Nav bar

Alhamisi, 17 Julai 2025

DKT. MHEDE AHITIMISHA MKUTANO WA WADAU WA TASNIA YA KUKU

Na. Hamis Hussein

Naibu Katibu Mkuu  Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Edwin Mhede amehitimisha  mkutano wa wadau wa tasnia ya kuku ujulikanao  (National Poultry Delivery Lab), uliofanyika kwa siku mbili katika Hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam. 

Akizungumza leo Julai 16, 2025 katika hafla ya kufunga Mkutano huo Dkt. Mhede amesisitiza kuundwa haraka kwa kamati ndogo ya kiufundi itakayoratibu na kufuatilia maazimio ya mkutano huo na kuahidi kushirikiana nayo  ili kuhakikisha kuwa  Wizara kwa kushirikiana na wadau, inakamilisha na kuzindua  Mkakati wa Tasnia ya Kuku.

Aidha, Dkt. Mhede amewapongeza wadau wa tasnia ya kuku walivyobainisha na kujadili changamoto na fursa za tasnia hiyo na kutoa mikakati ya kuinua tasnia hiyo , ikiwa ni hatua muhimu ya kuanisha masuala ya kuzingatia katika uandaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Tasnia ya Kuku Nchini.

Katika hatua nyingine Dkt. Mhede amesisitiza kuongeza wigo wa ushiriki wa wadau wengine katika mnyororo wa thamani ili kuhakikisha masuala yote ya kimkakati yanaingia katika  mapendekezo hayo.



DKT. KIJAJI AKABIDHI BOTI ZA UVUVI ZENYE THAMANI YA BIL.2

Na. Omary Mtamike

◼️Ni sehemu ya Boti 120 zinazotolewa na Serikali kwenye awamu ya pili

◼️Wavuvi 205 kunufaika

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amekabidhi boti 13 za Uvuvi zenye thamani ya takribani shilingi Bil. 2 kwa Vikundi vya mikoa ya Pwani na Dar-es-salaam ambazo zinatarajiwa kuwanufaisha zaidi ya Wavuvi 205  wa mikoa hiyo.

Mhe. Dkt. Kijaji amekabidhi boti hizo Julai 16, 2025 kwenye ufukwe wa Shirika la Uvuvi nchini (TAFICO) ambapo mkoa wa Pwani umekabidhiwa Boti 8 huku mkoa wa Dar-es-Salaam ukikabidhiwa boti 5 zote jumla zikiwa na uretu wa mita 12 na 14 ambazo zinajumuisha vifaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Nyavu, kamba, maboya, nyuzi, kitafuta samaki na boti saidizi maarufu kama dingi.

“Boti mlizopokea leo zimefanyiwa maboresho yote yaliyotokana na maoni mliyotoa kutoka kwenye boti za awamu ya kwanza na sisi kama Serikali tunatamani kuona mnaendelea mnafanikiwa kupitia boti hizo” Ameongeza Mhe. Dkt. Kijaji

Aidha Mhe. Dkt. Kijaji amebainisha kuwa ugawaji wa boti hizo ni sehemu ya mkakati wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan uliolenga kuboresha sekta ya Uvuvi nchini ambapo wanufaika wanajumuisha makundi manne ambavyo ni watu binafsi, makampuni na vikundi vya Wavuvi.

“Boti hizi zimechangia ongezeko la idadi ya watu wanaonufaika kutokana na Sekta ya Uvuvi ambapo mpaka zaidi zaidi ya Watu Milioni 6 wanapata vipato vyao kupitia sekta hii hivyo niwaombe wote mliopatiwa mikopo hii muirejeshe kwa wakati ili tuwawezeshe na wengine kukopeshwa “ Amesema Mhe. Dkt. Kijaji.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-Salaam Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe. Mikaya Dalmia amesema kuwa awamu ya kwanza ya mkopo wa boti hizo za Uvuvi iliufanya mkoa huo kuvuna takribani tani 18892 za samaki hivyo aliwataka wanufaika wa awamu ya pili kutumia vema fursa hiyo ili wavune zaidi ya kiwango hicho cha awamu iliyopita.

Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Shaib Ndemanga mbali na kuishukuru Serikali kwa boti hizo zinazotolewa kwa mkopo wenye masharti nafuu, amesema kuwa zitaboresha maisha ya wananchi wa mkoa huo ambao kwa kiasi kikubwa wanajishughulisha na shughuli za Uvuvi kwa ajili ya mahitaji ya Chakula na kukuza uchumi wao.

Boti hizo zilizotolewa leo ni sehemu ya Boti 120 zinazotarajiwa kutolewa kwenye awamu ya pili ya Mkopo huo wenye masharti nafuu ambapo mpaka kukamilika kwa awamu zote mbili jumla ya Boti 280 zinatarajiwa kukopeshwa kwa Wavuvi nchini.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (katikati), Viongozi na Watendaji wa Wizara na mikoa ya Pwani na Dar-es-Salaam wakikabidhi mfano wa ufunguo wa boti ya Uvuvi ikiwa ni ishara ya kukabidhi boti za kisasa za Uvuvi kwa Vikundi vya mikoa hiyo (kulia) Julai 16, 2025 jijini Dar-es-Salaam.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (kushoto) akikabidhi cheti kwa mwakilishi wa kikundi cha “Survival Women) kutoka Bagamoyo wakati wa Hafla ya ugawaji Boti za kisasa za Uvuvi awamu ya pili iliyofanyika Julai 16, 2025 jijini Dar-es-Salaam.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (katikati) akikabidhi zana za Uvuvi kwa wawakilishi wa vikundi vya mikoa ya Pwani na Dar-es-Salaam muda mfupi baada ya kuwakabidhi boti za kisasa za Uvuvi Julai 16, 2025 jijini Dar-es-Salaam.





Jumatano, 16 Julai 2025

DKT. MHEDE AFUNGUA MKUTANO WA WADAU WA TASNIA YA KUKU

Na. Hamis Hussein 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede amefungua Mkutano wa tasnia ya Kuku (National Poultry Delivery Lab) unaofanyika  katika Hoteli ya Serena, Jijini Dar-es-salaam kuanzia leo Julai 15-16, 2025. 

Mkutano huo umelenga kuwakutanisha wadau wa tasnia ya kuku ili kuchambua, kujadili na kutoa suluhisho ya namna ya kukabiliana na changamoto zinazopunguza ufanisi na ushindani wa tasnia ya Kuku nchini.

