Nav bar

Jumatano, 10 Novemba 2021

SERIKALI YAGAWA VIFARANGA 2600 KWA VIKUNDI VYA KINAMAMA MKURANGA

Katika jitihada za kuwakwamua kiuchumi wananchi hususan kinamama, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imegawa Vifaranga 2600 kwa  mashamba darasa mawili  katika kata ya Vikindu na Kimanzichana vilivyopo wilayani Mkuranga, mkoani Pwani.

Akizungumza mara baada ya kugawa vifaranga hivyo Novemba 9, 2021,  Kaimu Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Idara ya utafiti na  mafunzo, Dkt. Hassan  Mruttu  alisema vifaranga hivyo vitakaa katika mashamba hayo  kwa  wiki nne kabla ya kusambazwa katika vikundi 17 vya Wilaya hiyo.

Alisema   pamoja na kuwepo kwa vifaranga hivyo, pia vikundi hivyo vitapewa chakula cha kuvikuza  pamoja na wataalamu wa kusaidia ukuaji wa kuku katika Wilaya hiyo.

"Tumepokea vifaranga 2600, tumegawa katika mashamba darasa mawili  katika kikundi cha Kisawani na kikundi cha tujikomboe  hivi vitakaa hapa kwa wiki 4 na baadaye tutavisambaza kwa vikundi 17, ili kuwasaidia wakinamama kujikwamua kiuchumi," alisema Dkt. Mruttu

“Kuna tofauti kubwa kati ya mashamba ya mfano na mashamba darasa, hili ni shamba darasa, kwanzia Novemba 10, wataalamu watakuwa hapa na baada ya hapa tu nategemea wana kikundi wa vikundi hivi viwili mkawe waalimu kwa vikundi hivyo vingine 17,"alisema

Kwa upande wake Afisa mifugo na uvuvi wa Wilaya hiyo Bi. Anna Kiria aliwataka   wanakikundi kuongeza umakini katika kufuatilia mafunzo ili kuleta matokeo chanya katika uzalishaji.

" Vifaranga  hawa wanaitaji  usafi wa kutosha, umakini na kujitolea,   tutapewa mafunzo tuzingatie, na  mwisho tutapewa vyeti vitakavyotufanya na sisi kwenda kuwafundisha wenzetu," alisema Anna

 

Alisema halmashauri hiyo itafuatilia kwa ukaribu kuona kila mmoja anatimiza wajibu wake, na haitamvumlia mwana kikundi atakayekuwa sababu ya kukwamisha shughuli hiyo ya maendeleo.

Aidha mwenyekiti wa kikundi cha Kisawani kata ya Vikindu, Bi.Sintaweza  Omary, aliipongeza serikali ya awamu ya sita huku akiiomba kuongeza jitihada katika kuwasaidia wakinamama vijijini.

"Mradi huu utaenda kukuza uchumi wa wakinamama wa Mkuranga, hivyo tunamshukuru  Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hasan kwa kuwa kumbuka wakinamama na tunamuomba asichoke katika kuhakikisha wanajikwamua kupitia asilimia 10 zitolewazo katika halimashauri, "alisema


Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya utafiti na Mafunzo Dkt. Hassan Mruttu akiongea na wanakikundi wa kisawani (hawapo pichani) mara baada ya kuwasili kwa vifaranga kwa ajili ya mashamba darasa kwenye Wilaya ya mkuranga Mkoani Pwani  Novemba 09, 2021.

Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Mkuranga, Bi. Anna Kiria (kulia) akikabidhi vifaranga kwa mwenyekiti wa kikundi cha kisawani kata ya vikindu Wilaya ya Mkuranga Bi. Staweza Omary (kushoto) nyuma yao ni baadhi ya wanakikundi wa kisawani na watendaji kutoka Wizara ya Mifugo na uvuvi. Novemba 09, 2021.

Baadhi ya vifaranga vilivyowekwa kwenye Banda la kikundi cha kisawani kata ya Vikindu, Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani. Novemba 09, 2021


Katibu wa Mbunge wa jimbo la Mkuranga, Bi. Zuwena Mtulia (kushoto) akiweka maji kwenye vyombo vya kunywea maji vifaranga nje ya jengo la shamba darasa la  kikundi cha kisawani kata ya Vikindu Wilaya ya mkuranga mkoani Pwani, Novemba 09, 2021.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni