ndorobo kwa kutumia dawa ambao umefanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Mount Meru Jijini Arusha. (14.02.2022)


Mtafiti kiongozi wa Mradi wa kudhibiti ugonjwa wa ndorobo kwa njia ya dawa Tanzania, Dkt. Furaha Mramba akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua mkutano uliowakutanisha watafiti wa mifugo Africa kujadili namna ya kudhibiti ugonjwa wa Ndorobo kwa kutumia dawa ambao umefanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Mount Meru Jijini Arusha. (14.02.2022)

Baadhi ya washiriki wa mkutano uliowakutanisha watafiti wa mifugon Africa kujadili namna ya kudhibiti ugonjwa wa Ndorobo kwa kutumia dawa wakifuatilia mada zilizokuwa zinawasilishwa. Mkutano huo umefanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Mount Meru Jijini Arusha. (14.02.2022)


SEKTA YA MIFUGO YAENDELEA KUTOA MBEGU ZA MALISHO KWA WAFUGAJI

 

Wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakishirikiana na mmoja wa wafugaji (katikati) kupima katika mzani kiasi cha mbegu kwa ajili ya kuziandaa ili zipandwe katika shamba la mfugaji lililopo katika Kata ya Itiso, Wilayani Chamwino, Mkoani Dodoma Februari 14, 2023.

Sehemu ya Wafugaji na Viongozi wa Kata ya Itiso, Wilayani Chamwino, Mkoani Dodoma wakishiriki katika zoezi la upandaji wa malisho ya mifugo baada ya kupatiwa mafunzo na wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhusu umuhimu wa kupanda malisho kwa ajili ya mifugo yao. Elimu hiyo ilitolewa Februari 14, 2023.

Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho na Rasilimali ya Vyakula vya Wanyama, Dkt. Asimwe Rwiguza (kushoto) akiongea na wafugaji wa Kata ya Itiso, Wilayani Chamwino, Mkoani Dodoma Februari 14, 2023 alipowatembelea kwa lengo la kuwahamasisha kuhusu ulimaji wa malisho ili waondokane na utegemezi wa malisho ya asili jambo ambalo limekuwa  likipelekea migogoro kati yao na watumiaji wengine wa Ardhi.

Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho na Rasilimali ya Vyakula vya Wanyama, Dkt. Asimwe Rwiguza akishirikiana na wafugaji wa Kata ya Itiso, Wilayani Chamwino, Mkoani Dodoma kupanda malisho ya mifugo katika shamba la mmoja wa wafugaji wa Kata hiyo alipowatembelea Februari 14, 2023 kwa lengo la kuwahamasisha kuhusu ulimaji wa malisho ili waondokane na utegemezi wa malisho ya asili jambo ambalo limekuwa  likipelekea migogoro kati yao na watumiaji wengine wa Ardhi.

KIKAO CHA MPANGO WA UNYWAJI MAZIWA SHULENI CHAFANYIKA JIJINI DODOMA

 

Msajili wa Bodi ya Maziwa Nchini, Dkt. George Msalya(aliyesimama) akiongea neno la utangulizi kuhusu mpango wa unywaji maziwa shuleni kabla ya kumkaribisha Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko, Bw. Steve Michael (wakatikati) kwenye kikao cha kupitia Rasimu ya mpango wa unywaji maziwa shuleni, kilichofanyika Februari 14,2023, Ukumbi wa Royal Village, Dodoma. (Kulia) ni Afisa Tawala Mkuu, John Kusaja.

Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko, Bw.Steve Michael (wakatikati) akiongea jambo kwenye kikao cha kupitia Rasimu ya mpango wa unywaji maziwa shuleni, kuhusu namna bora ya kuweka mikakati muhimu ya kusaidia unywaji maziwa mashuleni ili kufikia malengo katika tasnia ya maziwa. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Royal Village, Dodoma 14 Februari 2023, (Kushoto) ni Msajili wa Bodi ya Maziwa Nchini, Dkt. George Msalya na (kulia) ni Afisa Tawala Mkuu,Bw. John Kusaja.

Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko, Bw. Steve Michael (waliokaa katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe waliohudhuria kikao cha kupitia Rasimu ya mpango wa unywaji maziwa shuleni, kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Royal Village. Dodoma, 14 Februari 2023.

Wajumbe wa kikao cha kupitia Rasimu ya mpango wa unywaji maziwa shuleni, wakiwa katika makundi kwa ajili ya kujadiliana na kuboresha Rasimu ya mpango wa unywaji maziwa shuleni na kutoa mawasilisho ya maboresho waliyoyafanya kwa kila kikundi, kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Royal Village,Dodoma Februari 14,2023.

Sehemu ya wajumbe waliohudhuria kikao cha kupitia Rasimu ya mpango wa unywaji maziwa shuleni wakiendelea na majadiliano kuhusu wasilisho la  rasimu ya mpango wa unywaji maziwa shuleni, kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Royal Village, Dodoma, Februari 14,2023.


Afisa Mifugo kutoka Idara ya Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko, Bw. Edson Kilyenyi akiwasilisha mpango wa Unywaji maziwa shuleni kwa wajumbe waliohudhuria kwenye kikao cha kupitia Rasimu ya mpango wa unywaji maziwa mashuleni, katika ukumbi wa Royal Village, Dodoma Februari 14,2023.