Akifungua Mkutano huo,  Dkt. Mhede alielezea kuwa tasnia ya kuku  imeajiri asilimia 65 ya vijana na asilimia 51 ya wanawake nchini

 "Tasnia ya Kuku inachagiza ukuaji wa sekta nyingine ikiwemo Kilimo kutokana na mahitaji makubwa  ya vyakula vya Kuku vinavyotokana na mahindi na soya  ambayo vimeifanya tasnia hii  ya kuku kuwa ya kimkakati nchini" alisema Dkt. Mhede.

Aidha, Dkt Mhede amewahimiza Washiriki wa mkutano huo kutumia jukwaa hilo kuchambua na kuanisha maeneo ya kimkakati ambayo yatatatua changamoto zinazoikabili tasnia hiyo pamoja na  kujenga uwezo kwa wafugaji  na wafanyabiashara  wa tasnia ya kuku ndani ya nchi ili waweze kuzalisha kwa tija na kuyafikia masoko.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede akifungua Mkutano wa tasnia ya Kuku (National Poultry Delivery Lab) unaofanyika  katika Hoteli ya Serena, Jijini Dar-es-salaam kuanzia leo Julai 15-16, 2025.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede, akiwa katika picha ya pamoja na Washiriki mara baada ya uzinduzi  wa Mkutano wa National Poultry Delivery Lab  unaofanyika katika hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam kuanzia Julai 15-16, 2025.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede akiwa katika mazungumzo na wadau kutoka Benki ya Dunia,  SAGCOT, pamoja na Shirika la IFAD kando ya Mkutano wa National Poultry Delivery Lab unaofanyika katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam kuanzia Julai 15- 16, 2025.


UTEKELEZAJI KAMPENI YA CHANJO: MIFUGO MILIONI 6 YACHANJWA NDANI YA WIKI 2

Na. Omary Mtamike

◼️Zoezi sasa kuendelea kwa miezi 2

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amebainisha kuwa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo imefanyika kwa mafanikio ambapo takribani Mifugo Milioni 6 imechanjwa na kutambuliwa tangu kuanza kwa kampeni hiyo Julai 02,2025 hadi sasa. 

Mhe. Dkt. Kijaji asema hayo wakati wa tukio la kuanza kwa kampeni hiyo mkoani Dodoma lililofanyika Wilaya ya Bahi Julai 15, 2025 ambapo ametoa shukrani kwa wafugaji kote nchini kwa namna walivyojitokeza tangu kuanza kwa zoezi hilo ambapo amewaomba kuendelea kufanya hivyo kwa kipindi chote cha miezi miwili ya utekelezaji wake.

“Mhe. Rais amedhamiria kutekeleza kampeni hii kwa wafugaji wote bila kumuacha hata mmoja na ndio maana amewawezesha maafisa Mifugo kwenye kata zote pikipiki na mafuta yake ili waweze kuwafikia wafugaji wote hivyo sitegemei kuona mtaalam yoyote wa Mifugo akiwa ofisini wakati wa utekelezaji wa kampeni hii” Ameongeza Mhe. Dkt. Kijaji

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa huo kwenye tukio hilo ambaye pia Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Joachim Nyingo amesema kuwa utekelezaji wa kampeni hiyo una manufaa kwa Watanzania wote ambapo wengi watanufaika kupitia mzunguko wa fedha zitakazotokana na kuuzwa kwa Mifugo hiyo kwenye masoko ya nje.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji kanda ya kati Bw. Saramba Mataji amewataka wafugaji wote kwenye kanda hiyo kuchangamkia fursa hiyo iliyotolewa na Serikali ili waweze kuondokana na changamoto ya upotevu wa Mifugo yao ambayo imekuwa ikiwasumbua kwa muda mrefu.

Kampeni hiyo ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo itaendelea kote nchini kwa kipindi cha miezi Miwili ambapo kwa mwaka huu ambapo Serikali imeshatoa takribani Shilingi Bilioni 69.2 kwa ajili ya utekelezaji wake.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (katikati) akitoa chanjo ya mdondo wa kuku kama ishara ya kuanza kwa utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo mkoani Dodoma Julai 15,2025. Kulia ni Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa huo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Joachim Nyingo na kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Bi. Albina Mtumbuka.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, Viongozi na Watendaji mbalimbali wa mkoa wa Dodoma (kushoto) wakishuhudia zoezi la uchanjaji linavyofanyika wakati wa hafla ya kuanza kwa Kampeni ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo Wilaya iliyofanyika Wilaya ya Bahi Julai 15, 2025.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akivalishwa skafu na vijana wa skauti mara baada ya kuwasili Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma Julai 15, 2025 ambako aliongoza Hafla ya kuanza kwa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo mkoani humo.


Jumanne, 15 Julai 2025

CHANJO NA UTAMBUZI NI MAPINDUZI YA SEKTA YA MIFUGO NCHINI-DKT.KIJAJI

Na. Omary Mtamike

◼️Serikali yadhamiria kuondokana na homa ya Mapafu ya Ng’ombe ifikapo 2030

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo itakuwa ni chachu ya mapinduzi wa sekta ya Mifugo nchini.

Mhe. Kijaji amesema hayo wakati wa ziara yake ya Ukaguzi wa utekelezaji wa kampeni hiyo Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro Julai 10, 2025 ambapo amebainisha kuwa kufanyika kwa kampeni hiyo kunaweka ukomo wa kutorosha mifugo katika nchi jirani ambako wafugaji walikuwa wanaenda kutafuta masoko kwenye nchi zilizopata ithibati ya Shirika la kimataifa la Afya ya wanyama (WOAH).

“Kwa hivi sasa baada ya kutangaza tu kuanza kwa kampeni hii tayari masoko ya kimataifa yameonesha dhamira ya kuhitaji Mifugo yetu hai na mazao yake na ninatamani itakapomalizika miaka 5 ya utekelezaji wa kampeni hii turejee kwa Mhe. Rais na kumuonesha namna alivyofanikiwa kubadili sekta yetu ya Mifugo” Ameongeza Mhe. Dkt. Kijaji.

Akielezea ubora wa hereni za kielektroniki zinazotumika kwenye zoezi la Utambuzi wa Mifugo, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo nchini Dkt. Benezeth Lutege amesema kuwa hereni hizo zimetengenezwa kwa kuzingatia ustawi wa wanyama ikiwa ni pamoja na kuwekewa kifaa maalum kinachoziwezesha kuzunguka sikioni pindi mnyama anapotembea.

