Taasisi za kifedha nchini zimehimizwa kutoa mikopo kwa wavuvi na wafanyabiashara wa dagaa kwa kuwa zao hilo lina tija kiafya na kiuchumi.
Hayo yamesemwa leo (26.11.2021) na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega wakati alipotembelea mwalo wa Igombe wilayani Ilemela mkoa wa Mwanza baada ya kufika kwenye moja ya banda linalotumika kukaangia dagaa na kukutana na wafanyabiashara hao.
Naibu Waziri Ulega amesema kuwa umefika wakati wa taasisi za kifedha pamoja na Halmashauri kuanza kuliangalia kundi hilo ambalo likiwezeshwa litaweza kuwahakikishia watanzania kuondokana na utapiamlo lakini pia kuongeza kipato kwa wahusika na taifa kwa ujumla.
“Dagaa ni zao la kimkakati kutokana na umuhimu wake kiafya na kiuchumi ndio maana tunaendelea kuzihamasisha taasisi za kifedha kuwakopesha wavuvi na wafanyabiashara wa dagaa ili waweze kuvua dagaa wengi kwa kutumia zana za kisasa, kuwahifadhi katika mazingira mazuri na kusafirishwa katika maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi,” alisema Naibu Waziri Ulega
Halmashauri kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotokana na makusanyo ya mapato ya ndani zimeshauriwa kuanza kuliangalia kundi hilo linalojishughulisha na mnyororo wa thamani wa dagaa kwanza kwa kuwakopesha ili waweze kuboresha mazingira wanayofanyia kazi kuanzia kwenye utengenezaji wa vichanja kwa ajili ya kuanikia dagaa, kukaangia hadi kwenye maghala ya kuhifadhia.
Lakini pia Naibu Waziri Ulega amewasihi wafanyabiashara hao kuwa waaminifu hasa kwenye urejeshaji wa mikopo kwani kumekuwepo na tatizo la baadhi ya vikundi kusumbua kwenye urejeshaji wa mikopo waliyopatiwa. Vilevile amewataka kuzingatia ubora katika uandaaji wa dagaa hao ili wanapopelekwa sokoni kusiwe na tatizo lolote.
Pia amewataka wataalam kutoka katika Halmashauri kuwa jirani na wafanyabiashara hao ili wawasaidie katika kuwashauri namna ya kupanga mipango yao itakayowasaidia waweze kujinyanyua kiuchumi.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akionja dagaa waliokuwa wanakaangwa katika mwalo wa Igombe ambapo amezisihi taasisi za kifedha pamoja na Halmashauri kutoa mikopo kwa wafanyabiashara hao wa dagaa ili waweze kuboresha mazingira na mitaji yao kwa kuwa biashara hiyo inalipa. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe. Hassan Masala. (26.11.2021)
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akimuangali samaki aina ya sangara mwenye uzito zaidi ya kilo 40 wakati alipotembelea Kampuni ya Y & P inayozalisha barafu na kugandisha samaki Jijini Mwanza. Mhe. Ulega amewahimiza wamiliki wa Kampuni hiyo kuongeza kasi katika kukamilisha taratibu zilizobaki ili waanze kuchakata samaki. (26.11.2021)