“Lakini pia hereni hizi mbali na kuwa na gamba gumu lisiloweza kuvunijika, maandishi yake yameandikwa kwa mionzi mikali na hivyo kutoweza kufutika hata yakikwanguliwa na kifaa chenye ncha kali” Ameongeza Dkt. Lutege.

Akizungumza kwa niaba ya wafugaji wa Mkoa wa Morogoro, Kiongozi wa kimila wa mikoa ya kanda ya Mashariki Chifu Kashu Moreto amesema kuwa chanjo hizo na hereni zinafuta fikra potofu waliyokuwa nayo wafugaji hapo awali ambapo waliamini mifugo inachanjwa na kutambuliwa ili itaifishwe na Serikali.

“Kwa bahati nzuri Rais wetu mpendwa ameongea maneno mazuri kwa kusema hereni zitatolewa bure hivyo mimi kwa kuwa ni kiongozi wa takribani mikoa 7 hivyo nitapiga kelele kwa wafugaji wenzangu wote tukachanje ila naomba Serikali iendelee kusimamia vema zoezi hili ili chanjo hizo ziendelee kuwa salama kwa Mifugo yetu” Amesema Chifu Kashu.

Ziara hiyo ya Mhe. Dkt. Kijaji iliyolenga kukagua utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo iliyozinduliwa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu Juni 16, 2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inatarajiwa kuhitimishwa katika Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (katikati) akitoa chanjo ya mdondo wa kuku kama ishara ya kuanza kwa utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo mkoani Morogoro Julai 10, 2025. Kushoto Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa huo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Doto Maulid na kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Japhary Kubecha.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji na baadhi ya Viongozi wa Wilaya ya Mvomero na wale wa wafugaji (kulia) wakishuhudia namna zoezi la utoaji wa chanjo za Mifugo linavyofanyika mara baada ya kuanza kwa utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo mkoani Morogoro Julai 10,2025.





PWANI KUCHANJA NA KUTAMBUA MIFUGO YOTE KWA SIKU 30

Na. Omary Mtamike

Uongozi wa mkoa wa Pwani umesema kuwa utatumia siku 30 pekee kuchanja na kutambuaMifugo yake badala ya miezi 2 iliyopangwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutekeleza zoezi hilo.

Ahadi hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Shaib Ndemanga ambaye pia alimwakilisha mkuu wa Mkoa huo kwenye ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji iliyolenga kukagua Utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo kwenye kwenye kijiji cha Miono Wilaya ya Chalinze.

“Tunajua nyie kama Wizara mmepanga kutekeleza awamu ya kwanza ya zoezi hili kwa miezi miwili lakini nikuhakikishie Mhe. Waziri mkoa wa Pwani kwa furaha tuliyonayo na namna tulivyopokea zoezi hili tutahakikisha tunamaliza ndani ya siku 30” Amesema Mhe. Ndemanga.

Akizungumza mara baada ya kushuhudia kuanza kwa utekelezaji wa kampeni hiyo mkoani Pwani, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ameupongeza mkoa huo kwa namna walivyopokea zoezi hilo alilolitaja kama sehemu ya maono makubwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa upande wa sekta ya Mifugo na wafugaji kwa ujumla.

“Tumeshaanza majadiliano na nchi 5 wanaohitaji kuchukua mifugo yetu ikiwa hai na hiyo inamaanisha kwa sasa soko la Mifugo yetu limeonekana na kwa hapa Pwani tuna kiwanda kikubwa cha kusindika nyama ambacho kitaweza kufikia asilimia 100 za uwezo wake tofauti na ilivyo sasa ambapo kinafanya kazi kwa asilimia 50 ya uwezo wake” Ameongeza Mhe. Dkt. Kijaji.

Naye Mwenyekiti wa chama cha Wafugaji mkoani humo Bw. Ngobere Msamau mbali na kuishukuru Serikali kutokana na chanjo hizo amemhakikishia Mhe. Dkt. Kijaji kuwa wataendelea kutekeleza ushauri na maelekezo yote wanayopewa na Serikali baada ya tija kubwa waliyoanza kuipata hivi sasa.

Ziara hiyo ya Mhe. Dkt. Kijaji iliyolenga kukagua utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo iliyozinduliwa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu Juni 16, 2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea katika mkoa wa Morogoro Julai 10, 2025.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (kushoto) akitoa chanjo ya mdondo wa kuku kama ishara ya kuanza kwa utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo mkoani Pwani Julai 09, 2025. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mhe. Petro Magoti.

Mkurugenzi wa huduma za Mifugo nchini Dkt. Benezeth Lutege (kushoto) akimweleza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, Viongozi na Watendaji mbalimbali wa Wizara hiyo na mkoa wa Pwani sifa za hereni za kielektroniki zitakazotumika kwenye zoezi la Utambuzi wa Mifugo wakati wa hafla ya kuanza kwa utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo mkoani humo Julai 09, 2025.

Wakuu wa Wilaya ya Bagamoyo na Kisarawe Mhe. Petro Magoti na Shaib Ndemanga wakielezwa namna mfumo wa utambuzi wa Mifugo kwa kutumia hereni za kielektroniki unavyofanya kazi wakati wa hafla ya kuanza kwa utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo mkoani Pwani Julai 09, 2025. Kushoto anayeshuhudia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji na Viongozi mbalimbali wa mkoa wa Pwani (kulia) wakishuhudia zoezi la uchanjaji linavyofanyika Kwenye kijiji cha Miono mkoani humo Julai 09, 2025.


SERIKALI YATOA ONYO KWA WATAKAOWATOZA WAFUGAJI FEDHA KWENYE KAZI UCHANJAJI NA UTAMBUZI WA MIFUGO

Na. Daudi Nyingo – Kalambo, Rukwa

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa onyo kwa wachanjaji au watumishi watakaohusika na kazi ya kutoa chanjo na utambuzi wa mifugo kote nchini watakaojiongoza vibaya na kujaribu kuwatoza wafugaji fedha za afua ya uchanjaji na utambuzi wa mifugo, kinyume na muongozo wa kitaifa uliotengezwa na Wizara kwa kuwashirikisha wadau wote na kisha ukazindiliwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo ya Kitaifa mnamo wa tarehe 16 Juni 2025 Wilayani Bariadi, Mkoa wa Simiyu.

Akizungumza leo tarehe 8 Julai 2025, katika Ranchi ya Taifa ya Kalambo (NARCO), Wilayani Nkasi na Kalambo, Mkoani Rukwa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede, alieleza kuwa, “shughuli zote za kuchanja na kutambua mifugo zinagharamiwa kikamilifu (kwa asilimia 100) na Serikali, hivyo basi wafugaji hawapaswi kulipia huduma hizo”.

“Tupo hapa NARCO Wilayani Nkasi na Kalambo, Wizara ya Mifugo tunaendelea na zoezi letu makini la utambuzi na uchanjaji wa mifugo. Tunachanja ng’ombe, mbuzi, kondoo, na kuku. Awamu hii tumefika hapa katika Ranchi ya Taifa ya Kalambo na tumekutana na idadi ya ng’ombe wapatao 36,000, wakiwemo wanaomilikiwa na Serikali kupitia NARCO, wananchi wapangaji ndani ya ranchi, pamoja na wafugaji majirani wanaozunguka uwanda huu wa malisho na machungani ya maeno ya Wilaya ya Kalambo na Nkasi ndani ya Mkoa wa Rukwa,”

“Zoezi hili limekuwa na mafanikio makubwa, ambapo hadi kufikia leo ng’ombe wapatao 1,500 tayari wamechanjwa na wananchi wameijitokeza kwa wingi kuonesha uelewa na mwamko wao mkubwa wa kuijenga sekta ya mifugo. Kazi hii pia inatoa elimu kwa wafugaji juu ya umuhimu wa chanjo na matumizi ya teknolojia ya kidijitali kwenye utambuzi wa mifugo ili kulinda usalama wake na kusaidia Serikali kuwa na takwimu sahihi kwa mipango ya kisera, kisheria na kiuwezeshaji,” alisema Dkt. Mhede.

Dkt. Mhede aliwataka watumishi wote wanaoshiriki katika utekelezaji wa zoezi hilo kuzingatia maadili na kuacha tabia ya kutoza wafugaji pesa kwani ni kinyume cha muongozo wa Serikali kwa kuwa gharama zote zimelipwa na Serikali na atakaekiuka atakuwa amekosa kukosa uadilifu wa kazi na ni usaliti kwa wafugaji na Taifa.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Ndugu Robert Msalika Makungu, alieleza kuwa kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo ni hatua kubwa ya kimkakati katika kulinda afya ya mifugo na kuboresha maisha ya wafugaji, hasa katika Mkoa wa Rukwa. 

“Tumeipokea kampeni hii kwa mikono miwili. Ni hatua muhimu sana kwa sababu inalenga kupunguza au kuondoa kabisa changamoto ya vifo vya mifugo vilivyokuwa vikisababishwa na magonjwa, hali iliyokuwa ikiathiri uchumi wa wafugaji wetu kwa kiasi kikubwa,” 

“Tunatarajia kuchanja zaidi ya ng’ombe laki nne katika mkoa wetu wa Rukwa, sambamba na mbuzi, kondoo na kuku. Tunaendelea kutoa elimu ya kutosha kwa jamii kuhakikisha kila mfugaji anashiriki na anafahamu umuhimu wa chanjo hizi. Serikali tayari imegharimia kila hatua ya zoezi hili, na sisi kama Mkoa tumejipanga kuhakikisha kila mnyama anafikiwa,” alisema Makungu.

Vile vile, Katibu Tawala huyo wa Mkoa wa Rukwa, alieleza kuwa Mkoa umejipanga kikamilifu kutekeleza kampeni hiyo kwa ufanisi, kwa kushirikiana na wataalamu wa mifugo katika ngazi zote. Alisisitiza kuwa Uongozi wa Mkoa umeweka utaratibu wa ufuatiliaji wa karibu kuhakikisha hakuna mfugaji anayetozwa gharama yoyote kuhusiana na chanjo au utambuzi wa mifugo, kwani Serikali tayari imegharamia kila hatua ya utekelezaji wa zoezi hilo. Aliongeza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka muongozo huo wa kitaifa.

Bi. Mgaya Myende, mfugaji kutoka kijiji cha Nkana, Wilayani Kalambo, alisema kuwa kushiriki kwake katika zoezi hilo la chanjo kumempa faraja kubwa, hasa baada ya kupatiwa huduma ya chanjo ya mifugo yake bila malipo. Alieleza kuwa chanjo zilizotolewa ni pamoja na ya mapafu kwa ng’ombe, mbuzi na kondoo, na kwa upande wa kuku zimetolewa chanjo za kideri, ndui na mafua. Alisema kuwa awali wafugaji wengi walikuwa wanaficha mifugo kwa kushindwa kumudu gharama, lakini kwa sasa anaamini wengi wataweza kuchanja mifugo yao yote.

Kwa upande wake, Bw. Benueli Makselo, mfugaji kutoka kijiji cha Sintali, Wilayani Kalambo, alifafanua kuwa amekuwa akifuatilia kwa makini agizo la Mheshimiwa Rais kuhusu kampeni hiyo. Aliona punguzo la gharama za chanjo kuwa ni neema kwa wafugaji wote akiwemo na yeye. Alieleza kuwa awali alikuwa analipa Shilingi 1,000 kwa kila ng’ombe, lakini sasa kuna ruzuku ya Serikali ambapo atachangia ununuzi wa chanjo kwa Shilingi 500, huku chanjo ya mbuzi na kondoo ikipungua kutoka Shilingi 600 hadi 300 kutokana na ruzuku ya Serikali. Pia, alieleza kufurahishwa na utoaji wa heleni za utambuzi bure, ambazo awali ziligharimu Shilingi 1,750 kwa kila ng’ombe. Alisisitiza kuwa hatua hiyo inawapa wafugaji ulinzi na urahisi wa kufuatilia mifugo yao endapo itapotea.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede akiongoza zoezi la uvishaji hereni kwa Ng’ombe alipotembelea wafugaji wa mkoa wa Rukwa Julai 08, 2025, ikiwa ni muendelezo wa zoezi la uhamasishaji utoaji chanjo na utambuzi wa mifugo iliyofanyika katika Ranchi ya Kalambo iliyopo kijiji cha Nkana, Wilaya ya Kalambo, Mkoani Rukwa.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede (kulia) akikabidhi vitendea kazi vitakavyotumika kwenye zoezi la uchanjaji na utambuzi wa mifugo Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Ndugu Msalika Makungu Julai 08, 2025, ikiwa ni muendelezo wa zoezi la uhamasishaji utoaji chanjo na utambuzi wa mifugo iliyofanyika katika Ranchi ya Kalambo iliyopo kijiji cha Nkana, Wilaya ya Kalambo, Mkoani Rukwa.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede (kulia) akishuhudia zoezi la uchanjaji wa mifugo Julai 08, 2025, ikiwa ni muendelezo wa zoezi la uhamasishaji utoaji chanjo na utambuzi wa mifugo iliyofanyika katika Ranchi ya Kalambo iliyopo kijiji cha Nkana, Wilaya ya Kalambo, Mkoani Rukwa.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Ndugu Msalika Makungu (wa pili kutoka kushoto) akishuhudia zoezi la uchanjaji wa mifugo Julai 08, 2025, ikiwa ni muendelezo wa zoezi la uhamasishaji utoaji chanjo na utambuzi wa mifugo iliyofanyika katika Ranchi ya Kalambo iliyopo kijiji cha Nkana, Wilaya ya Kalambo, Mkoani Rukwa.Wa nne kutoka kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede akiongoza zoezi la uvishaji hereni kwa Ng’ombe alipotembelea wafugaji wa mkoa wa Rukwa Julai 08, 2025, ikiwa ni muendelezo wa zoezi la uhamasishaji utoaji chanjo na utambuzi wa mifugo iliyofanyika katika Ranchi ya Kalambo iliyopo kijiji cha Nkana, Wilaya ya Kalambo, Mkoani Rukwa.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Ndugu Msalika Makungu akiongoza zoezi la uvishaji hereni kwa Ng’ombe Julai 08, 2025, ikiwa ni muendelezo wa zoezi la uhamasishaji utoaji chanjo na utambuzi wa mifugo iliyofanyika katika Ranchi ya Kalambo iliyopo kijiji cha Nkana, Wilaya ya Kalambo, Mkoani Rukwa.






Jumanne, 8 Julai 2025

WAFUGAJI MKOANI SINGIDA WAHAMASISHWA KUCHANJA NA KUTAMBUA MIFUGO YAO

Na Chiku Makwai, Singida

Wafugaji mkoani Singida wametakiwa Kushiriki kikamilifu katika zoezi la uchanjaji na utambuzi wa Mifugo yao ambapo utekelezaji wa zoezi hilo mkoani humo limeanza leo  Julai 8, 2025 katika Kijiji cha  Makunda kilichopo wilayani Iramba lengo likiwa ni kuikinga mifugo yao dhidi ya magonjwa na kuiboresha  kwa ajili ya Soko la Kimataifa.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt.Ashatu Kijaji, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mafunzo ya Mifugo (LITA) Dkt. Pius Mwambene  amesema zoezi hilo ambalo limeziduliwa mwezi June 16, 2025, na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan litaongeza tija kwa wafugaji kote nchini hivyo wanapaswa Kulizingatia.

Dkt. Mwambene amesema kuwa katika Kampeni ya Chanjo ambayo inaendelea nchini wafugaji watachanja mifugo yao kwa bei ya ruzuku baada ya Serikali kutoa bilioni 216 fedha za kitanzania kwa ajili ya zoezi hilo ambalo litafanyika kwa miaka mitano.

"Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alishazindua kampeni hii ya chanjo na ameridhia kuchangia nusu gharama ya chanjo ili kuwasaidia wafugaji kote nchini kuikinga mifugo yao dhidi ya magonjwa na kuimarisha biashara ya Mifugo na mazao yake katika masoko ndani na Kimataifa, hivyo wafugaji wa mkoa huu wa Singida jitokezeni na mshiriki kikamilifu kwenye kampeni hii" alisema Dkt. Mwambene.

Baadhi ya Wafugaji Wilayani Iramba wameishukuru Serikali kwa Kuwashika Mkono katika Chanjo ya Mifugo wakisisitiza kuwa Kabla ya Chanjo hiyo mifugo mingi imekuwa ikifa kutokana na Magonjwa Mbalimbali.

Utekelezaji wa zoezi hilo ulioenda sambamba na uhamasishaji wa wafugaji kushiriki kikamilifu kampeni hiyo  umefanyika leo Julai 8, 2025 katika Kijiji cha Makunda Wilayani Iramba Mkoa wa Singida na Mifugo zaidi ya Milioni 1 inatarajiwa kupewa chanjo mkoani humo.






MIFUGO YATAKIWA VITUONI KWA CHANJO NA UTAMBUZI

Na. Edward Kondela

Wafugaji wa Mkoa wa Kagera wametakiwa kuunga mkono juhudi za serikali za kufikisha mifugo katika vituo vya kutolea chanjo na utambuzi wa mifugo ili kufikia adhma ya serikali ya kudhibiti magonjwa na kupanua wigo wa masoko ya kimataifa.  

Akimwakilisha leo (08.07.2025) Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mkuu wa Wilaya ya Missenyi Mhe. Kanali Mstaafu Hamis Mahiga, wakati wa utekelezaji wa kampeni kimkoa katika wilaya hiyo, amesema ni muhimu wafugaji wakafuata ratiba kama itakavyoainishwa kwa ajili ya mifugo yao kuchanjwa na kutambuliwa.

Amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeridhia kugharamia mpango wa miaka mitano unaoanza 2025 hadi 2029 wenye thamani ya Shilingi Bilioni 216, kwa ajili ya uchanjaji na utambuzi wa mifugo kote nchini, hivyo ni muhimu wafugaji wa Mkoa wa Kagera kuhakikisha wanashiriki vyema kwa kuwa zoezi hilo siyo la hiari bali ni lazima.

Aidha, amewaasa viongozi wenzake kusimamia vyema zoezi la utoaji chanjo na utambuzi ili adhma ya serikali iweze kufikiwa ikiwemo kuhamasisha wafugaji na kutoa elimu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Michael, akimwakilisha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti, amebainisha kuwa Tanzania inaendelea kuuza nyama nje ya nchi hususan nchi za Mashariki ya Kati.

Ameongeza kuwa hadi sasa kuna takriban tani 14,000 ambazo zinaenda kwenye masoko hayo lakini bado kuna masoko kwenye mataifa mengine ikiwemo China na Bara la Ulaya ambayo yanahitaji kuuziwa nyama kutoka Tanzania.

Amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi inapita maeneo mbalimbali nchini, kuhamasisha Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliizindua Juni 16 mwaka huu mkoani Simiyu.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Mkoa wa Kagera Haji Abdul Majid Kayondo, amesema zoezi la chanjo wamekuwa wakilihitaji kwa muda mrefu na kwamba wamelipokea kwa mikono miwili na kumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amefafanua kuwa wenyewe kama chama wataweka hamasa kubwa kwa wafugaji hususan Wilaya ya Missenyi ambayo ni mojawapo ya wilaya yenye mifugo mingi mkoani humo.

Amewaasa wafugaji kushiriki vyema katika zoezi hilo na kutoficha mifugo ili kufikia adhma ya serikali katika kuwa na mifugo bora na yenye tija.

Serikali imetoa ruzuku kwa chanjo za mifugo katika kampeni hii ambapo kuku wanachanjwa bure, ng’ombe Shilingi 500 wakati mbuzi na kondoo Shilingi 300.

Mkuu wa Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera Mhe. Kanali Mstaafu Hamis Mahiga (kulia) akiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Michael, wakati wa utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo katika Mkoa wa Kagera. (08.07.2025)

Mmoja wa maafisa mifugo katika Mkoa wa Kagera akitoa chanjo kwa ng'ombe dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu (CBPP), wakati wa utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo katika Mkoa wa Kagera, iliyofanyika wilayani Missenyi. (08.07.2025)

Baadhi ya ng'ombe aina ya ankole wakiwa wameandaliwa kwa ajili ya kupatiwa chanjo dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu (CBPP), wakati wa utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo katika Mkoa wa Kagera, iliyofanyika wilayani Missenyi. (08.07.2025)

Mkuu wa Wilaya ya Missenyi Mhe. Kanali Mstaafu Hamis Mahiga, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kagera,  wakati wa utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo katika Mkoa wa Kagera, iliyofanyika wilayani Missenyi ambapo amewaasa wafugaji kufikisha mifugo katika vituo vya chanjo na utambuzi wa mifugo ili kufikia adhma ya serikali. (08.07.2025

Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Michael, akimwakilisha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti, wakati wa utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo katika Mkoa wa Kagera, iliyofanyika wilayani Missenyi ambapo amebainisha kuwa Tanzania inaendelea kuuza nyama nje ya nchi hususan nchi za Mashariki ya Kati. (08.07.2025)



MKOA WA SONGWE WAZINDUA RASMI PROGRAMU YA CHANJO NA UTAMBUZI WA MIFUGO

Na. Daudi Nyingo – Songwe

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imezindua rasmi programu ya kitaifa ya utoaji wa chanjo na utambuzi wa mifugo kwa Mkoa wa Songwe, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo kwa Mifugo iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa ziara yake mkoani Simiyu. Kupitia programu hiyo, zaidi ya ng’ombe 479,800 na kuku zaidi ya milioni 2.3 wanatarajiwa kunufaika katika Mkoa wa Songwe pekee, ikiwa ni sehemu ya mpango unaotekelezwa nchi nzima.

Uzinduzi wa programu hiyo kimkoa umefanyika leo, Jumatatu Julai 7, 2025, katika Kijiji cha Ndanga, Kata ya Mbuyuni, Wilaya ya Songwe, na kuongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt. Mhede amesema programu hiyo inalenga kukinga mifugo dhidi ya homa ya mapafu ya Ng’ombe na kwa upande wa kuku ni Kideri, ndui na mafua ambapo chanjo hizo zote  zimepata ruzuku kutoka Serikali ili kuwasaidia wafugaji kupata huduma hiyo.

“Katika siku ya kwanza ya uzinduzi, zaidi ya ng’ombe 1,500 wamechanjwa na kutambuliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, na wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Songwe,” 

“Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeamua kuwawezesha wafugaji kwa kutoa ruzuku kwenye zoezi hili. Wafugaji sasa watachangia Shilingi 500 tu kwa chanjo ya ng’ombe mmoja badala ya Sh1,000, huku kuku wakichanjwa bure,” amesema Dkt. Mhede.

Dkt. Mhede amefafanua kuwa mpango huo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuongeza thamani ya mazao ya mifugo. Baada ya kupatiwa chanjo na kutambuliwa, wafugaji wataweza kupata mikopo kupitia taasisi za kifedha na kushiriki kwenye biashara ya kimataifa na amesisitiza kuwa mifugo yote itakayochanjwa pia itatambuliwa kwa kuvishwa hereni za kielektroniki ambazo zitasaidia utambuzi wa haraka endapo mnyama atapotea au kuibiwa.

Kwa upande wake, Mshauri wa Mifugo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omary Ayubu Rajabu, amesema kuwa mkoa umeanza kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu umuhimu wa chanjo na utambuzi wa mifugo, pamoja na kushirikiana na viongozi wa wafugaji kufanikisha mpango huo.

“Tumejipanga kuhakikisha mifugo yote inapata chanjo na kutambuliwa. Tayari tumepokea chanjo na vifaa vyote kutoka Wizarani,” amesema Rajabu.

Nae Mwenyekiti wa Wafugaji Wilaya ya Songwe, Bw. Lushona Paul Makula, ametoa rai kwa wafugaji wote kutumia fursa hiyo adhimu.

“Tutahakikisha kila mfugaji anapata taarifa sahihi kuhusu zoezi hili. Tunaelewa baadhi ya wafugaji wamekuwa na tabia ya kuficha mifugo yao, lakini tutawafikia na kuwahamasisha washiriki,” ameeleza.

Wafugaji wa eneo hilo wameeleza shukrani zao kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha mpango huo ambao wamesema utakuwa mkombozi kwa mifugo yao. Mzee Mwajuma Doto Bulugu, mkazi wa Ndanga na mfugaji wa ng’ombe 240, amesema kuwa ng’ombe wake wote wamechanjwa na kutambuliwa, na kwamba wanaamini mpango huo utasaidia kukabiliana na magonjwa ya mifugo. Naye Julietha Mwalyehe, mfugaji kutoka Kijiji cha Mbuyuni, amesema kuwa kuku wake wote wamechanjwa bila malipo na ameeleza kuwa msaada huo kutoka kwa Rais Samia ni mkubwa kwa wafugaji.

Programu hiyo ya chanjo na utambuzi inaendelea kutekelezwa kote nchini kama sehemu ya juhudi za Serikali za kulinda afya ya mifugo na kuboresha maisha ya wafugaji.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede (kulia) akiongoza zoezi la uchanjaji wa mifugo (kuku) alipotembelea wafugaji wa mkoa wa Songwe Julai 07, 2025, ikiwa ni muendelezo wa zoezi la uhamasishaji utoaji chanjo na utambuzi wa mifugo iliyofanyika katika Kijiji cha Ndanga, Wilaya ya Songwe, Mkoani Songwe.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede (kushoto) akiongoza zoezi la uvishaji hereni kwa Ng’ombe alipotembelea wafugaji wa mkoa wa Songwe Julai 07, 2025, ikiwa ni muendelezo wa zoezi la uhamasishaji utoaji chanjo na utambuzi wa mifugo iliyofanyika katika Kijiji cha Ndanga, Wilaya ya Songwe, Mkoani Songwe.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede (kulia) akimuongoza Mwenyekiti wa Wafugaji Wilaya ya Songwe, Bw. Lushona Paul Makula kwenye zoezi la uchanjaji wa mifugo (kuku) alipotembelea wafugaji wa mkoa wa Songwe Julai 07, 2025, ikiwa ni muendelezo wa zoezi la uhamasishaji utoaji chanjo na utambuzi wa mifugo iliyofanyika katika Kijiji cha Ndanga, Wilaya ya Songwe, Mkoani Songwe.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede (katikati) akikagua baadhi ya mifugo iliyoletwa kwenye zoezi la chanjo na utambuzi mkoani Songwe Julai 07, 2025, ikiwa ni muendelezo wa zoezi la uhamasishaji utoaji chanjo na utambuzi wa mifugo iliyofanyika katika Kijiji cha Ndanga, Wilaya ya Songwe, Mkoani Songwe.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede (kulia) akikabidhi vitendea kazi vitakavyotumika kwenye zoezi la uchanjaji na utambuzi wa mifugo kwa Mshauri wa Mifugo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omary Ayubu Rajabu alipotembelea wafugaji wa mkoa huo Julai 07, 2025, ikiwa ni muendelezo wa zoezi la uhamasishaji utoaji chanjo na utambuzi wa mifugo iliyofanyika katika Kijiji cha Ndanga, Wilaya ya Songwe, Mkoani Songwe.


DKT. KIJAJI AKOSHWA NA UTAYARI WA WAFUGAJI KWENYE CHANJO NA UTAMBUZI

Na. Omary Mtamike

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amewashukuru wafugaji nchini kwa utayari wao kwenye utekelezaji wa mpango wa kuboresha sekta ya Mifugo nchini hususan upande wa kampeni ya Chanjo na Utambuzi iliyoasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Dkt. Kijaji ametoa shukrani hizo Julai 07, 2025 kwenye ziara yake ya ukaguzi wa utekelezaji wa kampeni hiyo Wilaya ya Urambo mkoani Tabora ambapo ameonesha kufurahishwa na ushirikiano ambao wafugaji wameutoa kwa Serikali kwenye maeneo yote aliyopita.

“Serikali inawahakikishia wafugaji kuwa daima itaendelea kuboresha mazingira yenu ya ufugaji na ndio maana mmeona wenyewe jinsi Rais Samia alivyoamua kugharamia utambuzi wa Mifugo yote nchini zoezi ambalo awali lililalamikiwa kutokana na gharama zilizokuwa zinatozwa za shilingi 700 kwa ng’ombe mmoja” Amesema Mhe. Dkt. Kijaji

Akigusia changamoto ya wafugaji wengi kukosa maeneo yao ya malisho, Mhe. Dkt. Kijaji ameeleza kuwa Rais Samia ametoa maelekezo kwa Wizara yake, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Ardhi kuainisha mipango ya matumizi bora ya ardhi ili wafugaji waoneshwe maeneo yao.

“Kwa hiyo kwa unyenyekevu nikuombe Mhe. Mkuu wa mkoa utusaidie kufahamu maeneo hayo na sisi Wizara tutahakikisha yanapata hati na kutambuliwa kama maeneo ya Wafugaji” Ameongeza Mhe. Dkt. Kijaji.

Ziara hiyo ya Mhe. Dkt. Kijaji iliyolenga kukagua utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo iliyozinduliwa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu Juni 16, 2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea katika mkoa wa Morogoro Julai 10, 2025.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (katkati) akitoa chanjo ya mdondo wa kuku kama ishara ya kuanza kwa utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo mkoani Tabora Julai 07,2025. Kulia ni Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa huo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mhe. Naipataki Tukai na kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Urambo Mhe. Khamis Mkanachi

Mkurugenzi wa huduma za Mifugo nchini Dkt. Benezeth Lutege (kulia) akimueleza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (kushoto) namna zoezi la Chanjo na Utambuzi linavyotekelezwa muda mfupi mara baada ya kufika kwenye shamba la Mifugo la kampuni ya “Bashe Diary Farm” lililopo Wilaya ya Uyui mkoani Tabora Julai 07, 2025.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji na Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Naipataki Tukai (kushoto) wakishuhudia zoezi la uchanjaji linavyofanyika Wilaya ya Urambo mkoani humo Julai 07, 2025.


MHE: MNYETI: “MASHAMBA YA SERIKALI YAACHWE KWA MANUFAA YA TAIFA”

Na. Edward Kondela – WMUV, Mwanza

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti amesema mashamba ya uzalishaji mifugo ya serikali lazima yaachwe yafanye shughuli za serikali kwa ajili ya manufaa ya taifa zima.

Naibu Waziri Mnyeti amebainisha hayo (07.07.2025) katika Shamba la Uzalishaji Mifugo la Serikali Mabuki lililopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, alipofanya ziara katika shamba hilo kufuatilia utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo, ambapo amesema mashamba hayo lazima yaendelezwe kwa kuwa ni rasilimali ya taifa.

Mhe. Mnyeti amesema kuwa mifugo iliyopo katika mashamba ya serikali ni kama mbegu ambazo lazima kuzitunza ili kutoharibu mbegu za asili za mifugo.

“Mashamba ya serikali ni rasilimali za watanzania wote lazima kulinda kwa pamoja, hizi ng’ombe ni kama mbegu tukiziharibu hizi mbegu ni kwamba tunaharibu kabisa ng’ombe zetu za asili.”

Naibu Waziri Mnyeti amebainisha hayo baada ya taarifa ya kuwepo kwa uvamizi wa mifugo kuingizwa katika Shamba la Uzalishaji Mifugo la Serikali Mabuki kwa ajili ya malisho.

“Ng’ombe 20,000 waliovamia Shamba la Mabuki siyo wa wafugaji wa Misungwi isipokuwa wafugaji wa Misungwi wamekuwa siyo waaminifu kwa kukumbatia makundi ya ng’ombe kutoka nje ya Misungwi halafu wanajifanya ni ng’ombe wao.” amebainisha Mhe. Mnyeti

Ameongeza kuwa hayuko tayari kuwatetea wafugaji wanaoingiza mifugo kwenye mashamba ya uzalishaji mifugo ya serikali kwa kuwa hata yeye ni mfugaji lakini anaheshimu maeneo yaliyotengwa na serikali, yakiwemo mashamba ya uzalishaji mifugo ya serikali na kwamba hayuko tayari kupeleka mifugo yake kwenye mashamba hayo bila kufuata utaratibu wa serikali.

Kuhusu utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kieletroniki, Mhe. Mnyeti amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameelekeza mifugo yote yenye sifa ya kuwekewa hereni lazima itambulike ili kuwezesha pia kufahamu idadi ya mifugo iliyopo nchini.

Aidha, amewaarifu wafugaji kuwa zoezi la uchanjaji wa mifugo linaenda sambamba na uwekaji wa hereni bure, ambapo hereni hizo pia zitasaidia katika kudhibiti wizi wa mifugo nchini.

Naye Kaimu Meneja wa Shamba la Uzalishaji Mifugo la Serikali Mabuki Bi. Lini Mwala amesema katika shamba hilo wanatarajia kuchanja ng’ombe zaidi ya 3,000, mbuzi na kondoo zaidi ya 1,500 katika kudhibiti magonjwa ya mifugo.

Akizungumza kwa niaba ya wafugaji wa Wilaya ya Misungwi, Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji katika wilaya hiyo Bw. Bukula Muhoja amesema kama chama kuanzia ngazi ya taifa walishaanza uhamasishaji kwa kutoa elimu kwa wafugaji ili wachanje mifugo yao.

Ameongeza kuwa kwa Wilaya ya Misungwi wamesimamia kila kata na kijiji kuhakikisha wanazungumza na wafugaji ili kuchanja mifugo yao na kwamba wamepokea kampeni hiyo kwa mikono miwili.

Kampeni hii serikali imetoa ruzuku ya asilimia 100 kwa kuku ambapo watachanjwa bure huku ng’ombe, mbuzi na kondoo ikitoa ruzuku ya asilimia 50.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti (katikati) akikagua hereni ya kieletroniki iliyowekwa kwenye sikio la ng'ombe wakati wa ziara ya utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo katika Shamba la Uzalishaji Mifugo la Serikali Mabuki, lililopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza. (07.07.2025)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti (katikati) akifuatilia namna taarifa muhimu za hereni za kieletroniki zinavyojazwa kwenye kishikwambi, wakati wa ziara ya utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo katika Shamba la Uzalishaji Mifugo la Serikali Mabuki, lililopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza. (07.07.2025

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi (udhibiti magonjwa yaenezwayo na wadudu), Dkt. Christopher Sikombe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza Mhe. Johari Samizi, juu ya taarifa muhimu zilizopo kwenye hereni za kieletroniki kwa ajili ya mifugo wakati wa ziara ya utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo katika Shamba la Uzalishaji Mifugo la Serikali Mabuki. (07.07.2025)


CHANJO NA UTAMBUZI KUIWEZESHA MIFUGO KUPATA BIMA

Na. Omary Mtamike

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo inayoendelea nchini itawawezesha wafugaji kupata bima ya Mifugo yao.

Mhe. Dkt. Kijaji amesema hayo Julai 06, 2025 wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa utekelezaji wa kampeni hiyo Wilaya ya Chato mkoani Geita ambapo ametoa rai kwa wafugaji hao kuchanja na kutambua mifugo yao yote ili waweze kunufaika na huduma hiyo.

“Huko nyuma wafugaji walikuwa wakilalamika mifugo yao kufa kwa kukosa malisho, Mhe. Rais ameiwezesha mifugo yote kukatiwa bima kwa kuwa itakuwa imeshafanyiwa utambuzi” Amesema Mhe. Dkt. Kijaji

Mhe. Dkt. Kijaji ameongeza kuwa zoezi hilo ni la miezi 2 hivyo amewasihi wafugaji kuhakikisha mifugo yao yote imechanjwa na kutambuliwa ndani ya kipindi hicho ” Ameongeza Mhe. Dkt. Kijaji

Akigusia faida za utambuzi wa Mifugo Mhe. Dkt. Kijaji amesema kuwa zoezi hilo litawasaidia wafugaji kuondokana na changamoto wa wizi wa Mifugo yao kwa kuwa kila mfugo utatambuliwa kwa nambari maalum zinazopatikana kwenye hereni za kielektroniki.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigela ameipongeza Wizara na Serikali kwa ujumla kwa kuwawezesha wataalam wa Mifugo mkoani kwake vitendea kazi vinavyowawezesha kuwahudumia wafugaji kwa urahisi.

“Chanjo hii ni salama kwa asilimia 100 na ndio maana miongoni mwa Mifugo iliyopata chanjo leo ni pamoja na ile ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na ya Naibu Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Doto Biteko na nikuhakikishie Mhe. Waziri sisi Geita tutahakikisha tunafikisha zaidi ya asilimia 70 ya Mifugo yote ndani ya miezi hii miwili ya kampeni” Amesema Mhe. Shigela

Ziara hiyo ya Mhe. Dkt. Kijaji iliyolenga kukagua utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo iliyozinduliwa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu Juni 16, 2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Tabora na Dodoma.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akitoa chanjo ya Ugonjwa wa mdondo wa kuku wakati wa ziara yake ya Ukaguzi wa utekelezaji wa zoezi la Kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo Wilaya ya Chato mkoani Geita Julai 06,2025. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigela.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji na Mbunge wa Jimbo la Chato Mhe. Dkt. Medard Kalemani (kushoto) wakishuhudia namna mfumo wa utambuzi wa Mifugo kielektroniki unavyofanyika wakati wa ziara ya Ukaguzi wa utekelezaji wa zoezi la Kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo wilayani Chato mkoani Geita Julai 06, 2025.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji na Mbunge wa jimbo la Chato Dkt. Medard Kalemani (kushoto) wakishuhudia namna zoezi la uchanjaji mifugo linavyofanyika wakati wa ukaguzi wa utekelezaji wa zoezi hilo Wilaya ya wilayani Chato mkoani Geita Julai 06, 2025.